57 Bible Verses About Creation
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
1 Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2 Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu.
3 Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa. 4 Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima na huo uzima ulikuwa nuru ya watu. 5 Nuru hungʼaa gizani nalo giza halikuishinda.
-
1 Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia. 2 Wakati huu dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya maji.
3 Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo. 4 Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema, ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza. 5 Mungu akaiita nuru “mchana,” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza.
6 Mungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji igawe maji na maji.” 7 Kwa hiyo Mungu akafanya nafasi, akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo. 8 Mungu akaiita hiyo nafasi “anga.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya pili.
9 Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja, pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo. 10 Mungu akaiita nchi kavu “ardhi,” nalo lile kusanyiko la maji akaliita “bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema.
11 Kisha Mungu akasema, “Ardhi na itoe mimea: miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo. 12 Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake, na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mungu akaona ya kuwa hili ni jema. 13 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tatu.
14 Mungu akasema, “Iwepo mianga kwenye nafasi ya anga ili itenganishe usiku na mchana, nayo iwe alama ya kutambulisha majira mbalimbali, siku na miaka, 15 nayo iwe mianga kwenye nafasi ya anga ya kutia nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo. 16 Mungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mungu akafanya nyota. 17 Mungu akaiweka katika nafasi ya anga iangaze dunia, 18 itawale usiku na mchana, na ikatenganishe nuru na giza. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 19 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne.
20 Mungu akasema, “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, nao ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.” 21 Kwa hiyo Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 22 Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni mwongezeke, mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia.” 23 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano.
24 Mungu akasema, “Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo ardhini na wanyama pori, kila mnyama kulingana na aina yake.” Ikawa hivyo. 25 Mungu akafanya wanyama pori kulingana na aina zake, wanyama wa kufugwa kulingana na aina zake, na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi kulingana na aina zake. Mungu akaona kuwa hili ni jema.
26 Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.”
27 Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,
kwa mfano wa Mungu alimuumba;
mwanaume na mwanamke aliwaumba.
28 Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”
29 Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote, na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa chakula chenu. 30 Nao wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani, na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi: yaani kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo.
31 Mungu akaona vyote alivyoumba, na tazama, ilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita.
-
1 Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya, kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza vimekwisha kupita, wala hapakuwepo na bahari tena. 2 Nikaona Mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe. 3 Nami nikasikia sauti kubwa kutoka kile kiti cha enzi ikisema, “Sasa makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao. Yeye atakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. 4 Atafuta kila chozi kutoka macho yao. Mauti haitakuwepo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”
5 Naye yule aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi akasema, “Tazama, nayafanya mambo yote kuwa mapya!” Kisha akasema, “Andika haya, maana maneno haya ni ya kuaminika tena ni kweli.”
-
12 mkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru. 13 Kwa maana ametuokoa kutoka ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa, 14 ambaye katika yeye tunao ukombozi, yaani msamaha wa dhambi.
15 Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16 Kwake yeye vitu vyote vilivyoko mbinguni na juu ya nchi viliumbwa: vitu vinavyoonekana na visivyoonekana, viwe ni viti vya enzi au falme, au wenye mamlaka au watawala; vitu vyote viliumbwa na yeye na kwa ajili yake. 17 Yeye alikuwepo kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja.
-
18 Nayahesabu mateso yetu ya wakati huu kuwa si kitu kulinganisha na utukufu utakaodhihirishwa kwetu. 19 Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu. 20 Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitiisha katika tumaini, 21 ili kwamba viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka kwa utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.
22 Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa maumivu kama utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa. 23 Wala si hivyo viumbe peke yao, bali hata sisi ambao ndio matunda ya kwanza ya Roho, kwa ndani tunalia kwa uchungu tukisubiri kwa shauku kufanywa wana wa Mungu, yaani, ukombozi wa miili yetu. 24 Kwa kuwa tuliokolewa kwa tumaini hili. Lakini kama kinachotumainiwa kikionekana hakiwi tumaini tena. Je, kuna mtu anayetumaini kupata kitu alicho nacho tayari? 25 Lakini tunapotumaini kupata kitu ambacho hatuna, basi twakingojea kwa saburi.
