62 Bible Verses About Suffering

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Suffering
  1. 21 Tangu wakati huo, Yesu alianza kuwaeleza wanafunzi wake kwamba hana budi kwenda Yerusalemu na kupata mateso mengi mikononi mwa wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa sheria, na kwamba itampasa auawe lakini siku ya tatu kufufuliwa.

    22 Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea akisema, “Haiwezekani, Bwana! Jambo hili kamwe halitakupata!”

    23 Lakini Yesu akageuka na kumwambia Petro, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

    24 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 25 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata.

  2. 18 “Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba ulinichukia mimi kabla yenu. 19 Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungeliwapenda kama vile unavyowapenda walio wake. Kwa sababu ninyi si wa ulimwengu, lakini mimi nimewachagua kutoka ulimwengu, hii ndiyo sababu ulimwengu unawachukia. 20 Kumbukeni lile neno nililowaambia, ‘Hakuna mtumishi aliye mkuu kuliko bwana wake.’ Kama wamenitesa mimi, nanyi pia watawatesa. Kama wamelishika neno langu, watalishika na neno lenu pia.

  3. 13 Siku moja watoto wa Ayubu walipokuwa wakifanya karamu wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, 14 akaja mjumbe kwa Ayubu na kusema, “Maksai walikuwa wakilima na punda walikuwa wakilisha karibu nao, 15 Waseba wakawashambulia na kuchukua mifugo. Kisha wakawaua watumishi kwa upanga, nami ndimi peke yangu niliyenusurika kukuletea habari!”

    16 Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Moto wa Mungu ulishuka kutoka mbinguni na kuteketeza kondoo na watumishi, nami ndimi peke yangu niliyenusurika kukuletea habari!”

    17 Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wakaldayo waliunda vikosi vitatu vya uvamizi na kuwaangukia ngamia wako na kuwachukua wakaondoka nao. Wakawaua watumishi kwa upanga, nami ndimi peke yangu niliyenusurika kukuletea habari.”

    18 Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wana wako na binti zako walipokuwa wakifanya karamu, wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, 19 ghafula upepo wenye nguvu ukavuma kutoka jangwani, nao ukaipiga nyumba hiyo pembe zake nne. Ikawaangukia hao watoto nao wamekufa, nami ndimi peke yangu niliyenusurika kukuletea habari!”

    20 Ndipo Ayubu akasimama, akararua joho lake na kunyoa nywele zake. Kisha akaanguka chini katika kuabudu 21 na kusema:

    “Nilitoka tumboni mwa mama yangu uchi,

    nami nitaondoka uchi,

    Bwana alinipa, naye Bwana ameviondoa,

    jina la Bwana litukuzwe.”

    22 Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi kwa kumlaumu Mungu kwa kufanya ubaya.

  4. 16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kwamba sisi tu watoto wa Mungu. 17 Hivyo, ikiwa sisi ni watoto, basi tu warithi, warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo, naam, tukiteswa pamoja naye tupate pia kutukuzwa pamoja naye.

    18 Nayahesabu mateso yetu ya wakati huu kuwa si kitu kulinganisha na utukufu utakaodhihirishwa kwetu. 19 Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu. 20 Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitiisha katika tumaini, 21 ili kwamba viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka kwa utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.

    22 Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa maumivu kama utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa. 23 Wala si hivyo viumbe peke yao, bali hata sisi ambao ndio matunda ya kwanza ya Roho, kwa ndani tunalia kwa uchungu tukisubiri kwa shauku kufanywa wana wa Mungu, yaani, ukombozi wa miili yetu.

  5. 3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote. 4 Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu. 5 Kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi ndani ya maisha yetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kwa njia ya Kristo. 6 Kama tunataabika, ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu; kama tukifarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu, iwaleteayo saburi ya mateso yale yale yanayotupata. 7 Nalo tumaini letu kwenu ni thabiti, kwa sababu tunajua kwamba kama vile mnavyoshiriki mateso yetu, ndivyo pia mnavyoshiriki katika faraja yetu.

