111 Bible Verses About The Mind

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About The Mind
  1. 1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.

    3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa.

  2. 4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! 5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

    8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo. 9 Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.

  3. 1 Ndugu zangu nilipokuja kwenu, sikuja na maneno ya ushawishi wala hekima ya hali ya juu nilipowahubiria siri ya Mungu. 2 Kwa kuwa niliamua kutokujua kitu chochote wakati nikiwa nanyi isipokuwa Yesu Kristo aliyesulubiwa. 3 Mimi nilikuja kwenu nikiwa dhaifu na mwenye hofu na kwa kutetemeka sana. 4 Kuhubiri kwangu na ujumbe wangu haukuwa kwa hekima na maneno ya ushawishi bali kwa madhihirisho ya nguvu za Roho 5 ili imani yenu isiwe imejengwa katika hekima ya wanadamu bali katika nguvu za Mungu.

    6 Lakini miongoni mwa watu waliokomaa twanena hekima, wala si hekima ya ulimwengu huu au ya watawala wa dunia hii wanaobatilika. 7 Sisi tunanena hekima ya Mungu ambayo ni siri, tena iliyofichika, ambayo Mungu aliikusudia kabla ya ulimwengu kuwepo, kwa ajili ya utukufu wetu. 8 Hakuna hata mtawala mmoja wa nyakati hizi aliyeelewa jambo hili. Kwa maana kama wangelielewa, wasingemsulubisha Bwana wa utukufu. 9 Lakini ni kama ilivyoandikwa:

    “Hakuna jicho limepata kuona,

    wala sikio limepata kusikia,

    wala hayakuingia moyoni wowote,

    yale Mungu amewaandalia

    wale wampendao”:

    10 Lakini mambo haya Mungu ametufunulia kwa Roho wake.

    Roho huchunguza kila kitu, hata mambo ya ndani sana ya Mungu. 11 Kwa maana ni nani anayejua mawazo ya mtu isipokuwa roho iliyo ndani ya huyo mtu? Vivyo hivyo hakuna mtu ajuaye mawazo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu. 12 Basi hatukupokea roho ya dunia bali Roho atokaye kwa Mungu, ili tuweze kuelewa kile kipawa ambacho Mungu ametupatia bure. 13 Haya ndiyo tusemayo, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya wanadamu bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua kweli za kiroho kwa maneno ya kiroho. 14 Mtu ambaye hana Roho hawezi kupokea mambo yatokayo kwa Roho wa Mungu, kwa kuwa ni upuzi kwake, naye hawezi kuyaelewa kwa sababu hayo yanaeleweka tu kwa upambanuzi wa rohoni. 15 Mtu wa kiroho hubainisha mambo yote, lakini yeye mwenyewe habainishwi na mtu yeyote.

    16 “Kwa maana ni nani aliyefahamu mawazo ya Bwana

    ili apate kumfundisha?”

    Lakini sisi tunayo mawazo ya Kristo.

  4. 1 Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu, wale ambao hawaenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho. 2 Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima katika Kristo Yesu imeniweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti. 3 Kwa maana kile ambacho sheria haikuwa na uwezo wa kufanya, kwa vile ilivyokuwa dhaifu katika mwili, Mungu kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe kwa mfano wa mwanadamu mwenye mwili ulio wa dhambi na kwa ajili ya dhambi, yeye aliihukumu dhambi katika mwili, 4 ili kwamba haki ipatikanayo kwa sheria itimizwe ndani yetu sisi, ambao hatuenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho.

    5 Kwa maana wale wanaoishi kwa kuufuata mwili huziweka nia zao katika vitu vya mwili, lakini wale wanaoishi kwa kufuata Roho, huziweka nia zao katika mambo ya Roho. 6 Kwa maana kuwa na nia ya mwili ni mauti, bali kuwa na nia inayoongozwa na Roho ni uzima na amani. 7 Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui na Mungu, kwa maana haiitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. 8 Wale wanaotawaliwa na mwili, hawawezi kumpendeza Mungu.

    9 Lakini ninyi, hamtawaliwi na mwili, bali na Roho, ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu. Mtu yeyote ambaye hana Roho wa Kristo, yeye si wa Kristo. 10 Lakini kama Kristo anakaa ndani yenu, miili yenu imekufa kwa sababu ya dhambi, lakini roho zenu zi hai kwa sababu ya haki. 11 Nanyi ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu kutoka kwa wafu ataihuisha pia miili yenu ambayo hufa, kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu.

  5. 16 Mimi siionei haya Injili ya Kristo kwa maana ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, kwanza kwa Myahudi na kwa Myunani pia. 17 Kwa maana katika Injili haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa, haki ile iliyo kwa njia ya imani hadi imani. Kama ilivyoandikwa: “Mwenye haki ataishi kwa imani.”

    18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao, 19 kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao. 20 Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.

    21 Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza. 22 Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga 23 na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizofanywa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vitambaavyo.

    24 Kwa hiyo, Mungu akawaacha wazifuate tamaa mbaya za mioyo yao katika uasherati, hata wakavunjiana heshima miili yao wao kwa wao. 25 Kwa sababu waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakaabudu na kutumikia kiumbe badala ya Muumba, ahimidiwaye milele! Amen.

    26 Kwa sababu hii, Mungu aliwaacha wavunjiane heshima kwa kufuata tamaa zao za aibu. Hata wanawake wao wakabadili matumizi ya asili ya miili yao wakaitumia isivyokusudiwa. 27 Vivyo hivyo wanaume pia wakiacha matumizi ya asili ya wanawake wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wakafanyiana matendo ya aibu na wanaume wengine nao wakapata katika maisha yao adhabu iliyowastahili kwa ajili ya upotovu wao.

    28 Nao kwa kuwa hawakuona umuhimu wa kudumisha ufahamu wa Mungu, yeye akawaachilia wafuate akili za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa. 29 Wakiwa wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji, 30 wasingiziaji, wanaomchukia Mungu, wajeuri, wenye kiburi na majivuno, wenye hila, wasiotii wazazi wao, 31 wajinga, wasioamini, wasio na huruma na wakatili. 32 Ingawa wanafahamu sheria ya haki ya Mungu kwamba watu wanaofanya mambo kama hayo wanastahili mauti, si kwamba wanaendelea kutenda hayo tu, bali pia wanakubaliana na wale wanaoyatenda.

  6. 17 Hivyo nawaambia hivi, nami nasisitiza katika Bwana kwamba, msiishi tena kama watu wa Mataifa waishivyo, katika ubatili wa mawazo yao. 18 Watu hao akili zao zimetiwa giza na wametengwa mbali na uzima wa Mungu kwa sababu ya ujinga wao kutokana na ugumu wa mioyo yao. 19 Wakiisha kufa ganzi, wamejitia katika mambo ya ufisadi na kupendelea kila aina ya uchafu, wakiendelea kutamani zaidi.

    20 Lakini ninyi, hivyo sivyo mlivyojifunza Kristo. 21 Kama hivyo ndivyo ilivyo, ninyi mmemsikia, tena mmefundishwa naye, vile kweli ilivyo katika Yesu. 22 Mlifundishwa kuuvua mwenendo wenu wa zamani, utu wenu wa kale, ulioharibiwa na tamaa zake za udanganyifu, 23 ili mfanywe upya roho na nia zenu, 24 mkajivike utu mpya, ulioumbwa sawasawa na mfano wa Mungu katika haki yote na utakatifu.

