80 Bible Verses About Working Hard

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Working Hard
  1. 22 Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu wa hapa duniani katika mambo yote. Fanyeni hivyo si wakiwepo tu, wala si kwa kutafuta upendeleo wao, bali kwa moyo mnyofu na kumcha Bwana. 23 Lolote mfanyalo, fanyeni kwa moyo kama watu wanaomtumikia Bwana, na si wanadamu, 24 kwa kuwa mnajua kwamba mtapokea urithi wenu kutoka kwa Bwana ukiwa thawabu yenu. Ni Bwana Yesu Kristo mnayemtumikia. 25 Yeyote atendaye mabaya atalipwa kwa ajili ya mabaya yake, wala hakuna upendeleo.

  2. 6 Ewe mvivu, mwendee mchwa;

    zitafakari njia zake ukapate hekima!

    7 Kwa maana yeye hana msimamizi,

    wala mwangalizi, au mtawala,

    8 lakini hujiwekea akiba wakati wa kiangazi

    na hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.

    9 Ewe mvivu, utalala hata lini?

    Utaamka lini kutoka usingizi wako?

    10 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo,

    bado kukunja mikono kidogo upate kupumzika:

    11 hivyo umaskini utakuja juu yako kama mnyangʼanyi,

    na kupungukiwa kutakujia kama mtu mwenye silaha.

  3. 6 Ndugu, tunawaagiza katika Jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni na kila ndugu ambaye ni mvivu na ambaye haishi kufuatana na maagizo tuliyowapa. 7 Maana ninyi wenyewe mnajua jinsi iwapasavyo kufuata mfano wetu. Sisi hatukuwa wavivu tulipokuwa pamoja nanyi, 8 wala hatukula chakula cha mtu yeyote pasipo kukilipia. Badala yake tulifanya kazi kwa bidii usiku na mchana, ili tusimlemee mtu yeyote miongoni mwenu. 9 Tulifanya hivi, si kwa sababu hatukuwa na haki ya kupata msaada kama huo, bali ndio sisi wenyewe tuwe kielelezo. 10 Kwa maana hata tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwapa amri kwamba: “Mtu yeyote asiyetaka kufanya kazi, hata kula asile.”

    11 Kwa kuwa tunasikia kwamba baadhi ya watu miongoni mwenu ni wavivu. Hawafanyi kazi bali hujishughulisha na mambo ya wengine. 12 Basi watu kama hao tunawaagiza na kuwahimiza katika Bwana Yesu Kristo, kwamba wafanye kazi kwa utulivu kwa ajili ya chakula chao wenyewe.

  4. 5 Kwa maana walio hai wanajua kwamba watakufa,

    lakini wafu hawajui chochote,

    hawana tuzo zaidi,

    hata kumbukumbu yao imesahaulika.

    6 Upendo wao, chuki yao na wivu wao

    vimetoweka tangu kitambo,

    kamwe hawatakuwa tena na sehemu

    katika lolote linalotendeka chini ya jua.

    7 Nenda, kula chakula chako kwa furaha, unywe divai yako kwa moyo wa shangwe, kwa maana sasa Mungu anakubali unachofanya. 8 Daima uvae nguo nyeupe na daima upake kichwa chako mafuta. 9 Furahia maisha na mke wako, umpendaye, siku zote za maisha ya ubatili uliyopewa na Mungu chini ya jua, siku zote za ubatili. Kwa maana hili ndilo fungu lako katika maisha na katika kazi yako ya taabu chini ya jua. 10 Lolote mkono wako upatalo kufanya, fanya kwa nguvu zako zote, kwa kuwa huko kuzimu, unakokwenda, hakuna kufanya kazi wala mipango wala maarifa wala hekima.

    11 Nimeona kitu kingine tena chini ya jua:

    Si wenye mbio washindao mashindano

    au wenye nguvu washindao vita,

    wala si wenye hekima wapatao chakula

    au wenye akili nyingi wapatao mali,

    wala wenye elimu wapatao upendeleo,

    lakini fursa huwapata wote.

