78 Bible Verses About Stars

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Stars
  1. 1 Baada ya Yesu kuzaliwa katika mji wa Bethlehemu huko Uyahudi, wakati wa utawala wa Mfalme Herode, wataalamu wa mambo ya nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu 2 wakiuliza, “Yuko wapi huyo aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota yake ikitokea mashariki, nasi tumekuja kumwabudu.”

    3 Mfalme Herode aliposikia jambo hili aliingiwa na hofu sana pamoja na watu wote wa Yerusalemu. 4 Herode akawaita pamoja viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, akawauliza ni mahali gani ambapo Kristo angezaliwa. 5 Nao wakamwambia, “Katika Bethlehemu ya Uyahudi, kwa maana hivyo ndivyo ilivyoandikwa na nabii:

    6 “ ‘Nawe, Bethlehemu, katika nchi ya Yuda,

    wewe si mdogo miongoni

    mwa watawala wa Yuda;

    kwa maana kutoka kwako atakuja mtawala

    atakayekuwa mchungaji

    wa watu wangu Israeli.’ ”

    7 Ndipo Herode akawaita wale wataalamu wa nyota kwa siri na kutaka kujua kutoka kwao uhakika kamili wa wakati ile nyota ilionekana. 8 Kisha akawatuma waende Bethlehemu akiwaambia, “Nendeni mkamtafute kwa bidii huyo mtoto. Nanyi mara mtakapomwona, mniletee habari ili na mimi niweze kwenda kumwabudu.”

    9 Baada ya kumsikia mfalme, wale wataalamu wa nyota wakaenda zao, nayo ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, nao wakaifuata mpaka iliposimama mahali pale alipokuwa mtoto. 10 Walipoiona ile nyota wakajawa na furaha kubwa mno. 11 Walipoingia ndani ya ile nyumba, wakamwona mtoto pamoja na Maria mama yake, wakamsujudu na kumwabudu yule mtoto Yesu. Ndipo wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane. 12 Nao wakiisha kuonywa katika ndoto wasirudi kwa Herode, wakarudi kwenda katika nchi yao kwa njia nyingine.

  2. 14 Mungu akasema, “Iwepo mianga kwenye nafasi ya anga ili itenganishe usiku na mchana, nayo iwe alama ya kutambulisha majira mbalimbali, siku na miaka, 15 nayo iwe mianga kwenye nafasi ya anga ya kutia nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo. 16 Mungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mungu akafanya nyota. 17 Mungu akaiweka katika nafasi ya anga iangaze dunia, 18 itawale usiku na mchana, na ikatenganishe nuru na giza. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 19 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne.

  3. 7 Husema na jua, nalo likaacha kuangaza;

    naye huizima mianga ya nyota.

    8 Yeye peke yake huzitandaza mbingu

    na kuyakanyaga mawimbi ya bahari.

    9 Yeye ndiye Muumba wa nyota za Dubu, na Orioni,

    Kilimia, na makundi ya nyota za kusini.

    10 Hutenda maajabu yasiyopimika,

    miujiza isiyoweza kuhesabiwa.

  4. 16 Katika mkono wake wa kuume alishika nyota saba, na kinywani mwake ulitoka upanga mkali wenye makali kuwili. Uso wake ulikuwa kama jua likingʼaa kwa nguvu zake zote.

    17 Nilipomwona, nilianguka miguuni pake kama aliyekufa. Ndipo akauweka mkono wake wa kuume juu yangu na kusema: “Usiogope, Mimi ndiye wa Kwanza na wa Mwisho. 18 Mimi ni Yeye Aliye Hai, niliyekuwa nimekufa, na tazama, ni hai milele na milele! Nami ninazo funguo za mauti na kuzimu.

    19 “Basi andika mambo uliyoyaona, yaliyopo na yale yatakayotukia baada ya haya. 20 Kuhusu siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume na vile vinara saba vya taa vya dhahabu ni hii: Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba, navyo vile vinara saba ni hayo makanisa saba.

  5. 9 Tazameni, siku ya Bwana inakuja,

    siku katili, yenye ghadhabu na hasira kali,

    kuifanya nchi kuwa ukiwa

    na kuwaangamiza wenye dhambi waliomo ndani yake.

    10 Nyota za mbinguni na makundi ya nyota

    havitatoa mwanga wake.

    Jua linalochomoza litatiwa giza

    na mwezi hautatoa nuru yake.

  6. 2 Msifuni, enyi malaika wake wote,

    msifuni yeye, enyi jeshi lake lote la mbinguni.

    3 Msifuni yeye, enyi jua na mwezi,

    msifuni yeye, enyi nyota zote zingʼaazo.

    4 Msifuni yeye, enyi mbingu zilizo juu sana,

    na ninyi maji juu ya anga.

    5 Vilisifu jina la Bwana

    kwa maana aliamuru navyo vikaumbwa.

    6 Aliviweka mahali pake milele na milele,

    alitoa amri ambayo haibadiliki milele.

  7. 3 Anawaponya waliovunjika mioyo

    na kuvifunga vidonda vyao.

    4 Huzihesabu nyota

    na huipa kila moja jina lake.

    5 Bwana wetu ni mkuu na mwenye uwezo mwingi,

    ufahamu wake hauna kikomo.

