71 Bible Verses About Alcohol

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Alcohol
  1. 1 Mvinyo ni mdhihaki na kileo ni mgomvi;

    yeyote apotoshwaye navyo hana hekima.

  2. 15 Kwa hiyo angalieni sana jinsi mnavyoenenda, si kama watu wasio na hekima, bali kama wenye hekima, 16 mkiukomboa wakati, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu. 17 Kwa hiyo msiwe wajinga, bali mpate kujua nini mapenzi ya Bwana. 18 Pia msilewe kwa mvinyo, ambamo ndani yake mna upotovu, bali mjazwe Roho. 19 Msemezane ninyi kwa ninyi kwa zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, mkimwimbia na kumsifu Bwana mioyoni mwenu, 20 siku zote mkimshukuru Mungu Baba kwa kila jambo katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

  3. 4 “Ee Lemueli, haifai wafalme,

    haifai wafalme kunywa mvinyo,

    haifai watawala kutamani sana kileo,

    5 wasije wakanywa na kusahau vile sheria inavyoamuru

    na kuwanyima haki zao wote walioonewa.

    6 Wape kileo wale wanaoangamia,

    mvinyo wale walio na uchungu,

    7 Wanywe na kusahau umaskini wao

    na wasikumbuke taabu yao tena.

    8 “Sema kwa ajili ya wale wasioweza kujisemea,

    kwa ajili ya haki za wote walioachwa ukiwa.

    9 Sema na uamue kwa haki,

    tetea haki za maskini na wahitaji.”

  4. 29 Ni nani mwenye ole?

    Ni nani mwenye huzuni?

    Ni nani mwenye ugomvi?

    Ni nani mwenye malalamiko?

    Ni nani aliye na majeraha yasiyo na sababu?

    Ni nani mwenye macho mekundu?

    30 Ni hao wakaao sana kwenye mvinyo,

    hao waendao kuonja mabakuli ya mvinyo uliochanganywa.

    31 Usiukodolee macho mvinyo wakati ukiwa mwekundu,

    wakati unapometameta kwenye bilauri,

    wakati ushukapo taratibu!

    32 Mwishowe huuma kama nyoka

    na kutia sumu yake kama nyoka mwenye sumu.

    33 Macho yako yataona mambo mageni

    na moyo wako kuwazia mambo yaliyopotoka.

    34 Utakuwa kama alalaye katikati ya bahari,

    alalaye juu ya kamba ya merikebu.

    35 Utasema, “Wamenipiga lakini sikuumia!

    Wamenichapa, lakini sisikii!

    Nitaamka lini

    ili nikanywe tena?”

  5. 17 Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka. 18 Lakini kama mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria.

    19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

  6. 29 Nina maana dhamiri ya huyo aliyekuambia, wala si kwa ajili ya dhamiri yako. Lakini kwa nini uhuru wangu uhukumiwe na dhamiri ya mtu mwingine? 30 Kama nikila kwa shukrani, kwa nini nashutumiwa kwa kile ambacho kwa hicho ninamshukuru Mungu?

    31 Basi, lolote mfanyalo, kama ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.

  7. 19 Sikiliza, mwanangu na uwe na hekima,

    weka moyo wako kwenye njia iliyo sawa.

    20 Usiwe miongoni mwa wanywao mvinyo,

    au wale walao nyama kwa pupa,

    21 kwa maana walevi na walafi huwa maskini,

    nako kusinzia huwavika matambara.

  8. 23 Acha kunywa maji peke yake, tumia divai kidogo kwa sababu ya tumbo lako na maumivu yako ya mara kwa mara.

  9. 14 Huyafanya majani ya mifugo yaote,

    na mimea kwa watu kulima,

    wajipatie chakula kutoka ardhini:

    15 divai ya kuufurahisha moyo wa mwanadamu,

    mafuta kwa ajili ya kungʼarisha uso wake,

    na mkate wa kutia mwili nguvu.

  10. 20 Usiiharibu kazi ya Mungu kwa ajili ya chakula. Hakika vyakula vyote ni safi, lakini ni kosa kula kitu chochote kinachomsababisha ndugu yako ajikwae. 21 Ni afadhali kutokula nyama wala kunywa divai au kufanya jambo lingine lolote litakalomsababisha ndugu yako ajikwae.

