108 Bible Verses About Being Humble

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Being Humble
  1. 1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, 2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. 3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.

    5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:

    6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,

    hakuona kule kuwa sawa na Mungu

    kuwa kitu cha kushikilia,

    7 bali alijifanya si kitu,

    akachukua hali hasa na mtumwa,

    naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.

    8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,

    alijinyenyekeza, akatii hata mauti:

    naam, mauti ya msalaba!

    9 Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana,

    na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina,

    10 ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe,

    la vitu vya mbinguni, na vya duniani,

    na vya chini ya nchi,

    11 na kila ulimi ukiri ya kwamba

    Yesu Kristo ni Bwana,

    kwa utukufu wa Mungu Baba.

  2. 4 Ninyi wanaume na wanawake wazinzi, hamjui ya kwamba urafiki na dunia ni uadui na Mungu? Kwa hiyo mtu yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hufanyika adui wa Mungu. 5 Au mwadhani kwamba Andiko lasema bure kuwa huyo Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu? 6 Lakini yeye hutupatia neema zaidi. Hii ndiyo sababu Andiko husema:

    “Mungu huwapinga wenye kiburi,

    lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

    7 Basi mtiini Mungu. Mpingeni ibilisi, naye atawakimbia. 8 Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu ninyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu ninyi wenye nia mbili. 9 Huzunikeni, ombolezeni na kulia. Kicheko chenu na kigeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa huzuni. 10 Jinyenyekezeni mbele za Bwana, naye atawainua.

  3. 5 Vivyo hivyo, ninyi mlio vijana watiini wazee. Nanyi nyote imewapasa kujivika unyenyekevu kila mtu kwa mwenzake, kwa kuwa,

    “Mungu huwapinga wenye kiburi,

    lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

    6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.

  4. 7 Alipoona jinsi wageni walivyokuwa wanachagua mahali pa heshima wakati wa kula, akawaambia mfano huu: 8 “Mtu akikualika arusini, usikae mahali pa mgeni wa heshima kwa kuwa inawezekana amealikwa mtu mheshimiwa kuliko wewe. 9 Kama mkifanya hivyo yule aliyewaalika ninyi wawili atakuja na kukuambia, ‘Mpishe huyu mtu kiti chako.’ Ndipo kwa aibu utalazimika kukaa katika nafasi ya chini kabisa. 10 Badala yake, unapoalikwa, chagua nafasi ya chini, ili yule mwenyeji wako atakapokuona atakuja na kukuambia, ‘Rafiki yangu, nenda kwenye nafasi iliyo bora zaidi.’ Kwa jinsi hii utakuwa umepewa heshima mbele ya wageni wenzako wote. 11 Kwa maana kila mtu ajikwezaye atashushwa, naye ajishushaye atakwezwa.”

  5. 28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

  6. 1 Basi, mimi niliye mfungwa wa Bwana, nawasihi mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa. 2 Kwa unyenyekevu wote na upole, mkiwa wavumilivu, mkichukuliana kwa upendo. 3 Jitahidini kudumisha umoja wa Roho katika kifungo cha amani.

  7. 13 “Wakati nitakapofunga mbingu ili isiwepo mvua, au nikiamuru nzige kula mazao ya nchi au nikituma tauni miongoni mwa watu wangu, 14 kama watu wangu, wanaoitwa kwa Jina langu, watajinyenyekesha na kuomba na kuutafuta uso wangu na kuacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi yao na nitaiponya nchi yao. 15 Sasa macho yangu yatafumbuka na masikio yangu yatasikiliza kwa makini maombi yaombwayo mahali hapa.

  8. 33 Kumcha Bwana humfundisha mtu hekima,

    nao unyenyekevu huja kabla ya heshima.

  9. 18 Kiburi hutangulia maangamizi,

    roho ya majivuno hutangulia maanguko.

    19 Ni afadhali kuwa mnyenyekevu katika roho

    miongoni mwa walioonewa

    kuliko kugawana nyara pamoja na wenye kiburi.

  10. 1 Wakati huo, wanafunzi wakamjia Yesu na kumuuliza, “Je, nani aliye mkuu kuliko wote katika Ufalme wa Mbinguni?”

    2 Yesu akamwita mtoto mdogo na kumsimamisha katikati yao. 3 Naye akasema: “Amin, nawaambia, msipookoka na kuwa kama watoto wadogo, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni. 4 Kwa hiyo mtu yeyote anyenyekeaye kama huyu mtoto, ndiye aliye mkuu kuliko wote katika Ufalme wa Mbinguni.

  11. 9 Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine: 10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. 11 Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. 12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’

    13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’

    14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”

    15 Pia, watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wachanga ili awaguse. Wanafunzi wake walipoona hivyo, wakawakemea. 16 Lakini Yesu akawaita wale watoto waje kwake, akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa. 17 Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”

  12. 4 Unyenyekevu na kumcha Bwana

    huleta utajiri, heshima na uzima.

