55 Bible Verses About Predestination

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Predestination
  1. 3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo. 4 Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo 5 alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo kwa furaha yake na mapenzi yake mwenyewe. 6 Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa.

  2. 28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. 29 Maana wale Mungu aliowajua tangu mwanzo, pia aliwachagua tangu mwanzo, wapate kufanana na mfano wa Mwanawe, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. 30 Nao wale Mungu aliotangulia kuwachagua, akawaita, wale aliowaita pia akawahesabia haki, nao wale aliowahesabia haki, pia akawatukuza.

    31 Tuseme nini basi kuhusu haya? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, ni nani awezaye kuwa kinyume chetu? 32 Ikiwa Mungu hakumhurumia Mwanawe, bali alimtoa kwa ajili yetu sote, atakosaje basi kutupatia vitu vyote kwa ukarimu pamoja naye?

  3. 9 Kwa maana ahadi yenyewe ilisema, “Nitakurudia tena wakati kama huu, naye Sara atapata mtoto wa kiume.”

    10 Wala si hivyo tu, bali pia watoto aliowazaa Rebeka walikuwa na baba huyo huyo mmoja, yaani, baba yetu Isaki. 11 Lakini, hata kabla hao mapacha hawajazaliwa au kufanya jambo lolote jema au baya, ili kwamba kusudi la Mungu la kuchagua lipate kusimama, 12 si kwa matendo, bali kwa yeye mwenye kuita, Rebeka aliambiwa, “Yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.” 13 Kama vile ilivyoandikwa, “Nimempenda Yakobo, lakini nimemchukia Esau.”

    14 Tuseme nini basi? Je, Mungu ni dhalimu? La, hasha! 15 Kwa maana Mungu alimwambia Mose,

    “Nitamrehemu yeye nimrehemuye,

    na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”

    16 Kwa hiyo haitegemei kutaka kwa mwanadamu au jitihada, bali hutegemea huruma ya Mungu. 17 Kwa maana Maandiko yamwambia Farao, “Nilikuinua kwa kusudi hili hasa, ili nipate kuonyesha uweza wangu juu yako, na ili Jina langu lipate kutangazwa duniani yote.”

    18 Kwa hiyo basi, Mungu humhurumia yeye atakaye kumhurumia na humfanya mgumu yeye atakaye kumfanya mgumu.

    19 Basi mtaniambia, “Kama ni hivyo, kwa nini basi bado Mungu anatulaumu? Kwa maana ni nani awezaye kupinga mapenzi yake?” 20 Lakini, ewe mwanadamu, u nani wewe ushindane na Mungu? “Je, kilichoumbwa chaweza kumwambia yeye aliyekiumba, ‘Kwa nini umeniumba hivi?’ ” 21 Je, mfinyanzi hana haki ya kufinyanga kutoka bonge moja vyombo vya udongo, vingine kwa matumizi ya heshima na vingine kwa matumizi ya kawaida?

    22 Iweje basi, kama Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake na kufanya uweza wake ujulikane, amevumilia kwa uvumilivu mwingi vile vyombo vya ghadhabu vilivyoandaliwa kwa uharibifu? 23 Iweje basi, kama yeye alitenda hivi ili kufanya wingi wa utukufu wake ujulikane kwa vile vyombo vya rehema yake, alivyotangulia kuvitengeneza kwa ajili ya utukufu wake, 24 yaani pamoja na sisi, ambao pia alituita, si kutoka kwa Wayahudi peke yao, bali pia kutoka kwa watu wa Mataifa?

  4. 11 Katika Kristo sisi nasi tumepata urithi, tukisha kuchaguliwa sawasawa na kusudi la Mungu, yeye ambaye hufanya mambo yote kulingana na kusudi la mapenzi yake, 12 ili kwamba, sisi tuliokuwa wa kwanza kuweka tumaini katika Kristo, tupate kuishi kwa sifa ya utukufu wake.

  5. 48 Watu wa Mataifa waliposikia haya wakafurahi na kulitukuza neno la Bwana; nao wote waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.

