30 Bible Verses About Success
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
1 Mwanangu, usisahau mafundisho yangu,
bali zitunze amri zangu moyoni mwako,
2 kwa kuwa zitakuongezea miaka mingi ya maisha yako
na kukuletea mafanikio.
3 Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe;
vifunge shingoni mwako,
viandike katika ubao wa moyo wako.
4 Ndipo utapata kibali na jina zuri
mbele za Mungu na mwanadamu.
5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote
wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6 katika njia zako zote mkiri yeye,
naye atayanyoosha mapito yako.
-
10 “Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, pia ni mwaminifu hata katika mambo makubwa, naye mtu ambaye si mwaminifu katika mambo madogo pia si mwaminifu katika mambo makubwa. 11 Ikiwa hamkuwa waaminifu katika mali ya kidunia, ni nani atakayewaaminia mali ya kweli?
-
14 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika:
“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye Amen, shahidi mwaminifu na wa kweli, mtawala wa uumbaji wote wa Mungu. 15 Nayajua matendo yako, ya kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungelikuwa moja au lingine. 16 Hivyo kwa kuwa u vuguvugu, si baridi wala moto, nitakutapika utoke kinywani mwangu. 17 Kwa maana unasema: ‘Mimi ni tajiri, nimejilimbikizia mali, wala sihitaji kitu chochote.’ Lakini hutambui ya kwamba wewe ni mnyonge, wa kuhurumiwa, maskini, kipofu, tena uliye uchi. 18 Nakushauri ununue kutoka kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, ili upate kuwa tajiri, na mavazi meupe ili uyavae upate kuficha aibu ya uchi wako, na mafuta ya kupaka macho yako ili upate kuona.
19 “Wale niwapendao, ninawakemea na kuwaadibisha. Hivyo uwe na bidii ukatubu. 20 Tazama! Nasimama mlangoni nabisha. Kama mtu yeyote akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia ndani na kula pamoja naye, naye pamoja nami.
21 “Yeye ashindaye nitampa haki ya kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi, kama vile mimi nilivyoshinda na nikaketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi. 22 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.”
-
13 Basi sikilizeni ninyi msemao, “Leo au kesho tutakwenda katika mji huu ama ule tukae humo mwaka mmoja, tufanye biashara na kupata faida.” 14 Lakini hamjui hata litakalotukia kesho. Maisha yenu ni nini? Ninyi ni ukungu ambao huonekana kwa kitambo kidogo kisha hutoweka. 15 Badala yake, inawapasa kusema, “Kama Bwana akipenda, tutaishi na kufanya hili ama lile.” 16 Kama ilivyo sasa, mnajisifu na kujigamba. Kujisifu kwa namna hiyo ni uovu. 17 Basi mtu yeyote anayejua jema limpasalo kutenda, lakini asilitende, mtu huyo anatenda dhambi.
-
1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.
-
24 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 25 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata. 26 Kwa maana, je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 27 Kwa maana Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, naye ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.
-
1 Baada ya kifo cha Mose mtumishi wa Bwana, Bwana akamwambia Yoshua mwana wa Nuni, msaidizi wa Mose: 2 “Mtumishi wangu Mose amekufa. Sasa basi, wewe pamoja na watu wote hawa, jiandaeni kuvuka huu Mto Yordani kuingia nchi ambayo karibu nitawapa wana wa Israeli. 3 Kila mahali nyayo za miguu yenu zitakapokanyaga nimewapa, kama vile nilivyomwahidi Mose. 4 Nchi yenu itaenea kuanzia jangwa hili hadi Lebanoni, tena kuanzia mto mkubwa wa Frati, yaani nchi yote ya Wahiti, hadi Bahari ile Kubwa iliyoko upande wa magharibi. 5 Hakuna mtu yeyote atakayeweza kushindana na wewe siku zote za maisha yako. Kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe, sitakuacha wala sitakupungukia.
