112 Bible Verses About Wealth
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
17 Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. 18 Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. 19 Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.
-
6 Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa. 7 Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu chochote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu. 8 Lakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo. 9 Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka huanguka kwenye majaribu, na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi. 10 Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.
11 Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole.
-
1 Basi sikilizeni, ninyi matajiri, lieni na kuomboleza kwa ajili ya hali mbaya sana inayowajia. 2 Utajiri wenu umeoza na mavazi yenu yameliwa na nondo. 3 Dhahabu yenu na fedha yenu vimeliwa na kutu. Kutu yake itashuhudia dhidi yenu nayo itaila miili yenu kama vile moto. Mmejiwekea hazina kwa ajili ya siku za mwisho. 4 Angalieni! Ule ujira wa vibarua waliolima mashamba yenu mliouzuia kwa hila unapiga kelele dhidi yenu na vilio vya wavunaji vimefika masikioni mwa Bwana Mwenye Nguvu Zote. 5 Mmeishi duniani kwa anasa na kwa starehe, mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa. 6 Mmewahukumu na kuwaua watu wenye haki, waliokuwa hawapingani nanyi.
-
13 Mtu mmoja katika umati wa watu akamwambia Yesu, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane naye urithi wetu.”
14 Lakini Yesu akamwambia, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa hakimu wenu au msuluhishi juu yenu?” 15 Ndipo Yesu akawaambia, “Jihadharini! Jilindeni na aina zote za choyo. Kwa maana maisha ya mtu hayatokani na wingi wa mali alizo nazo.”
16 Kisha akawaambia mfano huu: “Shamba la mtu mmoja tajiri lilizaa sana. 17 Akawaza moyoni mwake, ‘Nifanye nini? Sina mahali pa kuhifadhi mavuno yangu.’
18 “Ndipo huyo tajiri akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu za nafaka na kujenga nyingine kubwa zaidi na huko nitayahifadhi mavuno yangu yote na vitu vyangu. 19 Nami nitaiambia nafsi yangu, “Nafsi, unavyo vitu vingi vizuri ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi. Pumzika; kula, unywe, ufurahi.” ’
20 “Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe! Usiku huu uhai wako unatakiwa. Sasa hivyo vitu ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani?’
21 “Hivyo ndivyo ilivyo kwa wale wanaojiwekea mali lakini hawajitajirishi kwa Mungu.”
-
19 “Msijiwekee hazina duniani, mahali ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi huvunja na kuiba. 20 Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba. 21 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.
-
10 Yeyote apendaye fedha kamwe
hatosheki na fedha;
yeyote apendaye utajiri kamwe
hatosheki na kipato chake.
Hili nalo pia ni ubatili.
11 Mali ikiongezeka, ndivyo walaji
wanavyoongezeka.
Hii nayo inamfaidia nini mwenye mali
isipokuwa ni kushibisha macho yake?
12 Usingizi wa kibarua ni mtamu,
awe amekula kidogo au kingi,
lakini wingi wa mali
humnyima tajiri usingizi.
13 Nimeshaona uovu mzito chini ya jua:
Utajiri uliolimbikizwa kwa kujinyima
na kuleta madhara kwa mwenye mali,
14 au utajiri uliopotea kwa bahati mbaya,
hivyo kwamba wakati akiwa na mwana
hakuna chochote kilichobaki kwa ajili yake.
-
7 Kwa kuwa Bwana Mungu wenu anawaleta katika nchi nzuri, nchi yenye vijito na mabwawa ya maji, yenye chemchemi zinazotiririka mabondeni na katika vilima; 8 nchi yenye ngano na shayiri, mizabibu na mitini, mikomamanga, mafuta ya zeituni na asali; 9 nchi ambayo chakula hakitapungua na hamtakosa chochote; nchi ambayo miamba yake ni chuma na mnaweza kuchimba shaba kutoka kwenye vilima.
10 Wakati mtakapokwisha kula na kushiba, msifuni Bwana Mungu wenu kwa ajili ya nchi nzuri aliyowapa. 11 Jihadharini msimsahau Bwana Mungu wenu, mkashindwa kushika maagizo yake, sheria na amri zake ambazo ninawapa leo. 12 Angalia wakati mtakapokuwa mmekula na kushiba, mkajenga nyumba nzuri na kukaa humo, 13 na wakati makundi yenu ya ngʼombe na mbuzi na kondoo yatakapoongezeka na fedha na dhahabu yenu itakapoongezeka na vyote mlivyo navyo vitakapozidishwa, 14 basi mioyo yenu isiwe na kiburi mkamsahau Bwana Mungu wenu aliyewatoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa. 15 Aliwaongoza kupitia jangwa lile kubwa na la kutisha, nchi ile ya kiu isiyo na maji, yenye nyoka wa sumu na nge. Aliwatolea maji kutoka kwenye mwamba mgumu. 16 Aliwapa mana ya kula jangwani, kitu ambacho baba zenu hawakukijua, ili kuwanyenyekesha na kuwajaribu ninyi ili mwishoni apate kuwatendea mema. 17 Mnaweza kusema, “Uwezo wangu na nguvu za mikono yangu ndizo zilizonipatia utajiri huu.” 18 Lakini kumbukeni Bwana Mungu wenu, ndiye ambaye huwapa uwezo wa kupata utajiri, na hivyo kulithibitisha Agano lake, ambalo aliwaapia baba zenu, kama ilivyo leo.
-
9 Nawaambia, tumieni mali ya kidunia kujipatia marafiki, ili itakapokwisha, mkaribishwe katika makao ya milele.
10 “Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, pia ni mwaminifu hata katika mambo makubwa, naye mtu ambaye si mwaminifu katika mambo madogo pia si mwaminifu katika mambo makubwa. 11 Ikiwa hamkuwa waaminifu katika mali ya kidunia, ni nani atakayewaaminia mali ya kweli? 12 Nanyi kama hamkuwa waaminifu na mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?
-
4 Usijitaabishe ili kuupata utajiri,
uwe na hekima kuonyesha kujizuia.
5 Kufumba na kufumbua utajiri hutoweka,
huwa kama umepata mabawa ghafula,
ukaruka na kutoweka angani kama tai.