  6. 37 Wale wote anipao Baba watakuja kwangu na yeyote ajaye kwangu, sitamfukuzia nje kamwe. 38 Kwa kuwa nimeshuka kutoka mbinguni si ili kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake yeye aliyenituma. 39 Haya ndiyo mapenzi yake yeye aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho. 40 Kwa maana mapenzi ya Baba yangu ni kwamba kila mmoja amtazamaye, Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele, nami nitawafufua siku ya mwisho.”

  7. 23 Punde Petro na Yohana walipoachiliwa, walirudi kwa waumini wenzao wakawaeleza waliyoambiwa na viongozi wa makuhani na wazee. 24 Watu waliposikia hayo, wakainua sauti zao, wakamwomba Mungu kwa pamoja, wakisema, “Bwana Mwenyezi, uliyeziumba mbingu na nchi na bahari, na vitu vyote vilivyomo. 25 Wewe ulisema kwa Roho Mtakatifu kupitia kwa kinywa cha baba yetu Daudi, mtumishi wako, ukasema:

    “ ‘Mbona mataifa wanaghadhibika,

    na kabila za watu zinawaza ubatili?

    26 Wafalme wa dunia wamejipanga,

    na watawala wanakusanyika pamoja

    dhidi ya Bwana

    na dhidi ya Mpakwa Mafuta wake.’

    27 Ni kweli Herode na Pontio Pilato pamoja na watu wa Mataifa na Waisraeli, walikusanyika katika mji huu dhidi ya mwanao mtakatifu Yesu uliyemtia mafuta. 28 Wao wakafanya yale ambayo uweza wako na mapenzi yako yalikuwa yamekusudia yatokee tangu zamani. 29 Sasa, Bwana angalia vitisho vyao na utuwezeshe sisi watumishi wako kulinena neno lako kwa ujasiri mkuu. 30 Nyoosha mkono wako ili kuponya wagonjwa na kutenda ishara na miujiza kwa jina la Mwanao mtakatifu Yesu.”

  8. 1 Petro, mtume wa Yesu Kristo:

    Kwa wateule wa Mungu, wageni katika ulimwengu, waliotawanyika kote katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia. 2 Ni ninyi ambao mlichaguliwa tangu mwanzo na Mungu Baba kulingana na alivyotangulia kuwajua, kupitia kwa kazi ya utakaso wa Roho, katika utiifu kwa Yesu Kristo na kunyunyiziwa damu yake:

    Neema na amani ziwe kwenu kwa wingi.

  9. 14 Kama vile Mose alivyomwinua yule nyoka kule jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu. 15 Ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele.

    16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa. 18 Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. 19 Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu. 20 Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe. 21 Lakini yule aishiye kwa ukweli huja kwenye nuru, ili ionekane wazi kwamba matendo yake yametendeka katika Mungu.”

  10. 1 Basi nauliza: Je, Mungu amewakataa watu wake? La, hasha! Mimi mwenyewe ni Mwisraeli, tena uzao wa Abrahamu kutoka kabila la Benyamini. 2 Mungu hajawakataa watu wake, ambao yeye aliwajua tangu mwanzo. Je, hamjui yale Maandiko yasemayo kuhusu Eliya, jinsi alivyomlalamikia Mungu kuhusu Israeli? 3 Alisema, “Bwana, wamewaua manabii wako na kuzibomoa madhabahu zako, nimebaki mimi peke yangu, nao wanataka kuniua?” 4 Je, Mungu alimjibuje? “Nimejibakizia watu elfu saba ambao hawajapiga magoti kumwabudu Baali.” 5 Vivyo hivyo pia, sasa wapo mabaki waliochaguliwa kwa neema ya Mungu. 6 Lakini ikiwa wamechaguliwa kwa neema, si tena kwa msingi wa matendo. Kama ingekuwa kwa matendo, neema isingekuwa neema tena.

    7 Tuseme nini basi? Kile kitu ambacho Israeli alikitafuta kwa bidii hakukipata. Lakini waliochaguliwa walikipata. Waliobaki walifanywa wagumu, 8 kama ilivyoandikwa:

    “Mungu aliwapa bumbuazi la mioyo,

    macho ili wasiweze kuona,

    na masikio ili wasiweze kusikia,

    hadi leo.”

