32 Bible Verses About Purpose

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Purpose
  1. 28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. 29 Maana wale Mungu aliowajua tangu mwanzo, pia aliwachagua tangu mwanzo, wapate kufanana na mfano wa Mwanawe, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.

  2. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

  3. 20 Sikiliza mashauri na ukubali mafundisho,

    nawe mwishoni utakuwa na hekima.

    21 Kuna mipango mingi ndani ya moyo wa mtu,

    lakini kusudi la Bwana ndilo litakalosimama.

  4. 11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. 12 Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. 14 Nitaonekana kwenu,” asema Bwana, “nami nitawarudisha watu wenu waliotekwa. Nitawakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipokuwa nimewafukuzia, nami nitawarudisha mahali ambapo nilikuwa nimewatoa walipochukuliwa uhamishoni,” asema Bwana.

  5. 3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa. 4 Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja, 5 vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. 6 Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani. 7 Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe, 8 kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha.

  6. 4 Neno la Bwana lilinijia, kusema,

    5 “Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako, nilikujua;

    kabla hujazaliwa nilikutenga kwa kazi maalum;

    nilikuweka uwe nabii kwa mataifa.”

    6 Nami nikasema, “Aa, Bwana Mwenyezi, sijui kusema, kwani mimi ni mtoto mdogo tu.”

    7 Lakini Bwana akaniambia, “Usiseme, ‘Mimi ni mtoto mdogo tu.’ Utaenda popote nitakapokutuma na kunena lolote nitakalokuagiza. 8 Usiwaogope, kwa maana niko pamoja nawe nikuokoe,” asema Bwana.

    9 Kisha Bwana akaunyoosha mkono wake na kugusa kinywa changu, akaniambia, “Sasa nimeyaweka maneno yangu kinywani mwako. 10 Tazama, leo nimekuweka juu ya mataifa na falme ili kungʼoa na kubomoa, kuharibu na kuangamiza, kujenga na kupanda.”

  7. 42 Kesho yake, kulipopambazuka, Yesu alikwenda mahali pa faragha. Watu wengi wakawa wanamtafuta kila mahali, nao walipomwona wakajaribu kumzuia asiondoke. 43 Lakini yeye akawaambia, “Imenipasa kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa maana kwa kusudi hili nilitumwa.” 44 Naye aliendelea kuhubiri katika masinagogi ya Uyahudi.

  8. 7 Ndani yake tunao ukombozi kwa njia ya damu yake, yaani, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake 8 aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote. 9 Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Kristo, 10 ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani, kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Kristo.

    11 Katika Kristo sisi nasi tumepata urithi, tukisha kuchaguliwa sawasawa na kusudi la Mungu, yeye ambaye hufanya mambo yote kulingana na kusudi la mapenzi yake, 12 ili kwamba, sisi tuliokuwa wa kwanza kuweka tumaini katika Kristo, tupate kuishi kwa sifa ya utukufu wake.

  9. 9 ambaye alituokoa na kutuita katika mwito mtakatifu: si kwa kadiri ya matendo yetu mema bali kwa sababu ya kusudi lake mwenyewe na neema yake. Neema hii tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele.

  10. 10 Ni mimi nitangazaye mwisho tangu mwanzo,

    naam, tangu zamani za kale,

    mambo ambayo hayajatendeka.

    Ninasema: Kusudi langu ndilo litakalosimama,

    nami nitatenda mapenzi yangu yote.

    11 Kutoka mashariki ninaita ndege awindaye;

    kutoka nchi ya mbali,

    mtu atakayetimiza kusudi langu.

    Lile ambalo nimelisema, ndilo nitakalolitimiza;

    lile nililolipanga, ndilo nitakalolitenda.

  11. 13 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Amka mapema asubuhi, usimame mbele ya Farao, umwambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Waebrania: Waachie watu wangu waende, ili kwamba waweze kuniabudu, 14 au wakati huu nitaleta mapigo yangu yenye nguvu dhidi yako, maafisa wako na watu wako, ili upate kujua kuwa hakuna mwingine kama Mimi katika dunia yote. 15 Kwa kuwa mpaka sasa ningelikuwa nimenyoosha mkono wangu na kukupiga wewe na watu wako kwa pigo ambalo lingekufutilia mbali juu ya nchi. 16 Lakini nimekuinua wewe kwa kusudi hili hasa, ili nipate kukuonyesha uwezo wangu, na ili Jina langu lipate kutangazwa duniani yote. 17 Bado unaendelea kujiinua juu ya watu wangu, wala hutaki kuwaachia waende. 18 Kwa hiyo, kesho wakati kama huu nitaleta mvua mbaya sana ya mawe ambayo haijapata kunyesha katika nchi ya Misri, tangu siku ilipoumbwa mpaka leo.

