77 Bible Verses About Missions
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
16 Basi wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda hadi Galilaya kwenye ule mlima ambao Yesu alikuwa amewaagiza. 17 Walipomwona, wakamwabudu; lakini baadhi yao wakaona shaka. 18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”
-
Safari Ya Kwanza Ya Paulo Kueneza Injili
1 Katika kanisa huko Antiokia ya Shamu walikuwako manabii na walimu, yaani: Barnaba, Simeoni aitwaye Nigeri, Lukio Mkirene, Manaeni aliyekuwa amelelewa pamoja na Mfalme Herode Agripa, na Sauli. 2 Walipokuwa wakimwabudu Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, “Nitengeeni Sauli na Barnaba kwa kazi ile maalum niliyowaitia.” 3 Ndipo baada ya kufunga na kuomba, wakawawekea mikono yao na wakawatuma waende zao.
4 Hivyo, wakiwa wametumwa na Roho Mtakatifu, wakashuka kwenda Seleukia na kutoka huko wakasafiri baharini mpaka kisiwa cha Kipro. 5 Walipowasili katika mji wa Salami, wakahubiri neno la Mungu katika sinagogi la Wayahudi. Pia walikuwa na Yohana Marko kuwa msaidizi wao.
-
11 Kama yasemavyo Maandiko, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.” 12 Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. 13 Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.”
14 Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? 15 Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri habari njema!”
-
4 Wakati mmoja alipokuwa pamoja nao, aliwapa amri hii, “Msitoke Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba, ambayo mmenisikia nikisema habari zake. 5 Yohana aliwabatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”
6 Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamuuliza Yesu, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?”
7 Yesu akawaambia, “Si juu yenu kujua nyakati na majira ambayo Baba ameyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. 8 Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.”
-
15 Akawaambia, “Enendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. 16 Yeyote aaminiye na kubatizwa ataokoka. Lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa. 17 Nazo ishara hizi zitafuatana na wanaoamini: Kwa Jina langu watatoa pepo wachafu; watasema kwa lugha mpya; 18 watashika nyoka kwa mikono yao; na hata wakinywa kitu chochote cha kuua, hakitawadhuru kamwe; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona.”
-
44 Akawaambia, “Haya ndiyo yale niliyowaambia nilipokuwa bado niko pamoja nanyi, kwamba yote yaliyoandikwa kunihusu mimi katika Sheria ya Mose, Manabii na Zaburi hayana budi kutimizwa.”
45 Ndipo akafungua fahamu zao ili waweze kuyaelewa Maandiko. 46 Akawaambia, “Haya ndiyo yaliyoandikwa: Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu. 47 Toba na msamaha wa dhambi zitatangaziwa mataifa yote kupitia jina lake kuanzia Yerusalemu. 48 Ninyi ni mashahidi wa mambo haya.
49 “Tazama nitawatumia ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini hadi mtakapovikwa uwezo utokao juu.”
-
2 Dumuni sana katika maombi, mkikesha katika hayo pamoja na kushukuru. 3 Pia tuombeeni na sisi ili Mungu atufungulie mlango wa kunena, ili tupate kuitangaza siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake pia mimi nimefungwa. 4 Ombeni ili nipate kuitangaza Injili kwa udhahiri kama ipasavyo kunena. 5 Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. 6 Maneno yenu yawe yamejaa neema siku zote, yanayofaa, ili mjue jinsi iwapasavyo na inavyofaa kumjibu kila mtu.
-
1 Baada ya hayo, Bwana akawachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawili wawili katika kila mji na kila sehemu aliyokusudia kwenda baadaye. 2 Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini watendakazi ni wachache. Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watendakazi katika shamba lake la mavuno. 3 Haya! nendeni. Ninawatuma kama wana-kondoo katikati ya mbwa mwitu.
-
35 Yesu akazunguka katika miji yote na vijiji vyote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi. 36 Alipoona makutano, aliwahurumia kwa sababu walikuwa wanasumbuka bila msaada, kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. 37 Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache. 38 Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watendakazi katika shamba lake la mavuno.”
-
19 Ikawa jioni ya ile siku ya kwanza ya juma, wanafunzi wake walikuwa pamoja, milango ikiwa imefungwa kwa kuwaogopa Wayahudi. Naye Yesu aliwatokea, akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!” 20 Baada ya kusema haya, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Wanafunzi wake wakafurahi sana walipomwona Bwana.
21 Yesu akawaambia tena, “Amani iwe nanyi! Kama vile Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawatuma ninyi.” 22 Naye alipokwisha kusema haya, akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. 23 Mkimwondolea mtu yeyote dhambi zake, zitaondolewa, na yeyote msiyemwondolea dhambi zake, hazitaondolewa.”
-
Safari Ya Pili Ya Paulo Kueneza Injili
36 Baada ya muda, Paulo akamwambia Barnaba, “Turudi tukawatembelee ndugu katika miji yote tuliyohubiri neno la Bwana tuone jinsi wanavyoendelea.” 37 Barnaba alitaka wamchukue Yohana aitwaye Marko waende naye. 38 Lakini Paulo aliona si vyema kwa sababu aliwahi kuwaacha walipokuwa huko Pamfilia, hakutaka kuendelea kufanya kazi naye. 39 Pakatokea ubishi mkali kati ya Paulo na Barnaba kuhusu jambo hili, hivyo wakagawanyika. Barnaba akamchukua Yohana Marko wakasafiri baharini kwenda Kipro. 40 Lakini Paulo akamchagua Sila na akaondoka baada ya ndugu kuwatakia neema ya Bwana. 41 Akapitia Shamu na Kilikia, akiimarisha makanisa ya huko.
-
8 Kisha nikasikia sauti ya Bwana ikisema, “Nimtume nani? Ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?”
Nami nikasema, “Mimi hapa. Nitume mimi!”
9 Akasema, “Nenda ukawaambie watu hawa:
“ ‘Mtaendelea daima kusikiliza,
lakini kamwe hamtaelewa;
mtaendelea daima kutazama,
lakini kamwe hamtatambua.’
10 Fanya mioyo ya watu hawa kuwa migumu,
fanya masikio yao yasisikie,
na upofushe macho yao.