-
18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao, 19 kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao. 20 Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.
21 Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza. 22 Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga
-
3 Kwa imani tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, vitu vyote vinavyoonekana havikuumbwa kutoka kwa vitu vinavyoonekana.
4 Kwa imani Abeli alimtolea Mungu dhabihu bora zaidi kuliko Kaini. Kwa imani alishuhudiwa kuwa mwenye haki, Mungu mwenyewe akazishuhudia sadaka zake. Kwa imani bado ananena ingawa amekufa.
-
1 Kwa hiyo mbingu na dunia zikakamilika, pamoja na vyote vilivyomo.
2 Katika siku ya saba Mungu alikuwa amekamilisha kazi aliyokuwa akiifanya, hivyo siku ya saba akapumzika kutoka kazi zake zote. 3 Mungu akaibariki siku ya saba akaifanya takatifu, kwa sababu katika siku hiyo alipumzika kutoka kazi zote za kuumba alizokuwa amefanya.
4 Haya ndiyo maelezo ya mbingu na dunia wakati zilipoumbwa.
Bwana Mungu alipoziumba mbingu na dunia,
-
8 Kila mmoja wa hawa viumbe wanne wenye uhai alikuwa na mabawa sita, na kujawa na macho pande zote hadi chini ya mabawa. Usiku na mchana hawaachi kusema:
“Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
ni Bwana Mungu Mwenyezi,
aliyekuwako, aliyeko na atakayekuja.”
9 Kila mara viumbe hao wanne wenye uhai wanapomtukuza, kumheshimu na kumshukuru yeye aketiye kwenye kile kiti cha enzi, tena aishiye milele na milele, 10 wale wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake aketiye kwenye kiti cha enzi na kumwabudu yeye aliye hai milele na milele. Huziweka taji zao mbele ya kiti cha enzi, wakisema:
11 “Bwana wetu na Mungu wetu,
wewe unastahili kupokea utukufu
na heshima na uweza,
kwa maana ndiwe uliyeviumba vitu vyote,
na kwa mapenzi yako viliumbwa
na vimekuwako.”
-
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
1 Mbingu zinatangaza utukufu wa Mungu,
anga zahubiri kazi ya mikono yake.
2 Siku baada ya siku zinatoa habari,
usiku baada ya usiku zinatangaza maarifa.
3 Hakuna msemo wala lugha,
ambapo sauti zao hazisikiki.
4 Sauti yao imeenea duniani pote,
nayo maneno yao yameenea
hadi miisho ya ulimwengu.
Katika mbingu amepiga hema kwa ajili ya jua,
5 linafanana na bwana arusi
akitoka chumbani mwake,
kama shujaa afurahiavyo
kukamilisha kushindana kwake.
6 Huchomoza upande mmoja wa mbingu,
na kufanya mzunguko wake
hadi upande mwingine.
Hakuna kilichojificha joto lake.
-
25 “Utanilinganisha mimi na nani?
Au ni nani anayelingana nami?” asema yeye Aliye Mtakatifu.
26 Inueni macho yenu mtazame mbinguni:
Ni nani aliyeumba hivi vyote?
Ni yeye aletaye nje jeshi la nyota moja baada ya nyingine
na kuziita kila moja kwa jina lake.
Kwa sababu ya uweza wake mkuu na nguvu zake kuu,
hakuna hata mojawapo inayokosekana.
27 Kwa nini unasema, ee Yakobo,
nanyi ee Israeli, kulalamika,
“Njia yangu imefichwa Bwana asiione,
Mungu wangu hajali shauri langu?”
28 Je wewe, hufahamu?
Je wewe, hujasikia?
Bwana ni Mungu wa milele,
Muumba wa miisho ya dunia.
