56 Bible Verses About Pain

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Pain
  1. 16 Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. 17 Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi, 18 kwa sababu hatuangalii yale yanayoweza kuonekana bali yale yasiyoweza kuonekana. Kwa maana yale yanayoweza kuonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoweza kuonekana ni ya milele.

  2. 3 Nami nikasikia sauti kubwa kutoka kile kiti cha enzi ikisema, “Sasa makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao. Yeye atakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. 4 Atafuta kila chozi kutoka macho yao. Mauti haitakuwepo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”

  3. 16 Kwa mwanamke akasema,

    “Nitakuzidishia sana utungu wakati wa kuzaa kwako;

    kwa utungu utazaa watoto.

    Tamaa yako itakuwa kwa mumeo

    naye atakutawala.”

    17 Kwa Adamu akasema, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka kwenye mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’

    “Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako,

    kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo

    siku zote za maisha yako.

    18 Itazaa miiba na mibaruti kwa ajili yako,

    nawe utakula mimea ya shambani.

    19 Kwa jasho la uso wako

    utakula chakula chako

    hadi utakaporudi ardhini,

    kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo,

    kwa kuwa wewe u mavumbi

    na mavumbini wewe utarudi.”

  4. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2 ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

  5. 1 Barua hii ni kutoka kwangu mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu,

    Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, pamoja na watakatifu wote walioko Akaya yote:

    2 Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo iwe nanyi.

    3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote. 4 Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu. 5 Kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi ndani ya maisha yetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kwa njia ya Kristo. 6 Kama tunataabika, ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu; kama tukifarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu, iwaleteayo saburi ya mateso yale yale yanayotupata. 7 Nalo tumaini letu kwenu ni thabiti, kwa sababu tunajua kwamba kama vile mnavyoshiriki mateso yetu, ndivyo pia mnavyoshiriki katika faraja yetu.

    8 Ndugu wapendwa, hatutaki mkose kujua kuhusu zile taabu tulizopata huko Asia. Kwa maana tulilemewa na mizigo sana, kiasi cha kushindwa kuvumilia, hata tulikata tamaa ya kuishi.

  6. 7 Katika siku za maisha ya Yesu hapa duniani, alimtolea maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, yeye awezaye kumwokoa na mauti, naye Mungu akamsikia kwa sababu ya kutii kwake kwa unyenyekevu. 8 Ingawa alikuwa Mwana, alijifunza utiifu kutokana na mateso aliyoyapata, 9 na akiisha kukamilishwa, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wote wanaomtii. 10 Naye amewekwa na Mungu kuwa Kuhani Mkuu kwa mfano wa Melkizedeki.

  7. 1 Yesu alipokuwa akipita, akamwona mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa. 2 Wanafunzi wake wakamuuliza, “Rabi, ni nani aliyetenda dhambi, ni huyu mtu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?”

    3 Yesu akawajibu, “Huyu mtu wala wazazi wake hawakutenda dhambi. Alizaliwa kipofu ili kazi za Mungu zidhihirishwe katika maisha yake. 4 Yanipasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenituma wakati bado ni mchana, kwa kuwa usiku waja ambapo hakuna mtu awezaye kufanya kazi. 5 Wakati niko ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.”

  8. 22 Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa maumivu kama utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa.

  9. 2 Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3 kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. 4 Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu chochote.

  10. Zaburi ya Daudi. Funzo.

    1 Heri mtu yule ambaye amesamehewa makosa yake,

    ambaye dhambi zake zimefunikwa.

    2 Heri mtu yule ambaye Bwana

    hamhesabii dhambi,

    na ambaye rohoni mwake

    hamna udanganyifu.

    3 Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa

    kwa kulia kwa maumivu makali mchana kutwa.

    4 Usiku na mchana

    mkono wako ulinilemea,

    nguvu zangu zilinyonywa

    kama vile katika joto la kiangazi.

    5 Kisha nilikujulisha dhambi yangu

    wala sikuficha uovu wangu.

    Nilisema, “Nitaungama

    makosa yangu kwa Bwana.”

    Ndipo uliponisamehe

    hatia ya dhambi yangu.

  11. 18 Kwa nini maumivu yangu hayakomi,

    na jeraha langu ni la kuhuzunisha,

    wala haliponyeki?

    Je, utakuwa kwangu kama kijito cha udanganyifu,

    kama chemchemi iliyokauka?

