50 Bible Verses About Service

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Service
  1. 4 Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja, 5 vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. 6 Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani. 7 Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe, 8 kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha.

    9 Upendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema. 10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine. 11 Msiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana. 12 Kuweni na furaha katika tumaini, katika dhiki kuweni na saburi, dumuni katika maombi. 13 Changieni katika mahitaji ya watakatifu, wakaribisheni wageni.

  2. 9 Kuweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manungʼuniko. 10 Kila mmoja na atumie kipawa chochote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu. 11 Yeyote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Yeyote ahudumuye hana budi kuhudumu kwa nguvu zile anazopewa na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kwa njia ya Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye milele na milele. Amen.

  3. 13 Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo. 14 Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” 15 Kama mkiumana na kutafunana, angalieni, msije mkaangamizana.

  4. 1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, 2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. 3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.

    5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:

    6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,

    hakuona kule kuwa sawa na Mungu

    kuwa kitu cha kushikilia,

    7 bali alijifanya si kitu,

    akachukua hali hasa na mtumwa,

    naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.

    8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,

    alijinyenyekeza, akatii hata mauti:

    naam, mauti ya msalaba!

    9 Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana,

    na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina,

    10 ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe,

    la vitu vya mbinguni, na vya duniani,

    na vya chini ya nchi,

    11 na kila ulimi ukiri ya kwamba

    Yesu Kristo ni Bwana,

    kwa utukufu wa Mungu Baba.

  5. 34 “Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njooni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu; urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 35 Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, 36 nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’

    37 “Ndipo wale wenye haki watakapomjibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha? 38 Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha, au ukiwa uchi tukakuvika? 39 Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza, au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’

    40 “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’

  6. 23 Lolote mfanyalo, fanyeni kwa moyo kama watu wanaomtumikia Bwana, na si wanadamu, 24 kwa kuwa mnajua kwamba mtapokea urithi wenu kutoka kwa Bwana ukiwa thawabu yenu. Ni Bwana Yesu Kristo mnayemtumikia.

  7. 25 Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, nao wenye vyeo huonyesha mamlaka yao. 26 Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, 27 naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu hana budi kuwa mtumwa wenu: 28 kama vile ambavyo Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”

  8. 12 Alipomaliza kuwanawisha miguu yao, alivaa tena mavazi yake, akarudi alikokuwa ameketi, akawauliza, “Je, mmeelewa nililowafanyia? 13 Ninyi mnaniita mimi ‘Mwalimu’ na ‘Bwana,’ hii ni sawa, maana ndivyo nilivyo. 14 Kwa hiyo, ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewanawisha ninyi miguu, pia hamna budi kunawishana miguu ninyi kwa ninyi. 15 Mimi nimewawekea kielelezo kwamba imewapasa kutenda kama vile nilivyowatendea ninyi. 16 Amin, amin nawaambia, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala aliyetumwa si mkuu kuliko yule aliyemtuma. 17 Sasa kwa kuwa mmejua mambo haya, heri yenu ninyi kama mkiyatenda.

  9. 1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.

  10. 9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. 10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.

  11. 5 Ninyi watumwa, watiini hao walio mabwana zenu hapa duniani kwa heshima na kwa kutetemeka na kwa moyo mmoja, kama vile mnavyomtii Kristo. 6 Watiini, si tu wakati wakiwaona ili mpate upendeleo wao, bali mtumike kama watumwa wa Kristo, mkifanya mapenzi ya Mungu kwa moyo. 7 Tumikeni kwa moyo wote, kama vile mnamtumikia Bwana na si wanadamu. 8 Mkijua kwamba Bwana atampa kila mtu thawabu kwa lolote jema alilotenda, kama yeye ni mtumwa au ni mtu huru.

    9 Nanyi mabwana, watendeeni watumwa wenu kwa jinsi iyo hiyo. Msiwatishe, kwa kuwa mnajua ya kwamba yeye aliye Bwana wenu na Bwana wao yuko mbinguni, naye hana upendeleo.