    9 Naye Daudi anasema:

    “Karamu zao na ziwe tanzi na mtego wa kuwanasa,

    kitu cha kuwakwaza waanguke, na adhabu kwao.

    10 Macho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona,

    nayo migongo yao iinamishwe daima.”

  11. 9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba.

  12. 4 Neno la Bwana lilinijia, kusema,

    5 “Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako, nilikujua;

    kabla hujazaliwa nilikutenga kwa kazi maalum;

    nilikuweka uwe nabii kwa mataifa.”

  13. 8 Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu, 9 ambaye alituokoa na kutuita katika mwito mtakatifu: si kwa kadiri ya matendo yetu mema bali kwa sababu ya kusudi lake mwenyewe na neema yake. Neema hii tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele. 10 Lakini sasa imefunuliwa kwa kudhihirishwa kwake Mwokozi wetu, Kristo Yesu, ambaye amebatilisha mauti na kuleta uzima na kutokufa kwa njia ya Injili.

  14. 1 Paulo, mtumishi wa Mungu na mtume wa Yesu Kristo kwa ajili ya imani ya wateule wa Mungu na kuijua kweli iletayo utauwa: 2 imani na ujuzi ulioko katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu, asiyesema uongo, aliahidi hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, 3 naye kwa wakati wake aliouweka alilidhihirisha neno lake kwa njia ya mahubiri ambayo mimi nimewekewa amana kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu:

    4 Kwa Tito, mwanangu hasa katika imani tunayoshiriki sote:

    Neema iwe kwako na amani itokayo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu.

  15. 10 Ni mimi nitangazaye mwisho tangu mwanzo,

    naam, tangu zamani za kale,

    mambo ambayo hayajatendeka.

    Ninasema: Kusudi langu ndilo litakalosimama,

    nami nitatenda mapenzi yangu yote.

    11 Kutoka mashariki ninaita ndege awindaye;

    kutoka nchi ya mbali,

    mtu atakayetimiza kusudi langu.

    Lile ambalo nimelisema, ndilo nitakalolitimiza;

    lile nililolipanga, ndilo nitakalolitenda.

    12 Nisikilizeni, ninyi wenye mioyo migumu,

    ninyi mlio mbali na haki.

  16. 22 “Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kupitia kwake, kama ninyi wenyewe mjuavyo. 23 Huyu mtu akiisha kutolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu zamani, ninyi, kwa mikono ya watu wabaya, mlimuua kwa kumgongomea msalabani. 24 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana yeye kushikiliwa na nguvu za mauti.

  17. 4 Ndugu zetu mpendwao na Mungu, kwa kuwa tunajua kwamba Mungu amewachagua, 5 kwa sababu ujumbe wetu wa Injili haukuja kwenu kwa maneno matupu bali pia ulidhihirishwa katika nguvu na katika Roho Mtakatifu, tena ukiwa na uthibitisho kamili, kama vile ninyi wenyewe mnavyojua jinsi tulivyoenenda katikati yenu kwa ajili yenu.

  18. 29 Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti moja tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka chini pasipo Baba yenu kujua. 30 Hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. 31 Hivyo msiogope; kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.

  19. 15 Lakini ilipompendeza Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu na kuniita kwa neema yake, 16 alimdhihirisha Mwanawe kwangu, ili nipate kumhubiri miongoni mwa watu wa Mataifa. Mimi sikushauriana na mwanadamu yeyote, 17 wala sikupanda kwenda Yerusalemu kuwaona hao waliokuwa mitume kabla yangu, bali nilikwenda mara moja Arabuni na kisha nikarudi Dameski.

  20. 12 Kwa hiyo, wapenzi wangu, kama vile ambavyo mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwepo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka, 13 kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema.

  21. 13 Lakini imetupasa sisi kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu, ndugu mpendwao na Bwana, kwa sababu Mungu aliwachagua ninyi tangu mwanzo ili mwokolewe kwa kutakaswa na Roho kwa kuiamini kweli.

  22. 19 Ndipo Bwana akasema, “Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza Jina langu, Bwana, mbele ya uso wako. Nitamrehemu yeye nimrehemuye, na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”

  23. 20 Kwa maana Bwana mwenyewe ndiye aliifanya mioyo yao iwe migumu, ili kupigana vita dhidi ya Israeli ili apate kuwafutilia mbali pasipo huruma, kama Bwana alivyomwagiza Mose.