-
11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
14 Lakini, mlifanya vyema kushiriki nami katika taabu zangu. 15 Zaidi ya hayo, ninyi Wafilipi mnajua kwamba siku za kwanza nilipoanza kuhubiri Injili, nilipoondoka Makedonia, hakuna kanisa jingine lililoshiriki nami katika masuala ya kutoa na kupokea isipokuwa ninyi. 16 Kwa maana hata nilipokuwa huko Thesalonike, mliniletea msaada kwa ajili ya mahitaji yangu zaidi ya mara moja. 17 Si kwamba natafuta sana yale matoleo, bali natafuta sana ile faida itakayozidi sana kwa upande wenu. 18 Nimelipwa kikamilifu hata na zaidi; nimetoshelezwa kabisa sasa, kwa kuwa nimepokea kutoka kwa Epafrodito vile vitu mlivyonitumia, sadaka yenye harufu nzuri, dhabihu inayokubalika na ya kumpendeza Mungu. 19 Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu.
-
24 “Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.
-
5 Kwa nini niogope siku mbaya zinapokuja,
wakati wadanganyifu waovu wanaponizunguka,
6 wale wanaotegemea mali zao
na kujivunia utajiri wao mwingi?
7 Hakuna mwanadamu awaye yote
awezaye kuukomboa uhai wa mwingine,
au kumpa Mungu fidia kwa ajili yake.
8 Fidia ya uhai ni gharama kubwa,
hakuna malipo yoyote yanayotosha,
9 ili kwamba aishi milele
na asione uharibifu.
10 Wote wanaona kwamba watu wenye hekima hufa;
wajinga na wapumbavu vivyo hivyo huangamia
na kuwaachia wengine mali zao.
11 Makaburi yao yatabaki kuwa nyumba zao za milele,
makao yao vizazi vyote;
ingawa walikuwa na mashamba
na kuyaita kwa majina yao.
12 Lakini mwanadamu, licha ya utajiri wake, hadumu;
anafanana na mnyama aangamiaye.
-
21 Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo, na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
22 Yule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
23 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Amin, nawaambia, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mbinguni. 24 Tena nawaambia, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”
25 Wanafunzi wake waliposikia haya, walishangaa sana na kuuliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”
26 Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”
-
24 “Kama nimeweka tumaini langu kwenye dhahabu,
au kuiambia dhahabu safi, ‘Wewe ndiwe salama yangu,’
25 kama nimefurahia wingi wa utajiri wangu,
ustawi ambao mikono yangu ilikuwa imepata,
26 kama nimelitazama jua katika kungʼaa kwake
au mwezi ukienda kwa fahari yake,
27 hivyo moyo wangu kushawishiwa kwa siri,
au kubusu mkono wangu kwa kuviheshimu,
28 basi hiyo pia ingekuwa dhambi ya kuhukumiwa,
kwa kuwa ningekuwa si mwaminifu kwa Mungu aishiye juu sana.
-
28 Yeyote ategemeaye utajiri wake ataanguka,
bali mwenye haki atastawi kama jani bichi.
-
11 Fedha isiyo ya halali hupungua,
bali yeye akusanyaye fedha kidogo kidogo huongezeka.
-
33 Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwizi hakaribii wala nondo haharibu. 34 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo moyo wako utakapokuwa pia.
-
17 Yesu alipokuwa anaondoka, mtu mmoja akamkimbilia, akapiga magoti mbele yake, akamuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
18 Yesu akamwambia, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake. 19 Unazijua amri: ‘Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, usidanganye, waheshimu baba yako na mama yako.’ ”
20 Akamjibu, “Mwalimu, amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”
21 Yesu akamtazama na kumpenda, akamwambia, “Umepungukiwa na kitu kimoja. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho uwape maskini hizo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
22 Yule mtu aliposikia hayo, akasikitika sana. Akaondoka kwa huzuni kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
23 Yesu akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, “Itakuwa vigumu sana kwa wenye mali kuingia katika Ufalme wa Mungu!”
24 Wanafunzi wake wakashangazwa sana na maneno hayo. Lakini Yesu akawaambia tena, “Wanangu, tazama jinsi ilivyo vigumu kwa wale wanaotumainia mali kuingia katika Ufalme wa Mungu. 25 Ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”
26 Wanafunzi wake wakashangaa sana. Wakaulizana wao kwa wao, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”
27 Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu sivyo. Mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”
-
1 Ndugu zangu, kama waaminio katika imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe na upendeleo kwa watu. 2 Kwa maana kama akija mtu katika kusanyiko lenu akiwa amevaa pete ya dhahabu na mavazi mazuri, pia akaingia mtu maskini mwenye mavazi yaliyochakaa, 3 nanyi mkampa heshima yule aliyevaa mavazi mazuri na kumwambia, “Keti hapa mahali pazuri,” lakini yule maskini mkamwambia, “Wewe simama pale,” au “Keti hapa sakafuni karibu na miguu yangu,” 4 je, hamjawabagua na kuwa mahakimu mioyoni mwenu mkihukumu kwa mawazo yenu maovu?
5 Ndugu zangu, sikilizeni: Je, Mungu hakuwachagua wale walio maskini machoni pa ulimwengu kuwa matajiri katika imani na kuurithi Ufalme aliowaahidi wale wampendao? 6 Lakini ninyi mmemdharau yule aliye maskini. Je, hao matajiri si ndio wanaowadhulumu na kuwaburuta mahakamani? 7 Je, si wao wanaolikufuru Jina lile lililo bora sana mliloitiwa?
-
32 Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. 33 Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. 34 Wala hapakuwepo mtu yeyote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, 35 wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.
-
10 Usitumainie vya udhalimu
wala usijivune kwa vitu vya wizi;
ingawa utajiri wako utaongezeka,
usiviwekee moyo wako.
-
9 Mheshimu Bwana kwa mali zako na
kwa malimbuko ya mazao yako yote;
10 ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika,
viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya.
-
23 Hakikisha kuwa unajua hali ya makundi yako
ya kondoo na mbuzi,
angalia kwa bidii ngʼombe zako.
24 Kwa kuwa utajiri haudumu milele,
nayo taji haidumu vizazi vyote.
-
6 Wenye haki wataona na kuogopa,
watamcheka, wakisema,
7 “Huyu ni yule mtu ambaye
hakumfanya Mungu kuwa ngome yake,
bali alitumainia wingi wa utajiri wake,
na akawa hodari kwa kuwaangamiza wengine!”
-
19 Zaidi ya yote, Mungu anapompa mtu yeyote utajiri na milki, humwezesha kuvifurahia, kukubali fungu lake na kuwa na furaha katika kazi yake, hii ni karama ya Mungu. 20 Mara chache mtu huzifikiri siku za maisha yake, kwa sababu Mungu humfanya ashikwe na furaha ya moyoni.
-
31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia.
-
1 Hivyo Abramu akakwea kutoka Misri kwenda Negebu, yeye na mkewe na kila kitu alichokuwa nacho, pia Loti akaenda pamoja naye. 2 Wakati huo Abramu alikuwa tajiri sana wa mifugo, fedha na dhahabu.
-
7 Bwana humfanya mtu maskini naye hutajirisha,
hushusha na hukweza.
-
4 Utajiri haufaidi kitu katika siku ya ghadhabu,
bali haki huokoa kutoka mautini.
-
16 Yeye amwoneaye maskini ili kujiongezea mali,
naye ampaye tajiri zawadi, wote huwa maskini.
-
1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, mwambie mfalme wa Tiro, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:
“ ‘Kwa sababu moyo wako umejivuna
na umesema, “Mimi ni mungu;
nami ninaketi katika kiti cha enzi cha mungu
katika moyo wa bahari.”
Lakini wewe ni mwanadamu, wala si mungu,
ingawa unafikiri kuwa una hekima kama mungu.
3 Je, wewe una hekima kuliko Danieli?
Je, hakuna siri iliyofichika kwako?
4 Kwa hekima yako na ufahamu wako,
umejipatia utajiri,
nawe umejikusanyia dhahabu
na fedha katika hazina zako.
5 Kwa werevu wako mwingi katika biashara,
umeongeza utajiri wako
na kwa sababu ya utajiri wako
moyo wako umekuwa na kiburi.
6 “ ‘Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:
“ ‘Kwa sababu unafikiri una hekima,
mwenye hekima kama mungu,
7 mimi nitawaleta wageni dhidi yako,
taifa katili kuliko yote;
watafuta panga zao dhidi ya uzuri wa hekima yako,
na kuchafua fahari yako inayongʼaa.
8 Watakushusha chini shimoni,
nawe utakufa kifo cha kikatili
katika moyo wa bahari.
9 Je, wakati huo utasema, “Mimi ni mungu,”
mbele ya wale wanaokuua?
Utakuwa mwanadamu tu, wala si mungu,
mikononi mwa hao wanaokuua.
10 Utakufa kifo cha wasiotahiriwa
kwa mkono wa wageni.
Kwa kuwa mimi nimenena, asema Bwana Mwenyezi.’ ”
-
22 Ile mbegu iliyopandwa katika miiba ni yule mtu alisikiaye neno, lakini masumbufu ya maisha haya na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno na kulifanya lisizae matunda.
-
57 Ilipofika jioni, alifika mtu mmoja tajiri kutoka Arimathaya aitwaye Yosefu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu. 58 Akamwendea Pilato ili kumwomba mwili wa Yesu. Pilato akaamuru apewe. 59 Yosefu akauchukua mwili wa Yesu, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi, 60 na kuuweka katika kaburi lake mwenyewe jipya, alilokuwa amelichonga kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa katika ingilio la kaburi, akaenda zake.
-
5 Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,
“Kamwe sitakuacha,
wala sitakupungukia.”
6 Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,
“Bwana ni msaada wangu; sitaogopa.
Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”
-
17 Kwa maana unasema: ‘Mimi ni tajiri, nimejilimbikizia mali, wala sihitaji kitu chochote.’ Lakini hutambui ya kwamba wewe ni mnyonge, wa kuhurumiwa, maskini, kipofu, tena uliye uchi. 18 Nakushauri ununue kutoka kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, ili upate kuwa tajiri, na mavazi meupe ili uyavae upate kuficha aibu ya uchi wako, na mafuta ya kupaka macho yako ili upate kuona.
-
8 Uutenge mbali nami udanganyifu na uongo;
usinipe umaskini wala utajiri,
bali unipe chakula cha kunitosha kila siku.
9 Nisije nikawa na vingi vya kuzidi nikakukana
na kusema, ‘Bwana ni nani?’
Au nisije nikawa maskini nikaiba,
nami nikaliaibisha jina la Mungu wangu.
-
18 Mtawala mmoja akamuuliza Yesu, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
19 Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake. 20 Unazijua amri: ‘Usizini, usiue, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako.’ ”
21 Akajibu, “Amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”
22 Yesu aliposikia haya, akamwambia, “Bado kuna jambo moja ulilopungukiwa. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
23 Aliposikia jambo hili, alisikitika sana kwa maana alikuwa mtu mwenye mali nyingi. 24 Yesu akamtazama, akasema, “Tazama jinsi ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu! 25 Hakika ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”
26 Wale waliosikia haya wakauliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”
27 Yesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa wanadamu yanawezekana kwa Mungu.”
28 Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha vyote tulivyokuwa navyo tukakufuata!”
29 Yesu akajibu, “Amin, nawaambia, hakuna hata mtu aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu 30 ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya, na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.”
-
12 Isaki akapanda mazao katika nchi hiyo, kwa mwaka huo huo, akavuna mara mia, kwa sababu Bwana alimbariki. 13 Isaki akawa tajiri, mali zake zikaendelea kuongezeka mpaka akawa tajiri sana. 14 Akawa na mifugo ya kondoo na ngʼombe, na watumishi wengi sana, kiasi kwamba Wafilisti wakamwonea wivu.
-
22 Baraka ya Bwana hutajirisha,
wala haichanganyi huzuni.
-
22 Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi,
bali mali ya wenye dhambi imehifadhiwa
kwa ajili ya wenye haki.
23 Shamba la mtu maskini laweza kuzalisha chakula kingi,
bali dhuluma hukifutilia mbali.
-
6 Nyumba ya mwenye haki ina hazina kubwa,
bali mapato ya waovu huwaletea taabu.
-
17 Kwa sababu mnamwita Baba ahukumuye kila mtu kulingana na matendo yake pasipo upendeleo, enendeni kwa hofu ya kumcha Mungu wakati wenu wa kukaa hapa duniani kama wageni. 18 Kwa maana mnafahamu kwamba mlikombolewa kutoka mwenendo wenu usiofaa ambao mliurithi kutoka kwa baba zenu, si kwa vitu viharibikavyo kama fedha na dhahabu, 19 bali kwa damu ya thamani ya Kristo, yule Mwana-Kondoo asiye na dosari wala doa. 20 Yeye alichaguliwa kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu, lakini akadhihirishwa katika siku hizi za mwisho kwa ajili yenu. 21 Kupitia kwake mmemwamini Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu na akampa utukufu, ili imani yenu na tumaini lenu ziwe kwa Mungu.
-
4 “Ee Bwana, nijulishe mwisho wa maisha yangu
na hesabu ya siku zangu;
nijalie kujua jinsi maisha yangu
yanavyopita upesi.
5 Umefanya maisha yangu mafupi kama pumzi;
muda wangu wa kuishi ni kama
hauna thamani kwako.
Maisha ya kila mwanadamu
ni kama pumzi.
6 Hakika kila binadamu ni kama njozi
aendapo huku na huko:
hujishughulisha na mengi lakini ni ubatili;
anakusanya mali nyingi,
wala hajui ni nani atakayeifaidi.
-
6 “Je, watu wote hawatamsuta kwa dhihaka na kumbeza, wakisema,
“ ‘Ole wake yeye akusanyaye bidhaa zilizoibwa
na kujifanyia utajiri kwa kutoza kwa nguvu!
Ataendelea hivi kwa muda gani?’
7 Je, wadai wako hawatainuka ghafula?
Je, hawataamka na kukufanya utetemeke?
Kisha utakuwa mhanga kwao.
8 Kwa kuwa umeteka nyara mataifa mengi,
watu waliobaki watakuteka nyara wewe.
Kwa kuwa umemwaga damu ya mtu;
umeharibu nchi na miji, na kila mmoja ndani yake.
9 “Ole wake yeye ajengaye milki yake kwa mapato ya udhalimu,
awekaye kiota chake juu,
ili kukimbia makucha ya uharibifu!
10 Umefanya shauri la maangamizi ya watu wengi,
ukiaibisha nyumba yako mwenyewe, na kupotewa na maisha yako.
11 Mawe ya kuta yatapiga kelele,
na mihimili ya kazi ya mbao itarudisha mwangwi wake.
-
41 Kisha Yesu akaketi mkabala na sehemu ambapo sadaka zilikuwa zinawekwa na kuangalia umati wa watu wakiweka fedha zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. Matajiri wengi wakaweka kiasi kikubwa cha fedha. 42 Lakini mjane mmoja maskini akaja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba zenye thamani ya senti mbili.
43 Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka katika sanduku la hazina zaidi ya watu wengine wote. 44 Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali zao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake, akaweka kila kitu alichokuwa nacho, hata kile alichohitaji ili kuishi.”
-
13 “Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.”
-
6 Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu. 7 Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. 8 Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema.
-
9 Ndugu asiye na cheo kikubwa yampasa ajivunie hali hiyo maana ametukuzwa. 10 Lakini yeye aliye tajiri afurahi kwa kuwa ameshushwa, kwa sababu atatoweka kama ua la shambani. 11 Kwa maana jua kali lenye kuchoma huchomoza na kuliunguza, likayakausha majani, na ua lake likapukutika, nao uzuri wake huharibika. Vivyo hivyo tajiri naye atanyauka akiwa anaendelea na shughuli zake.
-
23 Hili ndilo asemalo Bwana:
“Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake,
au mwenye nguvu ajisifu katika nguvu zake,
wala tajiri ajisifu katika utajiri wake,
24 lakini yeye ajisifuye, na ajisifu kwa sababu hili:
kwamba ananifahamu na kunijua mimi,
kwamba mimi ndimi Bwana, nitendaye wema,
hukumu na haki duniani,
kwa kuwa napendezwa na haya,”
asema Bwana.
-
8 Efraimu hujisifu akisema,
“Mimi ni tajiri sana; nimetajirika.
Pamoja na utajiri wangu wote hawatakuta ndani yangu
uovu wowote au dhambi.”
-
19 “Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, ambaye aliishi kwa anasa kila siku. 20 Hapo penye mlango wake aliishi maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima. 21 Huyo Lazaro alitamani kujishibisha kwa makombo yaliyoanguka kutoka mezani kwa yule tajiri. Hata mbwa walikuwa wakija na kuramba vidonda vyake.
22 “Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Abrahamu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa. 23 Kule kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Abrahamu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa karibu yake. 24 Hivyo yule tajiri akamwita, ‘Baba Abrahamu, nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu.’
25 “Lakini Abrahamu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu. 26 Zaidi ya hayo, kati yetu na ninyi huko kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu yeyote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu.’
27 “Akasema, ‘Basi, nakuomba, umtume Lazaro aende nyumbani kwa baba yangu, 28 maana ninao ndugu watano. Awaonye, ili wasije nao wakafika mahali hapa pa mateso.’
29 “Abrahamu akamjibu, ‘Ndugu zako wana Maandiko ya Mose na Manabii, wawasikilize hao.’
30 “Yule tajiri akasema, ‘Hapana, baba Abrahamu, lakini mtu kutoka kwa wafu akiwaendea, watatubu.’
31 “Abrahamu akamwambia, ‘Kama wasipowasikiliza Mose na Manabii, hawataweza kushawishika hata kama mtu akifufuka kutoka kwa wafu.’ ”
-
9 Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri.
-
17 Nawapenda wale wanipendao,
na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.
18 Utajiri na heshima viko kwangu,
utajiri udumuo na mafanikio.
19 Tunda langu ni bora kuliko dhahabu safi;
kile nitoacho hupita fedha iliyo bora.
20 Natembea katika njia ya unyofu
katika mapito ya haki,
21 nawapa utajiri wale wanipendao
na kuzijaza hazina zao.
-
10 Je, bado nisahau, ee nyumba ya uovu,
hazina yako uliyopata kwa udanganyifu
na vipimo vilivyopunguka,
ambavyo vimelaaniwa?
11 Je, naweza kuhukumu kuwa
mtu mwenye mizani ya udanganyifu hana hatia,
aliye na mfuko wa mawe ya kupimia ya uongo?
12 Matajiri wake ni wajeuri;
watu wake ni waongo
na ndimi zao zinazungumza
kwa udanganyifu.
13 Kwa hiyo, nimeanza kukuharibu,
kuwaangamiza kwa sababu ya dhambi zenu.
-
14 Zile mbegu zilizoanguka kwenye miiba ni mfano wa wale wanaosikia, lakini wanapoendelea husongwa na masumbufu ya maisha haya, utajiri na anasa, nao hawakui.
-
1 Nataka mjue jinsi ninavyojitaabisha kwa ajili yenu na kwa ajili ya wale walioko Laodikia, na pia kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona mimi binafsi. 2 Kusudi langu ni watiwe moyo na kuunganishwa katika upendo, ili wapate ule utajiri wa ufahamu mkamilifu, ili waijue siri ya Mungu, yaani, Kristo mwenyewe, 3 ambaye ndani yake kumefichwa hazina zote za hekima na maarifa.
-
1 Kwa wazee waliomo miongoni mwenu, nawasihi mimi nikiwa mzee mwenzenu, shahidi wa mateso ya Kristo, na mshiriki katika utukufu utakaofunuliwa: 2 lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, kama Mungu anavyowataka mwe; si kwa tamaa ya fedha, bali mlio na bidii katika kutumika. 3 Msijifanye mabwana juu ya wale walio chini ya uangalizi wenu, bali kuweni vielelezo kwa hilo kundi.
