35 Bible Verses About Planning
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
13 Basi sikilizeni ninyi msemao, “Leo au kesho tutakwenda katika mji huu ama ule tukae humo mwaka mmoja, tufanye biashara na kupata faida.” 14 Lakini hamjui hata litakalotukia kesho. Maisha yenu ni nini? Ninyi ni ukungu ambao huonekana kwa kitambo kidogo kisha hutoweka. 15 Badala yake, inawapasa kusema, “Kama Bwana akipenda, tutaishi na kufanya hili ama lile.” 16 Kama ilivyo sasa, mnajisifu na kujigamba. Kujisifu kwa namna hiyo ni uovu. 17 Basi mtu yeyote anayejua jema limpasalo kutenda, lakini asilitende, mtu huyo anatenda dhambi.
-
11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. 12 Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.
-
1 Mipango ya moyoni ni ya mwanadamu,
bali jibu la ulimi hutoka kwa Bwana.
2 Njia zote za mtu huonekana safi machoni pake mwenyewe,
bali makusudi hupimwa na Bwana.
3 Mkabidhi Bwana lolote ufanyalo,
nayo mipango yako itafanikiwa.
4 Bwana hufanya kila kitu kwa kusudi lake mwenyewe;
hata waovu kwa siku ya maangamizi.
-
5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote
wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6 katika njia zako zote mkiri yeye,
naye atayanyoosha mapito yako.
7 Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe;
mche Bwana ukajiepushe na uovu.
-
9 Moyo wa mtu huifikiri njia yake,
bali Bwana huelekeza hatua zake.
-
20 Sikiliza mashauri na ukubali mafundisho,
nawe mwishoni utakuwa na hekima.
21 Kuna mipango mingi ndani ya moyo wa mtu,
lakini kusudi la Bwana ndilo litakalosimama.
-
8 “Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu,
wala njia zenu si njia zangu,”
asema Bwana.
9 “Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia,
ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu
na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.
10 Kama vile mvua na theluji
ishukavyo kutoka mbinguni,
nayo hairudi tena huko
bila kunywesha dunia
na kuichipusha na kuistawisha,
hivyo hutoa mbegu kwa mpanzi
na mkate kwa mlaji,
11 ndivyo lilivyo neno langu lile litokalo kinywani mwangu:
Halitanirudia tupu,
bali litatimiliza lile nililokusudia
na litafanikiwa katika kusudi lile nililolituma.
-
28 “Ni nani miongoni mwenu ambaye kama anataka kujenga nyumba, hakai kwanza chini na kufanya makisio ya gharama aone kama ana fedha za kutosha kukamilisha? 29 La sivyo, akiisha kuweka msingi, naye akiwa hana uwezo wa kuikamilisha, wote waionao wataanza kumdhihaki, 30 wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga lakini hakuweza kukamilisha.’
31 “Au ni mfalme gani atokaye kwenda kupigana vita na mfalme mwingine, ambaye hakai chini kwanza na kufikiri iwapo akiwa na jeshi la watu 10,000 ataweza kupigana na yule anayekuja na jeshi la watu 20,000? 32 Kama hawezi, basi wakati yule mwingine akiwa bado yuko mbali, yeye hutuma ujumbe wa watu na kuomba masharti ya amani. 33 Vivyo hivyo, yeyote miongoni mwenu ambaye hawezi kuacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
-
31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia. 34 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.
-
22 Mipango hushindwa kufanikiwa kwa ajili ya kukosa ushauri,
bali kukiwa na washauri wengi hufanikiwa.
-
11 Kisha nikaona kiti kikubwa cheupe cha enzi pamoja na yeye aliyeketi juu yake. Dunia na mbingu zikaukimbia uso wake wala mahali pao hapakuonekana. 12 Nami nikawaona wafu wakubwa na wadogo, wakiwa wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi na vitabu vikafunguliwa. Pia kitabu kingine kikafunguliwa ambacho ni kitabu cha uzima. Hao wafu wakahukumiwa sawasawa na matendo yao kama yalivyoandikwa ndani ya hivyo vitabu. 13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake, nayo mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Kila mtu akahukumiwa kulingana na yale aliyoyatenda. 14 Kisha mauti na Kuzimu zikatupwa katika ziwa la moto. Hii ndio mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. 15 Iwapo mtu jina lake halikuonekana katika kile kitabu cha uzima, alitupwa ndani ya lile ziwa la moto.
