55 Bible Verses About Sacrifice

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Sacrifice
  1. 29 Yesu akajibu, “Amin, nawaambia, hakuna hata mtu aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu 30 ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya, na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.”

  2. 1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.

  3. 11 Kila kuhani husimama siku kwa siku akifanya huduma yake ya ibada, na kutoa tena na tena dhabihu zile zile ambazo haziwezi kamwe kuondoa dhambi. 12 Lakini huyu kuhani akiisha kutoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi kwa wakati wote, aliketi mkono wa kuume wa Mungu. 13 Tangu wakati huo anangoja mpaka adui zake wawekwe chini ya miguu yake, 14 kwa sababu kwa dhabihu moja amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wote wanaotakaswa.

  4. 10 Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaohudumu katika hema hawana haki ya kula vile vitu vilivyowekwa juu yake.

    11 Kuhani mkuu huchukua damu ya wanyama na kuiingiza Patakatifu pa Patakatifu, kama sadaka ya dhambi, lakini miili ya hao wanyama huteketezwa nje ya kambi. 12 Vivyo hivyo, Yesu naye aliteswa nje ya lango la mji ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe. 13 Kwa hiyo, basi na tumwendee nje ya kambi, tukiichukua aibu aliyobeba. 14 Kwa kuwa hapa hatuna mji udumuo, bali tunautafuta ule ujao.

    15 Basi kwa njia ya Yesu, tuzidi kumtolea Mungu dhabihu ya sifa, yaani matunda ya midomo inayolikiri Jina lake. 16 Na msiache kutenda mema na kushirikiana vile vitu mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu.

  5. 1 Kwa hiyo, mfuateni Mungu kama watoto wapendwao, 2 mkiishi maisha ya upendo, kama vile Kristo alivyotupenda sisi akajitoa kwa ajili yetu kuwa sadaka yenye harufu nzuri na dhabihu kwa Mungu.

  6. 21 Lakini sasa, haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Sheria na Manabii wanaishuhudia. 22 Haki hii itokayo kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote wamwaminio. Kwa maana hapo hakuna tofauti, 23 kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, 24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu. 25 Yeye ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonyesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa. 26 Alifanya hivyo ili kuonyesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.

  7. 3 Baada ya muda Kaini akaleta baadhi ya mazao ya shamba kama sadaka kwa Bwana. 4 Lakini Abeli akaleta fungu nono kutoka baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. Bwana akamkubali Abeli pamoja na sadaka yake, 5 lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni.

    6 Kisha Bwana akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika? Kwa nini uso wako una huzuni? 7 Ukifanya lililo sawa, je, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, inakutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.”

  8. 11 Kristo alipokuja akiwa Kuhani Mkuu wa mambo mema ambayo tayari yameshawasili, alipitia kwenye hema iliyo kuu zaidi na bora zaidi, ambayo haikutengenezwa kwa mikono ya binadamu, hii ni kusema, ambayo si sehemu ya uumbaji huu. 12 Hakuingia kwa njia ya damu ya mbuzi na ya ndama; lakini aliingia Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kwa damu yake mwenyewe, akiisha kupata ukombozi wa milele. 13 Damu ya mbuzi na ya mafahali, na majivu ya mitamba walivyonyunyiziwa wale waliokuwa najisi kwa taratibu za kiibada viliwatakasa, hata kuwaondolea uchafu wa nje. 14 Basi ni zaidi aje damu ya Kristo, ambaye kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na waa, itatusafisha dhamiri zetu kutokana na matendo yaletayo mauti, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai!

  9. 12 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi. 13 Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. 14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru.

  10. 22 Kwa kweli sheria hudai kwamba, karibu kila kitu kitakaswe kwa damu, wala pasipo kumwaga damu, hakuna msamaha wa dhambi.