  24. 44 Hakuna mtu awezaye kuja kwangu kama asipovutwa na Baba aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho.

  25. 13 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Amka mapema asubuhi, usimame mbele ya Farao, umwambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Waebrania: Waachie watu wangu waende, ili kwamba waweze kuniabudu, 14 au wakati huu nitaleta mapigo yangu yenye nguvu dhidi yako, maafisa wako na watu wako, ili upate kujua kuwa hakuna mwingine kama Mimi katika dunia yote. 15 Kwa kuwa mpaka sasa ningelikuwa nimenyoosha mkono wangu na kukupiga wewe na watu wako kwa pigo ambalo lingekufutilia mbali juu ya nchi. 16 Lakini nimekuinua wewe kwa kusudi hili hasa, ili nipate kukuonyesha uwezo wangu, na ili Jina langu lipate kutangazwa duniani yote. 17 Bado unaendelea kujiinua juu ya watu wangu, wala hutaki kuwaachia waende. 18 Kwa hiyo, kesho wakati kama huu nitaleta mvua mbaya sana ya mawe ambayo haijapata kunyesha katika nchi ya Misri, tangu siku ilipoumbwa mpaka leo.

  26. 24 Bwana Mwenye Nguvu Zote ameapa,

    “Hakika, kama vile nilivyopanga, ndivyo itakavyokuwa,

    nami kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyosimama.

    25 Nitamponda Mwashuru katika nchi yangu,

    juu ya milima yangu nitawakanyagia chini.

    Nira yake itaondolewa kutoka kwa watu wangu,

    nao mzigo wake utaondolewa kutoka mabegani mwao.”

    26 Huu ndio mpango uliokusudiwa kwa ajili ya ulimwengu wote,

    huu ni mkono ulionyooshwa juu ya mataifa yote.

    27 Kwa kuwa Bwana Mwenye Nguvu Zote amekusudia,

    ni nani awezaye kumzuia?

    Mkono wake umenyooshwa,

    ni nani awezaye kuurudisha?

  27. 17 “Ee Bwana Mwenyezi, umeumba mbingu na nchi kwa uwezo wako mkuu na kwa mkono ulionyooshwa. Hakuna jambo lililo gumu usiloliweza. 18 Wewe huonyesha upendo kwa maelfu, lakini huleta adhabu kwa ajili ya dhambi za baba mapajani mwa watoto wao baada yao. Ee Mungu mkuu na mwenye uweza, ambaye jina lako ni Bwana Mwenye Nguvu Zote, 19 makusudi yako ni makuu, na matendo yako ni yenye uwezo. Macho yako yanaona njia zote za wanadamu, nawe humlipa kila mmoja kulingana na mwenendo wake, na kama yanavyostahili matendo yake.

  28. 20 Kama Bwana asingelifupisha siku hizo, kamwe asingeliokoka mtu yeyote. Lakini kwa ajili ya wateule, wale aliowachagua, amezifupisha siku hizo. 21 Wakati huo mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo huyu hapa!’ au, ‘Tazama, yuko kule,’ msisadiki. 22 Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara na maajabu ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule.

  29. 8 Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya. Siku hiyo Isaki alipoachishwa kunyonya, Abrahamu alifanya sherehe kubwa. 9 Lakini Sara aliona kuwa mwana ambaye Hagari, Mmisri, aliyemzalia Abrahamu alikuwa anadhihaki, 10 Sara akamwambia Abrahamu, “Mwondoe mwanamke huyo mtumwa pamoja na mwanawe, kwa kuwa mwana wa mwanamke mtumwa kamwe hatarithi pamoja na mwanangu Isaki.”

    11 Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa sababu lilimhusu mwanawe. 12 Lakini Mungu akamwambia, “Usihuzunike hivyo kwa sababu ya kijana na mtumishi wako wa kike. Sikiliza lolote Sara analokuambia, kwa sababu uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaki. 13 Nitamfanya huyu mwana wa mtumishi wako wa kike kuwa taifa pia, kwa sababu naye ni uzao wako.”

