87 Bible Verses About Miracles

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Miracles
  1. 18 Yesu alipokuwa akiwaambia mambo haya, mara akaingia kiongozi wa sinagogi akapiga magoti mbele yake, akamwambia, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini njoo uweke mkono wako juu yake, naye atakuwa hai.” 19 Yesu akaondoka akafuatana naye, nao wanafunzi wake pia wakaandamana naye.

    20 Wakati huo huo, mwanamke mmoja, ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, akaja nyuma ya Yesu, akagusa upindo wa vazi lake, 21 kwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikigusa tu vazi lake, nitaponywa.”

    22 Yesu akageuka, naye alipomwona akamwambia, “Binti, jipe moyo mkuu, imani yako imekuponya.” Naye yule mwanamke akapona kuanzia saa ile ile.

    23 Yesu alipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi na kuwaona waombolezaji wakipiga filimbi za maombolezo na watu wengi wakipiga kelele, 24 akawaambia, “Ondokeni! Kwa maana binti huyu hakufa, bali amelala.” Wakamcheka kwa dhihaka. 25 Lakini watu walipokwisha kutolewa nje, akaingia mle ndani na kumshika yule binti mkono, naye akaamka. 26 Habari hizi zikaenea katika maeneo yale yote.

    27 Yesu alipokuwa akiondoka mahali pale, vipofu wawili wakamfuata wakipiga kelele kwa nguvu na kusema, “Mwana wa Daudi, tuhurumie!”

    28 Alipoingia mle nyumbani wale vipofu wakamjia. Naye Yesu akawauliza, “Mnaamini kwamba ninaweza kufanya jambo hili?”

    Wakamjibu, “Ndiyo, Bwana.”

    29 Ndipo Yesu akagusa macho yao na kusema, “Iwe kwenu sawasawa na imani yenu.” 30 Macho yao yakafunguka. Yesu akawaonya vikali, akisema, “Angalieni mtu yeyote asijue kuhusu jambo hili.” 31 Lakini wao wakaenda na kueneza habari zake katika eneo lile lote.

    32 Walipokuwa wanatoka, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu na ambaye hakuweza kuongea aliletwa kwa Yesu. 33 Yule pepo mchafu alipotolewa, yule mtu aliyekuwa bubu akaongea. Ule umati wa watu ukastaajabu na kusema, “Jambo kama hili kamwe halijapata kuonekana katika Israeli.”

  2. 5 Filipo akateremkia mji mmoja wa Samaria akawahubiria habari za Kristo 6 Watu walipomsikia Filipo na kuona ishara na miujiza aliyofanya, wakasikiliza kwa bidii yale aliyosema. 7 Pepo wachafu wakawa wakiwatoka watu wengi huku wakipiga kelele na wengi waliopooza na viwete wakaponywa. 8 Hivyo pakawa na furaha kuu katika mji huo.

  3. 33 Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Ainea, ambaye alikuwa amepooza na kwa muda wa miaka minane alikuwa hajaondoka kitandani. 34 Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo anakuponya, inuka utandike kitanda chako.” Mara Ainea akainuka. 35 Watu wote wa Lida na Sharoni walipomwona Ainea akitembea wakamgeukia Bwana.

    36 Huko Yafa palikuwa na mwanafunzi jina lake Tabitha (ambalo kwa Kiyunani ni Dorkasi). Huyu alikuwa mkarimu sana, akitenda mema na kuwasaidia maskini. 37 Wakati huo akaugua, akafa na wakiisha kuuosha mwili wake wakauweka katika chumba cha ghorofani. 38 Kwa kuwa Yafa hapakuwa mbali sana na Lida, wanafunzi waliposikia kwamba Petro yuko huko waliwatuma watu wawili kwake ili kumwomba, “Tafadhali njoo huku pasipo kukawia.”

    39 Kwa hiyo Petro akainuka akaenda nao, naye alipowasili, wakampeleka hadi kwenye chumba cha ghorofani alipokuwa amelazwa. Wajane wengi walisimama karibu naye wakilia na kuonyesha majoho na nguo nyingine ambazo Dorkasi alikuwa amewashonea alipokuwa pamoja nao.