  13. 15 Kwa maana hili ndilo asemalo Aliye juu, yeye aliyeinuliwa sana,

    yeye aishiye milele, ambaye jina lake ni Mtakatifu:

    “Ninaishi mimi mahali palipoinuka na patakatifu,

    lakini pia pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu

    na mwenye roho ya unyenyekevu,

    ili kuzihuisha roho za wanyenyekevu

    na kuihuisha mioyo yao waliotubu.

  14. 12 Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi. 14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.

  15. 8 Amekuonyesha yaliyo mema, ee mwanadamu.

    Bwana anataka nini kwako?

    Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema,

    na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.

  16. 8 “Lakini ninyi msiitwe ‘Rabi,’ kwa sababu mnaye Bwana mmoja na ninyi nyote ni ndugu. 9 Nanyi msimwite mtu yeyote ‘Baba,’ hapa duniani, kwa maana mnaye Baba mmoja, naye yuko mbinguni. 10 Wala msiitwe ‘Mwalimu,’ kwa maana mnaye mwalimu mmoja tu, ndiye Kristo. 11 Yeye aliye mkuu kuliko ninyi nyote miongoni mwenu atakuwa mtumishi wenu. 12 Kwa kuwa yeyote anayejikweza atashushwa, na yeyote anayejinyenyekeza atakwezwa.

  17. 12 Kabla ya anguko moyo wa mtu hujaa kiburi,

    bali unyenyekevu hutangulia heshima.

  18. 25 Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, nao wenye vyeo huonyesha mamlaka yao. 26 Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, 27 naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu hana budi kuwa mtumwa wenu: 28 kama vile ambavyo Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”

  19. 2 Alikua mbele yake kama mche mwororo

    na kama mzizi katika nchi kavu.

    Hakuwa na uzuri wala utukufu wa kutuvutia kwake,

    hakuwa na chochote katika sura yake cha kutufanya tumtamani.

    3 Alidharauliwa na kukataliwa na wanadamu,

    mtu wa huzuni nyingi, ajuaye mateso.

    Kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,

    alidharauliwa, wala hatukumhesabu kuwa kitu.

    4 Hakika alichukua udhaifu wetu

    na akajitwika huzuni zetu,

    hata hivyo tulidhania kuwa amepigwa na Mungu,

    akapigwa sana naye, na kuteswa.

    5 Lakini alitobolewa kwa ajili ya makosa yetu,

    alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu;

    adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake,

    na kwa majeraha yake sisi tumepona.

    6 Sisi sote, kama kondoo, tumepotea,

    kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe,

    naye Bwana aliweka juu yake

    maovu yetu sisi sote.

    7 Alionewa na kuteswa,

    hata hivyo hakufungua kinywa chake;

    aliongozwa kama mwana-kondoo

    apelekwaye machinjoni,

    kama vile kondoo anyamazavyo mbele ya wao wamkataye manyoya,

    hivyo hakufungua kinywa chake.

    8 Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa.

    Nani awezaye kueleza kuhusu kizazi chake?

    Kwa maana alikatiliwa mbali na nchi ya walio hai,

    alipigwa kwa ajili ya makosa ya watu wangu.

  20. 3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa.

  21. 2 Kiburi kinapokuja, ndipo huja aibu,

    bali unyenyekevu huja na hekima.

    3 Uadilifu wa wenye haki huwaongoza,

    bali wasio waaminifu huharibiwa na hila yao.

  22. 5 Heri walio wapole,

    maana hao watairithi nchi.

  23. 34 Huwadhihaki wale wanaodhihaki,

    lakini huwapa neema wale wanyenyekevu.

  24. 23 Kiburi cha mtu humshusha,

    bali mtu mwenye roho ya unyenyekevu

    hupata heshima.

  25. 13 Ni nani aliye na hekima na ufahamu miongoni mwenu? Basi na aionyeshe hiyo kwa maisha yake mema na kwa matendo yake yaliyotendwa kwa unyenyekevu utokanao na hekima. 14 Lakini ikiwa mna wivu na ni wenye chuki na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu kwa ajili ya hayo wala msiikatae kweli. 15 Hekima ya namna hiyo haishuki kutoka mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyo ya kiroho, na ya kishetani. 16 Kwa maana panapokuwa na wivu na ubinafsi, ndipo penye machafuko na uovu wa kila namna.

    17 Lakini hekima itokayo mbinguni kwanza ni safi, kisha inapenda amani, tena ni ya upole, iliyo tayari kusikiliza wengine kwa unyenyekevu, iliyojaa huruma na matunda mema, isiyopendelea mtu, tena isiyokuwa na unafiki. 18 Mavuno ya haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.

  26. 2 Kumbuka jinsi Bwana Mungu wenu alivyowaongoza katika njia yote katika jangwa kwa miaka hii arobaini, kukunyenyekeza na kukujaribu ili ajue lililoko moyoni mwako, kwamba utayashika maagizo yake au la. 3 Alikudhili na kukufanya uone njaa kisha akulishe kwa mana, ambayo wewe wala baba zako hamkuijua, awafundishe kuwa mwanadamu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Bwana.