  8. 3 Nikiziangalia mbingu zako,

    kazi ya vidole vyako,

    mwezi na nyota,

    ulizoziratibisha,

    4 mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria,

    binadamu ni nani hata unamjali?

    5 Umemfanya chini kidogo kuliko viumbe wa mbinguni,

    ukamvika taji ya utukufu na heshima.

  9. 3 Wale wenye hekima watangʼaa kama mwanga wa mbingu, nao wale ambao huwaongoza wengi kutenda haki, watangʼaa kama nyota milele na milele.

  10. 17 “Namwona yeye, lakini si sasa;

    namtazama yeye, lakini si karibu.

    Nyota itatoka kwa Yakobo,

    fimbo ya ufalme itainuka kutoka kwa Israeli.

    Atawaponda Wamoabu vipaji vya nyuso

    na mafuvu yote ya wana wa Shethi.

  11. 6 Ambaye aliitandaza dunia juu ya maji,

    Fadhili zake zadumu milele.

    7 Ambaye aliumba mianga mikubwa,

    Fadhili zake zadumu milele.

    8 Jua litawale mchana,

    Fadhili zake zadumu milele.

    9 Mwezi na nyota vitawale usiku,

    Fadhili zake zadumu milele.

  12. 1 Baada ya jambo hili, neno la Bwana likamjia Abramu katika maono:

    “Usiogope, Abramu.

    Mimi ni ngao yako,

    na thawabu yako kubwa sana.”

    2 Lakini Abramu akasema, “Ee Bwana Mwenyezi, utanipa nini na mimi sina hata mtoto na atakayerithi nyumba yangu ni huyu Eliezeri Mdameski?” 3 Abramu akasema, “Hukunipa watoto, hivyo mtumishi katika nyumba yangu ndiye atakuwa mrithi wangu.”

    4 Ndipo neno la Bwana lilipomjia: “Mtu huyu hatakuwa mrithi wako, bali mwana atakayetoka katika viuno vyako mwenyewe ndiye atakayekuwa mrithi wako.” 5 Akamtoa nje na kusema, “Tazama juu kuelekea mbinguni na uhesabu nyota, kama hakika utaweza kuzihesabu.” Ndipo akamwambia, “Hivyo ndivyo uzao wako utakavyokuwa.”

    6 Abramu akamwamini Bwana, naye kwake hili likahesabiwa kuwa haki.

  13. 16 “Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu kushuhudia mambo haya kwa ajili ya makanisa. Mimi ndimi Shina na Mzao wa Daudi, ile Nyota ya Asubuhi ingʼaayo.”

  14. 8 (yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni,

    ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko

    na mchana kuwa usiku,

    ambaye huyaita maji ya bahari

    na kuyamwaga juu ya uso wa nchi:

    Bwana ndilo jina lake;

    9 yeye hufanya maangamizo kwenye ngome

    na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa),

  15. 39 Kwa maana nyama zote si za aina moja. Binadamu wana nyama ya aina moja, wanyama wana aina nyingine, kadhalika ndege na samaki wana nyama tofauti. 40 Pia kuna miili ya mbinguni na miili ya duniani, lakini fahari wa ile miili ya mbinguni ni wa aina moja na fahari wa ile miili ya duniani ni wa aina nyingine. 41 Jua lina fahari ya aina moja, mwezi nao una fahari yake na nyota pia, nazo nyota hutofautiana katika fahari.

  16. 10 Malaika wa tatu akaipiga tarumbeta yake, na nyota kubwa iliyokuwa ikiwaka kama taa ikaanguka toka angani, ikaangukia theluthi ya mito na chemchemi za maji. 11 Nyota hiyo inaitwa Uchungu. Theluthi ya maji yakawa machungu na watu wengi wakafa kutokana na maji hayo kwa maana yalikuwa machungu.

    12 Kisha malaika wa nne akaipiga tarumbeta yake, na theluthi ya jua, theluthi ya mwezi na theluthi ya nyota zikapigwa. Kwa hiyo theluthi moja ya mwanga ikawa giza. Theluthi ya mchana ikawa haina mwanga na pia theluthi ya usiku.

  17. 15 Hamkuona umbo la aina yoyote siku ambayo Bwana alizungumza nanyi kule Horebu kutoka kwenye moto. Kwa hiyo mjihadhari kwa uangalifu sana, 16 ili msije mkajichafua na kujitengenezea sanamu au kinyago chenye umbo lolote kama la mwanaume au mwanamke, 17 au kama mnyama aliye juu ya nchi au ndege yeyote arukaye angani, 18 au kama kiumbe kitambaacho juu ya ardhi au samaki yeyote aliye ndani ya maji. 19 Na utazamapo juu angani na ukaliona jua, mwezi na nyota na vyote vinavyoipamba mbingu, usije ukashawishiwa kuviinamia na kuviabudu vile ambavyo Bwana Mungu wenu alivyogawia mataifa yote chini ya mbingu. 20 Lakini kwenu ninyi, Bwana amewatoa kutoka kwenye tanuru ya kuyeyushia chuma, katika Misri kuwa watu wa urithi wake kama mlivyo sasa.