    8 Ndugu wapendwa, hatutaki mkose kujua kuhusu zile taabu tulizopata huko Asia. Kwa maana tulilemewa na mizigo sana, kiasi cha kushindwa kuvumilia, hata tulikata tamaa ya kuishi. 9 Kwa kweli, mioyoni mwetu tulihisi tumekabiliwa na hukumu ya kifo, ili tusijitegemee sisi wenyewe bali tumtegemee Mungu afufuaye wafu. 10 Yeye aliyetuokoa kwenye hatari kubwa ya kifo na atatuokoa tena. Kwake yeye tumeweka tumaini letu kwamba ataendelea kutuokoa. 11 Kama vile mlivyoungana kusaidiana nasi katika maombi, hivyo wengi watatoa shukrani kwa niaba yetu kwa ajili ya baraka za neema tulizopata kwa majibu ya maombi ya wengi.

  6. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

    6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. 7 Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.

  7. 18 Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu kwa heshima yote, si wale mabwana walio wema na wapole peke yao, bali pia wale walio wakali. 19 Kwa maana ni jambo la sifa kama mtu akivumilia anapoteswa kwa uonevu kwa ajili ya Mungu. 20 Kwani ni faida gani kwa mtu kustahimili anapopigwa kwa sababu ya makosa yake? Lakini kama mkiteswa kwa sababu ya kutenda mema, nanyi mkastahimili, hili ni jambo la kusifiwa mbele za Mungu.

    21 Ninyi mliitwa kwa ajili ya haya, kwa sababu Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akiwaachia kielelezo, ili mzifuate nyayo zake.

    22 “Yeye hakutenda dhambi,

    wala hila haikuonekana kinywani mwake.”

    23 Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakutishia, bali alijikabidhi kwa yeye ahukumuye kwa haki.

  8. 12 Wapenzi, msione ajabu kwa yale mateso yanayotukia miongoni mwenu, kana kwamba ni kitu kigeni kinachowapata. 13 Bali furahini kuwa mnashiriki katika mateso ya Kristo, ili mpate kufurahi zaidi wakati utukufu wake utakapofunuliwa. 14 Kama mkitukanwa kwa ajili ya jina la Kristo, mmebarikiwa, kwa sababu Roho wa utukufu na wa Mungu anakaa juu yenu. 15 Lakini asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu anayeteswa kwa kuwa ni muuaji, au mwizi, au mhalifu wa aina yoyote, au anayejishughulisha na mambo ya watu wengine. 16 Lakini kama ukiteseka kwa kuwa Mkristo, usihesabu jambo hilo kuwa ni aibu, bali mtukuze Mungu kwa sababu umeitwa kwa jina hilo.

  9. 3 Alidharauliwa na kukataliwa na wanadamu,

    mtu wa huzuni nyingi, ajuaye mateso.

    Kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,

    alidharauliwa, wala hatukumhesabu kuwa kitu.

    4 Hakika alichukua udhaifu wetu

    na akajitwika huzuni zetu,

    hata hivyo tulidhania kuwa amepigwa na Mungu,

    akapigwa sana naye, na kuteswa.

    5 Lakini alitobolewa kwa ajili ya makosa yetu,

    alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu;

    adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake,

    na kwa majeraha yake sisi tumepona.

    6 Sisi sote, kama kondoo, tumepotea,

    kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe,

    naye Bwana aliweka juu yake

    maovu yetu sisi sote.

  10. 2 Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3 kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. 4 Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu chochote.

  11. 7 Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, sasa nayahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. 8 Zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara tupu nikiyalinganisha na faida kubwa ipitayo kiasi cha kumjua Kristo Yesu Bwana wangu, ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote, nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Kristo. 9 Nami nionekane mbele zake bila kuwa na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu kwa njia ya imani. 10 Nataka nimjue Kristo na uweza wa kufufuka kwake na ushirika wa mateso yake, ili nifanane naye katika mauti yake, 11 ili kwa njia yoyote niweze kufikia ufufuo wa wafu.

  12. 8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza. 9 Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.