Wasije wakaona kwa macho yao,
na wakasikiliza kwa masikio yao,
wakaelewa kwa mioyo yao,
nao wakageuka, nikawaponywa.”
11 Ndipo nikasema, “Hadi lini, Ee Bwana?”
Naye akanijibu:
“Hadi miji iwe imeachwa magofu
na bila wakazi,
hadi nyumba zitakapobaki bila watu,
na mashamba yatakapoharibiwa na kuangamizwa,
12 hadi Bwana atakapokuwa amekwisha kumpeleka kila mmoja mbali sana,
na nchi itakapokuwa imeachwa kabisa.
-
6 Kwa hiyo watu wangu watalijua Jina langu;
kwa hiyo katika siku ile watajua
kwamba ndimi niliyetangulia kulisema.
Naam, ni mimi.”
7 Tazama jinsi miguu ya wale waletao habari njema
ilivyo mizuri juu ya milima,
wale wanaotangaza amani,
wanaoleta habari njema,
wanaotangaza wokovu,
wauambiao Sayuni,
“Mungu wako anatawala!”
8 Sikiliza! Walinzi wako wanapaza sauti zao,
pamoja wanapaza sauti zao kwa furaha.
Wakati Bwana atakaporejea Sayuni,
wataliona kwa macho yao wenyewe.
9 Pazeni sauti ya nyimbo za furaha pamoja,
enyi magofu ya Yerusalemu,
kwa maana Bwana amewafariji watu wake,
ameikomboa Yerusalemu.
10 Mkono mtakatifu wa Bwana umefunuliwa
machoni pa mataifa yote,
nayo miisho yote ya dunia itaona
wokovu wa Mungu wetu.
-
19 Basi wale waliotawanyika kwa ajili ya mateso yaliyotokana na kifo cha Stefano, wakasafiri hadi Foinike na Kipro na Antiokia. Nao hawakuhubiri lile Neno kwa mtu yeyote isipokuwa Wayahudi. 20 Lakini baadhi yao walikuwepo watu wa Kipro na Kirene, ambao walipokuja Antiokia walinena na Wayunani pia wakiwahubiria habari njema za Bwana Yesu. 21 Mkono wa Bwana ulikuwa pamoja nao, nayo idadi kubwa ya watu wakaamini na kumgeukia Bwana.
22 Habari hizi zilipofika masikioni mwa kanisa huko Yerusalemu, wakamtuma Barnaba aende Antiokia. 23 Alipofika na kuona madhihirisho ya neema ya Mungu, akafurahi na kuwatia moyo waendelee kuwa waaminifu kwa Bwana kwa mioyo yao yote.
-
14 Injili ya Ufalme itahubiriwa ulimwenguni kote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Ndipo mwisho utakapokuja.
-
5 Baada ya kupitia Makedonia nitakuja kwenu, maana ninakusudia kupitia Makedonia. 6 Huenda nitakaa nanyi kwa muda, au hata kukaa nanyi kipindi chote cha baridi, ili mweze kunisaidia katika safari yangu, popote niendapo. 7 Kwa maana sitaki niwaone sasa na kupita tu; natarajia kuwa nanyi kwa muda wa kutosha, kama Bwana akipenda. 8 Lakini nitakaa Efeso mpaka wakati wa Pentekoste, 9 kwa maana mlango mkubwa umefunguliwa kwangu kufanya kazi yenye matunda, nako huko kuna adui wengi wanaonipinga.
-
7 Badala yake walitambua kwamba nilikuwa nimekabidhiwa kazi ya kuhubiri Injili kwa watu wa Mataifa, kama vile Petro alivyokabidhiwa kuhubiri Injili kwa Wayahudi. 8 Kwa maana, Mungu aliyekuwa akitenda kazi katika huduma ya Petro kama mtume kwa Wayahudi, ndiye pia aliyekuwa anatenda kazi katika huduma yangu kama mtume kwa watu wa Mataifa. 9 Basi, Yakobo, Kefa na Yohana, walioonekana kama nguzo za kanisa, walitupa mkono wa shirika, mimi na Barnaba walipotambua ile neema niliyopewa. Wakakubali kwamba sisi twende kwa watu wa Mataifa na wao waende kwa Wayahudi. 10 Walichotuomba ni kwamba tuendelee kuwakumbuka maskini, jambo ambalo ndilo nililokuwa na shauku ya kulifanya.
-
7 Akawaita wale kumi na wawili, akawatuma wawili wawili, na kuwapa mamlaka kutoa pepo wachafu.
8 Akawaagiza akisema, “Msichukue chochote kwa ajili ya safari isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kwenye mikanda yenu. 9 Vaeni viatu, lakini msivae nguo ya ziada.” 10 Akawaambia, “Mkiingia kwenye nyumba yoyote, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo. 11 Kama mahali popote hawatawakaribisha wala kuwasikiliza, mtakapoondoka huko, kungʼuteni mavumbi kutoka kwenye miguu yenu ili kuwa ushuhuda dhidi yao.”
-
14 Fanyeni mambo yote bila kunungʼunika wala kushindana, 15 ili msiwe na lawama wala hatia, bali mwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka, ambacho ndani yake ninyi mnangʼaa kama mianga ulimwenguni. 16 Mkilishika neno la uzima, ili nipate kuona fahari siku ya Kristo kwamba sikupiga mbio wala kujitaabisha bure. 17 Lakini hata kama nikimiminwa kama sadaka ya kinywaji kwenye dhabihu na huduma itokayo katika imani yenu, mimi ninafurahi na kushangilia pamoja nanyi nyote. 18 Vivyo hivyo, ninyi nanyi imewapasa kufurahi na kushangilia pamoja nami.
19 Natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo hivi karibuni aje kwenu, ili nipate kufarijika moyo nitakapopata habari zenu. 20 Sina mtu mwingine kama yeye, ambaye ataangalia hali yenu kwa halisi.