  18. 1 Kukaonekana ishara kuu mbinguni: Palikuwa na mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ukiwa chini ya miguu yake, na taji ya nyota kumi na mbili ilikuwa kichwani mwake. 2 Alikuwa na mimba naye akilia kwa uchungu kwa kuwa alikuwa anakaribia kuzaa. 3 Kisha ishara nyingine ikaonekana mbinguni: Likaonekana joka kubwa jekundu lenye vichwa saba na pembe kumi na taji saba katika vichwa vyake. 4 Mkia wake ukakokota theluthi ya nyota zote angani na kuziangusha katika nchi. Ndipo lile joka likasimama mbele ya yule mwanamke aliyekuwa karibu kuzaa ili lipate kumla huyo mtoto mara tu atakapozaliwa.

  19. 42 Ndipo Mungu akageuka, akawaacha waabudu jeshi lote la mbinguni, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Manabii:

    “ ‘Je, mliniletea dhabihu na sadaka

    kwa miaka arobaini kule jangwani,

    ee nyumba ya Israeli?

    43 La, ninyi mliinua madhabahu ya Moleki,

    na nyota ya mungu wenu Refani,

    vinyago mlivyotengeneza ili kuviabudu.

    Kwa hiyo nitawapeleka mbali’ kuliko Babeli.

  20. 26 “Atakayeshinda na kutenda mapenzi yangu mpaka mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa:

    27 “ ‘Atawatawala kwa fimbo ya chuma,

    atawavunja vipande vipande

    kama chombo cha udongo’:

    kama vile mimi nilivyopokea mamlaka kutoka kwa Baba yangu. 28 Nami nitampa pia ile nyota ya asubuhi.

  21. 31 “Je, waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia?

    Waweza kulegeza kamba za Orioni?

    32 Waweza kuyaongoza makundi ya nyota kwa majira yake,

    au kuongoza Dubu na watoto wake?

    33 Je, unajua sheria zinazotawala mbingu?

    Waweza kuweka utawala wa Mungu duniani?

  22. 26 Inueni macho yenu mtazame mbinguni:

    Ni nani aliyeumba hivi vyote?

    Ni yeye aletaye nje jeshi la nyota moja baada ya nyingine

    na kuziita kila moja kwa jina lake.

    Kwa sababu ya uweza wake mkuu na nguvu zake kuu,

    hakuna hata mojawapo inayokosekana.

    27 Kwa nini unasema, ee Yakobo,

    nanyi ee Israeli, kulalamika,

    “Njia yangu imefichwa Bwana asiione,

    Mungu wangu hajali shauri langu?”

    28 Je wewe, hufahamu?

    Je wewe, hujasikia?

    Bwana ni Mungu wa milele,

    Muumba wa miisho ya dunia.

    Hatachoka wala kulegea,

    wala hakuna hata mmoja

    awezaye kuupima ufahamu wake.

    29 Huwapa nguvu waliolegea

    na huongeza nguvu za wadhaifu.

  23. 25 “Je, mliniletea dhabihu na sadaka

    kwa miaka arobaini kule jangwani,

    ee nyumba ya Israeli?

    26 Mmeyainua madhabahu ya mfalme wenu,

    Sikuthi mungu wenu mtawala,

    na Kiuni mungu wenu wa nyota,

    ambao mliwatengeneza wenyewe.

    27 Kwa sababu hiyo nitawapeleka uhamishoni mbali kupita Dameski,”

    asema Bwana, ambaye jina lake ni Mungu Mwenye Nguvu Zote.

  24. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

    1 Mbingu zinatangaza utukufu wa Mungu,

    anga zahubiri kazi ya mikono yake.

    2 Siku baada ya siku zinatoa habari,

    usiku baada ya usiku zinatangaza maarifa.

    3 Hakuna msemo wala lugha,

    ambapo sauti zao hazisikiki.

    4 Sauti yao imeenea duniani pote,

    nayo maneno yao yameenea

    hadi miisho ya ulimwengu.

    Katika mbingu amepiga hema kwa ajili ya jua,

    5 linafanana na bwana arusi

    akitoka chumbani mwake,

    kama shujaa afurahiavyo

    kukamilisha kushindana kwake.

    6 Huchomoza upande mmoja wa mbingu,

    na kufanya mzunguko wake

    hadi upande mwingine.

    Hakuna kilichojificha joto lake.

  25. 12 Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni,

    ewe nyota ya asubuhi, mwana wa mapambazuko!

    Umetupwa chini duniani,

    wewe uliyepata kuangusha mataifa!

    13 Ulisema moyoni mwako,

    “Nitapanda juu hadi mbinguni,

    nitakiinua kiti changu cha enzi

    juu ya nyota za Mungu,

    nitaketi nimetawazwa

    juu ya mlima wa kusanyiko,

    kwenye vimo vya juu sana vya Mlima Mtakatifu.

  26. 13 Ushauri wote uliopokea umekuchosha bure!

    Wanajimu wako na waje mbele,

    wale watazama nyota watabiriao mwezi baada ya mwezi,

    wao na wawaokoe na lile linalokuja juu yenu.

    14 Hakika wako kama mabua makavu;

    moto utawateketeza.

    Hawawezi hata kujiokoa wao wenyewe

    kutokana na nguvu za mwali wa moto.