  27. 27 Kwa kuwa moyo wako ulikuwa msikivu na ulijinyenyekeza mbele za Mungu uliposikia kile nilichosema dhidi ya mahali hapa na watu wake na kwa sababu ulijinyenyekeza mbele zangu na uliyararua mavazi yako na kulia mbele zangu, nimekusikia, asema Bwana.

  28. 8 Bwana ni mwema na mwenye adili,

    kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia zake.

    9 Huwaongoza wanyenyekevu katika haki,

    naye huwafundisha njia yake.

  29. 4 Kwa maana Bwana anapendezwa na watu wake,

    anawavika wanyenyekevu taji ya wokovu.

  30. 13 Kisha Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Mto Yordani ili Yohana ambatize. 14 Lakini Yohana akajitahidi kumzuia, akimwambia, “Mimi ninahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu nikubatize?”

    15 Lakini Yesu akamjibu, “Kubali hivi sasa, kwa maana ndivyo itupasavyo kwa njia hii kuitimiza haki yote.” Hivyo Yohana akakubali.

  31. 1 Hili ndilo asemalo Bwana,

    “Mbingu ni kiti changu cha enzi,

    nayo dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu.

    Iko wapi nyumba mtakayoijenga kwa ajili yangu?

    Mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi?

    2 Je, mkono wangu haukufanya vitu hivi vyote,

    hivyo vikapata kuwepo?”

    asema Bwana.

    “Mtu huyu ndiye ninayemthamini:

    yeye ambaye ni mnyenyekevu

    na mwenye roho yenye toba,

    atetemekaye asikiapo neno langu.

  32. 42 Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa wale wanaodhaniwa kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala watu kwa nguvu, nao wenye vyeo huonyesha mamlaka yao. 43 Lakini isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, 44 na yeyote anayetaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa mtumwa wa wote. 45 Kwa kuwa hata Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”

  33. 46 Naye Maria akasema:

    “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,

    47 nayo roho yangu inamfurahia

    Mungu Mwokozi wangu,

    48 kwa kuwa ameangalia kwa fadhili

    unyonge wa mtumishi wake.

    Hakika tangu sasa vizazi vyote vitaniita aliyebarikiwa,

    49 kwa maana yeye Mwenye Nguvu

    amenitendea mambo ya ajabu:

    jina lake ni takatifu.

  34. 27 Ahabu aliposikia maneno haya, akararua nguo zake, akavaa nguo za gunia na kufunga. Akalala na kujifunika nguo za gunia na kwenda kwa unyenyekevu.

    28 Ndipo neno la Bwana lilipomjia Eliya Mtishbi kusema, 29 “Umeona jinsi Ahabu alivyojinyenyekeza mbele zangu? Kwa kuwa amejishusha mwenyewe, sitaleta maafa haya wakati akiwa hai, lakini nitayaleta juu ya nyumba yake katika siku za mwanawe.”

  35. 9 Shangilia sana, ee Binti Sayuni!

    Piga kelele, Binti Yerusalemu!

    Tazama, Mfalme wako anakuja kwako,

    ni mwenye haki, naye ana wokovu,

    ni mpole, naye amepanda punda,

    mwana-punda, mtoto wa punda.

  36. 12 Alipomaliza kuwanawisha miguu yao, alivaa tena mavazi yake, akarudi alikokuwa ameketi, akawauliza, “Je, mmeelewa nililowafanyia? 13 Ninyi mnaniita mimi ‘Mwalimu’ na ‘Bwana,’ hii ni sawa, maana ndivyo nilivyo. 14 Kwa hiyo, ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewanawisha ninyi miguu, pia hamna budi kunawishana miguu ninyi kwa ninyi. 15 Mimi nimewawekea kielelezo kwamba imewapasa kutenda kama vile nilivyowatendea ninyi. 16 Amin, amin nawaambia, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala aliyetumwa si mkuu kuliko yule aliyemtuma. 17 Sasa kwa kuwa mmejua mambo haya, heri yenu ninyi kama mkiyatenda.

  37. 9 Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri.

  38. 24 Pia yakazuka mabishano katikati ya wanafunzi kwamba ni nani aliyeonekana kuwa mkuu kuliko wote miongoni mwao. 25 Yesu akawaambia, “Wafalme na watu wa Mataifa huwatawala watu kwa nguvu. Nao wenye mamlaka juu yao hujiita ‘Wafadhili.’ 26 Lakini ninyi msifanane nao. Bali yeye aliye mkuu kuliko wote miongoni mwenu, inampasa kuwa kama yeye aliye mdogo wa wote, naye atawalaye na awe kama yeye ahudumuye. 27 Kwani ni nani aliye mkuu? Ni yule aketiye mezani au ni yule ahudumuye? Si ni yule aliyekaa mezani? Lakini mimi niko miongoni mwenu kama yule ahudumuye.

  39. 26 Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika jamaa zenye vyeo. 27 Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima, Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu. 28 Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko, 29 ili mtu yeyote asijisifu mbele zake. 30 Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanyika kwetu hekima itokayo kwa Mungu, yaani haki, na utakatifu na ukombozi. 31 Hivyo, kama ilivyoandikwa: “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.”

  40. 6 Ingawa Bwana yuko juu,

    humwangalia mnyonge,

    bali mwenye kiburi

    yeye anamjua kutokea mbali.

