55 Bible Verses About Prosperity

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Prosperity
  1. 6 Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu. 7 Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. 8 Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema. 9 Kama ilivyoandikwa:

    “Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu

    akawapa maskini;

    haki yake hudumu milele.”

    10 Yeye ampaye mpanzi mbegu kwa ajili ya kupanda na mkate kuwa chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu. 11 Mtatajirishwa kwa kila namna ili mpate kuwa wakarimu kila wakati, na kupitia kwetu, ukarimu wenu utamletea Mungu shukrani.

    12 Huduma hii mnayofanya si tu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watakatifu, bali huzidi sana kwa shukrani nyingi apewazo Mungu.

  2. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ndiye mchungaji wangu,

    sitapungukiwa na kitu.

    2 Hunilaza katika malisho

    ya majani mabichi,

    kando ya maji matulivu huniongoza,

    3 hunihuisha nafsi yangu.

    Huniongoza katika njia za haki

    kwa ajili ya jina lake.

  3. 7 “Ninakuomba vitu viwili, Ee Bwana;

    usininyime kabla sijafa:

    8 Uutenge mbali nami udanganyifu na uongo;

    usinipe umaskini wala utajiri,

    bali unipe chakula cha kunitosha kila siku.

    9 Nisije nikawa na vingi vya kuzidi nikakukana

    na kusema, ‘Bwana ni nani?’

    Au nisije nikawa maskini nikaiba,

    nami nikaliaibisha jina la Mungu wangu.

  4. 11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. 12 Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. 14 Nitaonekana kwenu,” asema Bwana, “nami nitawarudisha watu wenu waliotekwa. Nitawakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipokuwa nimewafukuzia, nami nitawarudisha mahali ambapo nilikuwa nimewatoa walipochukuliwa uhamishoni,” asema Bwana.

  5. 6 Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa. 7 Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu chochote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu. 8 Lakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo. 9 Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka huanguka kwenye majaribu, na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi. 10 Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.

    11 Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole.

  6. 17 Mnaweza kusema, “Uwezo wangu na nguvu za mikono yangu ndizo zilizonipatia utajiri huu.” 18 Lakini kumbukeni Bwana Mungu wenu, ndiye ambaye huwapa uwezo wa kupata utajiri, na hivyo kulithibitisha Agano lake, ambalo aliwaapia baba zenu, kama ilivyo leo.

    19 Ikiwa mtamsahau Bwana Mungu wenu, mkaifuata miungu mingine, mkaiabudu na kuisujudia, ninashuhudia dhidi yenu leo kwamba hakika mtaangamizwa. 20 Kama mataifa Bwana aliyoyaangamiza mbele yenu, ndivyo ninyi mtakavyoangamizwa kwa kutokumtii Bwana Mungu wenu.

  7. 2 Mpendwa, naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya njema kama vile roho yako ifanikiwavyo.

  8. 7 Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. 8 Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”

  9. 8 “Je, mwanadamu atamwibia Mungu? Hata hivyo mnaniibia mimi.

    “Lakini mnauliza, ‘Tunakuibia kwa namna gani?’

    “Mnaniibia zaka na dhabihu. 9 Mko chini ya laana, ninyi taifa lote, kwa sababu mnaniibia mimi. 10 Leteni zaka kamili ghalani, ili kuwe na chakula katika nyumba yangu. Nijaribuni katika hili,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, “nanyi mwone kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni na kuwamwagieni baraka nyingi mpaka mkose nafasi ya kutosha. 11 Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu, wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. 12 “Ndipo mataifa yote yatawaita mliobarikiwa, kwa maana nchi yenu itakuwa ya kupendeza sana,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

  10. KITABU CHA KWANZA

    1 Heri mtu yule ambaye

    haendi katika shauri la watu waovu,

    wala hasimami katika njia ya wenye dhambi,

    au kuketi katika baraza la wenye mizaha.

    2 Bali huifurahia sheria ya Bwana,

    naye huitafakari hiyo sheria usiku na mchana.

