95 Bible Verses About Daughters
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
25 Amevikwa nguvu na heshima,
anaweza kucheka bila kuwa na hofu kwa siku zijazo.
26 Huzungumza kwa hekima
na mafundisho ya kuaminika yapo ulimini mwake.
27 Huangalia mambo ya nyumbani mwake
wala hali chakula cha uvivu.
28 Watoto wake huamka na kumwita aliyebarikiwa,
mumewe pia humsifu, akisema:
29 “Wanawake wengi hufanya vitu vyenye sifa nzuri,
lakini wewe umewapita wote.”
30 Kujipamba ili kuvutia ni udanganyifu na uzuri unapita upesi,
bali mwanamke anayemcha Bwana atasifiwa.
31 Mpe thawabu anayostahili,
nazo kazi zake na zimletee sifa kwenye lango la mji.
-
1 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, kwa kuwa hili ni jema. 2 “Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi, 3 “upate baraka na uishi siku nyingi duniani.”
4 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana.
-
3 Wana ni urithi utokao kwa Bwana,
watoto ni zawadi kutoka kwake.
4 Kama mishale mikononi mwa shujaa
ndivyo walivyo wana awazaao mtu katika ujana wake.
5 Heri mtu ambaye podo lake
limejazwa nao.
Hawataaibishwa wanaposhindana
na adui zao langoni.
-
3 Basi Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase hakuwa na wana waume ila mabinti tu, ambao majina yao yalikuwa Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirsa. 4 Wakamwendea kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi, wakasema: “Bwana alimwagiza Mose atupatie urithi miongoni mwa ndugu zetu.” Kwa hiyo Yoshua akawapa urithi pamoja na ndugu wa baba yao, kufuatana na agizo la Bwana. 5 Fungu la Manase lilikuwa na sehemu kumi za nchi, licha ya Gileadi na Bashani mashariki mwa Yordani, 6 kwa sababu wale binti za kabila la Manase walipokea urithi miongoni mwa wana wa kiume. Nchi ya Gileadi ilikuwa mali ya wazao wa Manase waliobaki.
-
6 Mfundishe mtoto njia impasayo kuiendea,
naye hataiacha hata akiwa mzee.
-
27 Idadi kubwa ya watu wakamfuata Yesu, wakiwamo wanawake waliokuwa wakimlilia na kumwombolezea. 28 Yesu akawageukia, akawaambia, “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi bali jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu. 29 Kwa maana wakati utafika mtakaposema, ‘Wamebarikiwa wanawake tasa, ambao matumbo yao hayakuzaa, wala matiti yao hayakunyonyesha!’
-
1 Watu walipoanza kuongezeka idadi katika uso wa dunia na watoto wa kike wakazaliwa kwao, 2 wana wa Mungu wakawaona kuwa hao binti za wanadamu walikuwa wazuri wa sura, wakaoa yeyote miongoni mwao waliyemchagua. 3 Ndipo Bwana akasema, “Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye ni wa kufa, siku zake zitakuwa miaka 120.”
4 Wanefili walikuwako duniani siku hizo, na baadaye, hao wana wa Mungu walipoingia kwa binti za wanadamu na kuzaa nao. Wanefili walikuwa mashujaa na watu waliojulikana wa zamani hizo.
5 Bwana akaona jinsi uovu wa mwanadamu ulivyokuwa mkubwa duniani, na ya kuwa kila mwelekeo wa mawazo ya moyo wake wakati wote ulikuwa mbaya tu. 6 Bwana akasikitika kwamba alimuumba mwanadamu duniani, moyo wa Mungu ukajaa masikitiko. 7 Kwa hiyo Bwana akasema, “Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemuumba kutoka kwenye uso wa dunia, wanadamu na wanyama, pamoja na viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Kwa maana nasikitika kuwaumba.” 8 Lakini Noa akapata kibali machoni pa Bwana.
-
13 kwa maana mkiishi kwa kuufuata mwili, mtakufa, lakini kama mkiyaua matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. 14 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio watoto wa Mungu. 15 Kwa maana hamkupokea roho ya utumwa iwaleteayo tena hofu, bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambaye kwa yeye twalia, “Abba, yaani, Baba,” 16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kwamba sisi tu watoto wa Mungu. 17 Hivyo, ikiwa sisi ni watoto, basi tu warithi, warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo, naam, tukiteswa pamoja naye tupate pia kutukuzwa pamoja naye.
18 Nayahesabu mateso yetu ya wakati huu kuwa si kitu kulinganisha na utukufu utakaodhihirishwa kwetu. 19 Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu. 20 Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitiisha katika tumaini, 21 ili kwamba viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka kwa utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.
22 Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa maumivu kama utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa.
-
6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.
8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo.
-
1 Kadhalika enyi wake, watiini waume zenu, ili kama kunao wasioamini lile neno, wapate kuvutwa na mwenendo wa wake zao pasipo neno, 2 kwa kuuona utakatifu na uchaji wa Mungu katika maisha yenu. 3 Kujipamba kwenu kusiwe kwa nje tu, kama vile kusuka nywele, kuvalia vitu vilivyofanyizwa kwa dhahabu na kwa mavazi. 4 Badala yake, kujipamba kwenu kuwe katika utu wenu wa moyoni, yaani uzuri usioharibika wa roho ya upole na utulivu, ambayo ni ya thamani sana machoni pa Mungu. 5 Kwa kuwa hivi ndivyo walivyokuwa wakijipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu. Wao walikuwa ni watiifu kwa waume zao, 6 kama Sara alivyomtii mumewe Abrahamu, hata akamwita bwana. Ninyi ni watoto wa Sara kama mkitenda yaliyo mema, bila kuogopa jambo lolote.
-
8 Siku iliyofuata tukaondoka, tukafika Kaisaria. Huko tukaenda nyumbani kwa mwinjilisti mmoja jina lake Filipo, aliyekuwa mmoja wa wale Saba, tukakaa kwake. 9 Filipo alikuwa na binti wanne mabikira waliokuwa wanatoa unabii.
10 Baada ya kukaa kwa siku kadhaa, akateremka nabii mmoja kutoka Uyahudi jina lake Agabo. 11 Alipotufikia akachukua mshipi wa Paulo akajifunga, akautumia kufunga mikono na miguu yake mwenyewe akasema, “Roho Mtakatifu anasema: ‘Hivi ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mwenye mshipi huu na kumkabidhi kwa watu wa Mataifa.’ ”
12 Tuliposikia maneno haya sisi na ndugu wengine tukamsihi Paulo asiende Yerusalemu. 13 Lakini Paulo akajibu, “Kwa nini mnalia na kunivunja moyo? Mimi niko tayari si kufungwa tu, bali hata kufa huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Yesu.” 14 Alipokuwa hashawishiki, tukaacha kumsihi, tukasema, “Mapenzi ya Bwana na yatendeke.”