  41. 5 Bwana wetu ni mkuu na mwenye uwezo mwingi,

    ufahamu wake hauna kikomo.

    6 Bwana huwahifadhi wanyenyekevu

    lakini huwashusha waovu mpaka mavumbini.

  42. 3 Yesu akijua ya kwamba Baba ameweka vitu vyote chini ya mamlaka yake na kwamba yeye alitoka kwa Mungu na alikuwa anarudi kwa Mungu, 4 hivyo aliondoka chakulani, akavua vazi lake la nje, akajifunga kitambaa kiunoni. 5 Kisha akamimina maji kwenye sinia na kuanza kuwanawisha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa kile kitambaa alichokuwa amejifunga kiunoni.

    6 Alipomfikia Simoni Petro, Petro akamwambia, “Bwana, je, wewe utaninawisha mimi miguu?”

    7 Yesu akamjibu, “Hivi sasa hutambui lile ninalofanya, lakini baadaye utaelewa.”

    8 Petro akamwambia, “La, wewe hutaninawisha miguu kamwe.”

    Yesu akamjibu, “Kama nisipokunawisha, wewe huna sehemu nami.”

  43. 18 Walipofika akawaambia, “Ninyi wenyewe mnajua jinsi nilivyoishi katikati yenu muda wote tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia. 19 Nilimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote na kwa machozi nikivumilia taabu na mapingamizi yaliyonipata kutokana na hila za Wayahudi. 20 Mnajua kwamba sikusita kuhubiri jambo lolote ambalo lingekuwa la kuwafaa ninyi, lakini nilifundisha hadharani na nyumba kwa nyumba. 21 Nimewashuhudia Wayahudi na Wayunani kwamba inawapasa kumgeukia Mungu kwa kutubu dhambi na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo.

  44. 16 Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge. Wala msiwe watu wenye kujivuna kwamba mnajua kila kitu.

  45. 8 Hatimaye, ninyi nyote kuweni na nia moja, wenye kuhurumiana, mkipendana kama ndugu, na mwe wasikitivu na wanyenyekevu. 9 Msilipe ovu kwa ovu, au jeuri kwa jeuri, bali barikini, kwa maana hili ndilo mliloitiwa ili mpate kurithi baraka. 10 Kwa maana,

    “Yeyote apendaye uzima

    na kuona siku njema,

    basi auzuie ulimi wake usinene mabaya,

    na midomo yake isiseme hila.

    11 Mtu huyo lazima aache uovu, akatende mema;

    lazima aitafute amani na kuifuatilia sana.

  46. 6 Viongozi wa Israeli na mfalme wakajinyenyekeza na kusema, “Bwana Mungu ni mwenye haki.”

    7 Bwana Mungu alipoona kwamba wamejinyenyekeza, neno hili la Bwana likamjia Shemaya: “Maadamu wamejinyenyekeza, sitawaangamiza bali hivi karibuni nitawapatia wokovu. Ghadhabu yangu haitamwagwa juu ya Yerusalemu kwa kupitia Shishaki.

  47. 5 “Mwambieni Binti Sayuni,

    ‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako,

    ni mnyenyekevu, naye amepanda punda,

    juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’ ”

  48. 33 Basi wakafika Kapernaumu na baada ya kuingia nyumbani akawauliza, “Mlikuwa mnabishana nini kule njiani?” 34 Lakini hawakumjibu, kwa sababu njiani walikuwa wakibishana kuhusu nani miongoni mwao alikuwa mkuu zaidi ya wote.

    35 Akaketi chini, akawaita wote kumi na wawili, akawaambia: “Kama mtu yeyote akitaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa wa mwisho na mtumishi wa wote.”

    36 Kisha akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha katikati yao. Akamkumbatia, akawaambia, 37 “Mtu yeyote amkaribishaye mmoja wa hawa watoto wadogo kwa Jina langu, anikaribisha mimi. Naye anikaribishaye mimi, amkaribisha Baba yangu aliyenituma.”

  49. 18 Mtu yeyote asiwaondolee thawabu yenu kwa kusisitiza kunyenyekea kwake na kuabudu malaika. Mtu kama huyo hudumu katika maono yake, akijivuna bila sababu katika mawazo ya kibinadamu. 19 Yeye amepoteza ushirikiano na Kichwa, ambaye kutoka kwake mwili wote unalishwa na kushikamanishwa pamoja kwa viungo na mishipa, nao hukua kwa ukuaji utokao kwa Mungu.

  50. 1 Wakumbushe watu kuwanyenyekea watawala na kuwatii wenye mamlaka, wawe tayari kutenda kila lililo jema. 2 Wasimnenee mtu yeyote mabaya, wasiwe wagomvi, bali wawe wapole, wakionyesha unyenyekevu kwa watu wote.