    12 Zaidi ya hayo, hakuna mwanadamu ajuaye wakati saa yake itakapokuja:

    Kama vile samaki wavuliwavyo katika wavu mkatili,

    au ndege wanaswavyo kwenye mtego,

    vivyo hivyo wanadamu hunaswa na nyakati mbaya

    zinazowaangukia bila kutazamia.

  5. 23 Kazi zote zinazofanywa kwa bidii huleta faida,

    bali mazungumzo matupu huelekea umaskini tu.

    24 Utajiri wa wenye hekima ni taji yao,

    bali upumbavu wa wapumbavu huzaa upumbavu.

  6. 15 Jitahidi kujionyesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtendakazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli.

  7. 4 Mvivu hutamani sana na hapati kitu,

    bali nafsi ya mwenye bidii

    hutoshelezwa kikamilifu.

  8. 5 Ninyi watumwa, watiini hao walio mabwana zenu hapa duniani kwa heshima na kwa kutetemeka na kwa moyo mmoja, kama vile mnavyomtii Kristo. 6 Watiini, si tu wakati wakiwaona ili mpate upendeleo wao, bali mtumike kama watumwa wa Kristo, mkifanya mapenzi ya Mungu kwa moyo. 7 Tumikeni kwa moyo wote, kama vile mnamtumikia Bwana na si wanadamu. 8 Mkijua kwamba Bwana atampa kila mtu thawabu kwa lolote jema alilotenda, kama yeye ni mtumwa au ni mtu huru.

    9 Nanyi mabwana, watendeeni watumwa wenu kwa jinsi iyo hiyo. Msiwatishe, kwa kuwa mnajua ya kwamba yeye aliye Bwana wenu na Bwana wao yuko mbinguni, naye hana upendeleo.

    10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi.

  9. 15 Bwana Mungu akamchukua huyo mtu, akamweka kwenye Bustani ya Edeni ailime na kuitunza.

  10. 10 Nanyi kwa kweli mnawapenda ndugu wote katika Makedonia nzima. Lakini ndugu, tunawasihi mzidi sana kuwapenda.

    11 Jitahidini kuishi maisha ya utulivu, kila mtu akijishughulisha na mambo yake mwenyewe na kufanya kazi kwa mikono yake, kama vile tulivyowaagiza, 12 ili maisha yenu ya kila siku yajipatie heshima kutoka kwa watu walio nje, ili msimtegemee mtu yeyote.

  11. 24 Mikono yenye bidii itatawala,

    bali uvivu huishia katika kazi za utumwa.

  12. 31 Basi, lolote mfanyalo, kama ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.

  13. 11 Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele,

    bali yeye afuataye mambo ya upuzi hana akili.

  14. 6 Mkulima mwenye bidii ya kazi ndiye anayestahili kuwa wa kwanza kupata fungu la mavuno. 7 Fikiri sana kuhusu haya nisemayo, kwa maana Bwana atakupa ufahamu katika mambo hayo yote.

    8 Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, yeye aliye wa uzao wa Daudi. Hii ndiyo Injili yangu, 9 ambayo kwayo ninateseka hata kufikia hatua ya kufungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu halifungwi. 10 Kwa hiyo ninavumilia mambo yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, kusudi wao nao wapate wokovu ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.

    11 Hili ni neno la kuaminiwa:

    Kwa maana kama tumekufa pamoja naye,

    tutaishi pia pamoja naye.

    12 Kama tukistahimili,

    pia tutatawala pamoja naye.

    Kama tukimkana yeye,

    naye atatukana sisi.

    13 Kama tusipoamini,

    yeye hudumu kuwa mwaminifu,

    kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.

  15. 4 Mikono mivivu hufanya mtu kuwa maskini

    lakini mikono yenye bidii huleta utajiri.

    5 Yeye akusanyaye mazao wakati wa kiangazi

    ni mwana mwenye hekima,

    lakini yeye alalaye wakati wa mavuno

    ni mwana mwenye kuaibisha.