    3 Mtu huyo ni kama mti uliopandwa

    kando ya vijito vya maji,

    ambao huzaa matunda kwa majira yake

    na majani yake hayanyauki.

    Lolote afanyalo hufanikiwa.

  11. 19 “Msijiwekee hazina duniani, mahali ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi huvunja na kuiba. 20 Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba. 21 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.

    22 “Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni nyofu, mwili wako wote utajaa nuru. 23 Lakini kama jicho lako ni ovu, mwili wako wote utajawa na giza. Kwa hiyo basi, kama nuru iliyomo ndani yako ni giza, hilo ni giza kuu namna gani!

    24 “Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.

  12. 9 Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri.

  13. 9 Mheshimu Bwana kwa mali zako na

    kwa malimbuko ya mazao yako yote;

    10 ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika,

    viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya.

  14. 22 Baraka ya Bwana hutajirisha,

    wala haichanganyi huzuni.

  15. 31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia.

  16. 10 Kisha mataifa yote ya dunia wataona kuwa unaitwa kwa jina la Bwana, nao watakuogopa. 11 Bwana atakupa kustawi kwa wingi, katika tunda la uzao wa tumbo lako, katika wanyama wachanga wa mifugo yako na katika mazao ya ardhi yako, katika nchi aliyowaapia baba zako kuwapa.

    12 Bwana atafungua mbingu, ghala zake za baraka, kukupa mvua kwa majira yake na kubariki kazi zako zote za mikono yako. Utakopesha mataifa mengi lakini hutakopa kwa yeyote. 13 Bwana atakufanya kichwa, wala si mkia. Kama utazingatia maagizo ya Bwana Mungu wako ninayokupa siku hii ya leo na kuyafuata kwa bidii, daima utakuwa juu, kamwe hutakuwa chini. 14 Usihalifu amri zangu zozote ninazokupa leo, kwa kwenda kuume au kushoto, kwa kufuata miungu mingine na kuitumikia.

  17. 11 Kwa kuwa Bwana ni jua na ngao,

    Bwana hutoa wema na heshima;

    hakuna kitu chema anachowanyima

    wale ambao hawana hatia.

    12 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote,

    heri ni mtu yule anayekutumaini wewe.

  18. 15 Zaidi ya hayo, ninyi Wafilipi mnajua kwamba siku za kwanza nilipoanza kuhubiri Injili, nilipoondoka Makedonia, hakuna kanisa jingine lililoshiriki nami katika masuala ya kutoa na kupokea isipokuwa ninyi. 16 Kwa maana hata nilipokuwa huko Thesalonike, mliniletea msaada kwa ajili ya mahitaji yangu zaidi ya mara moja. 17 Si kwamba natafuta sana yale matoleo, bali natafuta sana ile faida itakayozidi sana kwa upande wenu. 18 Nimelipwa kikamilifu hata na zaidi; nimetoshelezwa kabisa sasa, kwa kuwa nimepokea kutoka kwa Epafrodito vile vitu mlivyonitumia, sadaka yenye harufu nzuri, dhabihu inayokubalika na ya kumpendeza Mungu. 19 Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu.

  19. 1 Wakati huu Yosefu alikuwa amechukuliwa mpaka Misri. Mmisri aliyeitwa Potifa aliyekuwa mmojawapo wa maafisa wa Farao, mkuu wa ulinzi, akamnunua Yosefu kutoka kwa Waishmaeli waliomleta Misri.