    14 Kesho yake asubuhi na mapema, Abrahamu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hagari. Akaviweka mabegani mwa Hagari, akamwondoa pamoja na kijana. Hagari akashika njia, akatangatanga katika jangwa la Beer-Sheba.

  30. 1 Baada ya Yesu kusema haya, alitazama kuelekea mbinguni akawaombea na kusema:

    “Baba, saa imewadia. Umtukuze Mwanao, ili Mwanao apate kukutukuza wewe. 2 Kwa kuwa umempa mamlaka juu ya wote wenye mwili ili awape uzima wa milele wale uliompa.

  31. 23 Kwa kuwa nilipokuwa nikitembea mjini na kuangalia kwa bidii vitu vyenu vya kuabudiwa, niliona huko madhabahu moja iliyoandikwa: Kwa Mungu Asiyejulikana. Basi sasa kile ambacho mmekuwa mkikiabudu kama kisichojulikana, ndicho ninachowahubiria.

    24 “Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, yeye ndiye Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu. 25 Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji chochote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote. 26 Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi. 27 Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu. 28 ‘Kwa kuwa katika yeye tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni watoto wake.’

    29 “Kwa kuwa sisi ni watoto wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe, mfano uliotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu. 30 Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu. 31 Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.”

  32. 16 Si ninyi mlionichagua, bali mimi ndiye niliyewachagua ninyi na kuwaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kudumu. Ili nalo lolote mtakalomwomba Baba katika Jina langu, awape ninyi. 17 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane.

    18 “Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba ulinichukia mimi kabla yenu. 19 Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungeliwapenda kama vile unavyowapenda walio wake. Kwa sababu ninyi si wa ulimwengu, lakini mimi nimewachagua kutoka ulimwengu, hii ndiyo sababu ulimwengu unawachukia. 20 Kumbukeni lile neno nililowaambia, ‘Hakuna mtumishi aliye mkuu kuliko bwana wake.’ Kama wamenitesa mimi, nanyi pia watawatesa. Kama wamelishika neno langu, watalishika na neno lenu pia. 21 Watawatendea ninyi haya yote kwa ajili ya Jina langu, kwa sababu hawamjui yeye aliyenituma. 22 Kama sikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa hawana udhuru kwa ajili ya dhambi zao. 23 Yeyote anayenichukia mimi, anamchukia pia na Baba yangu. 24 Kama sikuwa nimefanya miujiza ambayo haijapata kufanywa na mtu mwingine yeyote, wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa wameiona miujiza hii na bado wakatuchukia mimi na Baba yangu. 25 Lakini hii ni kutimiza lile neno lililoandikwa kwenye Sheria kwamba, ‘Walinichukia pasipo sababu.’

    26 “Lakini atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, yaani, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi. 27 Ninyi nanyi itawapasa kushuhudia kwa sababu mmekuwa pamoja nami tangu mwanzo.

  33. 10 Kisha Bwana akasema, “Hakika nitakurudia tena majira kama haya mwakani na Sara mkeo atakuwa ana mwana.”

    Sara alikuwa akiwasikiliza kwenye ingilio la hema, lililokuwa nyuma yake. 11 Abrahamu na Sara walikuwa wazee tena waliosogea miaka, naye Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. 12 Hivyo Sara akacheka kimoyomoyo alipokuwa akiwaza, “Baada ya mimi kuwa mkongwe hivi na bwana wangu amezeeka, je, nitaweza kufurahia jambo hili?”

    13 Ndipo Bwana akamwambia Abrahamu, “Kwa nini Sara amecheka na kusema, ‘Kweli nitazaa mtoto nami sasa ni mzee?’ 14 Je, kuna jambo lolote gumu lisilowezekana kwa Bwana? Nitakurudia mwakani majira kama haya, naye Sara atakuwa na mwana.”

  34. Sehemu Ya Nne: Mungu Anazungumza

    1 Kisha Bwana akamjibu Ayubu kutoka upepo wa kisulisuli. Akasema:

    2 “Nani huyu atiaye mashauri yangu giza

    kwa maneno yasiyo na maarifa?

    3 Jikaze kama mwanaume;

    nitakuuliza swali,

    nawe unijibu.