Hatachoka wala kulegea,
wala hakuna hata mmoja
awezaye kuupima ufahamu wake.
-
6 Wewe peke yako ndiwe Bwana. Uliziumba mbingu, hata mbingu za mbingu na jeshi lote la mbinguni, dunia na vyote vilivyo ndani yake, na pia bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Huvipa vitu vyote uhai, nalo jeshi la mbinguni linakuabudu wewe.
-
5 Lakini wao kwa makusudi hupuuza ukweli huu, ya kwamba kwa neno la Mungu mbingu zilikuwepo tangu zamani, nayo dunia ilifanyizwa kutoka ndani ya maji na kwa maji. 6 Ulimwengu wa wakati ule uligharikishwa kwa hayo maji na kuangamizwa. 7 Lakini kwa neno lilo hilo, mbingu za sasa na dunia zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu.
8 Lakini wapenzi, msisahau neno hili: kwamba kwa Bwana, siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. 9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba.
10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; navyo vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilichomo ndani yake kitaunguzwa.
11 Kwa kuwa vitu vyote vitaharibiwa namna hii, je, ninyi imewapasa kuwa watu wa namna gani? Inawapasa kuishi maisha matakatifu na ya kumcha Mungu, 12 mkingojea na kuhimiza kuja kwa hiyo siku ya Mungu. Siku hiyo italeta mbingu kuchomwa moto na kutoweka, na vitu vya asili vitayeyuka kwa moto.
-
3 Nikiziangalia mbingu zako,
kazi ya vidole vyako,
mwezi na nyota,
ulizoziratibisha,
4 mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria,
binadamu ni nani hata unamjali?
5 Umemfanya chini kidogo kuliko viumbe wa mbinguni,
ukamvika taji ya utukufu na heshima.
6 Umemfanya mtawala juu ya kazi za mikono yako;
umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.
7 Mifugo na makundi yote pia,
naam, na wanyama wa kondeni,
8 ndege wa angani na samaki wa baharini,
naam, kila kiogeleacho katika njia za bahari.
-
6 kwetu sisi yuko Mungu mmoja, aliye Baba, ambaye vitu vyote vyatoka kwake na kwa ajili yake sisi twaishi; na kuna Bwana mmoja tu, Yesu Kristo, ambaye kwa yeye vitu vyote vimekuwepo na kwa yeye tunaishi.
-
7 Hutandaza anga la kaskazini mahali patupu;
naye huiningʼiniza dunia mahali pasipo na kitu.
8 Huyafungia maji kwenye mawingu yake,
hata hivyo mawingu hayapasuki kwa uzito wake.
9 Huufunika uso wa mwezi mpevu,
akitandaza mawingu juu yake.
10 Amechora mstari wa upeo juu ya uso wa maji,
ameweka mpaka wa nuru na giza.
11 Nguzo za mbingu nazo zatetemeka,
zinatishika anapozikemea.
12 Kwa nguvu zake aliisukasuka bahari;
kwa hekima yake alimkata Rahabu vipande vipande.
13 Aliisafisha anga kwa pumzi yake;
kwa mkono wake alimchoma joka aendaye mbio.
14 Haya ni mambo madogo tu katika matendo yake;
tazama jinsi ulivyo mdogo mnongʼono tunaousikia kumhusu!
Ni nani basi awezaye kuelewa
ngurumo za nguvu zake?”
-
5 Bwana hupenda uadilifu na haki;
dunia imejaa upendo wake usiokoma.
6 Kwa neno la Bwana mbingu ziliumbwa,
jeshi lao la angani kwa pumzi ya kinywa chake.
-
1 Msifuni Bwana.
Msifuni Bwana kutoka mbinguni,
msifuni juu vileleni.
2 Msifuni, enyi malaika wake wote,
msifuni yeye, enyi jeshi lake lote la mbinguni.
3 Msifuni yeye, enyi jua na mwezi,
msifuni yeye, enyi nyota zote zingʼaazo.