    40 Petro akawatoa wote nje ya kile chumba, kisha akapiga magoti akaomba, akaugeukia ule mwili akasema, “Tabitha, inuka.” Akafumbua macho yake na alipomwona Petro, akaketi. 41 Petro akamshika mkono akamwinua, ndipo akawaita wale watakatifu na wajane akamkabidhi kwao akiwa hai. 42 Habari hizi zikajulikana sehemu zote za Yafa na watu wengi wakamwamini Bwana.

  4. 11 Mungu akafanya miujiza mingi isiyo ya kawaida kwa mkono wa Paulo, 12 hivi kwamba leso au vitambaa vilivyokuwa vimegusa mwili wa Paulo viliwekwa juu ya wagonjwa, nao wakapona magonjwa yao, na pepo wachafu wakawatoka.

    13 Basi baadhi ya Wayahudi wenye kutangatanga huku na huko wakitoa pepo wachafu wakajaribu kutumia jina la Bwana Yesu wale wenye pepo wakisema, “Kwa jina la Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo, nakuamuru utoke.” 14 Wana saba wa Skewa, Myahudi aliyekuwa kiongozi wa makuhani, walikuwa wanafanya hivyo. 15 Lakini pepo mchafu akawajibu, “Yesu namjua na Paulo pia namjua, lakini ninyi ni nani?” 16 Kisha yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia, akawashambulia vikali, akawashinda nguvu wote, wakatoka ndani ya ile nyumba wakikimbia wakiwa uchi na wenye majeraha.

    17 Habari hii ikajulikana kwa Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawajaa wote, nalo jina la Bwana Yesu likaheshimiwa sana. 18 Wengi wa wale waliokuwa wameamini wakati huu wakaja na kutubu waziwazi kuhusu matendo yao maovu.

  5. 1 Mose akamjibu, “Itakuwaje kama hawataniamini au kunisikiliza, waseme, ‘Bwana hakukutokea’?”

    2 Ndipo Bwana akamwambia, “Ni nini hicho kilicho mkononi mwako?”

    Akajibu, “Fimbo.”

    3 Bwana akasema, “Itupe chini.”

    Mose akaitupa chini hiyo fimbo nayo ikawa nyoka, naye akaikimbia. 4 Kisha Bwana akamwambia, “Nyoosha mkono wako umkamate mkiani.” Basi Mose akanyoosha mkono akamkamata yule nyoka, naye akabadilika tena kuwa fimbo mkononi mwake. 5 Bwana akasema, “Hivi ndivyo Waisraeli watakavyoamini kuwa Bwana, Mungu wa baba zao, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo, amekutokea wewe.”

    6 Kisha Bwana akamwambia, “Weka mkono wako ndani ya joho lako.” Basi Mose akaweka mkono wake ndani ya joho lake, naye alipoutoa, ulikuwa na ukoma, mweupe kama theluji.

    7 Mungu akamwambia, “Sasa urudishe tena huo mkono ndani ya joho lako.” Basi Mose akaurudisha mkono wake ndani ya joho lake na alipoutoa, ulikuwa mzima, kama sehemu zingine za mwili wake.

  6. 32 Elisha alipofika kwenye ile nyumba, mtoto alikuwa amelala juu ya kitanda chake angali amekufa. 33 Akaingia ndani, akajifungia yeye na yule mtoto, akamwomba Bwana. 34 Kisha akapanda kitandani, akalala juu ya yule mtoto, mdomo wake juu ya mdomo wa mtoto, macho yake juu ya macho ya mtoto, mikono yake juu ya mikono ya mtoto. Naye alipojinyoosha juu yake, mwili wa mtoto ukapata joto. 35 Elisha akajiondoa juu yake na kuanza kutembeatembea ndani ya chumba, kisha akarudi tena kitandani na kujinyoosha tena juu ya mtoto mara nyingine. Mtoto akapiga chafya mara saba, akafungua macho yake.