  7. 1 Basi, kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo alikoketi mkono wa kuume wa Mungu. 2 Yafikirini mambo yaliyo juu, wala si ya duniani. 3 Kwa maana ninyi mlikufa, nao uhai wenu sasa umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. 4 Wakati Kristo, aliye uzima wenu, atakapotokea, ndipo nanyi mtakapotokea pamoja naye katika utukufu.

    5 Kwa hiyo, ueni kabisa chochote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: yaani uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na ulafi, ambayo ndiyo ibada ya sanamu. 6 Kwa sababu ya mambo haya, ghadhabu ya Mungu inakuja. 7 Ninyi pia zamani mlienenda katika mambo haya mlipoishi maisha hayo. 8 Lakini sasa yawekeni mbali nanyi mambo kama haya yote: yaani hasira, ghadhabu, uovu, masingizio na lugha chafu kutoka midomoni mwenu. 9 Msiambiane uongo, kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake, 10 nanyi mmevaa utu mpya, unaofanywa upya katika ufahamu sawasawa na mfano wa Muumba wake. 11 Hapa hakuna Myunani wala Myahudi, aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, asiyestaarabika wala aliyestaarabika, mtumwa wala mtu huru, bali Kristo ni yote, na ndani ya wote.

  8. 1 Basi, mimi Paulo ninawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Kristo, mimi niliye “mwoga” ninapokuwa pamoja nanyi ana kwa ana, lakini mwenye ujasiri nikiwa mbali nanyi! 2 Nawaomba nitakapokuja kwenu nisiwe na ujasiri dhidi ya watu fulani, kama ninavyotazamia kwa wale wanaodhani kwamba tunaishi kwa kufuata namna ya ulimwengu huu. 3 Ingawa tunaishi duniani, hatupigani vita kama ulimwengu ufanyavyo. 4 Silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome, 5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu, na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo, 6 tena tukiwa tayari kuadhibu kila tendo la kutotii, kutii kwenu kutakapokamilika.

    7 Angalieni yale yaliyo machoni penu. Kama mtu yeyote anaamini kuwa yeye ni mali ya Kristo, basi kumbuka kuwa kama ulivyo wa Kristo, vivyo hivyo na sisi ndivyo tulivyo.

  9. 1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, 2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. 3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.

    5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:

    6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,

    hakuona kule kuwa sawa na Mungu

    kuwa kitu cha kushikilia,

    7 bali alijifanya si kitu,

    akachukua hali hasa na mtumwa,

    naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.

    8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,

    alijinyenyekeza, akatii hata mauti:

    naam, mauti ya msalaba!

    9 Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana,

    na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina,

    10 ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe,

    la vitu vya mbinguni, na vya duniani,

    na vya chini ya nchi,

    11 na kila ulimi ukiri ya kwamba

    Yesu Kristo ni Bwana,

    kwa utukufu wa Mungu Baba.

    12 Kwa hiyo, wapenzi wangu, kama vile ambavyo mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwepo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka,

  10. 13 Kwa hiyo, tayarisheni nia zenu kwa kazi; mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa Yesu Kristo atakapodhihirishwa. 14 Kama watoto watiifu, msifuate tamaa zenu mbaya wakati mlipoishi kwa ujinga. 15 Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, nanyi kuweni watakatifu katika mwenendo wenu wote. 16 Kwa maana imeandikwa: “Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”

  11. 7 Tuseme nini basi? Kwamba sheria ni dhambi? La, hasha! Lakini, isingekuwa kwa sababu ya sheria, nisingalijua dhambi. Nisingalijua kutamani ni nini kama sheria haikusema, “Usitamani.” 8 Lakini dhambi kwa kupata nafasi katika amri, hii ikazaa ndani yangu kila aina ya tamaa. Kwa maana pasipo sheria, dhambi imekufa. 9 Wakati fulani nilikuwa hai pasipo sheria, lakini amri ilipokuja, dhambi ikawa hai, nami nikafa. 10 Nikaona kwamba ile amri iliyokusudiwa kuleta uzima, ilileta mauti. 11 Kwa maana dhambi kwa kupata nafasi katika amri, ilinidanganya, na kupitia katika hiyo amri, ikaniua. 12 Hivyo basi, sheria yenyewe ni takatifu, na amri ni takatifu na ya haki, tena ni njema.

    13 Je, kile kilicho chema basi kilikuwa mauti kwangu? La, hasha! Lakini ili dhambi itambuliwe kuwa ni dhambi, ilileta mauti ndani yangu kupitia kile kilichokuwa chema, ili kwa njia ya amri dhambi izidi kuwa mbaya kupita kiasi.

    14 Kwa maana tunajua kwamba sheria ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kimwili nikiwa nimeuzwa kwenye utumwa wa dhambi. 15 Sielewi nitendalo, kwa maana lile ninalotaka kulitenda, silitendi, lakini ninatenda lile ninalolichukia. 16 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, ni kwamba ninakubali kuwa sheria ni njema. 17 Lakini, kwa kweli si mimi tena nitendaye lile nisilotaka bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. 18 Kwa maana ninafahamu kwamba hakuna jema lolote likaalo ndani yangu, yaani, katika asili yangu ya dhambi. Kwa kuwa nina shauku ya kutenda lililo jema, lakini siwezi kulitenda. 19 Sitendi lile jema nitakalo kutenda, bali lile baya nisilolitaka, ndilo nitendalo. 20 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, si mimi tena nifanyaye hivyo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.

    21 Hivyo naiona sheria ikitenda kazi. Ninapotaka kutenda jema, jambo baya liko papo hapo. 22 Kwa maana katika utu wangu wa ndani naifurahia sheria ya Mungu. 23 Lakini ninaona kuna sheria nyingine inayotenda kazi katika viungo vya mwili wangu inayopigana vita dhidi ya ile sheria ya akili yangu. Sheria hii inanifanya mateka wa ile sheria ya dhambi inayofanya kazi katika viungo vya mwili wangu.

    24 Ole wangu mimi maskini! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?

    25 Ashukuriwe Mungu kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu! Hivyo basi, mimi mwenyewe kwa akili zangu ni mtumwa wa sheria ya Mungu, lakini katika asili ya dhambi ni mtumwa wa sheria ya dhambi.

  12. 36 “Mwalimu, ni amri ipi katika Sheria iliyo kuu kuliko zote?”

    37 Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’ 38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. 39 Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’

  13. 6 Kwa sababu hii nakukumbusha uchochee ile karama ya Mungu, iliyowekwa ndani yako nilipokuwekea mikono yangu. 7 Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.

    8 Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu, 9 ambaye alituokoa na kutuita katika mwito mtakatifu: si kwa kadiri ya matendo yetu mema bali kwa sababu ya kusudi lake mwenyewe na neema yake. Neema hii tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele. 10 Lakini sasa imefunuliwa kwa kudhihirishwa kwake Mwokozi wetu, Kristo Yesu, ambaye amebatilisha mauti na kuleta uzima na kutokufa kwa njia ya Injili. 11 Nami nimewekwa kuwa mhubiri, mtume na mwalimu wa Injili hii. 12 Hii ndiyo sababu ninateseka namna hii, lakini sioni haya kwa maana ninamjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kuwa anaweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hadi siku ile.

    13 Shika kwa uthabiti kielelezo cha mafundisho yenye uzima yale uliyoyasikia kwangu, pamoja na imani na upendo katika Kristo Yesu. 14 Ilinde ile amana uliyokabidhiwa kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu.