-
17 Lakini ili kuzuia jambo hili lisiendelee kuenea zaidi kwa watu, ni lazima tuwaonye watu hawa ili wasiseme tena na mtu yeyote kwa jina la Yesu.” 18 Kisha wakawaita tena ndani na kuwaamuru wasiseme wala kufundisha kamwe kwa hili jina la Yesu.
19 Lakini Petro na Yohana wakajibu, “Amueni ninyi wenyewe iwapo ni haki mbele za Mungu kuwatii ninyi kuliko kumtii Mungu. 20 Lakini sisi hatuwezi kuacha kusema yale tuliyoyaona na kuyasikia.”
-
18 Kwa maana sitathubutu kusema kitu chochote zaidi ya kile ambacho Kristo amefanya kwa kunitumia mimi katika kuwaongoza watu wa Mataifa wamtii Mungu kwa yale niliyosema na kufanya, 19 kwa nguvu za ishara na miujiza, kwa uweza wa Roho wa Mungu, hivyo kuanzia Yerusalemu hadi maeneo yote ya kandokando yake mpaka Iliriko, nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa ukamilifu. 20 Hivyo ni nia yangu kuhubiri Habari Njema, si pale ambapo Kristo amekwisha kujulikana, ili nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine. 21 Lakini kama ilivyoandikwa:
“Wale ambao hawajahubiriwa habari zake wataona,
nao wale ambao hawajazisikia watafahamu.”
-
1 Baada ya haya, Paulo akaondoka Athene akaenda Korintho. 2 Huko akakutana na Myahudi mmoja jina lake Akila, mwenyeji wa Ponto, ambaye alikuwa amewasili karibuni kutoka Italia pamoja na mkewe Prisila, kwa sababu Klaudio alikuwa ameamuru Wayahudi wote waondoke Rumi. Paulo akaenda kuwaona, 3 naye kwa kuwa alikuwa mtengeneza mahema kama wao, akakaa na kufanya kazi pamoja nao. 4 Kila Sabato Paulo alikuwa akihojiana nao katika sinagogi, akijitahidi kuwashawishi Wayahudi na Wayunani.
-
1 Bwana akawa amemwambia Abramu, “Ondoka kutoka nchi yako, uache jamii yako na nyumba ya baba yako, uende hadi nchi nitakayokuonyesha.
2 “Mimi nitakufanya taifa kubwa
na nitakubariki,
Nitalikuza jina lako,
nawe utakuwa baraka.
3 Nitawabariki wale wanaokubariki,
na yeyote akulaaniye nitamlaani;
na kupitia kwako mataifa yote duniani
yatabarikiwa.”
-
1 Mwimbieni Bwana wimbo mpya;
mwimbieni Bwana dunia yote.
2 Mwimbieni Bwana, lisifuni jina lake;
tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.
3 Tangazeni utukufu wake katikati ya mataifa,
matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.
-
13 “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.
14 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. 15 Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani ya ile nyumba. 16 Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
-
1 Yesu kisha akawaita wale kumi na wawili pamoja, akawapa mamlaka na uwezo wa kutoa pepo wachafu wote na kuponya magonjwa yote, 2 kisha akawatuma waende wakahubiri Ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa. 3 Akawaagiza akisema, “Msichukue chochote safarini: sio fimbo, wala mkoba, wala mkate, wala fedha, hata msichukue kanzu ya ziada. 4 Katika nyumba yoyote mwingiayo, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo. 5 Kama watu wasipowakaribisha, mnapoondoka katika mji wao, kungʼuteni mavumbi kutoka kwenye miguu yenu ili kuwa ushuhuda dhidi yao.” 6 Hivyo wale wanafunzi wakaondoka wakaenda kutoka kijiji hadi kijiji, wakihubiri habari njema na kuponya wagonjwa kila mahali.
-
37 Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”
38 Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. 39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu, na kwa wote walio mbali, na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”
40 Petro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.” 41 Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa na siku ile waliongezeka watu wapatao 3,000.
42 Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali.
-
4 Kwa hiyo wale waliotawanyika wakalihubiri neno la Mungu kila mahali walipokwenda. 5 Filipo akateremkia mji mmoja wa Samaria akawahubiria habari za Kristo 6 Watu walipomsikia Filipo na kuona ishara na miujiza aliyofanya, wakasikiliza kwa bidii yale aliyosema. 7 Pepo wachafu wakawa wakiwatoka watu wengi huku wakipiga kelele na wengi waliopooza na viwete wakaponywa. 8 Hivyo pakawa na furaha kuu katika mji huo.
-
47 Kwa maana hili ndilo Bwana alilotuamuru:
“ ‘Nimewafanya ninyi kuwa nuru kwa watu wa Mataifa,
ili mpate kuuleta wokovu hadi miisho ya dunia.’ ”
-
26 Kutoka Atalia wakasafiri baharini wakarudi Antiokia, ambako walikuwa wamesifiwa kwa ajili ya neema ya Mungu kutokana na ile huduma waliyokuwa wameikamilisha. 27 Walipowasili Antiokia wakaliita kanisa pamoja na kutoa taarifa ya yale yote Mungu aliyokuwa ametenda kupitia kwao na jinsi alivyokuwa amefungua mlango wa imani kwa ajili ya watu wa Mataifa.
-
4 Walipokuwa wakienda mji kwa mji, wakawa wanawapa maamuzi yaliyotolewa na mitume na wazee huko Yerusalemu ili wayafuate. 5 Hivyo makanisa yakawa imara katika imani na kuongezeka kiidadi kila siku.
6 Paulo pamoja na wenzake wakasafiri sehemu za Frigia na Galatia, kwa kuwa Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kulihubiri neno huko Asia. 7 Walipofika mpaka wa Misia, wakajaribu kuingia Bithinia lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu. 8 Kwa hiyo wakapita Misia, wakafika Troa. 9 Wakati wa usiku Paulo akaona maono, mtu wa Makedonia amesimama akimsihi, “Vuka uje huku Makedonia utusaidie.” 10 Baada ya Paulo kuona maono haya, tulijiandaa kwa haraka kuondoka kwenda Makedonia tukiwa tumesadiki kuwa Mungu alikuwa ametuita kuhubiri habari njema huko.
