32 Bible Verses About Surrender
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.
-
25 Umati mkubwa wa watu ulikuwa ukisafiri pamoja na Yesu, naye akageuka, akawaambia, 26 “Mtu yeyote anayekuja kwangu hawezi kuwa mwanafunzi wangu kama hatanipenda mimi zaidi ya baba yake na mama yake, mke wake na watoto wake, ndugu zake na dada zake, naam, hata maisha yake mwenyewe. 27 Yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
28 “Ni nani miongoni mwenu ambaye kama anataka kujenga nyumba, hakai kwanza chini na kufanya makisio ya gharama aone kama ana fedha za kutosha kukamilisha? 29 La sivyo, akiisha kuweka msingi, naye akiwa hana uwezo wa kuikamilisha, wote waionao wataanza kumdhihaki, 30 wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga lakini hakuweza kukamilisha.’
31 “Au ni mfalme gani atokaye kwenda kupigana vita na mfalme mwingine, ambaye hakai chini kwanza na kufikiri iwapo akiwa na jeshi la watu 10,000 ataweza kupigana na yule anayekuja na jeshi la watu 20,000? 32 Kama hawezi, basi wakati yule mwingine akiwa bado yuko mbali, yeye hutuma ujumbe wa watu na kuomba masharti ya amani. 33 Vivyo hivyo, yeyote miongoni mwenu ambaye hawezi kuacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
-
24 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 25 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata. 26 Kwa maana, je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 27 Kwa maana Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, naye ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.
-
23 Kisha akawaambia wote, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate. 24 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayaokoa.
-
20 Nimesulubiwa pamoja na Kristo, wala si mimi tena ninayeishi, bali Kristo ndiye aishiye ndani yangu. Uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani ya Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu. 21 Siibatilishi neema ya Mungu, kwa maana kama haki ingeweza kupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure!”
-
34 Ndipo akauita ule umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akasema, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 35 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili atayaokoa. 36 Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? 37 Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 38 Mtu yeyote akinionea aibu mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu naye atamwonea aibu wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”
-
3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.
5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:
6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,
hakuona kule kuwa sawa na Mungu
kuwa kitu cha kushikilia,
7 bali alijifanya si kitu,
akachukua hali hasa na mtumwa,
naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.
8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,
alijinyenyekeza, akatii hata mauti:
naam, mauti ya msalaba!
9 Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana,
na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina,
10 ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe,
la vitu vya mbinguni, na vya duniani,
na vya chini ya nchi,
11 na kila ulimi ukiri ya kwamba
Yesu Kristo ni Bwana,
kwa utukufu wa Mungu Baba.
-
5 Vivyo hivyo, ninyi mlio vijana watiini wazee. Nanyi nyote imewapasa kujivika unyenyekevu kila mtu kwa mwenzake, kwa kuwa,
“Mungu huwapinga wenye kiburi,
lakini huwapa wanyenyekevu neema.”
6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.
-
11 Vivyo hivyo, jihesabuni wafu katika dhambi lakini mlio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu. 12 Kwa hiyo, msiruhusu dhambi itawale ndani ya miili yenu, ipatikanayo na kufa, ili kuwafanya mzitii tamaa mbaya. 13 Wala msivitoe viungo vya miili yenu vitumike kama vyombo vya uovu vya kutenda dhambi, bali jitoeni kwa Mungu, kama watu waliotolewa kutoka mautini kuingia uzimani. Nanyi vitoeni viungo vya miili yenu kwake kama vyombo vya haki. 14 Kwa maana dhambi haitakuwa na mamlaka juu yenu, kwa sababu hampo chini ya sheria, bali chini ya neema.
-
7 Basi mtiini Mungu. Mpingeni ibilisi, naye atawakimbia.
-
19 Je, hamjui ya kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe, 20 kwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu.
-
1 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli na Baba yangu ndiye mkulima. 2 Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata, nalo kila tawi lizaalo, hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi. 3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililonena nanyi. 4 Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda lisipokaa ndani ya mzabibu, vivyo hivyo ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kuzaa matunda.
5 “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lolote. 6 Mtu yeyote asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi kama hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea. 7 Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo, nanyi mtatendewa.
-
35 Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba kwamba kama ingewezekana saa hiyo ya mateso imwondokee. 36 Akasema, “Abba, Baba, mambo yote yawezekana kwako. Niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali vile upendavyo wewe.”
-
28 Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha kila kitu na kukufuata wewe!”
29 Yesu akasema, “Amin, nawaambia, hakuna mtu yeyote aliyeacha nyumba, ndugu wa kiume au wa kike, au mama au baba, au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, 30 ambaye hatalipwa mara mia katika ulimwengu huu: nyumba, ndugu wa kiume na wa kike, mama na baba na watoto, mashamba pamoja na mateso, kisha uzima wa milele katika ulimwengu ujao.
-
16 Je, hamjui kwamba mnapojitoa kwa mtu yeyote kama watumwa watiifu, ninyi ni watumwa wa yule mnayemtii, aidha watumwa wa dhambi, ambayo matokeo yake ni mauti, au watumwa wa utii ambao matokeo yake ni haki? 17 Lakini Mungu ashukuriwe kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa. 18 Nanyi, mkiisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki.
19 Ninasema kwa namna ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wenu wa hali ya asili. Kama vile mlivyokuwa mkivitoa viungo vya miili yenu kama watumwa wa mambo machafu na uovu uliokuwa ukiongezeka zaidi, hivyo sasa vitoeni viungo vyenu kama watumwa wa haki inayowaelekeza mpate kutakaswa.
