89 Bible Verses About Decision Making
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote
wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6 katika njia zako zote mkiri yeye,
naye atayanyoosha mapito yako.
7 Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe;
mche Bwana ukajiepushe na uovu.
8 Hii itakuletea afya mwilini mwako,
na mafuta kwenye mifupa yako.
-
2 Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3 kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. 4 Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu chochote. 5 Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa. 6 Lakini anapoomba, lazima aamini wala asiwe na shaka, kwa sababu mtu aliye na shaka ni kama wimbi la bahari, lililochukuliwa na upepo na kutupwa huku na huku. 7 Mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapata kitu chochote kutoka kwa Bwana.
-
13 Hivyo nikawapa ninyi nchi ambayo hamkuitaabikia na miji ambayo hamkuijenga na mnaishi ndani yake na kula toka kwa mashamba ya mizabibu na mizeituni msiyoipanda.’
14 “Sasa basi mcheni Bwana na kumtumikia kwa uaminifu wote. Itupeni mbali miungu ambayo baba zenu waliiabudu huko ngʼambo ya Mto Frati na huko Misri, nanyi mtumikieni Bwana. 15 Lakini msipoona vyema kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia, kama ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ngʼambo Frati, au miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Bwana.”
-
6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.
8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo. 9 Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.
-
28 Sasa basi, watoto wapendwa, kaeni ndani yake, ili atakapofunuliwa, tuwe na ujasiri, wala tusiaibike mbele zake wakati wa kuja kwake.
29 Kama mkijua kuwa yeye ni mwenye haki, mwajua kwamba kila atendaye haki amezaliwa naye.
-
31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia. 34 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.
-
26 Vivyo hivyo, Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa sababu hatujui kuomba ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa uchungu usioweza kutamkwa. 27 Naye Mungu aichunguzaye mioyo, anaijua nia ya Roho, kwa sababu Roho huwaombea watakatifu sawasawa na mapenzi ya Mungu.
28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. 29 Maana wale Mungu aliowajua tangu mwanzo, pia aliwachagua tangu mwanzo, wapate kufanana na mfano wa Mwanawe, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. 30 Nao wale Mungu aliotangulia kuwachagua, akawaita, wale aliowaita pia akawahesabia haki, nao wale aliowahesabia haki, pia akawatukuza.
-
4 Nionyeshe njia zako, Ee Bwana,
nifundishe mapito yako,
5 niongoze katika kweli yako na kunifundisha,
kwa maana wewe ni Mungu Mwokozi wangu,
nalo tumaini langu liko kwako wakati wote.
-
14 Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani, 15 na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. 16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, 17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.
-
1 Ni kitu gani kinachosababisha mapigano na ugomvi miongoni mwenu? Je, haya hayatokani na tamaa zenu zinazoshindana ndani yenu? 2 Mnatamani lakini hampati, kwa hiyo mwaua. Mwatamani kupata lakini hampati vile mnavyotaka, kwa hiyo mnajitia katika magomvi na mapigano. Mmepungukiwa kwa sababu hammwombi Mungu. 3 Mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya, ili mpate kuvitumia hivyo mtakavyopata kwa tamaa zenu.
4 Ninyi wanaume na wanawake wazinzi, hamjui ya kwamba urafiki na dunia ni uadui na Mungu? Kwa hiyo mtu yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hufanyika adui wa Mungu. 5 Au mwadhani kwamba Andiko lasema bure kuwa huyo Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu? 6 Lakini yeye hutupatia neema zaidi. Hii ndiyo sababu Andiko husema:
“Mungu huwapinga wenye kiburi,
lakini huwapa wanyenyekevu neema.”
7 Basi mtiini Mungu. Mpingeni ibilisi, naye atawakimbia. 8 Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu ninyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu ninyi wenye nia mbili. 9 Huzunikeni, ombolezeni na kulia. Kicheko chenu na kigeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa huzuni. 10 Jinyenyekezeni mbele za Bwana, naye atawainua.
11 Ndugu, msineneane mabaya ninyi kwa ninyi. Mtu yeyote anayesema mabaya dhidi ya ndugu yake au kumhukumu anasema dhidi ya sheria na kuihukumu. Unapoihukumu sheria, basi huishiki sheria bali umekuwa hakimu wa kuihukumu hiyo sheria. 12 Yuko Mtoa sheria mmoja tu na yeye peke yake ndiye Hakimu, ndiye awezaye kuokoa au kuangamiza. Lakini wewe ni nani hata umhukumu jirani yako?
13 Basi sikilizeni ninyi msemao, “Leo au kesho tutakwenda katika mji huu ama ule tukae humo mwaka mmoja, tufanye biashara na kupata faida.” 14 Lakini hamjui hata litakalotukia kesho. Maisha yenu ni nini? Ninyi ni ukungu ambao huonekana kwa kitambo kidogo kisha hutoweka. 15 Badala yake, inawapasa kusema, “Kama Bwana akipenda, tutaishi na kufanya hili ama lile.” 16 Kama ilivyo sasa, mnajisifu na kujigamba. Kujisifu kwa namna hiyo ni uovu. 17 Basi mtu yeyote anayejua jema limpasalo kutenda, lakini asilitende, mtu huyo anatenda dhambi.
-
8 Ndipo nuru yako itajitokeza kama mapambazuko
na uponyaji wako utatokea upesi;
ndipo haki yako itakapokutangulia mbele yako,
na utukufu wa Bwana utakuwa mlinzi nyuma yako.
9 Ndipo utaita, naye Bwana atajibu,
utalia kuomba msaada,
naye atasema: Mimi hapa.
“Kama ukiiondoa nira ya udhalimu,
na kunyoosha kidole na kuzungumza maovu,
10 nanyi kama mkimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi zenu
na kutosheleza mahitaji ya walioonewa,
ndipo nuru yenu itakapongʼaa gizani,
nao usiku wenu utakuwa kama adhuhuri.
11 Bwana atakuongoza siku zote,
atayatosheleza mahitaji yako katika nchi kame,
naye ataitia nguvu mifupa yako.
Utakuwa kama bustani iliyonyweshwa vizuri,
kama chemchemi ambayo maji yake hayakauki kamwe.