    36 Elisha akamwita Gehazi na kumwambia, “Mwite huyo Mshunami.” Naye akafanya hivyo. Yule Mshunami alipokuja, Elisha akasema, “Mchukue mwanao.” 37 Akaingia ndani, akaanguka miguuni pa Elisha na kusujudu hadi nchi. Kisha akamchukua mwanawe na kutoka nje.

    38 Elisha akarudi Gilgali, nako huko kulikuwa na njaa katika eneo lile. Wakati wana wa kundi la manabii walipokuwa wanakutana naye, akamwambia mtumishi wake, “Teleka chungu kikubwa jikoni uwapikie manabii.”

    39 Mmoja wao akatoka kwenda mashambani kuchuma mboga na akapata mtango mwitu. Akachuma matango na kujaza nguo yake aliyoikunja ili kubebea. Aliporudi, akayakatakata na kuyatumbukiza ndani ya chungu, ingawa hakuna aliyejua ni nini. 40 Mchuzi ukagawiwa watu, lakini walipoanza kula, wakalia, “Ee mtu wa Mungu, kuna mauti ndani ya chungu.” Nao hawakuweza kula.

    41 Elisha akasema, “Leteni unga.” Akauweka ndani ya chungu na kusema, “Wagawie watu ili wale.” Wala hapakuwa na kitu chochote chenye madhara ndani ya chungu.

    42 Akaja mtu kutoka Baal-Shalisha, akimletea mtu wa Mungu mikate ishirini ya shayiri iliyookwa kutokana na nafaka ya kwanza, pamoja na masuke ya nafaka mpya. Elisha akasema, “Wape watu ili wale.”

    43 Mtumishi wake akamuuliza, “Nitawezaje kuandaa hii mbele ya watu mia?”

    Lakini Elisha akajibu, “Wape watu ili wale. Kwa maana hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Watakula na kusaza.’ ” 44 Basi akaiandaa mbele yao ile mikate, wakala na baadhi yake wakasaza, sawasawa na neno la Bwana.

  7. 23 Naye alipoingia kwenye mashua, wanafunzi wake wakamfuata. 24 Ghafula, kukainuka dhoruba kali baharini hata mashua ikaanza kufunikwa na mawimbi, lakini Yesu alikuwa amelala usingizi. 25 Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, tuokoe! Tunazama!”

    26 Naye Yesu akawaambia, “Kwa nini mnaogopa, enyi wa imani haba?” Kisha akaamka na kukemea dhoruba na mawimbi, nako kukawa shwari kabisa.

    27 Wale watu wakashangaa, wakisema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata upepo na mawimbi vinamtii!”

    28 Walipofika ngʼambo katika nchi ya Wagerasi, watu wawili waliopagawa na pepo wachafu walitoka makaburini nao wakakutana naye. Watu hawa walikuwa wakali mno kiasi kwamba hakuna mtu aliyeweza kupita njia ile. 29 Wakapiga kelele, “Una nini nasi, Mwana wa Mungu? Umekuja hapa kututesa kabla ya wakati ulioamriwa?”

    30 Mbali kidogo kutoka pale walipokuwa, kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakilisha. 31 Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu, “Ukitutoa humu, turuhusu twende kwenye lile kundi la nguruwe.”

    32 Akawaambia, “Nendeni!” Hivyo wakatoka na kuwaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likateremka gengeni kwa kasi, likaingia katika ziwa na kufa ndani ya maji. 33 Wale watu waliokuwa wakiwachunga hao nguruwe wakakimbia wakaingia mjini, wakaeleza yote kuhusu yale yaliyowatokea wale waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu.

  8. 22 “Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kupitia kwake, kama ninyi wenyewe mjuavyo. 23 Huyu mtu akiisha kutolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu zamani, ninyi, kwa mikono ya watu wabaya, mlimuua kwa kumgongomea msalabani. 24 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana yeye kushikiliwa na nguvu za mauti.

  9. 1 Baada ya Yesu kumaliza kutoa maagizo kwa wanafunzi wake kumi na wawili, aliondoka hapo akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.