    10 Nanyi mkiisha kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Kristo, yeye mwenyewe atawarejesha na kuwatia nguvu, akiwaimarisha na kuwathibitisha. 11 Uweza una yeye milele na milele. Amen.

    12 Kwa msaada wa Silvano, ambaye ninamhesabu kuwa ndugu mwaminifu, nimewaandikia waraka huu mfupi ili kuwatia moyo, na kushuhudia kwamba hii ni neema halisi ya Mungu. Simameni imara katika neema hiyo.

  13. 1 Kwa sababu hii, kwa kuwa tumezungukwa na wingu kubwa namna hii la mashahidi, basi na tuweke kando kila kitu kinachotuzuia na ile dhambi inayotuzinga kwa urahisi, nasi tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa kwa ajili yetu. 2 Basi na tumtazame sana Yesu mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu, yeye ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake alistahimili msalaba, bila kujali aibu ya huo msalaba, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. 3 Mtafakarini sana yeye aliyestahimili upinzani mkuu namna hii kutoka kwa watu wenye dhambi, ili kwamba msije mkachoka na kukata tamaa.

    4 Katika kushindana kwenu dhidi ya dhambi, bado hamjapigana kiasi cha kumwaga damu yenu.

  14. 1 Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya, kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza vimekwisha kupita, wala hapakuwepo na bahari tena. 2 Nikaona Mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe. 3 Nami nikasikia sauti kubwa kutoka kile kiti cha enzi ikisema, “Sasa makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao. Yeye atakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. 4 Atafuta kila chozi kutoka macho yao. Mauti haitakuwepo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”

  15. 1 Yesu alipokuwa akipita, akamwona mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa. 2 Wanafunzi wake wakamuuliza, “Rabi, ni nani aliyetenda dhambi, ni huyu mtu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?”

    3 Yesu akawajibu, “Huyu mtu wala wazazi wake hawakutenda dhambi. Alizaliwa kipofu ili kazi za Mungu zidhihirishwe katika maisha yake.

  16. 27 Lakini lolote litakalotukia, mwenende kama ipasavyo Injili ya Kristo, ili kwamba nikija na kuwaona au ikiwa sipo, nipate kusikia haya juu yenu: Kuwa mnasimama imara katika roho moja, mkiishindania imani ya Injili kwa umoja, 28 wala msitishwe na wale wanaowapinga. Hii ni ishara kwao kuwa wataangamia, lakini ninyi mtaokolewa, na hii ni kazi ya Mungu. 29 Kwa maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, bali pia kuteswa kwa ajili yake, 30 kwa kuwa mnashiriki mashindano yale yale mliyoyaona nikiwa nayo na ambayo hata sasa mnasikia kuwa bado ninayo.

  17. 12 Kwa maana macho ya Bwana

    huwaelekea wenye haki,

    na masikio yake yako makini

    kusikiliza maombi yao.

    Bali uso wa Bwana uko kinyume

    na watendao maovu.”

    13 Basi, ni nani atakayewadhuru mkiwa wenye juhudi katika kutenda mema? 14 Lakini mmebarikiwa hata kama ikiwalazimu kuteseka kwa ajili ya haki. “Msiogope vitisho vyao, wala msiwe na wasiwasi.” 15 Bali mtakaseni Kristo kuwa Bwana mioyoni mwenu. Siku zote mwe tayari kumjibu mtu yeyote atakayewauliza kuhusu sababu ya tumaini lililomo ndani yenu. Lakini fanyeni hivyo kwa upole na kwa heshima, 16 mkizitunza dhamiri zenu ziwe safi, ili wale wasemao mabaya dhidi ya mwenendo wenu mzuri katika Kristo waaibike kwa ajili ya masingizio yao.

    17 Kwa maana ni afadhali kupata mateso kwa ajili ya kutenda mema, kama kuteseka huko ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kuteseka kwa kutenda maovu.

  18. 16 Kwa mwanamke akasema,

    “Nitakuzidishia sana utungu wakati wa kuzaa kwako;

    kwa utungu utazaa watoto.