-
12 “Siku moja nilipokuwa katika mojawapo ya safari hizi nikiwa ninakwenda Dameski, nilikuwa na mamlaka na agizo kutoka kwa kiongozi wa makuhani. 13 Ilikuwa yapata adhuhuri, ee mfalme, nilipokuwa njiani, niliona nuru kutoka mbinguni kali kuliko jua, ikingʼaa kunizunguka pande zote mimi na wale niliokuwa pamoja nao. 14 Wote tulipokuwa tumeanguka chini, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya Kiebrania, ‘Sauli, Sauli, mbona unanitesa? Ni vigumu kwako kuupiga teke mchokoo.’
15 “Nikauliza, ‘Ni nani wewe, Bwana?’
“Naye Bwana akajibu, ‘Ni Mimi Yesu unayemtesa. 16 Sasa inuka usimame kwa miguu yako. Nimekutokea ili nikuteue uwe mtumishi na shahidi wa mambo ambayo umeyaona, na yale nitakayokuonyesha. 17 Nitakuokoa kutoka kwa watu wako na watu wa Mataifa ambao ninakutuma kwao, 18 uyafumbue macho yao ili wageuke kutoka gizani waingie nuruni, na kutoka kwenye nguvu za Shetani wamgeukie Mungu, ili wapate msamaha wa dhambi na sehemu miongoni mwa wale waliotakaswa kwa kuniamini mimi.’
-
18 Haya yote yanatokana na Mungu, ambaye ametupatanisha sisi na nafsi yake kwa njia ya Yesu Kristo na kutupata sisi huduma ya upatanisho: 19 Kwamba Mungu alikuwa ndani ya Kristo akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake mwenyewe, akiwa hawahesabii watu dhambi zao. Naye ametukabidhi sisi ujumbe huu wa upatanisho. 20 Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Kristo, kana kwamba Mungu anawasihi kupitia kwa vinywa vyetu. Nasi twawaomba sana ninyi kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu. 21 Kwa maana Mungu alimfanya yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu kwake yeye.
-
10 Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
sifa zake toka miisho ya dunia,
ninyi mshukao chini baharini,
na vyote vilivyomo ndani yake,
enyi visiwa na wote wakaao ndani yake.
11 Jangwa na miji yake na vipaze sauti zao;
makao anamoishi Kedari na yashangilie.
Watu wa Sela waimbe kwa furaha,
na wapige kelele kutoka vilele vya milima.
12 Wampe Bwana utukufu,
na kutangaza sifa zake katika visiwa.
-
1 Nisikilizeni, enyi visiwa, sikieni hili,
ninyi mataifa mlio mbali:
Kabla sijazaliwa, Bwana aliniita,
tangu kuzaliwa kwangu, amelitaja jina langu.
2 Akafanya kinywa changu kuwa kama upanga ulionolewa,
katika uvuli wa mkono wake akanificha;
akanifanya kuwa mshale uliosuguliwa,
na kunificha katika podo lake.
3 Akaniambia, “Wewe u mtumishi wangu,
Israeli, ambaye katika yeye
nitaonyesha utukufu wangu.”
4 Lakini nilisema, “Nimetumika bure,
nimetumia nguvu zangu bure bila faida.
Hata hivyo linalonistahili liko mkononi mwa Bwana,
nao ujira wangu uko kwa Mungu wangu.”
5 Sasa Bwana asema:
yeye aliyeniumba tumboni kuwa mtumishi wake,
kumrudisha tena Yakobo kwake
na kumkusanyia Israeli,
kwa maana nimepata heshima machoni pa Bwana,
naye Mungu wangu amekuwa nguvu yangu;
6 yeye asema:
“Je, ni jambo dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu
ili kurejeza makabila ya Yakobo,
na kuwarudisha wale Waisraeli niliowahifadhi?
Pia nitakufanya uwe nuru kwa ajili ya watu wa Mataifa,
ili upate kuleta wokovu wangu hata miisho ya dunia.”
-
1 Ndipo neno la Bwana likamjia Yona mara ya pili: 2 “Ondoka uende katika mji mkubwa wa Ninawi, ukautangazie ujumbe ninaokupa.”
-
23 Yesu akapita katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu.
-
16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.
-
1 Laiti mngenivumilia kidogo katika upumbavu wangu! Naam, nivumilieni kidogo. 2 Ninawaonea wivu, wivu wa Kimungu, kwa kuwa mimi niliwaposea mume mmoja, ili niwalete kwa Kristo kama mabikira safi. 3 Lakini nina hofu kuwa, kama vile Eva alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Kristo. 4 Kwa sababu kama mtu akija na kuwahubiria Yesu mwingine ambaye si yule tuliyemhubiri, au kama mkipokea roho mwingine ambaye si yule mliyempokea, au Injili tofauti na ile mliyoikubali, ninyi mnaitii kwa urahisi. 5 Lakini sidhani ya kuwa mimi ni dhalili sana kuliko hao “mitume wakuu.” 6 Inawezekana mimi nikawa si mnenaji hodari, lakini ni hodari katika elimu. Jambo hili tumelifanya liwe dhahiri kwenu kwa njia zote.
7 Je, nilitenda dhambi kwa kujishusha ili kuwainua ninyi kwa kuwahubiria Injili ya Mungu pasipo malipo? 8 Niliyanyangʼanya makanisa mengine kwa kupokea misaada kutoka kwao ili niweze kuwahudumia ninyi. 9 Nami nilipokuwa pamoja nanyi, nikipungukiwa na chochote, sikuwa mzigo kwa mtu yeyote, kwa maana ndugu waliotoka Makedonia walinipatia mahitaji yangu. Kwa hiyo nilijizuia kuwa mzigo kwenu kwa njia yoyote, nami nitaendelea kujizuia. 10 Kwa hakika kama vile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hakuna mtu yeyote katika Akaya nzima atakayenizuia kujivunia jambo hili. 11 Kwa nini? Je, ni kwa sababu siwapendi? Mungu anajua ya kuwa nawapenda! 12 Nami nitaendelea kufanya lile ninalofanya sasa ili nisiwape nafasi wale ambao wanatafuta nafasi ya kuhesabiwa kuwa sawa na sisi katika mambo wanayojisifia.