4 Msifuni yeye, enyi mbingu zilizo juu sana,
na ninyi maji juu ya anga.
5 Vilisifu jina la Bwana
kwa maana aliamuru navyo vikaumbwa.
6 Aliviweka mahali pake milele na milele,
alitoa amri ambayo haibadiliki milele.
7 Mtukuzeni Bwana kutoka duniani,
ninyi viumbe vikubwa vya baharini na vilindi vyote vya bahari,
8 umeme wa radi na mvua ya mawe, theluji na mawingu,
pepo za dhoruba zinazofanya amri zake,
9 ninyi milima na vilima vyote,
miti ya matunda na mierezi yote,
10 wanyama wa mwituni na mifugo yote,
viumbe vidogo na ndege warukao,
-
KITABU CHA NNE
Maombi ya Mose, mtu wa Mungu.
1 Bwana, wewe umekuwa makao yetu
katika vizazi vyote.
2 Kabla ya kuzaliwa milima
au hujaumba dunia na ulimwengu,
wewe ni Mungu tangu milele hata milele.
-
17 “Tazama, nitaumba
mbingu mpya na dunia mpya.
Mambo ya zamani hayatakumbukwa,
wala hayatakuja akilini.
18 Lakini furahini na kushangilia daima
katika hivi nitakavyoumba,
kwa kuwa nitaumba Yerusalemu uwe wa kupendeza,
nao watu wake wawe furaha.
19 Nami nitaifurahia Yerusalemu
na kuwafurahia watu wangu;
sauti ya maombolezo na ya kilio
haitasikika humo tena.
-
24 “Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, yeye ndiye Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu. 25 Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji chochote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote. 26 Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi. 27 Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu. 28 ‘Kwa kuwa katika yeye tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni watoto wake.’
-
7 Bwana Mungu alimuumba mtu kutoka mavumbi ya ardhi, akampulizia pumzi ya uhai puani mwake, naye mtu akawa kiumbe hai.
-
25 Hapo mwanzo uliweka misingi ya dunia,
nazo mbingu ni kazi ya mikono yako.
26 Hizi zitatoweka, lakini wewe utadumu,
zote zitachakaa kama vazi.
Utazibadilisha kama nguo
nazo zitaondoshwa.
27 Lakini wewe, U yeye yule,
nayo miaka yako haikomi kamwe.
-
5 Hili ndilo asemalo Mungu, Bwana,
yeye aliyeziumba mbingu na kuzitanda,
aliyeitandaza dunia na vyote vitokavyo humo,
awapaye watu wake pumzi,
na uzima kwa wale waendao humo:
6 “Mimi, Bwana, nimekuita katika haki;
nitakushika mkono wako.
Nitakulinda na kukufanya
kuwa Agano kwa ajili ya watu
na nuru kwa Mataifa,
7 kuwafungua macho wale wasioona,
kuwaacha huru kutoka kifungoni waliofungwa jela,
na kuwafungua kutoka gerezani
wale wanaokaa gizani.
8 “Mimi ndimi Bwana; hilo ndilo Jina langu!
Sitampa mwingine utukufu wangu
wala sanamu sifa zangu.
9 Tazama, mambo ya kwanza yametokea,
nami natangaza mambo mapya;
kabla hayajatokea
nawatangazia habari zake.”
10 Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
sifa zake toka miisho ya dunia,
ninyi mshukao chini baharini,
na vyote vilivyomo ndani yake,
enyi visiwa na wote wakaao ndani yake.
-
1 Zamani Mungu alisema na baba zetu kwa njia ya manabii mara nyingi na kwa njia mbalimbali, 2 lakini katika siku hizi za mwisho anasema nasi kwa njia ya Mwanawe, ambaye amemweka kuwa mrithi wa vitu vyote, na ambaye kupitia kwake aliuumba ulimwengu.
-
7 “Lakini ulizeni wanyama, nao watawafundisha,
au ndege wa angani, nao watawaambia;
8 au zungumzeni na dunia, nayo itawafundisha,
au acheni samaki wa baharini wawape taarifa.