  11. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni nia iyo hiyo kwa maana mtu aliyekwisha kuteswa katika mwili ameachana na dhambi. 2 Kwa hivyo, haishi maisha yake yaliyobaki ya kuishi hapa duniani kwa tamaa mbaya za wanadamu, bali anaishi kwa mapenzi ya Mungu. 3 Maana wakati uliopita mmekwisha kutumia muda wa kutosha katika maisha yenu mkifanya yale ambayo wapagani hupenda kutenda: wakiishi katika uasherati, tamaa mbaya, ulevi, karamu za ulafi, vileo, ngoma mbaya, na ibada chukizo za sanamu. 4 Wao hushangaa kwamba ninyi hamjiingizi pamoja nao katika huo wingi wa maisha ya ufisadi, nao huwatukana ninyi. 5 Lakini itawapasa wao kutoa hesabu mbele zake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa.

  12. 1 Bwana akamwambia Mose, 2 “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Ikiwa mwanaume au mwanamke anataka kuweka nadhiri maalum, nadhiri ya kutengwa kwa ajili ya Bwana kama Mnadhiri, 3 ni lazima ajitenge na mvinyo na kinywaji kingine chochote chenye chachu, na kamwe asinywe siki itokanayo na mvinyo au itokanayo na kinywaji kingine chenye chachu. Kamwe asinywe maji ya zabibu wala kula zabibu mbichi au kavu. 4 Kwa muda wote atakaokuwa Mnadhiri, kamwe hatakula chochote kitokanacho na mzabibu, sio mbegu wala maganda.

  13. 22 Ole wao walio mashujaa kwa kunywa mvinyo,

    nao walio hodari katika kuchanganya vileo,

    23 wale wanaoachilia wenye hatia kwa kupokea hongo,

    lakini huwanyima haki wasio na hatia.

  14. 9 Je, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wahanithi, wala walawiti, 10 wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyangʼanyi hawataurithi Ufalme wa Mungu. 11 Baadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Yesu Kristo na katika Roho wa Mungu wetu.

  15. 8 Vivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali.

  16. 1 Inakupasa kufundisha itikadi sahihi. 2 Wafundishe wazee kuwa na kiasi, wastahivu, wenye busara na wanyofu katika imani, upendo na saburi.

    3 Vivyo hivyo, wafundishe wanawake wazee kuwa na mwenendo wa utakatifu, wala wasiwe wasingiziaji au walevi, bali wafundishe yale yaliyo mema,

  17. 8 Kisha Bwana akamwambia Aroni, 9 “Wewe na wanao msinywe mvinyo wala kinywaji kingine kilichochachuka wakati mwingiapo katika Hema la Kukutania, la sivyo mtakufa. Hili litakuwa Agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. 10 Ni lazima mtenganishe kilicho kitakatifu na kile kilicho cha kawaida, kati ya yaliyo najisi na yaliyo safi, 11 na lazima mwafundishe Waisraeli amri zote ambazo Bwana aliwapa kupitia Mose.”

  18. 7 Hawa pia wanapepesuka kwa sababu ya mvinyo,

    wanayumbayumba kwa sababu ya kileo:

    Makuhani na manabii wanapepesuka kwa sababu ya kileo,

    wanachanganyikiwa kwa sababu ya mvinyo;

    wanapepesuka wanapoona maono,

    wanajikwaa wanapotoa maamuzi.

    8 Meza zote zimejawa na matapishi

    wala hakuna sehemu hata ndogo

    isiyokuwa na uchafu.

  19. 19 Je, hamjui ya kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe, 20 kwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu.

  20. 11 Ole wao wale waamkao asubuhi na mapema

    wakikimbilia kunywa vileo,

    wale wakawiao sana mpaka usiku,

    mpaka wamewaka kwa mvinyo.

    12 Wana vinubi na zeze kwenye karamu zao,

    matari, filimbi na mvinyo,

    lakini hawayajali matendo ya Bwana,

    wala hawana heshima kwa ajili ya kazi ya mikono yake.

  21. 13 Basi na tuenende kwa adabu kama inavyopasa wakati wa mchana, si kwa kufanya karamu za ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu.