  12. 34 Lakini hawakumjibu, kwa sababu njiani walikuwa wakibishana kuhusu nani miongoni mwao alikuwa mkuu zaidi ya wote.

    35 Akaketi chini, akawaita wote kumi na wawili, akawaambia: “Kama mtu yeyote akitaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa wa mwisho na mtumishi wa wote.”

  13. 11 Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, 12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa 13 mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo.

    14 Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. 15 Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo. 16 Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.

  14. 10 Mungu si mdhalimu: yeye hataisahau kazi yenu na upendo ule mlioonyesha kwa ajili yake katika kuwahudumia watakatifu na hata sasa mnaendelea kuwahudumia. 11 Nasi twataka kila mmoja wenu aonyeshe bidii iyo hiyo ili mpate kujua uhakika kamili wa lile tumaini mpaka mwisho, 12 ili msije mkawa wavivu, bali mpate kuwaiga wale ambao kwa imani na saburi hurithi zile ahadi.

  15. 58 Kwa hiyo, ndugu zangu wapenzi, simameni imara, msitikisike, mzidi sana katika kuitenda kazi ya Bwana, kwa maana mnajua ya kuwa, kazi yenu katika Bwana si bure.

  16. 2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo.

  17. 38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”

  18. 25 Mtu yeyote anayependa maisha yake atayapoteza, naye ayachukiaye maisha yake katika ulimwengu huu atayaokoa hata kwa uzima wa milele. 26 Mtu yeyote akinitumikia lazima anifuate, nami mahali nilipo ndipo mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu akinitumikia, Baba yangu atamheshimu.

  19. 17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo? 18 Watoto wapendwa, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli.

  20. 11 Mtumikieni Bwana kwa hofu

    na mshangilie kwa kutetemeka.

    12 Mbusu Mwana, asije akakasirika

    nawe ukaangamizwa katika njia yako,

    kwa maana hasira yake inaweza kuwaka ghafula.

    Heri wote wanaomkimbilia.

  21. 12 Huduma hii mnayofanya si tu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watakatifu, bali huzidi sana kwa shukrani nyingi apewazo Mungu. 13 Kwa sababu ya huduma ambayo mmejithibitisha wenyewe, watu watamtukuza Mungu kwa ajili ya utiifu ufuatanao na ukiri wenu wa Injili ya Kristo, na kwa ukarimu wenu wa kushiriki pamoja nao na pia wengine wote.

  22. 14 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. 15 Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani ya ile nyumba. 16 Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

  23. 24 “Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.

  24. 15 Lakini msipoona vyema kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia, kama ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ngʼambo Frati, au miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Bwana.”

  25. 24 Lakini hakikisheni mnamcha Bwana na kumtumikia kwa uaminifu kwa moyo wenu wote; tafakarini mambo makubwa aliyoyatenda kwa ajili yenu.

  26. 11 Yeye aliye mkuu kuliko ninyi nyote miongoni mwenu atakuwa mtumishi wenu.

  27. 30 Yesu akamjibu akasema, “Mtu mmoja alikuwa akiteremka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, naye akaangukia mikononi mwa wanyangʼanyi. Wakampiga, wakaondoka, wakamwacha akiwa karibu kufa. 31 Kuhani mmoja alikuwa akipitia njia ile, alipomwona huyo mtu, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani. 32 Vivyo hivyo, Mlawi mmoja naye alipofika mahali pale, alimwona, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani 33 Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa akisafiri alipomwona, alimhurumia. 34 Akaenda alipokuwa na akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake, akampeleka mpaka kwenye nyumba ya wageni na kumtunza. 35 Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbili akampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yoyote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’

    36 “Ni yupi basi miongoni mwa hawa watatu wewe unadhani ni jirani yake yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyangʼanyi?”

    37 Yule mtaalamu wa sheria akajibu, “Ni yule aliyemhurumia.”

    Ndipo Yesu akamwambia, “Nenda, ukafanye vivyo hivyo.”