-
4 Na akujalie haja ya moyo wako,
na aifanikishe mipango yako yote.
-
28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.
-
6 Ewe mvivu, mwendee mchwa;
zitafakari njia zake ukapate hekima!
7 Kwa maana yeye hana msimamizi,
wala mwangalizi, au mtawala,
8 lakini hujiwekea akiba wakati wa kiangazi
na hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.
9 Ewe mvivu, utalala hata lini?
Utaamka lini kutoka usingizi wako?
10 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo,
bado kukunja mikono kidogo upate kupumzika:
11 hivyo umaskini utakuja juu yako kama mnyangʼanyi,
na kupungukiwa kutakujia kama mtu mwenye silaha.
-
5 Mipango ya mwenye bidii huelekeza kwenye faida,
kama vile kwa hakika pupa huelekeza kwenye umaskini.
-
1 Usijisifu kwa ajili ya kesho,
kwa kuwa hujui ni nini kitakachozaliwa kwa siku moja.
-
16 Kisha akawaambia mfano huu: “Shamba la mtu mmoja tajiri lilizaa sana. 17 Akawaza moyoni mwake, ‘Nifanye nini? Sina mahali pa kuhifadhi mavuno yangu.’
18 “Ndipo huyo tajiri akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu za nafaka na kujenga nyingine kubwa zaidi na huko nitayahifadhi mavuno yangu yote na vitu vyangu. 19 Nami nitaiambia nafsi yangu, “Nafsi, unavyo vitu vingi vizuri ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi. Pumzika; kula, unywe, ufurahi.” ’
20 “Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe! Usiku huu uhai wako unatakiwa. Sasa hivyo vitu ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani?’
21 “Hivyo ndivyo ilivyo kwa wale wanaojiwekea mali lakini hawajitajirishi kwa Mungu.”
22 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake: “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. 23 Maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi. 24 Fikirini ndege! Wao hawapandi wala hawavuni, hawana ghala wala popote pa kuhifadhi nafaka; lakini Mungu huwalisha. Ninyi ni wa thamani zaidi kuliko ndege! 25 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake? 26 Kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini basi kuyasumbukia hayo mengine?
-
1 Ndugu, kuhusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanyika kwetu pamoja mbele zake, tunawasihi, 2 msiyumbishwe kwa urahisi wala msitiwe wasiwasi na roho wala neno au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu, isemayo kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwako. 3 Mtu yeyote na asiwadanganye kwa namna yoyote kwa maana siku ile haitakuja mpaka uasi utokee kwanza, na yule mtu wa kuasi adhihirishwe, yule ambaye amehukumiwa kuangamizwa kabisa. 4 Yeye atapingana na kujitukuza juu ya kila kitu kiitwacho Mungu au kinachoabudiwa, ili kujiweka juu katika Hekalu la Mungu, akijitangaza mwenyewe kuwa ndiye Mungu.
5 Je, hamkumbuki ya kwamba nilipokuwa pamoja nanyi niliwaambia mambo haya?
-
8 Asubuhi uniletee neno la upendo wako usiokoma,
kwa kuwa nimeweka tumaini langu kwako.
Nionyeshe njia nitakayoiendea,
kwa kuwa kwako nainua nafsi yangu.
-
17 Kwa hiyo kuna tumaini kwa siku zijazo,”
asema Bwana.
“Watoto wako watarudi nchi yao yenyewe.
-
8 Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea;
nitakushauri na kukuangalia.
-
12 Tufundishe kuzihesabu siku zetu vizuri,
ili tujipatie moyo wa hekima.
-
18 Fanya mipango kwa kutafuta mashauri,
ukipigana vita, tafuta maelekezo.
-
27 Maliza kazi zako za nje,
nawe uweke mashamba yako tayari,
baada ya hayo, jenga nyumba yako.
-
23 Hakikisha kuwa unajua hali ya makundi yako
ya kondoo na mbuzi,
angalia kwa bidii ngʼombe zako.
24 Kwa kuwa utajiri haudumu milele,
nayo taji haidumu vizazi vyote.
