39 Bible Verses About Obedience

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Obedience
  1. 19 Ndugu zangu wapendwa, fahamuni jambo hili: Kila mtu awe mwepesi wa kusikiliza, lakini asiwe mwepesi wa kusema wala wa kukasirika. 20 Kwa maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu. 21 Kwa hiyo, ondoleeni mbali uchafu wote na uovu ambao umezidi kuwa mwingi, mkalipokee kwa unyenyekevu lile Neno lililopandwa ndani yenu ambalo laweza kuokoa nafsi zenu.

    22 Basi kuweni watendaji wa Neno wala msiwe wasikiaji tu, huku mkijidanganya nafsi zenu. 23 Kwa maana kama mtu ni msikiaji tu wa Neno wala hatendi kile linachosema, yeye ni kama mtu ajitazamaye uso wake kwenye kioo 24 na baada ya kujiona alivyo, huenda zake na mara husahau jinsi alivyo. 25 Lakini yeye anayeangalia kwa bidii katika sheria kamilifu, ile iletayo uhuru, naye akaendelea kufanya hivyo bila kusahau alichosikia, bali akalitenda, atabarikiwa katika kile anachofanya.

  2. 15 “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu.

  3. 17 Kwa maana ikiwa kutokana na kosa la mtu mmoja, mauti ilitawala kupitia huyo mtu mmoja, zaidi sana wale wanaopokea wingi wa neema ya Mungu na karama yake ya kuhesabiwa haki, watatawala katika uzima kwa njia ya huyo mtu mmoja, yaani, Yesu Kristo.

    18 Kwa hiyo, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta adhabu kwa watu wote, vivyo hivyo pia kwa tendo la haki la mtu mmoja lilileta kuhesabiwa haki ambako huleta uzima kwa wote. 19 Kwa maana kama vile kwa kutokutii kwa yule mtu mmoja wengi walifanywa wenye dhambi, vivyo hivyo kwa kutii kwa mtu mmoja wengi watafanywa wenye haki.

  4. 16 Je, hamjui kwamba mnapojitoa kwa mtu yeyote kama watumwa watiifu, ninyi ni watumwa wa yule mnayemtii, aidha watumwa wa dhambi, ambayo matokeo yake ni mauti, au watumwa wa utii ambao matokeo yake ni haki? 17 Lakini Mungu ashukuriwe kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa. 18 Nanyi, mkiisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki.

  5. 22 Ndipo Yuda, siyo Iskariote, akamwambia, “Bwana, itakuwaje kwamba utajidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?”

    23 Yesu akamjibu, “Mtu yeyote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake. 24 Mtu yeyote asiyenipenda hayashiki maneno yangu na maneno niliyowapa si yangu bali ni ya Baba aliyenituma.

  6. 18 “Njooni basi tuhojiane,”

    asema Bwana.

    “Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu,

    zitakuwa nyeupe kama theluji;

    ingawa ni nyekundu sana kama damu,

    zitakuwa nyeupe kama sufu.

    19 Kama mkikubali na kutii,

    mtakula mema ya nchi,

    20 lakini kama mkikataa na kuasi,

    mtaangamizwa kwa upanga.”

    Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena.

  7. 21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22 Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’ 23 Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’

    24 “Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. 25 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, na upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba. Lakini haikuanguka; kwa sababu msingi wake ulikuwa kwenye mwamba. 26 Naye kila anayesikia haya maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. 27 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.”

  8. 22 Lakini Samweli akajibu:

    “Je, Bwana anafurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu

    kama vile kuitii sauti ya Bwana?

    Kutii ni bora zaidi kuliko dhabihu,

    nako kusikia ni bora

    kuliko mafuta ya kondoo dume.

    23 Kwa maana kuasi ni kama dhambi ya uaguzi,

    nao ukaidi ni kama uovu wa kuabudu sanamu.

    Kwa sababu umelikataa neno la Bwana,

    naye amekukataa wewe

    kuendelea kuwa mfalme.”

  9. 21 Yeyote mwenye amri zangu na kuzishika ndiye anipendaye, naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”

  10. 10 Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. 11 Nimewaambia mambo haya ili furaha yangu iwe ndani yenu na furaha yenu iwe kamili. 12 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi. 13 Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. 14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru.