    2 Bwana alikuwa pamoja na Yosefu, naye akastawi, Yosefu akaishi nyumbani kwa bwana wake Mmisri. 3 Potifa alipoona kuwa Bwana alikuwa pamoja na Yosefu na kwamba Bwana alimfanikisha kwa kila kitu alichokifanya, 4 Yosefu alipata kibali machoni pa Potifa, akamfanya mhudumu wake. Potifa akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, naye akamkabidhi kuwa mwangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho. 5 Kuanzia wakati huo Potifa alipomweka Yosefu kuwa msimamizi wa nyumba na mali zake zote alizokuwa nazo, Bwana aliibariki nyumba ya Mmisri huyo kwa sababu ya Yosefu. Baraka ya Bwana ilikuwa juu ya kila kitu alichokuwa nacho Potifa, nyumbani na shambani. 6 Kwa hiyo Potifa akamwachia Yosefu uangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho, Yosefu alipokuwa katika uongozi, Potifa hakuwa na sababu ya kujishughulisha na kitu chochote isipokuwa chakula alichokula.

    Yosefu alikuwa mwenye umbo zuri na sura ya kuvutia;

  20. 27 Wale wanaofurahia hukumu yangu ya haki

    wapige kelele za shangwe na furaha;

    hebu waseme siku zote, “Bwana atukuzwe,

    ambaye amefurahia mafanikio ya mtumishi wake.”

  21. 3 Mtumaini Bwana na utende yaliyo mema;

    Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama.

    4 Jifurahishe katika Bwana

    naye atakupa haja za moyo wako.

    5 Mkabidhi Bwana njia yako,

    mtumaini yeye, naye atatenda hili:

  22. 24 Kuna mtu atoaye kwa ukarimu, hata hivyo hupata zaidi,

    mwingine huzuia, lakini huwa maskini.

    25 Mtu mkarimu atastawi;

    yeye awaburudishaye wengine

    ataburudishwa mwenyewe.

  23. 4 Mvivu hutamani sana na hapati kitu,

    bali nafsi ya mwenye bidii

    hutoshelezwa kikamilifu.

  24. 20 Hivi ndivyo Hezekia alivyofanya katika Yuda yote, akifanya lile lililo jema, sawa na la uaminifu mbele za Bwana Mungu wake. 21 Naye katika kila kitu alichofanya katika huduma kwenye Hekalu la Mungu na katika utii kwa sheria na amri, alimtafuta Mungu wake na kufanya kazi kwa moyo wake wote. Naye hivyo akafanikiwa.

  25. Wimbo wa kwenda juu.

    1 Heri ni wale wote wamchao Bwana,

    waendao katika njia zake.

    2 Utakula matunda ya kazi yako;

    baraka na mafanikio vitakuwa vyako.

  26. 38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”

  27. 1 Siku zilipokaribia za Daudi kufa, akampa mwanawe Solomoni agizo.

    2 Akasema, “Mimi ninakaribia kwenda njia ya dunia yote. Hivyo uwe hodari, jionyeshe kuwa mwanaume, 3 shika lile Bwana Mungu wako analokuagiza: Enenda katika njia zake, ushike maagizo na amri zake, sheria zake na kanuni zake, kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Mose, ili upate kustawi katika yote ufanyayo na popote uendako, 4 ili kwamba Bwana aweze kunitimizia ahadi yake: ‘Kama wazao wako wakiangalia sana wanavyoishi, na kama wakienenda kwa uaminifu mbele zangu kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote, kamwe hutakosa kuwa na mtu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli.’

  28. 8 Onjeni mwone kwamba Bwana ni mwema,

    heri mtu yule anayemkimbilia.

    9 Mcheni Bwana enyi watakatifu wake,

    kwa maana wale wamchao

    hawapungukiwi na chochote.

    10 Wana simba wenye nguvu

    hutindikiwa na kuona njaa,

    bali wale wamtafutao Bwana

    hawatakosa kitu chochote kilicho chema.

    11 Njooni, watoto wangu, mnisikilize,

    nitawafundisha kumcha Bwana.

  29. 25 Mtu mwenye tamaa huchochea fitina,

    bali yule amtegemeaye Bwana atafanikiwa.

  30. 13 Mtu mmoja katika umati wa watu akamwambia Yesu, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane naye urithi wetu.”

    14 Lakini Yesu akamwambia, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa hakimu wenu au msuluhishi juu yenu?” 15 Ndipo Yesu akawaambia, “Jihadharini! Jilindeni na aina zote za choyo. Kwa maana maisha ya mtu hayatokani na wingi wa mali alizo nazo.”