    Hapa hakuna makaa ya kumtia mtu yeyote joto;

    hapa hakuna moto wa kuota.

    15 Hayo ndiyo yote wanayoweza kuwatendea ninyi,

    hawa ambao umetaabika nao

    na kufanya nao biashara tangu utoto.

    Kila mmoja atatoroka;

    hakuna yeyote awezaye kukuokoa.

  27. 4 “Ulikuwa wapi nilipoweka misingi ya dunia?

    Niambie, kama unafahamu.

    5 Ni nani aliyeweka alama vipimo vyake?

    Hakika wewe unajua!

    Ni nani aliyenyoosha kamba ya kupimia juu yake?

    6 Je, misingi yake iliwekwa juu ya nini,

    au ni nani aliyeweka jiwe la pembeni,

    7 wakati nyota za asubuhi zilipoimba pamoja,

    na malaika wote walipokuwa wakipiga kelele kwa furaha?

  28. 8 Vivyo hivyo, hawa waotao ndoto huutia mwili unajisi, hukataa kuwa chini ya mamlaka na kunena mabaya juu ya wenye mamlaka. 9 Lakini hata malaika mkuu Mikaeli alipokuwa anashindana na ibilisi juu ya mwili wa Mose, hakuthubutu kumlaumu, bali alimwambia, “Bwana na akukemee!” 10 Lakini watu hawa hunena mabaya dhidi ya mambo wasiyoyafahamu. Na katika mambo yale wanayoyafahamu kwa hisia kama wanyama wasio na akili, hayo ndiyo hasa yanayowaharibu.

    11 Ole wao! Kwa kuwa wanaifuata njia ya Kaini, wamekimbilia faida katika kosa la Balaamu na kuangamia katika uasi wa Kora.

    12 Watu hawa ni dosari katika karamu zenu za upendo, wakila pamoja nanyi bila hofu, wakijilisha pasipo hofu. Wao ni mawingu yasiyokuwa na maji, yakichukuliwa na upepo, miti isiyo na matunda wakati wa mapukutiko, ambayo hunyauka, iliyokufa mara mbili na kungʼolewa kabisa. 13 Wao ni mawimbi makali ya bahari, yakitoa povu la aibu yao wenyewe, ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba waliowekewa milele.

  29. 7 Nitakapokuzimisha, nitafunika mbingu

    na kuzitia nyota zake giza;

    nitalifunika jua kwa wingu,

    nao mwezi hautatoa nuru yake.

    8 Mianga yote itoayo nuru angani

    nitaitia giza juu yako;

    nitaleta giza juu ya nchi yako,

    asema Bwana Mwenyezi.

  30. 29 “Mara baada ya dhiki ya siku zile,

    “ ‘jua litatiwa giza,

    nao mwezi hautatoa nuru yake;

    nazo nyota zitaanguka kutoka angani,

    na nguvu za anga zitatikisika.’

    30 “Ndipo itakapotokea ishara ya Mwana wa Adamu angani, na makabila yote ya dunia yataomboleza. Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya angani, katika uwezo na utukufu mkuu.

  31. 10 Mbele yao dunia inatikisika,

    anga linatetemeka,

    jua na mwezi vinatiwa giza,

    na nyota hazitoi mwanga wake tena.

    11 Bwana anatoa mshindo wa ngurumo

    mbele ya jeshi lake;

    majeshi yake hayana idadi,

    ni wenye nguvu nyingi

    wale ambao hutii agizo lake.

    Siku ya Bwana ni kuu,

    ni ya kutisha.

    Ni nani anayeweza kuistahimili?

  32. 24 “Lakini katika siku hizo, baada ya hiyo dhiki,

    “ ‘jua litatiwa giza

    nao mwezi hautatoa nuru yake;

    25 nazo nyota zitaanguka kutoka angani,

    na nguvu za anga zitatikisika.’

    26 “Ndipo watu wote watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu. 27 Naye atawatuma malaika wake wawakusanye wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka miisho ya dunia hadi miisho ya mbingu.

  33. 19 Nasi tunalo pia neno la hakika zaidi la unabii, ambalo mtafanya vyema mkiliangalia kwa bidii, kama vile nuru inavyongʼaa gizani, hadi kupambazuka na nyota ya asubuhi izuke mioyoni mwenu. 20 Zaidi ya yote, yawapasa mjue kwamba hakuna unabii katika Maandiko uliofasiriwa kama alivyopenda nabii mwenyewe. 21 Kwa maana unabii haukuja kamwe kwa mapenzi ya mwanadamu, bali watu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

  34. 4 Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani mkuu, makuhani waliomfuata kwa cheo, na mabawabu kuondoa kutoka kwenye Hekalu la Bwana vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali na Ashera na jeshi lote la mianga ya angani! Akavichoma nje ya Yerusalemu katika mashamba ya Bonde la Kidroni, na kuyachukua hayo majivu mpaka Betheli. 5 Akawafukuza makuhani wa kipagani waliokuwa wameteuliwa na wafalme wa Yuda kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji ya Yuda na ile iliyozunguka Yerusalemu, yaani wale waliofukiza uvumba kwa Baali, kwa jua na mwezi, kwa makundi ya nyota, na jeshi lote la angani.