-
13 Atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza awatie katika kweli yote. Yeye hatanena kwa ajili yake mwenyewe, bali atanena yale yote atakayosikia, naye atawaonyesha mambo yajayo. 14 Atanitukuza mimi, kwa maana atayachukua yaliyo yangu na kuwajulisha ninyi. 15 Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu. Ndiyo maana nimesema Roho atachukua yaliyo yangu na kuwajulisha ninyi.
-
1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.
-
15 Tazama, naweka mbele yako leo uzima na mafanikio, mauti na maangamizo. 16 Ninakuamuru leo kwamba umpende Bwana Mungu wako, utembee katika njia zake, na kutunza maagizo yake, amri na sheria zake; ndipo utakapoishi na kuongezeka, naye Bwana Mungu wako atakubariki katika nchi unayoingia kuimiliki.
17 Lakini kama moyo wako ukigeukia mbali ukawa huna utii, kama umevutwa kuisujudia miungu mingine na kuiabudu, 18 nakutangazia leo hii kwamba hakika utaangamizwa. Hutaishi maisha marefu katika nchi unayovuka Yordani kuiingia na kuimiliki.
19 Leo ninaziita mbingu na nchi kama mashahidi dhidi yako kwamba nimeweka mbele yako uzima na mauti, baraka na laana. Basi sasa chagueni uzima, ili wewe na watoto wako mpate kuishi, 20 na ili upate kumpenda Bwana Mungu wako, uisikilize sauti yake na kuambatana naye. Kwa kuwa Bwana ndiye uzima wako, na atakupa wingi wa siku ili upate kuishi katika nchi aliyoapa kuwapa baba zako Abrahamu, Isaki na Yakobo.
-
1 Mwanangu, kama utayakubali maneno yangu
na kuyaweka akiba maagizo yangu ndani mwako,
2 kutega sikio lako kwenye hekima
na kuweka moyo wako katika ufahamu,
3 na kama ukiita busara
na kuita kwa sauti ufahamu,
4 na kama utaitafuta kama fedha
na kuitafuta sana kama hazina iliyofichwa,
5 ndipo utakapoelewa kumcha Bwana
na kupata maarifa ya Mungu.
6 Kwa maana Bwana hutoa hekima,
na kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.
-
26 Kwa hiyo Mose akasimama kwenye ingilio la kambi, akasema, “Yeyote aliye upande wa Bwana, aje upande wangu.” Walawi wote wakamjia.
-
8 Hivyo Abramu akamwambia Loti, “Pasiwe na ugomvi wowote kati yangu na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wako, kwa kuwa sisi ni ndugu. 9 Je, nchi yote haiko mbele yako? Tutengane. Kama ukielekea kushoto, nitakwenda kulia; kama ukielekea kulia, mimi nitakwenda kushoto.”
10 Loti akatazama akaona lile bonde lote la Yordani kuwa lilikuwa na maji tele, kama bustani ya Bwana, kama nchi ya Misri, kuelekea Soari. (Hii ilikuwa kabla Bwana hajaharibu Sodoma na Gomora.) 11 Hivyo Loti akajichagulia bonde lote la Yordani, akaelekea upande wa mashariki. Watu hao wawili wakatengana:
-
8 Asubuhi uniletee neno la upendo wako usiokoma,
kwa kuwa nimeweka tumaini langu kwako.
Nionyeshe njia nitakayoiendea,
kwa kuwa kwako nainua nafsi yangu.
-
15 “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu. 16 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele. 17 Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye anakaa ndani yenu.
-
31 Basi, lolote mfanyalo, kama ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.
-
16 Furahini siku zote; 17 ombeni bila kukoma; 18 shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.
19 Msiuzime moto wa Roho Mtakatifu; 20 msiyadharau maneno ya unabii. 21 Jaribuni kila kitu. Yashikeni yaliyo mema. 22 Jiepusheni na uovu wa kila namna.
-
24 Kwa imani, Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. 25 Akachagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha kwa anasa za dhambi kwa kitambo kidogo tu. 26 Aliona kushutumiwa kwa ajili ya Kristo ni utajiri mkubwa zaidi kuliko hazina za Misri, maana alikuwa anatazamia kupata thawabu baadaye.
-
21 Eliya akasimama mbele ya watu na kusema, “Mtasitasita katika mawazo mawili hadi lini? Ikiwa Bwana ndiye Mungu, mfuateni yeye; lakini ikiwa Baali ni Mungu, basi mfuateni yeye.”
Lakini watu hawakusema kitu.
-
26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
-
Zaburi ya Daudi.
1 Bwana ndiye mchungaji wangu,
sitapungukiwa na kitu.
2 Hunilaza katika malisho
ya majani mabichi,
kando ya maji matulivu huniongoza,
3 hunihuisha nafsi yangu.
Huniongoza katika njia za haki
kwa ajili ya jina lake.
4 Hata kama nikipita katikati
ya bonde la uvuli wa mauti,
sitaogopa mabaya,
kwa maana wewe upo pamoja nami;
fimbo yako na mkongojo wako
vyanifariji.
5 Waandaa meza mbele yangu
machoni pa adui zangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
kikombe changu kinafurika.
6 Hakika wema na upendo vitanifuata
siku zote za maisha yangu,
nami nitakaa nyumbani mwa Bwana
milele.
-
7 Sheria ya Bwana ni kamilifu,
ikihuisha nafsi.
Shuhuda za Bwana ni za kuaminika,
zikimpa mjinga hekima.
8 Maagizo ya Bwana ni kamili,
nayo hufurahisha moyo.
Amri za Bwana huangaza,
zatia nuru machoni.
9 Kumcha Bwana ni utakatifu,
nako kwadumu milele.
Amri za Bwana ni za hakika,
nazo zina haki.
10 Ni za thamani kuliko dhahabu,
kuliko dhahabu iliyo safi sana,
ni tamu kuliko asali,
kuliko asali kutoka kwenye sega.
11 Kwa hizo mtumishi wako anaonywa,
katika kuzishika kuna thawabu kubwa.