    16 Kisha akawaambia mfano huu: “Shamba la mtu mmoja tajiri lilizaa sana. 17 Akawaza moyoni mwake, ‘Nifanye nini? Sina mahali pa kuhifadhi mavuno yangu.’

    18 “Ndipo huyo tajiri akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu za nafaka na kujenga nyingine kubwa zaidi na huko nitayahifadhi mavuno yangu yote na vitu vyangu. 19 Nami nitaiambia nafsi yangu, “Nafsi, unavyo vitu vingi vizuri ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi. Pumzika; kula, unywe, ufurahi.” ’

    20 “Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe! Usiku huu uhai wako unatakiwa. Sasa hivyo vitu ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani?’

    21 “Hivyo ndivyo ilivyo kwa wale wanaojiwekea mali lakini hawajitajirishi kwa Mungu.”

  31. 7 Mlipeni kila mtu kile mnachodaiwa. Kama mnadaiwa kodi lipeni kodi, kama ni ushuru, lipeni ushuru, astahiliye hofu, mhofu, astahiliye heshima, mheshimu.

    8 Msidaiwe kitu na mtu yeyote, isipokuwa kupendana, kwa maana yeye ampendaye mwenzake, ameitimiza sheria. 9 Kwa kuwa amri hizi zisemazo, “Usizini,” “Usiue,” “Usiibe,” “Usitamani,” na amri nyingine zote, zinajumlishwa katika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”

  32. 6 Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote.

    7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. 8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. 9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. 10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.

  33. 2 Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3 kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. 4 Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu chochote. 5 Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa. 6 Lakini anapoomba, lazima aamini wala asiwe na shaka, kwa sababu mtu aliye na shaka ni kama wimbi la bahari, lililochukuliwa na upepo na kutupwa huku na huku. 7 Mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapata kitu chochote kutoka kwa Bwana.

  34. 14 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika:

    “Haya ndiyo maneno yake yeye aliye Amen, shahidi mwaminifu na wa kweli, mtawala wa uumbaji wote wa Mungu. 15 Nayajua matendo yako, ya kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungelikuwa moja au lingine. 16 Hivyo kwa kuwa u vuguvugu, si baridi wala moto, nitakutapika utoke kinywani mwangu. 17 Kwa maana unasema: ‘Mimi ni tajiri, nimejilimbikizia mali, wala sihitaji kitu chochote.’ Lakini hutambui ya kwamba wewe ni mnyonge, wa kuhurumiwa, maskini, kipofu, tena uliye uchi. 18 Nakushauri ununue kutoka kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, ili upate kuwa tajiri, na mavazi meupe ili uyavae upate kuficha aibu ya uchi wako, na mafuta ya kupaka macho yako ili upate kuona.

    19 “Wale niwapendao, ninawakemea na kuwaadibisha. Hivyo uwe na bidii ukatubu.

  35. 17 Nawapenda wale wanipendao,

    na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.

    18 Utajiri na heshima viko kwangu,

    utajiri udumuo na mafanikio.

    19 Tunda langu ni bora kuliko dhahabu safi;

    kile nitoacho hupita fedha iliyo bora.

    20 Natembea katika njia ya unyofu

    katika mapito ya haki,

    21 nawapa utajiri wale wanipendao

    na kuzijaza hazina zao.

  36. 10 Mwizi huja ili aibe, kuua na kuangamiza. Mimi nimekuja ili wapate uzima kisha wawe nao tele.

  37. 12 Isaki akapanda mazao katika nchi hiyo, kwa mwaka huo huo, akavuna mara mia, kwa sababu Bwana alimbariki. 13 Isaki akawa tajiri, mali zake zikaendelea kuongezeka mpaka akawa tajiri sana. 14 Akawa na mifugo ya kondoo na ngʼombe, na watumishi wengi sana, kiasi kwamba Wafilisti wakamwonea wivu.