  35. 12 Nikatazama akiivunja ile lakiri ya sita. Pakatokea tetemeko kuu la nchi, na jua likawa jeusi kama nguo ya gunia iliyotengenezwa kwa singa za mbuzi, na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu. 13 Nyota zilizo angani zikaanguka ardhini kama vile matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. 14 Anga ikatoweka kama vile karatasi isokotwavyo, na kila mlima na kila kisiwa kikaondolewa mahali pake.

  36. 15 Jua na mwezi vitatiwa giza,

    na nyota hazitatoa mwanga wake tena.

  37. 10 “Kisha livunje lile gudulia wale walio pamoja nawe wakiwa wanaangalia, 11 uwaambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo: Nitalivunja taifa hili na mji huu kama gudulia hili la mfinyanzi lilivyovunjwa, nalo haliwezi kutengenezeka tena. Watawazika waliokufa huko Tofethi hata isiwepo nafasi zaidi. 12 Hivi ndivyo nitakavyopafanya mahali hapa na kwa wale waishio ndani yake, asema Bwana. Nitaufanya mji huu kama Tofethi. 13 Nyumba zilizoko Yerusalemu na zile za wafalme wa Yuda zitatiwa unajisi kama mahali hapa, Tofethi: yaani nyumba zote ambazo walifukiza uvumba juu ya mapaa yake kwa jeshi lote la angani, na kumimina dhabihu za vinywaji kwa miungu mingine.’ ”

  38. 35 Hili ndilo asemalo Bwana,

    yeye aliyeweka jua

    liwake mchana,

    yeye anayeamuru mwezi na nyota

    kungʼaa usiku,

    yeye aichafuaye bahari

    ili mawimbi yake yangurume;

    Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake:

    36 “Ikiwa amri hizi zitaondoka machoni pangu,”

    asema Bwana,

    “ndipo wazao wa Israeli watakoma

    kuwa taifa mbele yangu daima.”

    37 Hili ndilo asemalo Bwana:

    “Ikiwa mbingu zilizo juu zitaweza kupimika

    na misingi ya dunia chini

    ikaweza kuchunguzwa,

    ndipo nitakapowakataa wazao wote wa Israeli

    kwa sababu ya yote waliyoyatenda,”

    asema Bwana.

  39. 5 Bwana hupenda uadilifu na haki;

    dunia imejaa upendo wake usiokoma.

    6 Kwa neno la Bwana mbingu ziliumbwa,

    jeshi lao la angani kwa pumzi ya kinywa chake.

    7 Ameyakusanya maji ya bahari

    kama kwenye chungu;

    vilindi vya bahari

    ameviweka katika ghala.

    8 Dunia yote na imwogope Bwana,

    watu wote wa dunia wamche.

  40. 1 Njooni karibu, enyi mataifa, nanyi msikilize;

    sikilizeni kwa makini,

    enyi kabila za watu!

    Dunia na isikie, navyo vyote vilivyo ndani yake,

    ulimwengu na vyote vitokavyo ndani yake!

    2 Bwana ameyakasirikia mataifa yote;

    ghadhabu yake ni juu ya majeshi yao yote.

    Atawaangamiza kabisa,

    atawatia mikononi mwa wachinjaji.

    3 Waliouawa watatupwa nje,

    maiti zao zitatoa uvundo,

    milima itatota kwa damu zao.

    4 Nyota zote za mbinguni zitayeyuka

    na anga litasokotwa kama kitabu,

    jeshi lote la angani litaanguka

    kama majani yaliyonyauka kutoka kwenye mzabibu,

    kama tini iliyonyauka kutoka kwenye mtini.

  41. 16 Wakayaacha maagizo yote ya Bwana Mungu wao na kujitengenezea sanamu mbili, walizozisubu katika sura ya ndama na nguzo ya Ashera. Wakasujudia mianga yote ya angani, na wakamtumikia Baali. 17 Wakawatoa kafara wana wao na mabinti zao katika moto. Wakafanya uaguzi na uchawi, nao wakajiuza wenyewe katika kutenda uovu machoni pa Bwana, wakamghadhibisha.

    18 Basi Bwana akawakasirikia sana Israeli na kuwaondoa kwenye uwepo wake. Ni kabila la Yuda tu lililobaki; 19 na hata hivyo nao Yuda hawakuzishika amri za Bwana Mungu wao. Wakafuata desturi ambazo Israeli walikuwa wamezianzisha. 20 Kwa hiyo Bwana aliwakataa watu wote wa Israeli; akawatesa na kuwaachia katika mikono ya wateka nyara hadi alipowaondoa kutoka kwenye uwepo wake.

  42. 1 “ ‘Wakati huo, asema Bwana, mifupa ya wafalme na maafisa wa Yuda, mifupa ya makuhani na manabii, na mifupa ya watu wa Yerusalemu itaondolewa kutoka makaburi yao. 2 Itawekwa wazi kwa jua, na mwezi, na nyota zote za mbingu, ambazo walizipenda na kuzitumikia, na ambazo wamezifuata kutafuta ushauri na kuziabudu. Hawatakusanywa pamoja au kuzikwa, lakini watakuwa kama mavi yaliyotapakaa juu ya ardhi. 3 Popote nitakapowafukuzia, mabaki wote wa kizazi hiki kiovu watatamani kufa kuliko kuishi, asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.’