  11. 5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:

    6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,

    hakuona kule kuwa sawa na Mungu

    kuwa kitu cha kushikilia,

    7 bali alijifanya si kitu,

    akachukua hali hasa na mtumwa,

    naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.

    8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,

    alijinyenyekeza, akatii hata mauti:

    naam, mauti ya msalaba!

  12. 13 Kwa hiyo, tayarisheni nia zenu kwa kazi; mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa Yesu Kristo atakapodhihirishwa. 14 Kama watoto watiifu, msifuate tamaa zenu mbaya wakati mlipoishi kwa ujinga. 15 Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, nanyi kuweni watakatifu katika mwenendo wenu wote. 16 Kwa maana imeandikwa: “Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”

    17 Kwa sababu mnamwita Baba ahukumuye kila mtu kulingana na matendo yake pasipo upendeleo, enendeni kwa hofu ya kumcha Mungu wakati wenu wa kukaa hapa duniani kama wageni.

  13. 2 Hivi ndivyo tunavyojua kwamba tunawapenda watoto wa Mungu, kwa kumpenda Mungu na kuzitii amri zake. 3 Huku ndiko kumpenda Mungu, yaani, kuzitii amri zake. Nazo amri zake si nzito.

  14. 27 Ikawa Yesu alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katikati ya ule umati wa watu akapaza sauti akasema, “Limebarikiwa tumbo lililokuzaa na matiti uliyonyonya!”

    28 Yesu akajibu, “Wamebarikiwa zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulitii.”

  15. 14 Ndugu zangu, yafaa nini ikiwa mtu atadai kuwa anayo imani lakini hana matendo? Je, imani kama hiyo yaweza kumwokoa? 15 Ikiwa ndugu yako au dada hana mavazi wala chakula, 16 mmoja wenu akamwambia, “Enenda zako kwa amani, ukaote moto na kushiba,” pasipo kumpatia yale mahitaji ya mwili aliyopungukiwa, yafaa nini? 17 Vivyo hivyo, imani peke yake kama haikuambatana na matendo, imekufa.

    18 Lakini mtu mwingine atasema, “Wewe unayo imani; mimi ninayo matendo.”

    Nionyeshe imani yako pasipo matendo nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo. 19 Unaamini kwamba kuna Mungu mmoja. Vyema! Hata mashetani yanaamini hivyo na kutetemeka.

    20 Ewe mpumbavu! Je, wataka kujua kwamba imani bila matendo haifai kitu? 21 Je, Abrahamu baba yetu hakuhesabiwa haki kwa kile alichotenda, alipomtoa mwanawe Isaki madhabahuni? 22 Unaona jinsi ambavyo imani yake na matendo yake vilikuwa vinatenda kazi pamoja, nayo imani yake ikakamilishwa na kile alichotenda. 23 Kwa njia hiyo yakatimizwa yale Maandiko yasemayo, “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki,” naye akaitwa rafiki wa Mungu. 24 Mnaona ya kwamba mtu huhesabiwa haki kwa yale anayotenda wala si kwa imani peke yake.

    25 Vivyo hivyo, hata Rahabu, yule kahaba, hakuhesabiwa haki kwa yale aliyotenda alipowapokea wale wapelelezi na kuwaambia waende njia nyingine? 26 Kama vile ambavyo mwili pasipo roho umekufa, kadhalika nayo imani pasipo matendo imekufa.

  16. 15 Basi malaika wa Bwana akamwita Abrahamu kutoka mbinguni mara ya pili, 16 akasema, “Ninaapa kwa nafsi yangu, asema Bwana, kwamba kwa sababu umefanya jambo hili na hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee, 17 hakika nitakubariki, na nitauzidisha uzao wako kama nyota za angani na kama mchanga ulioko pwani. Wazao wako watamiliki miji ya adui zao, 18 na kupitia uzao wako mataifa yote duniani yatabarikiwa, kwa sababu umenitii.”

  17. 7 Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. 8 Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi.

  18. 1 Watoto wangu wapendwa, nawaandikia haya ili msitende dhambi. Lakini kama mtu yeyote akitenda dhambi, tunaye Mwombezi kwa Baba: ndiye Yesu Kristo, Mwenye Haki. 2 Yeye ndiye dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu, wala si kwa ajili ya dhambi zetu tu, bali pia kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote.