  14. 3 Utamlinda katika amani kamilifu

    yeye ambaye moyo wake ni thabiti

    kwa sababu anakutumaini wewe.

    4 Mtumaini Bwana milele,

    kwa kuwa Bwana, Bwana, ni Mwamba wa milele.

  15. 1 Yakobo, mtumwa wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo:

    Kwa makabila kumi na mawili yaliyotawanyika ulimwenguni:

    Salamu.

    2 Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3 kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. 4 Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu chochote. 5 Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa. 6 Lakini anapoomba, lazima aamini wala asiwe na shaka, kwa sababu mtu aliye na shaka ni kama wimbi la bahari, lililochukuliwa na upepo na kutupwa huku na huku. 7 Mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapata kitu chochote kutoka kwa Bwana. 8 Yeye ni mtu mwenye nia mbili, mwenye kusitasita katika njia zake zote.

  16. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2 ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

    6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. 7 Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.

    9 Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake! 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. 11 Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kupitia kwake tumepata upatanisho.

  17. 24 Kwa kuwa tuliokolewa kwa tumaini hili. Lakini kama kinachotumainiwa kikionekana hakiwi tumaini tena. Je, kuna mtu anayetumaini kupata kitu alicho nacho tayari? 25 Lakini tunapotumaini kupata kitu ambacho hatuna, basi twakingojea kwa saburi.

    26 Vivyo hivyo, Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa sababu hatujui kuomba ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa uchungu usioweza kutamkwa. 27 Naye Mungu aichunguzaye mioyo, anaijua nia ya Roho, kwa sababu Roho huwaombea watakatifu sawasawa na mapenzi ya Mungu.

    28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. 29 Maana wale Mungu aliowajua tangu mwanzo, pia aliwachagua tangu mwanzo, wapate kufanana na mfano wa Mwanawe, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.

  18. 20 Mwanangu, yasikilize kwa makini yale ninayokuambia;

    sikiliza kwa makini maneno yangu.

    21 Usiruhusu yaondoke machoni pako,

    yahifadhi ndani ya moyo wako;

    22 kwa sababu ni uzima kwa wale wanaoyapata

    na afya kwa mwili wote wa mwanadamu.

    23 Zaidi ya yote, linda moyo wako, kuliko yote uyalindayo,

    maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.

  19. 6 Mtafuteni Bwana maadamu anapatikana;

    mwiteni maadamu yu karibu.

    7 Mtu mwovu na aiache njia yake,

    na mtu mbaya na ayaache mawazo yake.

    Yeye na amrudie Bwana, naye atamrehemu,

    arudi kwa Mungu wetu, kwa kuwa atamsamehe bure kabisa.

    8 “Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu,

    wala njia zenu si njia zangu,”

    asema Bwana.

    9 “Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia,

    ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu

    na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.

    10 Kama vile mvua na theluji

    ishukavyo kutoka mbinguni,

    nayo hairudi tena huko

    bila kunywesha dunia

    na kuichipusha na kuistawisha,

    hivyo hutoa mbegu kwa mpanzi

    na mkate kwa mlaji,

    11 ndivyo lilivyo neno langu lile litokalo kinywani mwangu:

    Halitanirudia tupu,

    bali litatimiliza lile nililokusudia

    na litafanikiwa katika kusudi lile nililolituma.

  20. 6 Usile chakula cha mtu mchoyo,

    usitamani vyakula vyake vitamu,

    7 kwa maana yeye ni aina ya mtu

    ambaye kila mara anafikiri juu ya gharama.

    Anakuambia, “Kula na kunywa,”

    lakini moyo wake hauko pamoja nawe.

  21. 8 Naye atakapokuja, atauthibitishia ulimwengu kuhusu dhambi, haki na hukumu. 9 Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi, 10 kwa habari ya haki, kwa sababu ninakwenda kwa Baba, nanyi hamtaniona tena, 11 kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.

    12 “Bado ninayo mambo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili sasa. 13 Atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza awatie katika kweli yote. Yeye hatanena kwa ajili yake mwenyewe, bali atanena yale yote atakayosikia, naye atawaonyesha mambo yajayo. 14 Atanitukuza mimi, kwa maana atayachukua yaliyo yangu na kuwajulisha ninyi. 15 Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu. Ndiyo maana nimesema Roho atachukua yaliyo yangu na kuwajulisha ninyi.

    16 “Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona.”

  22. 1 Kwa hiyo huna udhuru wowote, wewe utoaye hukumu kwa mwingine, kwa maana katika jambo lolote unalowahukumu wengine, unajihukumu wewe mwenyewe kwa sababu wewe unayehukumu unafanya mambo hayo hayo. 2 Basi tunajua kwamba hukumu ya Mungu dhidi ya wale wafanyao mambo kama hayo ni ya kweli. 3 Hivyo wewe mwanadamu, utoapo hukumu juu yao na bado unafanya mambo yale yale, unadhani utaepuka hukumu ya Mungu? 4 Au waudharau wingi wa wema, ustahimili na uvumilivu wake, bila kujua kuwa wema wa Mungu wakuelekeza kwenye toba?

    5 Lakini kwa sababu ya ukaidi wenu na mioyo yenu isiyotaka kutubu, mnajiwekea akiba ya ghadhabu dhidi yenu wenyewe kwa siku ile ya ghadhabu ya Mungu, wakati hukumu yake ya haki itakapodhihirishwa. 6 Kwa maana Mungu atamlipa kila mtu sawasawa na matendo yake. 7 Wale ambao kwa kuvumilia katika kutenda mema hutafuta utukufu, heshima na maisha yasiyoharibika, Mungu atawapa uzima wa milele. 8 Lakini kwa wale watafutao mambo yao wenyewe na wale wanaokataa kweli na kuzifuata njia mbaya, kutakuwa na ghadhabu na hasira ya Mungu. 9 Kutakuwa na taabu na dhiki kwa kila mmoja atendaye maovu, Myahudi kwanza na mtu wa Mataifa pia, 10 bali utukufu, heshima na amani kwa ajili ya kila mmoja atendaye mema, kwa Myahudi kwanza, kisha kwa mtu wa Mataifa. 11 Kwa maana Mungu hana upendeleo.

    12 Watu wote waliotenda dhambi pasipo sheria wataangamia pasipo sheria, nao wote wale waliotenda dhambi chini ya sheria watahukumiwa kwa sheria. 13 Kwa maana si wale wanaoisikia sheria ambao ni wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale wanaoitii sheria ndio watakaohesabiwa haki. 14 (Naam, wakati wa watu wa Mataifa, ambao hawana sheria, wanapofanya kwa asili mambo yatakiwayo na sheria, wao ni sheria kwa nafsi zao wenyewe, hata ingawa hawana sheria. 15 Wao wanaonyesha kwamba lile linalotakiwa na sheria limeandikwa kwenye mioyo yao, ambayo pia dhamiri zao zikiwashuhudia, nayo mawazo yao yenye kupingana yatawashtaki au kuwatetea.) 16 Hili litatukia siku hiyo Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu kwa njia ya Yesu Kristo, kama isemavyo Injili yangu.

  23. 14 Kwa maana nikiomba kwa lugha, roho yangu inaomba, lakini akili yangu haina matunda. 15 Nifanyeje basi? Nitaomba kwa roho, na pia nitaomba kwa akili yangu. Nitaimba kwa roho na nitaimba kwa akili yangu pia. 16 Ikiwa unabariki kwa roho, mtu mwingine atakayejikuta miongoni mwa hao wasiojua, atawezaje kusema “Amen” katika kushukuru kwako, wakati haelewi unachosema?