    2 Yohana aliposikia akiwa gerezani mambo ambayo Kristo alikuwa akiyafanya, aliwatuma wanafunzi wake 3 ili wakamuulize, “Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?”

    4 Yesu akajibu, “Rudini mkamwambie Yohana yale mnayosikia na kuyaona: 5 Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema. 6 Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa na mimi.”

  10. 8 Bwana akamwambia Mose na Aroni, 9 “Farao atakapowaambia, ‘Fanyeni muujiza,’ basi mwambie Aroni, ‘Chukua fimbo yako na uitupe chini mbele ya Farao,’ nayo fimbo itakuwa nyoka.”

    10 Ndipo Mose na Aroni wakaenda kwa Farao wakafanya sawasawa kama vile Bwana alivyoagiza. Aroni akaitupa ile fimbo yake chini mbele ya Farao na maafisa wake, nayo ikawa nyoka. 11 Farao naye akawaita watu wenye maarifa na wachawi na waganga wa Kimisri, nao wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao. 12 Kila mmoja alitupa fimbo yake chini, nayo ikawa nyoka. Lakini fimbo ya Aroni ikazimeza zile fimbo zao. 13 Hata hivyo moyo wa Farao ukawa mgumu, naye hakuwasikiliza Mose na Aroni, sawasawa kama vile Bwana alivyokuwa amesema.

  11. 30 Yesu alifanya miujiza mingine mingi mbele za wanafunzi wake, ambayo haikuandikwa katika kitabu hiki. 31 Lakini haya yameandikwa ili mweze kuamini ya kuwa Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu, na kwa kumwamini mpate uzima katika jina lake.

  12. 3 Hivyo Paulo na Barnaba wakakaa huko kwa muda wa kutosha wakihubiri kwa ujasiri juu ya Bwana, ambaye alithibitisha ujumbe wa neema yake kwa kuwawezesha kufanya ishara na miujiza.

  13. 3 Paulo alikuwa amekusanya mzigo wa kuni na alipokuwa anaweka kwenye moto kwa ajili ya joto, nyoka mwenye sumu akatoka humo na kujisokotea mkononi mwake. 4 Wale wenyeji wa kile kisiwa walipomwona yule nyoka akiningʼinia mkononi mwa Paulo, wakaambiana, “Huyu mtu lazima awe ni muuaji, ingawa ameokoka kutoka baharini, haki haijamwacha aishi.” 5 Lakini Paulo akamkungʼutia yule nyoka ndani ya moto wala yeye hakupata madhara yoyote. 6 Watu walikuwa wanangoja avimbe au aanguke ghafula na kufa. Lakini baada ya kungoja kwa muda mrefu na kuona kwamba hakuna chochote kisicho cha kawaida kilichomtokea, wakabadili mawazo yao na kuanza kusema kwamba yeye ni mungu.

    7 Basi karibu na sehemu ile, palikuwa na shamba kubwa la mtu mmoja kiongozi wa kile kisiwa, aliyeitwa Publio. Alitupokea na akatuhudumia kwa ukarimu mkubwa kwa muda wa siku tatu. 8 Baba yake Publio alikuwa mgonjwa kitandani, akiwa anaumwa homa na kuhara damu. Paulo akaingia ndani ili kumwona na baada ya maombi, akaweka mikono juu yake na kumponya. 9 Jambo hili lilipotukia, watu wote wa kisiwa kile waliokuwa wagonjwa wakaja, nao wakaponywa.

  14. 8 Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo. 9 Mtu mwingine imani kwa huyo Roho na mwingine karama za kuponya kwa huyo Roho mmoja. 10 Kwa mwingine matendo ya miujiza, kwa mwingine unabii kwa mwingine kupambanua roho, kwa mwingine aina mbalimbali za lugha, na kwa mwingine bado, tafsiri za lugha. 11 Haya yote hufanywa na huyo huyo Roho mmoja, Roho naye humgawia kila mtu, kama apendavyo.

  15. 24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa. 25 Angalieni, nimekwisha kuwaambia mapema.