9 Ni nani miongoni mwa hawa wote asiyejua
kwamba mkono wa Bwana ndio uliofanya hili?
10 Mkononi mwake kuna uhai wa kila kiumbe,
na pumzi ya wanadamu wote.
-
3 Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu,
mfalme mkuu juu ya miungu yote.
4 Mkononi mwake mna vilindi vya dunia,
na vilele vya milima ni mali yake.
5 Bahari ni yake, kwani ndiye aliifanya,
na mikono yake iliumba nchi kavu.
-
12 Ni nani aliyepima maji ya bahari
kwenye konzi ya mkono wake,
au kuzipima mbingu kwa shibiri yake?
Ni nani aliyeyashika mavumbi ya dunia katika kikapu,
au kupima milima kwenye kipimio
na vilima kwenye mizani?
13 Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Bwana,
au kumfundisha akiwa kama mshauri wake?
-
18 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana,
yeye aliyeumba mbingu,
ndiye Mungu;
yeye aliyeifanya dunia na kuiumba,
yeye ndiye aliiwekea misingi imara,
hakuiumba ili iwe tupu,
bali aliiumba ikaliwe na viumbe vyake.
Anasema:
“Mimi ndimi Bwana,
wala hakuna mwingine.
-
17 “Ee Bwana Mwenyezi, umeumba mbingu na nchi kwa uwezo wako mkuu na kwa mkono ulionyooshwa. Hakuna jambo lililo gumu usiloliweza.
-
4 Roho wa Mungu ameniumba;
pumzi ya Mwenyezi hunipa uhai.
-
Zaburi ya Daudi.
1 Dunia ni mali ya Bwana, na vyote vilivyomo ndani yake,
ulimwengu, na wote waishio ndani yake,
2 maana aliiwekea misingi yake baharini
na kuifanya imara juu ya maji.
-
24 Ee Bwana, jinsi matendo yako yalivyo mengi!
Kwa hekima ulizifanya zote,
dunia imejaa viumbe vyako.
25 Pale kuna bahari, kubwa na yenye nafasi tele,
imejaa viumbe visivyo na idadi,
vitu vyenye uhai vikubwa na vidogo.
-
10 Huyo Neno alikuwako ulimwenguni na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua.
-
15 “Enyi watu, kwa nini mnafanya mambo haya? Sisi ni wanadamu tu kama ninyi! Tunawaletea habari njema, tukiwaambia kwamba mgeuke mtoke katika mambo haya yasiyofaa, mmwelekee Mungu aliye hai, aliyeziumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo. 16 Zamani aliwaachia mataifa waishi walivyotaka. 17 Lakini hakuacha kuwaonyesha watu uwepo wake: Ameonyesha wema kwa kuwanyeshea mvua toka mbinguni na kuwapa mazao kwa majira yake, naye amewapa chakula tele na kuijaza mioyo yenu na furaha.”
-
38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.
-
17 Kwa Adamu akasema, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka kwenye mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’
“Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako,
kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo
siku zote za maisha yako.
18 Itazaa miiba na mibaruti kwa ajili yako,
nawe utakula mimea ya shambani.
19 Kwa jasho la uso wako
utakula chakula chako
hadi utakaporudi ardhini,
kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo,
kwa kuwa wewe u mavumbi
na mavumbini wewe utarudi.”
-
9 Kwa maana Mungu alisema, na ikawa,
aliamuru na ikasimama imara.
-
24 Hii ndiyo siku Bwana aliyoifanya,
tushangilie na kufurahi ndani yake.
-
8 Msaada wetu ni katika jina la Bwana,
Muumba wa mbingu na dunia.
-
6 Bwana hufanya lolote apendalo,
mbinguni na duniani,
katika bahari na vilindi vyake vyote.
7 Hufanya mawingu kupanda kutoka miisho ya dunia;
hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua
na huleta upepo kutoka ghala zake.