    19 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana:

    “Kama ukitubu, nitakurejeza

    ili uweze kunitumikia;

    kama ukinena maneno yenye maana,

    wala si ya upuzi,

    utakuwa mnenaji wangu.

    Watu hawa ndio watakaokugeukia,

    wala si wewe utakayewageukia wao.

  12. 5 Nanyi mmesahau yale maneno ya kuwaonya yanayowataja ninyi kuwa wana, yakisema:

    “Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana,

    wala usikate tamaa akikukemea,

    6 kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao,

    na humwadhibu kila mmoja

    anayemkubali kuwa mwana.”

    7 Vumilieni taabu kwa ajili ya kufunzwa adabu. Mungu anawatendea ninyi kama watoto wake, kwa maana ni mtoto yupi asiyeadibishwa na mzazi wake? 8 Kama hakuna kuadibishwa (ambalo ni fungu la watoto wote), basi ninyi ni watoto wa haramu wala si watoto halali. 9 Tena, sisi sote tunao baba wa kimwili, waliotuadibisha nasi tukawaheshimu kwa ajili ya hilo. Je, si inatupasa kujinyenyekeza zaidi kwa Baba wa roho zetu ili tuishi? 10 Baba zetu walituadibisha kwa kitambo kidogo kama wao wenyewe walivyoona vyema, lakini Mungu hutuadibisha kwa faida yetu ili tupate kushiriki utakatifu wake. 11 Kuadibishwa wakati wowote hakuonekani kuwa kitu cha kufurahisha bali chenye maumivu kinapotekelezwa. Lakini baadaye huzaa matunda ya haki na amani kwa wale waliofunzwa nayo.

  13. 6 Bwana akamwambia Shetani, “Vema sana, kwa hiyo, yeye yumo mikononi mwako, lakini lazima umwachie uhai wake.”

    7 Basi Shetani akatoka mbele za Bwana naye akampiga Ayubu kwa majipu mabaya tangu nyayo za miguu yake hadi utosi wa kichwa. 8 Ndipo Ayubu akachukua kigae na kujikuna nacho huku akiketi kwenye majivu.

    9 Mke wake akamwambia, “Je, bado unashikamana na uadilifu wako? Mlaani Mungu nawe ukafe!”

    10 Akamjibu, “Unazungumza kama vile ambavyo mwanamke mpumbavu yeyote angenena. Je, tupokee mema mikononi mwa Mungu, nasi tusipokee na udhia?”

    Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi katika kusema kwake.

    11 Basi marafiki watatu wa Ayubu, ndio Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi na Sofari Mnaamathi, waliposikia juu ya taabu yote iliyompata Ayubu, wakajipanga toka manyumbani mwao, nao wakakutana pamoja kwa makubaliano kwenda kumtuliza katika taabu hiyo na kumfariji. 12 Walipomwona kwa mbali, ilikuwa vigumu kumtambua. Wakaanza kulia kwa sauti kubwa, wakayararua majoho yao na kujirushia mavumbi juu ya vichwa vyao. 13 Kisha wakaketi chini kwenye udongo pamoja na Ayubu kwa siku saba usiku na mchana. Hakuna yeyote aliyesema naye neno, kwa sababu waliona jinsi mateso yake yalivyokuwa makubwa.

  14. 22 Yeye hasikii kingine isipokuwa maumivu ya mwili wake mwenyewe,

    naye huomboleza kwa ajili yake mwenyewe.”

  15. 17 Usiku mifupa yangu inachoma;

    maumivu yanayonitafuna hayatulii kamwe.

    18 Kwa uwezo wake mkuu Mungu huwa kwangu kama nguo;

    hushikamana nami kama ukosi wa vazi langu.

  16. 7 Viuno vyangu vimejaa maumivu yaunguzayo,

    hakuna afya mwilini mwangu.

  17. 2 Tupatieni nafasi mioyoni mwenu. Hatujamkosea mtu yeyote, hatujampotosha mtu yeyote, wala hatujamdhulumu mtu yeyote. 3 Sisemi haya ili kuwahukumu, kwa kuwa nilisema mwanzo, kwamba ninyi mko mioyoni mwetu hata kwa kufa pamoja au kuishi pamoja. 4 Mara nyingi najivuna kwa ajili yenu; naona fahari juu yenu. Nimejawa na faraja. Nina furaha kupita kiasi katika mateso yetu yote.