-
9 Enyi wanawake wenye kuridhika sana,
amkeni na mnisikilize.
Enyi binti mnaojisikia kuwa salama,
sikieni lile ninalotaka kuwaambia!
10 Muda zaidi kidogo ya mwaka mmoja,
ninyi mnaojisikia salama mtatetemeka,
mavuno ya zabibu yatakoma
na mavuno ya matunda hayatakuwepo.
11 Tetemekeni, enyi wanawake wenye kuridhika,
tetemekeni kwa hofu, enyi binti mnaojisikia salama!
Vueni nguo zenu,
vaeni nguo ya gunia viunoni mwenu.
-
18 “Mimi nitakuwa Baba kwenu,
nanyi mtakuwa wanangu na binti zangu,
asema Bwana Mwenyezi.”
-
13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
-
29 Wazao wa Manase:
kutoka kwa Makiri, ukoo wa Wamakiri (Makiri alikuwa baba wa Gileadi);
kutoka kwa Gileadi, ukoo wa Wagileadi.
30 Hawa ndio waliokuwa wazao wa Gileadi:
kutoka kwa Iezeri, ukoo wa Waiezeri;
kutoka kwa Heleki, ukoo wa Waheleki;
31 kutoka kwa Asirieli, ukoo wa Waasirieli;
kutoka kwa Shekemu, ukoo wa Washekemu;
32 kutoka kwa Shemida, ukoo wa Washemida;
kutoka kwa Heferi, ukoo wa Waheferi.
33 (Selofehadi mwana wa Heferi hakuzaa wana, bali alikuwa na watoto wa kike tu, ambao majina yao yalikuwa Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirsa.)
34 Hizi ndizo zilizokuwa koo za Manase; wale waliohesabiwa walikuwa 52,700.
-
1 Binti za Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, walikuwa wa koo za Manase mwana wa Yosefu. Majina ya hao binti yalikuwa Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirsa. Walikaribia 2 ingilio la Hema la Kukutania na kusimama mbele ya Mose, kuhani Eleazari, viongozi na kusanyiko lote, wakasema, 3 “Baba yetu alikufa jangwani. Hakuwa miongoni mwa wafuasi wa Kora, ambao walifungamana pamoja dhidi ya Bwana, lakini alikufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe na hakuacha wana. 4 Kwa nini jina la baba yetu lifutike kutoka ukoo wake kwa sababu hakuwa na mwana? Tupatie milki miongoni mwa ndugu za baba yetu.”
5 Kwa hiyo Mose akalileta shauri lao mbele za Bwana, 6 naye Bwana akamwambia Mose, 7 “Wanachosema binti za Selofehadi ni sawa. Ni lazima kwa hakika uwape milki kama urithi miongoni mwa ndugu za baba yao, na kubadili urithi wa baba yao uwe wao.
8 “Waambie Waisraeli, ‘Ikiwa mtu atakufa naye hakuacha mwana, utampa binti yake urithi wake. 9 Ikiwa hana binti, wape ndugu zake wa kiume urithi wake. 10 Ikiwa hana ndugu wa kiume toa urithi wake kwa ndugu za baba yake. 11 Ikiwa baba yake hakuwa na ndugu wa kiume, toa urithi wake kwa ndugu wa karibu katika ukoo wake, ili aumiliki. Hili litakuwa dai la sheria kwa Waisraeli, kama Bwana alivyomwamuru Mose.’ ”
-
13 Tena alikuwa na wana saba na binti watatu. 14 Binti wa kwanza aliitwa Yemima, wa pili Kesia na wa tatu Keren-Hapuki. 15 Hapakuwepo mahali popote katika nchi ile yote palipopatikana wanawake wazuri kama binti za Ayubu; naye baba yao akawapa urithi pamoja na ndugu zao.
-
4 Sina furaha kubwa kuliko hii, kusikia kwamba watoto wangu wanaenenda katika kweli.
-
9 Baada ya hayo, watu wa Yuda wakateremka kupigana na Wakanaani walioishi katika nchi ya vilima, yaani, Negebu na nchi chini ya vilima vya magharibi. 10 Yuda wakakabiliana na Wakanaani walioishi Hebroni (ambayo hapo kwanza iliitwa Kiriath-Arba) na kuwashinda Sheshai, Ahimani na Talmai.
11 Kutoka huko wakasonga mbele kukabiliana na watu walioishi Debiri (ambao hapo kwanza uliitwa Kiriath-Seferi.) 12 Kalebu akasema, “Nitamwoza binti yangu Aksa kwa mtu atakayeweza kupigana na kuteka Kiriath-Seferi.” 13 Basi Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa huyo Kalebu, akawashinda, kwa hiyo Kalebu akamtoa binti yake Aksa akaolewa naye.
14 Siku moja Aksa alipokuja kwa Othnieli, alimsihi Othnieli amwombe baba yake, Kalebu, shamba. Aksa aliposhuka kutoka juu ya punda wake, Kalebu akamuuliza, “Je, wataka nikufanyie nini?”
15 Akamjibu, “Naomba unifanyie jambo moja la hisani. Kwa kuwa umenipa ardhi huko Negebu, nipe pia chemchemi za maji.” Ndipo Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini.
-
22 Msikilize baba yako, aliyekuzaa,
wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee.
23 Nunua kweli wala usiiuze,
pata hekima, adabu na ufahamu.
24 Baba wa mwenye haki ana furaha kubwa,
naye aliye na mwana mwenye hekima humfurahia.
25 Baba yako na mama yako na wafurahi,
mama aliyekuzaa na ashangilie!
-
12 Alisema, “Usizidi kufurahi,
ee Bikira Binti Sidoni, sasa umepondwa!
“Simama, vuka uende Kitimu;
hata huko hutapata pumziko.”
-
20 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote, kwa maana hivi ndivyo inavyompendeza Bwana.
21 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.
-
12 Waheshimu baba yako na mama yako, ili upate kuishi siku nyingi katika nchi anayokupa Bwana Mungu wako.
-
16 Kalebu akasema, “Nitamwoza binti yangu Aksa kwa mtu atakayeweza kupigana na kuteka Kiriath-Seferi.” 17 Basi Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu yake Kalebu, akauteka; hivyo Kalebu akamtoa Aksa binti yake aolewe naye.