  16. 18 Ndipo Wayahudi wakamuuliza, “Unaweza kutuonyesha ishara gani ili kuthibitisha mamlaka uliyo nayo ya kufanya mambo haya?”

    19 Yesu akawajibu, “Libomoeni hili Hekalu, nami nitalijenga tena kwa siku tatu!”

    20 Wale Wayahudi wakamjibu, “Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita, nawe wasema utalijenga kwa siku tatu?” 21 Lakini yeye Hekalu alilozungumzia ni mwili wake. 22 Baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake wakakumbuka yale aliyokuwa amesema. Ndipo wakayaamini Maandiko na yale maneno Yesu aliyokuwa amesema.

  17. 46 Hivyo Yesu akaja tena mpaka Kana ya Galilaya, kule alikokuwa amebadili maji kuwa divai. Huko kulikuwepo na afisa mmoja wa mfalme, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu. 47 Huyo mtu aliposikia kwamba Yesu alikuwa amewasili Galilaya kutoka Uyahudi, alimwendea na kumwomba ili aje kumponya mwanawe, aliyekuwa mgonjwa karibu ya kufa.

    48 Yesu akamwambia, “Ninyi watu msipoona ishara na miujiza kamwe hamtaamini.”

    49 Yule afisa wa mfalme akamwambia, “Bwana, tafadhali shuka kabla mwanangu hajafa.”

    50 Yesu akamjibu, “Enenda zako, mwanao yu hai.”

    Yule afisa akaamini yale maneno Yesu aliyomwambia, akaondoka akaenda zake. 51 Alipokuwa bado yuko njiani, akakutana na watumishi wake wakamwambia kwamba mwanawe yu mzima. 52 Akawauliza saa ambayo alianza kupata nafuu. Wakamwambia, “Jana yapata saa saba, homa ilimwacha.”

    53 Ndipo baba wa huyo mtoto akakumbuka kuwa huo ndio wakati ambapo Yesu alikuwa amemwambia, “Mwanao yu hai.” Kwa hiyo yeye pamoja na wote wa nyumbani mwake wakamwamini Yesu.

  18. 11 Kisha nikamwona mnyama mwingine, akipanda juu kutoka dunia. Alikuwa na pembe mbili kama mwana-kondoo, lakini akanena kama joka. 12 Akatumia mamlaka yote ya yule mnyama wa kwanza kwa niaba yake, naye akawafanya wote wakaao duniani kumwabudu yule mnyama wa kwanza, ambaye jeraha lake la mauti lilipona. 13 Naye akafanya ishara kuu na za ajabu, hata kusababisha moto kushuka toka mbinguni kuja duniani watu wakiona waziwazi. 14 Kwa sababu ya zile ishara alizokuwa amepewa uwezo wa kuzifanya kwa niaba ya yule mnyama wa kwanza, akawadanganya wakaao duniani. Akawaamuru wasimamishe sanamu kwa heshima ya yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini akaishi.

  19. 8 Katika mji wa Listra, alikuwako kiwete, ambaye alikuwa amelemaa tangu kuzaliwa na hakuwa ametembea kamwe. 9 Alimsikiliza Paulo alipokuwa akihubiri. Paulo alipomtazama akaona ana imani ya kuponywa. 10 Paulo akapaza sauti, “Simama kwa miguu yako!” Mara yule mtu akasimama upesi akaanza kutembea!

  20. 29 Sasa, Bwana angalia vitisho vyao na utuwezeshe sisi watumishi wako kulinena neno lako kwa ujasiri mkuu. 30 Nyoosha mkono wako ili kuponya wagonjwa na kutenda ishara na miujiza kwa jina la Mwanao mtakatifu Yesu.”

    31 Walipokwisha kuomba, mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.

  21. 17 Huyu msichana alikuwa akimfuata Paulo na sisi akipiga kelele, “Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, wao wanawatangazieni njia ya wokovu.” 18 Akaendelea kufanya hivi kwa siku nyingi, lakini Paulo akiwa ameudhika sana, akageuka na kumwambia yule pepo mchafu, “Ninakuamuru katika jina la Yesu Kristo, umtoke!” Yule pepo mchafu akamtoka saa ile ile.