    23 Kwa hiyo, ilikuwa muhimu kwa nakala za vitu vile vya mbinguni vitakaswe kwa dhabihu hizi, lakini vitu halisi vya mbinguni vilihitaji dhabihu bora kuliko hizi. 24 Kwa maana Kristo hakuingia kwenye patakatifu palipofanywa kwa mikono ya mwanadamu, ambao ni mfano wa kile kilicho halisi. Yeye aliingia mbinguni penyewe, ili sasa aonekane mbele za Mungu kwa ajili yetu. 25 Wala hakuingia mbinguni ili apate kujitoa mwenyewe mara kwa mara, kama vile kuhani mkuu aingiavyo Patakatifu pa Patakatifu kila mwaka kwa damu ambayo si yake mwenyewe. 26 Ingekuwa hivyo, ingempasa Kristo kuteswa mara nyingi tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Lakini sasa ametokea mara moja tu katika mwisho wa nyakati aiondoe dhambi kwa kujitoa mwenyewe kuwa dhabihu. 27 Kama vile mwanadamu alivyowekewa kufa mara moja tu na baada ya kufa akabili hukumu, 28 vivyo hivyo Kristo alitolewa mara moja tu kuwa dhabihu ili azichukue dhambi za watu wengi. Naye atakuja mara ya pili, sio kuchukua dhambi, bali kuwaletea wokovu wale wanaomngoja kwa shauku.

  11. 20 Kisha Noa akamjengea Bwana madhabahu, akachukua baadhi ya wale wanyama na ndege wote walio safi, akatoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. 21 Bwana akasikia harufu nzuri ya kupendeza, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena ardhi kwa sababu ya mwanadamu, hata ingawa kila mwelekeo wa moyo wake ni mbaya tangu ujana. Kamwe sitaangamiza tena viumbe hai vyote kama nilivyofanya.

    22 “Kwa muda dunia idumupo,

    wakati wa kupanda na wa kuvuna,

    wakati wa baridi na wa joto,

    wakati wa kiangazi na wa masika,

    usiku na mchana

    kamwe havitakoma.”

  12. 1 Bwana akamwita Mose na kusema naye kutoka kwenye Hema la Kukutania, akamwambia, 2 “Sema na Waisraeli na uwaambie, ‘Yeyote miongoni mwenu aletapo sadaka ya mnyama kwa Bwana, alete mnyama kama sadaka yake kutoka kundi lake la ngʼombe au la kondoo na mbuzi.

    3 “ ‘Kama sadaka hiyo ni ya kuteketezwa kutoka kwenye kundi la ngʼombe, atamtoa ngʼombe dume asiye na dosari. Ni lazima amlete kwenye ingilio la Hema la Kukutania ili aweze kukubalika kwa Bwana. 4 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka ya kuteketezwa, nayo itakubaliwa kwa niaba yake ili kufanya upatanisho kwa ajili yake.

  13. 22 Lakini Samweli akajibu:

    “Je, Bwana anafurahia sadaka za kuteketezwa na dhabihu

    kama vile kuitii sauti ya Bwana?

    Kutii ni bora zaidi kuliko dhabihu,

    nako kusikia ni bora

    kuliko mafuta ya kondoo dume.

  14. 24 Mtu yeyote asitafute yaliyo yake mwenyewe, bali kila mtu atafute yale yanayowafaa wengine.

    25 Kuleni chochote kinachouzwa sokoni, bila kuuliza swali lolote kwa ajili ya dhamiri. 26 Kwa maana, “Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana.”

    27 Kama ukikaribishwa chakula na mtu asiyeamini nawe ukikubali kwenda, kula kila kitu kitakachowekwa mbele yako bila kuuliza maswali kwa ajili ya dhamiri. 28 Lakini kama mtu yeyote akikuambia, “Hiki kimetolewa kafara kwa sanamu,” basi usikile kwa ajili ya huyo aliyekuambia na kwa ajili ya dhamiri. 29 Nina maana dhamiri ya huyo aliyekuambia, wala si kwa ajili ya dhamiri yako. Lakini kwa nini uhuru wangu uhukumiwe na dhamiri ya mtu mwingine? 30 Kama nikila kwa shukrani, kwa nini nashutumiwa kwa kile ambacho kwa hicho ninamshukuru Mungu?