  28. 25 Yesu akawaambia, “Wafalme na watu wa Mataifa huwatawala watu kwa nguvu. Nao wenye mamlaka juu yao hujiita ‘Wafadhili.’ 26 Lakini ninyi msifanane nao. Bali yeye aliye mkuu kuliko wote miongoni mwenu, inampasa kuwa kama yeye aliye mdogo wa wote, naye atawalaye na awe kama yeye ahudumuye. 27 Kwani ni nani aliye mkuu? Ni yule aketiye mezani au ni yule ahudumuye? Si ni yule aliyekaa mezani? Lakini mimi niko miongoni mwenu kama yule ahudumuye.

  29. 35 Katika kila jambo nimewaonyesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii imetupasa kuwasaidia wadhaifu, mkikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe jinsi alivyosema, ‘Ni heri kutoa kuliko kupokea.’ ”

  30. 4 Vivyo hivyo, ndugu zangu, ninyi mmeifia sheria kwa njia ya mwili wa Kristo, ili mweze kuwa mali ya mwingine, yeye ambaye alifufuliwa kutoka kwa wafu, ili tupate kuzaa matunda kwa Mungu. 5 Kwa maana tulipokuwa tunatawaliwa na asili ya dhambi, tamaa za dhambi zilizochochewa na sheria zilikuwa zikitenda kazi katika miili yetu, hivyo tulizaa matunda ya mauti. 6 Lakini sasa, kwa kufia kile kilichokuwa kimetufunga kwanza, tumewekwa huru kutokana na sheria ili tutumike katika njia mpya ya Roho, wala si katika njia ya zamani ya sheria iliyoandikwa.

  31. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

  32. 12 Namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu, kwa sababu aliniona mwaminifu, akaniteua kwa kazi yake. 13 Ingawa wakati fulani nilikuwa mwenye kukufuru, mtesaji na mwenye jeuri, lakini nilipata rehema kwa sababu nilitenda hivyo kwa kutojua na kutoamini kwangu. 14 Neema ya Bwana wetu ilimiminwa juu yangu kwa wingi, ikiambatana na imani na upendo ulio katika Kristo Yesu.

  33. 2 Mwabuduni Bwana kwa furaha;

    njooni mbele zake kwa nyimbo za shangwe.

  34. 18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”

  35. 2 Watawatenga na masinagogi. Naam, saa yaja ambayo mtu yeyote atakayewaua atadhani kwa kufanya hivyo anamtumikia Mungu.

  36. 28 Yeye ambaye amekuwa akiiba, asiibe tena, lakini lazima ajishughulishe, afanye kitu kifaacho kwa mikono yake mwenyewe, ili awe na kitu cha kuwagawia wahitaji.

  37. 17 Lakini hata kama nikimiminwa kama sadaka ya kinywaji kwenye dhabihu na huduma itokayo katika imani yenu, mimi ninafurahi na kushangilia pamoja nanyi nyote.

  38. 13 Damu ya mbuzi na ya mafahali, na majivu ya mitamba walivyonyunyiziwa wale waliokuwa najisi kwa taratibu za kiibada viliwatakasa, hata kuwaondolea uchafu wa nje. 14 Basi ni zaidi aje damu ya Kristo, ambaye kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na waa, itatusafisha dhamiri zetu kutokana na matendo yaletayo mauti, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai!

  39. 22 Basi kuweni watendaji wa Neno wala msiwe wasikiaji tu, huku mkijidanganya nafsi zenu. 23 Kwa maana kama mtu ni msikiaji tu wa Neno wala hatendi kile linachosema, yeye ni kama mtu ajitazamaye uso wake kwenye kioo 24 na baada ya kujiona alivyo, huenda zake na mara husahau jinsi alivyo. 25 Lakini yeye anayeangalia kwa bidii katika sheria kamilifu, ile iletayo uhuru, naye akaendelea kufanya hivyo bila kusahau alichosikia, bali akalitenda, atabarikiwa katika kile anachofanya.