  22. 2 Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha, 3 asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha.

  23. 7 Nenda, kula chakula chako kwa furaha, unywe divai yako kwa moyo wa shangwe, kwa maana sasa Mungu anakubali unachofanya.

  24. 15 Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Bwana, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji chochote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu hata kabla ya kuzaliwa kwake.

  25. 33 Kwa maana Yohana Mbatizaji alikuja, alikuwa hali mkate wala hanywi divai, nanyi mkasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’ 34 Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nanyi mnasema: ‘Tazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’ 35 Nayo hekima huthibitishwa kuwa kweli na watoto wake wote.”

  26. 20 Noa akawa mkulima, akawa mtu wa kwanza kupanda mizabibu. 21 Alipokunywa huo mvinyo wake akalewa na akalala uchi kwenye hema lake. 22 Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake na kuwaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. 23 Lakini Shemu na Yafethi wakachukua nguo wakaitanda mabegani mwao wote wawili, kisha wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao. Nyuso zao zilielekea upande mwingine ili wasiuone uchi wa baba yao.

  27. 17 Wala watu hawaweki divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Kama wakifanya hivyo, viriba vitapasuka nayo divai itamwagika, navyo viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya, na hivyo divai na viriba huwa salama.”

  28. 6 Basi ilikuwepo mitungi sita ya kuhifadhia maji iliyotengenezwa kwa mawe kwa ajili ya kujitakasa kwa desturi ya Kiyahudi; kila mtungi ungeweza kuchukua vipipa viwili au vitatu.

    7 Yesu akawaambia wale watumishi, “Ijazeni hiyo mitungi maji.” Nao wakaijaza ile mitungi mpaka juu.

    8 Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kidogo, mpelekeeni mkuu wa meza.”

    Hivyo wakachota, wakampelekea. 9 Yule mkuu wa meza akayaonja yale maji ambayo yalikuwa yamebadilika kuwa divai. Hakujua divai hiyo ilikotoka ingawa wale watumishi waliochota yale maji wao walifahamu. Basi akamwita bwana arusi kando 10 akamwambia, “Watu wote hutoa kwanza divai nzuri, kisha huleta ile divai hafifu wageni wakisha kunywa vya kutosha, lakini wewe umeiweka ile nzuri kupita zote mpaka sasa.”

    11 Huu, ndio uliokuwa muujiza wa kwanza Yesu aliofanya Kana ya Galilaya. Hivyo Yesu alidhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.

  29. 8 Lakini chakula hakituleti karibu na Mungu, wala hatupotezi chochote tusipokula, wala hatuongezi chochote kama tukila.

    9 Lakini angalieni jinsi mnavyotumia uhuru wenu usije ukawa kikwazo kwao walio dhaifu. 10 Kwa maana kama mtu yeyote mwenye dhamiri dhaifu akiwaona ninyi wenye ujuzi huu mkila katika hekalu la sanamu, je, si atatiwa moyo kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu? 11 Kwa njia hiyo, huyo ndugu mwenye dhamiri dhaifu, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, ataangamia kwa sababu ya ujuzi wenu. 12 Mnapotenda dhambi dhidi ya ndugu zenu kwa njia hii na kujeruhi dhamiri zao zilizo dhaifu, mnamkosea Kristo. 13 Kwa hiyo, kama kile ninachokula kitamfanya ndugu yangu aanguke katika dhambi, sitakula nyama kamwe, nisije nikamfanya ndugu yangu aanguke.

  30. 17 Mtu apendaye anasa atakuwa maskini,

    yeyote apendaye mvinyo na mafuta kamwe hatakuwa tajiri.

  31. 13 “Siku zinakuja,” asema Bwana,

    “wakati mvunaji atatanguliwa na mkulima,

    naye mpanzi atatanguliwa na yeye akamuaye zabibu.

    Divai mpya itadondoka kutoka milimani,

    na kutiririka kutoka vilima vyote.

    14 Nitawarejesha tena watu wangu Israeli waliohamishwa;

    wataijenga tena miji iliyoachwa magofu,

    nao wataishi ndani mwake.

    Watapanda mizabibu na kunywa divai yake;

    watalima bustani na kula matunda yake.

