35 Bible Verses About Planting Seeds

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Planting Seeds
  1. 7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. 8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. 9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. 10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.

  2. 1 Siku iyo hiyo Yesu akatoka nje ya nyumba, akaketi kando ya bahari. 2 Umati mkubwa mno wa watu ukakusanyika kumzunguka, hata ikabidi aingie katika chombo na kuketi humo, nao watu wote wakawa wamesimama ukingoni mwa bahari. 3 Ndipo akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema: “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. 4 Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila. 5 Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba. 6 Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina. 7 Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba hiyo ikakua, ikaisonga hiyo mimea. 8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri ambapo zilitoa mazao, nyingine mara mia moja, nyingine mara sitini, na nyingine mara thelathini. 9 Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

  3. 18 “Sikilizeni basi maana ya ule mfano wa mpanzi: 19 Mtu yeyote anaposikia neno la Ufalme naye asilielewe, yule mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake. Hii ndiyo ile mbegu iliyopandwa kando ya njia. 20 Ile mbegu iliyopandwa kwenye sehemu yenye mawe ni mtu yule ambaye hulisikia neno na mara hulipokea kwa furaha. 21 Lakini kwa kuwa hana mizizi yenye kina ndani yake, lile neno hudumu kwa muda mfupi tu. Kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, yeye mara huchukizwa. 22 Ile mbegu iliyopandwa katika miiba ni yule mtu alisikiaye neno, lakini masumbufu ya maisha haya na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno na kulifanya lisizae matunda. 23 Lakini ile mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri ni yule mtu ambaye hulisikia neno na kulielewa. Naye hakika huzaa matunda, akizaa mara mia, au mara sitini, au mara thelathini ya mbegu iliyopandwa.”

  4. 4 Umati mkubwa wa watu ulipokuwa ukija kwa Yesu kutoka kila mji, akawaambia mfano huu: 5 “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia; zikakanyagwa, nao ndege wa angani wakazila. 6 Mbegu nyingine zilianguka penye miamba, nazo zilipoota, hiyo mimea ikakauka kwa kukosa unyevu. 7 Nazo mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo ile miiba ikakua pamoja nazo, na kuisonga hiyo mimea. 8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri. Zikaota na kuzaa mara mia moja zaidi ya mbegu alizopanda.”

    Baada ya kusema haya, Yesu akapaza sauti, akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

    9 Wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano huo. 10 Naye akasema, “Ninyi mmepewa kufahamu siri za Ufalme wa Mungu, lakini kwa wengine nazungumza kwa mifano, ili,

    “ ‘ingawa wanatazama, wasione;

    ingawa wanasikiliza, wasielewe.’

    11 “Maana ya mfano huu ni hii: Mbegu ni neno la Mungu. 12 Zile zilizoanguka kando ya njia ni wale ambao husikia neno, naye ibilisi anakuja na kuliondoa neno kutoka mioyoni mwao, ili wasije wakaamini na kuokoka. 13 Zile mbegu zilizoanguka kwenye mwamba ni wale ambao hulipokea neno kwa furaha wanapolisikia, lakini hawana mizizi. Wanaamini kwa muda mfupi, lakini wakati wa kujaribiwa huiacha imani. 14 Zile mbegu zilizoanguka kwenye miiba ni mfano wa wale wanaosikia, lakini wanapoendelea husongwa na masumbufu ya maisha haya, utajiri na anasa, nao hawakui. 15 Lakini zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo mzuri ni mfano wa wale ambao hulisikia neno la Mungu na kulishika kwa moyo mnyofu wa utiifu, nao kwa kuvumilia kwingi huzaa matunda.

  5. 36 Ninyi wapumbavu kiasi gani? Mpandacho hakiwi hai kama hakikufa. 37 Mpandapo, hampandi mwili ule utakao kuwa, bali mwapanda mbegu tu, pengine ya ngano au ya kitu kingine. 38 Lakini Mungu huipa mbegu umbo kama alivyokusudia mwenyewe na kila aina ya mbegu huipa umbo lake.

  6. 6 Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu. 7 Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. 8 Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema. 9 Kama ilivyoandikwa:

    “Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu

    akawapa maskini;

    haki yake hudumu milele.”

    10 Yeye ampaye mpanzi mbegu kwa ajili ya kupanda na mkate kuwa chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu. 11 Mtatajirishwa kwa kila namna ili mpate kuwa wakarimu kila wakati, na kupitia kwetu, ukarimu wenu utamletea Mungu shukrani.

  7. 5 Wapandao kwa machozi

    watavuna kwa nyimbo za shangwe.

    6 Yeye azichukuaye mbegu zake

    kwenda kupanda, huku akilia,

    atarudi kwa nyimbo za shangwe,

    akichukua miganda ya mavuno yake.