  22. 22 Kisha Mose akawaongoza Israeli kutoka Bahari ya Shamu na kuingia katika Jangwa la Shuri. Kwa siku tatu walisafiri jangwani bila kupata maji. 23 Walipofika Mara, hawakuweza kunywa maji yake kwa sababu yalikuwa machungu. (Ndiyo sababu mahali hapo panaitwa Mara) 24 Kwa hiyo watu wakamnungʼunikia Mose, wakisema, “Tunywe nini?”

    25 Ndipo Mose akamlilia Bwana, naye Bwana akamwonyesha kipande cha mti. Akakitupa ndani ya maji, nayo maji yakawa matamu.

    Huko Bwana akawapa amri na sheria na huko akawajaribu. 26 Mungu akasema, “Kama mkisikiliza kwa bidii sauti ya Bwana Mungu wenu na kuyafanya yaliyo sawa machoni pake, kama mkiyatii maagizo yake na kuzishika amri zake zote, sitaleta juu yenu ugonjwa wowote niliowaletea Wamisri, kwa kuwa Mimi ndimi Bwana, niwaponyaye.”

    27 Kisha wakafika Elimu, mahali palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na miti sabini ya mitende, wakapiga kambi huko karibu na maji.

  23. 23 Wakati huo huo katika sinagogi lao palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, 24 naye akapiga kelele akisema, “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”

    25 Lakini Yesu akamkemea, akamwambia, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!” 26 Yule pepo mchafu akamtikisatikisa huyo mtu kwa nguvu, kisha akamtoka akipiga kelele kwa sauti kubwa.

    27 Watu wote wakashangaa, hata wakaulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!” 28 Sifa zake zikaanza kuenea haraka katika eneo lote la karibu na Galilaya.

    29 Mara walipotoka katika sinagogi, walikwenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea. 30 Mama mkwe wa Simoni alikuwa kitandani, ana homa, nao wakamweleza Yesu habari zake. 31 Hivyo Yesu akamwendea, akamshika mkono na kumwinua. Kisha homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia.

    32 Jioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Yesu wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu. 33 Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo. 34 Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme, kwa sababu walimjua yeye ni nani.

  24. 1 Kwa hiyo, imetupasa kuwa waangalifu sana kuhusu kile tulichosikia, ili tusije tukakiacha. 2 Kwa kuwa kama ujumbe ulionenwa na malaika ulikuwa imara, na kila uasi na kutokutii kulipata adhabu ya haki, 3 je, sisi tutapaje kupona kama tusipojali wokovu mkuu namna hii? Wokovu huu, ambao mwanzo ulitangazwa na Bwana, ulithibitishwa kwetu na wale waliomsikia. 4 Pia Mungu aliushuhudia kwa ishara, maajabu na kwa miujiza mbalimbali, na karama za Roho Mtakatifu alizozigawa kulingana na mapenzi yake.

  25. 20 Akawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu ndogo. Ninawaambia kweli, mkiwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mtauambia mlima huu, ‘Ondoka hapa uende pale,’ nao utaondoka. Wala hakutakuwa na jambo lisilowezekana kwenu. [

  26. 1 Siku ya tatu kulikuwa na arusi katika mji wa Kana ya Galilaya, naye mama yake Yesu alikuwepo pale. 2 Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wamealikwa arusini pia. 3 Divai ilipokwisha, mama yake Yesu akamwambia, “Wameishiwa na divai.”

    4 Yesu akamwambia, “Mwanamke, nina nini nawe? Saa yangu haijawadia.”

    5 Mama yake akawaambia wale watumishi, “Lolote atakalowaambia, fanyeni.”

    6 Basi ilikuwepo mitungi sita ya kuhifadhia maji iliyotengenezwa kwa mawe kwa ajili ya kujitakasa kwa desturi ya Kiyahudi; kila mtungi ungeweza kuchukua vipipa viwili au vitatu.

    7 Yesu akawaambia wale watumishi, “Ijazeni hiyo mitungi maji.” Nao wakaijaza ile mitungi mpaka juu.

    8 Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kidogo, mpelekeeni mkuu wa meza.”