    31 Basi, lolote mfanyalo, kama ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu. 32 Msiwe kikwazo kwa mtu yeyote, wawe Wayahudi au Wayunani, au kwa kanisa la Mungu, 33 kama hata mimi ninavyojaribu kumpendeza kila mtu kwa kila namna. Kwa maana sitafuti mema kwa ajili yangu mwenyewe bali kwa ajili ya wengi, ili waweze kuokolewa.

  15. 4 Kwa imani Abeli alimtolea Mungu dhabihu bora zaidi kuliko Kaini. Kwa imani alishuhudiwa kuwa mwenye haki, Mungu mwenyewe akazishuhudia sadaka zake. Kwa imani bado ananena ingawa amekufa.

  16. 16 Wewe hupendezwi na dhabihu, au ningaliileta,

    hufurahii sadaka za kuteketezwa.

    17 Bali dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika,

    moyo uliovunjika wenye toba,

    Ee Mungu, hutaudharau.

  17. 2 Njia zote za mwanadamu huonekana sawa kwake,

    bali Bwana huupima moyo.

    3 Kufanya yaliyo sawa na haki inakubalika

    zaidi kwa Bwana kuliko dhabihu.

  18. 6 Kwa maana nataka rehema, wala si dhabihu,

    kumkubali Mungu zaidi

    kuliko sadaka za kuteketezwa.

  19. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.

  20. 1 Watoto wangu wapendwa, nawaandikia haya ili msitende dhambi. Lakini kama mtu yeyote akitenda dhambi, tunaye Mwombezi kwa Baba: ndiye Yesu Kristo, Mwenye Haki. 2 Yeye ndiye dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu, wala si kwa ajili ya dhambi zetu tu, bali pia kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote.

  21. 7 Ondoeni chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu, kama vile mlivyo. Kwa maana Kristo, Mwana-Kondoo wetu wa Pasaka amekwisha tolewa kuwa dhabihu.

  22. 9 Hivi ndivyo Mungu alivyoonyesha pendo lake kwetu: Mungu alimtuma Mwanawe wa pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kupitia kwake. 10 Hili ndilo pendo: si kwamba tulimpenda Mungu, bali yeye alitupenda, akamtuma Mwanawe, ili yeye awe dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu.

  23. 10 Sikieni neno la Bwana,

    ninyi watawala wa Sodoma;

    sikilizeni sheria ya Mungu wetu,

    enyi watu wa Gomora!

    11 Bwana anasema, “Wingi wa sadaka zenu,

    ni kitu gani kwangu?

    Ninazo sadaka za kuteketezwa nyingi kupita kiasi,

    za kondoo dume na mafuta ya wanyama walionona.

    Sipendezwi na damu za mafahali

    wala za wana-kondoo na mbuzi.

    12 Mnapokuja kujihudhurisha mbele zangu,

    ni nani aliyewataka ninyi mfanye hivyo,

    huku kuzikanyaga nyua zangu?

    13 Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana!

    Uvumba wenu ni chukizo kwangu.

    Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada:

    siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu.

    14 Sikukuu zenu za Miandamo ya Mwezi, na sikukuu zenu zilizoamriwa:

    moyo wangu unazichukia.

    Zimekuwa mzigo kwangu,

    nimechoka kuzivumilia.

  24. 28 Mwalimu mmoja wa sheria akaja, akawasikia wakijadiliana. Akiona kwamba Yesu amewajibu vyema, naye akamuuliza, “Katika amri zote, ni ipi iliyo kuu?”

    29 Yesu akajibu, “Amri iliyo kuu ndiyo hii: ‘Sikia ee Israeli. Bwana Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. 30 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’ 31 Ya pili ndiyo hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.”

    32 Yule mwalimu wa sheria akamwambia Yesu, “Mwalimu, umejibu vyema kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye. 33 Kumpenda Mungu kwa moyo wote na kwa akili zote na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama mtu anavyojipenda mwenyewe ni bora zaidi kuliko kutoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu zote.”