    3 Maana sisi wenyewe wakati fulani tulikuwa wajinga, wasiotii, tukiwa watumwa wa tamaa mbaya na anasa za kila aina. Tuliishi katika uovu na wivu, tukichukiwa na kuchukiana sisi kwa sisi. 4 Lakini wema na upendo wa Mungu Mwokozi wetu ulipofunuliwa, 5 alituokoa, si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda, bali kwa sababu ya rehema zake. Alituokoa kwa kutuosha kwa kuzaliwa mara ya pili na kwa kufanywa wapya kwa njia ya Roho Mtakatifu, 6 ambaye Mungu alitumiminia kwa wingi kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu, 7 ili kwamba, tukiisha kuhesabiwa haki kwa neema yake, tupate kuwa warithi tukiwa na tumaini la uzima wa milele. 8 Hili ni neno la kuaminiwa. Nami nataka uyasisitize mambo haya, ili wale ambao wamemwamini Mungu wapate kuwa waangalifu kujitoa kwa ajili ya kutenda mema wakati wote. Mambo haya ni mazuri tena ya manufaa kwa kila mtu.

    9 Lakini jiepushe na maswali ya kipuzi, mambo ya koo, mabishano na ugomvi kuhusu sheria, kwa sababu hayana faida, tena ni ubatili.

  51. 10 mimi sistahili fadhili na uaminifu wako wote ulionitendea mimi mtumishi wako. Nilikuwa na fimbo tu mkononi mwangu nilipovuka mto huu wa Yordani, lakini sasa ninayo makundi mawili.

  52. 5 Ndipo nikalia, “Ole wangu! Nimeangamia! Kwa kuwa mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninaishi katikati ya watu wenye midomo michafu, nayo macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana Mwenye Nguvu Zote.”

  53. 43 Lakini ni kwa nini mimi nimepata upendeleo kiasi hiki, hata mama wa Bwana wangu afike kwangu?

  54. 16 Yosefu akamjibu Farao, “Siwezi kuifasiri, lakini Mungu atampa Farao jibu analolihitaji.”

  55. 10 Mpaka leo hawajajinyenyekeza au kuonyesha heshima, wala hawajafuata sheria yangu na amri nilizoweka mbele yenu na baba zenu.

  56. 27 Yule mwanamke akajibu, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka kwenye meza za bwana zao.”

  57. 29 Bibi arusi ni wa bwana arusi. Lakini rafiki yake bwana arusi anayesimama karibu naye na kusikiliza kutoka kwake, hufurahi sana aisikiapo sauti ya bwana arusi. Kwa sababu hii furaha yangu imekamilika. 30 Yeye hana budi kuwa mkuu zaidi na mimi nizidi kuwa mdogo.”

  58. 30 “Mimi siwezi kufanya jambo lolote peke yangu. Ninavyosikia ndivyo ninavyohukumu, nayo hukumu yangu ni ya haki kwa kuwa sitafuti kufanya mapenzi yangu mwenyewe, bali mapenzi yake yeye aliyenituma.

    31 “Kama ningejishuhudia mimi mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. 32 Lakini yuko mwingine anishuhudiaye na ninajua kwamba ushuhuda wake ni wa kweli.

  59. 22 “Lakini wewe mwanawe, ee Belshaza, hukujinyenyekeza, ingawa ulifahamu haya yote. 23 Badala yake, umejiinua dhidi ya Bwana wa mbingu. Uliletewa vikombe vya Hekalu lake, nawe na wakuu wako, wake zako na masuria wako mlivitumia kwa kunywea mvinyo. Ukaisifu miungu ya fedha na dhahabu, ya shaba, chuma, miti na mawe, miungu ambayo haiwezi kuona, au kusikia wala kufahamu. Lakini hukumheshimu Mungu ambaye anaushikilia uhai wako na njia zako zote mkononi mwake.

  60. 5 Yesu alipoingia Kapernaumu, jemadari mmoja alimjia, kumwomba msaada, 6 akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani na amepooza, tena ana maumivu makali ya kutisha.”

    7 Yesu akamwambia, “Nitakuja na kumponya.”

    8 Lakini yule jemadari akamwambia, “Bwana, mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona. 9 Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.”

    10 Yesu aliposikia maneno haya, alishangaa, akawaambia wale waliomfuata, “Amin, nawaambia, hata katika Israeli sijapata kuona yeyote mwenye imani kubwa namna hii. 11 Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaki na Yakobo katika Ufalme wa Mbinguni. 12 Lakini warithi wa Ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwako kilio na kusaga meno.”

    13 Kisha Yesu akamwambia yule jemadari, “Nenda na iwe kwako sawasawa na imani yako.” Naye yule mtumishi akapona saa ile ile.

  61. 27 Kisha Abrahamu akasema tena: “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri wa kuzungumza na Bwana, ingawa mimi si kitu bali ni mavumbi na majivu;

  62. 3 Kwa hiyo Mose na Aroni wakaenda kwa Farao na kumwambia, “Hili ndilo Bwana, Mungu wa Waebrania, asemalo: ‘Utaendelea hata lini kukataa kunyenyekea mbele yangu? Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu.

  63. 3 (Basi Mose alikuwa mtu mnyenyekevu sana, mnyenyekevu kuliko mtu mwingine yeyote katika uso wa dunia.)