    3 Basi katika hili twajua ya kuwa tumemjua, tukizishika amri zake. 4 Mtu yeyote asemaye kuwa, “Ninamjua,” lakini hazishiki amri zake, ni mwongo, wala ndani ya mtu huyo hamna kweli. 5 Lakini mtu yeyote anayelitii neno lake, upendo wa Mungu umekamilika ndani yake kweli kweli. Katika hili twajua kuwa tumo ndani yake. 6 Yeyote anayesema anakaa ndani yake hana budi kuenenda kama Yesu alivyoenenda.

  19. 21 Wapendwa, kama mioyo yetu haituhukumu, tunao ujasiri mbele za Mungu, 22 lolote tuombalo, twalipokea kutoka kwake, kwa sababu tumezitii amri zake na kutenda yale yanayompendeza. 23 Hii ndiyo amri yake: kwamba tuliamini Jina la Mwanawe, Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi kama yeye alivyotuamuru. 24 Wale wote wanaozishika amri zake hukaa ndani yake na yeye ndani yao. Hivi ndivyo tunavyojua kwamba anakaa ndani yetu. Nasi twajua hili kwa njia ya Roho yule aliyetupa.

  20. 1 Kila mtu na atii mamlaka inayotawala, kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu, nazo mamlaka zilizopo zimewekwa na Mungu. 2 Kwa hiyo yeye anayeasi dhidi ya mamlaka inayotawala anaasi dhidi ya kile kilichowekwa na Mungu, nao wale wafanyao hivyo watajiletea hukumu juu yao wenyewe.

  21. 46 “Kwa nini mnaniita, ‘Bwana, Bwana,’ nanyi hamfanyi ninayowaambia? 47 Nitawaonyesha jinsi alivyo mtu yule anayekuja kwangu na kusikia maneno yangu na kuyatenda. 48 Yeye ni kama mtu aliyejenga nyumba, akachimba chini sana, na kuweka msingi kwenye mwamba. Mafuriko yalipokuja, maji ya ghafula yaliipiga ile nyumba, lakini haikutikisika, kwa sababu ilikuwa imejengwa vizuri.

  22. 1 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, kwa kuwa hili ni jema. 2 “Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi, 3 “upate baraka na uishi siku nyingi duniani.”

  23. 1 Heri wale walio waadilifu katika njia zao,

    wanaoenenda katika sheria ya Bwana.

    2 Heri wale wanaozishika shuhuda zake,

    wamtafutao kwa moyo wao wote.

    3 Wasiofanya lolote lililo baya,

    wanaoenenda katika njia zake.

    4 Umetoa maagizo yako

    ili tuyatii kwa ukamilifu.

    5 Laiti mwenendo wangu ungekuwa imara

    katika kuyatii maagizo yako!

    6 Hivyo mimi sitaaibishwa

    ninapozingatia amri zako zote.

    7 Nitakusifu kwa moyo mnyofu

    ninapojifunza sheria zako za haki.

    8 Nitayatii maagizo yako;

    usiniache kabisa.

    9 Kijana aifanye njia yake kuwa safi jinsi gani?

    Ni kwa kutii, akilifuata neno lako.

    10 Ninakutafuta kwa moyo wangu wote,

    usiniache niende mbali na amri zako.

    11 Nimelificha neno lako moyoni mwangu

    ili nisikutende dhambi.

  24. 12 Kwa hiyo, wapenzi wangu, kama vile ambavyo mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwepo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka, 13 kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema.

  25. 18 Ninyi wake, watiini waume zenu, kama inavyostahili katika Bwana.

    19 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, wala msiwe na uchungu dhidi yao.

    20 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote, kwa maana hivi ndivyo inavyompendeza Bwana.

    21 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

    22 Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu wa hapa duniani katika mambo yote. Fanyeni hivyo si wakiwepo tu, wala si kwa kutafuta upendeleo wao, bali kwa moyo mnyofu na kumcha Bwana. 23 Lolote mfanyalo, fanyeni kwa moyo kama watu wanaomtumikia Bwana, na si wanadamu, 24 kwa kuwa mnajua kwamba mtapokea urithi wenu kutoka kwa Bwana ukiwa thawabu yenu. Ni Bwana Yesu Kristo mnayemtumikia. 25 Yeyote atendaye mabaya atalipwa kwa ajili ya mabaya yake, wala hakuna upendeleo.