  8. 5 Kwani, Apolo ni nani? Naye Paulo ni nani? Ni watumishi tu ambao kupitia wao mliamini, kama vile Bwana alivyompa kila mtu huduma yake. 6 Mimi nilipanda mbegu, Apolo akatia maji, lakini Mungu ndiye aliikuza. 7 Hivyo mwenye kupanda na mwenye kutia maji si kitu, bali Mungu peke yake ambaye huifanya ikue. 8 Apandaye mbegu ana lengo sawa na yule atiaye maji na kila mmoja atalipwa kulingana na kazi yake. 9 Kwa kuwa sisi tu watendakazi pamoja na Mungu. Ninyi ni shamba la Mungu, jengo la Mungu.

  9. 6 Panda mbegu yako asubuhi,

    nako jioni usiruhusu mikono yako ilegee,

    kwa maana hujui ni ipi itakayofanikiwa,

    kwamba ni hii au ni ile,

    au kwamba zote zitafanikiwa sawasawa.

  10. 26 Pia akawaambia, “Ufalme wa Mungu unafanana na mtu apandaye mbegu shambani. 27 Akiisha kuzipanda, usiku na mchana, akiwa amelala au ameamka, mbegu huota na kukua pasipo yeye kujua ikuavyo. 28 Udongo huifanya iote kuwa mche, halafu suke, kisha nafaka kamili kwenye suke. 29 Lakini nafaka inapokuwa imekomaa, mara mkulima huingia shambani na mundu wa kuvunia, maana mavuno yamekuwa tayari.”

  11. 24 Amin, amin nawaambia, mbegu ya ngano isipoanguka ardhini na kufa, hubakia kama mbegu peke yake. Lakini ikifa huzaa mbegu nyingi.

  12. 11 Kisha Mungu akasema, “Ardhi na itoe mimea: miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo. 12 Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake, na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mungu akaona ya kuwa hili ni jema.

  13. 22 “Kwa muda dunia idumupo,

    wakati wa kupanda na wa kuvuna,

    wakati wa baridi na wa joto,

    wakati wa kiangazi na wa masika,

    usiku na mchana

    kamwe havitakoma.”

  14. 7 Kwa hiyo, ndugu zangu, vumilieni hadi kuja kwake Bwana. Angalieni jinsi mkulima angojavyo ardhi itoe mavuno yake yaliyo ya thamani na jinsi anavyovumilia kwa ajili ya kupata mvua za kwanza na za mwisho. 8 Ninyi nanyi vumilieni, tena simameni imara, kwa sababu kuja kwa Bwana kumekaribia. 9 Ndugu zangu, msinungʼunikiane msije mkahukumiwa. Hakimu amesimama mlangoni!

    10 Ndugu zangu, waangalieni manabii walionena kwa Jina la Bwana, ili kuwa mfano wa uvumilivu katika kukabiliana na mateso. 11 Kama mnavyojua, tunawahesabu kuwa wabarikiwa wale waliovumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wake Ayubu na mmeona kile ambacho hatimaye Bwana alimtendea. Bwana ni mwingi wa huruma, na amejaa rehema.

  15. 9 Kwa maana imeandikwa katika Sheria ya Mose: “Usimfunge maksai kinywa apurapo nafaka.” Je, Mungu hapa anahusika na ngʼombe? 10 Je, Mungu hasemi haya hasa kwa ajili yetu? Hakika yameandikwa kwa ajili yetu, kwa sababu mtu anapolima na mpuraji akapura nafaka, wote wanapaswa kufanya hivyo wakiwa na tumaini la kushiriki mavuno. 11 Je, ikiwa sisi tulipanda mbegu ya kiroho miongoni mwenu, itakuwa ni jambo kubwa iwapo tutavuna vitu vya mwili kutoka kwenu?

  16. 3 Kwa miaka sita mtapanda mazao katika mashamba yenu, nanyi kwa miaka sita mtaikata mizabibu yenu matawi na kuvuna mazao yake. 4 Lakini mwaka wa saba nchi lazima iwe na Sabato ya mapumziko, Sabato kwa Bwana. Msipande mbegu katika mashamba yenu, wala msikate mizabibu yenu matawi. 5 Msivune na kuweka akiba kinachoota chenyewe, wala kuvuna na kusindika zabibu ambayo hamkuhudumia mashamba yake. Nchi lazima iwe na mwaka wa mapumziko.

  17. 11 Mwaka wa hamsini utakuwa yubile kwenu, msipande wala msivune kile kiotacho chenyewe, au kuvuna zabibu zisizohudumiwa. 12 Kwa kuwa ni yubile, nayo itakuwa takatifu kwenu; mtakula tu kile kilichotoka moja kwa moja mashambani.