  24. 9 Moyo ni mdanganyifu kuliko vitu vyote,

    ni mwovu kupita kiasi.

    Ni nani awezaye kuujua?

    10 “Mimi Bwana huchunguza moyo

    na kuzijaribu nia,

    ili kumlipa mtu kwa kadiri ya mwenendo wake,

    kwa kadiri ya matendo yake yanavyostahili.”

  25. 9 Kwa sababu hii, tangu siku ile tuliposikia habari zenu, hatujakoma kuomba kwa ajili yenu na kumsihi Mungu awajaze ninyi maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote ya kiroho na ufahamu. 10 Nasi tunaomba haya ili mpate kuishi maisha yanayostahili mbele za Bwana, na mpate kumpendeza kwa kila namna: mkizaa matunda kwa kila kazi njema, mkikua katika kumjua Mungu, 11 mkiwa mmetiwa nguvu kwa uwezo wote kwa kadiri ya nguvu yake yenye utukufu, ili mpate kuwa na wingi wa saburi na uvumilivu. Nanyi kwa furaha 12 mkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru. 13 Kwa maana ametuokoa kutoka ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa, 14 ambaye katika yeye tunao ukombozi, yaani msamaha wa dhambi.

  26. 17 Je, hamwelewi kwamba chochote kiingiacho kinywani huenda tumboni, na hatimaye hutolewa nje kikiwa uchafu? 18 Lakini kitokacho kinywani hutoka moyoni, na hiki ndicho kimtiacho mtu unajisi. 19 Kwa maana ndani ya moyo hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na masingizio. 20 Haya ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.”

  27. 5 Mtu mmoja anaitukuza siku fulani kuwa ni bora kuliko nyingine, na mwingine anaona kuwa siku zote ni sawa. Basi kila mmoja awe na hakika na yale anayoamini.

  28. 16 Hivyo tangu sasa hatumwangalii mtu yeyote kwa mtazamo wa kibinadamu. Ingawa wakati fulani tulimwangalia Kristo kwa namna ya kibinadamu, hatumwangalii tena hivyo. 17 Kwa hiyo kama mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya. 18 Haya yote yanatokana na Mungu, ambaye ametupatanisha sisi na nafsi yake kwa njia ya Yesu Kristo na kutupata sisi huduma ya upatanisho: 19 Kwamba Mungu alikuwa ndani ya Kristo akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake mwenyewe, akiwa hawahesabii watu dhambi zao. Naye ametukabidhi sisi ujumbe huu wa upatanisho.

  29. 4 Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema, 5 hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema. 6 Mungu alitufufua pamoja na Kristo na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu, 7 ili katika ule ulimwengu ujao apate kuonyesha wingi wa neema yake isiyopimika, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Kristo Yesu. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

  30. 30 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’ 31 Ya pili ndiyo hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.”

  31. 33 Tazama jinsi kilivyo kina cha utajiri

    wa hekima na maarifa ya Mungu!

    Tazama jinsi ambavyo hukumu zake hazichunguziki,

    na ambavyo njia zake zisivyotafutikana!

    34 “Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Bwana?

    Au ni nani ambaye amekuwa mshauri wake?”

    35 “Au ni nani aliyempa chochote

    ili arudishiwe?”

    36 Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, viko kwake na kwa ajili yake.

    Utukufu ni wake milele! Amen.

  32. 21 Hapo kwanza mlikuwa mmetengana na Mungu, na mlikuwa adui zake katika nia zenu kwa sababu ya mienendo yenu mibaya. 22 Lakini sasa Mungu amewapatanisha ninyi kwa njia ya mwili wa Kristo kupitia mauti, ili awalete mbele zake mkiwa watakatifu, bila dosari wala lawama, 23 ikiwa mnaendelea katika imani yenu mkiwa imara na thabiti, pasipo kuliacha tumaini lililoahidiwa katika Injili. Hii ndiyo ile Injili mliyoisikia, ambayo imehubiriwa kwa kila kiumbe chini ya mbingu, na ambayo mimi Paulo nimekuwa mtumwa wake.

  33. 14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.

    15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu.

  34. 1 Kwa sababu hii, kwa kuwa tumezungukwa na wingu kubwa namna hii la mashahidi, basi na tuweke kando kila kitu kinachotuzuia na ile dhambi inayotuzinga kwa urahisi, nasi tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa kwa ajili yetu. 2 Basi na tumtazame sana Yesu mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu, yeye ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake alistahimili msalaba, bila kujali aibu ya huo msalaba, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. 3 Mtafakarini sana yeye aliyestahimili upinzani mkuu namna hii kutoka kwa watu wenye dhambi, ili kwamba msije mkachoka na kukata tamaa.

    4 Katika kushindana kwenu dhidi ya dhambi, bado hamjapigana kiasi cha kumwaga damu yenu.

  35. 14 Yesu akaita tena ule umati wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni, kila mmoja wenu na mwelewe jambo hili. 15 Hakuna kitu kinachomwingia mtu kimtiacho unajisi, lakini kile kimtokacho ndicho kimtiacho unajisi. [ 16 Kama mtu yeyote ana masikio ya kusikia na asikie.]”

    17 Akiisha kuuacha ule umati wa watu na kuingia ndani, wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano ule. 18 Akawajibu, “Je, hata nanyi hamwelewi? Je, hamfahamu kwamba kitu kimwingiacho mtu hakimtii unajisi? 19 Mtu akila kitu hakiingii moyoni mwake bali tumboni, na baadaye hutolewa nje ya mwili wake.” (Kwa kusema hivi, Yesu alivihalalisha vyakula vyote kuwa ni “safi.”)

    20 Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. 21 Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, 22 tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu. 23 Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.”

  36. 6 Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’ ” (yaani ili kumleta Kristo chini) 7 “au ‘Ni nani atashuka kwenda kuzimu?’ ” (yaani ili kumleta Kristo kutoka kwa wafu.) 8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, lile neno la imani tunalolihubiri. 9 Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. 10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu.

  37. 12 Kwa hiyo, kwa kuwa tunalo tumaini hili, tuna ujasiri sana. 13 Sisi si kama Mose, ambaye ilimpasa kuweka utaji ili kufunika uso wake ili Waisraeli wasiuone ule mngʼao uliokuwa juu yake hadi ulipofifia na hatimaye kutoweka. 14 Lakini akili zao zilipumbazwa, kwa maana mpaka leo utaji ule ule hufunika wakati Agano la Kale linasomwa. Huo utaji haujaondolewa, kwa maana ni katika Kristo peke yake unaondolewa. 15 Hata leo Sheria ya Mose inaposomwa, utaji hufunika mioyo yao. 16 Lakini wakati wowote mtu anapomgeukia Bwana, utaji unaondolewa. 17 Basi Bwana ndiye Roho. Mahali alipo Roho wa Bwana hapo pana uhuru. 18 Nasi sote, tukiwa na nyuso zisizotiwa utaji tunadhihirisha utukufu wa Bwana, kama kwenye kioo. Nasi tunabadilishwa ili tufanane naye, toka utukufu hadi utukufu mkuu zaidi, utokao kwa Bwana, ambaye ndiye Roho.