  26. 4 Sikia, ee Israeli: Bwana Mungu wako, Bwana ni mmoja. 5 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. 6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. 7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo. 8 Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako. 9 Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.

  27. 59 Nimezifikiri njia zangu

    na nimeelekeza hatua zangu katika mausia yako.

    60 Nitafanya haraka bila kuchelewa

    kuzitii amri zako.

    61 Hata waovu wanifunge kwa kamba,

    sitasahau sheria yako.

    62 Usiku wa manane ninaamka kukushukuru

    kwa sababu ya sheria zako za haki.

  28. 13 Hii ndiyo jumla ya maneno;

    yote yamekwisha sikiwa:

    Mche Mungu, nawe uzishike amri zake,

    maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.

    14 Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi,

    pamoja na kila neno la siri,

    likiwa jema au baya.

  29. 1 Wakumbushe watu kuwanyenyekea watawala na kuwatii wenye mamlaka, wawe tayari kutenda kila lililo jema.

  30. 16 Bwana Mungu wako anakuagiza leo kufuata amri hizi na sheria; zishike kwa bidii kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote. 17 Umetangaza leo kwamba Bwana ndiye Mungu wako na kwamba utafuata njia zake, kwamba utayashika maagizo yake, amri zake na sheria zake nawe utamtii. 18 Naye Bwana ametangaza leo kwamba ninyi ni taifa lake, hazina yake ya thamani kama alivyoahidi, ili kwamba mpate kuyashika maagizo yake yote.

  31. 50 Kwa maana yeyote afanyaye mapenzi ya Baba yangu wa mbinguni, huyo ndiye ndugu yangu, na dada yangu na mama yangu.”

  32. 3 Akaingia katika mojawapo ya hizo mashua ambayo ilikuwa ya Simoni, akamwomba aisogeze ndani ya maji kidogo kutoka ufuoni. Kisha akaketi na kufundisha watu akiwa mle ndani ya mashua.

    4 Alipomaliza kunena, akamwambia Simoni, “Sasa peleka mashua hadi kilindini kisha mshushe nyavu zenu mkavue samaki.”

    5 Simoni akamjibu, “Bwana, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha na hatukuvua chochote. Lakini, kwa neno lako nitazishusha nyavu.”

  33. 6 Kwa maana Mungu atamlipa kila mtu sawasawa na matendo yake. 7 Wale ambao kwa kuvumilia katika kutenda mema hutafuta utukufu, heshima na maisha yasiyoharibika, Mungu atawapa uzima wa milele. 8 Lakini kwa wale watafutao mambo yao wenyewe na wale wanaokataa kweli na kuzifuata njia mbaya, kutakuwa na ghadhabu na hasira ya Mungu. 9 Kutakuwa na taabu na dhiki kwa kila mmoja atendaye maovu, Myahudi kwanza na mtu wa Mataifa pia, 10 bali utukufu, heshima na amani kwa ajili ya kila mmoja atendaye mema, kwa Myahudi kwanza, kisha kwa mtu wa Mataifa. 11 Kwa maana Mungu hana upendeleo.

  34. 22 Msikilize baba yako, aliyekuzaa,

    wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee.

  35. 16 Mtu mmoja akamjia Yesu na kumuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?”

    17 Yesu akamjibu, “Mbona unaniuliza habari ya mema? Aliye mwema ni Mmoja tu. Lakini ukitaka kuingia uzimani, zitii amri.”

  36. 2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo.

  37. 13 Mimi ni Alfa na Omega, wa Kwanza na wa Mwisho, Mwanzo na Mwisho.

    14 “Wamebarikiwa wale wafuao mavazi yao, ili wapate haki ya kuuendea huo mti wa uzima na kuuingia huo mji kupitia kwenye malango yake.

  38. 29 Laiti kama mioyo yao ingekuwa na mwelekeo wa kuniogopa na kuzishika amri zangu zote daima, ili kwamba wafanikiwe wao pamoja na watoto wao milele!

  39. 18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”