  64. 29 Watu watakaposhushwa, nawe ukasema, ‘Wainue!’

    ndipo atamwokoa aliyevunjika moyo.

  65. 1 Usijisifu kwa ajili ya kesho,

    kwa kuwa hujui ni nini kitakachozaliwa kwa siku moja.

    2 Mwache mwingine akusifu,

    wala si kinywa chako mwenyewe;

    mtu mwingine afanye hivyo

    na si midomo yako mwenyewe.

  66. 1 “Angalieni msitende wema wenu mbele ya watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni.

    2 “Hivyo mnapowapa wahitaji, msipige panda mbele yenu kama wafanyavyo wanafiki katika masinagogi na mitaani, ili wasifiwe na watu. Amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao. 3 Lakini ninyi mtoapo sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa kushoto usijue mkono wako wa kuume unachofanya, 4 ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo Baba yako wa mbinguni, yeye aonaye sirini atakupa thawabu kwa wazi.

    5 “Nanyi msalipo, msiwe kama wanafiki, maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na kando ya barabara ili waonekane na watu. Amin nawaambia, wao wamekwisha kupata thawabu yao. 6 Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango na umwombe Baba yako aliye sirini. Naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako. 7 Nanyi mnaposali msiseme maneno kama wafanyavyo watu wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa maneno yao. 8 Msiwe kama wao, kwa sababu Baba yenu anajua kile mnachohitaji kabla hamjamwomba.

  67. 19 Hatagombana wala hatapiga kelele,

    wala hakuna atakayesikia sauti yake njiani.

    20 Mwanzi uliopondeka hatauvunja,

    na utambi unaofuka moshi hatauzima,

    mpaka atakapoifanya haki ishinde.

  68. 37 Akamchukua Petro pamoja na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kufadhaika. 38 Kisha Yesu akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe pamoja nami.”

    39 Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe.”

  69. 18 Lakini Daudi akamwambia Sauli, “Mimi ni nani, nayo jamaa yangu ni nini au ukoo wa baba yangu katika Israeli, kwamba mimi niwe mkwewe mfalme?” 19 Basi ulipofika wakati wa Daudi kupewa Merabu, binti Sauli, huyo binti aliozwa kwa Adrieli, Mmeholathi.

    20 Basi Mikali binti Sauli alimpenda Daudi, nao walipomwambia Sauli juu ya jambo hili, likampendeza. 21 Sauli akawaza, “Nitampa Daudi binti yangu, ili apate kuwa mtego kwake, ili kwamba mkono wa Wafilisti upate kuwa juu yake.” Hivyo Sauli akamwambia Daudi, “Sasa unayo nafasi ya pili ya kuwa mkwe wangu.”

    22 Ndipo Sauli akawaagiza watumishi wake, akisema, “Zungumzeni na Daudi kwa siri na kumwambia, ‘Tazama, mfalme amependezwa nawe, nao watumishi wake wote wanakupenda. Basi na uwe mkwewe mfalme.’ ”

    23 Watumishi wa Sauli wakarudia hayo maneno kwa Daudi. Lakini Daudi akasema, “Je, mnafikiri ni jambo dogo kuwa mkwewe mfalme? Mimi ni mtu maskini tu, na nisiyejulikana sana.”

  70. 2 Nafsi yangu itajisifu katika Bwana,

    walioonewa watasikia na wafurahi.

  71. 32 Maskini wataona na kufurahi:

    ninyi mnaomtafuta Mungu, mioyo yenu na iishi!

    33 Bwana huwasikia wahitaji

    wala hadharau watu wake waliotekwa.

  72. 11 Macho ya mtu mwenye majivuno yatanyenyekezwa

    na kiburi cha wanadamu kitashushwa,

    Bwana peke yake ndiye atakayetukuzwa siku hiyo.

  73. 19 Mara nyingine tena wanyenyekevu watafurahi katika Bwana,

    wahitaji watafurahi katika yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

  74. 4 Bwana Mwenyezi amenipa ulimi uliofundishwa,

    ili kujua neno limtegemezalo aliyechoka.

    Huniamsha asubuhi kwa asubuhi,

    huamsha sikio langu lisikie kama mtu afundishwaye.

    5 Bwana Mwenyezi amezibua masikio yangu,

    nami sikuwa mwasi,

    wala sikurudi nyuma.

    6 Niliwapa mgongo wangu wale wanipigao,

    mashavu yangu wale wangʼoao ndevu zangu;

    sikuuficha uso wangu kutokana na fedheha

    na kutemewa mate.

  75. 37 Basi mimi, Nebukadneza, humhimidi, na humtukuza na kumsifu Mfalme wa mbinguni, kwa sababu kila kitu afanyacho ni haki, na njia zake zote ni adili. Nao waendao kwa kiburi anaweza kuwashusha.

  76. 3 Mtafuteni Bwana, enyi nyote wanyenyekevu wa nchi,

    ninyi ambao hufanya lile analoamuru.

    Tafuteni haki, tafuteni unyenyekevu;

    labda mtahifadhiwa

    siku ya hasira ya Bwana.