    15 Nitaipanda Israeli katika nchi yao wenyewe,

    hawatangʼolewa tena

    kutoka nchi ambayo nimewapa,”

    asema Bwana Mungu wenu.

  32. 18 Kwa maana Yohana Mbatizaji alikuja, alikuwa hali wala hanywi, nao wanasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’ 19 Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nao wanasema, ‘Tazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’ Lakini hekima huthibitishwa kuwa kweli kwa matendo yake.”

  33. 34 “Jihadharini mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na fadhaa za maisha haya, nayo siku ile ikawakuta ninyi bila kutazamia kama vile mtego unasavyo.

  34. 26 Tumieni hiyo fedha kununua chochote ukitakacho: ngʼombe, kondoo, divai au kinywaji chochote chenye chachu au chochote mnachotaka. Kisha ninyi na wa nyumbani mwenu mtaila mbele za Bwana Mungu wenu na kufurahi.

  35. 11 katika ukahaba,

    divai ya zamani na divai mpya,

    ambavyo huondoa ufahamu

    12 wa watu wangu.

    Hutaka shauri kutoka kwa sanamu ya mti

    nao hujibiwa na fimbo ya mti.

    Roho ya ukahaba imewapotosha,

    hawana uaminifu kwa Mungu wao.

    13 Wanatoa dhabihu juu ya vilele vya milima

    na sadaka za kuteketezwa juu ya vilima,

    chini ya mialoni, milibua na miela,

    ambako kuna vivuli vizuri.

    Kwa hiyo binti zenu wamegeukia ukahaba

    na wake za wana wenu uzinzi.

  36. 48 Lakini kama huyo mtumishi ni mwovu, naye akasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu atakawia muda mrefu,’ 49 kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, na kula na kunywa pamoja na walevi. 50 Basi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. 51 Atamkata vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wanafiki, mahali ambako kutakuwa ni kulia na kusaga meno.

  37. 12 “Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini si vitu vyote vyenye faida. “Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini sitatawaliwa na kitu chochote.

  38. 4 Bali ninyi, ndugu, hampo gizani hata siku ile iwakute ghafula kama mwizi. 5 Ninyi nyote ni wana wa nuru na wana wa mchana. Sisi si wana wa giza wala wa usiku. 6 Kwa hiyo basi, tusilale kama watu wengine walalavyo, bali tukeshe na kuwa na kiasi. 7 Kwa kuwa wote walalao hulala usiku na wale walewao hulewa usiku. 8 Lakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo.

  39. 9 Mheshimu Bwana kwa mali zako na

    kwa malimbuko ya mazao yako yote;

    10 ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika,

    viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya.

  40. 13 Lakini wengine wakawadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa divai!”

  41. 1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.

    3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa.

  42. 11 Lakini sasa nawaandikia kwamba msishirikiane na mtu yeyote anayejiita ndugu, hali akiwa ni mzinzi, au mwenye tamaa mbaya, mwabudu sanamu au msingiziaji, mlevi au mdhalimu. Mtu kama huyo hata msile naye.

  43. 7 Kwa kuwa mwangalizi, kama wakili wa Mungu, imempasa kuwa mtu asiye na lawama, asiwe mwenye majivuno au mwepesi wa hasira, wala mlevi, wala asiwe mtu mwenye tamaa ya mapato yasiyo ya halali. 8 Bali awe mkarimu, anayependa mema, mwenye kiasi, mwenye haki, mwadilifu, mnyofu, mtakatifu na mwenye kuitawala nafsi yake.

  44. 5 Kwa muda wa miaka arobaini niliyowaongoza jangwani, nguo zenu hazikuchakaa, wala viatu miguuni mwenu. 6 Hamkula mkate na hamkunywa divai wala kileo chochote. Nilifanya hivi ili mpate kujua kuwa mimi ndimi Bwana Mungu wenu.

  45. 6 Juu ya mlima huu Bwana Mwenye Nguvu Zote ataandaa

    karamu ya vinono kwa mataifa yote,

    karamu ya mvinyo wa zamani,

    nyama nzuri sana na divai zilizo bora sana.

    7 Juu ya mlima huu ataharibu

    sitara ihifadhiyo mataifa yote,

    kile kifuniko kifunikacho mataifa yote,

    8 yeye atameza mauti milele.

    Bwana Mwenyezi atafuta machozi katika nyuso zote;

    ataondoa aibu ya watu wake duniani kote.

    Bwana amesema hili.

    9 Katika siku ile watasema,

    “Hakika huyu ndiye Mungu wetu;

    tulimtumaini, naye akatuokoa.

    Huyu ndiye Bwana, tuliyemtumaini;

    sisi tushangilie na kufurahia katika wokovu wake.”

  46. 1 “Njooni, ninyi nyote wenye kiu,

    njooni kwenye maji;

    nanyi ambao hamna fedha,

    njooni, nunueni na mle!

    Njooni, nunueni divai na maziwa

    bila fedha na bila gharama.

  47. 14 ‘Yonadabu mwana wa Rekabu aliwaagiza wanawe wasinywe divai, na agizo hilo wamelishika mpaka leo hawanywi divai, kwa sababu wanatii amri ya baba yao. Lakini nimenena nanyi tena na tena, lakini hamkunitii mimi.

  48. 21 Kuhani yeyote asinywe mvinyo aingiapo katika ukumbi wa ndani. 22 Wasioe wanawake wajane wala walioachika, inawapasa kuoa wanawake bikira wenye heshima wa Israeli au wajane wa makuhani. 23 Watawafundisha watu wangu tofauti kati ya vitu vitakatifu na vitu vya kawaida na kuwaonyesha jinsi ya kupambanua kati ya vitu najisi na vitu safi.

  49. 15 “Ole wake yeye awapaye jirani zake kileo,

    akiimimina kutoka kwenye kiriba

    cha mvinyo mpaka wamelewa,

    ili apate kutazama miili yao iliyo uchi.

    16 Utajazwa na aibu badala ya utukufu.

    Sasa ni zamu yako! Kunywa na ujifunue!

    Kikombe kutoka kwenye mkono wa kuume wa Bwana kinakujia,

    na aibu itafunika utukufu wako.

    17 Ukatili ulioifanyia Lebanoni utakufunika,

    na uharibifu uliowafanyia wanyama utakutisha.

    Kwa sababu umemwaga damu ya mtu;

    umeharibu nchi na miji na kila mmoja aliyeko ndani yake.

  50. 27 Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, “Nyweni nyote katika kikombe hiki. 28 Hii ndiyo damu yangu ya Agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. 29 Lakini ninawaambia, tangu sasa sitakunywa tena katika uzao huu wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya pamoja nanyi katika Ufalme wa Baba yangu.”

  51. 8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza.

  52. 9 Malaika wa tatu akawafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Kama mtu yeyote anamwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa chapa yake kwenye kipaji chake cha uso au kwenye mkono wake, 10 yeye pia atakunywa mvinyo wa hasira kali ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake pasipo kuchanganywa na maji. Naye atateswa kwa moto uwakao na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo. 11 Nao moshi wa mateso yao hupanda juu milele na milele. Hakuna mapumziko, mchana wala usiku, kwa wale wamwabuduo huyo mnyama na sanamu yake, au kwa yeyote anayepokea chapa ya jina lake.”

  53. 28 Mungu na akupe umande kutoka mbinguni

    na utajiri wa duniani:

    wingi wa nafaka na divai mpya.

  54. 18 Kama mtu ana mwana mkaidi na mwasi ambaye hamtii baba yake na mama yake, na hasikii wazazi wanapomrudi, 19 baba yake na mama yake watamleta kwa wazee kwenye lango la mji wake. 20 Watawaambia wazee, “Huyu mwanetu ni mkaidi na mwasi. Hatutii sisi, yeye ni mpotovu na mlevi.” 21 Kisha wanaume wote wa mjini mwake watampiga kwa mawe mpaka afe. Ndivyo imewapasa kuondoa maovu kati yenu. Israeli yote itasikia hili na kuogopa.

  55. 8 Katika mwaka wa ishirini na sita wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha akawa mfalme wa Israeli, naye akatawala huko Tirsa kwa miaka miwili.