18 Siku moja Aksa alipokuja kwa Othnieli, alimsihi Othnieli amwombe baba yake, Kalebu, shamba. Aksa aliposhuka kutoka juu ya punda wake, Kalebu akamuuliza, “Je, wataka nikufanyie nini?”
19 Akamjibu, “Naomba unifanyie jambo moja la hisani. Kwa kuwa umenipa ardhi huko Negebu, nipe pia chemchemi za maji.” Basi Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini.
-
28 “Hata itakuwa, baada ya hayo,
nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili.
Wana wenu na binti zenu watatabiri,
wazee wenu wataota ndoto,
na vijana wenu wataona maono.
29 Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake,
katika siku zile nitamimina Roho wangu.
-
14 Imba, ee Binti Sayuni;
paza sauti, ee Israeli!
Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote,
ee Binti Yerusalemu!
15 Bwana amekuondolea adhabu yako,
amewarudisha nyuma adui zako.
Bwana, Mfalme wa Israeli, yu pamoja nawe;
kamwe hutaogopa tena madhara yoyote.
16 Katika siku hiyo watauambia Yerusalemu,
“Usiogope, ee Sayuni;
usiiache mikono yako ilegee.
17 Bwana Mungu wako yu pamoja nawe,
yeye ni mwenye nguvu kuokoa.
Atakufurahia kwa furaha kubwa,
atakutuliza kwa pendo lake,
atakufurahia kwa kuimba.”
18 “Huzuni katika sikukuu zilizoamriwa
nitaziondoa kwenu;
hizo ni mzigo na fedheha kwenu.
19 Wakati huo nitawashughulikia
wote waliokudhulumu;
nitaokoa vilema na kukusanya
wale ambao wametawanywa.
Nitawapa sifa na heshima
katika kila nchi ambayo waliaibishwa.
-
25 Hapo palikuwa na mwanamke aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na miwili. 26 Mwanamke huyu alikuwa ameteseka sana kwa mikono ya matabibu wengi, na kutumia kila kitu alichokuwa nacho. Lakini badala ya kupona, hali yake ilizidi kuwa mbaya. 27 Alikuwa amesikia habari za Yesu, naye akaja kwa nyuma yake kwenye umati wa watu, akaligusa vazi lake, 28 kwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikiweza kuligusa vazi lake tu, nitaponywa.” 29 Mara kutoka damu kwake kukakoma, naye akajisikia mwilini mwake amepona kabisa.
30 Ghafula Yesu akatambua kuwa nguvu zimemtoka. Akaugeukia ule umati wa watu na kuuliza, “Ni nani aliyegusa mavazi yangu?”
31 Wanafunzi wake wakamjibu, “Unaona jinsi umati wa watu unavyokusonga. Wawezaje kuuliza, ‘Ni nani aliyenigusa?’ ”
32 Lakini Yesu akaangalia pande zote ili aone ni nani aliyemgusa. 33 Yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni pake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote. 34 Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”
35 Alipokuwa bado anaongea, watu wakafika kutoka nyumbani kwa Yairo. Wakamwambia, “Binti yako amekufa. Kwa nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?”
36 Aliposikia hayo waliyosema, Yesu akamwambia huyo kiongozi wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”
37 Hakumruhusu mtu mwingine yeyote amfuate isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, nduguye Yakobo. 38 Walipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi, Yesu akaona ghasia, watu wakilia na kuomboleza kwa sauti kubwa. 39 Alipokwisha kuingia ndani, akawaambia, “Kwa nini mnafanya ghasia na kulia? Mtoto hajafa, bali amelala tu.” 40 Wale watu wakamcheka kwa dharau.
Lakini yeye akawatoa wote nje, akawachukua baba na mama wa yule mtoto, pamoja na wale wanafunzi aliokuwa nao. Wakaingia ndani mpaka pale alipokuwa yule mtoto. 41 Akamshika mtoto mkono, akamwambia, “Talitha koum!” (maana yake ni, “Msichana, nakuambia: amka!”) 42 Mara yule msichana akasimama, akaanza kutembea (alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili). Walipoona haya, wakastaajabu sana. 43 Yesu akawaagiza kwa ukali wasimweleze mtu yeyote jambo hilo, naye akawaambia wampe yule msichana chakula.
-
53 Watafarakana baba dhidi ya mwanawe na mwana dhidi ya babaye, mama dhidi ya bintiye na binti dhidi ya mamaye, naye mama mkwe dhidi ya mkwewe na mkwe dhidi ya mama mkwe wake.”
-
24 “ ‘ “Bwana akubariki
na kukulinda;
25 Bwana akuangazie nuru ya uso wake
na kukufadhili;
26 Bwana akugeuzie uso wake
na kukupa amani.” ’
-
3 Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe;
vifunge shingoni mwako,
viandike katika ubao wa moyo wako.
4 Ndipo utapata kibali na jina zuri
mbele za Mungu na mwanadamu.
5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote
wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6 katika njia zako zote mkiri yeye,
naye atayanyoosha mapito yako.
-
8 “Sema kwa ajili ya wale wasioweza kujisemea,
kwa ajili ya haki za wote walioachwa ukiwa.
9 Sema na uamue kwa haki,
tetea haki za maskini na wahitaji.”
10 Mke mwenye sifa nzuri, ni nani awezaye kumpata?
Yeye ni wa thamani sana kuliko marijani.
11 Mume wake anamwamini kikamilifu
wala hakosi kitu chochote cha thamani.
12 Humtendea mumewe mema, wala si mabaya,
siku zote za maisha yake.
-
44 “ ‘Kila mtu atumiaye maneno ya mithali hii, atayatumia juu yako: “Alivyo mama, ndivyo alivyo bintiye.” 45 Wewe ni binti halisi wa mama yako, ambaye alimchukia kabisa mume wake na watoto wake, tena wewe ni dada halisi wa dada zako, waliowachukia kabisa waume zao na watoto wao. Mama yako alikuwa Mhiti na baba yako alikuwa Mwamori. 46 Dada yako mkubwa alikuwa Samaria, aliyeishi upande wako wa kaskazini na binti zake, pamoja na dada yake, naye dada yako mdogo, aliyeishi kusini yako pamoja na binti zake, alikuwa Sodoma.
-
9 Shangilia sana, ee Binti Sayuni!
Piga kelele, Binti Yerusalemu!