-
104 Ninapata ufahamu kutoka mausia yako,
kwa hiyo ninachukia kila njia ya upotovu.
105 Neno lako ni taa ya miguu yangu
na mwanga katika njia yangu.
-
38 Ikawa Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakienda Yerusalemu, akaingia kwenye kijiji kimoja ambapo mwanamke mmoja aliyeitwa Martha alimkaribisha nyumbani kwake. 39 Martha alikuwa na mdogo wake aliyeitwa Maria, ambaye aliketi chini miguuni mwa Bwana akisikiliza yale aliyokuwa akisema. 40 Lakini Martha alikuwa akihangaika na maandalizi yote yaliyokuwa yafanyike. Martha akaja kwa Yesu na kumuuliza, “Bwana, hujali kwamba ndugu yangu ameniachia kazi zote mwenyewe? Basi mwambie anisaidie.”
41 Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, mbona unasumbuka na kuhangaika na mengi? 42 Lakini kunahitajika kitu kimoja tu. Maria amechagua kile kilicho bora, wala hakuna mtu atakayemwondolea.”
-
15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.
-
11 Ole wao! Kwa kuwa wanaifuata njia ya Kaini, wamekimbilia faida katika kosa la Balaamu na kuangamia katika uasi wa Kora.
12 Watu hawa ni dosari katika karamu zenu za upendo, wakila pamoja nanyi bila hofu, wakijilisha pasipo hofu. Wao ni mawingu yasiyokuwa na maji, yakichukuliwa na upepo, miti isiyo na matunda wakati wa mapukutiko, ambayo hunyauka, iliyokufa mara mbili na kungʼolewa kabisa. 13 Wao ni mawimbi makali ya bahari, yakitoa povu la aibu yao wenyewe, ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba waliowekewa milele.
14 Enoki, mtu wa saba kuanzia Adamu alitoa unabii kuhusu watu hawa, akisema: “Tazama, Bwana anakuja pamoja na maelfu kwa maelfu ya watakatifu wake, 15 ili kumhukumu kila mmoja na kuwapatiliza wote wasiomcha Mungu kwa matendo yao yote ya uasi waliyoyatenda, pamoja na maneno yote ya kuchukiza ambayo wenye dhambi wamesema dhidi yake.” 16 Watu hawa ni wenye kunungʼunika na wenye kutafuta makosa; wao hufuata tamaa zao mbaya, hujisifu kwa maneno makuu kuhusu wao wenyewe na kuwasifu mno watu wenye vyeo kwa ajili ya kujipatia faida.
17 Lakini ninyi wapenzi, kumbukeni yale mitume wa Bwana Yesu Kristo waliyonena zamani. 18 Kwa kuwa waliwaambia, “Siku za mwisho kutakuwa na watu wenye kudhihaki, watakaofuata tamaa zao wenyewe za upotovu.” 19 Hawa ndio watu wanaowagawa ninyi, wafuatao tamaa zao za asili, wala hawana Roho.
20 Lakini ninyi wapendwa, jijengeni katika imani yenu iliyo takatifu sana tena ombeni katika Roho Mtakatifu. 21 Jilindeni katika upendo wa Mungu mkitazamia kwa furaha rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo ili awalete katika uzima wa milele.
22 Wahurumieni walio na mashaka; 23 wengine waokoeni kwa kuwanyakua kutoka kwenye moto; nao wengine wahurumieni mkiwa na hofu, mkichukia hata vazi lenye mawaa na kutiwa unajisi na mwili.
24 Kwake yeye awezaye kuwalinda ninyi msianguke na kuwaleta mbele za utukufu wake mkuu bila dosari na kwa furaha ipitayo kiasi: 25 kwake yeye Mungu pekee Mwokozi wetu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu, utukufu, ukuu, uweza na mamlaka ni vyake tangu milele, sasa na hata milele! Amen.
-
9 Hivyo mpe mtumishi wako moyo wa ufahamu ili kutawala watu wako na kupambanua kati ya mema na mabaya. Kwa maana, ni nani awezaye kutawala watu wako hawa walio wengi hivi?”
10 Bwana akapendezwa kwamba Solomoni ameliomba jambo hili. 11 Basi Mungu akamwambia, “Kwa kuwa umeomba neno hili na hukuomba maisha marefu au upate utajiri kwa nafsi yako, wala adui zako wafe, bali umeomba ufahamu katika kutoa haki, 12 nitafanya lile uliloomba. Nitakupa moyo wa hekima na wa ufahamu, kiasi kwamba hajakuwepo mtu mwingine kama wewe, wala kamwe hatakuwepo baada yako. 13 Zaidi ya hayo, nitakupa yale ambayo hukuomba, yaani utajiri na heshima, ili kwamba maisha yako yote hapatakuwa na mtu kama wewe miongoni mwa wafalme. 14 Nawe kama ukienenda katika njia zangu na kutii sheria na amri zangu kama baba yako Daudi alivyofanya, nitakupa maisha marefu.”
-
14 Pasipo ushauri wa hekima taifa huanguka,
bali washauri wengi hufanya ushindi uwe wa hakika.
-
2 Hivyo Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake pamoja na wote waliokuwa naye, “Iondoeni miungu ya kigeni ile iliyoko katikati yenu, jitakaseni na mkabadilishe nguo zenu. 3 Kisha njooni, twende Betheli, mahali nitakapomjengea Mungu madhabahu, aliyenijibu katika siku ya shida yangu, ambaye amekuwa pamoja nami popote nilipokwenda.”
-
23 Ee Mungu, nichunguze, uujue moyo wangu,
nijaribu na ujue mawazo yangu.
24 Uone kama kuna njia iletayo machukizo ndani yangu,
uniongoze katika njia ya milele.
-
36 Yosefu, Mlawi kutoka Kipro, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake Mwana wa Faraja), 37 aliuza shamba alilokuwa nalo, akaleta hizo fedha alizopata na kuziweka miguuni pa mitume.