    Tamaa yako itakuwa kwa mumeo

    naye atakutawala.”

    17 Kwa Adamu akasema, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka kwenye mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’

    “Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako,

    kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo

    siku zote za maisha yako.

    18 Itazaa miiba na mibaruti kwa ajili yako,

    nawe utakula mimea ya shambani.

    19 Kwa jasho la uso wako

    utakula chakula chako

    hadi utakaporudi ardhini,

    kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo,

    kwa kuwa wewe u mavumbi

    na mavumbini wewe utarudi.”

  19. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

  20. 7 Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. 8 Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.

  21. 6 Katika hili mnafurahi sana, ingawa sasa kwa kitambo kidogo mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna nyingi. 7 Haya yamewajia ili kwamba imani yenu, iliyo ya thamani kuliko dhahabu ipoteayo, ingawa hujaribiwa kwa moto, ionekane kuwa halisi na imalizie katika sifa, utukufu na heshima wakati Yesu Kristo atadhihirishwa. 8 Ingawa hamjamwona, mnampenda; tena ingawa sasa hammwoni, mnamwamini na kujawa na furaha isiyoneneka yenye utukufu usioelezeka. 9 Maana mnaupokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu.

  22. 16 Nami nitamwonyesha jinsi impasavyo kuteseka kwa ajili ya Jina langu.”

  23. 23 Je, wao ni watumishi wa Kristo? (Nanena kiwazimu.) Mimi ni zaidi yao. Nimefanya kazi kwa bidii kuwaliko wao, nimefungwa gerezani mara kwa mara, nimechapwa mijeledi sana, na nimekabiliwa na mauti mara nyingi. 24 Mara tano nimechapwa na Wayahudi viboko arobaini kasoro kimoja. 25 Mara tatu nilichapwa kwa fimbo, mara moja nilipigwa kwa mawe, mara tatu nimevunjikiwa na meli, nimekaa kilindini usiku kucha na mchana kutwa, 26 katika safari za mara kwa mara. Nimekabiliwa na hatari za kwenye mito, hatari za wanyangʼanyi, hatari kutoka kwa watu wangu mwenyewe, hatari kutoka kwa watu wa Mataifa; hatari mijini, hatari nyikani, hatari baharini; na hatari kutoka kwa ndugu wa uongo. 27 Nimekuwa katika kazi ngumu na taabu, katika kukesha mara nyingi; ninajua kukaa njaa na kuona kiu; nimefunga kula chakula mara nyingi; nimehisi baridi na kuwa uchi. 28 Zaidi ya hayo yote, nakabiliwa na mzigo wa wajibu wangu kwa makanisa yote. 29 Je, ni nani aliye mdhaifu, nami nisijisikie mdhaifu? Je, nani aliyekwazwa, nami nisiudhike?

  24. 35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga? 36 Kama ilivyoandikwa:

    “Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;

    tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.”

    37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

  25. 8 Twataabika kila upande lakini hatuangamizwi; twaona wasiwasi lakini hatukati tamaa; 9 twateswa lakini hatuachwi; twatupwa chini lakini hatupondwi. 10 Siku zote twachukua katika mwili kufa kwake Yesu ili kwamba uzima wa Yesu uweze kudhihirika katika miili yetu. 11 Kwa maana sisi tulio hai siku zote tumetolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili kwamba uzima wake upate kudhihirishwa katika mwili wetu upatikanao na mauti.

  26. 16 Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. 17 Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi, 18 kwa sababu hatuangalii yale yanayoweza kuonekana bali yale yasiyoweza kuonekana. Kwa maana yale yanayoweza kuonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoweza kuonekana ni ya milele.

  27. 8 Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, yeye aliye wa uzao wa Daudi. Hii ndiyo Injili yangu, 9 ambayo kwayo ninateseka hata kufikia hatua ya kufungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu halifungwi. 10 Kwa hiyo ninavumilia mambo yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, kusudi wao nao wapate wokovu ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.

    11 Hili ni neno la kuaminiwa:

    Kwa maana kama tumekufa pamoja naye,

    tutaishi pia pamoja naye.