6 “Uwe hodari na shujaa, kwa sababu wewe ndiwe utakayewaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa. 7 Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. 8 Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”
-
2 Bwana alikuwa pamoja na Yosefu, naye akastawi, Yosefu akaishi nyumbani kwa bwana wake Mmisri. 3 Potifa alipoona kuwa Bwana alikuwa pamoja na Yosefu na kwamba Bwana alimfanikisha kwa kila kitu alichokifanya, 4 Yosefu alipata kibali machoni pa Potifa, akamfanya mhudumu wake. Potifa akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, naye akamkabidhi kuwa mwangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho. 5 Kuanzia wakati huo Potifa alipomweka Yosefu kuwa msimamizi wa nyumba na mali zake zote alizokuwa nazo, Bwana aliibariki nyumba ya Mmisri huyo kwa sababu ya Yosefu. Baraka ya Bwana ilikuwa juu ya kila kitu alichokuwa nacho Potifa, nyumbani na shambani. 6 Kwa hiyo Potifa akamwachia Yosefu uangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho, Yosefu alipokuwa katika uongozi, Potifa hakuwa na sababu ya kujishughulisha na kitu chochote isipokuwa chakula alichokula.
Yosefu alikuwa mwenye umbo zuri na sura ya kuvutia;
-
1 Siku zilipokaribia za Daudi kufa, akampa mwanawe Solomoni agizo.
2 Akasema, “Mimi ninakaribia kwenda njia ya dunia yote. Hivyo uwe hodari, jionyeshe kuwa mwanaume, 3 shika lile Bwana Mungu wako analokuagiza: Enenda katika njia zake, ushike maagizo na amri zake, sheria zake na kanuni zake, kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Mose, ili upate kustawi katika yote ufanyayo na popote uendako, 4 ili kwamba Bwana aweze kunitimizia ahadi yake: ‘Kama wazao wako wakiangalia sana wanavyoishi, na kama wakienenda kwa uaminifu mbele zangu kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote, kamwe hutakosa kuwa na mtu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli.’
-
3 Mkabidhi Bwana lolote ufanyalo,
nayo mipango yako itafanikiwa.
-
11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo.
-
11 Ee Bwana, tega sikio lako na usikie maombi ya huyu mtumishi wako, na maombi ya watumishi wako wanaofurahia kuliheshimu Jina lako. Nipe leo, mimi mtumishi wako, mafanikio kwa kunipa kibali mbele ya mtu huyu.”
Kwa maana nilikuwa mnyweshaji wa mfalme.
-
1 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia. 2 Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Naenda kuwaandalia makao. 3 Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo. 4 Ninyi mnajua njia ya kufika ninakokwenda.”
5 Tomaso akamwambia, “Bwana, sisi hatujui unakokwenda, tutaijuaje njia?”
6 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu.
-
8 Zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara tupu nikiyalinganisha na faida kubwa ipitayo kiasi cha kumjua Kristo Yesu Bwana wangu, ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote, nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Kristo. 9 Nami nionekane mbele zake bila kuwa na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu kwa njia ya imani. 10 Nataka nimjue Kristo na uweza wa kufufuka kwake na ushirika wa mateso yake, ili nifanane naye katika mauti yake, 11 ili kwa njia yoyote niweze kufikia ufufuo wa wafu.
12 Si kwamba nimekwisha kufikia, au kwamba nimekwisha kuwa mkamilifu, la hasha! Bali nakaza mwendo ili nipate kile ambacho kwa ajili yake, nimeshikwa na Kristo Yesu. 13 Ndugu zangu, sijihesabu kuwa nimekwisha kushika. Lakini ninafanya jambo moja: Ninasahau mambo yale yaliyopita, nakaza mwendo kufikia yale yaliyo mbele. 14 Nakaza mwendo nifikie ile alama ya ushindi iliyowekwa ili nipate tuzo ya mwito mkuu wa Mungu ambao nimeitiwa huko juu mbinguni katika Kristo Yesu.