-
35 Ndipo alipowaambia wajumbe wa baraza, “Enyi watu wa Israeli, fikirini kwa uangalifu mnayotaka kuwatendea watu hawa. 36 Kwa maana wakati uliopita, aliinuka mtu mmoja jina lake Theuda, alijidai kuwa yeye ni mtu maarufu, akapata wafuasi wapatao 400 walioambatana naye. Lakini aliuawa, na wafuasi wake wote wakatawanyika, wakawa si kitu. 37 Baada yake, alitokea Yuda Mgalilaya wakati wa kuorodhesha watu, naye akaongoza kundi la watu kuasi. Yeye pia aliuawa, nao wafuasi wake wakatawanyika. 38 Kwa hiyo, kwa habari ya jambo hili nawashauri, jiepusheni na watu hawa. Waacheni waende zao! Kwa maana kama kusudi lao na shughuli yao imetokana na mwanadamu, haitafanikiwa. 39 Lakini ikiwa imetoka kwa Mungu, hamtaweza kuwazuia watu hawa. Badala yake mtajikuta mnapigana na Mungu.”
-
8 Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea;
nitakushauri na kukuangalia.
9 Usiwe kama farasi au nyumbu
wasio na akili,
ambao ni lazima waongozwe kwa lijamu na hatamu
la sivyo hawatakukaribia.
-
22 Mipango hushindwa kufanikiwa kwa ajili ya kukosa ushauri,
bali kukiwa na washauri wengi hufanikiwa.
-
18 Basi wanafunzi wa Yohana pamoja na Mafarisayo walikuwa wakifunga. Baadhi ya watu wakamjia Yesu na kumuuliza, “Mbona wanafunzi wa Yohana na wa Mafarisayo hufunga lakini wanafunzi wako hawafungi?”
19 Yesu akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wawezaje kufunga wakati angali pamoja nao? Wakati bwana arusi bado yuko pamoja nao, hawawezi kufunga. 20 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Siku hiyo ndipo watakapofunga.
21 “Hakuna mtu ashoneaye kiraka cha nguo mpya kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, kile kiraka kipya kitachanika kutoka ile nguo iliyochakaa, nayo itachanika zaidi. 22 Wala hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, ile divai mpya itavipasua hivyo viriba, nayo hiyo divai itamwagika na viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya.”
-
1 Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo:
Kwa wale ambao kwa njia ya haki ya Mungu na Mwokozi wetu Yesu Kristo mmepokea imani iliyo na thamani kama yetu:
2 Neema na amani iwe kwenu kwa wingi katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu.
3 Uweza wake wa uungu umetupatia mambo yote tunayohitaji kwa ajili ya uzima na uchaji wa Mungu, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. 4 Kwa sababu hiyo, ametukirimia ahadi zake kuu na za thamani kupitia mambo haya, ili kupitia hayo mpate kuwa washiriki wa asili ya uungu, na kuokoka kutoka upotovu ulioko duniani unaosababishwa na tamaa mbaya.
5 Kwa sababu hii hasa, jitahidini sana katika imani yenu kuongeza wema; na katika wema, maarifa; 6 katika maarifa, kiasi; katika kiasi, saburi; katika saburi, utauwa; 7 katika utauwa, upendano wa ndugu; na katika upendano wa ndugu, upendo. 8 Kwa maana haya yakiwa ndani yenu kwa wingi na kuzidi kuongezeka, yanawasaidia msikose bidii wala kutozaa matunda katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. 9 Lakini mtu yeyote asipokuwa na mambo haya haoni mbali, na ni kipofu, naye amesahau kule kutakaswa kutoka dhambi zake za zamani.
10 Kwa hiyo, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuuthibitisha wito wenu na uteule wenu. Kwa maana mkifanya hivyo, hamtajikwaa kamwe, 11 na mtajaliwa kwa ukarimu mwingi kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
-
4 Watu wa Daudi wakasema, “Hii ndiyo siku aliyonena Bwana akikuambia, ‘Nitamtia adui yako mikononi mwako ili wewe umtendee utakavyo.’ ” Basi Daudi akanyemelea bila kuonekana na kukata upindo wa joho la Sauli.
5 Baada ya hilo, dhamiri ya Daudi ikataabika kwa kukata upindo wa joho la Sauli. 6 Akawaambia watu wake, “Bwana na apishie mbali nisije nikafanya jambo kama hilo kwa bwana wangu, yeye ambaye ni mpakwa mafuta wa Bwana, au kuinua mkono wangu dhidi yake; kwani yeye ni mpakwa mafuta wa Bwana.” 7 Kwa maneno haya Daudi akawaonya watu wake na hakuwaruhusu wamshambulie Sauli. Naye Sauli akaondoka pangoni na kwenda zake.
-
16 Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, hatuhitaji kujitetea mbele zako kuhusu jambo hili. 17 Ikiwa tutatupwa ndani ya tanuru iwakayo moto, Mungu tunayemtumikia anaweza kutuokoa na moto, naye atatuokoa kutoka mkononi mwako, ee mfalme. 18 Lakini hata ikiwa hatatuokoa, ee mfalme, tunataka ufahamu kwamba, hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”
-
27 Ni kweli Herode na Pontio Pilato pamoja na watu wa Mataifa na Waisraeli, walikusanyika katika mji huu dhidi ya mwanao mtakatifu Yesu uliyemtia mafuta. 28 Wao wakafanya yale ambayo uweza wako na mapenzi yako yalikuwa yamekusudia yatokee tangu zamani.
-
6 Mwanamke alipoona ya kuwa tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula na la kupendeza macho, tena linatamanika kwa kujipatia hekima, basi akachuma katika matunda yake, akala, pia akampa mumewe, aliyekuwa pamoja naye, naye akala.
-
4 Ndipo neno la Bwana lilipomjia: “Mtu huyu hatakuwa mrithi wako, bali mwana atakayetoka katika viuno vyako mwenyewe ndiye atakayekuwa mrithi wako.” 5 Akamtoa nje na kusema, “Tazama juu kuelekea mbinguni na uhesabu nyota, kama hakika utaweza kuzihesabu.” Ndipo akamwambia, “Hivyo ndivyo uzao wako utakavyokuwa.”