  16. 10 Nina furaha kubwa katika Bwana kwamba hatimaye mmeanza upya kushughulika tena na maisha yangu. Kweli mmekuwa mkinifikiria lakini mlikuwa hamjapata nafasi ya kufanya hivyo. 11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

  17. 3 Mkabidhi Bwana lolote ufanyalo,

    nayo mipango yako itafanikiwa.

  18. 30 Nilipita karibu na shamba la mvivu,

    karibu na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili,

    31 miiba ilikuwa imeota kila mahali,

    ardhi ilikuwa imefunikwa na magugu, na

    ukuta wa mawe ulikuwa umebomoka.

    32 Nikatafakari moyoni mwangu lile nililoliona,

    nami nikajifunza somo kutokana na niliyoyaona:

    33 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo,

    bado kukunja mikono kidogo upate kupumzika:

    34 hivyo umaskini utakuja juu yako kama mnyangʼanyi,

    na kupungukiwa kutakujia kama mtu mwenye silaha.

  19. 17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.

  20. 28 Yeye ambaye amekuwa akiiba, asiibe tena, lakini lazima ajishughulishe, afanye kitu kifaacho kwa mikono yake mwenyewe, ili awe na kitu cha kuwagawia wahitaji.

  21. 12 Kwa hiyo, wapenzi wangu, kama vile ambavyo mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwepo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka, 13 kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema.

    14 Fanyeni mambo yote bila kunungʼunika wala kushindana, 15 ili msiwe na lawama wala hatia, bali mwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka, ambacho ndani yake ninyi mnangʼaa kama mianga ulimwenguni. 16 Mkilishika neno la uzima, ili nipate kuona fahari siku ya Kristo kwamba sikupiga mbio wala kujitaabisha bure. 17 Lakini hata kama nikimiminwa kama sadaka ya kinywaji kwenye dhabihu na huduma itokayo katika imani yenu, mimi ninafurahi na kushangilia pamoja nanyi nyote.

  22. Wimbo wa kwenda juu. Wa Solomoni.

    1 Bwana asipoijenga nyumba,

    wajengao hufanya kazi bure.

    Bwana asipoulinda mji,

    walinzi wakesha bure.

    2 Mnajisumbua bure kuamka mapema

    na kuchelewa kulala,

    mkitaabikia chakula:

    kwa maana yeye huwapa usingizi wapenzi wake.

  23. 17 Wema wa Bwana Mungu wetu uwe juu yetu;

    uzithibitishe kazi za mikono yetu:

    naam, uzithibitishe kazi za mikono yetu.

  24. 8 Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini.

  25. 24 Sasa nafurahia kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu, na katika mwili wangu ninatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, ambao ni kanisa. 25 Mimi nimekuwa mtumishi wa kanisa kwa wajibu alionipa Mungu ili kuwaletea ninyi Neno la Mungu kwa ukamilifu: 26 Hii ni siri iliyokuwa imefichika tangu zamani na kwa vizazi vingi, lakini sasa imefunuliwa kwa watakatifu. 27 Kwao, Mungu amechagua kujulisha miongoni mwa watu wa Mataifa utukufu wa utajiri wa siri hii, ambayo ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu.

    28 Yeye ndiye tunayemtangaza, tukimwonya kila mtu na kumfundisha kila mtu kwa hekima yote ili tuweze kumleta kila mmoja akiwa amekamilika katika Kristo. 29 Kwa ajili ya jambo hili, ninajitaabisha, nikijitahidi kwa kadiri ya nguvu zake ambazo hutenda kazi ndani yangu kwa uweza mwingi.

  26. 7 Katika kila jambo uwe kielelezo kwa kutenda mema. Katika mafundisho yako uonyeshe uadilifu, utaratibu, 8 na usemi sahihi usio na lawama, ili wanaokupinga watahayari, wakose neno lolote baya la kusema juu yetu.