-
12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
-
10 Lakini wewe umeyajua mafundisho yangu, mwenendo, makusudi, imani, uvumilivu, upendo, ustahimilivu, 11 mateso na taabu, yaani mambo yote yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Listra, mateso yote niliyostahimili, lakini Bwana aliniokoa katika hayo yote. 12 Naam, yeyote anayetaka kuishi maisha ya utauwa ndani ya Kristo Yesu atateswa. 13 Lakini watu waovu na wadanganyaji watazidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. 14 Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani, 15 na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. 16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, 17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.
-
18 Lakini kumbukeni Bwana Mungu wenu, ndiye ambaye huwapa uwezo wa kupata utajiri, na hivyo kulithibitisha Agano lake, ambalo aliwaapia baba zenu, kama ilivyo leo.
-
KITABU CHA KWANZA
1 Heri mtu yule ambaye
haendi katika shauri la watu waovu,
wala hasimami katika njia ya wenye dhambi,
au kuketi katika baraza la wenye mizaha.
2 Bali huifurahia sheria ya Bwana,
naye huitafakari hiyo sheria usiku na mchana.
3 Mtu huyo ni kama mti uliopandwa
kando ya vijito vya maji,
ambao huzaa matunda kwa majira yake
na majani yake hayanyauki.
Lolote afanyalo hufanikiwa.
-
3 Mtumaini Bwana na utende yaliyo mema;
Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama.
4 Jifurahishe katika Bwana
naye atakupa haja za moyo wako.
5 Mkabidhi Bwana njia yako,
mtumaini yeye, naye atatenda hili:
-
21 Bwana alikuwa pamoja naye, akamhurumia na kumpa kibali mbele ya msimamizi wa gereza. 22 Kwa hiyo msimamizi wa gereza akamweka Yosefu awe mkuu wa wafungwa pamoja na kusimamia yote ambayo yalitendeka mle gerezani. 23 Msimamizi wa gereza hakujishughulisha tena na kitu chochote kilichokuwa chini ya uangalizi wa Yosefu, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja na Yosefu akimfanikisha kwa kila alichofanya.
-
1 Mwanangu, kama utayakubali maneno yangu
na kuyaweka akiba maagizo yangu ndani mwako,
2 kutega sikio lako kwenye hekima
na kuweka moyo wako katika ufahamu,
3 na kama ukiita busara
na kuita kwa sauti ufahamu,
4 na kama utaitafuta kama fedha
na kuitafuta sana kama hazina iliyofichwa,
5 ndipo utakapoelewa kumcha Bwana
na kupata maarifa ya Mungu.
6 Kwa maana Bwana hutoa hekima,
na kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.
7 Anahifadhi ushindi kwa ajili ya mwadilifu,
yeye ni ngao kwa wale wasio na lawama,
8 kwa kuwa hulinda mwenendo wa mwenye haki
na kuhifadhi njia ya waaminifu wake.
-
22 Mipango hushindwa kufanikiwa kwa ajili ya kukosa ushauri,
bali kukiwa na washauri wengi hufanikiwa.
-
7 Tangu wakati wa baba zenu mmegeukia mbali na amri zangu nanyi hamkuzishika. Nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
“Lakini mnauliza, ‘Tutarudi kwa namna gani?’
8 “Je, mwanadamu atamwibia Mungu? Hata hivyo mnaniibia mimi.
“Lakini mnauliza, ‘Tunakuibia kwa namna gani?’
“Mnaniibia zaka na dhabihu. 9 Mko chini ya laana, ninyi taifa lote, kwa sababu mnaniibia mimi. 10 Leteni zaka kamili ghalani, ili kuwe na chakula katika nyumba yangu. Nijaribuni katika hili,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, “nanyi mwone kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni na kuwamwagieni baraka nyingi mpaka mkose nafasi ya kutosha. 11 Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu, wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. 12 “Ndipo mataifa yote yatawaita mliobarikiwa, kwa maana nchi yenu itakuwa ya kupendeza sana,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
-
33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia.