13 Watu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Kristo. 14 Wala hii si ajabu, kwa kuwa hata Shetani mwenyewe hujigeuza aonekane kama malaika wa nuru. 15 Kwa hiyo basi si ajabu, kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili.
-
10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi. 12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 13 Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara. 14 Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15 nayo miguu yenu ifungiwe utayari tuupatao kwa Injili ya amani. 16 Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17 Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho, ambao ni Neno la Mungu. 18 Mkiomba kwa Roho siku zote katika sala zote na maombi, mkikesha kila wakati mkiwaombea watakatifu wote.
19 Niombeeni na mimi pia, ili kila nifunguapo kinywa changu, nipewe maneno ya kusema, niweze kutangaza siri ya Injili kwa ujasiri, 20 ambayo mimi ni balozi wake katika vifungo. Ombeni ili nipate kuhubiri kwa ujasiri kama inipasavyo.
-
1 Neno la Bwana lilimjia Yona mwana wa Amitai: 2 “Nenda katika mji mkubwa wa Ninawi ukahubiri juu yake, kwa sababu uovu wake umekuja juu mbele zangu.”
3 Lakini Yona alimkimbia Bwana na kuelekea Tarshishi. Alishuka mpaka Yafa, ambapo alikuta meli iliyokuwa imepangwa kuelekea bandari ile. Baada ya kulipa nauli, akapanda melini na kuelekea Tarshishi ili kumkimbia Bwana. 4 Ndipo Bwana akatuma upepo mkali baharini, nayo dhoruba kali sana ikavuma hata meli ikawa hatarini kuvunjika.
-
1 Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.
2 Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:
“Tazama, nitamtuma mjumbe wangu mbele yako,
atakayetengeneza njia mbele yako”:
3 “sauti ya mtu aliaye nyikani.
‘Itengenezeni njia ya Bwana,
yanyoosheni mapito yake.’ ”
4 Yohana alikuja, akibatiza huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi. 5 Watu kutoka Uyahudi wote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea. Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani. 6 Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. 7 Naye alihubiri akisema, “Baada yangu atakuja yeye aliye na uwezo kuniliko mimi, ambaye sistahili hata kuinama na kulegeza kamba za viatu vyake. 8 Mimi nawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.”
-
35 Je, ninyi hamsemi, ‘Bado miezi minne tuvune?’ Inueni macho yenu myaangalie mashamba jinsi mazao yalivyo tayari kuvunwa! 36 Mvunaji tayari anapokea mshahara wake, naye anakusanya mazao kwa ajili ya uzima wa milele. Ili yeye apandaye na yeye avunaye wafurahi pamoja. 37 Hivyo kule kusema, ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna,’ ni kweli kabisa. 38 Niliwatuma mkavune mazao ambayo hamkupanda, wengine walifanya kazi ngumu, nanyi mmevuna faida ya taabu yao.”
-
16 Lakini ninapohubiri Injili siwezi kujisifu maana ninalazimika kuhubiri. Ole wangu nisipoihubiri Injili!
-
14 Kwa kuwa upendo wa Kristo unatutia nguvu, kwa sababu tunasadiki kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote, kwa hiyo wote walikufa. 15 Naye alikufa kwa ajili ya watu wote, ili kwamba wote wanaoishi wasiishi tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa na kufufuliwa tena kwa ajili yao.
-
11 Ndugu zangu, nataka mjue kwamba Injili niliyowahubiria haikutokana na wanadamu. 12 Kwa maana mimi sikuipokea hiyo Injili kutoka kwa mwanadamu, wala sikufundishwa na mtu, bali niliipata kwa ufunuo kutoka kwa Yesu Kristo.
13 Ninyi mmekwisha kusikia juu ya maisha yangu ya zamani nilipokuwa katika dini ya Kiyahudi, jinsi nilivyolitesa kanisa la Mungu kwa nguvu na kujaribu kuliangamiza. 14 Nami niliendelea sana katika dini ya Kiyahudi kuliko Wayahudi wengi wa rika yangu maana nilijitahidi sana katika desturi za baba zangu. 15 Lakini ilipompendeza Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu na kuniita kwa neema yake, 16 alimdhihirisha Mwanawe kwangu, ili nipate kumhubiri miongoni mwa watu wa Mataifa. Mimi sikushauriana na mwanadamu yeyote, 17 wala sikupanda kwenda Yerusalemu kuwaona hao waliokuwa mitume kabla yangu, bali nilikwenda mara moja Arabuni na kisha nikarudi Dameski.
18 Kisha baada ya miaka mitatu nilipanda kwenda Yerusalemu kuonana na Kefa na nilikaa naye siku kumi na tano. 19 Lakini sikumwona mtume mwingine yeyote isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana. 20 Nawahakikishia mbele za Mungu kuwa ninayowaandikia si uongo. 21 Baadaye nilikwenda sehemu za Syria na Kilikia. 22 Lakini mimi binafsi sikujulikana kwa makanisa ya huko Uyahudi yaliyo katika Kristo. 23 Wao walisikia habari tu kwamba, “Mtu yule ambaye hapo kwanza alikuwa akitutesa sasa anahubiri imani ile ile aliyokuwa akijaribu kuiangamiza.” 24 Nao wakamtukuza Mungu kwa sababu yangu.
-
9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. 10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.
-
1 Awali ya yote, nasihi kwamba dua, sala, maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya watu wote: 2 kwa ajili ya wafalme na wale wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi kwa amani na utulivu, katika uchaji wote wa Mungu na utakatifu. 3 Jambo hili ni jema, tena linapendeza machoni pa Mungu Mwokozi wetu, 4 anayetaka watu wote waokolewe na wafikie kuijua kweli. 5 Kwa maana kuna Mungu mmoja na mpatanishi mmoja kati ya Mungu na wanadamu, yaani mwanadamu Kristo Yesu, 6 aliyejitoa mwenyewe kuwa fidia kwa ajili ya wanadamu wote: jambo hili lilishuhudiwa kwa wakati wake ufaao. 7 Nami kwa kusudi hili nimewekwa niwe mhubiri na mtume (nasema kweli katika Kristo wala sisemi uongo), mwalimu wa watu wa Mataifa katika imani na kweli.