  27. 8 Ikumbuke siku ya Sabato, uitakase. 9 Kwa siku sita utafanya kazi na kutenda shughuli zako zote, 10 lakini siku ya saba ni Sabato kwa Bwana Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wako wa kiume au wa kike, wala wanyama wako, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. 11 Kwa kuwa kwa siku sita, Bwana aliumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo, lakini akapumzika siku ya saba. Kwa hiyo Bwana akaibariki siku ya Sabato na kuifanya takatifu.

  28. 33 Sikutamani fedha wala dhahabu wala vazi la mtu yeyote. 34 Ninyi wenyewe mnajua kwamba mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. 35 Katika kila jambo nimewaonyesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii imetupasa kuwasaidia wadhaifu, mkikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe jinsi alivyosema, ‘Ni heri kutoa kuliko kupokea.’ ”

  29. 17 Kwa Adamu akasema, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka kwenye mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’

    “Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako,

    kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo

    siku zote za maisha yako.

    18 Itazaa miiba na mibaruti kwa ajili yako,

    nawe utakula mimea ya shambani.

    19 Kwa jasho la uso wako

    utakula chakula chako

    hadi utakaporudi ardhini,

    kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo,

    kwa kuwa wewe u mavumbi

    na mavumbini wewe utarudi.”

  30. 1 Ndipo Bwana akamwambia Mose, 2 “Tazama, nimemchagua Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, 3 nami nimemjaza Roho wa Mungu, pamoja na ustadi, uwezo na ujuzi katika aina zote za ufundi, 4 ili kubuni michoro ya kupendeza katika ufundi wa dhahabu, fedha na shaba, 5 kuchonga vito na kuvitia mahali, kufanya ufundi kwa mbao, na kujishughulisha na aina zote za ufundi. 6 Tena nimemteua Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, ili kumsaidia. Pia mafundi wote nimewapa ustadi wa kutengeneza kila kitu nilichokuamuru wewe:

  31. 2 Utakula matunda ya kazi yako;

    baraka na mafanikio vitakuwa vyako.

  32. 58 Kwa hiyo, ndugu zangu wapenzi, simameni imara, msitikisike, mzidi sana katika kuitenda kazi ya Bwana, kwa maana mnajua ya kuwa, kazi yenu katika Bwana si bure.

  33. 1 Kwa hiyo mbingu na dunia zikakamilika, pamoja na vyote vilivyomo.

    2 Katika siku ya saba Mungu alikuwa amekamilisha kazi aliyokuwa akiifanya, hivyo siku ya saba akapumzika kutoka kazi zake zote. 3 Mungu akaibariki siku ya saba akaifanya takatifu, kwa sababu katika siku hiyo alipumzika kutoka kazi zote za kuumba alizokuwa amefanya.

  34. 9 Mtu aliye mlegevu katika kazi yake

    ni ndugu na yule anayeharibu.

    10 Jina la Bwana ni ngome imara,

    wenye haki huikimbilia na kuwa salama.

  35. 13 Usiupende usingizi la sivyo utakuwa maskini,

    uwe macho nawe utakuwa na chakula cha akiba.

  36. 12 Tunafanya kazi kwa bidii kwa mikono yetu wenyewe. Tunapolaaniwa, tunabariki, tunapoteswa, tunastahimili, 13 tunaposingiziwa, tunajibu kwa upole. Mpaka sasa tumekuwa kama takataka ya dunia na uchafu wa ulimwengu.

  37. 9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa.

  38. 4 Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema, 5 hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema. 6 Mungu alitufufua pamoja na Kristo na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu, 7 ili katika ule ulimwengu ujao apate kuonyesha wingi wa neema yake isiyopimika, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Kristo Yesu. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

  39. 13 Mvivu husema, “Yuko simba barabarani,

    simba mkali anazunguka mitaa!”

    14 Kama vile mlango ugeukavyo kwenye bawaba zake,

    ndivyo mvivu ajigeuzavyo kitandani mwake.

    15 Mtu mvivu hutumbukiza mkono wake kwenye sahani,

    naye huchoka kuupeleka kwenye kinywa chake.

    16 Mtu mvivu ni mwenye hekima machoni pake mwenyewe,

    kuliko watu saba wawezao kujibu kwa busara.

  40. 24 Hakuna kitu bora anachoweza kufanya mtu zaidi ya kula na kunywa na kuridhika katika kazi yake. Hili nalo pia, ninaona, latokana na mkono wa Mungu,

  41. 18 Ndipo nikatambua kwamba ni vyema na sahihi kwa mtu kula na kunywa na kutosheka katika kazi yake ngumu chini ya jua katika siku chache za maisha yake Mungu alizompa, kwa maana hili ndilo fungu lake. 19 Zaidi ya yote, Mungu anapompa mtu yeyote utajiri na milki, humwezesha kuvifurahia, kukubali fungu lake na kuwa na furaha katika kazi yake, hii ni karama ya Mungu. 20 Mara chache mtu huzifikiri siku za maisha yake, kwa sababu Mungu humfanya ashikwe na furaha ya moyoni.

  42. 37 Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.”

  43. 15 Uvivu huleta usingizi mzito,

    naye mtu mzembe huona njaa.

  44. 5 Mipango ya mwenye bidii huelekeza kwenye faida,

    kama vile kwa hakika pupa huelekeza kwenye umaskini.

  45. 5 “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lolote.

  46. 9 Upendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema. 10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine. 11 Msiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana. 12 Kuweni na furaha katika tumaini, katika dhiki kuweni na saburi, dumuni katika maombi. 13 Changieni katika mahitaji ya watakatifu, wakaribisheni wageni.

  47. 2 Nayajua matendo yako, bidii yako na saburi yako. Najua kuwa huwezi kuvumiliana na watu waovu na ya kwamba umewajaribu wale wanaojifanya kuwa mitume na kumbe sio, nawe umewatambua kuwa ni waongo. 3 Umevumilia na kustahimili taabu kwa ajili ya Jina langu, wala hukuchoka.

  48. 19 Mwezi hugawanya majira,

    na jua hutambua wakati wake wa kutua.

    20 Unaleta giza, kunakuwa usiku,

    wanyama wote wa mwituni huzurura.

    21 Simba hunguruma kwa mawindo yao,

    na kutafuta chakula chao kutoka kwa Mungu.

    22 Jua huchomoza, nao huondoka,

    hurudi na kulala katika mapango yao.

    23 Kisha mwanadamu huenda kazini mwake,

    katika kazi yake mpaka jioni.

  49. 26 Kama siki ilivyo kwa meno na moshi kwa macho,

    ndivyo alivyo mvivu kwa wale waliomtuma.

  50. 4 Mvivu halimi kwa majira;

    kwa hiyo wakati wa mavuno hutazama

    lakini hapati chochote.

  51. 13 Mvivu husema, “Yuko simba nje!”

    au, “Nitauawa katika mitaa!”

  52. 16 Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

  53. 16 Kwa hiyo Wayahudi wakaanza kumsumbua Yesu, kwa sababu alikuwa anafanya mambo kama hayo siku ya Sabato. 17 Yesu akawajibu, “Baba yangu anafanya kazi yake daima hata siku hii ya leo, nami pia ninafanya kazi.”

  54. 5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote

    wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

    6 katika njia zako zote mkiri yeye,

    naye atayanyoosha mapito yako.

  55. 25 Kutamani sana kwa mvivu kutakuwa kifo chake,

    kwa sababu mikono yake haitaki kufanya kazi.

  56. 14 Usimwonee mtu maskini na mhitaji ambaye umemwajiri, akiwa ni nduguyo Mwisraeli au mgeni anayeishi katika mojawapo ya miji yenu.

  57. 19 Njia ya mvivu imezibwa na miiba,

    bali njia ya mwenye haki ni barabara kuu.

  58. 15 Yeye huamka kungali bado giza

    huwapa jamaa yake chakula

    na mafungu kwa watumishi wake wa kike.

  59. 10 Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo na neema yake kwangu haikuwa kitu bure. Bali nilizidi sana kufanya kazi kuliko mitume wote, lakini haikuwa mimi, bali ni ile neema ya Mungu iliyokuwa pamoja nami.

  60. 9 Ndugu zetu, mnakumbuka juhudi yetu na taabu yetu. Tulifanya kazi usiku na mchana, ili tusimlemee mtu yeyote wa kwenu wakati tulipokuwa tunawahubiria Injili ya Mungu.

  61. 30 Kisha Mose akawaambia Waisraeli, “Tazameni, Bwana amemchagua Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, 31 naye amemjaza Roho wa Mungu, pamoja na ustadi, na uwezo na ujuzi katika aina zote za ufundi, 32 ili kubuni michoro ya kupendeza katika ufundi wa dhahabu, fedha na shaba, 33 kuchonga vito na kuvitia mahali, kufanya ufundi kwa mbao, na kujishughulisha na aina zote za ufundi wa kupendeza. 34 Tena amempa yeye pamoja na Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, uwezo wa kufundisha wengine. 35 Amewajaza ustadi wa kufanya kazi za aina zote zifanywazo na mafundi, na wenye kubuni michoro, pia na watarizi kwa rangi za buluu, zambarau, nyekundu na kitani safi, na wafumaji: wote wakiwa mafundi na wabunifu hodari.

  62. 11 Fedha isiyo ya halali hupungua,

    bali yeye akusanyaye fedha kidogo kidogo huongezeka.

  63. 24 Mtu mvivu hutumbukiza mkono wake kwenye sahani,

    lakini hawezi hata kuupeleka kwenye kinywa chake!

  64. 27 Huangalia mambo ya nyumbani mwake

    wala hali chakula cha uvivu.

  65. 4 Lakini nilisema, “Nimetumika bure,

    nimetumia nguvu zangu bure bila faida.

    Hata hivyo linalonistahili liko mkononi mwa Bwana,

    nao ujira wangu uko kwa Mungu wangu.”

  66. 38 Ikawa Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakienda Yerusalemu, akaingia kwenye kijiji kimoja ambapo mwanamke mmoja aliyeitwa Martha alimkaribisha nyumbani kwake. 39 Martha alikuwa na mdogo wake aliyeitwa Maria, ambaye aliketi chini miguuni mwa Bwana akisikiliza yale aliyokuwa akisema. 40 Lakini Martha alikuwa akihangaika na maandalizi yote yaliyokuwa yafanyike. Martha akaja kwa Yesu na kumuuliza, “Bwana, hujali kwamba ndugu yangu ameniachia kazi zote mwenyewe? Basi mwambie anisaidie.”

    41 Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, mbona unasumbuka na kuhangaika na mengi? 42 Lakini kunahitajika kitu kimoja tu. Maria amechagua kile kilicho bora, wala hakuna mtu atakayemwondolea.”

  67. 47 “Yule mtumishi anayefahamu vyema mapenzi ya bwana wake na asijiandae wala kufanya kama apendavyo bwana wake, atapigwa kwa mapigo mengi. 48 Lakini yeyote ambaye hakujua naye akafanya yale yastahiliyo kupigwa, atapigwa kidogo. Yeyote aliyepewa vitu vingi, atadaiwa vingi; na yeyote aliyekabidhiwa vingi, kwake vitatakiwa vingi.

  68. 10 “Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, pia ni mwaminifu hata katika mambo makubwa, naye mtu ambaye si mwaminifu katika mambo madogo pia si mwaminifu katika mambo makubwa.

  69. 38 Niliwatuma mkavune mazao ambayo hamkupanda, wengine walifanya kazi ngumu, nanyi mmevuna faida ya taabu yao.”