25 Wakati majani makavu yameondolewa
na mapya yamechipua,
nayo majani toka milimani yamekusanywa,
26 wana-kondoo watakupatia mavazi
na mbuzi thamani ya shamba.
27 Utakuwa na maziwa mengi ya mbuzi
kukulisha wewe na jamaa yako,
na kuwalisha watumishi wako wa kike.
-
1 Kuna wakati kwa ajili ya kila jambo,
nayo majira kwa kila tendo chini ya mbingu:
2 wakati wa kuzaliwa na wakati wa kufa,
wakati wa kupanda na wakati wa kungʼoa yaliyopandwa,
3 wakati wa kuua na wakati wa kuponya,
wakati wa kubomoa,
na wakati wa kujenga,
4 wakati wa kulia na wakati wa kucheka,
wakati wa kuomboleza na wakati wa kucheza,
5 wakati wa kutawanya mawe na wakati wa kukusanya mawe,
wakati wa kukumbatia na wakati wa kutokumbatia,
6 wakati wa kutafuta na wakati wa kupoteza,
wakati wa kuweka na wakati wa kutupa,
7 wakati wa kurarua na wakati wa kushona,
wakati wa kunyamaza na wakati wa kuzungumza,
8 wakati wa kupenda na wakati wa kuchukia,
wakati wa vita na wakati wa amani.
-
10 Lolote mkono wako upatalo kufanya, fanya kwa nguvu zako zote, kwa kuwa huko kuzimu, unakokwenda, hakuna kufanya kazi wala mipango wala maarifa wala hekima.
-
29 Huwapa nguvu waliolegea
na huongeza nguvu za wadhaifu.
30 Hata vijana huchoka na kulegea,
nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,
31 bali wale wamtumainio Bwana
atafanya upya nguvu zao.
Watapaa juu kwa mbawa kama tai;
watapiga mbio wala hawatachoka,
watatembea kwa miguu wala hawatazimia.
-
10 Hili ndilo asemalo Bwana: “Miaka sabini itakapotimia kwa ajili ya Babeli, nitakuja kwenu na kutimiza ahadi yangu ya rehema ya kuwarudisha mahali hapa.
-
24 “Majuma sabini yameamriwa kwa ajili ya watu wako na kwa ajili ya mji wako mtakatifu, ili kumaliza makosa, kukomesha dhambi, kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, kuleta haki ya milele, kutia muhuri maono na unabii, na pia kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu sana.
25 “Ujue na kuelewa hili: Tangu kutolewa kwa amri ya kuutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu mpaka kuja kwa Mpakwa mafuta, aliye mtawala, kutakuwako majuma saba na majuma sitini na mawili. Barabara zitajengwa tena pamoja na mahandaki, lakini katika wakati wa taabu. 26 Baada ya majuma sitini na mawili, Mpakwa Mafuta atakatiliwa mbali, wala hatabaki na kitu. Watu wa mtawala atakayekuja watauharibu mji pamoja na mahali patakatifu. Mwisho utakuja kama mafuriko: Vita vitaendelea mpaka mwisho, nao ukiwa umeamriwa. 27 Mtawala huyo atathibitisha agano na watu wengi kwa juma moja. Katikati ya juma hilo atakomesha dhabihu na sadaka. Mahali pa dhabihu katika Hekalu atasimamisha chukizo la uharibifu, hadi mwisho ulioamriwa utakapomiminwa juu yake yeye aletaye uharibifu.”
-
1 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia. 2 Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Naenda kuwaandalia makao. 3 Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo.
-
6 Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamuuliza Yesu, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?”
7 Yesu akawaambia, “Si juu yenu kujua nyakati na majira ambayo Baba ameyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. 8 Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.”
9 Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena.
10 Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake Mbinguni, tazama ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao, 11 wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda Mbinguni, atarudi tena jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake Mbinguni.”
-
6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.
-
8 Lakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo. 9 Kwa maana Mungu hakutuita ili tupate ghadhabu bali tupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. 10 Yeye alikufa kwa ajili yetu ili hata kama tuko macho au tumelala, tupate kuishi pamoja naye.
-
3 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa rehema zake kuu ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima kupitia kwa kufufuka kwa Yesu Kristo kutoka kwa wafu, 4 ili tuupate urithi usioharibika, usio na uchafu, ule usionyauka: uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu,
Shows Read in context, Share and Copy.