42 Bible Verses About Learning
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
14 Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani, 15 na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. 16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, 17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.
-
1 Sikilizeni wanangu, mafundisho ya baba yenu;
sikilizeni kwa makini na mpate ufahamu.
2 Ninawapa mafundisho ya maana,
kwa hiyo msiyaache mafundisho yangu.
3 Nilipokuwa mvulana mdogo katika nyumba ya baba yangu,
ningali mchanga na mtoto pekee kwa mama yangu,
4 baba alinifundisha akisema,
“Yashike maneno yangu yote kwa moyo wako wote;
yashike maagizo yangu na wewe utaishi.
5 Pata hekima, pata ufahamu;
usiyasahau maneno yangu wala usiyaache.
6 Usimwache hekima naye atakuweka salama;
mpende, naye atakulinda.
7 Hekima ni bora kuliko vitu vyote; kwa hiyo jipe hekima.
Hata ikikugharimu vyote ulivyo navyo, pata ufahamu.
-
25 Wakati huo Yesu alisema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. 26 Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.
27 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu: Hakuna mtu amjuaye Mwana ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.
28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”
-
22 Basi kuweni watendaji wa Neno wala msiwe wasikiaji tu, huku mkijidanganya nafsi zenu. 23 Kwa maana kama mtu ni msikiaji tu wa Neno wala hatendi kile linachosema, yeye ni kama mtu ajitazamaye uso wake kwenye kioo 24 na baada ya kujiona alivyo, huenda zake na mara husahau jinsi alivyo. 25 Lakini yeye anayeangalia kwa bidii katika sheria kamilifu, ile iletayo uhuru, naye akaendelea kufanya hivyo bila kusahau alichosikia, bali akalitenda, atabarikiwa katika kile anachofanya.
26 Kama mtu akidhani ya kuwa anayo dini lakini hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hujidanganya moyoni mwake, wala dini yake mtu huyo haifai kitu. 27 Dini iliyo safi, isiyo na uchafu, inayokubalika mbele za Mungu Baba yetu, ndiyo hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda usitiwe madoa na dunia.
-
4 Sikia, ee Israeli: Bwana Mungu wako, Bwana ni mmoja. 5 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. 6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. 7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo. 8 Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako. 9 Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.
-
1 Mithali za Solomoni mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli:
2 Kwa kupata hekima na nidhamu;
kwa kufahamu maneno ya busara;
3 kwa kujipatia nidhamu na busara,
kufanya lililo sawa, haki na bila kupendelea;
4 huwapa busara wajinga,
maarifa na akili kwa vijana;
5 wenye hekima na wasikilize nao waongeze elimu yao,
wenye kupambanua na wapate mwongozo;
6 kwa kufahamu mithali na mifano,
misemo na vitendawili vya wenye hekima.
-
9 Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.
-
7 Kumcha Bwana ndicho chanzo cha maarifa,
lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu.
-
1 Mwanangu, kama utayakubali maneno yangu
na kuyaweka akiba maagizo yangu ndani mwako,
2 kutega sikio lako kwenye hekima
na kuweka moyo wako katika ufahamu,
3 na kama ukiita busara
na kuita kwa sauti ufahamu,
4 na kama utaitafuta kama fedha
na kuitafuta sana kama hazina iliyofichwa,
5 ndipo utakapoelewa kumcha Bwana
na kupata maarifa ya Mungu.
6 Kwa maana Bwana hutoa hekima,
na kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.
7 Anahifadhi ushindi kwa ajili ya mwadilifu,
yeye ni ngao kwa wale wasio na lawama,
8 kwa kuwa hulinda mwenendo wa mwenye haki
na kuhifadhi njia ya waaminifu wake.
-
6 Mfundishe mtoto njia impasayo kuiendea,
naye hataiacha hata akiwa mzee.
-
19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”
-
10 Nina furaha kubwa katika Bwana kwamba hatimaye mmeanza upya kushughulika tena na maisha yangu. Kweli mmekuwa mkinifikiria lakini mlikuwa hamjapata nafasi ya kufanya hivyo. 11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
-
9 Kwa hiyo Mose akaandika sheria hii na kuwapa makuhani, wana wa Lawi, waliochukua Sanduku la Agano la Bwana na wazee wote wa Israeli. 10 Kisha Mose akawaamuru, akasema: “Mwishoni mwa kila miaka saba, katika mwaka wa kufuta madeni, wakati wa Sikukuu ya Vibanda, 11 Waisraeli wote wanapokuja mbele za Bwana Mungu wenu mahali atakapopachagua, utasoma sheria hii mbele yao masikioni mwao. 12 Kusanya watu wote, wanaume, wanawake, watoto na wageni wanaoishi katika miji yenu, ili waweze kusikia na kujifunza kumcha Bwana Mungu wenu na kufuata kwa bidii maneno yote ya sheria hii. 13 Watoto wao, ambao hawaijui sheria hii, lazima waisikie na kujifunza kumcha Bwana Mungu wenu kwa muda mtakaoishi katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”
-
4 Nionyeshe njia zako, Ee Bwana,
nifundishe mapito yako,
5 niongoze katika kweli yako na kunifundisha,
kwa maana wewe ni Mungu Mwokozi wangu,
nalo tumaini langu liko kwako wakati wote.