    5 Kwa maana hata tulipoingia Makedonia, miili yetu haikuwa na raha. Tulisumbuliwa kila upande, kwa nje kulikuwa na mapigano na mioyoni mwetu tulikuwa na hofu. 6 Bali Mungu, yeye awafarijie wenye huzuni, alitufariji kwa kufika kwake Tito. 7 Lakini si kule kuja kwa Tito tu, bali pia kwa faraja mliyompa. Alitueleza jinsi mlivyonionea shauku, huzuni yenu kubwa na juhudi yenu kwa ajili yangu, ili kwamba furaha yangu ipate kuwa kubwa kuliko wakati wowote.

    8 Hata kama niliwahuzunisha kwa barua yangu, sijutii. Ingawa nilijuta kwa muda mfupi, kwa kuwa najua kwamba barua yangu iliwaumiza, lakini ni kwa kitambo tu, 9 lakini sasa nina furaha, si kwa sababu mlihuzunika, bali kwa kuwa huzuni hiyo iliwafanya mtubu. Kwa maana mlihuzunishwa kama Mungu alivyokusudia watu wahuzunike na hivyo sisi hatukuwadhuru kwa njia yoyote.

    10 Kwa maana huzuni ya kimungu huleta toba iletayo wokovu na wala haina majuto. Lakini huzuni ya kidunia husababisha mauti. 11 Tazameni jinsi huzuni hii ya kimungu ilivyoleta faida ndani yenu: bidii mliyo nayo, juhudi mliyofanya kujitetea, uchungu wenu, hofu yenu, upendo wenu, shauku yenu na jinsi mlivyokuwa tayari kutoa adhabu inayostahili. Kwa kila njia mmejithibitisha kuwa safi katika jambo hilo.

  18. 15 Ee Bwana, ninakungojea wewe,

    Ee Bwana Mungu wangu, utajibu.

    16 Kwa kuwa nilisema, “Usiwaache wafurahie,

    wala wasijitukuze juu yangu

    mguu wangu unapoteleza.”

    17 Kwa maana ninakaribia kuanguka,

    na maumivu yangu yananiandama siku zote.

    18 Naungama uovu wangu,

    ninataabishwa na dhambi yangu.

  19. Wimbo. Zaburi ya wana wa Kora. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa mahalathi leanothi. Utenzi wa Hemani Mwezrahi.

    1 Ee Bwana, Mungu uniokoaye,

    nimelia mbele zako usiku na mchana.

    2 Maombi yangu yafike mbele zako,

    utegee kilio changu sikio lako.

    3 Kwa maana nafsi yangu imejaa taabu,

    na maisha yangu yanakaribia kaburi.

  20. 47 Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe. Ni afadhali kwako kuingia katika Ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili lakini ukatupwa jehanamu, 48 mahali ambako

    “ ‘funza wake hawafi,

    wala moto wake hauzimiki.’

  21. 33 Yesu alipomwona Maria akilia na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye pia wakilia, Yesu alisikia uchungu moyoni, akafadhaika sana. 34 Akauliza, “Mmemweka wapi?”

    Wakamwambia, “Bwana, njoo upaone.”

    35 Yesu akalia machozi.

  22. 1 Hivyo nilikusudia moyoni mwangu nisifanye ziara nyingine yenye kuwaumiza ninyi. 2 Kwa kuwa kama nikiwahuzunisha ninyi, ni nani aliyebaki wa kunifurahisha isipokuwa ninyi ambao nimewahuzunisha? 3 Niliandika hivyo kama nilivyofanya, ili nikija nisihuzunishwe na wale watu ambao wangenifanya nifurahi. Nina uhakika na ninyi nyote, kwamba wote mngeshiriki furaha yangu. 4 Kwa maana niliwaandikia kutokana na dhiki kubwa na kutaabika sana kwa moyo wangu tena kwa machozi mengi, shabaha yangu si ili niwasababishe mhuzunike bali kuwaonyesha kina cha upendo wangu kwenu.

    5 Lakini ikiwa mtu yeyote amesababisha huzuni, kwa kiasi fulani hakunihuzunisha mimi kama vile alivyowahuzunisha ninyi nyote, ili nisiwe mkali kupita kiasi.