  38. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii kwa rehema za Mungu, hatukati tamaa. 2 Tumekataa mambo ya siri na ya aibu, wala hatufuati njia za udanganyifu, tukichanganya Neno la Mungu na uongo. Kinyume cha hayo, tunadhihirisha kweli waziwazi na kujitambulisha wenyewe kwenye dhamiri ya kila mtu mbele za Mungu. 3 Hata nayo Injili yetu kama imetiwa utaji, ni kwa wale tu wanaopotea. 4 Kwa habari yao, mungu wa dunia hii amepofusha akili za wasioamini, ili wasione nuru ya Injili ya utukufu wa Kristo, aliye sura ya Mungu. 5 Kwa maana hatujihubiri sisi wenyewe ila tunamhubiri Yesu Kristo kuwa ni Bwana na sisi ni watumishi wenu kwa ajili ya Yesu. 6 Kwa kuwa Mungu, yeye aliyesema, “Nuru na ingʼae gizani,” ameifanya nuru yake ingʼae mioyoni mwetu ili kutupatia nuru ya maarifa ya utukufu wa Mungu katika uso wa Kristo.

  39. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

  40. 5 Bwana akaona jinsi uovu wa mwanadamu ulivyokuwa mkubwa duniani, na ya kuwa kila mwelekeo wa mawazo ya moyo wake wakati wote ulikuwa mbaya tu. 6 Bwana akasikitika kwamba alimuumba mwanadamu duniani, moyo wa Mungu ukajaa masikitiko. 7 Kwa hiyo Bwana akasema, “Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemuumba kutoka kwenye uso wa dunia, wanadamu na wanyama, pamoja na viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Kwa maana nasikitika kuwaumba.”

  41. 3 Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe;

    vifunge shingoni mwako,

    viandike katika ubao wa moyo wako.

    4 Ndipo utapata kibali na jina zuri

    mbele za Mungu na mwanadamu.

    5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote

    wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

    6 katika njia zako zote mkiri yeye,

    naye atayanyoosha mapito yako.

    7 Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe;

    mche Bwana ukajiepushe na uovu.

    8 Hii itakuletea afya mwilini mwako,

    na mafuta kwenye mifupa yako.

  42. 13 Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Bwana,

    au kumfundisha akiwa kama mshauri wake?

    14 Ni nani ambaye Bwana ametaka shauri kwake ili kumwelimisha,

    naye ni nani aliyemfundisha njia iliyo sawa?

    Ni nani aliyemfundisha maarifa

    au kumwonyesha mapito ya ufahamu?

    15 Hakika mataifa ni kama tone ndani ya ndoo,

    ni kama vumbi jembamba juu ya mizani,

    huvipima visiwa kana kwamba vilikuwa vumbi laini.

    16 Lebanoni hautoshi kwa moto wa madhabahuni,

    wala wanyama wake hawatoshi kwa sadaka za kuteketezwa.

    17 Mbele yake mataifa yote ni kama si kitu,

    yanaonekana yasio na thamani

    na zaidi ya bure kabisa.

  43. 28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

  44. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

  45. 16 Kwa hiyo mtu asiwahukumu ninyi kuhusu vyakula au vinywaji, au kuhusu kuadhimisha sikukuu za dini, au Sikukuu za Mwezi Mwandamo au siku ya Sabato. 17 Hizi zilikuwa kivuli cha mambo ambayo yangekuja, lakini ile iliyo halisi imo ndani ya Kristo. 18 Mtu yeyote asiwaondolee thawabu yenu kwa kusisitiza kunyenyekea kwake na kuabudu malaika. Mtu kama huyo hudumu katika maono yake, akijivuna bila sababu katika mawazo ya kibinadamu. 19 Yeye amepoteza ushirikiano na Kichwa, ambaye kutoka kwake mwili wote unalishwa na kushikamanishwa pamoja kwa viungo na mishipa, nao hukua kwa ukuaji utokao kwa Mungu.

    20 Kwa kuwa mlikufa pamoja na Kristo, mkayaacha yale mafundisho ya msingi ya ulimwengu huu, kwa nini bado mnaishi kama ninyi ni wa ulimwengu? Kwa nini mnajitia chini ya amri: 21 “Msishike! Msionje! Msiguse!”? 22 Haya yote mwisho wake ni kuharibika yanapotumiwa, kwa sababu msingi wake ni katika maagizo na mafundisho ya wanadamu. 23 Kwa kweli amri kama hizo huonekana kama zina hekima, katika namna za ibada walizojitungia wenyewe, na unyenyekevu wa uongo na kuutawala mwili kwa ukali, lakini hayafai kitu katika kuzuia tamaa za mwili.

  46. 3 Ikiwa mtu yeyote atafundisha mafundisho mapotovu wala hakubaliani na mafundisho manyofu ya Bwana wetu Yesu Kristo na yale ya utauwa, 4 huyo amejivuna wala hajui kitu chochote. Yeye amejaa tamaa ya mabishano na ugomvi kuhusu maneno ambavyo matokeo yake ni wivu na mapigano, maneno ya ukorofi, shuku mbaya, 5 na kuzozana kusikokoma kati ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, na ambao hudhani kwamba utauwa ni njia ya kupata faida.

    6 Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa. 7 Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu chochote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu. 8 Lakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo. 9 Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka huanguka kwenye majaribu, na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi. 10 Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.

  47. 15 Kwa wale walio safi, kila kitu ni safi kwao. Lakini kwa wale waliopotoka na wasioamini, hakuna chochote kilicho safi. Kwa kweli nia zao na dhamiri zao zimepotoka. 16 Wanadai kumjua Mungu, lakini kwa matendo yao wanamkana. Hao watu ni chukizo, wasiotii, wasiofaa kwa jambo lolote jema.

  48. 10 Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli

    baada ya siku zile, asema Bwana.

    Nitaziweka sheria zangu katika nia zao

    na kuziandika mioyoni mwao.

    Nitakuwa Mungu wao,

    nao watakuwa watu wangu.

  49. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni nia iyo hiyo kwa maana mtu aliyekwisha kuteswa katika mwili ameachana na dhambi. 2 Kwa hivyo, haishi maisha yake yaliyobaki ya kuishi hapa duniani kwa tamaa mbaya za wanadamu, bali anaishi kwa mapenzi ya Mungu. 3 Maana wakati uliopita mmekwisha kutumia muda wa kutosha katika maisha yenu mkifanya yale ambayo wapagani hupenda kutenda: wakiishi katika uasherati, tamaa mbaya, ulevi, karamu za ulafi, vileo, ngoma mbaya, na ibada chukizo za sanamu. 4 Wao hushangaa kwamba ninyi hamjiingizi pamoja nao katika huo wingi wa maisha ya ufisadi, nao huwatukana ninyi. 5 Lakini itawapasa wao kutoa hesabu mbele zake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa. 6 Kwa kuwa hii ndiyo sababu Injili ilihubiriwa hata kwa wale waliokufa, ili wahukumiwe sawasawa na wanadamu wengine katika mwili, lakini katika roho waishi kulingana na Mungu aishivyo.

    7 Mwisho wa mambo yote umekaribia. Kwa hiyo kuweni na akili tulivu na kiasi, mkikesha katika kuomba. 8 Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi. 9 Kuweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manungʼuniko. 10 Kila mmoja na atumie kipawa chochote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu. 11 Yeyote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Yeyote ahudumuye hana budi kuhudumu kwa nguvu zile anazopewa na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kwa njia ya Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye milele na milele. Amen.

  50. 6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.

    8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza. 9 Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.