-
11 Ukuu na uweza, ni vyako, Ee Bwana,
na utukufu na enzi na uzuri,
kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani
ni chako wewe.
Ee Bwana, ufalme ni wako;
umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote.
12 Utajiri na heshima vyatoka kwako;
wewe ndiwe utawalaye vitu vyote.
Mikononi mwako kuna nguvu na uweza
ili kuinua na kuwapa wote nguvu,
-
Sehemu Ya Kwanza: Habari Za Awali
1 Katika nchi ya Usi paliishi mtu ambaye aliitwa Ayubu. Mtu huyu alikuwa hana hatia, naye alikuwa mkamilifu; alimcha Mungu na kuepukana na uovu. 2 Alikuwa na wana saba na binti watatu, 3 naye alikuwa na kondoo elfu saba, ngamia elfu tatu, jozi mia tano za maksai, na punda mia tano, tena alikuwa na idadi kubwa ya watumishi. Alikuwa mtu mkuu sana miongoni mwa watu wa Mashariki.
-
16 Afadhali kuwa na kidogo pamoja na kumcha Bwana,
kuliko mali nyingi pamoja na ghasia.
17 Afadhali chakula cha mboga mahali palipo na upendo
kuliko nyama ya ndama iliyonona pamoja na chuki.
-
27 Mtu mwenye tamaa huletea jamaa yake taabu,
bali yeye achukiaye rushwa ataishi.
-
1 Heri kuchagua jina jema kuliko utajiri mwingi,
kuheshimiwa ni bora kuliko fedha au dhahabu.
-
11 Kama kware aanguaye mayai asiyoyataga,
ndivyo alivyo mtu apataye mali kwa njia zisizo za haki.
Maisha yake yafikapo katikati, siku zitamwacha,
na mwishoni atabainika kuwa mpumbavu.
-
4 Kwa nini unajivunia mabonde yako,
kujivunia mabonde yako yaliyozaa sana?
Ee binti usiye mwaminifu, unayeutumainia utajiri wako na kusema,
‘Ni nani atakayenishambulia?’
-
23 Kazi zote zinazofanywa kwa bidii huleta faida,
bali mazungumzo matupu huelekea umaskini tu.
-
6 Mali iliyopatikana kwa ulimi wa uongo
ni mvuke upitao upesi na mtego wa kufisha.
-
11 Mtu tajiri anaweza kuwa na hekima machoni pake mwenyewe,
bali mtu maskini mwenye ufahamu atamfichua.
-
26 Kwa yule mtu anayempendeza Mungu, Mungu humpa hekima, maarifa na furaha, bali kwa mwenye dhambi Mungu humpa kazi ya kukusanya na kuhifadhi utajiri ili Mungu ampe yule anayempenda. Hili nalo pia ni ubatili, ni kukimbiza upepo.
-
8 “Je, mwanadamu atamwibia Mungu? Hata hivyo mnaniibia mimi.
“Lakini mnauliza, ‘Tunakuibia kwa namna gani?’
“Mnaniibia zaka na dhabihu. 9 Mko chini ya laana, ninyi taifa lote, kwa sababu mnaniibia mimi. 10 Leteni zaka kamili ghalani, ili kuwe na chakula katika nyumba yangu. Nijaribuni katika hili,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, “nanyi mwone kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni na kuwamwagieni baraka nyingi mpaka mkose nafasi ya kutosha. 11 Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu, wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. 12 “Ndipo mataifa yote yatawaita mliobarikiwa, kwa maana nchi yenu itakuwa ya kupendeza sana,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
-
44 Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika. 45 Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.
-
1 Basi sasa ndugu, nataka ninyi mjue kuhusu ile neema ambayo Mungu amewapa makanisa ya Makedonia. 2 Pamoja na majaribu makali na taabu walizopata, furaha waliyokuwa nayo ilikuwa kubwa, ingawa walikuwa maskini kupindukia, kwa upande wao walifurika kwa wingi wa ukarimu. 3 Kwa maana nashuhudia kwamba wao walitoa kwa kadiri wawezavyo, hata na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe, 4 wakitusihi kwa bidii wapewe fursa ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watakatifu.
-
7 Ndani yake tunao ukombozi kwa njia ya damu yake, yaani, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake 8 aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote. 9 Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Kristo, 10 ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani, kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Kristo.
-
13 Basi sikilizeni ninyi msemao, “Leo au kesho tutakwenda katika mji huu ama ule tukae humo mwaka mmoja, tufanye biashara na kupata faida.” 14 Lakini hamjui hata litakalotukia kesho. Maisha yenu ni nini? Ninyi ni ukungu ambao huonekana kwa kitambo kidogo kisha hutoweka. 15 Badala yake, inawapasa kusema, “Kama Bwana akipenda, tutaishi na kufanya hili ama lile.” 16 Kama ilivyo sasa, mnajisifu na kujigamba. Kujisifu kwa namna hiyo ni uovu. 17 Basi mtu yeyote anayejua jema limpasalo kutenda, lakini asilitende, mtu huyo anatenda dhambi.
-
27 Hezekia alikuwa na utajiri mwingi sana na heshima, naye akajifanyia hazina kwa ajili ya fedha yake na dhahabu na kwa ajili ya vito vyake vya thamani, vikolezi, ngao na aina zote za vyombo vya thamani. 28 Akajenga pia maghala ya kuhifadhi mavuno ya nafaka, divai mpya na mafuta. Akatengeneza mabanda kwa ajili ya aina mbalimbali za mifugo, na mazizi kwa ajili ya kondoo na mbuzi. 29 Akajenga vijiji na kujipatia idadi kubwa ya kondoo na mbuzi, pamoja na ngʼombe kwa kuwa Mungu alikuwa amempa utajiri mwingi sana.
30 Ilikuwa ni Hezekia aliyeziba njia za kutolea maji za chemchemi za juu za Gihoni na kuyaelekeza maji kutiririkia upande wa magharibi wa Mji wa Daudi. Akafanikiwa katika kila kitu alichofanya. 31 Lakini wakati wajumbe walipotumwa na watawala wa Babeli kumuuliza juu ya ishara ambayo ilitokea katika nchi, Mungu alimwacha ili kumjaribu na kujua kila kitu kilichokuwa moyoni mwake.
32 Matukio mengine ya utawala wa Hezekia na matendo yake ya kujitoa kwa moyo yameandikwa katika maono ya nabii Isaya mwana wa Amozi kwenye kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.