  25. 21 Kwa maana Mungu alimfanya yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu kwake yeye.

  26. 5 Ee Bwana Mungu wangu,

    umefanya mambo mengi ya ajabu.

    Mambo uliyopanga kwa ajili yetu

    hakuna awezaye kukuhesabia;

    kama ningesema na kuyaelezea,

    yangekuwa mengi mno kuyaelezea.

    6 Dhabihu na sadaka hukuvitaka,

    lakini umefungua masikio yangu;

    sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi

    hukuzihitaji.

    7 Ndipo niliposema, “Mimi hapa, nimekuja:

    imeandikwa kunihusu katika kitabu.

    8 Ee Mungu wangu,

    natamani kuyafanya mapenzi yako;

    sheria yako iko ndani ya moyo wangu.”

    9 Nimehubiri haki katika kusanyiko kubwa,

    sikufunga mdomo wangu,

    Ee Bwana, kama ujuavyo.

    10 Sikuficha haki yako moyoni mwangu;

    ninasema juu ya uaminifu wako na wokovu wako.

    Sikuficha upendo wako na kweli yako

    mbele ya kusanyiko kubwa.

    11 Ee Bwana, usizuilie huruma zako,

    upendo wako na kweli yako daima vinilinde.

  27. 12 Lakini Yesu aliposikia hayo, akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, lakini wale walio wagonjwa ndio wanaohitaji tabibu. 13 Nendeni mkajifunze maana ya maneno haya: ‘Nataka rehema, wala si dhabihu.’ Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

  28. 23 Kisha akawaambia wote, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate. 24 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayaokoa.

  29. 1 Kwa maana kila kuhani mkuu anayechaguliwa miongoni mwa wanadamu anawekwa kuwawakilisha kwa mambo yanayomhusu Mungu, ili apate kutoa matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi. 2 Kwa kuwa yeye mwenyewe ni dhaifu, aweza kuwachukulia kwa upole wale wasiojua na kupotoka. 3 Hii ndiyo sababu inampasa kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe na vivyo hivyo kwa ajili ya dhambi za watu. 4 Hakuna anayejitwalia heshima hii mwenyewe; ni lazima aitwe na Mungu, kama vile Aroni alivyoitwa.

  30. 4 Mnapokuja kwake, yeye aliye Jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu bali kwa Mungu ni teule na la thamani kwake, 5 ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mnajengwa kuwa nyumba ya kiroho, ili mpate kuwa ukuhani mtakatifu, mkitoa dhabihu za kiroho zinazokubaliwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.

  31. 3 Mose alipokwenda na kuwaambia watu maneno yote na sheria zote za Bwana, wakaitikia kwa sauti moja, “Kila kitu alichosema Bwana tutakifanya.” 4 Ndipo Mose akaandika kila kitu Bwana alichokuwa amesema.

    Akaamka kesho yake asubuhi na mapema na kujenga madhabahu chini ya mlima na kusimamisha nguzo kumi na mbili za mawe kuwakilisha makabila kumi na mawili ya Israeli. 5 Kisha akawatuma vijana wanaume wa Kiisraeli, nao wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu za mafahali wachanga kuwa sadaka za amani kwa Bwana. 6 Mose akachukua nusu ya damu ya wale wanyama na kuiweka kwenye mabakuli na nusu nyingine akainyunyiza juu ya madhabahu. 7 Kisha akachukua kile Kitabu cha Agano na kuwasomea watu. Nao wakajibu, “Tutafanya kila kitu alichosema Bwana, nasi tutatii.”

    8 Ndipo Mose akachukua ile damu, akawanyunyizia wale watu, akasema, “Hii ni damu ya agano ambalo Bwana amelifanya nanyi kufuatana na maneno haya yote.”

  32. 8 Wakati mletapo dhabihu za wanyama walio vipofu, je, hilo si kosa? Mnapoleta dhabihu zilizo vilema au wanyama wagonjwa, je, hilo si kosa? Jaribuni kuvitoa kwa mtawala wenu! Je, angefurahishwa nanyi? Je, atawakubalia?” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

  33. 6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. 7 Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.