-
71 Ilikuwa vyema mimi kupata shida
ili nipate kujifunza maagizo yako.
72 Sheria inayotoka kinywani mwako ina thamani kubwa kwangu
kuliko maelfu ya vipande vya fedha na dhahabu.
73 Mikono yako ilinifanya na kuniumba,
nipe ufahamu niweze kujifunza amri zako.
-
15 Jitahidi kujionyesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtendakazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli.
-
19 Kwa maana nimemchagua yeye, ili awaongoze watoto wake na jamaa yake kufuata njia ya Bwana, kwa kuwa waadilifu na kutenda haki, ili Bwana atimize ahadi yake kwa Abrahamu.”
-
9 Mfundishe mtu mwenye hekima
naye atakuwa na hekima zaidi;
mfundishe mtu mwadilifu
naye atazidi kufundishika.
-
27 Mtu mwenye maarifa hutumia maneno kwa kujizuia,
naye mtu mwenye ufahamu ana moyo wa utulivu.
28 Hata mtu mpumbavu hudhaniwa kuwa na hekima kama akinyamaza,
na mwenye ufahamu kama akiuzuia ulimi wake.
-
15 Moyo wa mwenye ufahamu hujipatia maarifa,
masikio ya mwenye hekima huyatafuta maarifa.
-
16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu.
-
42 Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali. 43 Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume. 44 Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika. 45 Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake. 46 Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe, 47 wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa wale waliokuwa wakiokolewa.
-
1 Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake, kwamba: 2 Hubiri Neno; kuwa tayari wakati ufaao na wakati usiofaa; karipia, kemea na utie moyo kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri. 3 Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima. Badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe, watajikusanyia idadi kubwa ya walimu wapate kuwaambia yale ambayo masikio yao yanayowasha yanatamani kuyasikia.
-
18 Yawekeni haya maneno yangu katika mioyo yenu na akili zenu, yafungeni kama alama juu ya mikono yenu na kwenye paji za nyuso zenu. 19 Wafundisheni watoto wenu, yazungumzeni wakati mketipo nyumbani na wakati mtembeapo njiani, wakati mlalapo na wakati mwamkapo. 20 Yaandikeni juu ya miimo ya nyumba zenu na juu ya malango yenu, 21 ili kwamba siku zenu na siku za watoto wenu zipate kuwa nyingi katika nchi ile Bwana aliyoapa kuwapa baba zenu, kama zilivyo nyingi siku za mbingu juu ya nchi.
-
8 Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako,
wala usiyaache mafundisho ya mama yako.
9 Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako,
na mkufu wa kuipamba shingo yako.
-
42 Kila siku, Hekaluni na nyumba kwa nyumba, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema kwamba Yesu ndiye Kristo.
-
11 Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, 12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa 13 mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo.
14 Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. 15 Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo.
-
1 Wale wote walio chini ya kongwa la utumwa inawapasa kuwahesabu mabwana zao kuwa wanastahili heshima yote, ili jina la Mungu lisitukanwe wala mafundisho yetu. 2 Wale watumwa ambao wana mabwana waaminio, haiwapasi kupunguza heshima yao kwa sababu wao ni ndugu. Badala yake, wawatumikie hata vizuri zaidi, kwa sababu wale wanaonufaika na huduma yao ni waaminio, ambao ni wapenzi wao. Fundisha mambo haya na uwahimize kuyafuata.
3 Ikiwa mtu yeyote atafundisha mafundisho mapotovu wala hakubaliani na mafundisho manyofu ya Bwana wetu Yesu Kristo na yale ya utauwa, 4 huyo amejivuna wala hajui kitu chochote. Yeye amejaa tamaa ya mabishano na ugomvi kuhusu maneno ambavyo matokeo yake ni wivu na mapigano, maneno ya ukorofi, shuku mbaya, 5 na kuzozana kusikokoma kati ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, na ambao hudhani kwamba utauwa ni njia ya kupata faida.
-
14 Watu wetu hawana budi kujifunza kutenda mema, ili waweze kuyakimu mahitaji ya kila siku, wasije wakaishi maisha yasiyokuwa na matunda.
-
5 Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa. 6 Lakini anapoomba, lazima aamini wala asiwe na shaka, kwa sababu mtu aliye na shaka ni kama wimbi la bahari, lililochukuliwa na upepo na kutupwa huku na huku. 7 Mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapata kitu chochote kutoka kwa Bwana.