Tazama, Mfalme wako anakuja kwako,
ni mwenye haki, naye ana wokovu,
ni mpole, naye amepanda punda,
mwana-punda, mtoto wa punda.
10 Nitaondoa magari ya vita kutoka Efraimu
na farasi wa vita kutoka Yerusalemu,
nao upinde wa vita utavunjwa.
Atatangaza amani kwa mataifa.
Utawala wake utaenea kutoka bahari hadi bahari,
na kutoka Mto Frati hadi mwisho wa dunia.
-
22 Yesu akageuka, naye alipomwona akamwambia, “Binti, jipe moyo mkuu, imani yako imekuponya.” Naye yule mwanamke akapona kuanzia saa ile ile.
23 Yesu alipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi na kuwaona waombolezaji wakipiga filimbi za maombolezo na watu wengi wakipiga kelele, 24 akawaambia, “Ondokeni! Kwa maana binti huyu hakufa, bali amelala.” Wakamcheka kwa dhihaka. 25 Lakini watu walipokwisha kutolewa nje, akaingia mle ndani na kumshika yule binti mkono, naye akaamka. 26 Habari hizi zikaenea katika maeneo yale yote.
-
4 Haya yalitukia ili litimie lile lililonenwa na nabii, akisema:
5 “Mwambieni Binti Sayuni,
‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako,
ni mnyenyekevu, naye amepanda punda,
juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’ ”
6 Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama Yesu alivyokuwa amewaagiza.
-
7 Vumilieni taabu kwa ajili ya kufunzwa adabu. Mungu anawatendea ninyi kama watoto wake, kwa maana ni mtoto yupi asiyeadibishwa na mzazi wake? 8 Kama hakuna kuadibishwa (ambalo ni fungu la watoto wote), basi ninyi ni watoto wa haramu wala si watoto halali. 9 Tena, sisi sote tunao baba wa kimwili, waliotuadibisha nasi tukawaheshimu kwa ajili ya hilo. Je, si inatupasa kujinyenyekeza zaidi kwa Baba wa roho zetu ili tuishi? 10 Baba zetu walituadibisha kwa kitambo kidogo kama wao wenyewe walivyoona vyema, lakini Mungu hutuadibisha kwa faida yetu ili tupate kushiriki utakatifu wake. 11 Kuadibishwa wakati wowote hakuonekani kuwa kitu cha kufurahisha bali chenye maumivu kinapotekelezwa. Lakini baadaye huzaa matunda ya haki na amani kwa wale waliofunzwa nayo.
-
13 Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani;
uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu.
14 Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa
kwa namna ya ajabu na ya kutisha;
kazi zako ni za ajabu,
ninajua hayo kikamilifu.
15 Umbile langu halikufichika kwako,
nilipoumbwa mahali pa siri.
Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi,
16 macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika.
Siku zangu zote ulizonipangia
ziliandikwa katika kitabu chako
kabla haijakuwepo hata moja.
-
27 Asubuhi na mapema siku iliyofuata, Abrahamu akaamka na kurudi mahali pale aliposimama mbele za Bwana. 28 Akatazama upande wa Sodoma na Gomora, kuelekea nchi yote ya tambarare, akaona moshi mzito ukipanda kutoka kwenye nchi, kama moshi utokao kwenye tanuru.
29 Kwa hiyo Mungu alipoiangamiza miji ya tambarare alimkumbuka Abrahamu, akamtoa Loti kutoka kwenye lile janga lililoharibu miji ile ambamo Loti alikuwa ameishi.
30 Loti na binti zake wawili waliondoka Soari na kufanya makao yao kule milimani, kwa maana aliogopa kukaa Soari. Yeye na binti zake wawili waliishi katika pango. 31 Siku moja binti mkubwa akamwambia yule mdogo, “Baba yetu ni mzee na hakuna mwanaume mahali hapa atakayekutana na sisi kimwili, kama ilivyo desturi ya mahali pote duniani. 32 Tumnyweshe baba yetu mvinyo kisha tukutane naye kimwili ili tuhifadhi uzao wetu kupitia baba yetu.”
33 Usiku ule walimnywesha baba yao mvinyo, alipolewa binti yake mkubwa akaingia na kukutana naye kimwili. Baba yao hakujua wakati binti yake alipoingia kulala naye wala alipotoka.
34 Siku iliyofuata binti mkubwa akamwambia yule mdogo, “Usiku uliopita mimi nilikutana kimwili na baba yangu. Tumnyweshe divai tena, usiku huu nawe ukutane naye kimwili ili tuweze kuhifadhi uzao wetu kupitia baba yetu.” 35 Kwa hiyo wakamnywesha baba yao mvinyo tena usiku ule, naye binti yake mdogo akaingia, akakutana naye kimwili. Kwa mara nyingine baba yao hakujua binti yake alipolala naye wala alipoondoka.
36 Hivyo binti wawili wa Loti wakapata mimba kwa baba yao. 37 Binti mkubwa akamzaa mwana, akamwita jina lake Moabu; ndio baba wa Wamoabu hata leo. 38 Binti mdogo naye pia akamzaa mwana, naye akamwita Benami; ndiye baba wa Waamoni hata leo.
-
8 Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako,
wala usiyaache mafundisho ya mama yako.
9 Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako,
na mkufu wa kuipamba shingo yako.
-
17 Mrudi mwanao, naye atakupa amani,
atakufurahisha nafsi yako.
-
13 Watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wake wakawakemea. 14 Yesu alipoona yaliyokuwa yakitukia, akachukizwa. Akawaambia wanafunzi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa. 15 Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.” 16 Akawachukua watoto mikononi mwake, akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.
-
21 Mwanamke anapokuwa na utungu wa kuzaa huwa na maumivu kwa sababu saa yake imewadia. Lakini mtoto akiisha kuzaliwa, yule mwanamke husahau maumivu hayo kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtoto ulimwenguni. 22 Hivyo ninyi mna maumivu sasa, lakini nitawaona tena, nayo mioyo yenu itafurahi na furaha yenu hakuna awaondoleaye.
-
12 Wale watu wawili wakamwambia Loti, “Una mtu mwingine yeyote hapa, wakwe zako, wana au binti, ama yeyote mwingine aliye wako katika mji huu? Waondoe hapa, 13 kwa sababu tunapaangamiza mahali hapa. Kilio kwa Bwana dhidi ya watu wa hapa ni kikubwa kiasi kwamba ametutuma kupaangamiza.”