  35. 25 Wakati huo Yesu alisema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. 26 Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.

    27 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu: Hakuna mtu amjuaye Mwana ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.

  36. 10 Kwa habari ya wokovu huu, wale manabii waliosema kuhusu neema ambayo ingewajia ninyi, walitafuta kwa bidii na kwa uangalifu mkubwa, 11 wakijaribu kujua ni wakati upi na katika mazingira gani ambayo Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao alionyesha, alipotabiri kuhusu mateso ya Kristo na utukufu ule ambao ungefuata. 12 Walidhihirishiwa kwamba walikuwa hawajihudumii wao wenyewe, bali waliwahudumia ninyi, waliponena kuhusu mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiria ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Hata malaika wanatamani kuyafahamu mambo haya.

  37. 13 Kisha Bwana akamwambia, “Ujue hakika kwamba wazao wako watakuwa wageni kwenye nchi ambayo si yao, nao watafanywa watumwa na kuteswa kwa miaka mia nne. 14 Lakini nitaliadhibu taifa lile watakalolitumikia kama watumwa, na baadaye watatoka huko na mali nyingi. 15 Wewe, hata hivyo utakwenda kwa baba zako kwa amani na kuzikwa katika uzee mwema. 16 Katika kizazi cha nne wazao wako watarudi hapa, kwa maana dhambi ya Waamori bado haijafikia kipimo kilichojaa.”

  38. 4 Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake, “Sogeeni karibu nami.” Waliposogea, akasema, “Mimi ni ndugu yenu Yosefu, yule ambaye mlimuuza Misri! 5 Sasa, msihuzunike wala msijichukie wenyewe kwa kuniuza huku, kwa sababu ilikuwa ni ili kuokoa maisha ya watu ndiyo sababu Mungu alinituma niwatangulie ninyi. 6 Kwa miaka miwili sasa imekuwepo njaa katika nchi, pia kwa miaka mitano ijayo hapatakuwepo kulima wala kuvuna. 7 Lakini Mungu alinitanguliza mbele yenu ili kuhifadhi mabaki kwa ajili yenu katika nchi, na kuokoa maisha yenu kwa wokovu mkuu.

    8 “Kwa hiyo basi, si ninyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Alinifanya kuwa baba kwa Farao, bwana wa watu wa nyumbani mwake wote, na mtawala wa Misri yote.

  39. 1 Kwa nini mataifa wanashauriana kufanya mabaya,

    na kabila za watu kula njama bure?

    2 Wafalme wa dunia wanajipanga

    na watawala wanajikusanya pamoja

    dhidi ya Bwana

    na dhidi ya Mpakwa Mafuta wake.

    3 Wanasema, “Tuvunje minyororo yao

    na kuvitupilia mbali vifungo vyao.”

    4 Yeye atawalaye mbinguni hucheka,

    Bwana huwadharau.

  40. 13 Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani;

    uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu.

    14 Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa

    kwa namna ya ajabu na ya kutisha;

    kazi zako ni za ajabu,

    ninajua hayo kikamilifu.

    15 Umbile langu halikufichika kwako,

    nilipoumbwa mahali pa siri.

    Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi,

    16 macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika.

    Siku zangu zote ulizonipangia

    ziliandikwa katika kitabu chako

    kabla haijakuwepo hata moja.

    17 Tazama jinsi yalivyo ya thamani mawazo yako kwangu, Ee Mungu!

    Jinsi jumla yake ilivyo kubwa!

  41. 35 Mataifa yote ya dunia

    yanahesabiwa kuwa si kitu.

    Hufanya kama atakavyo

    kwa majeshi ya mbinguni,

    na kwa mataifa ya dunia.

    Hakuna anayeweza kuuzuia mkono wake

    au kumwambia, “Umefanya nini wewe?”

  42. 9 Moyo wa mtu huifikiri njia yake,

    bali Bwana huelekeza hatua zake.

  43. 5 Bwana asema, “Siku zinakuja,

    nitakapomwinulia Daudi Tawi lenye haki,

    Mfalme atakayetawala kwa hekima,

    na kutenda lililo haki na sawa katika nchi.

    6 Katika siku zake, Yuda ataokolewa

    na Israeli ataishi salama.