-
11 “Waambie hivi: ‘Miungu hii, ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia kutoka dunia na kutoka chini ya mbingu.’ ”
12 Lakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake,
akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake,
na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake.
-
2 “Hili ndilo Bwana asemalo, yeye aliyeumba dunia, Bwana aliyeifanya na kuithibitisha, Bwana ndilo jina lake: 3 ‘Niite nami nitakuitika na kukuambia mambo makuu na yasiyochunguzika, usiyoyajua.’
-
6 Lakini tangu mwanzo wa uumbaji, ‘Mungu aliwaumba mwanaume na mwanamke. 7 Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja.’ 8 Kwa hiyo hawatakuwa wawili tena, bali mwili mmoja.
-
17 Kama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Yeye ni baba yetu mbele za Mungu, ambaye yeye alimwamini, yule Mungu anaye fufua waliokufa, na kuvitaja vile vitu ambavyo haviko kana kwamba vimekwisha kuwako.
-
36 Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, viko kwake na kwa ajili yake.
Utukufu ni wake milele! Amen.
-
13 Lakini kufuatana na ahadi yake, sisi tunatazamia mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki hukaa ndani yake.
-
6 Mwanamke alipoona ya kuwa tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula na la kupendeza macho, tena linatamanika kwa kujipatia hekima, basi akachuma katika matunda yake, akala, pia akampa mumewe, aliyekuwa pamoja naye, naye akala.
-
1 Hii ni orodha iliyoandikwa ya vizazi vya Adamu.
Wakati Mungu alipomuumba Adamu, alimfanya kwa sura ya Mungu. 2 Aliwaumba mwanaume na mwanamke, akawabariki. Walipokwisha kuumbwa, akawaita “mwanadamu.”
3 Adamu alipokuwa ameishi miaka 130, alikuwa na mwana aliyekuwa na sura yake, mwenye kufanana naye. Akamwita Sethi.
-
17 Itakuwa ishara kati yangu na Waisraeli milele, kwa kuwa kwa muda wa siku sita Bwana aliumba mbingu na dunia, na siku ya saba akaacha kufanya kazi, akapumzika.’ ”
18 Bwana alipomaliza kusema na Mose juu ya Mlima Sinai, Mungu akampa vile vibao viwili vya Ushuhuda, vibao vya mawe vilivyoandikwa kwa kidole cha Mungu.
-
4 Kwa maana kwako miaka elfu
ni kama siku moja iliyokwisha pita,
au kama kesha la usiku.
-
5 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu,
lakini Bwana aliziumba mbingu.
-
1 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Ee Bwana Mungu wangu, wewe ni mkuu sana,
umejivika utukufu na enzi.
2 Amejifunika katika nuru kama vile kwa vazi,
amezitandaza mbingu kama hema
3 na kuziweka nguzo za orofa yake juu ya maji.
Huyafanya mawingu kuwa gari lake,
na hupanda kwenye mbawa za upepo.
4 Huzifanya pepo kuwa wajumbe wake,
miali ya moto watumishi wake.
5 Ameiweka dunia kwenye misingi yake,
haiwezi kamwe kuondoshwa.
6 Uliifunika kwa kilindi kama kwa vazi,
maji yalisimama juu ya milima.
-
15 Kwa maana katika Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu!
-
4 Kwa maana kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, wala hakuna kitu chochote cha kukataliwa kama kikipokewa kwa shukrani,
-
3 Mwana ni mngʼao wa utukufu wa Mungu na mfano halisi wa nafsi yake, akivihifadhi vitu vyote kwa neno lake lenye uweza. Akiisha kufanya utakaso kwa ajili ya dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Aliye Mkuu huko mbinguni.
-
13 Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi na baharini na vyote vilivyomo ndani yake vikiimba:
“Sifa na heshima na utukufu na uweza
ni vyake yeye aketiye juu ya hicho kiti cha enzi
na kwa Mwana-Kondoo,
milele na milele!”
Shows Read in context, Share and Copy.