  34. 3 Kwa maana kile ambacho sheria haikuwa na uwezo wa kufanya, kwa vile ilivyokuwa dhaifu katika mwili, Mungu kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe kwa mfano wa mwanadamu mwenye mwili ulio wa dhambi na kwa ajili ya dhambi, yeye aliihukumu dhambi katika mwili, 4 ili kwamba haki ipatikanayo kwa sheria itimizwe ndani yetu sisi, ambao hatuenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho.

    5 Kwa maana wale wanaoishi kwa kuufuata mwili huziweka nia zao katika vitu vya mwili, lakini wale wanaoishi kwa kufuata Roho, huziweka nia zao katika mambo ya Roho. 6 Kwa maana kuwa na nia ya mwili ni mauti, bali kuwa na nia inayoongozwa na Roho ni uzima na amani. 7 Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui na Mungu, kwa maana haiitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. 8 Wale wanaotawaliwa na mwili, hawawezi kumpendeza Mungu.

  35. 17 Kwa sababu mnamwita Baba ahukumuye kila mtu kulingana na matendo yake pasipo upendeleo, enendeni kwa hofu ya kumcha Mungu wakati wenu wa kukaa hapa duniani kama wageni. 18 Kwa maana mnafahamu kwamba mlikombolewa kutoka mwenendo wenu usiofaa ambao mliurithi kutoka kwa baba zenu, si kwa vitu viharibikavyo kama fedha na dhahabu, 19 bali kwa damu ya thamani ya Kristo, yule Mwana-Kondoo asiye na dosari wala doa. 20 Yeye alichaguliwa kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu, lakini akadhihirishwa katika siku hizi za mwisho kwa ajili yenu. 21 Kupitia kwake mmemwamini Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu na akampa utukufu, ili imani yenu na tumaini lenu ziwe kwa Mungu.

  36. 45 Kwa kuwa hata Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”

  37. 29 Siku iliyofuata, Yohana alimwona Yesu akimjia akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu!

  38. 5 Toeni dhabihu zilizo haki;

    mtegemeeni Bwana.

  39. 3 Alidharauliwa na kukataliwa na wanadamu,

    mtu wa huzuni nyingi, ajuaye mateso.

    Kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,

    alidharauliwa, wala hatukumhesabu kuwa kitu.

    4 Hakika alichukua udhaifu wetu

    na akajitwika huzuni zetu,

    hata hivyo tulidhania kuwa amepigwa na Mungu,

    akapigwa sana naye, na kuteswa.

    5 Lakini alitobolewa kwa ajili ya makosa yetu,

    alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu;

    adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake,

    na kwa majeraha yake sisi tumepona.

    6 Sisi sote, kama kondoo, tumepotea,

    kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe,

    naye Bwana aliweka juu yake

    maovu yetu sisi sote.

  40. 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. 11 Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kupitia kwake tumepata upatanisho.

  41. 16 Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Yesu Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu. 17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo? 18 Watoto wapendwa, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli. 19 Basi hivi ndivyo tutakavyoweza kujua ya kuwa sisi tu wa kweli na hivyo twaithibitisha mioyo yetu mbele za Mungu

  42. 37 “Yeyote ampendaye baba yake au mama yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. Yeyote ampendaye mwanawe au binti yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. 38 Tena yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata, hastahili kuwa wangu.

  43. 26 Walipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu.”

    27 Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, “Nyweni nyote katika kikombe hiki. 28 Hii ndiyo damu yangu ya Agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. 29 Lakini ninawaambia, tangu sasa sitakunywa tena katika uzao huu wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya pamoja nanyi katika Ufalme wa Baba yangu.”

  44. 7 Ndani yake tunao ukombozi kwa njia ya damu yake, yaani, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake

  45. 4 Nimewatoa kutoka Misri na kuwakomboa

    kutoka nchi ya utumwa.