-
11 Wapenzi, ninawasihi, mkiwa kama wageni na wapitaji hapa ulimwenguni, epukeni tamaa mbaya za mwili ambazo hupigana vita na roho zenu. 12 Kuweni na mwenendo mzuri mbele ya watu wasiomjua Mungu, ili kama wanawasingizia kuwa watenda mabaya, wayaone matendo yenu mema nao wamtukuze Mungu siku atakapokuja kwetu.
-
17 Samweli akamwambia, “Ingawa zamani ulijiona mdogo machoni pako mwenyewe, Je, hukuwa kiongozi wa kabila za Israeli? Bwana alikutia mafuta kuwa mfalme juu ya Israeli. 18 Naye akakutuma kwa kazi maalum, akisema, ‘Nenda ukaangamize kabisa wale watu waovu, wale Waamaleki, upigane nao vita mpaka utakapowaangamiza kabisa.’ 19 Kwa nini hukumtii Bwana? Kwa nini ulivamia nyara na kufanya uovu machoni pa Bwana?”
20 Sauli akasema, “Lakini nilimtii Bwana. Nilikamilisha ile kazi ambayo Bwana alinituma. Niliwaangamiza Waamaleki kabisa na kumleta Agagi mfalme wao. 21 Askari walichukua kondoo na ngʼombe kutoka kwenye nyara, zile ambazo ni nzuri sana zimewekwa wakfu kwa Mungu, ili zitolewe dhabihu kwa Bwana Mungu wako huko Gilgali.”
22 Lakini Samweli akajibu:
“Je, Bwana anafurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu
kama vile kuitii sauti ya Bwana?
Kutii ni bora zaidi kuliko dhabihu,
nako kusikia ni bora
kuliko mafuta ya kondoo dume.
23 Kwa maana kuasi ni kama dhambi ya uaguzi,
nao ukaidi ni kama uovu wa kuabudu sanamu.
Kwa sababu umelikataa neno la Bwana,
naye amekukataa wewe
kuendelea kuwa mfalme.”
-
38 Yesu akawajibu, “Twendeni mahali pengine kwenye vijiji jirani, ili niweze kuhubiri huko pia, kwa sababu hicho ndicho nilichokuja kukifanya.” 39 Kwa hiyo akazunguka Galilaya kote, akihubiri katika masinagogi yao na kutoa pepo wachafu.
-
26 “Mtu yeyote anayekuja kwangu hawezi kuwa mwanafunzi wangu kama hatanipenda mimi zaidi ya baba yake na mama yake, mke wake na watoto wake, ndugu zake na dada zake, naam, hata maisha yake mwenyewe.
-
18 Mtawala mmoja akamuuliza Yesu, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
19 Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake. 20 Unazijua amri: ‘Usizini, usiue, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako.’ ”
21 Akajibu, “Amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”
22 Yesu aliposikia haya, akamwambia, “Bado kuna jambo moja ulilopungukiwa. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
23 Aliposikia jambo hili, alisikitika sana kwa maana alikuwa mtu mwenye mali nyingi. 24 Yesu akamtazama, akasema, “Tazama jinsi ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu! 25 Hakika ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”
26 Wale waliosikia haya wakauliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”
27 Yesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa wanadamu yanawezekana kwa Mungu.”
28 Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha vyote tulivyokuwa navyo tukakufuata!”
29 Yesu akajibu, “Amin, nawaambia, hakuna hata mtu aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu 30 ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya, na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.”
-
26 Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika jamaa zenye vyeo. 27 Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima, Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu. 28 Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko, 29 ili mtu yeyote asijisifu mbele zake. 30 Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanyika kwetu hekima itokayo kwa Mungu, yaani haki, na utakatifu na ukombozi. 31 Hivyo, kama ilivyoandikwa: “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.”
-
16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.
-
14 Nasi twawasihi, ndugu, waonyeni walio wavivu, watieni moyo waoga, wasaidieni wanyonge na kuwavumilia watu wote.
-
27 Dini iliyo safi, isiyo na uchafu, inayokubalika mbele za Mungu Baba yetu, ndiyo hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda usitiwe madoa na dunia.
-
18 “Nami, kwa sababu ya matendo yao na mawazo yao, niko karibu kuja na kukusanya mataifa yote na lugha zote, nao watakuja na kuuona utukufu wangu.
19 “Nitaweka ishara katikati yao, nami nitapeleka baadhi ya hao walionusurika kwa mataifa, hadi Tarshishi, kwa Puli na Waludi (wanaojulikana kama wapiga upinde), kwa Tubali na Uyunani, hadi visiwa vya mbali ambavyo havijasikia juu ya sifa zangu au kuuona utukufu wangu. Watatangaza utukufu wangu miongoni mwa mataifa.
-
18 “Roho wa Bwana yu juu yangu,
kwa sababu amenitia mafuta
kuwahubiria maskini habari njema.
Amenituma kuwatangazia wafungwa
kufunguliwa kwao,
na vipofu kupata kuona tena,
kuwaweka huru wanaoonewa,
19 na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika.”
-
18 Waliposikia haya hawakuwa na la kupinga zaidi. Nao wakamwadhimisha Mungu wakisema, “Basi, Mungu amewapa hata watu wa Mataifa toba iletayo uzima wa milele.”
-
13 Basi, ni nani atakayewadhuru mkiwa wenye juhudi katika kutenda mema? 14 Lakini mmebarikiwa hata kama ikiwalazimu kuteseka kwa ajili ya haki. “Msiogope vitisho vyao, wala msiwe na wasiwasi.” 15 Bali mtakaseni Kristo kuwa Bwana mioyoni mwenu. Siku zote mwe tayari kumjibu mtu yeyote atakayewauliza kuhusu sababu ya tumaini lililomo ndani yenu. Lakini fanyeni hivyo kwa upole na kwa heshima, 16 mkizitunza dhamiri zenu ziwe safi, ili wale wasemao mabaya dhidi ya mwenendo wenu mzuri katika Kristo waaibike kwa ajili ya masingizio yao.