    Hili ndilo jina atakaloitwa:

    Bwana Haki Yetu.

  44. 10 Alipokuwa peke yake, watu waliokuwepo naye pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili wakamuuliza kuhusu mifano yake. 11 Naye akawaambia, “Ninyi mmepewa kujua siri ya Ufalme wa Mungu. Lakini kwa wale walioko nje, kila kitu husemwa kwao kwa mifano, 12 ili,

    “ ‘daima waone lakini wasitambue,

    daima wasikie lakini wasielewe;

    wasije wakageuka, wakatubu na kusamehewa!’ ”

    13 Kisha Yesu akawauliza, “Hamwelewi maana ya mfano huu? Basi mtaelewaje mifano mingine? 14 Yule mpanzi hupanda neno. 15 Hawa ndio wale walio kando ya njia ambako neno lilipandwa. Walisikiapo neno, Shetani huja mara na kulinyakua lile neno lililopandwa ndani yao. 16 Nazo zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye miamba, ni wale wanaolisikia neno, na mara hulipokea kwa furaha. 17 Lakini kwa kuwa hawana mizizi, wao hudumu kwa muda mfupi tu. Kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, mara wao huiacha imani. 18 Lakini wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye miiba, hulisikia lile neno; 19 lakini masumbufu ya maisha haya, na udanganyifu wa mali na tamaa ya mambo mengine huja na kulisonga lile neno na kulifanya lisizae. 20 Wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri, hulisikia lile neno, wakalipokea na kuzaa mazao. Wao huzaa mara thelathini, au mara sitini, au mara mia ya mbegu iliyopandwa.”

  45. 4 Niliwatesa watu wa Njia hii hadi kufa, nikiwakamata waume kwa wake na kuwatupa gerezani, 5 kama kuhani mkuu na baraza zima la wazee wanavyoweza kushuhudia kunihusu. Hata nilipokea barua kutoka kwao kwenda kwa ndugu wale wa Dameski, nami nikaenda huko ili kuwaleta watu hawa Yerusalemu kama wafungwa ili waadhibiwe.

    6 “Nilipokuwa njiani kuelekea Dameski, yapata saa sita mchana, ghafula nuru kubwa kutoka mbinguni ikanimulika kotekote. 7 Nikaanguka chini, nikasikia sauti ikiniambia, ‘Sauli, Sauli! Mbona unanitesa?’

    8 “Nikajibu, ‘Wewe ni nani Bwana?’

    “Naye akaniambia, ‘Mimi ni Yesu wa Nazareti unayemtesa.’ 9 Basi wale watu waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia sauti ya yule aliyekuwa akisema nami.

    10 “Nikauliza, ‘Nifanye nini Bwana?’

    “Naye Bwana akaniambia, ‘Inuka uingie Dameski, huko utaambiwa yote yakupasayo kufanya.’

  46. 5 Mose anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.” 6 Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’ ” (yaani ili kumleta Kristo chini) 7 “au ‘Ni nani atashuka kwenda kuzimu?’ ” (yaani ili kumleta Kristo kutoka kwa wafu.) 8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, lile neno la imani tunalolihubiri. 9 Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. 10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu. 11 Kama yasemavyo Maandiko, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.” 12 Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. 13 Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.”

    14 Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? 15 Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri habari njema!”

    16 Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” 17 Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo.

  47. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

  48. 3 Uweza wake wa uungu umetupatia mambo yote tunayohitaji kwa ajili ya uzima na uchaji wa Mungu, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. 4 Kwa sababu hiyo, ametukirimia ahadi zake kuu na za thamani kupitia mambo haya, ili kupitia hayo mpate kuwa washiriki wa asili ya uungu, na kuokoka kutoka upotovu ulioko duniani unaosababishwa na tamaa mbaya.

    5 Kwa sababu hii hasa, jitahidini sana katika imani yenu kuongeza wema; na katika wema, maarifa; 6 katika maarifa, kiasi; katika kiasi, saburi; katika saburi, utauwa; 7 katika utauwa, upendano wa ndugu; na katika upendano wa ndugu, upendo. 8 Kwa maana haya yakiwa ndani yenu kwa wingi na kuzidi kuongezeka, yanawasaidia msikose bidii wala kutozaa matunda katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. 9 Lakini mtu yeyote asipokuwa na mambo haya haoni mbali, na ni kipofu, naye amesahau kule kutakaswa kutoka dhambi zake za zamani.