-
8 Lakini Hamori akawaambia, “Moyo wa mwanangu Shekemu umeelekea kwa binti yenu. Tafadhali mpeni awe mke wake. 9 Oaneni na sisi, tupeni binti zenu, nanyi mchukue binti zetu. 10 Mwaweza kuishi katikati yetu, nchi ni wazi kwenu. Ishini ndani yake, fanyeni biashara humu na mjipatie mali.”
-
9 “ ‘Ikiwa binti wa kuhani anajitia unajisi kwa kufanya ukahaba, anamwaibisha baba yake; lazima achomwe kwa moto.
-
3 “Wakati mwanamwali anayeishi bado nyumbani kwa baba yake atakapoweka nadhiri kwa Bwana, ama amejifunga mwenyewe kwa ahadi, 4 na baba yake akasikia kuhusu nadhiri au ahadi yake lakini asimwambie lolote, ndipo nadhiri zake zote na kila ahadi aliyoiweka na kujifunga kwayo itathibitika. 5 Lakini kama baba yake akimkataza wakati anapoisikia, hakuna nadhiri wala ahadi yake yoyote aliyojifunga kwayo itakayosimama; Bwana atamweka huru huyo mwanamwali kwa sababu baba yake amemkataza.
-
6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. 7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo.
-
14 Wanawake wakamwambia Naomi: “Ahimidiwe Bwana, asiyekuacha bila kuwa na jamaa wa karibu wa kukomboa. Na awe mashuhuri katika Israeli yote! 15 Atakurejeshea uhai wako na kukuangalia katika siku za uzee wako. Kwa maana mkweo ambaye anakupenda, na ambaye kwako ni bora zaidi ya watoto wa kiume saba, ndiye alimzaa.”
-
11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo.
-
10 “Angalia ili usimdharau mmojawapo wa hawa wadogo, kwa maana nawaambia, malaika wao mbinguni daima wanauona uso wa Baba yangu aliye mbinguni. [ 11 Kwa maana Mwana wa Adamu alikuja kuokoa kile kilichopotea.]
12 “Mwaonaje? Ikiwa mtu ana kondoo mia moja, na mmoja wao akapotea, je, hatawaacha wale tisini na tisa vilimani na kwenda kumtafuta huyo mmoja aliyepotea? 13 Naye akishampata, amin, nawaambia, hufurahi zaidi kwa ajili ya huyo kondoo mmoja kuliko wale tisini na tisa ambao hawakupotea. 14 Vivyo hivyo, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmojawapo wa hawa wadogo apotee.
-
17 “ ‘Katika siku za mwisho, asema Mungu,
nitamimina Roho wangu
juu ya wote wenye mwili.
Wana wenu na binti zenu watatabiri,
vijana wenu wataona maono,
na wazee wenu wataota ndoto.
-
1 Usimkemee mzee kwa ukali bali umshawishi kama vile angekuwa ni baba yako. Uwatendee vijana kama vile ndugu zako; 2 nao wanawake wazee uwatendee kama mama zako, na wanawake vijana kama dada zako, katika usafi wote.
-
5 Basi katika mji wa ngome ya Shushani palikuwa na Myahudi wa kabila ya Benyamini, jina lake Mordekai mwana wa Yairi, mwana wa Shimei, mwana wa Kishi, 6 ambao walichukuliwa uhamishoni kutoka Yerusalemu na Mfalme Nebukadneza wa Babeli, wakiwa miongoni mwa waliochukuliwa mateka pamoja na Mfalme Yekonia wa Yuda. 7 Mordekai alikuwa na binamu yake msichana aliyeitwa Hadasa, ambaye alimlea kwa kuwa hakuwa na baba wala mama. Msichana huyu, ambaye pia alijulikana kwa jina la Esta, alikuwa na umbo na sura ya kupendeza, naye Mordekai alimtunza kama binti yake mwenyewe baada ya baba yake na mama yake kufariki.
8 Wakati agizo na amri ya mfalme lilitangazwa, wanawali wengi waliletwa kwenye ngome ya mji wa Shushani na kuwekwa chini ya uangalizi wa Hegai. Pia Esta alipelekwa katika jumba la mfalme na akakabidhiwa Hegai, aliyekuwa mkuu wa nyumba ya wanawake. 9 Msichana huyu alimpendeza na kupata kibali mbele zake. Mara moja akaanza kumpa matunzo ya uzuri na chakula maalum. Alimpa Esta vijakazi saba waliochaguliwa kutoka jumba la kifalme, na kumhamishia yeye pamoja na vijakazi wake katika sehemu bora zaidi katika nyumba ya wanawake.
10 Esta alikuwa hajadhihirisha uraia wala kabila lake, kwa sababu Mordekai alikuwa amemkataza. 11 Kila siku Mordekai alikuwa akitembeatembea karibu na ua wa nyumba ya wanawake kujua Esta alivyoendelea na kuona yaliyokuwa yakitendeka kwake.
-
34 “Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga. 35 Kwa maana nimekuja kumfitini
“ ‘mtu na babaye,
binti na mamaye,
mkwe na mama mkwe wake;
36 nao adui za mtu watakuwa
ni wale watu wa nyumbani kwake.’
-
1 Wakati huo, wanafunzi wakamjia Yesu na kumuuliza, “Je, nani aliye mkuu kuliko wote katika Ufalme wa Mbinguni?”
2 Yesu akamwita mtoto mdogo na kumsimamisha katikati yao. 3 Naye akasema: “Amin, nawaambia, msipookoka na kuwa kama watoto wadogo, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni. 4 Kwa hiyo mtu yeyote anyenyekeaye kama huyu mtoto, ndiye aliye mkuu kuliko wote katika Ufalme wa Mbinguni.
5 “Yeyote amkaribishaye mtoto mdogo kama huyu kwa Jina langu, anikaribisha mimi. 6 Lakini kama mtu yeyote akimsababisha mmojawapo wa hawa wadogo wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa katika kilindi cha bahari.
7 “Ole kwa ulimwengu kwa sababu ya yale mambo yanayosababisha watu kutenda dhambi! Mambo hayo lazima yawepo, lakini ole wake mtu yule ambaye huyasababisha.
-
40 Basi Yesu aliporudi, umati mkubwa wa watu ukampokea kwa furaha, kwani walikuwa wakimngojea. 41 Kisha mtu mmoja, jina lake Yairo, aliyekuwa kiongozi wa sinagogi, akaja na kuanguka miguuni mwa Yesu, akimwomba afike nyumbani kwake, 42 kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa anakufa.