    26 Kama mtu akidhani ya kuwa anayo dini lakini hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hujidanganya moyoni mwake, wala dini yake mtu huyo haifai kitu. 27 Dini iliyo safi, isiyo na uchafu, inayokubalika mbele za Mungu Baba yetu, ndiyo hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda usitiwe madoa na dunia.

  40. 25 Mtakapoingia katika nchi Bwana atakayowapa kama alivyoahidi, shikeni desturi hii. 26 Watoto wenu watakapowauliza, ‘Sikukuu hii ina maana gani kwenu?’ 27 Basi waambieni, ‘Hii ni dhabihu ya Pasaka kwa Bwana, ambaye alipita juu ya nyumba za Waisraeli katika nchi ya Misri na hakudhuru nyumba zetu alipowapiga Wamisri.’ ” Ndipo watu wa Israeli waliposujudu na kuabudu.

  41. 5 Lakini mwe waangalifu sana kushika amri na sheria zile Mose mtumishi wa Bwana alizowapa: yaani kumpenda Bwana Mungu wenu na kuenenda katika njia zake zote, kutii amri zake, kushikamana naye kwa uthabiti na kumtumikia kwa moyo wenu wote na roho yenu yote.”

  42. 17 Yeye amhurumiaye maskini humkopesha Bwana,

    naye atamtuza kwa aliyotenda.

  43. 42 Kama yeyote akimpa hata kikombe cha maji baridi mmoja wa hawa wadogo kwa kuwa ni mwanafunzi wangu, amin, nawaambia, hataikosa thawabu yake.”

  44. 35 Mmoja wao, mtaalamu wa sheria, akamuuliza swali ili kumjaribu, akisema, 36 “Mwalimu, ni amri ipi katika Sheria iliyo kuu kuliko zote?”

    37 Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’ 38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. 39 Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ 40 Amri hizi mbili ndizo msingi wa Sheria na Manabii.”

  45. 12 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi. 13 Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. 14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru.

  46. 18 Walipofika akawaambia, “Ninyi wenyewe mnajua jinsi nilivyoishi katikati yenu muda wote tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia. 19 Nilimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote na kwa machozi nikivumilia taabu na mapingamizi yaliyonipata kutokana na hila za Wayahudi. 20 Mnajua kwamba sikusita kuhubiri jambo lolote ambalo lingekuwa la kuwafaa ninyi, lakini nilifundisha hadharani na nyumba kwa nyumba. 21 Nimewashuhudia Wayahudi na Wayunani kwamba inawapasa kumgeukia Mungu kwa kutubu dhambi na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo.

  47. 4 Kuna aina mbalimbali za karama, lakini Roho ni yule yule. 5 Kuna huduma za aina mbalimbali, lakini Bwana ni yule yule. 6 Kisha kuna tofauti za kutenda kazi, lakini ni Mungu yule yule atendaye kazi zote kwa watu wote.

    7 Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote. 8 Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo. 9 Mtu mwingine imani kwa huyo Roho na mwingine karama za kuponya kwa huyo Roho mmoja. 10 Kwa mwingine matendo ya miujiza, kwa mwingine unabii kwa mwingine kupambanua roho, kwa mwingine aina mbalimbali za lugha, na kwa mwingine bado, tafsiri za lugha. 11 Haya yote hufanywa na huyo huyo Roho mmoja, Roho naye humgawia kila mtu, kama apendavyo.

  48. 15 Basi kwa njia ya Yesu, tuzidi kumtolea Mungu dhabihu ya sifa, yaani matunda ya midomo inayolikiri Jina lake. 16 Na msiache kutenda mema na kushirikiana vile vitu mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu.

  49. 15 Kwa maana ni mapenzi ya Mungu kwamba kwa kutenda mema mnyamazishe maneno ya kijinga ya watu wapumbavu. 16 Ishini kama watu huru, lakini msitumie uhuru wenu kama kisingizio cha kutenda uovu, bali ishini kama watumishi wa Mungu.

  50. 19 Nayajua matendo yako, upendo wako na imani yako, huduma na saburi yako na kwamba matendo yako ya sasa yamezidi yale ya kwanza.