-
24 “Shikeni maagizo haya yawe kanuni ya kudumu kwenu na kwa ajili ya wazao wenu. 25 Mtakapoingia katika nchi Bwana atakayowapa kama alivyoahidi, shikeni desturi hii. 26 Watoto wenu watakapowauliza, ‘Sikukuu hii ina maana gani kwenu?’ 27 Basi waambieni, ‘Hii ni dhabihu ya Pasaka kwa Bwana, ambaye alipita juu ya nyumba za Waisraeli katika nchi ya Misri na hakudhuru nyumba zetu alipowapiga Wamisri.’ ” Ndipo watu wa Israeli waliposujudu na kuabudu.
-
9 Mwe waangalifu, na makini ili msije mkasahau mambo ambayo mliyaona kwa macho yenu, wala kuyaacha yaondoke moyoni mwenu siku zote za uhai wenu. Mwafundishe hayo watoto wenu na watoto wao baada yao.
10 Kumbuka siku uliyosimama mbele za Bwana Mungu wako kule Horebu, wakati aliponiambia, “Wakutanishe watu mbele yangu wasikie maneno yangu ili kwamba waweze kujifunza kuniheshimu kwa muda wote watakaoishi katika nchi, nao waweze kuwafundisha watoto wao maneno hayo.”
-
1 Mose akawaita Israeli wote, akawaambia:
Ee Israeli, sikilizeni amri na sheria ninazowatangazia leo. Jifunzeni, na mwe na hakika kuzifuata.
-
6 “Uwe hodari na shujaa, kwa sababu wewe ndiwe utakayewaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa. 7 Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. 8 Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi.
-
4 Hatutayaficha kwa watoto wao;
tutakiambia kizazi kijacho
matendo yastahiliyo sifa ya Bwana,
uweza wake, na maajabu aliyoyafanya.
5 Aliagiza amri kwa Yakobo
na akaweka sheria katika Israeli,
ambazo aliwaamuru baba zetu
wawafundishe watoto wao,
6 ili kizazi kijacho kizijue,
pamoja na watoto ambao watazaliwa,
nao pia wapate kuwaeleza watoto wao.
7 Ndipo wangeweka tumaini lao kwa Mungu,
nao wasingesahau matendo yake,
bali wangalizishika amri zake.
8 Ili wasifanane na baba zao,
waliokuwa kizazi cha ukaidi na uasi,
ambao roho zao hazikuwa na uaminifu kwake,
ambao roho zao hazikumwamini.
-
11 Mwanangu, usiidharau adhabu ya Bwana
na usichukie kukaripiwa naye,
12 kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao,
kama vile baba afanyavyo
kwa mwana apendezwaye naye.
-
20 Mwanangu, zishike amri za baba yako,
wala usiyaache mafundisho ya mama yako.
21 Yafunge katika moyo wako daima,
yakaze kuizunguka shingo yako.
22 Wakati utembeapo, yatakuongoza;
wakati ulalapo, yatakulinda;
wakati uamkapo, yatazungumza nawe.
23 Kwa maana amri hizi ni taa,
mafundisho haya ni mwanga
na maonyo ya maadili ni njia ya uzima,
-
10 “Kumcha Bwana ndicho chanzo cha hekima,
na kumjua Aliye Mtakatifu ni ufahamu.
-
11 Maneno ya wenye hekima ni kama mchokoro, mithali zao zilizokusanywa pamoja ni kama misumari iliyogongomewa ikawa imara, yaliyotolewa na Mchungaji mmoja. 12 Tena zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo, hakuna mwisho wa kutunga vitabu vingi, nako kusoma sana huuchosha mwili.
13 Hii ndiyo jumla ya maneno;
yote yamekwisha sikiwa:
Mche Mungu, nawe uzishike amri zake,
maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.
14 Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi,
pamoja na kila neno la siri,
likiwa jema au baya.
-
15 Wayahudi wakastaajabia mafundisho yake wakasema, “Mtu huyu amepataje kujua mambo haya bila kufundishwa?”
-
1 Sisi tulio na nguvu, hatuna budi kuchukuliana na kushindwa kwa wale walio dhaifu wala si kujipendeza nafsi zetu wenyewe. 2 Kila mmoja wetu inampasa kumpendeza jirani yake kwa mambo mema, ili kumjenga katika imani. 3 Kwa maana hata Kristo hakujipendeza mwenyewe, bali kama ilivyoandikwa: “Matukano yao wale wanaokutukana wewe yalinipata mimi.” 4 Kwa maana kila kitu kilichoandikwa zamani, kiliandikwa kutufundisha, ili kwamba kwa saburi na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini.
5 Mungu atoaye saburi na faraja, awajalie ninyi roho ya umoja miongoni mwenu mnapomfuata Kristo Yesu,
-
16 Bila shaka yoyote, siri ya utauwa ni kubwa:
Alidhihirishwa katika mwili wa kibinadamu,
akathibitishwa kuwa na haki katika Roho,
akaonekana na malaika,
akahubiriwa miongoni mwa mataifa,
akaaminiwa ulimwenguni,
akachukuliwa juu katika utukufu.
Shows Read in context, Share and Copy.