-
34 Lakini Farisayo mmoja, jina lake Gamalieli, aliyekuwa mwalimu wa sheria, aliyeheshimiwa na watu wote, akasimama mbele ya baraza akaamuru mitume watolewe nje kwa muda. 35 Ndipo alipowaambia wajumbe wa baraza, “Enyi watu wa Israeli, fikirini kwa uangalifu mnayotaka kuwatendea watu hawa. 36 Kwa maana wakati uliopita, aliinuka mtu mmoja jina lake Theuda, alijidai kuwa yeye ni mtu maarufu, akapata wafuasi wapatao 400 walioambatana naye. Lakini aliuawa, na wafuasi wake wote wakatawanyika, wakawa si kitu. 37 Baada yake, alitokea Yuda Mgalilaya wakati wa kuorodhesha watu, naye akaongoza kundi la watu kuasi. Yeye pia aliuawa, nao wafuasi wake wakatawanyika. 38 Kwa hiyo, kwa habari ya jambo hili nawashauri, jiepusheni na watu hawa. Waacheni waende zao! Kwa maana kama kusudi lao na shughuli yao imetokana na mwanadamu, haitafanikiwa. 39 Lakini ikiwa imetoka kwa Mungu, hamtaweza kuwazuia watu hawa. Badala yake mtajikuta mnapigana na Mungu.”
-
8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.
-
2 Katika kiburi chake, mwovu humtesa maskini,
waovu na wanaswe katika hila wanazozitunga.
3 Hujivunia tamaa za moyo wake;
humbariki mlafi na kumtukana Bwana.
4 Katika kiburi chake, mwovu hamtafuti Mungu,
katika mawazo yake yote
hakuna nafasi ya Mungu.
5 Njia zake daima hufanikiwa;
hujivuna na amri zako ziko mbali naye,
huwacheka kwa dharau adui zake wote.
6 Anajisemea mwenyewe, “Hakuna kitakachonitikisa,
daima nitakuwa na furaha,
kamwe sitakuwa na shida.”
-
16 Kisha akawaambia mfano huu: “Shamba la mtu mmoja tajiri lilizaa sana. 17 Akawaza moyoni mwake, ‘Nifanye nini? Sina mahali pa kuhifadhi mavuno yangu.’
18 “Ndipo huyo tajiri akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu za nafaka na kujenga nyingine kubwa zaidi na huko nitayahifadhi mavuno yangu yote na vitu vyangu. 19 Nami nitaiambia nafsi yangu, “Nafsi, unavyo vitu vingi vizuri ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi. Pumzika; kula, unywe, ufurahi.” ’
20 “Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe! Usiku huu uhai wako unatakiwa. Sasa hivyo vitu ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani?’
21 “Hivyo ndivyo ilivyo kwa wale wanaojiwekea mali lakini hawajitajirishi kwa Mungu.”
-
6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.
-
1 Lakini yakupasa ufahamu jambo hili, kwamba siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari. 2 Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kumkufuru Mungu, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio watakatifu, 3 wasio na upendo, wasiopenda kupatanishwa, wasingiziaji, wasiozuia tamaa zao, wakatili, wasiopenda mema, 4 wasaliti, wakaidi, waliojaa majivuno, wapendao anasa zaidi kuliko kumpenda Mungu: 5 wakiwa na mfano wa utauwa kwa nje, lakini wakizikana nguvu za Mungu. Jiepushe na watu wa namna hiyo.
6 Miongoni mwao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu na kuwachukua mateka wanawake wajinga, waliolemewa na dhambi zao na kuyumbishwa na aina zote za tamaa mbaya. 7 Wakijifunza siku zote lakini kamwe wasiweze kufikia ujuzi wa kweli.
Shows Read in context, Share and Copy.