  43. 10 Pembe hiyo ikaendelea kukua hadi kufikia jeshi la mbinguni, nayo ikalitupa baadhi ya jeshi la vitu vya angani hapa chini duniani, na kulikanyaga.

  44. 15 Basi malaika wa Bwana akamwita Abrahamu kutoka mbinguni mara ya pili, 16 akasema, “Ninaapa kwa nafsi yangu, asema Bwana, kwamba kwa sababu umefanya jambo hili na hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee, 17 hakika nitakubariki, na nitauzidisha uzao wako kama nyota za angani na kama mchanga ulioko pwani. Wazao wako watamiliki miji ya adui zao, 18 na kupitia uzao wako mataifa yote duniani yatabarikiwa, kwa sababu umenitii.”

  45. 1 Ndipo Bildadi Mshuhi akajibu:

    2 “Mamlaka na kuheshimiwa ni vyake Mungu;

    yeye huthibitisha amani katika mbingu juu.

    3 Je, majeshi yake yaweza kuhesabika?

    Ni nani asiyeangaziwa na nuru yake?

    4 Mtu awezaje kuwa mwadilifu mbele za Mungu?

    Awezaje mtu aliyezaliwa na mwanamke kuwa safi?

    5 Ikiwa hata mwezi sio mwangavu

    nazo nyota si safi machoni pake,

    6 sembuse mtu ambaye ni funza:

    mwanadamu ambaye ni buu tu!”

  46. 4 “Nitaiadhibu Yuda

    na wote wakaao Yerusalemu.

    Kutoka mahali hapa nitakatilia mbali

    kila mabaki ya Baali,

    majina ya wapagani na makuhani

    waabuduo sanamu:

    5 wale ambao husujudu juu ya mapaa

    kuabudu jeshi la vitu vya angani,

    wale ambao husujudu na kuapa kwa Bwana

    na ambao pia huapa kwa Malkamu,

    6 wale wanaoacha kumfuata Bwana,

    wala hawamtafuti Bwana

    wala kutaka shauri lake.

  47. 12 Kwa hiyo, wapenzi wangu, kama vile ambavyo mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwepo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka, 13 kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema.

    14 Fanyeni mambo yote bila kunungʼunika wala kushindana, 15 ili msiwe na lawama wala hatia, bali mwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka, ambacho ndani yake ninyi mnangʼaa kama mianga ulimwenguni. 16 Mkilishika neno la uzima, ili nipate kuona fahari siku ya Kristo kwamba sikupiga mbio wala kujitaabisha bure.

  48. 22 Baba zako walioshuka kwenda Misri jumla yao walikuwa sabini, na sasa Bwana Mungu wako amekufanya wengi kama nyota za angani.

  49. 2 Ikiwa mwanaume au mwanamke anayeishi kati ya mojawapo ya miji akupayo Bwana, anakutwa anafanya uovu mbele za Bwana Mungu wenu, kwa kuvunja Agano lake, 3 naye amekwenda kinyume na agizo langu kuabudu miungu mingine na kuisujudia, kama vile jua, mwezi au nyota za angani, 4 hili likiwa limeletwa mbele yenu, ni lazima kulichunguza kikamilifu. Ikiwa ni kweli na kuwa limehakikishwa kwamba hili ni chukizo lililofanyika katika Israeli, 5 mchukueni huyo mwanaume au mwanamke ambaye amelifanya tendo hili ovu kwenye lango la mji wenu na kumpiga mawe mtu huyo mpaka afe. 6 Kwa ushuhuda wa mashahidi wawili au watatu mtu huyo atauawa, bali hakuna mtu atakayeuawa kwa ushuhuda wa shahidi mmoja tu. 7 Ni lazima kwanza mikono ya mashahidi itangulie kumuua huyo mtu, kisha mikono ya watu wote. Ni lazima mwondoe uovu miongoni mwenu.

  50. 1 Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na mitano. Mama yake aliitwa Hefsiba. 2 Akafanya maovu machoni pa Bwana, akafuata desturi za machukizo za mataifa ambayo Bwana aliyafukuza mbele ya Waisraeli. 3 Akajenga upya mahali pa juu pa kuabudia miungu ambapo Hezekia baba yake alikuwa amepabomoa. Pia akasimamisha madhabahu za Baali na kutengeneza nguzo ya Ashera, kama Ahabu mfalme wa Israeli alivyofanya. Akalisujudia jeshi lote la angani na kuliabudu. 4 Akajenga madhabahu katika Hekalu la Bwana, ambamo Bwana alikuwa amesema, “Katika Yerusalemu nitaliweka Jina langu.” 5 Katika nyua zote mbili za Hekalu la Bwana, akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la angani. 6 Akamtoa kafara mwanawe mwenyewe katika moto, akafanya uchawi na uaguzi, na akataka shauri kwa wapiga ramli na kwa mizimu. Akafanya maovu mengi sana machoni mwa Bwana na kumghadhibisha.