-
16 Ajapokusanya fedha nyingi kama mavumbi,
na mavazi kama malundo ya udongo wa mfinyanzi,
17 yale yote mtu mwovu aliyojiwekea akiba, mwenye haki atayavaa,
naye asiye na hatia ataigawanya fedha yake.
-
1 Msifuni Bwana.
Heri mtu yule amchaye Bwana,
mtu yule apendezwaye sana na amri zake.
2 Watoto wake watakuwa wenye uwezo katika nchi,
kizazi cha watu waadilifu kitabarikiwa.
3 Nyumbani mwake kuna mali na utajiri,
haki yake hudumu milele.
-
2 Hazina zilizopatikana kwa njia mbaya hazifai,
lakini uadilifu huokoa kutoka mautini.
-
5 “Basi nitakuja karibu nanyi ili kuhukumu. Nami nitakuwa mwepesi kushuhudia dhidi ya wachawi, wazinzi, waapao kwa uongo, wanaopunja vibarua malipo yao, wanaowaonea wajane na yatima, na wanaowanyima wageni haki, lakini hawaniogopi mimi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
-
44 “Ufalme wa Mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba.”
45 “Tena, Ufalme wa Mbinguni unafanana na mfanyabiashara aliyekuwa akitafuta lulu safi. 46 Alipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua.”
-
24 “Lakini ole wenu ninyi mlio matajiri,
kwa sababu mmekwisha kupokea faraja yenu.
-
10 Yeye ampaye mpanzi mbegu kwa ajili ya kupanda na mkate kuwa chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu. 11 Mtatajirishwa kwa kila namna ili mpate kuwa wakarimu kila wakati, na kupitia kwetu, ukarimu wenu utamletea Mungu shukrani.
-
7 Nimekuwa mtumishi wa Injili hii kwa kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa nguvu yake itendayo kazi. 8 Ingawa mimi ni mdogo kuliko aliye mdogo kabisa miongoni mwa watakatifu wote, nilipewa neema hii: ili niwahubirie watu wa Mataifa kuhusu utajiri usiopimika ulio ndani ya Kristo, 9 na kuweka wazi kwa kila mtu siri hii iliyokuwa imefichwa tangu zamani katika Mungu, aliyeumba vitu vyote. 10 Ili sasa kwa njia ya Kanisa, hekima yote ya Mungu ipate kujulikana kwa watawala na wenye mamlaka katika ulimwengu wa roho, 11 sawasawa na kusudi lake la milele katika Kristo Yesu Bwana wetu. 12 Ndani yake na kwa njia ya imani katika yeye twaweza kumkaribia Mungu kwa uhuru na kwa ujasiri. 13 Kwa hiyo, nawaomba msikate tamaa kwa sababu ya mateso yangu kwa ajili yenu, hayo ni utukufu wenu.
-
23 Lolote mfanyalo, fanyeni kwa moyo kama watu wanaomtumikia Bwana, na si wanadamu, 24 kwa kuwa mnajua kwamba mtapokea urithi wenu kutoka kwa Bwana ukiwa thawabu yenu. Ni Bwana Yesu Kristo mnayemtumikia.
-
1 Hili ni neno la kuaminiwa, kwamba mtu akitamani kazi ya uangalizi, atamani kazi nzuri. 2 Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha, 3 asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha. 4 Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia. 5 (Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kanisa la Mungu?) 6 Asiwe mtu aliyeokoka karibuni asije akajivuna na kuangukia kwenye hukumu ile ile ya ibilisi. 7 Inampasa pia awe na sifa njema kwa watu walio nje, ili asije akalaumiwa na kuanguka kwenye mtego wa ibilisi.
-
8 Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini.
-
17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo?
-
25 “Kama ukimkopesha mmojawapo wa watu wangu fedha ambaye ni mhitaji, usiwe kama mtu mkopesha fedha; usimtoze riba.
-
13 “ ‘Usimdhulumu wala kumwibia jirani yako.
“ ‘Usishikilie mshahara wa kibarua usiku kucha hadi asubuhi.
-
11 Mungu akamwambia Solomoni, “Kwa kuwa jambo hili ndilo shauku ya moyo wako na hukuomba mali, utajiri au heshima, wala kifo kwa ajili ya adui zako, nawe kwa kuwa hukuomba maisha marefu, bali umeomba hekima na maarifa ili kuongoza watu wangu ambao nimekufanya uwe mfalme juu yao, 12 kwa hiyo utapewa hekima na maarifa. Tena nitakupa pia mali, utajiri na heshima, ambavyo hakuna mfalme yeyote aliyekuwepo kabla yako amewahi kuwa navyo, na hakuna yeyote baada yako atakayekuwa navyo.”
-
3 Bwana hawaachi waadilifu kukaa njaa,
lakini hupinga tamaa ya mtu mwovu.
4 Mikono mivivu hufanya mtu kuwa maskini
lakini mikono yenye bidii huleta utajiri.
-
8 Yeye aongezaye utajiri wake kwa riba kubwa mno
hukusanya kwa ajili ya mwingine,
ambaye atawahurumia maskini.
-
26 Kwa maana, je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?
-
8 Lakini Zakayo akasimama na kumwambia Bwana, “Tazama, Bwana! Sasa hivi nusu ya mali yangu ninawapa maskini, nami kama nimemdhulumu mtu yeyote kitu chochote, nitamrudishia mara nne ya hicho kiwango.”
-
15 Kwa sababu hii, tangu niliposikia juu ya imani yenu katika Bwana Yesu na upendo wenu kwa watakatifu wote, 16 sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, nikiwakumbuka katika maombi yangu. 17 Nazidi kumwomba Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awajalieni ninyi roho ya hekima na ya ufunuo, ili mpate kumjua zaidi. 18 Ninaomba pia kwamba macho ya mioyo yenu yatiwe nuru ili mpate kujua tumaini mliloitiwa, utajiri wa urithi wa utukufu wake kwa watakatifu 19 na uweza wake mkuu usiolinganishwa kwa ajili yetu sisi tuaminio. Uweza huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na ile nguvu kuu mno 20 aliyoitumia katika Kristo alipomfufua kutoka kwa wafu, na akamketisha mkono wake wa kuume huko mbinguni, 21 juu sana kuliko falme zote na mamlaka, enzi na milki, na juu ya kila jina litajwalo, si katika ulimwengu huu tu, bali katika ule ujao pia. 22 Naye Mungu ameweka vitu vyote viwe chini ya miguu yake na amemfanya yeye awe kichwa cha vitu vyote kwa ajili ya Kanisa, 23 ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake yeye aliye yote katika yote.