  38. 7 Bwana humfanya mtu maskini naye hutajirisha,

    hushusha na hukweza.

    8 Humwinua maskini kutoka mavumbini

    na humwinua mhitaji kutoka lundo la majivu;

    huwaketisha pamoja na wakuu

    na kuwafanya warithi kiti cha enzi cha heshima.

    “Kwa kuwa misingi ya dunia ni ya Bwana;

    juu yake ameuweka ulimwengu.

    9 Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake,

    lakini waovu watanyamazishwa kwenye giza.

    “Si kwa nguvu mtu hushinda;

  39. 23 Kama Bwana akipendezwa na njia ya mtu,

    yeye huimarisha hatua zake,

    24 ajapojikwaa, hataanguka,

    kwa maana Bwana

    humtegemeza kwa mkono wake.

    25 Nilikuwa kijana na sasa ni mzee,

    lakini sijaona kamwe wenye haki wameachwa

    au watoto wao wakiombaomba chakula.

    26 Wakati wote ni wakarimu na hukopesha bila masharti.

    Watoto wao watabarikiwa.

  40. 2 Hazina zilizopatikana kwa njia mbaya hazifai,

    lakini uadilifu huokoa kutoka mautini.

    3 Bwana hawaachi waadilifu kukaa njaa,

    lakini hupinga tamaa ya mtu mwovu.

    4 Mikono mivivu hufanya mtu kuwa maskini

    lakini mikono yenye bidii huleta utajiri.

    5 Yeye akusanyaye mazao wakati wa kiangazi

    ni mwana mwenye hekima,

    lakini yeye alalaye wakati wa mavuno

    ni mwana mwenye kuaibisha.

    6 Baraka huwa taji kichwani mwa mwenye haki,

    lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.

  41. 3 “ ‘Ikiwa mtafuata amri zangu na kuwa waangalifu kutii maagizo yangu, 4 nitawanyeshea mvua katika majira yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, na miti ya mashambani itazaa matunda yake. 5 Kupura nafaka kwenu kutaendelea mpaka wakati wa kuvuna zabibu. Pia kuvuna zabibu kutaendelea mpaka wakati wa kupanda mbegu, nanyi mtakula na kushiba, na mtaishi salama katika nchi yenu.

  42. 1 Kama ukimtii Bwana Mungu wako kwa bidii na kufuata amri zake zote ninazokupa leo kwa bidii, Bwana Mungu wako atakuweka juu ya mataifa yote katika dunia. 2 Baraka hizi zote zitakuja juu yako na kukupata, kama ukimtii Bwana Mungu wako:

  43. 15 Yeshuruni alinenepa na kupiga teke;

    alikuwa na chakula tele,

    akawa mzito na akapendeza sana.

    Akamwacha Mungu aliyemuumba,

    na kumkataa Mwamba Mwokozi wake.

  44. 11 Bali wanyenyekevu watairithi nchi

    na wafurahie amani tele.

  45. 1 Heri kuchagua jina jema kuliko utajiri mwingi,

    kuheshimiwa ni bora kuliko fedha au dhahabu.

    2 Tajiri na maskini wanafanana kwa hili:

    Bwana ni Muumba wao wote.

  46. 11 Hekima, kama ulivyo urithi, ni kitu chema

    na huwafaidia wale walionalo jua.

    12 Hekima ni ulinzi kama fedha ilivyo ulinzi,

    lakini faida ya maarifa ni hii:

    kwamba hekima huhifadhi maisha ya aliye nayo.

    13 Tafakari kile Mungu alichokitenda:

    Nani awezaye kunyoosha

    kile ambacho yeye amekipinda?

    14 Nyakati zikiwa nzuri, ufurahi,

    lakini nyakati zikiwa mbaya, tafakari:

    Mungu amefanya hiyo moja,

    naam, sanjari na hiyo nyingine.

    Kwa hiyo, mwanadamu hawezi kugundua

    kitu chochote kuhusu maisha yake ya baadaye.