    10 Nanyi mkiisha kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Kristo, yeye mwenyewe atawarejesha na kuwatia nguvu, akiwaimarisha na kuwathibitisha. 11 Uweza una yeye milele na milele. Amen.

  51. 4 Sikia, ee Israeli: Bwana Mungu wako, Bwana ni mmoja. 5 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. 6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. 7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo. 8 Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako. 9 Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.

  52. 14 Maneno ya kinywa changu

    na mawazo ya moyo wangu,

    yapate kibali mbele zako, Ee Bwana,

    Mwamba wangu na Mkombozi wangu.

  53. 10 Ee Mungu, uniumbie moyo safi,

    uifanye upya roho ya uthabiti ndani yangu.

  54. 44 Akawaambia, “Haya ndiyo yale niliyowaambia nilipokuwa bado niko pamoja nanyi, kwamba yote yaliyoandikwa kunihusu mimi katika Sheria ya Mose, Manabii na Zaburi hayana budi kutimizwa.”

    45 Ndipo akafungua fahamu zao ili waweze kuyaelewa Maandiko. 46 Akawaambia, “Haya ndiyo yaliyoandikwa: Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu. 47 Toba na msamaha wa dhambi zitatangaziwa mataifa yote kupitia jina lake kuanzia Yerusalemu.

  55. 16 “Hili ndilo Agano nitakalofanya nao

    baada ya siku hizo, asema Bwana.

    Nitaziweka sheria zangu mioyoni mwao,

    na kuziandika katika nia zao.”

    17 Kisha aongeza kusema:

    “Dhambi zao na kutokutii kwao

    sitakumbuka tena.”

  56. 19 Mungu si mtu, hata aseme uongo,

    wala yeye si mwanadamu, hata ajute.

    Je, anasema, kisha asitende?

    Je, anaahidi, asitimize?

  57. 11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo.

  58. 31 “Siku zinakuja,” asema Bwana,

    “nitakapofanya agano jipya

    na nyumba ya Israeli

    na nyumba ya Yuda.

    32 Halitafanana na agano

    nililofanya na baba zao

    wakati nilipowashika mkono

    kuwaongoza watoke Misri,

    kwa sababu walivunja agano langu,

    ijapokuwa nilikuwa mume kwao,”

    asema Bwana.

    33 “Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli

    baada ya siku zile,” asema Bwana.

    “Nitaweka sheria yangu katika nia zao,

    na kuiandika mioyoni mwao.

    Nitakuwa Mungu wao,

    nao watakuwa watu wangu.

    34 Mtu hatamfundisha tena jirani yake,

    wala mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘Mjue Bwana Mungu,’

    kwa sababu wote watanijua mimi,

    tangu aliye mdogo kabisa kwao, hadi aliye mkuu sana,”

    asema Bwana.

    “Kwa sababu nitasamehe uovu wao,

    wala sitazikumbuka dhambi zao tena.”

  59. 27 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Usizini.’ 28 Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. 29 Jicho lako la kuume likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima ukatupwa jehanamu. 30 Kama mkono wako wa kuume ukikusababisha kutenda dhambi, ukate, uutupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe jehanamu.

  60. 25 Wakati huo mtaalamu mmoja wa sheria alisimama ili kumjaribu Yesu, akamuuliza, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”

    26 Yesu akamjibu, “Imeandikwaje katika Sheria? Kwani unasoma nini humo?”

    27 Akajibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote’; tena, ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ ”

    28 Yesu akamwambia, “Umejibu vyema. Fanya hivyo nawe utaishi.”

  61. 25 Yesu akawaambia, “Ninyi ni wajinga kiasi gani, nanyi ni wazito mioyoni mwenu kuamini mambo yote yaliyonenwa na manabii!

  62. 10 Nawasihi ndugu zangu, katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi, ili pasiwepo na matengano katikati yenu na kwamba mwe na umoja kikamilifu katika nia na katika kusudi. 11 Ndugu zangu, nimepata habari kutoka kwa baadhi ya watu wa nyumbani mwa Kloe kwamba kuna magomvi katikati yenu. 12 Maana yangu ni kwamba: Mmoja wenu husema, “Mimi ni wa Paulo”; mwingine, “Mimi ni wa Apolo”; mwingine, “Mimi ni wa Kefa,” na mwingine, “Mimi ni wa Kristo.”

    13 Je, Kristo amegawanyika? Je, Paulo ndiye alisulubishwa kwa ajili yenu? Je, mlibatizwa kwa jina la Paulo? 14 Nashukuru kwamba sikumbatiza mtu yeyote isipokuwa Krispo na Gayo. 15 Kwa hiyo hakuna mtu yeyote anayeweza kusema kwamba alibatizwa kwa jina langu. 16 (Naam, niliwabatiza pia watu wa nyumbani mwa Stefana. Lakini zaidi ya hao sijui kama nilimbatiza mtu mwingine yeyote.) 17 Kwa maana Kristo hakunituma ili kubatiza bali kuhubiri Injili; sio kwa maneno ya hekima ya kibinadamu, ili msalaba wa Kristo usije ukakosa nguvu yake.

  63. 3 Kama nilivyokusihi wakati nilipokwenda Makedonia, endelea kubaki Efeso, ili kwamba upate kuwaagiza watu wasiendelee kufundisha mafundisho ya uongo 4 wala wasitoe muda wao kwa hadithi za kubuniwa na orodha za majina ya vizazi visivyo na mwisho, ambazo huchochea mabishano badala ya mpango wa Mungu utokanao na imani. 5 Kusudi la maagizo haya ni upendo utokao katika moyo safi, dhamiri njema na imani ya kweli. 6 Watu wengine wamepotoka kutoka haya na kugeukia majadiliano yasiyo na maana kwa kuwa, 7 wanataka kuwa walimu wa sheria, lakini hawajui mambo yale wanayosema wala hayo wanayoyatumainia kwa uthabiti.

  64. 13 Ni nani aliye na hekima na ufahamu miongoni mwenu? Basi na aionyeshe hiyo kwa maisha yake mema na kwa matendo yake yaliyotendwa kwa unyenyekevu utokanao na hekima. 14 Lakini ikiwa mna wivu na ni wenye chuki na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu kwa ajili ya hayo wala msiikatae kweli. 15 Hekima ya namna hiyo haishuki kutoka mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyo ya kiroho, na ya kishetani. 16 Kwa maana panapokuwa na wivu na ubinafsi, ndipo penye machafuko na uovu wa kila namna.

    17 Lakini hekima itokayo mbinguni kwanza ni safi, kisha inapenda amani, tena ni ya upole, iliyo tayari kusikiliza wengine kwa unyenyekevu, iliyojaa huruma na matunda mema, isiyopendelea mtu, tena isiyokuwa na unafiki. 18 Mavuno ya haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.

  65. 4 Umati wa watu wenye zogo waliokuwa miongoni mwao walitamani sana chakula kingine, Waisraeli wakaanza kulia tena na kusema, “Laiti tungekuwa na nyama tule! 5 Tunakumbuka wale samaki tuliokula huko Misri bila gharama, pia yale matango, matikitimaji, mboga, vitunguu, na vitunguu saumu. 6 Lakini sasa tumepoteza hamu ya chakula; hatuoni kitu kingine chochote isipokuwa hii mana!”

  66. 35 Je, wewe hutuma umeme wa radi kwenye njia zake?

    Je, hutoa taarifa kwako kukuambia, ‘Sisi tuko hapa’?