17 Kwa maana ni afadhali kupata mateso kwa ajili ya kutenda mema, kama kuteseka huko ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kuteseka kwa kutenda maovu.
-
10 Kila mmoja na atumie kipawa chochote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu.
-
1 Roho wa Bwana Mwenyezi yu juu yangu,
kwa sababu Bwana amenitia mafuta
kuwahubiria maskini habari njema.
Amenituma kuwaganga waliovunjika moyo,
kuwatangazia mateka uhuru wao,
na hao waliofungwa
habari za kufunguliwa kwao;
2 kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,
na siku ya kisasi ya Mungu wetu,
kuwafariji wote waombolezao,
3 na kuwapa mahitaji
wale wanaohuzunika katika Sayuni,
ili kuwapa taji ya uzuri badala ya majivu,
mafuta ya furaha badala ya maombolezo,
vazi la sifa badala ya roho ya kukata tamaa.
Nao wataitwa mialoni ya haki,
pando la Bwana,
ili kuonyesha utukufu wake.
4 Watajenga upya magofu ya zamani
na kupatengeneza mahali palipoachwa ukiwa zamani;
watafanya upya miji iliyoharibiwa,
iliyoachwa ukiwa kwa vizazi vingi.
-
5 Hawa kumi na wawili, Yesu aliwatuma akawaagiza: “Msiende miongoni mwa watu wa Mataifa, wala msiingie mji wowote wa Wasamaria. 6 Lakini afadhali mshike njia kuwaendea kondoo wa nyumba ya Israeli waliopotea. 7 Wakati mnapokwenda, hubirini mkisema, ‘Ufalme wa Mbinguni umekaribia.’ 8 Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo wachafu. Mmepata bure, toeni bure.
-
16 “Tazama, ninawatuma kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Kwa hiyo mwe werevu kama nyoka na wapole kama hua.
17 “Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kuwapiga kwenye masinagogi yao. 18 Nanyi mtaburutwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao na kwa watu wa Mataifa. 19 Lakini watakapowapeleka humo, msisumbuke kufikiria mtakalosema, kwa maana mtapewa la kusema wakati huo. 20 Kwa sababu si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho wa Baba yenu atakayekuwa akinena kupitia kwenu.
21 “Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, naye baba atamsaliti mtoto wake. Watoto nao wataasi dhidi ya wazazi wao na kusababisha wauawe. 22 Watu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu. Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa. 23 Wakiwatesa katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Amin, amin nawaambia, hamtamaliza miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Adamu kuja.
24 “Mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake, wala mtumishi hamzidi bwana wake. 25 Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa mkuu wa nyumba ameitwa Beelzebuli, je, si watawaita zaidi wale wa nyumbani mwake!
-
42 Kesho yake, kulipopambazuka, Yesu alikwenda mahali pa faragha. Watu wengi wakawa wanamtafuta kila mahali, nao walipomwona wakajaribu kumzuia asiondoke. 43 Lakini yeye akawaambia, “Imenipasa kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa maana kwa kusudi hili nilitumwa.”
-
30 Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu, ambaye ninyi mlimuua kwa kumtundika kwenye msalaba. 31 Mungu alimtukuza, akamweka mkono wake wa kuume kuwa Kiongozi na Mwokozi ili awape Israeli toba na msamaha wa dhambi. 32 Nasi tu mashahidi wa mambo haya, vivyo hivyo na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii.”
-
30 Kornelio akajibu, “Siku nne zilizopita, nilikuwa nyumbani nikisali saa kama hii, saa tisa alasiri. Ghafula mtu aliyevaa nguo zilizongʼaa akasimama mbele yangu, 31 akasema, ‘Kornelio, maombi yako yamesikiwa na sadaka zako kwa maskini zimekumbukwa mbele za Mungu. 32 Basi tuma watu waende Yafa wakaulize mtu mmoja Simoni aitwaye Petro, yeye ni mgeni katika nyumba ya Simoni mtengenezaji ngozi, ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.’ 33 Nilituma watu kwako mara moja, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tuko hapa mbele za Mungu kuyasikiliza yote ambayo Bwana amekuamuru kutuambia.”
34 Ndipo Petro akafungua kinywa chake akasema, “Mungu hana upendeleo, 35 Lakini katika kila taifa, kila mtu amchaye na kutenda yaliyo haki hukubaliwa naye. 36 Ninyi mnajua ule ujumbe uliotumwa kwa Israeli, ukitangaza habari njema za amani kwa Yesu Kristo. Yeye ni Bwana wa wote. 37 Mnajua yale yaliyotukia katika Uyahudi wote kuanzia Galilaya baada ya mahubiri ya Yohana Mbatizaji: 38 Jinsi Mungu alivyomtia Yesu wa Nazareti mafuta katika Roho Mtakatifu na jinsi alivyokwenda huku na huko akitenda mema na kuponya wote waliokuwa wameonewa na nguvu za ibilisi, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye.
39 “Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyoyafanya katika Uyahudi na Yerusalemu. Wakamuua kwa kumtundika msalabani. 40 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu siku ya tatu na akamwezesha kuonekana na watu. 41 Hakuonekana kwa watu wote, lakini kwetu sisi tuliochaguliwa na Mungu kuwa mashahidi, ambao tulikula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. 42 Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote na kushuhudia kwamba ndiye alitiwa mafuta na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu. 43 Manabii wote walishuhudia juu yake kwamba kila mtu amwaminiye hupokea msamaha wa dhambi katika Jina lake.”
44 Wakati Petro alikuwa akisema maneno haya, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wakisikiliza ule ujumbe. 45 Wale wa tohara walioamini waliokuja na Petro walishangaa kwa kuona kuwa kipawa cha Roho Mtakatifu kimemwagwa juu ya watu wa Mataifa. 46 Kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha mpya na kumwadhimisha Mungu.
Ndipo Petro akasema, 47 “Je, kuna mtu yeyote anayeweza kuzuia watu hawa wasibatizwe kwa maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea.” 48 Kwa hiyo akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Wakamsihi Petro akae nao kwa siku chache.