  47. 5 Hili ndilo asemalo Bwana:

    “Amelaaniwa yeye amtegemeaye mwanadamu,

    ategemeaye mwenye mwili

    kwa ajili ya nguvu zake,

    ambaye moyo wake

    umemwacha Bwana.

    6 Atakuwa kama kichaka cha jangwani;

    hataona mafanikio yatakapokuja.

    Ataishi katika sehemu zisizo na maji,

    katika nchi ya chumvi ambapo

    hakuna yeyote aishiye humo.

    7 “Lakini amebarikiwa mtu ambaye tumaini lake ni katika Bwana,

    ambaye matumaini yake ni katika Bwana.

    8 Atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji

    uenezao mizizi yake karibu na kijito cha maji.

    Hauogopi wakati wa joto ujapo;

    majani yake ni mabichi daima.

    Hauna hofu katika mwaka wa ukame

    na hautaacha kuzaa matunda.”

  48. 1 Israeli alikuwa mzabibu uliostawi sana,

    alijizalia matunda mwenyewe.

    Kadiri matunda yake yalivyoongezeka,

    alijenga madhabahu zaidi;

    kadiri nchi yake ilivyostawi,

    alipamba mawe yake ya ibada.

    2 Moyo wao ni mdanganyifu,

    nao sasa lazima wachukue hatia yao.

    Bwana atabomoa madhabahu zao

    na kuharibu mawe yao ya ibada.

  49. 11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

  50. 1 Ni kitu gani kinachosababisha mapigano na ugomvi miongoni mwenu? Je, haya hayatokani na tamaa zenu zinazoshindana ndani yenu? 2 Mnatamani lakini hampati, kwa hiyo mwaua. Mwatamani kupata lakini hampati vile mnavyotaka, kwa hiyo mnajitia katika magomvi na mapigano. Mmepungukiwa kwa sababu hammwombi Mungu. 3 Mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya, ili mpate kuvitumia hivyo mtakavyopata kwa tamaa zenu.

    4 Ninyi wanaume na wanawake wazinzi, hamjui ya kwamba urafiki na dunia ni uadui na Mungu? Kwa hiyo mtu yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hufanyika adui wa Mungu.

  51. 27 Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,

    kwa mfano wa Mungu alimuumba;

    mwanaume na mwanamke aliwaumba.

    28 Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”

    29 Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote, na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa chakula chenu. 30 Nao wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani, na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi: yaani kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo.

  52. 1 Bwana akawa amemwambia Abramu, “Ondoka kutoka nchi yako, uache jamii yako na nyumba ya baba yako, uende hadi nchi nitakayokuonyesha.

    2 “Mimi nitakufanya taifa kubwa

    na nitakubariki,

    Nitalikuza jina lako,

    nawe utakuwa baraka.

    3 Nitawabariki wale wanaokubariki,

    na yeyote akulaaniye nitamlaani;

    na kupitia kwako mataifa yote duniani

    yatabarikiwa.”

  53. 23 Kama ukimrudia Mwenyezi, utarudishwa upya:

    Kama ukiuondoa uovu uwe mbali na hema lako,

    24 kama dhahabu yako ukiihesabu kama mavumbi,

    dhahabu yako ya Ofiri kama miamba ya mabondeni,

    25 ndipo Mwenyezi atakuwa dhahabu yako,

    naye atakuwa fedha yako iliyo bora.

    26 Hakika ndipo utakapojifurahisha kwa Mwenyezi,

    nawe utamwinulia Mungu uso wako.

    27 Utamwomba yeye, naye atakusikia,

    nawe utazitimiza nadhiri zako.

  54. 23 Kazi zote zinazofanywa kwa bidii huleta faida,

    bali mazungumzo matupu huelekea umaskini tu.

  55. 32 Ikiwa Mungu hakumhurumia Mwanawe, bali alimtoa kwa ajili yetu sote, atakosaje basi kutupatia vitu vyote kwa ukarimu pamoja naye?