    12 Kama tukistahimili,

    pia tutatawala pamoja naye.

    Kama tukimkana yeye,

    naye atatukana sisi.

  28. 12 Naam, yeyote anayetaka kuishi maisha ya utauwa ndani ya Kristo Yesu atateswa.

  29. 14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

  30. 3 Ndugu, imetubidi kumshukuru Mungu kwa ajili yenu siku zote, kama ulivyo wajibu wetu, kwa sababu imani yenu inakua zaidi na zaidi na upendo wa kila mmoja wenu alio nao kwa mwenzake unazidi kuongezeka. 4 Ndiyo sababu miongoni mwa makanisa ya Mungu, tunajivuna kuhusu saburi yenu na imani mliyo nayo katika mateso yote na dhiki mnazostahimili.

    5 Haya yote ni uthibitisho kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na kwa sababu hiyo ninyi mtahesabiwa kwamba mnastahili kuwa wa Ufalme wa Mungu, mnaoteswa kwa ajili wake.

  31. 9 Lakini twamwona Yesu, aliyefanywa chini kidogo kuliko malaika, sasa akiwa amevikwa taji ya utukufu na heshima kwa sababu alistahimili mauti, ili kwamba kwa neema ya Mungu apate kuonja mauti kwa ajili ya kila mtu.

    10 Ili kuwaleta wana wengi katika utukufu, ilifaa kwamba Mungu, ambaye ni kwa ajili yake na kupitia kwake kila kitu kimekuwepo, amkamilishe mwanzilishi wa wokovu wao kwa njia ya mateso.

  32. 7 Kwa hiyo, ndugu zangu, vumilieni hadi kuja kwake Bwana. Angalieni jinsi mkulima angojavyo ardhi itoe mavuno yake yaliyo ya thamani na jinsi anavyovumilia kwa ajili ya kupata mvua za kwanza na za mwisho. 8 Ninyi nanyi vumilieni, tena simameni imara, kwa sababu kuja kwa Bwana kumekaribia. 9 Ndugu zangu, msinungʼunikiane msije mkahukumiwa. Hakimu amesimama mlangoni!

    10 Ndugu zangu, waangalieni manabii walionena kwa Jina la Bwana, ili kuwa mfano wa uvumilivu katika kukabiliana na mateso. 11 Kama mnavyojua, tunawahesabu kuwa wabarikiwa wale waliovumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wake Ayubu na mmeona kile ambacho hatimaye Bwana alimtendea. Bwana ni mwingi wa huruma, na amejaa rehema.

  33. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni nia iyo hiyo kwa maana mtu aliyekwisha kuteswa katika mwili ameachana na dhambi. 2 Kwa hivyo, haishi maisha yake yaliyobaki ya kuishi hapa duniani kwa tamaa mbaya za wanadamu, bali anaishi kwa mapenzi ya Mungu.

  34. 71 Ilikuwa vyema mimi kupata shida

    ili nipate kujifunza maagizo yako.

  35. 10 Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki,

    maana Ufalme wa Mbinguni ni wao.

    11 “Heri ninyi watu watakapowashutumu, na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu. 12 Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo walivyowatesa manabii waliokuwa kabla yenu.

  36. 40 Wakapokea ushauri wa Gamalieli. Wakawaita mitume ndani, wakaamuru wachapwe mijeledi, kisha wakawaagiza wasinene tena kwa jina la Yesu, wakawaachia waende zao.

    41 Nao mitume wakatoka nje ya baraza, wakiwa wamejaa furaha kwa sababu wamehesabiwa kustahili kupata aibu kwa ajili ya jina la Yesu. 42 Kila siku, Hekaluni na nyumba kwa nyumba, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema kwamba Yesu ndiye Kristo.

  37. 50 Faraja yangu katika mateso yangu ni hii:

    Ahadi yako inahifadhi maisha yangu.

  38. 13 Hakuna jaribu lolote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu; hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kutokea ili mweze kustahimili.