    9 Zimri, mmoja wa maafisa wake, aliyekuwa na amri juu ya nusu ya magari yake ya vita, akafanya hila mbaya dhidi ya Ela. Wakati huo Ela alikuwa Tirsa, akilewa katika nyumba ya Arsa, mtu aliyekuwa msimamizi wa jumba la kifalme huko Tirsa. 10 Zimri akaingia, akampiga na kumuua katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Kisha Zimri akaingia mahali pake kuwa mfalme.

  56. 9 Hawanywi tena mvinyo pamoja na wimbo,

    kileo ni kichungu kwa wanywaji wake.

  57. 1 Mfalme Belshaza alifanya karamu kubwa kwa ajili ya maelfu ya wakuu wake na akanywa mvinyo pamoja nao. 2 Wakati Belshaza alipokuwa akinywa mvinyo wake, aliamuru viletwe vile vikombe vya dhahabu na fedha ambavyo Nebukadneza baba yake alikuwa amevichukua kutoka hekaluni huko Yerusalemu, ili mfalme na wakuu wake, wake zake na masuria wake waweze kuvinywea. 3 Kwa hiyo wakavileta vile vikombe vya dhahabu ambavyo vilikuwa vimechukuliwa kutoka Hekalu la Mungu huko Yerusalemu, naye mfalme na wakuu wake, wake zake na masuria wake wakavinywea. 4 Walipokuwa wakinywa mvinyo, wakaisifu miungu ya dhahabu na fedha, ya shaba, chuma, miti na mawe.

  58. 3 Sikula chakula kizuri; nyama wala divai havikugusa midomo yangu; nami sikujipaka mafuta kamwe mpaka majuma matatu yalipotimia.

  59. 19 Ingawa mimi ni huru, wala si mtumwa wa mtu yeyote, nimejifanya kuwa mtumwa wa kila mtu, ili niweze kuwavuta wengi kadri iwezekanavyo. 20 Kwa Wayahudi, nilikuwa kama Myahudi, ili niwapate Wayahudi. Kwa watu wale walio chini ya sheria, nilikuwa kama aliye chini ya sheria (ingawa mimi siko chini ya sheria), ili niweze kuwapata wale walio chini ya sheria. 21 Kwa watu wasio na sheria nilikuwa kama asiye na sheria (ingawa siko huru mbali na sheria ya Mungu, bali niko chini ya sheria ya Kristo), ili niweze kuwapata wale wasio na sheria. 22 Kwa walio dhaifu nilikuwa dhaifu, ili niweze kuwapata walio dhaifu. Nimekuwa mtu wa hali zote kwa watu wote ili kwa njia yoyote niweze kuwaokoa baadhi yao. 23 Nafanya haya yote kwa ajili ya Injili, ili nipate kushiriki baraka zake.

  60. 20 Kisha kuhani ataviinua mbele za Bwana kama sadaka ya kuinua; ni vitakatifu na ni mali ya kuhani, pamoja na kile kidari kilichoinuliwa na lile paja lililotolewa. Baada ya hayo, Mnadhiri anaweza kunywa divai.

  61. 13 “Lakini mzabibu ukaijibu, ‘Je, niache kutoa divai yangu inayofurahisha miungu na wanadamu ili nikawe juu ya miti?’

  62. 1 Waisraeli wakafanya maovu tena mbele za Bwana. Hivyo Bwana akawatia mikononi mwa Wafilisti kwa muda wa miaka arobaini.

    2 Basi palikuwa na mtu mmoja wa Sora, aliyeitwa Manoa, wa kabila la Wadani, naye alikuwa na mke ambaye alikuwa tasa na hakuwa na mtoto. 3 Malaika wa Bwana akamtokea huyo mwanamke na kumwambia, “Wewe ni tasa na huna mtoto, lakini utachukua mimba na utamzaa mtoto mwanaume. 4 Lakini ujihadhari sana usinywe mvinyo wala kileo kingine chochote, wala usile kitu chochote kilicho najisi, 5 kwa kuwa utachukua mimba na utamzaa mtoto mwanaume. Wembe usipite kichwani pake, kwa kuwa huyo mwana atakuwa Mnadhiri wa Mungu, aliyewekwa wakfu kwa ajili ya Mungu tangu tumboni mwa mama yake, naye ataanza kuwaokoa Waisraeli kutoka mikononi mwa Wafilisti.”

    6 Ndipo huyo mwanamke akamwendea mumewe na kumweleza kuwa, “Mtu wa Mungu alinijia. Kule kuonekana kwake kulikuwa kama kwa malaika wa Mungu, wa kutisha sana. Sikumuuliza alikotoka wala hakuniambia jina lake. 7 Lakini aliniambia, ‘Utachukua mimba na utazaa mtoto mwanaume. Basi sasa, usinywe mvinyo wala kileo kingine chochote wala usile kitu kilicho najisi, kwa kuwa huyo mtoto atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni mwa mama yake mpaka kufa kwake.’ ”

  63. 14 naye akamwambia, “Utaendelea kulewa mpaka lini? Achilia mbali mvinyo wako.”

    15 Hana akajibu, “Si hivyo bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye huzuni kubwa. Mimi sijanywa mvinyo wala kileo, nilikuwa ninaumimina moyo wangu kwa Bwana.

  64. 13 Kwa ukaribisho wa Daudi, Uria akala na kunywa pamoja naye, Daudi akamlevya. Lakini jioni Uria alitoka kwenda kulala juu ya mkeka wake miongoni mwa watumishi wa bwana wake, hakwenda nyumbani.

  65. 18 “Njooni basi tuhojiane,”

    asema Bwana.

    “Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu,

    zitakuwa nyeupe kama theluji;

    ingawa ni nyekundu sana kama damu,

    zitakuwa nyeupe kama sufu.

  66. 10 Furaha na shangwe zimeondolewa

    kutoka mashamba ya matunda;

    hakuna yeyote aimbaye wala apazaye sauti

    katika mashamba ya mizabibu;

    hakuna yeyote akanyagaye zabibu shinikizoni,

    kwa kuwa nimekomesha makelele.

  67. 12 Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote,

    aliwaita siku ile

    ili kulia na kuomboleza,

    kungʼoa nywele zenu na kuvaa nguo ya gunia.

    13 Lakini tazama, kuna furaha na sherehe,

    kuchinja ngʼombe na kuchinja kondoo,

    kula nyama na kunywa mvinyo!

    Mnasema, “Tuleni na kunywa,

    kwa kuwa kesho tutakufa!”

  68. 1 Ole kwa lile taji la maua, kiburi cha walevi wa Efraimu,

    kwa ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake,

    uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba:

    kwa ule mji, kiburi cha wale walioshushwa na mvinyo!

  69. 8 Bwana ameapa kwa mkono wake wa kuume

    na kwa mkono wake wenye nguvu:

    “Kamwe sitawapa tena adui zenu

    nafaka zenu kama chakula chao;

    kamwe wageni hawatakunywa tena

    divai mpya ambayo mmeitaabikia,

    9 lakini wale waivunao nafaka wataila

    na kumsifu Bwana,

    nao wale wakusanyao zabibu watainywa divai yake

    katika nyua za patakatifu pangu.”

  70. 10 Mwizi huja ili aibe, kuua na kuangamiza. Mimi nimekuja ili wapate uzima kisha wawe nao tele.

  71. 1 Kila mtu na atii mamlaka inayotawala, kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu, nazo mamlaka zilizopo zimewekwa na Mungu. 2 Kwa hiyo yeye anayeasi dhidi ya mamlaka inayotawala anaasi dhidi ya kile kilichowekwa na Mungu, nao wale wafanyao hivyo watajiletea hukumu juu yao wenyewe. 3 Kwa kuwa watawala hawawatishi watu wale wanaotenda mema bali wale wanaotenda mabaya. Je, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Basi tenda lile lililo jema naye atakusifu. 4 Kwa maana mwenye mamlaka ni mtumishi wa Mungu kwa ajili ya mema. Lakini kama ukitenda mabaya, basi ogopa, kwa kuwa hauinui upanga bila sababu. Yeye ni mtumishi wa Mungu, mjumbe wa Mungu wa kutekeleza adhabu juu ya watenda mabaya. 5 Kwa hiyo ni lazima kutii wenye mamlaka, si kwa sababu ya kuogopa adhabu iwezayo kutolewa, bali pia kwa ajili ya dhamiri.