    36 Ni nani aliyeujalia moyo hekima

    au kuzipa akili ufahamu?

    37 Nani mwenye hekima ya kuyahesabu mawingu?

    Ni nani awezaye kuinamisha magudulia ya mbinguni

  67. KITABU CHA KWANZA

    1 Heri mtu yule ambaye

    haendi katika shauri la watu waovu,

    wala hasimami katika njia ya wenye dhambi,

    au kuketi katika baraza la wenye mizaha.

    2 Bali huifurahia sheria ya Bwana,

    naye huitafakari hiyo sheria usiku na mchana.

    3 Mtu huyo ni kama mti uliopandwa

    kando ya vijito vya maji,

    ambao huzaa matunda kwa majira yake

    na majani yake hayanyauki.

    Lolote afanyalo hufanikiwa.

  68. 22 Moyo wenye furaha ni dawa nzuri,

    bali roho iliyopondeka hukausha mifupa.

  69. 21 Kuna mipango mingi ndani ya moyo wa mtu,

    lakini kusudi la Bwana ndilo litakalosimama.

  70. 26 Nitawapa moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu, nitaondoa ndani yenu moyo wenu wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama. 27 Nami nitaweka Roho yangu ndani yenu na kuwafanya ninyi mfuate amri zangu na kuwafanya kuwa waangalifu kuzishika sheria zangu.

  71. 30 “Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami, na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya. 31 Kwa hiyo nawaambia, kila dhambi na kufuru watu watasamehewa, lakini mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa. 32 Mtu yeyote atakayesema neno dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini yeyote anenaye neno dhidi ya Roho Mtakatifu hatasamehewa, iwe katika ulimwengu huu au katika ulimwengu ujao.

    33 “Ufanye mti kuwa mzuri, nayo matunda yake yatakuwa mazuri. Au ufanye mti kuwa mbaya, na matunda yake yatakuwa mabaya. Kwa maana mti hutambulika kwa matunda yake. 34 Enyi uzao wa nyoka! Mnawezaje kunena mambo mema, wakati ninyi ni waovu? Kwa maana kinywa cha mtu huyanena yale yaliyoujaza moyo wake. 35 Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka hazina ya mambo mema yaliyohifadhiwa ndani yake, naye mtu mwovu hutoa yaliyo maovu kutoka hazina ya mambo maovu yaliyohifadhiwa ndani yake. 36 Lakini nawaambia, katika siku ya hukumu watu watatoa hesabu kuhusu kila neno lisilo maana walilonena. 37 Kwa maana kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.”

  72. 27 Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.

  73. 17 Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo.

  74. 16 Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge. Wala msiwe watu wenye kujivuna kwamba mnajua kila kitu.

  75. 26 Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika jamaa zenye vyeo. 27 Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima, Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu. 28 Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko, 29 ili mtu yeyote asijisifu mbele zake. 30 Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanyika kwetu hekima itokayo kwa Mungu, yaani haki, na utakatifu na ukombozi. 31 Hivyo, kama ilivyoandikwa: “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.”

  76. 6 Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote.

    7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. 8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. 9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. 10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.

  77. 12 Namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu, kwa sababu aliniona mwaminifu, akaniteua kwa kazi yake. 13 Ingawa wakati fulani nilikuwa mwenye kukufuru, mtesaji na mwenye jeuri, lakini nilipata rehema kwa sababu nilitenda hivyo kwa kutojua na kutoamini kwangu. 14 Neema ya Bwana wetu ilimiminwa juu yangu kwa wingi, ikiambatana na imani na upendo ulio katika Kristo Yesu.

    15 Msemo huu ni wa kweli na unaostahili kukubalika, usemao kwamba: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, ambao mimi ndiye niliye mbaya kuliko wote. 16 Lakini kwa sababu hiyo nilipata rehema, ili katika mimi, niliyekuwa mwenye dhambi kuliko wote, Kristo Yesu apate kuonyesha uvumilivu wake usio na kikomo, ili niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini na wapate uzima wa milele.

  78. 8 Kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Mose, vivyo hivyo watu hawa hupingana na ile kweli. Hawa ni watu wenye akili zilizopotoka, ambao wamekataliwa kwa mambo ya imani.

  79. 1 Wakumbushe watu kuwanyenyekea watawala na kuwatii wenye mamlaka, wawe tayari kutenda kila lililo jema. 2 Wasimnenee mtu yeyote mabaya, wasiwe wagomvi, bali wawe wapole, wakionyesha unyenyekevu kwa watu wote.

    3 Maana sisi wenyewe wakati fulani tulikuwa wajinga, wasiotii, tukiwa watumwa wa tamaa mbaya na anasa za kila aina. Tuliishi katika uovu na wivu, tukichukiwa na kuchukiana sisi kwa sisi. 4 Lakini wema na upendo wa Mungu Mwokozi wetu ulipofunuliwa, 5 alituokoa, si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda, bali kwa sababu ya rehema zake. Alituokoa kwa kutuosha kwa kuzaliwa mara ya pili na kwa kufanywa wapya kwa njia ya Roho Mtakatifu, 6 ambaye Mungu alitumiminia kwa wingi kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu, 7 ili kwamba, tukiisha kuhesabiwa haki kwa neema yake, tupate kuwa warithi tukiwa na tumaini la uzima wa milele. 8 Hili ni neno la kuaminiwa. Nami nataka uyasisitize mambo haya, ili wale ambao wamemwamini Mungu wapate kuwa waangalifu kujitoa kwa ajili ya kutenda mema wakati wote. Mambo haya ni mazuri tena ya manufaa kwa kila mtu.

    9 Lakini jiepushe na maswali ya kipuzi, mambo ya koo, mabishano na ugomvi kuhusu sheria, kwa sababu hayana faida, tena ni ubatili. 10 Mtu anayesababisha mafarakano, mwonye mara ya kwanza, kisha mwonye mara ya pili. Baada ya hapo, usihusike naye tena. 11 Kwa kuwa unajua kwamba mtu kama huyo amepotoka na tena ni mwenye dhambi. Yeye amejihukumu mwenyewe.

  80. 5 Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,

    “Kamwe sitakuacha,

    wala sitakupungukia.”

    6 Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,

    “Bwana ni msaada wangu; sitaogopa.

    Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”

  81. 14 Rehoboamu akatenda maovu kwa sababu hakuuelekeza moyo wake katika kumtafuta Bwana Mungu.

  82. 7 Sheria ya Bwana ni kamilifu,

    ikihuisha nafsi.

    Shuhuda za Bwana ni za kuaminika,

    zikimpa mjinga hekima.

    8 Maagizo ya Bwana ni kamili,

    nayo hufurahisha moyo.

    Amri za Bwana huangaza,

    zatia nuru machoni.

    9 Kumcha Bwana ni utakatifu,

    nako kwadumu milele.

    Amri za Bwana ni za hakika,

    nazo zina haki.

    10 Ni za thamani kuliko dhahabu,

    kuliko dhahabu iliyo safi sana,

    ni tamu kuliko asali,

    kuliko asali kutoka kwenye sega.

  83. 15 Ninatafakari maagizo yako

    na kuziangalia njia zako.

    16 Ninafurahia maagizo yako,

    wala sitalipuuza neno lako.

  84. 23 Ee Mungu, nichunguze, uujue moyo wangu,

    nijaribu na ujue mawazo yangu.

    24 Uone kama kuna njia iletayo machukizo ndani yangu,

    uniongoze katika njia ya milele.