  77. 51 Ndipo akashuka pamoja nao hadi Nazareti, naye alikuwa mtiifu kwao. Lakini mama yake akayaweka moyoni mwake mambo haya yote.

  78. 15 “Usiogope, Ewe binti Sayuni;

    tazama, Mfalme wako anakuja,

    amepanda mwana-punda!”

  79. 1 Basi, mimi Paulo ninawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Kristo, mimi niliye “mwoga” ninapokuwa pamoja nanyi ana kwa ana, lakini mwenye ujasiri nikiwa mbali nanyi!

  80. 23 Kwa kweli amri kama hizo huonekana kama zina hekima, katika namna za ibada walizojitungia wenyewe, na unyenyekevu wa uongo na kuutawala mwili kwa ukali, lakini hayafai kitu katika kuzuia tamaa za mwili.

  81. 15 Msemo huu ni wa kweli na unaostahili kukubalika, usemao kwamba: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, ambao mimi ndiye niliye mbaya kuliko wote.

  82. 11 Lakini Mose akamwambia Mungu, “Mimi ni nani hata niende kwa Farao kuwatoa Waisraeli nchini Misri?”

  83. 18 Ndipo Mfalme Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za Bwana, akasema:

    “Ee Bwana Mwenyezi, mimi ni nani, na jamaa yangu ni nini, hata umenileta mpaka hapa nilipo? 19 Naam, kana kwamba hili halitoshi machoni pako, Ee Bwana Mwenyezi, wewe umenena pia kuhusu siku zijazo za nyumba ya mtumishi wako. Je, hii ndiyo njia yako ya kawaida ya kushughulika na mwanadamu, Ee Bwana Mwenyezi?

  84. 28 Wewe huwaokoa wanyenyekevu,

    lakini macho yako ni juu ya wenye kiburi

    ili uwashushe.

  85. 7 “Sasa, Ee Bwana Mungu wangu, umemfanya mtumishi wako mfalme badala ya baba yangu Daudi. Lakini mimi ni mtoto mdogo tu, wala sijui jinsi ya kutekeleza wajibu wangu.

  86. 24 Katika siku hizo, Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Akamwomba Bwana, ambaye alimjibu na kumpa ishara. 25 Lakini moyo wa Hezekia ukajaa majivuno na hakuonyesha itikio kwa wema aliotendewa, kwa hiyo ghadhabu ya Bwana ikawa juu yake na juu ya Yuda na Yerusalemu. 26 Ndipo Hezekia akatubu kwa ajili ya kiburi cha moyo wake, kama walivyofanya watu wa Yerusalemu, kwa hiyo ghadhabu ya Bwana haikuja juu yao katika siku za Hezekia.

  87. 27 Wewe huwaokoa wanyenyekevu,

    lakini huwashusha wenye kiburi.

  88. 17 Majivuno ya mwanadamu yatashushwa,

    na kiburi cha wanadamu kitanyenyekezwa,

    Bwana peke yake ndiye atatukuzwa siku hiyo,

    18 nazo sanamu zitatoweka kabisa.

  89. 8 Simoni Petro alipoona haya yaliyotukia, alianguka miguuni mwa Yesu na kumwambia, “Bwana, ondoka kwangu. Mimi ni mtu mwenye dhambi!”

  90. 11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

  91. 10 Mose akamwambia Bwana, “Ee Bwana, kamwe sijapata kuwa msemaji kwa ufasaha wakati uliopita wala tangu ulipoanza kuzungumza na mtumishi wako. Ulimi wangu ni mzito kuzungumza.”

  92. 17 Mnaweza kusema, “Uwezo wangu na nguvu za mikono yangu ndizo zilizonipatia utajiri huu.” 18 Lakini kumbukeni Bwana Mungu wenu, ndiye ambaye huwapa uwezo wa kupata utajiri, na hivyo kulithibitisha Agano lake, ambalo aliwaapia baba zenu, kama ilivyo leo.

  93. 7 Bwana humfanya mtu maskini naye hutajirisha,

    hushusha na hukweza.

  94. 21 Sauli akajibu, “Je, mimi si Mbenyamini, kutoka kabila dogo kuliko yote ya Israeli, nao ukoo wangu si ndio mdogo kuliko koo zote za kabila la Benyamini? Kwa nini uniambie jambo la namna hiyo?”

  95. 8 “Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: Nilikutoa wewe kutoka machungani na kutoka kuandama kundi la kondoo na mbuzi ili kuwaongoza watu wangu Israeli.

  96. 18 Mwambieni mfalme wa Yuda, ambaye amewatuma kumuuliza Bwana, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli, kuhusu maneno uliyoyasikia: 19 Kwa kuwa moyo wako ulikuwa msikivu na ulijinyenyekeza mbele za Bwana uliposikia kile nilichosema dhidi ya mahali hapa na watu wake, kwamba wangelaaniwa na kuachwa ukiwa, basi kwa sababu uliyararua mavazi yako na kulia mbele zangu, nimekusikia, asema Bwana. 20 Kwa hiyo nitakukusanya kwa baba zako, nawe utazikwa kwa amani. Macho yako hayataona maafa yote nitakayoleta juu ya mahali hapa.’ ”

    Basi wakapeleka jibu lake kwa mfalme.