  39. 8 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna andika:

    “Haya ndiyo maneno yake yeye aliye wa Kwanza na wa Mwisho, aliyekufa kisha akafufuka. 9 Naijua dhiki yako na umaskini wako, lakini wewe ni tajiri! Nayajua masingizio ya wale wasemao kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali wao ni sinagogi la Shetani. 10 Usiogope mateso yatakayokupata. Nakuambia ibilisi atawatia baadhi yenu gerezani ili kuwajaribu, nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.

  40. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa utenzi wa “Kulungu wa Alfajiri.” Zaburi ya Daudi.

    1 Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?

    Kwa nini uko mbali hivyo kuniokoa?

    Mbali hivyo na maneno ya kuugua kwangu?

    2 Ee Mungu wangu, ninalia mchana, lakini hunijibu,

    hata usiku, sinyamazi.

  41. 21 Wakahubiri habari njema katika mji huo na kupata wanafunzi wengi. Kisha wakarudi Listra, Ikonio na Antiokia, 22 wakiwaimarisha wanafunzi na kuwatia moyo waendelee kudumu katika imani. Wakawaonya wakisema, “Imetupasa kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa kupitia katika taabu nyingi.”

  42. 2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo.

  43. 11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

    14 Lakini, mlifanya vyema kushiriki nami katika taabu zangu.

  44. 24 Sasa nafurahia kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu, na katika mwili wangu ninatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, ambao ni kanisa. 25 Mimi nimekuwa mtumishi wa kanisa kwa wajibu alionipa Mungu ili kuwaletea ninyi Neno la Mungu kwa ukamilifu: 26 Hii ni siri iliyokuwa imefichika tangu zamani na kwa vizazi vingi, lakini sasa imefunuliwa kwa watakatifu.

  45. 8 Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu, 9 ambaye alituokoa na kutuita katika mwito mtakatifu: si kwa kadiri ya matendo yetu mema bali kwa sababu ya kusudi lake mwenyewe na neema yake. Neema hii tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele. 10 Lakini sasa imefunuliwa kwa kudhihirishwa kwake Mwokozi wetu, Kristo Yesu, ambaye amebatilisha mauti na kuleta uzima na kutokufa kwa njia ya Injili. 11 Nami nimewekwa kuwa mhubiri, mtume na mwalimu wa Injili hii. 12 Hii ndiyo sababu ninateseka namna hii, lakini sioni haya kwa maana ninamjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kuwa anaweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hadi siku ile.

  46. 10 Kwa ajili ya Kristo sisi ni wajinga, lakini ninyi mna hekima sana ndani ya Kristo. Sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu. Tunadharauliwa, lakini ninyi mnaheshimiwa. 11 Mpaka saa hii tuna njaa na kiu, tu uchi, tumepigwa na hatuna makao. 12 Tunafanya kazi kwa bidii kwa mikono yetu wenyewe. Tunapolaaniwa, tunabariki, tunapoteswa, tunastahimili, 13 tunaposingiziwa, tunajibu kwa upole. Mpaka sasa tumekuwa kama takataka ya dunia na uchafu wa ulimwengu.

  47. 1 Ninyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaroga? Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele yenu kwamba amesulubiwa. 2 Nataka nijifunze neno moja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa kushika sheria, au kwa kuyaamini yale mliyosikia? 3 Je, ninyi ni wajinga kiasi hicho? Baada ya kuanza kwa Roho, je, sasa mwataka kumalizia katika mwili? 4 Je, mlipata mateso kiasi hicho bure? Ni kama kweli yalikuwa bure! 5 Je, Mungu huwapa Roho wake na kufanya miujiza katikati yenu kwa sababu mnatii sheria, au kwa sababu mnaamini kile mlichosikia?

    6 Kama vile “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”

  48. 3 Vumilia taabu pamoja nasi kama askari mwema wa Kristo Yesu.

  49. 9 Mke wake akamwambia, “Je, bado unashikamana na uadilifu wako? Mlaani Mungu nawe ukafe!”

    10 Akamjibu, “Unazungumza kama vile ambavyo mwanamke mpumbavu yeyote angenena. Je, tupokee mema mikononi mwa Mungu, nasi tusipokee na udhia?”

    Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi katika kusema kwake.

  50. 10 Lakini yalikuwa ni mapenzi ya Bwana

    kumchubua na kumsababisha ateseke.

    Ingawa Bwana amefanya maisha yake

    kuwa sadaka ya hatia,

    ataona uzao wake na kuishi siku nyingi,

    nayo mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake.

  51. 41 “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. 42 Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, 43 nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza, na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’

    44 “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’

    45 “Naye atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’

    46 “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”

  52. 9 “Lakini ninyi jihadharini. Kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kupigwa mijeledi katika masinagogi. Mtashtakiwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao. 10 Nayo habari njema lazima ihubiriwe kwanza kwa mataifa yote kabla ule mwisho haujawadia. 11 Mtakapokamatwa na kushtakiwa, msisumbuke awali kuhusu mtakalosema. Semeni tu lolote mtakalopewa wakati huo, kwa kuwa si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho Mtakatifu.

    12 “Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, naye baba atamsaliti mtoto wake. Watoto nao wataasi dhidi ya wazazi wao na kusababisha wauawe. 13 Watu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu. Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa.

  53. 42 akisema, “Baba, kama ni mapenzi yako, niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo, bali mapenzi yako yatendeke.”

  54. 13 Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.

  55. 5 Bwana akaona jinsi uovu wa mwanadamu ulivyokuwa mkubwa duniani, na ya kuwa kila mwelekeo wa mawazo ya moyo wake wakati wote ulikuwa mbaya tu. 6 Bwana akasikitika kwamba alimuumba mwanadamu duniani, moyo wa Mungu ukajaa masikitiko. 7 Kwa hiyo Bwana akasema, “Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemuumba kutoka kwenye uso wa dunia, wanadamu na wanyama, pamoja na viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Kwa maana nasikitika kuwaumba.”

  56. 2 Kumbuka jinsi Bwana Mungu wenu alivyowaongoza katika njia yote katika jangwa kwa miaka hii arobaini, kukunyenyekeza na kukujaribu ili ajue lililoko moyoni mwako, kwamba utayashika maagizo yake au la. 3 Alikudhili na kukufanya uone njaa kisha akulishe kwa mana, ambayo wewe wala baba zako hamkuijua, awafundishe kuwa mwanadamu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Bwana.

  57. 25 Moyo wa wasiwasi humlemea mtu,

    bali neno la huruma humfurahisha.

  58. 1 Kisha Yesu akaongozwa na Roho Mtakatifu kwenda nyikani ili akajaribiwe na ibilisi. 2 Baada ya kufunga siku arobaini usiku na mchana, hatimaye akaona njaa. 3 Mjaribu akamjia na kumwambia, “Ikiwa wewe ndiye Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate.”

    4 Lakini Yesu akajibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’ ”

  59. 46 Ilipofika saa tisa, Yesu akapaza sauti akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”)

    47 Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia hayo, wakasema, “Anamwita Eliya.”

    48 Ghafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo, akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Yesu ili anywe. 49 Wengine wakasema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Eliya atakuja kumwokoa.”

    50 Yesu alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake.

  60. 15 Kisha akawaambia, “Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu. 16 Kwa maana, nawaambia, sitaila tena Pasaka mpaka itakapotimizwa katika Ufalme wa Mungu.”

    17 Akiisha kukichukua kikombe, akashukuru, akasema, “Chukueni hiki mnywe wote. 18 Kwa maana nawaambia tangu sasa sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi Ufalme wa Mungu utakapokuja.”

    19 Kisha akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa, akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”

    20 Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, imwagikayo kwa ajili yenu.

  61. 26 Kama kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia pamoja nacho, kama kiungo kimoja kikipewa heshima, viungo vyote hufurahi pamoja nacho.

  62. 12 Heri mtu anayevumilia wakati wa majaribu, kwa sababu akiisha kushinda hilo jaribio atapewa taji la uzima Mungu alilowaahidia wale wampendao.