  85. 19 Nitawapa moyo mmoja na kuweka roho mpya ndani yao, nitaondoa kutoka ndani yao moyo wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama. 20 Kisha watafuata amri zangu na kuwa waangalifu kutii sheria zangu. Watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao. 21 Lakini kwa wale ambao mioyo yao imeambatana na vinyago vyao vya upotovu na sanamu zao za machukizo, nitaleta juu ya vichwa vyao yale waliyotenda asema Bwana Mwenyezi.”

  86. 10 Yesu alipokuwa akila chakula ndani ya nyumba ya Mathayo, watoza ushuru wengi na “wenye dhambi” wakaja kula pamoja naye na wanafunzi wake. 11 Mafarisayo walipoona mambo haya, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”

    12 Lakini Yesu aliposikia hayo, akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, lakini wale walio wagonjwa ndio wanaohitaji tabibu. 13 Nendeni mkajifunze maana ya maneno haya: ‘Nataka rehema, wala si dhabihu.’ Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

  87. 10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. 11 Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. 12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’

    13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’

    14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”

  88. 35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga? 36 Kama ilivyoandikwa:

    “Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;

    tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.”

    37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

  89. 13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

  90. 16 Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. 17 Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi, 18 kwa sababu hatuangalii yale yanayoweza kuonekana bali yale yasiyoweza kuonekana. Kwa maana yale yanayoweza kuonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoweza kuonekana ni ya milele.

  91. 3 Lakini nina hofu kuwa, kama vile Eva alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Kristo.

  92. 1 Kwa habari zenu, mlikuwa wafu katika makosa na dhambi zenu, 2 ambazo mlizitenda mlipofuatisha namna ya ulimwengu huu na za yule mtawala wa ufalme wa anga, yule roho atendaye kazi sasa ndani ya wale wasiotii. 3 Sisi sote pia tuliishi katikati yao hapo zamani, tukitimiza tamaa za asili yetu ya dhambi na kufuata tamaa zake na mawazo yake. Nasi kwa asili tulikuwa wana wa ghadhabu, kama mtu mwingine yeyote.

  93. 10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi. 12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 13 Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara. 14 Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15 nayo miguu yenu ifungiwe utayari tuupatao kwa Injili ya amani. 16 Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17 Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho, ambao ni Neno la Mungu. 18 Mkiomba kwa Roho siku zote katika sala zote na maombi, mkikesha kila wakati mkiwaombea watakatifu wote.

    19 Niombeeni na mimi pia, ili kila nifunguapo kinywa changu, nipewe maneno ya kusema, niweze kutangaza siri ya Injili kwa ujasiri, 20 ambayo mimi ni balozi wake katika vifungo. Ombeni ili nipate kuhubiri kwa ujasiri kama inipasavyo.

  94. 11 Tunayo mengi ya kusema kuhusu habari ya ukuhani huu, lakini ni vigumu kuyaeleza, kwa sababu ninyi ni wazito wa kuelewa. 12 Kwa hakika, ingawa mpaka wakati huu ingewapasa kuwa walimu, bado mnahitaji mtu wa kuwafundisha tena hatua za awali za kweli ya Neno la Mungu. Mnahitaji maziwa, wala si chakula kigumu! 13 Kwa maana yeyote aishiye kwa kunywa maziwa bado yeye ni mtoto mchanga, hana ujuzi katika mafundisho kuhusu neno la haki. 14 Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu wazima, ambao kwa kujizoeza wamejifunza kupambanua kati ya mema na mabaya.

  95. 21 Bwana akasikia harufu nzuri ya kupendeza, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena ardhi kwa sababu ya mwanadamu, hata ingawa kila mwelekeo wa moyo wake ni mbaya tangu ujana. Kamwe sitaangamiza tena viumbe hai vyote kama nilivyofanya.

  96. 24 Bwana akatuagiza tutii amri hizi zote na kumcha Bwana Mungu wetu, ili tupate kustawi na kuendelea kuwa hai kama ilivyo leo. 25 Kama tukizitii kwa bidii amri hizi zote mbele za Bwana Mungu wetu, kama alivyotuamuru sisi, hiyo itakuwa haki yetu.”

  97. 7 Uovu hutoka katika mioyo yao iliyokufa ganzi,

    majivuno maovu kutoka mioyoni mwao hauna kikomo.

  98. 2 Njia zote za mtu huonekana safi machoni pake mwenyewe,

    bali makusudi hupimwa na Bwana.

    3 Mkabidhi Bwana lolote ufanyalo,

    nayo mipango yako itafanikiwa.

    4 Bwana hufanya kila kitu kwa kusudi lake mwenyewe;

    hata waovu kwa siku ya maangamizi.

  99. 4 Moyo wa mtu mwenye hamaki utafahamu na kuelewa,

    nao ulimi wenye kigugumizi utanena kwa ufasaha.

  100. 6 Kwa kuwa mpumbavu hunena upumbavu,

    moyo wake hushughulika na uovu:

    Hutenda mambo yasiyo ya kumcha Mungu,

    na hueneza habari za makosa kuhusu Bwana;

    yeye huwaacha wenye njaa bila kitu,

    na wenye kiu huwanyima maji.

  101. 16 Akili yake na ibadilishwe kutoka ile ya mwanadamu na apewe akili ya mnyama, mpaka nyakati saba zipite juu yake.

  102. 31 Yesu akawajibu, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa. 32 Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi wapate kutubu.”

  103. 34 “Jihadharini mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na fadhaa za maisha haya, nayo siku ile ikawakuta ninyi bila kutazamia kama vile mtego unasavyo. 35 Kwa maana kama vile mtego unasavyo, ndivyo siku hiyo itakavyowapata wanadamu wote waishio katika uso wa dunia yote. 36 Kesheni daima na mwombe ili mweze kuokoka na yale yote yatakayotokea na kusimama mbele ya Mwana wa Adamu.”

  104. 9 Yesu akamjibu, “Filipo, nimekaa nanyi muda huu wote hata usinijue? Mtu yeyote aliyeniona mimi, amemwona Baba. Sasa wawezaje kusema, ‘Tuonyeshe Baba’? 10 Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambia siyasemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba akaaye ndani yangu ndiye atendaye hizi kazi. 11 Nisadiki mimi kwamba niko ndani ya Baba na Baba yuko ndani yangu, la sivyo, niaminini kwa sababu ya zile kazi nizitendazo.

  105. 37 Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”

  106. 2 Walipokuwa wakimwabudu Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, “Nitengeeni Sauli na Barnaba kwa kazi ile maalum niliyowaitia.”

  107. 5 Mungu atoaye saburi na faraja, awajalie ninyi roho ya umoja miongoni mwenu mnapomfuata Kristo Yesu, 6 ili kwa moyo mmoja mpate kumtukuza Mungu aliye Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.

  108. 11 Hatimaye, ndugu zangu, kwaherini. Kuweni wakamilifu, mkafarijike, kuweni wa nia moja, kaeni kwa amani. Naye Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi.

  109. 1 Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na kongwa la utumwa.

  110. 14 Lakini kila mtu hujaribiwa wakati anapovutwa na kudanganywa na tamaa zake mwenyewe zilizo mbaya. 15 Basi ile tamaa mbaya ikishachukua mimba, huzaa dhambi, nayo ile dhambi ikikomaa, huzaa mauti.

    16 Ndugu zangu wapendwa, msidanganyike.

  111. 7 Basi mtiini Mungu. Mpingeni ibilisi, naye atawakimbia.