Yesu alipokuwa akienda, umati wa watu ukamsonga sana. 43 Katika umati huo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa na tatizo la kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Tena alikuwa amegharimia yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya matibabu, wala hakuna yeyote aliyeweza kumponya. 44 Huyo mwanamke akaja kwa nyuma ya Yesu na kugusa upindo wa vazi lake. Mara kutokwa damu kwake kukakoma.
45 Yesu akauliza, “Ni nani aliyenigusa?”
Watu wote walipokana, Petro akasema, “Bwana, huu umati wa watu unakusonga na kukusukuma kila upande.”
46 Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, kwa maana nimetambua kuwa nguvu zimenitoka.”
47 Yule mwanamke alipofahamu ya kuwa hawezi kuendelea kujificha, alikuja akitetemeka, akaanguka miguuni mwa Yesu. Akaeleza mbele ya watu wote kwa nini alimgusa na jinsi alivyoponywa mara. 48 Basi Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.”
49 Yesu alipokuwa bado anasema, akaja mtumishi kutoka nyumbani kwa Yairo, yule kiongozi wa sinagogi, kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Usiendelee kumsumbua Mwalimu.”
50 Yesu aliposikia jambo hili, akamwambia Yairo, “Usiogope. Amini tu, naye binti yako atapona.”
51 Walipofika nyumbani kwa Yairo, hakumruhusu mtu yeyote aingie ndani naye isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, pamoja na baba na mama wa yule binti. 52 Wakati ule ule watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili ya huyo binti. Yesu akawaambia, “Acheni kulia. Huyu binti hajafa, ila amelala.”
53 Wao wakamcheka kwa dharau, wakijua kuwa amekwisha kufa. 54 Yesu akamshika yule binti mkono na kuita, “Binti, amka!” 55 Roho yake ikamrudia, naye akainuka mara moja. Akaamuru apewe kitu cha kula. 56 Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote juu ya yale yaliyotukia.
-
10 Basi Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo siku ya Sabato. 11 Wakati huo huo akaja mwanamke mmoja aliyekuwa na pepo mchafu, naye alikuwa amepinda mgongo kwa muda wa miaka kumi na minane, wala alikuwa hawezi kunyooka wima. 12 Yesu alipomwona, akamwita, akamwambia, “Mwanamke, uwe huru, umepona ugonjwa wako.” 13 Yesu alipomwekea mikono yake, mara akasimama wima akaanza kumtukuza Mungu.
14 Lakini kiongozi wa sinagogi akakasirika kwa sababu Yesu alikuwa ameponya mtu siku ya Sabato. Akaambia ule umati wa watu, “Kuna siku sita ambazo watu wanapaswa kufanya kazi. Katika siku hizo, njooni mponywe, lakini si katika siku ya Sabato.”
15 Lakini Bwana akamjibu, “Enyi wanafiki! Je, kila mmoja wenu hamfungulii ngʼombe wake au punda wake kutoka zizini akampeleka kumnywesha maji siku ya Sabato? 16 Je, huyu mwanamke, ambaye ni binti wa Abrahamu, aliyeteswa na Shetani akiwa amemfunga kwa miaka yote hii kumi na minane, hakustahili kufunguliwa kutoka kifungo hicho siku ya Sabato?”
17 Aliposema haya, wapinzani wake wakaaibika, lakini watu wakafurahi kwa ajili ya mambo ya ajabu aliyoyafanya.
-
15 Pia, watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wachanga ili awaguse. Wanafunzi wake walipoona hivyo, wakawakemea. 16 Lakini Yesu akawaita wale watoto waje kwake, akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa. 17 Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”
-
1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.
-
3 Ninamshukuru Mungu, ninayemtumikia kwa dhamiri safi, kama walivyofanya baba zangu, ninapokukumbuka usiku na mchana katika maombi yangu. 4 Nikiyakumbuka machozi yako, ninatamani sana kukuona ili nipate kujawa na furaha. 5 Nimekuwa nikiikumbuka imani yako ya kweli, waliokuwa nayo bibi yako Loisi na mama yako Eunike na ambayo mimi ninasadiki sasa wewe pia unayo.
-
17 Kila kitolewacho kilicho chema na kilicho kamili, hutoka juu, na hushuka kutoka kwa Baba wa mianga, ambaye kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka. 18 Kwa mapenzi yake mwenyewe alituzaa kwa neno la kweli, kusudi tuwe kama mazao ya kwanza katika viumbe vyake vyote.
-
6 Loti akatoka nje kuonana nao, akaufunga mlango nyuma yake, 7 akasema, “La hasha, rafiki zangu. Msifanye jambo hili ovu. 8 Tazama, ninao binti wawili ambao kamwe hawajakutana kimwili na mwanaume. Acha niwatoe nje kwenu, nanyi mnaweza kuwafanyia lolote mnalotaka. Lakini msiwafanyie chochote watu hawa, kwa sababu wako kwenye ulinzi chini ya dari langu.”
-
21 Ndipo Yakobo akamwambia Labani, “Nipe mke wangu. Muda wangu umekamilika, nami nataka nikutane naye kimwili.”
22 Basi Labani akaalika watu wote wa mahali pale na akafanya karamu.
23 Lakini ilipofika jioni, akamchukua Lea binti yake akampa Yakobo, naye Yakobo akakutana naye kimwili. 24 Naye Labani akamtoa Zilpa, mtumishi wake wa kike, kuwa mtumishi wa Lea, binti yake.
25 Kesho yake asubuhi, Yakobo akagundua kuwa amepewa Lea! Basi Yakobo akamwambia Labani, “Ni jambo gani hili ulilonitendea? Nilikutumikia kwa ajili ya Raheli, sivyo? Kwa nini umenidanganya?”
26 Labani akajibu, “Si desturi yetu kumwoza binti mdogo kabla ya kumwoza binti mkubwa. 27 Maliza juma la arusi ya binti huyu, kisha pia nitakupa huyu binti mdogo, kwa kutumika miaka mingine saba.”
28 Naye Yakobo akafanya hivyo. Akamaliza juma na Lea, kisha Labani akampa Raheli binti yake kuwa mke wake. 29 Labani akamtoa Bilha mtumishi wake wa kike kwa Raheli ili kuwa mtumishi wake. 30 Pia Yakobo akakutana na Raheli kimwili, naye akampenda Raheli zaidi kuliko Lea. Yakobo akamtumikia Labani kwa miaka mingine saba.
-
15 “ ‘Usikutane kimwili na mkwe wako, yeye ni mke wa mwanao; usiwe na mahusiano kama hayo naye.