6 Abramu akamwamini Bwana, naye kwake hili likahesabiwa kuwa haki.
-
19 Lakini Yosefu akawaambia, “Msiogope. Je, mimi ni badala ya Mungu? 20 Mlikusudia kunidhuru, lakini Mungu alikusudia mema, ili litimie hili linalofanyika sasa, kuokoa maisha ya watu wengi.
-
4 Sikia, ee Israeli: Bwana Mungu wako, Bwana ni mmoja. 5 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. 6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. 7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo. 8 Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako. 9 Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.
-
36 Gideoni akamwambia Mungu, “Kama utawaokoa Waisraeli kwa mkono wangu, kama ulivyoahidi: 37 tazama, nitaweka ngozi ya kondoo kwenye kiwanja cha kupuria nafaka, na kama utakuwepo umande juu ya ngozi tu, nayo ardhi yote ikiwa kavu, ndipo nitakapojua kuwa utaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema.” 38 Hivyo ndivyo ilivyotokea. Gideoni akaamka asubuhi na mapema kesho yake, akaikamua ile ngozi, umande ukatoka, maji ya kujaa bakuli.
39 Kisha Gideoni akamwambia Bwana, “Usinikasirikie. Ninaomba nifanye ombi moja lingine. Niruhusu nifanye jaribio jingine moja kwa ngozi hii. Wakati huu uifanye ngozi hii kavu na ardhi yote ifunikwe na umande.” 40 Usiku ule Mungu akafanya hivyo. Ngozi ile ilikuwa kavu, nayo ardhi yote ikafunikwa na umande.
-
4 Jambo moja ninamwomba Bwana,
hili ndilo ninalolitafuta:
niweze kukaa nyumbani mwa Bwana
siku zote za maisha yangu,
niutazame uzuri wa Bwana
na kumtafuta hekaluni mwake.
-
9 Mcheni Bwana enyi watakatifu wake,
kwa maana wale wamchao
hawapungukiwi na chochote.
10 Wana simba wenye nguvu
hutindikiwa na kuona njaa,
bali wale wamtafutao Bwana
hawatakosa kitu chochote kilicho chema.
11 Njooni, watoto wangu, mnisikilize,
nitawafundisha kumcha Bwana.
12 Yeyote kati yenu anayependa uzima
na kutamani kuziona siku nyingi njema,
13 basi auzuie ulimi wake na mabaya,
na midomo yake kutokana na kusema uongo.
14 Aache uovu, atende mema,
aitafute amani na kuifuatilia.
15 Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,
na masikio yake yako makini kusikiliza kilio chao.
-
13 Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake,
ndivyo Bwana anavyowahurumia wale wanaomcha;
14 kwa kuwa anajua tulivyoumbwa,
anakumbuka kwamba sisi tu mavumbi.
-
9 Kijana aifanye njia yake kuwa safi jinsi gani?
Ni kwa kutii, akilifuata neno lako.
-
11 Nimelificha neno lako moyoni mwangu
ili nisikutende dhambi.
-
10 “Kumcha Bwana ndicho chanzo cha hekima,
na kumjua Aliye Mtakatifu ni ufahamu.
-
23 Hili ndilo asemalo Bwana:
“Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake,
au mwenye nguvu ajisifu katika nguvu zake,
wala tajiri ajisifu katika utajiri wake,
24 lakini yeye ajisifuye, na ajisifu kwa sababu hili:
kwamba ananifahamu na kunijua mimi,
kwamba mimi ndimi Bwana, nitendaye wema,
hukumu na haki duniani,
kwa kuwa napendezwa na haya,”
asema Bwana.
-
8 Lakini Danieli alikusudia kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme na divai, naye akamwomba mkuu wa maafisa ruhusa ili asijinajisi kwa njia hii.
-
8 Amekuonyesha yaliyo mema, ee mwanadamu.
Bwana anataka nini kwako?
Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema,
na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.
-
19 Yesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.” 20 Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.
-
13 “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.
14 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. 15 Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani ya ile nyumba. 16 Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
-
12 Kwa hiyo chochote mnachotaka mtendewe na watu, ninyi nanyi watendeeni vivyo hivyo. Kwa kuwa hii ndiyo Sheria na Manabii.
-
35 Mmoja wao, mtaalamu wa sheria, akamuuliza swali ili kumjaribu, akisema, 36 “Mwalimu, ni amri ipi katika Sheria iliyo kuu kuliko zote?”
37 Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’ 38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. 39 Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ 40 Amri hizi mbili ndizo msingi wa Sheria na Manabii.”
-
1 Yesu akaingia Yeriko, naye alikuwa anapita katikati ya huo mji. 2 Tazama, palikuwa na mtu mmoja mkuu wa watoza ushuru naye alikuwa tajiri, jina lake Zakayo. 3 Yeye alikuwa akijitahidi kumwona Yesu ni mtu wa namna gani. Lakini kutokana na umati mkubwa wa watu hakuweza kwa sababu alikuwa mfupi wa kimo. 4 Kwa hiyo akatangulia mbio mbele ya umati wa watu akapanda juu ya mkuyu ili amwone Yesu, kwa sababu angeipitia njia ile.
5 Yesu alipofika pale chini ya huo mkuyu, akatazama juu, akamwambia, “Zakayo, shuka upesi, kwa maana leo nitakuwa mgeni nyumbani kwako!” 6 Hivyo Zakayo akashuka upesi, akamkaribisha Yesu nyumbani kwake kwa furaha kubwa.
7 Watu wote walipoona hivyo, wakaanza kunungʼunika wakisema, “Amekwenda kuwa mgeni wa ‘mtu mwenye dhambi.’ ”
8 Lakini Zakayo akasimama na kumwambia Bwana, “Tazama, Bwana! Sasa hivi nusu ya mali yangu ninawapa maskini, nami kama nimemdhulumu mtu yeyote kitu chochote, nitamrudishia mara nne ya hicho kiwango.”
9 Ndipo Yesu akamwambia, “Leo, wokovu umeingia nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Abrahamu. 10 Kwa maana Mwana wa Adamu amekuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”
-
36 “Kwa hiyo Israeli wote na wajue jambo hili kwa uhakika kwamba: Mungu amemfanya huyu Yesu, ambaye ninyi mlimsulubisha, kuwa Bwana na Kristo.”