-
15 Msiupende ulimwengu wala mambo yaliyo ulimwenguni. Kama mtu yeyote akiupenda ulimwengu, upendo wa Baba haumo ndani yake. 16 Kwa maana kila kitu kilichomo ulimwenguni, yaani tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima, havitokani na Baba bali hutokana na ulimwengu. 17 Nao ulimwengu unapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu milele.
-
16 Kesho yake asubuhi na mapema Yoshua akawaamuru Israeli kuja mbele kabila kwa kabila; na Yuda akatwaliwa. 17 Koo za Yuda zikaja mbele, naye akawatwaa Wazera. Akaamuru ukoo wa Wazera kuja mbele jamaa kwa jamaa, nayo jamaa ya Zabdi ikatwaliwa. 18 Yoshua akaamuru watu wa jamaa ya Zabdi kuja mbele mtu kwa mtu, naye Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, akatwaliwa.
19 Ndipo Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, mtukuze Bwana, Mungu wa Israeli, nawe ukiri kwake. Niambie ni nini ulichotenda; usinifiche.”
20 Akani akamjibu Yoshua, “Ni kweli! Nimetenda dhambi dhidi ya Bwana, Mungu wa Israeli. Hili ndilo nililofanya: 21 Nilipoona katika nyara joho zuri la kutoka Babeli, shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu ya uzito wa shekeli hamsini, nikavitamani na nikavichukua. Tazama, vimefichwa ardhini ndani ya hema langu, pamoja na hiyo fedha chini yake.”
22 Kwa hiyo Yoshua akatuma wajumbe, nao wakapiga mbio mpaka hemani, tazama, vile vitu vilikuwa vimefichwa hemani mwake, pamoja na ile fedha chini yake. 23 Wakavichukua vile vitu toka mle hemani, wakamletea Yoshua pamoja na Waisraeli wote, na wakavitandaza mbele za Bwana.
24 Basi Yoshua, pamoja na Israeli yote, wakamchukua Akani mwana wa Zera, pamoja na ile fedha, lile joho, ile kabari ya dhahabu, wanawe na binti zake, ngʼombe, punda na kondoo wake, hema yake pamoja na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta katika Bonde la Akori. 25 Yoshua akasema, “Kwa nini umeleta taabu hii juu yetu? Bwana ataleta taabu juu yako leo hii.”
Ndipo Israeli yote ikampiga Akani kwa mawe, na baada ya kuwapiga jamaa yake yote kwa mawe, wakawateketeza kwa moto.
-
7 Mtu mmoja hujifanya tajiri, kumbe hana chochote;
mwingine hujifanya maskini, kumbe ana utajiri mwingi.
8 Utajiri wa mtu waweza kukomboa maisha yake,
bali mtu maskini hasikii kitisho.
-
23 Mtu maskini huomba kuhurumiwa
bali tajiri hujibu kwa ukali.
-
8 Kulikuwepo mwanadamu aliye peke yake,
hakuwa na mwana wala ndugu.
Hapakuwa na mwisho wa kazi yake,
hata hivyo macho yake
hayakutosheka na utajiri wake.
Aliuliza, “Ninajitaabisha hivi kwa ajili ya nani,
nami kwa nini ninajinyima kufurahia?”
Hili pia ni ubatili,
ni shughuli yenye taabu!
-
36 Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake?
-
1 Bwana akawa amemwambia Abramu, “Ondoka kutoka nchi yako, uache jamii yako na nyumba ya baba yako, uende hadi nchi nitakayokuonyesha.
2 “Mimi nitakufanya taifa kubwa
na nitakubariki,
Nitalikuza jina lako,
nawe utakuwa baraka.
3 Nitawabariki wale wanaokubariki,
na yeyote akulaaniye nitamlaani;
na kupitia kwako mataifa yote duniani
yatabarikiwa.”
-
22 Mfalme Solomoni alikuwa mkuu zaidi kwa utajiri na hekima kuliko wafalme wote wa dunia.
-
22 “Uliwapa falme na mataifa, ukiwagawia hata mipaka ya mbali. Wakaimiliki nchi ya Sihoni mfalme wa Heshboni, na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani. 23 Uliwafanya wana wao kuwa wengi kama nyota za angani, nawe ukawaleta katika nchi ambayo uliwaambia baba zao kuingia na kuimiliki. 24 Wana wao wakaingia na kuimiliki nchi. Uliwatiisha Wakanaani mbele yao, walioishi katika nchi, ukawatia Wakanaani mikononi mwao, pamoja na wafalme wao na watu wa nchi, wawafanyie kama wapendavyo. 25 Wakateka miji yenye ngome na nchi yenye rutuba, wakamiliki nyumba zilizojazwa na vitu vizuri vya kila aina, visima vilivyochimbwa tayari, mashamba ya mizabibu, mashamba ya mizeituni na miti yenye matunda kwa wingi. Wakala, wakashiba nao wakanawiri sana, wakajifurahisha katika wema wako mwingi.
26 “Lakini hawakukutii nao wakaasi dhidi yako, wakatupa sheria zako nyuma yao. Wakawaua manabii wako, waliowaonya ili wakurudie, na wakafanya makufuru makubwa. 27 Hivyo ukawatia mikononi mwa adui zao, ambao waliwatesa. Lakini walipoteswa, wakakulilia wewe. Kutoka mbinguni uliwasikia, nawe kwa huruma zako kuu ukawapa waokozi, waliowaokoa kutoka mikononi mwa adui zao.
28 “Lakini mara walipokuwa na raha, wakafanya maovu tena machoni pako. Kisha ukawaacha mikononi mwa adui zao, nao wakawatawala. Walipokulilia tena, ukasikia kutoka mbinguni, na kwa huruma zako ukawaokoa kila mara.
29 “Ukawaonya warudi katika sheria yako, lakini wakawa na kiburi na hawakutii amri zako. Wakatenda dhambi dhidi ya maagizo yako ambayo kwayo mtu ataishi kama akiyatii. Kwa ukaidi wakakugeuzia kisogo, wakawa na shingo ngumu na wakakataa kusikiliza. 30 Kwa miaka mingi ulikuwa mvumilivu kwao. Kwa njia ya Roho wako ukawaonya kupitia manabii wako. Hata hivyo hawakujali, basi ukawatia mikononi mwa mataifa jirani. 31 Lakini kwa rehema zako kuu hukuwakomesha wala kuwaacha, kwa kuwa wewe ni Mungu mwenye neema na rehema.
-
20 Mtu mwaminifu atabarikiwa sana,
bali yeye atamaniye kupata utajiri kwa haraka
hataacha kuadhibiwa.
21 Kuonyesha upendeleo si vizuri,
hata hivyo mtu atafanya kosa kwa kipande cha mkate.