    10 Kwa hiyo, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuuthibitisha wito wenu na uteule wenu. Kwa maana mkifanya hivyo, hamtajikwaa kamwe, 11 na mtajaliwa kwa ukarimu mwingi kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.

  49. 15 Nami nitaweka uadui

    kati yako na huyo mwanamke,

    na kati ya uzao wako na wake,

    yeye atakuponda kichwa,

    nawe utamuuma kisigino.”

  50. 1 Bwana akawa amemwambia Abramu, “Ondoka kutoka nchi yako, uache jamii yako na nyumba ya baba yako, uende hadi nchi nitakayokuonyesha.

    2 “Mimi nitakufanya taifa kubwa

    na nitakubariki,

    Nitalikuza jina lako,

    nawe utakuwa baraka.

    3 Nitawabariki wale wanaokubariki,

    na yeyote akulaaniye nitamlaani;

    na kupitia kwako mataifa yote duniani

    yatabarikiwa.”

  51. 30 Hakuna hekima, wala akili, wala mpango

    unaoweza kufaulu dhidi ya Bwana.

  52. 18 “Tazama mtumishi wangu niliyemchagua,

    mpendwa wangu, ninayependezwa naye.

    Nitaweka Roho wangu juu yake,

    naye atatangaza haki kwa mataifa.

    19 Hatagombana wala hatapiga kelele,

    wala hakuna atakayesikia sauti yake njiani.

    20 Mwanzi uliopondeka hatauvunja,

    na utambi unaofuka moshi hatauzima,

    mpaka atakapoifanya haki ishinde.

    21 Katika Jina lake mataifa

    wataweka tumaini lao.”

  53. 44 Akawaambia, “Haya ndiyo yale niliyowaambia nilipokuwa bado niko pamoja nanyi, kwamba yote yaliyoandikwa kunihusu mimi katika Sheria ya Mose, Manabii na Zaburi hayana budi kutimizwa.”

    45 Ndipo akafungua fahamu zao ili waweze kuyaelewa Maandiko. 46 Akawaambia, “Haya ndiyo yaliyoandikwa: Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu. 47 Toba na msamaha wa dhambi zitatangaziwa mataifa yote kupitia jina lake kuanzia Yerusalemu.

  54. 22 Wakati huo ilikuwa Sikukuu ya Kuwekwa wakfu kwa Hekalu huko Yerusalemu, nao ulikuwa wakati wa majira ya baridi. 23 Naye Yesu alikuwa akitembea ndani ya Hekalu katika ukumbi wa Solomoni. 24 Wayahudi wakamkusanyikia wakamuuliza, “Utatuweka katika hali ya mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo tuambie waziwazi.”

    25 Yesu akawajibu, “Nimewaambia, lakini hamwamini. Mambo ninayoyatenda kwa jina la Baba yangu yananishuhudia. 26 Lakini hamwamini, kwa sababu ninyi si wa kundi la kondoo wangu. 27 Kondoo wangu huisikia sauti yangu nami nawajua, nao hunifuata, 28 nami ninawapa uzima wa milele, hawataangamia kamwe wala hakuna mtu atakayewapokonya kutoka mikono yangu. 29 Baba yangu aliyenipa hawa ni mkuu kuliko wote na hakuna awezaye kuwapokonya kutoka mikononi mwake.

  55. 22 Kwa maana Mose alisema, ‘Bwana Mungu wenu atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu. Itawapasa kumtii huyo kwa kila jambo atakalowaambia. 23 Mtu yeyote ambaye hatamsikiliza huyo nabii, atatupiliwa mbali kabisa na watu wake.’

    24 “Naam, manabii wote tangu Samweli na waliokuja baada yake, wote walitabiri kuhusu siku hizi. 25 Ninyi ndio wana wa manabii na wa Agano ambalo Mungu alifanya na baba zenu, akimwambia Abrahamu, ‘Kupitia kwa uzao wako, watu wote wa ulimwengu watabarikiwa.’