  51. 23 Daudi hakuwahesabu watu waliokuwa chini ya miaka ishirini, kwa sababu Bwana alikuwa ameahidi kuwafanya Israeli kuwa wengi kama nyota za angani.

  52. 6 Wewe peke yako ndiwe Bwana. Uliziumba mbingu, hata mbingu za mbingu na jeshi lote la mbinguni, dunia na vyote vilivyo ndani yake, na pia bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Huvipa vitu vyote uhai, nalo jeshi la mbinguni linakuabudu wewe.

  53. 8 Kwa imani Abrahamu, alipoitwa aende mahali ambapo Mungu angempa baadaye kuwa urithi, alitii na akaenda, ingawa hakujua anakokwenda. 9 Kwa imani alifanya maskani yake katika nchi ya ahadi kama mgeni katika nchi ya kigeni; aliishi katika mahema, kama Isaki na Yakobo walivyofanya, waliokuwa pia warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. 10 Kwa maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi ya kudumu ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.

    11 Kwa imani Abrahamu, ingawa alikuwa mzee wa umri, naye Sara mwenyewe aliyekuwa tasa, alipokea uwezo wa kuwa baba kwa sababu alimhesabu Mungu aliyemwahidi kuwa mwaminifu na kwamba angetimiza ahadi yake. 12 Hivyo kutokana na huyu huyu ambaye alikuwa sawa na mfu, wakazaliwa wazao wengi kama nyota za mbinguni na kama mchanga wa pwani usiohesabika.

  54. 9 Kisha akaota ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake akisema, “Sikilizeni, nimeota ndoto nyingine, wakati huu jua, mwezi na nyota kumi na moja zilikuwa zinanisujudia.”

    10 Alipomwambia baba yake pamoja na ndugu zake, baba yake akamkemea akisema, “Ni ndoto gani hii uliyoota? Hivi kweli mama yako na mimi na ndugu zako tutakuja kukusujudia wewe hadi nchi?”

  55. 1 Malaika wa tano akaipiga tarumbeta yake, nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka toka angani hadi ardhini. Nyota hiyo ilipewa ufunguo wa lile Shimo.

  56. 11 “Hili ndilo asemalo Bwana,

    yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na Muumba wake:

    Kuhusu mambo yatakayokuja,

    je, unaniuliza habari za watoto wangu,

    au kunipa amri kuhusu kazi za mikono yangu?

    12 Mimi ndiye niliyeumba dunia

    na kumuumba mwanadamu juu yake.

    Mikono yangu mwenyewe ndiyo iliyozitanda mbingu,

    nikayapanga majeshi yake yote ya angani.

  57. 1 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika:

    “Haya ndiyo maneno ya yule aliyezishika zile nyota saba katika mkono wake wa kuume na ambaye hutembea kati ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu. 2 Nayajua matendo yako, bidii yako na saburi yako. Najua kuwa huwezi kuvumiliana na watu waovu na ya kwamba umewajaribu wale wanaojifanya kuwa mitume na kumbe sio, nawe umewatambua kuwa ni waongo. 3 Umevumilia na kustahimili taabu kwa ajili ya Jina langu, wala hukuchoka.

    4 “Lakini nina neno dhidi yako: Umeuacha upendo wako wa kwanza. 5 Kumbuka basi ni wapi ulikoangukia! Tubu na ukafanye matendo yale ya kwanza. Kama usipotubu, nitakuja kwako na kukiondoa kinara chako cha taa kutoka mahali pake. 6 Lakini una jambo hili kwa upande wako: Unayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo nami pia nayachukia.

    7 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa haki ya kula matunda toka kwa mti wa uzima, ambao uko katika paradiso ya Mungu.

  58. 21 Basi tuliendelea na kazi, nusu ya watu wakishikilia mikuki, kuanzia mawio ya jua hadi nyota zilipoonekana. 22 Wakati huo pia niliwaambia watu, “Kila mtu na msaidizi wake wakae ndani ya Yerusalemu wakati wa usiku, ili waweze kutumika kama walinzi wakati wa usiku, na kufanya kazi wakati wa mchana.” 23 Mimi, wala ndugu zangu, wala watu wangu, wala walinzi waliokuwa pamoja nami hatukuvua nguo zetu. Kila mmoja alikuwa na silaha yake, hata alipokwenda kuchota maji.

  59. 9 Nyota zake za alfajiri na ziwe giza;

    nao ungojee mwanga bila mafanikio,

    wala usiuone mwonzi wa kwanza

    wa mapambazuko,

  60. 12 “Je, Mungu hayuko katika mbingu za juu?

    Juu kuliko nyota zilizo juu sana!

  61. 22 Nitawafanya wazao wa Daudi mtumishi wangu na Walawi wanaohudumu mbele zangu wengi, wasioweza kuhesabika kama nyota za angani, tena wasiopimika kama mchanga wa ufuoni mwa bahari.’ ”

  62. 25 “Kutakuwa na ishara katika jua, mwezi na nyota. Hapa duniani, mataifa yatakuwa katika dhiki na fadhaa kutokana na ngurumo na misukosuko ya bahari. 26 Watu watazimia roho kutokana na hofu kuu na kuyaona yale mambo yanayotokea duniani, kwa maana nguvu za angani zitatikisika. 27 Wakati huo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni pamoja na uweza na utukufu mkuu.