  70. 20 Basi kila mmoja wenu na abaki katika hali aliyoitwa nayo. 21 Je, wewe ulipoitwa ulikuwa mtumwa? Jambo hilo lisikusumbue. Ingawaje unaweza kupata uhuru, tumia nafasi uliyo nayo sasa kuliko wakati mwingine wowote. 22 Kwa maana yeyote aliyeitwa katika Bwana akiwa mtumwa yeye ni mtu huru kwa Bwana, kama vile yeyote aliyekuwa huru alipoitwa yeye ni mtumwa wa Kristo. 23 Mlinunuliwa kwa gharama; msiwe watumwa wa wanadamu. 24 Ndugu zangu, kama kila mtu alivyoitwa, akae katika wito wake alioitiwa na Mungu.

  71. 11 Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, 12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa 13 mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo.

    14 Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. 15 Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo. 16 Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.

  72. 1 Paulo, Silvano na Timotheo:

    Kwa kanisa la Wathesalonike, ninyi mlio ndani ya Mungu Baba yetu na ndani ya Bwana Yesu Kristo:

    Neema iwe kwenu na amani.

    2 Siku zote tunamshukuru Mungu kwa ajili yenu ninyi nyote, tukiwataja kwenye maombi yetu daima. 3 Tunaikumbuka daima kazi yenu ya imani mbele za Mungu aliye Baba yetu, taabu yenu katika upendo na saburi yenu ya tumaini katika Bwana wetu Yesu Kristo.

  73. 14 Nasi twawasihi, ndugu, waonyeni walio wavivu, watieni moyo waoga, wasaidieni wanyonge na kuwavumilia watu wote.

  74. 9 Mjane yeyote asiwekwe kwenye orodha ya wajane isipokuwa awe ametimiza umri wa miaka sitini, na ambaye alikuwa mke wa mume mmoja, 10 awe ameshuhudiwa kwa matendo yake mema, aliyewalea watoto wake vizuri, aliye mkarimu, aliyewanawisha watakatifu miguu, aliyewasaidia wenye shida na aliyejitolea kwa ajili ya matendo mema ya kila namna.

    11 Lakini kwa habari za wajane vijana usiwaweke kwenye orodha hiyo, maana tamaa zao za kimaumbile zikizidi kule kujitoa kwao kwa Kristo, watataka kuolewa tena. 12 Nao kwa njia hiyo watajiletea hukumu kwa kukiuka ahadi yao ya kwanza. 13 Zaidi ya hayo, wajane kama hao huwa na tabia ya uvivu wakizurura nyumba kwa nyumba, wala hawawi wavivu tu, bali pia huwa wasengenyaji, wajiingizao katika mambo yasiyowahusu na kusema mambo yasiyowapasa kusema. 14 Hivyo nawashauri wajane vijana waolewe, wazae watoto na wasimamie nyumba zao, wasije wakampa adui nafasi ya kutushutumu. 15 Kwa maana kwa kweli wajane wengine wamepotoka ili kumfuata Shetani.

    16 Lakini kama mwanamke yeyote aaminiye ana wajane katika jamaa yake, inampasa awasaidie wala si kuwaacha wakililemea kanisa, ili kanisa liweze kuwasaidia wale ambao ni wajane kweli kweli.

  75. 3 Vumilia taabu pamoja nasi kama askari mwema wa Kristo Yesu.

  76. 21 Basi ikiwa mtu amejitakasa na kujitenga na hayo niliyoyataja, atakuwa chombo maalum, kilichotengwa na ambacho kinamfaa mwenye nyumba, kimeandaliwa tayari kwa kila kazi njema.

  77. 14 Watu wetu hawana budi kujifunza kutenda mema, ili waweze kuyakimu mahitaji ya kila siku, wasije wakaishi maisha yasiyokuwa na matunda.

  78. 4 Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu chochote.

  79. 12 Heri mtu anayevumilia wakati wa majaribu, kwa sababu akiisha kushinda hilo jaribio atapewa taji la uzima Mungu alilowaahidia wale wampendao.

  80. 13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika: Wamebarikiwa wafu wafao katika Bwana tangu sasa.”

    “Naam,” asema Roho, “watapumzika kutoka taabu zao, kwa kuwa matendo yao yatawafuata.”