37 Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”
38 Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. 39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu, na kwa wote walio mbali, na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”
40 Petro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.” 41 Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa na siku ile waliongezeka watu wapatao 3,000.
-
19 “Kwa hivyo uamuzi wangu ni kwamba, tusiwataabishe watu wa Mataifa wanaomgeukia Mungu. 20 Badala yake, tuwaandikie kwamba wajiepushe na vyakula vilivyonajisiwa kwa kutolewa sanamu, wajiepushe na uasherati, au kula mnyama aliyenyongwa, na damu. 21 Kwa maana katika kila mji kwa vizazi vilivyopita, Mose amekuwa na wale wanaotangaza sheria yake kwa kuwa imekuwa ikisomwa kwa sauti kubwa katika masinagogi kila Sabato.”
22 Mitume na wazee pamoja na kanisa lote, wakaamua kuwachagua baadhi ya watu wao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Wakamchagua Yuda aitwaye Barsaba pamoja na Sila, watu wawili waliokuwa viongozi miongoni mwa ndugu.
-
28 Kwa maana imempendeza Roho Mtakatifu na sisi tusiwatwike mzigo wowote mkubwa zaidi ya mambo haya yafuatayo ambayo ni ya lazima: 29 Kwamba mjiepushe na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na mjiepushe na uasherati. Mkiyaepuka mambo haya, mtakuwa mmefanya vyema.
Kwaherini.
-
6 Paulo pamoja na wenzake wakasafiri sehemu za Frigia na Galatia, kwa kuwa Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kulihubiri neno huko Asia. 7 Walipofika mpaka wa Misia, wakajaribu kuingia Bithinia lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu. 8 Kwa hiyo wakapita Misia, wakafika Troa. 9 Wakati wa usiku Paulo akaona maono, mtu wa Makedonia amesimama akimsihi, “Vuka uje huku Makedonia utusaidie.” 10 Baada ya Paulo kuona maono haya, tulijiandaa kwa haraka kuondoka kwenda Makedonia tukiwa tumesadiki kuwa Mungu alikuwa ametuita kuhubiri habari njema huko.
-
25 Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. 26 Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka. 27 Yule mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza iko wazi, akachomoa upanga wake akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wote wametoroka. 28 Lakini Paulo akapiga kelele kwa sauti kubwa, akasema, “Usijidhuru kwa maana sisi sote tuko hapa!”
29 Yule askari wa gereza akaagiza taa ziletwe, akaingia ndani ya kile chumba cha gereza, akapiga magoti akitetemeka mbele ya Paulo na Sila. 30 Kisha akawaleta nje akisema, “Bwana zangu, nifanye nini nipate kuokoka?”
31 Wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu Kristo, nawe utaokoka, pamoja na watu wa nyumbani mwako.” 32 Wakamwambia neno la Bwana yeye pamoja na wote waliokuwako nyumbani mwake. 33 Wakati ule ule, yule mkuu wa gereza akawachukua, akawaosha majeraha yao, kisha akabatizwa yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake bila kuchelewa. 34 Akawapandisha nyumbani mwake akawaandalia chakula, yeye pamoja na nyumba yake yote wakafurahi sana kwa kuwa sasa walikuwa wamemwamini Mungu.
-
9 Kwa kuwa amri hizi zisemazo, “Usizini,” “Usiue,” “Usiibe,” “Usitamani,” na amri nyingine zote, zinajumlishwa katika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” 10 Upendo haumfanyii jirani jambo baya. Kwa hiyo upendo ndio utimilifu wa sheria.
-
15 Kwa kuwa nilikuwa na uhakika wa mambo haya, nilitaka nije kwenu kwanza, ili mpate faida mara mbili. 16 Nilipanga kuwatembelea nikiwa safarini kwenda Makedonia na kurudi tena kwenu nikitoka Makedonia, ili mnisafirishe katika safari yangu ya kwenda Uyahudi. 17 Nilipopanga jambo hili, je, nilikuwa kigeugeu? Au ninafanya mipango yangu kwa hali ya mwili, ili niseme, “Ndiyo, ndiyo” na “Siyo, siyo” wakati huo huo?
18 Hakika kama Mungu alivyo mwaminifu, maneno yetu kwenu hayajawa “Ndiyo na Siyo.” 19 Kwa kuwa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, ambaye tulimhubiri kwenu: Mimi, Silvano na Timotheo, hakuwa “Ndiyo” na “Siyo,” bali kwake yeye siku zote ni “Ndiyo.”
-
20 Nimesulubiwa pamoja na Kristo, wala si mimi tena ninayeishi, bali Kristo ndiye aishiye ndani yangu. Uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani ya Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu.
-
12 Kwa hiyo, wapenzi wangu, kama vile ambavyo mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwepo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka, 13 kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema.
-
10 Basi kulikuwako na njaa katika nchi, naye Abramu akashuka kwenda Misri kukaa huko kwa muda, kwa maana njaa ilikuwa kali. 11 Alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, “Ninajua ya kwamba wewe ni mwanamke mzuri wa sura. 12 Wakati Wamisri watakapokuona, watasema, ‘Huyu ni mke wake.’ Ndipo wataniua, lakini wewe watakuacha hai. 13 Sema wewe ni dada yangu, ili nitendewe mema kwa ajili yako, na maisha yangu yatahifadhiwa kwa sababu yako.”
-
1 Basi Sarai, mkewe Abramu, alikuwa hajamzalia watoto. Lakini alikuwa na mtumishi wa kike Mmisri jina lake Hagari, 2 hivyo Sarai akamwambia Abramu, “Bwana amenizuilia kupata watoto. Nenda, ukakutane kimwili na mtumishi wangu wa kike, huenda nitaweza kupata watoto kupitia kwake.”
Abramu akakubaliana na lile Sarai alilosema. 3 Hivyo baada ya Abramu kuishi katika nchi ya Kanaani miaka kumi, Sarai akamchukua mtumishi wake wa kike wa Kimisri, Hagari na kumpa mumewe awe mke wake.