  23. 23 Je, wao ni watumishi wa Kristo? (Nanena kiwazimu.) Mimi ni zaidi yao. Nimefanya kazi kwa bidii kuwaliko wao, nimefungwa gerezani mara kwa mara, nimechapwa mijeledi sana, na nimekabiliwa na mauti mara nyingi. 24 Mara tano nimechapwa na Wayahudi viboko arobaini kasoro kimoja. 25 Mara tatu nilichapwa kwa fimbo, mara moja nilipigwa kwa mawe, mara tatu nimevunjikiwa na meli, nimekaa kilindini usiku kucha na mchana kutwa, 26 katika safari za mara kwa mara. Nimekabiliwa na hatari za kwenye mito, hatari za wanyangʼanyi, hatari kutoka kwa watu wangu mwenyewe, hatari kutoka kwa watu wa Mataifa; hatari mijini, hatari nyikani, hatari baharini; na hatari kutoka kwa ndugu wa uongo. 27 Nimekuwa katika kazi ngumu na taabu, katika kukesha mara nyingi; ninajua kukaa njaa na kuona kiu; nimefunga kula chakula mara nyingi; nimehisi baridi na kuwa uchi.

  24. 22 Akajibu, “Wakati mtoto alipokuwa bado yungali hai, nilifunga na kulia. Nilifikiri, ‘Nani ajuaye? Bwana aweza kunirehemu ili kumwacha mtoto aishi.’ 23 Lakini sasa kwa kuwa amekufa, kwa nini nifunge? Je, naweza kumrudisha tena? Mimi nitakwenda kwake, lakini yeye hatanirudia mimi.”

  25. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa utenzi wa “Kulungu wa Alfajiri.” Zaburi ya Daudi.

    1 Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?

    Kwa nini uko mbali hivyo kuniokoa?

    Mbali hivyo na maneno ya kuugua kwangu?

  26. 18 Bwana yu karibu na waliovunjika moyo,

    na huwaokoa waliopondeka roho.

  27. 5 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka?

    Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu?

    Weka tumaini lako kwa Mungu,

    kwa sababu bado nitamsifu,

    Mwokozi wangu na 6 Mungu wangu.

    Nafsi yangu inasononeka ndani yangu;

    kwa hiyo nitakukumbuka

    kutoka nchi ya Yordani,

    katika vilele vya Hermoni,

    kutoka Mlima Mizari.

  28. 9 Ninamwambia Mungu Mwamba wangu,

    “Kwa nini umenisahau?

    Kwa nini niendelee kuomboleza,

    nikiwa nimeonewa na adui?”

    10 Mifupa yangu inateseka kwa maumivu makali

    adui zangu wanaponidhihaki,

    wakiniambia mchana kutwa,

    “Yuko wapi Mungu wako?”

    11 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka?

    Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu?

    Weka tumaini lako kwa Mungu,

    kwa sababu bado nitamsifu,

    Mwokozi wangu na Mungu wangu.

  29. 11 Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaki na Yakobo katika Ufalme wa Mbinguni. 12 Lakini warithi wa Ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwako kilio na kusaga meno.”

  30. 54 Kwa hiyo, mwili huu wa kuharibika utakapovaa kutokuharibika, nao huu mwili wa kufa utakapovaa kutokufa, ndipo lile neno lililoandikwa litakapotimia: “Mauti imemezwa kwa kushinda.”

    55 “Kuko wapi, ee mauti, kushinda kwako?

    Uko wapi, ee mauti, uchungu wako?”

    56 Uchungu wa mauti ni dhambi na nguvu ya dhambi ni sheria. 57 Lakini ashukuriwe Mungu, yeye atupaye ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.

    58 Kwa hiyo, ndugu zangu wapenzi, simameni imara, msitikisike, mzidi sana katika kuitenda kazi ya Bwana, kwa maana mnajua ya kuwa, kazi yenu katika Bwana si bure.

  31. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

  32. 32 Basi niseme nini zaidi? Sina wakati wa kusema habari za Gideoni, Baraka, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samweli na manabii, 33 ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitekeleza haki, na wakapokea ahadi za Mungu; walifunga vinywa vya simba, 34 wakazima makali ya miali ya moto, na wakaepuka kuuawa kwa upanga; udhaifu wao uligeuka kuwa nguvu; pia walikuwa hodari vitani na kuyafukuza majeshi ya wageni. 35 Wanawake walipokea watu wao waliokuwa wamekufa, wakafufuliwa. Lakini wengine waliteswa, nao wakakataa kufunguliwa, ili wapate ufufuo ulio bora zaidi. 36 Wengine walidhihakiwa na kupigwa, hata walifungwa minyororo na kutiwa gerezani. 37 Walipigwa kwa mawe; walipasuliwa vipande viwili kwa msumeno; waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na mbuzi, wakiwa maskini, wakiteswa na kutendwa mabaya, 38 watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao. Walizunguka majangwani na milimani, katika mapango na katika mahandaki ardhini.

    39 Hawa wote walishuhudiwa vyema kwa sababu ya imani yao, lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea yale yaliyoahidiwa. 40 Kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea kitu kilicho bora zaidi ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.

  33. 20 Kwani ni faida gani kwa mtu kustahimili anapopigwa kwa sababu ya makosa yake? Lakini kama mkiteswa kwa sababu ya kutenda mema, nanyi mkastahimili, hili ni jambo la kusifiwa mbele za Mungu.

    21 Ninyi mliitwa kwa ajili ya haya, kwa sababu Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akiwaachia kielelezo, ili mzifuate nyayo zake.

    22 “Yeye hakutenda dhambi,

    wala hila haikuonekana kinywani mwake.”

    23 Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakutishia, bali alijikabidhi kwa yeye ahukumuye kwa haki. 24 Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili tufe kwa mambo ya dhambi, bali tupate kuishi katika haki. Kwa kupigwa kwake, ninyi mmeponywa.

  34. 19 Kwa hiyo, wale wanaoteswa kulingana na mapenzi ya Mungu, wajikabidhi kwa Muumba wao aliye mwaminifu, huku wakizidi kutenda mema.

  35. 15 Nami nitaweka uadui

    kati yako na huyo mwanamke,

    na kati ya uzao wako na wake,

    yeye atakuponda kichwa,

    nawe utamuuma kisigino.”

  36. 8 Basi Kaini akamwambia ndugu yake Abeli, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Abeli ndugu yake, akamuua.

  37. 11 Waganga hawakuweza kusimama mbele ya Mose kwa sababu ya majipu yale yaliyokuwa miilini mwao na juu ya miili ya Wamisri wote.

  38. 10 Ndipo bado ningekuwa na hii faraja,

    furaha yangu katika maumivu makali:

    kwamba sikuwa nimeyakana maneno yake yeye Aliye Mtakatifu.

  39. 6 “Lakini kama nikisema, maumivu yangu bado hayatulizwi;

    nami kama nikijizuia, wala hayaondoki.

  40. 19 Mtu anaweza kutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake,

    kwa dhiki za mfululizo katika mifupa yake,

    20 kiasi kwamba maisha yake yenyewe yanakataa chakula

    nayo nafsi yake ikakichukia kabisa hata chakula kizuri.

    21 Nyama ya mwili wake huisha kwa kukonda,

    nayo mifupa yake ambayo mwanzoni ilikuwa imefichika,

    sasa inatokeza nje.

    22 Nafsi yake inakaribia kaburi,

    nao uhai wake karibu na wajumbe wa kifo.

  41. 3 Hakuna afya mwilini mwangu

    kwa sababu ya ghadhabu yako,

    mifupa yangu haina uzima

    kwa sababu ya dhambi zangu.

    4 Maovu yangu yamenifunika

    kama mzigo usiochukulika.

    5 Majeraha yangu yameoza na yananuka,

    kwa sababu ya upumbavu wa dhambi zangu.

  42. 3 Anawaponya waliovunjika mioyo

    na kuvifunga vidonda vyao.

    4 Huzihesabu nyota

    na huipa kila moja jina lake.

    5 Bwana wetu ni mkuu na mwenye uwezo mwingi,

    ufahamu wake hauna kikomo.

  43. 7 Sasa basi wanangu, nisikilizeni;

    msiache ninalowaambia.

    8 Njia zenu ziwe mbali naye,

    msiende karibu na mlango wa nyumba yake,

    9 usije ukatoa nguvu zako nzuri kwa wengine

    na miaka yako kwa aliye mkatili,

    10 wageni wasije wakasherehekea utajiri wako

    na jitihada yako ikatajirisha

    nyumba ya mwanaume mwingine.

    11 Mwishoni mwa maisha yako utalia kwa uchungu,

    wakati nyama na mwili wako vimechakaa.

    12 Utasema, “Tazama jinsi gani nilivyochukia adhabu!

    Tazama jinsi moyo wangu ulivyodharau maonyo!

    13 Sikuwatii walimu wangu

    wala kuwasikiliza wakufunzi wangu.

    14 Nimefika ukingoni mwa maangamizi kabisa

    katikati ya kusanyiko lote.”

  44. 28 Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuua roho. Afadhali mwogopeni yeye awezaye kuiangamiza roho na mwili katika jehanamu.

  45. 38 Kisha Yesu akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe pamoja nami.”

  46. 16 Je, huyu mwanamke, ambaye ni binti wa Abrahamu, aliyeteswa na Shetani akiwa amemfunga kwa miaka yote hii kumi na minane, hakustahili kufunguliwa kutoka kifungo hicho siku ya Sabato?”

  47. 28 “Ndipo kutakuwako kilio na kusaga meno, mtakapowaona Abrahamu, Isaki, Yakobo na manabii wote wakiwa katika Ufalme wa Mungu, lakini ninyi mkiwa mmetupwa nje.

  48. 33 Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walipomsulubisha Yesu pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wake wa kushoto.

  49. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

  50. 17 Paulo akiwa Mileto, alituma mjumbe kwenda Efeso kuwaita wazee wa kanisa waje wakutane naye. 18 Walipofika akawaambia, “Ninyi wenyewe mnajua jinsi nilivyoishi katikati yenu muda wote tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia. 19 Nilimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote na kwa machozi nikivumilia taabu na mapingamizi yaliyonipata kutokana na hila za Wayahudi. 20 Mnajua kwamba sikusita kuhubiri jambo lolote ambalo lingekuwa la kuwafaa ninyi, lakini nilifundisha hadharani na nyumba kwa nyumba. 21 Nimewashuhudia Wayahudi na Wayunani kwamba inawapasa kumgeukia Mungu kwa kutubu dhambi na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo.

    22 “Nami sasa nimesukumwa na Roho, ninakwenda Yerusalemu wala sijui ni nini kitakachonipata huko. 23 Ila ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu amenionya kuwa vifungo na mateso vinaningoja. 24 Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani kwangu, kama kuyamaliza mashindano na kukamilisha ile kazi Bwana Yesu aliyonipa, yaani, kazi ya kuishuhudia Injili ya neema ya Mungu.

  51. 15 Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao.

  52. 27 Kweli alikuwa mgonjwa, tena karibu ya kufa. Lakini Mungu alimhurumia, wala si yeye tu, bali hata na mimi alinihurumia, nisipatwe na huzuni juu ya huzuni.

  53. 13 Lakini ndugu, hatutaki mkose kujua kuhusu wale waliolala mauti, ili msihuzunike kama watu wengine wasiokuwa na tumaini.

  54. 12 Wapenzi, msione ajabu kwa yale mateso yanayotukia miongoni mwenu, kana kwamba ni kitu kigeni kinachowapata. 13 Bali furahini kuwa mnashiriki katika mateso ya Kristo, ili mpate kufurahi zaidi wakati utukufu wake utakapofunuliwa. 14 Kama mkitukanwa kwa ajili ya jina la Kristo, mmebarikiwa, kwa sababu Roho wa utukufu na wa Mungu anakaa juu yenu.

  55. 8 (kwa sababu yale matendo mapotovu aliyoyaona na kuyasikia huyo mtu mwenye haki alipoishi miongoni mwao yalimhuzunisha siku baada ya siku):

  56. 12 Nikatazama akiivunja ile lakiri ya sita. Pakatokea tetemeko kuu la nchi, na jua likawa jeusi kama nguo ya gunia iliyotengenezwa kwa singa za mbuzi, na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu. 13 Nyota zilizo angani zikaanguka ardhini kama vile matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. 14 Anga ikatoweka kama vile karatasi isokotwavyo, na kila mlima na kila kisiwa kikaondolewa mahali pake.

    15 Ndipo wafalme wa dunia, wakuu wote, majemadari, matajiri, wenye nguvu na kila mtu, mtumwa na mtu huru, wakajificha katika mapango na kwenye miamba ya milima. 16 Wakaiita milima na miamba wakisema, “Tuangukieni, mkatufiche na uso wake yeye aketiye kwenye kiti cha enzi, na mkatuepushe na ghadhabu ya Mwana-Kondoo! 17 Kwa maana siku ile kuu ya ghadhabu yao imewadia. Je, ni nani awezaye kustahimili?”