-
21 Wakahubiri habari njema katika mji huo na kupata wanafunzi wengi. Kisha wakarudi Listra, Ikonio na Antiokia, 22 wakiwaimarisha wanafunzi na kuwatia moyo waendelee kudumu katika imani. Wakawaonya wakisema, “Imetupasa kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa kupitia katika taabu nyingi.” 23 Nao baada ya kuwateua wazee katika kila kanisa, kwa kufunga na kuomba wakawakabidhi kwa Bwana waliyemwamini.
-
10 Basi, sasa nenda. Ninakutuma kwa Farao ili kuwatoa watu wangu Waisraeli kutoka Misri.”
-
7 Lakini Bwana akaniambia, “Usiseme, ‘Mimi ni mtoto mdogo tu.’ Utaenda popote nitakapokutuma na kunena lolote nitakalokuagiza. 8 Usiwaogope, kwa maana niko pamoja nawe nikuokoe,” asema Bwana.
9 Kisha Bwana akaunyoosha mkono wake na kugusa kinywa changu, akaniambia, “Sasa nimeyaweka maneno yangu kinywani mwako.
-
12 Kisha Yeremia akawaambia maafisa wote na watu wote: “Bwana amenituma kutoa unabii dhidi ya nyumba hii na mji huu mambo yote mliyoyasikia. 13 Sasa tengenezeni njia zenu na matendo yenu, na kumtii Bwana Mungu wenu. Ndipo Bwana atawahurumia na kuacha kuleta maafa aliyokuwa ameyatamka dhidi yenu.
-
3 Akaniambia: “Mwanadamu, ninakutuma kwa Waisraeli, kwa taifa asi ambalo limeniasi mimi, wao na baba zao wananikosea mimi hadi leo. 4 Watu ambao ninakutuma kwao ni wapotovu na wakaidi. Waambie, ‘Hivi ndivyo anavyosema Bwana Mwenyezi.’
-
3 Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni mkabala na Hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea wakamuuliza faraghani, 4 “Tafadhali tuambie, mambo haya yatatukia lini? Nayo dalili ya kuwa hayo yote yanakaribia kutimia itakuwa gani?”
5 Yesu akawaambia: “Jihadharini mtu yeyote asiwadanganye. 6 Wengi watakuja kwa Jina langu wakidai, ‘Mimi ndiye,’ nao watawadanganya wengi. 7 Msikiapo habari za vita na uvumi wa vita, msiwe na hofu. Mambo haya hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado. 8 Taifa litainuka dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na mitetemeko sehemu mbalimbali na njaa. Haya yatakuwa ndio mwanzo wa utungu.
9 “Lakini ninyi jihadharini. Kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kupigwa mijeledi katika masinagogi. Mtashtakiwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao. 10 Nayo habari njema lazima ihubiriwe kwanza kwa mataifa yote kabla ule mwisho haujawadia. 11 Mtakapokamatwa na kushtakiwa, msisumbuke awali kuhusu mtakalosema. Semeni tu lolote mtakalopewa wakati huo, kwa kuwa si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho Mtakatifu.
12 “Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, naye baba atamsaliti mtoto wake. Watoto nao wataasi dhidi ya wazazi wao na kusababisha wauawe. 13 Watu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu. Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa.
-
27 Yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
-
10 Huko Dameski alikuwepo mwanafunzi mmoja jina lake Anania. Bwana alimwita katika maono, “Anania!”
Akajibu, “Mimi hapa Bwana.”
11 Bwana akamwambia, “Ondoka uende katika barabara iitwayo Nyofu ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu kutoka Tarso, jina lake Sauli, kwa maana wakati huu anaomba, 12 katika maono amemwona mtu aitwaye Anania akija na kuweka mikono juu yake ili apate kuona tena.”
13 Anania akajibu, “Bwana, nimesikia kutoka kwa watu wengi habari nyingi kuhusu mtu huyu na madhara yote aliyowatendea watakatifu wako huko Yerusalemu. 14 Naye amekuja hapa Dameski akiwa na mamlaka kutoka kwa viongozi wa makuhani ili awakamate wote wanaotaja jina lako.”
15 Lakini Bwana akamwambia Anania, “Nenda! Mtu huyu ni chombo changu kiteule nilichokichagua, apate kulichukua Jina langu kwa watu wa Mataifa na wafalme wao na mbele ya watu wa Israeli. 16 Nami nitamwonyesha jinsi impasavyo kuteseka kwa ajili ya Jina langu.”
17 Kisha Anania akaenda kwenye ile nyumba, akaingia ndani. Akaweka mikono yake juu ya Sauli akasema, “Ndugu Sauli, Bwana Yesu aliyekutokea njiani amenituma kwako ili upate kuona tena na ujazwe Roho Mtakatifu.” 18 Ghafula vitu kama magamba vikaanguka chini, kutoka machoni mwa Sauli, akapata kuona tena. Akasimama, akabatizwa.
-
19 Ingawa mimi ni huru, wala si mtumwa wa mtu yeyote, nimejifanya kuwa mtumwa wa kila mtu, ili niweze kuwavuta wengi kadri iwezekanavyo. 20 Kwa Wayahudi, nilikuwa kama Myahudi, ili niwapate Wayahudi. Kwa watu wale walio chini ya sheria, nilikuwa kama aliye chini ya sheria (ingawa mimi siko chini ya sheria), ili niweze kuwapata wale walio chini ya sheria. 21 Kwa watu wasio na sheria nilikuwa kama asiye na sheria (ingawa siko huru mbali na sheria ya Mungu, bali niko chini ya sheria ya Kristo), ili niweze kuwapata wale wasio na sheria. 22 Kwa walio dhaifu nilikuwa dhaifu, ili niweze kuwapata walio dhaifu. Nimekuwa mtu wa hali zote kwa watu wote ili kwa njia yoyote niweze kuwaokoa baadhi yao. 23 Nafanya haya yote kwa ajili ya Injili, ili nipate kushiriki baraka zake.
Shows Read in context, Share and Copy.