  97. 12 Alifanya maovu machoni pa Bwana Mungu wake, wala hakujinyenyekeza mbele ya nabii Yeremia, ambaye alinena neno la Bwana.

  98. 4 “Mimi sistahili kabisa: ninawezaje kukujibu wewe?

    Nauweka mkono wangu juu ya kinywa changu.

    5 Nimesema mara moja, lakini sina jibu;

    naam, nimesema mara mbili,

    lakini sitasema tena.”

  99. 4 “Ulisema, ‘Sikiliza sasa, nami nitanena;

    nitakuuliza swali, nawe yakupasa kunijibu.’

    5 Masikio yangu yalikuwa yamesikia habari zako,

    lakini sasa macho yangu yamekuona.

    6 Kwa hiyo najidharau mwenyewe,

    na kutubu katika mavumbi na majivu.”

  100. Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.

    1 Moyo wangu hauna kiburi, Ee Bwana,

    macho yangu hayajivuni;

    sijishughulishi na mambo makuu kunizidi

    wala mambo ya ajabu mno kwangu.

    2 Lakini nimetuliza na kunyamazisha nafsi yangu;

    kama mtoto aliyeachishwa kunyonya na mama yake,

    kama mtoto aliyeachishwa kunyonya

    ndivyo ilivyo nafsi iliyoko ndani yangu.

  101. 2 Usiwe mwepesi kuzungumza,

    usiwe na haraka katika moyo wako

    kuzungumza lolote mbele za Mungu.

    Mungu yuko mbinguni

    nawe uko duniani,

    kwa hiyo maneno yako

    na yawe machache.

  102. 15 Lakini niseme nini?

    Amesema nami, naye yeye mwenyewe amelitenda hili.

    Nitatembea kwa unyenyekevu

    katika miaka yangu yote

    kwa sababu ya haya maumivu makali

    ya nafsi yangu.

  103. 23 Hili ndilo asemalo Bwana:

    “Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake,

    au mwenye nguvu ajisifu katika nguvu zake,

    wala tajiri ajisifu katika utajiri wake,

    24 lakini yeye ajisifuye, na ajisifu kwa sababu hili:

    kwamba ananifahamu na kunijua mimi,

    kwamba mimi ndimi Bwana, nitendaye wema,

    hukumu na haki duniani,

    kwa kuwa napendezwa na haya,”

    asema Bwana.

  104. 46 Kukazuka mabishano miongoni mwa wanafunzi kuhusu ni nani miongoni mwao atakayekuwa mkuu kuliko wote. 47 Lakini Yesu akayatambua mawazo yao, naye akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha kando yake. 48 Kisha akawaambia, “Yeyote amkaribishaye mtoto huyu mdogo kwa Jina langu, anikaribisha mimi, na yeyote atakayenikaribisha mimi, atakuwa amemkaribisha yeye aliyenituma. Kwa maana yeye aliye mdogo miongoni mwenu, ndiye aliye mkuu kuliko wote.”

  105. 24 Je, hamjui kwamba katika mashindano ya mbio wote wanaoshindana hukimbia, lakini ni mmoja wao tu apewaye tuzo? Kwa hiyo kimbieni katika mashindano kwa jinsi ambavyo mtapata tuzo.

    25 Kila mmoja anayeshiriki katika mashindano hufanya mazoezi makali. Wao hufanya hivyo ili wapokee taji isiyodumu, lakini sisi tunafanya hivyo ili kupata taji idumuyo milele. 26 Kwa hiyo mimi sikimbii kama mtu akimbiaye bila lengo, sipigani kama mtu anayepiga hewa, 27 la, bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha ili nikiisha kuwahubiria wengine, mimi nisiwe mtu wa kukataliwa.

  106. 30 Kama ni lazima nijisifu, basi nitajisifia yale mambo yanayoonyesha udhaifu wangu.

  107. 1 Kwa sababu hii, kwa kuwa tumezungukwa na wingu kubwa namna hii la mashahidi, basi na tuweke kando kila kitu kinachotuzuia na ile dhambi inayotuzinga kwa urahisi, nasi tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa kwa ajili yetu. 2 Basi na tumtazame sana Yesu mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu, yeye ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake alistahimili msalaba, bila kujali aibu ya huo msalaba, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. 3 Mtafakarini sana yeye aliyestahimili upinzani mkuu namna hii kutoka kwa watu wenye dhambi, ili kwamba msije mkachoka na kukata tamaa.

    4 Katika kushindana kwenu dhidi ya dhambi, bado hamjapigana kiasi cha kumwaga damu yenu.

  108. 3 Kujipamba kwenu kusiwe kwa nje tu, kama vile kusuka nywele, kuvalia vitu vilivyofanyizwa kwa dhahabu na kwa mavazi. 4 Badala yake, kujipamba kwenu kuwe katika utu wenu wa moyoni, yaani uzuri usioharibika wa roho ya upole na utulivu, ambayo ni ya thamani sana machoni pa Mungu.