-
1 Sisi tulio na nguvu, hatuna budi kuchukuliana na kushindwa kwa wale walio dhaifu wala si kujipendeza nafsi zetu wenyewe. 2 Kila mmoja wetu inampasa kumpendeza jirani yake kwa mambo mema, ili kumjenga katika imani. 3 Kwa maana hata Kristo hakujipendeza mwenyewe, bali kama ilivyoandikwa: “Matukano yao wale wanaokutukana wewe yalinipata mimi.”
-
11 Wapenzi, ninawasihi, mkiwa kama wageni na wapitaji hapa ulimwenguni, epukeni tamaa mbaya za mwili ambazo hupigana vita na roho zenu. 12 Kuweni na mwenendo mzuri mbele ya watu wasiomjua Mungu, ili kama wanawasingizia kuwa watenda mabaya, wayaone matendo yenu mema nao wamtukuze Mungu siku atakapokuja kwetu.
13 Kwa ajili ya Bwana, tiini kila mamlaka iliyowekwa na wanadamu: Kwa mfalme kwani ndiye aliye na mamlaka ya juu zaidi, 14 au kwa maafisa aliowaweka, kwa kuwa mfalme amewatuma ili kuwaadhibu wale wanaokosa, na kuwapongeza wale watendao mema. 15 Kwa maana ni mapenzi ya Mungu kwamba kwa kutenda mema mnyamazishe maneno ya kijinga ya watu wapumbavu.
-
16 Mtu mmoja akamjia Yesu na kumuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?”
17 Yesu akamjibu, “Mbona unaniuliza habari ya mema? Aliye mwema ni Mmoja tu. Lakini ukitaka kuingia uzimani, zitii amri.”
18 Yule mtu akamuuliza, “Amri zipi?”
Yesu akamjibu, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, 19 waheshimu baba yako na mama yako, na umpende jirani yako kama nafsi yako.”
20 Yule kijana akasema, “Hizi zote nimezishika. Je, bado nimepungukiwa na nini?”
21 Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo, na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
22 Yule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
-
8 Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu ninyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu ninyi wenye nia mbili.
-
10 Jinyenyekezeni mbele za Bwana, naye atawainua.
-
1 Kwa hiyo, kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni nia iyo hiyo kwa maana mtu aliyekwisha kuteswa katika mwili ameachana na dhambi. 2 Kwa hivyo, haishi maisha yake yaliyobaki ya kuishi hapa duniani kwa tamaa mbaya za wanadamu, bali anaishi kwa mapenzi ya Mungu. 3 Maana wakati uliopita mmekwisha kutumia muda wa kutosha katika maisha yenu mkifanya yale ambayo wapagani hupenda kutenda: wakiishi katika uasherati, tamaa mbaya, ulevi, karamu za ulafi, vileo, ngoma mbaya, na ibada chukizo za sanamu. 4 Wao hushangaa kwamba ninyi hamjiingizi pamoja nao katika huo wingi wa maisha ya ufisadi, nao huwatukana ninyi. 5 Lakini itawapasa wao kutoa hesabu mbele zake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa.
-
28 Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha vyote tulivyokuwa navyo tukakufuata!”
29 Yesu akajibu, “Amin, nawaambia, hakuna hata mtu aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu 30 ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya, na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.”
-
34 Lakini Yesu akawajibu, “Chakula changu ni kufanya mapenzi ya Mungu ambaye amenituma na kuikamilisha kazi yake.
-
24 Amin, amin nawaambia, mbegu ya ngano isipoanguka ardhini na kufa, hubakia kama mbegu peke yake. Lakini ikifa huzaa mbegu nyingi. 25 Mtu yeyote anayependa maisha yake atayapoteza, naye ayachukiaye maisha yake katika ulimwengu huu atayaokoa hata kwa uzima wa milele.
-
24 Mtu yeyote asitafute yaliyo yake mwenyewe, bali kila mtu atafute yale yanayowafaa wengine.
-
10 “Tulieni, mjue ya kwamba mimi ndimi Mungu;
nitatukuzwa katikati ya mataifa,
nitatukuzwa katika dunia.”
-
15 na uniite siku ya taabu;
nami nitakuokoa, nawe utanitukuza.”
-
27 Baada ya haya, Yesu alitoka na kumwona mtoza ushuru mmoja jina lake Lawi akiwa amekaa forodhani, mahali pake pa kutoza ushuru. Akamwambia, “Nifuate.” 28 Naye Lawi akaacha kila kitu, akaondoka, akamfuata.
-
38 Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
-
28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.
-
19 Ingawa mimi ni huru, wala si mtumwa wa mtu yeyote, nimejifanya kuwa mtumwa wa kila mtu, ili niweze kuwavuta wengi kadri iwezekanavyo. 20 Kwa Wayahudi, nilikuwa kama Myahudi, ili niwapate Wayahudi. Kwa watu wale walio chini ya sheria, nilikuwa kama aliye chini ya sheria (ingawa mimi siko chini ya sheria), ili niweze kuwapata wale walio chini ya sheria. 21 Kwa watu wasio na sheria nilikuwa kama asiye na sheria (ingawa siko huru mbali na sheria ya Mungu, bali niko chini ya sheria ya Kristo), ili niweze kuwapata wale wasio na sheria. 22 Kwa walio dhaifu nilikuwa dhaifu, ili niweze kuwapata walio dhaifu. Nimekuwa mtu wa hali zote kwa watu wote ili kwa njia yoyote niweze kuwaokoa baadhi yao. 23 Nafanya haya yote kwa ajili ya Injili, ili nipate kushiriki baraka zake.
-
17 Kwa hiyo kama mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya.
Shows Read in context, Share and Copy.