  12. 33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia.

  13. 18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”

  14. 26 Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.”

    27 Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,

    kwa mfano wa Mungu alimuumba;

    mwanaume na mwanamke aliwaumba.

    28 Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”

  15. 2 “Ninajua ya kuwa unaweza kufanya mambo yote,

    wala hakuna mpango wako unaoweza kuzuilika.

  16. 8 Bwana atatimiza kusudi lake kwangu,

    Ee Bwana, upendo wako wadumu milele:

    usiziache kazi za mikono yako.

  17. 13 Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani;

    uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu.

    14 Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa

    kwa namna ya ajabu na ya kutisha;

    kazi zako ni za ajabu,

    ninajua hayo kikamilifu.

  18. 4 Nimekutukuza wewe duniani kwa kuitimiza ile kazi uliyonipa niifanye.

  19. 7 Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. 8 Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.

  20. 7 Nimekuwa mtumishi wa Injili hii kwa kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa nguvu yake itendayo kazi. 8 Ingawa mimi ni mdogo kuliko aliye mdogo kabisa miongoni mwa watakatifu wote, nilipewa neema hii: ili niwahubirie watu wa Mataifa kuhusu utajiri usiopimika ulio ndani ya Kristo, 9 na kuweka wazi kwa kila mtu siri hii iliyokuwa imefichwa tangu zamani katika Mungu, aliyeumba vitu vyote. 10 Ili sasa kwa njia ya Kanisa, hekima yote ya Mungu ipate kujulikana kwa watawala na wenye mamlaka katika ulimwengu wa roho, 11 sawasawa na kusudi lake la milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.

  21. 14 Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani, 15 na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. 16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, 17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.

  22. 13 Hii ndiyo jumla ya maneno;

    yote yamekwisha sikiwa:

    Mche Mungu, nawe uzishike amri zake,

    maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.

    14 Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi,

    pamoja na kila neno la siri,

    likiwa jema au baya.

  23. 22 “Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kupitia kwake, kama ninyi wenyewe mjuavyo. 23 Huyu mtu akiisha kutolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu zamani, ninyi, kwa mikono ya watu wabaya, mlimuua kwa kumgongomea msalabani. 24 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana yeye kushikiliwa na nguvu za mauti.

  24. 3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo. 4 Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo 5 alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo kwa furaha yake na mapenzi yake mwenyewe. 6 Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa.

  25. 10 Kama vile mvua na theluji

    ishukavyo kutoka mbinguni,

    nayo hairudi tena huko

    bila kunywesha dunia

    na kuichipusha na kuistawisha,

    hivyo hutoa mbegu kwa mpanzi

    na mkate kwa mlaji,

    11 ndivyo lilivyo neno langu lile litokalo kinywani mwangu:

    Halitanirudia tupu,

    bali litatimiliza lile nililokusudia

    na litafanikiwa katika kusudi lile nililolituma.

  26. 13 “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.

    14 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. 15 Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani ya ile nyumba. 16 Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

    17 “Msidhani kwamba nimekuja kufuta Sheria au Manabii; sikuja kuondoa bali kutimiza.

  27. 16 Sasa inuka usimame kwa miguu yako. Nimekutokea ili nikuteue uwe mtumishi na shahidi wa mambo ambayo umeyaona, na yale nitakayokuonyesha.

  28. 19 Basi mtaniambia, “Kama ni hivyo, kwa nini basi bado Mungu anatulaumu? Kwa maana ni nani awezaye kupinga mapenzi yake?”

  29. 22 Ninamtuma kwenu kwa ajili ya kusudi hili hasa, ili mpate kujua hali yetu, na awatie moyo.

  30. 12 Kwa hiyo, wapenzi wangu, kama vile ambavyo mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwepo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka, 13 kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema.

  31. 9 Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu walio milki ya Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu. 10 Mwanzo ninyi mlikuwa si taifa, lakini sasa ninyi ni taifa la Mungu. Mwanzo mlikuwa hamjapata rehema, lakini sasa mmepata rehema.

  32. 15 Msiupende ulimwengu wala mambo yaliyo ulimwenguni. Kama mtu yeyote akiupenda ulimwengu, upendo wa Baba haumo ndani yake. 16 Kwa maana kila kitu kilichomo ulimwenguni, yaani tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima, havitokani na Baba bali hutokana na ulimwengu. 17 Nao ulimwengu unapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu milele.