22 Mtu mchoyo ana tamaa ya kupata utajiri,
naye hana habari kuwa umaskini unamngojea.
-
8 ‘Fedha ni mali yangu na dhahabu ni mali yangu,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
-
12 Watoza ushuru nao wakaja ili wabatizwe, wakamuuliza, “Bwana na sisi inatupasa tufanyeje?”
13 Akawaambia, “Msichukue zaidi ya kiwango mlichopangiwa.”
14 Askari nao wakamuuliza, “Je, nasi inatupasa tufanye nini?”
Akawaambia, “Msimdhulumu mtu wala msimshtaki mtu kwa uongo, bali mridhike na mishahara yenu.”
-
25 Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akapoteza au kuangamiza nafsi yake?
-
11 Walipokuwa wanasikiliza haya, Yesu akaendelea kuwaambia mfano, kwa sababu alikuwa anakaribia Yerusalemu na watu walikuwa wakidhani ya kuwa Ufalme wa Mungu ulikuwa unakuja saa iyo hiyo. 12 Hivyo akawaambia: “Mtu mmoja mwenye cheo kikubwa alisafiri kwenda nchi ya mbali ili akapokee madaraka ya kuwa mfalme, kisha arudi. 13 Hivyo akawaita kumi miongoni mwa watumishi wake, na akawapa kila mmoja fungu la fedha. Akawaambia, ‘Fanyeni biashara na fedha hizi mpaka nitakaporudi.’
14 “Lakini raiya wa nchi yake walimchukia wakapeleka ujumbe na kusema, ‘Hatutaki huyu mtu awe mfalme wetu.’
15 “Hata hivyo alirudi akiwa amekwisha kupokea mamlaka ya ufalme, akawaita wale watumishi wake aliokuwa amewaachia fedha, ili afahamu ni faida kiasi gani kila mmoja wao aliyopata kwa kufanya biashara.
16 “Wa kwanza akaja na kusema, ‘Bwana, kutokana na fedha uliyoniachia, nimepata faida mara kumi zaidi.’
17 “Yule bwana akamjibu, ‘Umefanya vizuri mtumishi mwema! Kwa sababu umekuwa mwaminifu katika wajibu mdogo sana, nakupa mamlaka juu ya miji kumi.’
18 “Wa pili naye akaja. Akasema, ‘Bwana, fedha yako imeleta faida mara tano zaidi.’
19 “Bwana wake akajibu, ‘Nakupa mamlaka juu ya miji mitano.’
20 “Kisha akaja yule mtumishi mwingine, akasema, ‘Bwana, hii hapa fedha yako. Niliitunza vizuri kwenye kitambaa. 21 Nilikuogopa, kwa sababu wewe ni mtu mgumu. Unachukua ambapo hukuweka kitu, na unavuna mahali ambapo hukupanda kitu.’
22 “Bwana wake akamjibu, ‘Nitakuhukumu kwa maneno yako mwenyewe, wewe mtumishi mwovu! Kama ulifahamu kwamba mimi ni mtu mgumu, nichukuaye mahali ambapo sikuweka kitu na kuvuna mahali ambapo sikupanda, 23 kwa nini basi hukuweka fedha zangu kwa watoa riba, ili nitakaporudi nichukue iliyo yangu na riba yake?’
24 “Ndipo akawaambia wale waliokuwa wamesimama karibu, ‘Mnyangʼanyeni fungu lake la fedha, mkampe yule mwenye kumi.’
25 “Wakamwambia, ‘Bwana, mbona; tayari anayo mafungu kumi!’
26 “Akawajibu, ‘Nawaambia kwamba kila aliye na kitu, ataongezewa. Lakini yule asiye na kitu, hata alicho nacho atanyangʼanywa. 27 Lakini wale adui zangu ambao hawakutaka mimi niwe mfalme juu yao. Waleteni hapa mkawaue mbele yangu.’ ”
-
6 Kwa sababu hii mnalipa kodi, kwa maana watawala ni watumishi wa Mungu, ambao hutumia muda wao wote kutawala. 7 Mlipeni kila mtu kile mnachodaiwa. Kama mnadaiwa kodi lipeni kodi, kama ni ushuru, lipeni ushuru, astahiliye hofu, mhofu, astahiliye heshima, mheshimu.
8 Msidaiwe kitu na mtu yeyote, isipokuwa kupendana, kwa maana yeye ampendaye mwenzake, ameitimiza sheria.
-
10 Walichotuomba ni kwamba tuendelee kuwakumbuka maskini, jambo ambalo ndilo nililokuwa na shauku ya kulifanya.
-
6 Ndugu, tunawaagiza katika Jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni na kila ndugu ambaye ni mvivu na ambaye haishi kufuatana na maagizo tuliyowapa. 7 Maana ninyi wenyewe mnajua jinsi iwapasavyo kufuata mfano wetu. Sisi hatukuwa wavivu tulipokuwa pamoja nanyi, 8 wala hatukula chakula cha mtu yeyote pasipo kukilipia. Badala yake tulifanya kazi kwa bidii usiku na mchana, ili tusimlemee mtu yeyote miongoni mwenu. 9 Tulifanya hivi, si kwa sababu hatukuwa na haki ya kupata msaada kama huo, bali ndio sisi wenyewe tuwe kielelezo. 10 Kwa maana hata tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwapa amri kwamba: “Mtu yeyote asiyetaka kufanya kazi, hata kula asile.”
11 Kwa kuwa tunasikia kwamba baadhi ya watu miongoni mwenu ni wavivu. Hawafanyi kazi bali hujishughulisha na mambo ya wengine. 12 Basi watu kama hao tunawaagiza na kuwahimiza katika Bwana Yesu Kristo, kwamba wafanye kazi kwa utulivu kwa ajili ya chakula chao wenyewe.
-
23 Kwa imani, wazazi wa Mose walimficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa, kwa sababu waliona kuwa si mtoto wa kawaida, wala hawakuiogopa amri ya mfalme.
24 Kwa imani, Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. 25 Akachagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha kwa anasa za dhambi kwa kitambo kidogo tu. 26 Aliona kushutumiwa kwa ajili ya Kristo ni utajiri mkubwa zaidi kuliko hazina za Misri, maana alikuwa anatazamia kupata thawabu baadaye. 27 Kwa imani Mose aliondoka Misri bila kuogopa ghadhabu ya mfalme. Alivumilia kwa sababu alimwona yeye asiyeonekana kwa macho. 28 Kwa imani akaadhimisha Pasaka na kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wazaliwa wa Israeli.
Shows Read in context, Share and Copy.