-
10 Akamwambia, “Binti yangu, ubarikiwe na Bwana. Wema huu wa sasa ni mkuu kushinda hata ule ulioonyesha mwanzoni. Hukuwakimbilia vijana, wakiwa matajiri au maskini. 11 Sasa, binti yangu, usiogope. Nitakufanyia yote uliyoomba. Kwa maana mji wote wa watu wangu wanakujua ya kwamba wewe ni mwanamke mwenye tabia nzuri. 12 Ingawa ni kweli kwamba mimi ndiye jamaa aliye karibu, bado kuna mtu mwingine wa jamaa aliye karibu zaidi wa kukomboa kuliko mimi.
-
17 Sauli akamwambia Daudi, “Huyu hapa binti yangu mkubwa Merabu. Nitakupa umwoe, endapo tu utanitumikia kwa ushujaa na kupigana vita vya Bwana.” Kwa maana Sauli alisema moyoni mwake, “Sitainua mkono wangu dhidi yake. Acha mkono wa Wafilisti uwe juu yake.”
18 Lakini Daudi akamwambia Sauli, “Mimi ni nani, nayo jamaa yangu ni nini au ukoo wa baba yangu katika Israeli, kwamba mimi niwe mkwewe mfalme?” 19 Basi ulipofika wakati wa Daudi kupewa Merabu, binti Sauli, huyo binti aliozwa kwa Adrieli, Mmeholathi.
20 Basi Mikali binti Sauli alimpenda Daudi, nao walipomwambia Sauli juu ya jambo hili, likampendeza. 21 Sauli akawaza, “Nitampa Daudi binti yangu, ili apate kuwa mtego kwake, ili kwamba mkono wa Wafilisti upate kuwa juu yake.” Hivyo Sauli akamwambia Daudi, “Sasa unayo nafasi ya pili ya kuwa mkwe wangu.”
-
1 Solomoni akafanya urafiki na Mfalme Farao wa Misri na kumwoa binti yake. Akamleta huyo binti katika Mji wa Daudi mpaka alipomaliza kujenga jumba lake la kifalme na Hekalu la Bwana, pamoja na ukuta kuzunguka Yerusalemu.
-
37 “Yeyote ampendaye baba yake au mama yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. Yeyote ampendaye mwanawe au binti yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu.
-
15 “Usiogope, Ewe binti Sayuni;
tazama, Mfalme wako anakuja,
amepanda mwana-punda!”
-
14 Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani, 15 na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. 16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, 17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.
-
1 Inakupasa kufundisha itikadi sahihi. 2 Wafundishe wazee kuwa na kiasi, wastahivu, wenye busara na wanyofu katika imani, upendo na saburi.
3 Vivyo hivyo, wafundishe wanawake wazee kuwa na mwenendo wa utakatifu, wala wasiwe wasingiziaji au walevi, bali wafundishe yale yaliyo mema, 4 ili waweze kuwafundisha wanawake vijana kuwa na kiasi, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao, 5 wawe waaminifu, watakatifu, wakitunza vyema nyumba zao, wema, watiifu kwa waume zao, ili mtu yeyote asije akalikufuru neno la Mungu.
-
6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.
8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza. 9 Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.
10 Nanyi mkiisha kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Kristo, yeye mwenyewe atawarejesha na kuwatia nguvu, akiwaimarisha na kuwathibitisha. 11 Uweza una yeye milele na milele. Amen.
-
3 Ninataka uape kwa Bwana, Mungu wa mbingu na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke kutoka binti za Wakanaani, ambao ninaishi miongoni mwao,
-
12 “ ‘Ikiwa mtu atakutana kimwili na mke wa mwanawe, lazima wote wawili wauawe. Walichokifanya ni upotovu; damu yao itakuwa juu ya vichwa vyao wenyewe.
-
15 Lakini msipoona vyema kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia, kama ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ngʼambo Frati, au miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Bwana.”
-
29 Ndipo Roho wa Bwana akaja juu ya Yefta. Akapita katikati ya Gileadi na Manase, pia akapita katika Mispa ya Gileadi, na kutokea huko akasonga mbele kushambulia Waamoni. 30 Naye Yefta akaweka nadhiri mbele za Bwana akisema, “Ikiwa utawatia Waamoni mikononi mwangu, 31 chochote kile kitakachotoka katika mlango wa nyumba yangu cha kwanza ili kunilaki nirudipo kwa amani katika kuwashinda Waamoni, kitakuwa ni cha Bwana na nitakitoa kuwa sadaka ya kuteketezwa.”
32 Ndipo Yefta akavuka kupigana na hao Waamoni, naye Bwana akawatia mkononi mwake. 33 Akawapiga kwa ushindi mkubwa kuanzia Aroeri mpaka karibu na Minithi na kuendelea mpaka Abel-Keramimu, miji yote iliyopigwa ni ishirini. Basi Israeli wakawashinda Waamoni.
34 Yefta aliporudi nyumbani Mispa, tazama, binti yake akatoka ili kumlaki kwa matari na kucheza. Alikuwa ndiye mtoto pekee, hakuwa na mwana wala binti mwingine. 35 Alipomwona akararua mavazi yake akalia, “Ee! Binti yangu! Umenifanya niwe na huzuni na kunyongʼonyea sana, kwa kuwa nimeweka nadhiri kwa Bwana, ambayo siwezi kuivunja.”
36 Akajibu, “Baba yangu, umetoa neno lako kwa Bwana. Nitendee mimi kama vile ulivyoahidi, kwa kuwa Bwana amekupa ushindi dhidi ya adui zako Waamoni.” 37 Naye akamwambia baba yake, “Naomba nifanyiwe jambo hili. Nipewe miezi miwili ili kuzunguka vilimani nikaulilie ubikira wangu, mimi na wenzangu.”
38 Baba yake akamwambia, “Waweza kwenda.” Naye akamwacha aende kwa miezi miwili. Hivyo akaondoka pamoja na wasichana wenzake, naye akaulilia ubikira wake huko vilimani kwa sababu asingeolewa kamwe. 39 Baada ya hiyo miezi miwili, alirejea kwa baba yake, naye baba yake akamtendea kama alivyokuwa ametoa nadhiri yake. Naye alikuwa bikira.
Nayo ikawa desturi katika Israeli, 40 kwamba kila mwaka binti wa Israeli huenda kwa siku nne ili kumkumbuka huyo binti wa Yefta, Mgileadi.