    Nilimtuma Mose awaongoze,

    pia Aroni na Miriamu.

    5 Watu wangu, kumbukeni jinsi Balaki mfalme wa Moabu

    alivyofanya shauri

    na kile Balaamu mwana wa Beori alichojibu.

    Kumbukeni safari yenu kutoka Shitimu mpaka Gilgali,

    ili mfahamu matendo ya haki ya Bwana.”

    6 Nimjie Bwana na kitu gani na kusujudu

    mbele za Mungu aliyetukuka?

    Je, nije mbele zake na sadaka za kuteketezwa,

    nije na ndama za mwaka mmoja?

    7 Je, Bwana atafurahishwa na kondoo dume elfu,

    au mito elfu kumi ya mafuta?

    Je, nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa ajili ya kosa langu,

    mtoto wangu mwenyewe

    kwa ajili ya dhambi ya nafsi yangu?

    8 Amekuonyesha yaliyo mema, ee mwanadamu.

    Bwana anataka nini kwako?

    Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema,

    na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.

  46. 24 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 25 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata. 26 Kwa maana, je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?

  47. 6 Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu. 7 Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. 8 Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema.

  48. 5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:

    6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,

    hakuona kule kuwa sawa na Mungu

    kuwa kitu cha kushikilia,

    7 bali alijifanya si kitu,

    akachukua hali hasa na mtumwa,

    naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.

    8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,

    alijinyenyekeza, akatii hata mauti:

    naam, mauti ya msalaba!

  49. 26 Kama tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi. 27 Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao, utakaowaangamiza adui za Mungu. 28 Yeyote aliyeikataa sheria ya Mose alikufa pasipo huruma kwa ushahidi wa watu wawili au watatu. 29 Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani anayostahili kupewa mtu aliyemkanyaga Mwana wa Mungu chini ya nyayo zake, yeye aliyeifanya damu ya Agano iliyomtakasa kuwa kitu najisi na kumtendea maovu Roho wa neema? 30 Kwa kuwa tunamjua yeye aliyesema, “Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza.” Tena asema, “Bwana atawahukumu watu wake.”

  50. 21 “ ‘Usimtoe mtoto wako yeyote awe kafara kwa mungu Moleki, kwani hutalinajisi kamwe jina la Mungu wako. Mimi ndimi Bwana.

  51. 21 “Ninachukia, ninazidharau sikukuu zenu za dini;

    siwezi kuvumilia makusanyiko yenu.

    22 Hata ingawa mnaniletea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za nafaka,

    sitazikubali.

    Ingawa mnaniletea sadaka nzuri za amani,

    sitazitambua.

    23 Niondoleeni kelele za nyimbo zenu!

    Sitasikiliza sauti za vinubi vyenu.

    24 Lakini acheni haki itiririke kama mto,

    na uadilifu uwe kama kijito kisichokauka!

  52. 3 Kama nikitoa mali yote niliyo nayo na kama nikijitolea mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo, hainifaidi kitu.

  53. 14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

  54. 26 Kwa kuwa ilitupasa tuwe na Kuhani Mkuu wa namna hii, yaani, aliye mtakatifu, asiye na lawama, asiye na dosari, aliyetengwa na wenye dhambi na kuinuliwa juu ya mbingu. 27 Yeye hahitaji kutoa dhabihu siku kwa siku kwa ajili ya dhambi, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu kama wale makuhani wakuu wengine. Yeye alitoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zao mara moja tu, alipojitoa mwenyewe. 28 Kwa kuwa sheria huwaweka makuhani wakuu watu ambao ni dhaifu; lakini lile neno la kiapo, lililokuja baada ya sheria, lilimweka Mwana, ambaye amefanywa kuwa mkamilifu milele.

  55. 17 Kwa imani Abrahamu, alipojaribiwa na Mungu, alimtoa Isaki kuwa dhabihu. Yeye aliyekuwa amezipokea ahadi za Mungu alikuwa tayari kumtoa mwanawe, aliyekuwa mwanawe pekee awe dhabihu.