  18. 18 “ ‘Fuateni amri zangu, mwe waangalifu kutii amri zangu, nanyi mtaishi salama katika nchi. 19 Kisha nchi itazaa matunda yake, nanyi mtakula na kushiba na kuishi humo kwa salama. 20 Mwaweza kuuliza, “Tutakula nini katika mwaka wa saba ikiwa hatutapanda wala kuvuna mazao yetu?” 21 Nitawapelekeeni baraka ya pekee katika mwaka wa sita, kwamba nchi itazalisha mazao ya kutosha kwa miaka mitatu. 22 Mnapopanda mwaka wa nane, mtakula mavuno ya miaka iliyopita. Pia mtaendelea kuyala mazao hayo hadi mvune mavuno ya mwaka wa tisa.

  19. 6 Mmepanda vingi, lakini mmevuna haba. Mnakula lakini hamshibi, mnakunywa, lakini hamtosheki. Mnavaa nguo, lakini hamsikii joto. Mnapata mishahara, lakini inatoweka kama imewekwa kwenye mfuko uliotobokatoboka.”

  20. 9 Usipande aina mbili za mbegu katika shamba lako la mizabibu; ikiwa utafanya hivyo, si mazao utakayopanda tu yatakuwa najisi, bali nayo matunda ya shamba la mizabibu pia.

  21. 35 Je, ninyi hamsemi, ‘Bado miezi minne tuvune?’ Inueni macho yenu myaangalie mashamba jinsi mazao yalivyo tayari kuvunwa! 36 Mvunaji tayari anapokea mshahara wake, naye anakusanya mazao kwa ajili ya uzima wa milele. Ili yeye apandaye na yeye avunaye wafurahi pamoja. 37 Hivyo kule kusema, ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna,’ ni kweli kabisa. 38 Niliwatuma mkavune mazao ambayo hamkupanda, wengine walifanya kazi ngumu, nanyi mmevuna faida ya taabu yao.”

  22. 8 Yeye aupandaye uovu huvuna taabu,

    nayo fimbo ya ghadhabu yake itaangamizwa.

  23. 1 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli na Baba yangu ndiye mkulima. 2 Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata, nalo kila tawi lizaalo, hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi. 3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililonena nanyi. 4 Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda lisipokaa ndani ya mzabibu, vivyo hivyo ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kuzaa matunda.

    5 “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lolote. 6 Mtu yeyote asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi kama hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea. 7 Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo, nanyi mtatendewa. 8 Kwa hiyo Baba yangu hutukuzwa, kwa vile mzaavyo matunda mengi, nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.

  24. 18 Mavuno ya haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.

  25. 22 Basi kwa kuwa mmejitakasa nafsi zenu kwa kuitii ile kweli hata mkawa na upendo wa ndugu usio na unafiki, basi pendaneni kwa dhati kutoka moyoni. 23 Kwa maana mmezaliwa upya, si kwa mbegu ile iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika, kupitia kwa neno la Mungu lililo hai na linalodumu milele.

  26. 12 Isaki akapanda mazao katika nchi hiyo, kwa mwaka huo huo, akavuna mara mia, kwa sababu Bwana alimbariki. 13 Isaki akawa tajiri, mali zake zikaendelea kuongezeka mpaka akawa tajiri sana.

  27. 21 “Kwa siku sita utafanya kazi, lakini siku ya saba utapumzika, hata ikiwa ni majira ya kulima au ya kuvuna lazima upumzike.

  28. 5 Yeye akusanyaye mazao wakati wa kiangazi

    ni mwana mwenye hekima,

    lakini yeye alalaye wakati wa mavuno

    ni mwana mwenye kuaibisha.

  29. 4 Mvivu halimi kwa majira;

    kwa hiyo wakati wa mavuno hutazama

    lakini hapati chochote.

  30. 4 Yeyote atazamaye upepo hatapanda,

    yeyote aangaliaye mawingu hatavuna.

  31. 23 Pia atawapa mvua kwa ajili ya mbegu mnazootesha ardhini, chakula kinachotoka ardhini kitakuwa kizuri sana, tena tele. Katika siku ile, ngʼombe wenu watalisha katika shamba pana la majani.

  32. 13 Watapanda ngano lakini watavuna miiba;

    watajitaabisha lakini hawatafaidi chochote.

    Kwa hiyo beba aibu ya mavuno yako

    kwa sababu ya hasira kali ya Bwana Mungu.”

  33. 12 Jipandieni wenyewe haki,

    vuneni matunda ya upendo usio na kikomo,

    vunjeni ardhi yenu isiyolimwa;

    kwa kuwa ni wakati wa kumtafuta Bwana,

    mpaka atakapokuja

    na kuwanyeshea juu yenu haki.

    13 Lakini mmepanda uovu,

    mkavuna ubaya,

    mmekula tunda la udanganyifu.

    Kwa sababu mmetegemea nguvu zenu wenyewe

    na wingi wa mashujaa wenu,

  34. 15 Mtapanda lakini hamtavuna;

    mtakamua zeituni lakini

    hamtatumia mafuta yake.

    Mtakamua zabibu

    lakini hamtakunywa hiyo divai.

  35. 9 Yeyote aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wa Mungu wakaa ndani yake, wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa na Mungu.