-
1 Watu walipoona kuwa Mose amekawia sana kushuka kutoka mlimani, walimkusanyikia Aroni na kumwambia, “Njoo, tutengenezee miungu itakayotutangulia. Kwa maana huyu jamaa yetu Mose aliyetupandisha kutoka Misri, hatujui jambo lililompata.”
2 Aroni akawajibu, “Vueni vipuli vya dhahabu ambavyo wake zenu, wana wenu na binti zenu wamevaa, mkaniletee.” 3 Kwa hiyo watu wote wakavua vipuli vyao, wakavileta kwa Aroni. 4 Akavichukua vile vitu walivyomkabidhi, akavifanyiza kwa kusubu sanamu yenye umbo la ndama, akaichonga kwa kutumia chombo. Kisha wakasema, “Hii ndiyo miungu yenu, ee Israeli, iliyowapandisha kutoka Misri.”
-
12 Na sasa, ee Israeli, Bwana Mungu wako anataka nini kwako ila kumcha Bwana Mungu wako, kwenda katika njia zake, kumpenda na kumtumikia Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote, 13 na kuyashika maagizo ya Bwana na amri zake ninazokupa leo kwa mafanikio yako mwenyewe?
-
23 Lakini Gideoni akawaambia, “Mimi sitatawala juu yenu, wala wanangu hawatatawala juu yenu. Bwana ndiye atakayetawala juu yenu ninyi.” 24 Naye akasema, “Ninalo ombi moja, kwamba kila mmoja wenu anipatie kipuli kutoka kwenye fungu lake la nyara.” (Ilikuwa desturi ya Waishmaeli kuvaa vipuli vya dhahabu.)
25 Wakajibu, “Tutafurahi kuvitoa.” Hivyo wakatanda vazi chini na kila mwanaume akatupia juu yake pete kutoka kwenye fungu lake la nyara. 26 Uzito wa pete za dhahabu alizoomba zilifikia shekeli 1,700, bila kuhesabu mapambo mengine, pete za masikio na mavazi ya zambarau yaliyovaliwa na wafalme wa Midiani, au mikufu iliyokuwa kwenye shingo za ngamia zao. 27 Gideoni akatengeneza kisibau kwa kutumia ile dhahabu, ambacho alikiweka katika mji wake, yaani, Ofra. Waisraeli wote wakafanya uasherati kwa kukiabudu huko, nacho kikawa mtego kwa Gideoni na jamaa yake.
-
1 Katika mwanzo wa mwaka mpya, wakati wafalme watokapo kwenda vitani, Daudi akamtuma Yoabu pamoja na watu wa mfalme na jeshi lote la Israeli. Wakawaangamiza Waamoni na kuuzunguka kwa jeshi mji wa Raba. Lakini Daudi akabaki Yerusalemu.
2 Ikawa siku moja wakati wa jioni Daudi aliinuka kitandani mwake na kutembeatembea juu ya paa la jumba lake la kifalme. Kutokea kule kwenye paa, akamwona mwanamke akioga. Mwanamke huyo alikuwa mzuri sana wa sura, 3 naye Daudi akatuma mtu mmoja kuuliza habari za huyo mwanamke. Huyo mtu akamwambia Daudi, “Je, huyu si Bathsheba binti Eliamu, naye ni mke wa Uria, Mhiti?” 4 Ndipo Daudi akatuma wajumbe kumleta. Huyo mwanamke akaja kwa Daudi, Daudi akakutana naye kimwili. (Huyo mwanamke ndipo tu alikuwa amejitakasa kutoka siku zake za hedhi.) Kisha akarudi nyumbani kwake.
-
14 Tafuteni mema, wala si mabaya,
ili mpate kuishi.
Ndipo Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote atakuwa pamoja nanyi,
kama msemavyo yupo nanyi.
15 Yachukieni maovu, yapendeni mema;
dumisheni haki mahakamani.
Yamkini Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote
atawahurumia mabaki ya Yosefu.
-
1 Neno la Bwana lilimjia Yona mwana wa Amitai: 2 “Nenda katika mji mkubwa wa Ninawi ukahubiri juu yake, kwa sababu uovu wake umekuja juu mbele zangu.”
3 Lakini Yona alimkimbia Bwana na kuelekea Tarshishi. Alishuka mpaka Yafa, ambapo alikuta meli iliyokuwa imepangwa kuelekea bandari ile. Baada ya kulipa nauli, akapanda melini na kuelekea Tarshishi ili kumkimbia Bwana. 4 Ndipo Bwana akatuma upepo mkali baharini, nayo dhoruba kali sana ikavuma hata meli ikawa hatarini kuvunjika. 5 Mabaharia wote waliogopa na kila mmoja akamlilia mungu wake mwenyewe. Nao wakatupa mizigo baharini ili meli ipungue uzito.
Lakini Yona alikuwa ameteremkia chumba cha ndani ya meli, mahali ambapo alilala na kupatwa na usingizi mzito. 6 Nahodha akamwendea na kusema, “Wewe unawezaje kulala? Amka ukamwite mungu wako! Huenda akatuangalia, tusiangamie.”
-
31 “Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti cha enzi cha utukufu wake. 32 Mataifa yote watakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi. 33 Atawaweka kondoo upande wake wa kuume, na mbuzi upande wake wa kushoto.
34 “Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njooni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu; urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 35 Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, 36 nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’
37 “Ndipo wale wenye haki watakapomjibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha? 38 Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha, au ukiwa uchi tukakuvika? 39 Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza, au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’
40 “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’
41 “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. 42 Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, 43 nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza, na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’
44 “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’
45 “Naye atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’
46 “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”
-
14 Kisha mmojawapo wa wale kumi na wawili, aitwaye Yuda Iskariote, alikwenda kwa viongozi wa makuhani 15 na kuuliza, “Mtanipa nini nikimtia Yesu mikononi mwenu?” Wakamlipa vipande thelathini vya fedha. 16 Tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Yesu.
-
1 Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri pamoja dhidi ya Yesu ili kumuua. 2 Wakamfunga, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato, ambaye alikuwa mtawala wa Kirumi.