  63. 20 Kulipokuwa hakuna kuonekana kwa jua wala nyota kwa siku nyingi, nayo dhoruba ikiwa inaendelea kuwa kali, hatimaye tulikata kabisa tamaa ya kuokoka.

  64. 4 Nitafanya wazao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa nchi hizi zote na kutokana na uzao wako mataifa yote yatabarikiwa,

  65. 1 Mkumbuke Muumba wako

    siku za ujana wako,

    kabla hazijaja siku za taabu,

    wala haijakaribia miaka utakaposema,

    “Mimi sifurahii hiyo”:

    2 kabla jua na nuru,

    nao mwezi na nyota havijatiwa giza,

    kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua;

    3 siku ile walinzi wa nyumba watakapotetemeka,

    nao watu wenye nguvu watakapojiinamisha,

    wakati wasagao watakapokoma kwa sababu ya uchache,

    nao wachunguliao madirishani kutiwa giza;

    4 wakati milango ya kuingia barabarani itakapofungwa

    na sauti ya kusaga kufifia;

    wakati watu wataamshwa kwa sauti ya ndege,

    lakini nyimbo zao zote zikififia;

    5 wakati watu watakapoogopa kilichoinuka juu

    na hatari zitakazokuwepo barabarani;

    wakati mlozi utakapochanua maua

    na panzi kujikokota

    nawe usiwe na shauku ya kitu chochote.

    Ndipo mwanadamu aiendea nyumba yake ya milele

    nao waombolezaji wakizunguka barabarani.

    6 Mkumbuke Muumba wako: kabla haijakatika kamba ya fedha,

    au bakuli la dhahabu halijavunjika;

    kabla mtungi kuvunjika kwenye chemchemi,

    au gurudumu kuvunjika kisimani,

    7 nayo mavumbi kurudi ardhini yalikotoka,

    na roho kurudi kwa Mungu aliyeitoa.

    8 Mhubiri asema, “Ubatili! Ubatili!

    Kila kitu ni ubatili!”

  66. 13 Wakumbuke watumishi wako Abrahamu, Isaki na Israeli, ambao uliwaapia kwa nafsi yako mwenyewe: ‘Nitawafanya uzao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa wazao wako nchi hii yote ambayo niliwaahidia, nayo itakuwa urithi wao milele.’ ”

  67. 1 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika:

    “Haya ndiyo maneno ya aliye na zile Roho saba za Mungu na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, kwamba una sifa ya kuwa hai, lakini umekufa.

  68. 10 Bwana Mungu wenu ameongeza hesabu yenu, hivi kwamba leo ninyi ni wengi kama nyota za angani.

  69. 1 Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia.

  70. 16 Mchana ni wako, nao usiku ni wako pia,

    uliziweka jua na mwezi.

  71. 19 Mwezi hugawanya majira,

    na jua hutambua wakati wake wa kutua.

  72. 16 Ndipo akanileta mpaka kwenye ukumbi wa ndani wa nyumba ya Bwana, nako huko katika ingilio la Hekalu, kati ya baraza na madhabahu, walikuwepo wanaume wapatao ishirini na watano. Wakiwa wamelipa kisogo Hekalu la Bwana na kuelekeza nyuso zao upande wa mashariki, wakilisujudia jua huko mashariki.

    17 Akaniambia, “Je, umeona hili mwanadamu? Je, ni jambo dogo sana kwa nyumba ya Yuda kufanya machukizo wanayoyafanya hapa? Je, ni lazima pia waijaze nchi dhuluma na kuendelea siku zote kunikasirisha? Watazame wanavyonibania pua kana kwamba ninanuka! 18 Kwa hiyo nitashughulika nao kwa hasira, sitawaonea huruma wala kuwaachilia. Wajapopiga makelele masikioni mwangu, sitawasikiliza.”

  73. 3 Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo. 4 Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema, ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza. 5 Mungu akaiita nuru “mchana,” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza.

  74. 1 Kwa hiyo mbingu na dunia zikakamilika, pamoja na vyote vilivyomo.

    2 Katika siku ya saba Mungu alikuwa amekamilisha kazi aliyokuwa akiifanya, hivyo siku ya saba akapumzika kutoka kazi zake zote. 3 Mungu akaibariki siku ya saba akaifanya takatifu, kwa sababu katika siku hiyo alipumzika kutoka kazi zote za kuumba alizokuwa amefanya.

  75. 26 kama nimelitazama jua katika kungʼaa kwake

    au mwezi ukienda kwa fahari yake,

    27 hivyo moyo wangu kushawishiwa kwa siri,

    au kubusu mkono wangu kwa kuviheshimu,

    28 basi hiyo pia ingekuwa dhambi ya kuhukumiwa,

    kwa kuwa ningekuwa si mwaminifu kwa Mungu aishiye juu sana.

  76. 5 Ee Bwana, mbingu zinayasifu maajabu yako,

    uaminifu wako pia katika kusanyiko la watakatifu.

  77. 31 Jua litageuzwa kuwa giza

    na mwezi kuwa mwekundu kama damu,

    kabla ya kuja siku ya Bwana

    ile kuu na ya kutisha.

  78. 1 Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2 Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu.

    3 Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa.