38 Bible Verses About Education

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Education
  1. 7 Kumcha Bwana ndicho chanzo cha maarifa,

    lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu.

    8 Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako,

    wala usiyaache mafundisho ya mama yako.

    9 Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako,

    na mkufu wa kuipamba shingo yako.

  2. 14 Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani, 15 na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. 16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, 17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.

  3. 4 Sikia, ee Israeli: Bwana Mungu wako, Bwana ni mmoja. 5 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. 6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. 7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo. 8 Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako. 9 Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.

  4. 11 Mwanamke na ajifunze kwa utulivu na kwa utiifu wote. 12 Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha au kuwa na mamlaka juu ya mwanaume. Mwanamke inampasa kukaa kimya. 13 Kwa maana Adamu aliumbwa kwanza, kisha Eva. 14 Wala si Adamu aliyedanganywa, bali ni mwanamke aliyedanganywa akawa mkosaji. 15 Lakini mwanamke ataokolewa kwa kuzaa kwake, kama wakiendelea kudumu katika imani, upendo na utakatifu, pamoja na kuwa na kiasi.

  5. 6 Mfundishe mtoto njia impasayo kuiendea,

    naye hataiacha hata akiwa mzee.

  6. 1 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, kwa kuwa hili ni jema. 2 “Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi, 3 “upate baraka na uishi siku nyingi duniani.”

    4 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana.

  7. 12 Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi. 14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.

    15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.

  8. 4 Nionyeshe njia zako, Ee Bwana,

    nifundishe mapito yako,

    5 niongoze katika kweli yako na kunifundisha,

    kwa maana wewe ni Mungu Mwokozi wangu,

    nalo tumaini langu liko kwako wakati wote.

  9. 10 “Kumcha Bwana ndicho chanzo cha hekima,

    na kumjua Aliye Mtakatifu ni ufahamu.

  10. 18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”

  11. 15 Jitahidi kujionyesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtendakazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli.

  12. 25 Wakati huo Yesu alisema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. 26 Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.

    27 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu: Hakuna mtu amjuaye Mwana ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.

    28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

  13. 13 Mkamate sana elimu, usimwache aende zake;

    mshike, maana yeye ni uzima wako.

  14. 9 Mfundishe mtu mwenye hekima

    naye atakuwa na hekima zaidi;

    mfundishe mtu mwadilifu

    naye atazidi kufundishika.

  15. 3 “Mimi ni Myahudi, niliyezaliwa Tarso huko Kilikia, lakini nimelelewa katika mji huu. Miguuni mwa Gamalieli, nilifundishwa kikamilifu katika sheria ya baba zetu, na nikawa mwenye juhudi kwa ajili ya Mungu kama kila mmoja wenu alivyo leo.

  16. 24 Sasa nafurahia kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu, na katika mwili wangu ninatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, ambao ni kanisa. 25 Mimi nimekuwa mtumishi wa kanisa kwa wajibu alionipa Mungu ili kuwaletea ninyi Neno la Mungu kwa ukamilifu: 26 Hii ni siri iliyokuwa imefichika tangu zamani na kwa vizazi vingi, lakini sasa imefunuliwa kwa watakatifu. 27 Kwao, Mungu amechagua kujulisha miongoni mwa watu wa Mataifa utukufu wa utajiri wa siri hii, ambayo ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu.

    28 Yeye ndiye tunayemtangaza, tukimwonya kila mtu na kumfundisha kila mtu kwa hekima yote ili tuweze kumleta kila mmoja akiwa amekamilika katika Kristo. 29 Kwa ajili ya jambo hili, ninajitaabisha, nikijitahidi kwa kadiri ya nguvu zake ambazo hutenda kazi ndani yangu kwa uweza mwingi.

  17. 11 Mambo haya yaagize na kuyafundisha. 12 Mtu yeyote asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe kielelezo kizuri kwa waumini katika usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi. 13 Fanya bidii kusoma Maandiko hadharani, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja. 14 Usiache kutumia kipawa kilicho ndani yako, ambacho ulipewa kwa neno la unabii wakati wazee walikuwekea mikono.

    15 Uwe na bidii katika mambo haya; ujitolee kwa ajili ya mambo haya kikamilifu, ili kila mtu aone kuendelea kwako. 16 Jilinde sana nafsi yako na mafundisho yako. Dumu katika hayo, kwa maana kwa kufanya hivyo, utajiokoa wewe mwenyewe pamoja na wale wanaokusikia.

  18. 3 Ikiwa mtu yeyote atafundisha mafundisho mapotovu wala hakubaliani na mafundisho manyofu ya Bwana wetu Yesu Kristo na yale ya utauwa, 4 huyo amejivuna wala hajui kitu chochote. Yeye amejaa tamaa ya mabishano na ugomvi kuhusu maneno ambavyo matokeo yake ni wivu na mapigano, maneno ya ukorofi, shuku mbaya, 5 na kuzozana kusikokoma kati ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, na ambao hudhani kwamba utauwa ni njia ya kupata faida.

  19. 19 Wafundisheni watoto wenu, yazungumzeni wakati mketipo nyumbani na wakati mtembeapo njiani, wakati mlalapo na wakati mwamkapo. 20 Yaandikeni juu ya miimo ya nyumba zenu na juu ya malango yenu,

  20. 16 Ni bora kiasi gani kupata hekima kuliko dhahabu,

    kuchagua ufahamu kuliko fedha!

  21. 15 Moyo wa mwenye ufahamu hujipatia maarifa,

    masikio ya mwenye hekima huyatafuta maarifa.

  22. 3 Kisha mfalme akamwagiza Ashpenazi, mkuu wa maafisa wa mfalme, kumletea baadhi ya Waisraeli kutoka jamaa ya mfalme na kutoka jamaa kuu, 4 vijana wanaume wasio na dosari mwilini, wenye sura nzuri, wanaoonyesha kipaji katika kila aina ya elimu, wenye ufahamu mzuri, wepesi kuelewa, na waliofuzu kuhudumu katika jumba la kifalme. Alikuwa awafundishe lugha na maandiko ya Wakaldayo. 5 Mfalme akawaagizia kiasi cha chakula na divai ya kila siku kutoka meza ya mfalme. Walikuwa wafundishwe kwa miaka mitatu, na hatimaye waingie kwenye utumishi wa mfalme.

    6 Baadhi ya hawa vijana walitoka Yuda: nao ni Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria. 7 Mkuu wa maafisa akawapa majina mapya: Danieli akamwita Belteshaza, Hanania akamwita Shadraki, Mishaeli akamwita Meshaki, na Azaria akamwita Abednego.

  23. 17 Mungu akawapa hawa vijana wanne maarifa na ufahamu wa kila aina ya maandiko na elimu. Naye Danieli aliweza kufahamu maono na aina zote za ndoto.

  24. 17 “Msidhani kwamba nimekuja kufuta Sheria au Manabii; sikuja kuondoa bali kutimiza. 18 Kwa maana, amin nawaambia, mpaka mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yoyote kutoka kwenye Sheria, mpaka kila kitu kiwe kimetimia. 19 Kwa hiyo, yeyote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, lakini yeyote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika Ufalme wa Mbinguni. 20 Kwa maana nawaambia, haki yenu isipozidi haki ya Mafarisayo na walimu wa sheria, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni.

  25. 26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia.

  26. 9 Mwe waangalifu, na makini ili msije mkasahau mambo ambayo mliyaona kwa macho yenu, wala kuyaacha yaondoke moyoni mwenu siku zote za uhai wenu. Mwafundishe hayo watoto wenu na watoto wao baada yao.

    10 Kumbuka siku uliyosimama mbele za Bwana Mungu wako kule Horebu, wakati aliponiambia, “Wakutanishe watu mbele yangu wasikie maneno yangu ili kwamba waweze kujifunza kuniheshimu kwa muda wote watakaoishi katika nchi, nao waweze kuwafundisha watoto wao maneno hayo.”

  27. 8 Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea;

    nitakushauri na kukuangalia.

  28. 66 Nifundishe maarifa na uamuzi mzuri,

    kwa kuwa ninaamini amri zako.

  29. 6 Kwa maana Bwana hutoa hekima,

    na kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.

  30. 1 Sikilizeni wanangu, mafundisho ya baba yenu;

    sikilizeni kwa makini na mpate ufahamu.

    2 Ninawapa mafundisho ya maana,

    kwa hiyo msiyaache mafundisho yangu.

    3 Nilipokuwa mvulana mdogo katika nyumba ya baba yangu,

    ningali mchanga na mtoto pekee kwa mama yangu,

    4 baba alinifundisha akisema,

    “Yashike maneno yangu yote kwa moyo wako wote;

    yashike maagizo yangu na wewe utaishi.

    5 Pata hekima, pata ufahamu;

    usiyasahau maneno yangu wala usiyaache.

    6 Usimwache hekima naye atakuweka salama;

    mpende, naye atakulinda.

    7 Hekima ni bora kuliko vitu vyote; kwa hiyo jipe hekima.

    Hata ikikugharimu vyote ulivyo navyo, pata ufahamu.

  31. 12 Hekima ni ulinzi kama fedha ilivyo ulinzi,

    lakini faida ya maarifa ni hii:

    kwamba hekima huhifadhi maisha ya aliye nayo.

  32. 9 Mhubiri hakuwa tu na hekima, bali aliwagawia watu maarifa pia. Alitafakari na kutafiti na akaweka katika utaratibu mithali nyingi. 10 Mhubiri alitafiti ili kupata maneno sahihi na kila alichoandika kilikuwa sawa na kweli.

    11 Maneno ya wenye hekima ni kama mchokoro, mithali zao zilizokusanywa pamoja ni kama misumari iliyogongomewa ikawa imara, yaliyotolewa na Mchungaji mmoja. 12 Tena zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo, hakuna mwisho wa kutunga vitabu vingi, nako kusoma sana huuchosha mwili.

    13 Hii ndiyo jumla ya maneno;

    yote yamekwisha sikiwa:

    Mche Mungu, nawe uzishike amri zake,

    maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.

    14 Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi,

    pamoja na kila neno la siri,

    likiwa jema au baya.

  33. 22 Mose akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa mtu hodari kwa maneno na matendo.

  34. 1 Sisi tulio na nguvu, hatuna budi kuchukuliana na kushindwa kwa wale walio dhaifu wala si kujipendeza nafsi zetu wenyewe. 2 Kila mmoja wetu inampasa kumpendeza jirani yake kwa mambo mema, ili kumjenga katika imani. 3 Kwa maana hata Kristo hakujipendeza mwenyewe, bali kama ilivyoandikwa: “Matukano yao wale wanaokutukana wewe yalinipata mimi.” 4 Kwa maana kila kitu kilichoandikwa zamani, kiliandikwa kutufundisha, ili kwamba kwa saburi na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini.

    5 Mungu atoaye saburi na faraja, awajalie ninyi roho ya umoja miongoni mwenu mnapomfuata Kristo Yesu, 6 ili kwa moyo mmoja mpate kumtukuza Mungu aliye Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.

  35. 8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo. 9 Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.

  36. 3 Kama nilivyokusihi wakati nilipokwenda Makedonia, endelea kubaki Efeso, ili kwamba upate kuwaagiza watu wasiendelee kufundisha mafundisho ya uongo 4 wala wasitoe muda wao kwa hadithi za kubuniwa na orodha za majina ya vizazi visivyo na mwisho, ambazo huchochea mabishano badala ya mpango wa Mungu utokanao na imani. 5 Kusudi la maagizo haya ni upendo utokao katika moyo safi, dhamiri njema na imani ya kweli. 6 Watu wengine wamepotoka kutoka haya na kugeukia majadiliano yasiyo na maana kwa kuwa, 7 wanataka kuwa walimu wa sheria, lakini hawajui mambo yale wanayosema wala hayo wanayoyatumainia kwa uthabiti.

  37. 2 Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha,

  38. 2 Nayo mambo yale uliyonisikia nikiyasema mbele ya mashahidi wengi, uwakabidhi watu waaminifu watakaoweza kuwafundisha watu wengine vilevile.