-
8 Baada yake, Ibzani wa Bethlehemu akawa mwamuzi wa Israeli. 9 Alikuwa na wana thelathini na binti thelathini. Akawaoza binti zake kwa watu wengine nje ya ukoo wake, na kuwatwalia wanawe wanawake thelathini toka nje ya ukoo wake. Ibzani akawa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka saba. 10 Ibzani akafa, akazikwa huko Bethlehemu.
-
16 Bwana asema,
“Wanawake wa Sayuni wana kiburi,
wanatembea na shingo ndefu,
wakikonyeza kwa macho yao,
wanatembea kwa hatua za madaha,
wakiwa na mapambo ya njuga kwenye vifundo vya miguu yao.
17 Kwa hiyo Bwana ataleta majipu kwenye vichwa vya wanawake wa Sayuni;
Bwana atazifanya ngozi za vichwa vyao kuwa vipara.”
-
18 “Mwanadamu, omboleza kwa ajili ya makundi ya wajeuri wa Misri na uwatupe kuzimu yeye na binti za mataifa yenye nguvu, waende huko pamoja nao washukao shimoni.
-
18 Ikimbieni zinaa. Dhambi zingine zote atendazo mtu ziko nje ya mwili wake, lakini yeye aziniye hutenda dhambi ndani ya mwili wake mwenyewe.
-
23 Kabla imani hii haijaja tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ile imani ifunuliwe. 24 Hivyo, sheria ilikuwa kiongozi kutufikisha kwa Kristo, ili tupate kuhesabiwa haki kwa imani. 25 Lakini sasa kwa kuwa ile imani imekuja, hatusimamiwi tena na sheria.
26 Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani. 27 Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo. 28 Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu. 29 Nanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.
-
7 Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.
-
20 Adamu akamwita mkewe Eva, kwa kuwa atakuwa mama wa wote walio hai.
-
9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”
-
22 Walipokuwa wakijiburudisha, watu waovu wa mji huo, wakaizingira ile nyumba. Wakagonga mlango na kusema na yule mzee mwenye nyumba, “Mtoe nje yule mtu aliyeingia kwako, tupate kumlawiti.”
23 Yule mwenye nyumba akatoka nje na kuwaambia, “Hapana, ndugu zangu msiwe waovu namna hii, ninawasihi. Kwa kuwa huyu mtu ni mgeni wangu msifanye jambo hili la aibu. 24 Tazameni, hapa yupo binti yangu ambaye ni bikira na suria wa huyu mtu. Nitawatoleeni hawa sasa, mkawatwae kwa nguvu na kuwafanyia lolote mtakalo. Lakini kwa mtu huyu msimfanyie jambo ovu hivyo.”
25 Lakini wale watu hawakumsikia. Hivyo yule mtu akamtoa yule suria wake nje kwa wale watu, nao wakambaka na kumnajisi usiku ule kucha mpaka asubuhi. Kulipoanza kupambazuka wakamwachia aende. 26 Alfajiri yule mwanamke akarudi kwenye ile nyumba bwana wake alikokuwa, akaanguka chini mlangoni, akalala pale hata kulipopambazuka.
27 Bwana wake alipoamka asubuhi na kufungua mlango wa nyumba na kutoka nje ili kuendelea na safari yake, tazama, yule suria wake alikuwa ameanguka pale penye ingilio la nyumba na mikono yake ikiwa penye kizingiti cha chini. 28 Akamwambia yule suria, “Inuka, twende.” Lakini hakujibu. Yule bwana akamwinua akampandisha juu ya punda wake, wakaondoka kwenda nyumbani.
29 Alipofika nyumbani, akachukua kisu na kumkatakata yule suria kiungo kwa kiungo, sehemu kumi na mbili, na kuvipeleka hivyo vipande katika sehemu zote za Israeli. 30 Kila mtu aliyeona akasema, “Jambo la namna hii halijaonekana wala kutendeka, tangu Israeli walipopanda kutoka Misri. Fikirini juu ya jambo hili! Tafakarini juu ya jambo hili! Tuambieni tufanye nini!”
-
1 Wana wa Israeli walikuwa wameapa kwa kiapo kule Mispa: “Hapana mtu yeyote atakayemwoza binti yake kwa Wabenyamini.”
-
24 “Enyi binti za Israeli,
lieni kwa ajili ya Sauli,
ambaye aliwavika nguo
nyekundu na maridadi,
ambaye aliremba mavazi yenu
kwa mapambo ya dhahabu.
-
6 Wana wa wana ni taji la wazee,
nao wazazi ni fahari ya watoto wao.
-
22 Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:
“Tazama, nitawaashiria watu wa Mataifa,
nitainua bendera yangu kwa mataifa;
watawaleta wana wako mikononi yao,
na kuwabeba binti zenu juu ya mabega yao.
-
13 Kisha watoto wadogo wakaletwa kwa Yesu ili aweke mikono yake juu yao na awaombee. Lakini wanafunzi wake wakawakemea wale waliowaleta.
14 Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mbinguni ni wa wale walio kama hawa.”
-
41 Naye Elizabeti aliposikia salamu ya Maria, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akaruka. Elizabeti akajazwa na Roho Mtakatifu, 42 akapaza sauti kwa nguvu akasema, “Umebarikiwa wewe miongoni mwa wanawake, naye mtoto utakayemzaa amebarikiwa. 43 Lakini ni kwa nini mimi nimepata upendeleo kiasi hiki, hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? 44 Mara tu niliposikia sauti ya salamu yako, mtoto aliyeko tumboni mwangu aliruka kwa furaha. 45 Amebarikiwa yeye aliyeamini kwamba lile Bwana alilomwambia litatimizwa.”
46 Naye Maria akasema:
“Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,
47 nayo roho yangu inamfurahia
Mungu Mwokozi wangu,
-
6 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu.
-
7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. 8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. 9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa.
-
32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.
-
7 “Kama mtu akimuuza binti yake kuwa mtumwa, hataachwa huru kama watumwa wa kiume waachiwavyo. 8 Kama hakumpendeza bwana wake aliyemchagua, huyo bwana atamwacha akombolewe. Hatakuwa na haki ya kumuuza kwa wageni, kwa sababu huyo bwana atakuwa amekosa uaminifu. 9 Kama akimchagua aolewe na mwanawe, ni lazima ampe haki za kuwa binti yake. 10 Ikiwa huyo mwana aliyeozwa mtumwa mwanamke ataoa mwanamke mwingine, ni lazima aendelee kumtosheleza huyo mke wa kwanza kwa chakula, mavazi na haki zote za ndoa.
Shows Read in context, Share and Copy.