-
10 Kisha Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, akaenda kwa viongozi wa makuhani ili kumsaliti Yesu kwao. 11 Walifurahi sana kusikia jambo hili na wakaahidi kumpa fedha. Hivyo yeye akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti.
-
9 “Kwa hiyo nawaambia: Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango. 10 Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.
11 “Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba samaki, atampa nyoka badala yake? 12 Au mtoto akimwomba yai atampa nge? 13 Basi ikiwa ninyi mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wale wamwombao!”
-
16 Kisha akawaambia mfano huu: “Shamba la mtu mmoja tajiri lilizaa sana. 17 Akawaza moyoni mwake, ‘Nifanye nini? Sina mahali pa kuhifadhi mavuno yangu.’
18 “Ndipo huyo tajiri akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu za nafaka na kujenga nyingine kubwa zaidi na huko nitayahifadhi mavuno yangu yote na vitu vyangu. 19 Nami nitaiambia nafsi yangu, “Nafsi, unavyo vitu vingi vizuri ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi. Pumzika; kula, unywe, ufurahi.” ’
20 “Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe! Usiku huu uhai wako unatakiwa. Sasa hivyo vitu ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani?’
21 “Hivyo ndivyo ilivyo kwa wale wanaojiwekea mali lakini hawajitajirishi kwa Mungu.”
-
26 “Mtu yeyote anayekuja kwangu hawezi kuwa mwanafunzi wangu kama hatanipenda mimi zaidi ya baba yake na mama yake, mke wake na watoto wake, ndugu zake na dada zake, naam, hata maisha yake mwenyewe. 27 Yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
28 “Ni nani miongoni mwenu ambaye kama anataka kujenga nyumba, hakai kwanza chini na kufanya makisio ya gharama aone kama ana fedha za kutosha kukamilisha? 29 La sivyo, akiisha kuweka msingi, naye akiwa hana uwezo wa kuikamilisha, wote waionao wataanza kumdhihaki, 30 wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga lakini hakuweza kukamilisha.’
31 “Au ni mfalme gani atokaye kwenda kupigana vita na mfalme mwingine, ambaye hakai chini kwanza na kufikiri iwapo akiwa na jeshi la watu 10,000 ataweza kupigana na yule anayekuja na jeshi la watu 20,000? 32 Kama hawezi, basi wakati yule mwingine akiwa bado yuko mbali, yeye hutuma ujumbe wa watu na kuomba masharti ya amani.
-
1 Lakini mtu mmoja jina lake Anania pamoja na mkewe Safira waliuza kiwanja. 2 Huku mkewe akijua kikamilifu, Anania alificha sehemu ya fedha alizopata, akaleta kiasi kilichobaki na kukiweka miguuni pa mitume.
3 Petro akamuuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? 4 Je, kabla hujauza hicho kiwanja si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, fedha ulizopata si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu bali Mungu.”
5 Anania aliposikia maneno haya akaanguka chini na kufa. Hofu kuu ikawapata wote waliosikia jambo lililokuwa limetukia. 6 Vijana wakaja, wakaufunga mwili wake sanda, wakamchukua nje kumzika.
7 Saa tatu baadaye mkewe Anania akaingia, naye hana habari ya mambo yaliyotukia. 8 Petro akamuuliza, “Niambie, je, mliuza kiwanja kwa thamani hii?” Akajibu, “Ndiyo, tuliuza kwa thamani hiyo.”
9 Ndipo Petro akamwambia, “Imekuwaje mkakubaliana kumjaribu Roho wa Bwana? Tazama! Nyayo za vijana waliomzika mumeo ziko mlangoni, wewe nawe watakuchukua nje.”
10 Saa ile ile akaanguka chini miguuni mwake na kufa. Nao wale vijana wakaingia, wakamkuta amekufa, wakamchukua wakamzika kando ya mumewe. 11 Hofu kuu ikalipata kanisa lote pamoja na watu wote waliosikia juu ya matukio haya.
-
Mateso Na Kuenea Kwa Injili
1 Basi ikawa katika siku hizo, wakati idadi ya wanafunzi ilipokuwa ikiongezeka sana, palitokea manungʼuniko kati ya Wayahudi wa Kiyunani, dhidi ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahaulika katika mgawanyo wa chakula wa kila siku. 2 Wale mitume kumi na wawili wakakusanya wanafunzi wote pamoja wakasema, “Haitakuwa vyema sisi kuacha huduma ya neno la Mungu ili kuhudumu mezani. 3 Kwa hiyo ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, watu wenye sifa njema, waliojawa na Roho Mtakatifu na hekima, ambao tunaweza kuwakabidhi kazi hii, 4 nasi tutatumia muda wetu kuomba na huduma ya neno.”
-
14 Kisha wakalia tena kwa sauti. Orpa akambusu mama mkwe wake, akaenda zake, lakini Ruthu akaambatana naye.
15 Naomi akamwambia, “Tazama, mwenzako anarejea kwa watu wake na kwa miungu yake. Rudi pamoja naye.”
16 Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakokwenda nami nitakwenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. 17 Pale utakapofia nami nitafia hapo, na papo hapo nitazikwa. Bwana na aniadhibu vikali, kama kitu kingine chochote kitanitenga nawe isipokuwa kifo.” 18 Naomi alipotambua kwamba Ruthu amenuia kufuatana naye, hakuendelea kumsihi tena.
19 Kwa hiyo hao wanawake wawili wakaondoka, wakafika Bethlehemu. Walipofika Bethlehemu, mji mzima ulitaharuki, wanawake wakashangaa, wakasema, “Huyu aweza kuwa ni Naomi?”
20 Akawaambia, “Msiniite tena Naomi, niiteni Mara, kwa sababu Mwenyezi amenitendea mambo machungu sana. 21 Mimi niliondoka hali nimejaa, lakini Bwana amenirudisha mtupu. Kwa nini kuniita Naomi? Bwana amenitendea mambo machungu; Mwenyezi ameniletea msiba.”
22 Kwa hiyo Naomi alirudi pamoja na Ruthu Mmoabu mkwe wake, nao wakafika Bethlehemu mwanzoni mwa kuvuna shayiri.
Shows Read in context, Share and Copy.