    Hivyo wakachota, wakampelekea. 9 Yule mkuu wa meza akayaonja yale maji ambayo yalikuwa yamebadilika kuwa divai. Hakujua divai hiyo ilikotoka ingawa wale watumishi waliochota yale maji wao walifahamu. Basi akamwita bwana arusi kando 10 akamwambia, “Watu wote hutoa kwanza divai nzuri, kisha huleta ile divai hafifu wageni wakisha kunywa vya kutosha, lakini wewe umeiweka ile nzuri kupita zote mpaka sasa.”

    11 Huu, ndio uliokuwa muujiza wa kwanza Yesu aliofanya Kana ya Galilaya. Hivyo Yesu alidhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.

  27. 20 Lakini yule mnyama akakamatwa pamoja na huyo nabii wa uongo ambaye alikuwa amefanya ishara kwa niaba ya huyo mnyama, ambaye kwa ishara hizi aliwadanganya wale waliopokea chapa ya huyo mnyama na kuiabudu sanamu yake. Hawa wawili wakatupwa wakiwa hai ndani ya ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti.

  28. 5 Bwana akamjibu Mose, “Pita mbele ya watu. Wachukue pamoja nawe baadhi ya wazee wa Israeli, ichukue mkononi mwako ile fimbo uliyopiga nayo Mto Naili, nawe uende. 6 Huko nitasimama mbele yako karibu na mwamba wa Horebu. Uupige mwamba na maji yatatoka ndani yake kwa ajili ya watu kunywa.” Kwa hiyo Mose akafanya haya mbele ya wazee wa Israeli. 7 Naye akapaita mahali pale Masa, na Meriba kwa sababu Waisraeli waligombana na kumjaribu Bwana wakisema, “Je, Bwana yu pamoja nasi au la?”

  29. 23 Watu hawa watatu walianguka ndani ya tanuru iwakayo moto wakiwa wamefungwa kwa uthabiti sana.

    24 Ndipo Mfalme Nebukadneza akashangaa, akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hawakuwa watu watatu ambao tuliwafunga na kuwatupa ndani ya moto?”

    Washauri wakajibu, “Hakika, ee mfalme.”

    25 Mfalme akasema, “Tazama! Naona watu wanne wakitembeatembea ndani ya moto, hawajafungwa wala kudhurika, naye mtu yule wa nne anaonekana kama mwana wa miungu.”

    26 Ndipo Nebukadneza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iwakayo moto na kupaza sauti, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, tokeni! Njooni hapa!”

    Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka ndani ya moto. 27 Nao maliwali, wasimamizi, watawala na washauri wa mfalme wakakusanyika kuwazunguka. Waliona kwamba moto haukudhuru miili yao, wala unywele wa vichwa vyao haukuungua, majoho yao hayakuungua, wala hapakuwepo na harufu ya moto kwenye miili yao.

    28 Ndipo Nebukadneza akasema, “Ahimidiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, ambaye amemtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake. Walimtumaini na kukaidi amri ya mfalme, nao wakawa tayari kufa kuliko kutumikia au kuabudu mungu mwingine yeyote isipokuwa Mungu wao. 29 Kwa hiyo ninaamuru kwamba watu wa taifa lolote au lugha yoyote watakaosema kitu chochote dhidi ya Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego wakatwe vipande vipande na nyumba zao zifanywe kuwa malundo ya kokoto, kwa maana hakuna mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.”

  30. 14 Walipowafikia wale wanafunzi wengine, wakawakuta wamezungukwa na umati mkubwa wa watu na baadhi ya walimu wa sheria wakibishana nao. 15 Mara wale watu walipomwona Yesu, wakastaajabu sana, wakamkimbilia ili kumsalimu.

    16 Akawauliza wanafunzi wake, “Mnabishana nao kuhusu nini?”

    17 Mtu mmoja miongoni mwa ule umati wa watu akajibu, “Mwalimu, nilimleta kwako mwanangu ambaye ana pepo mchafu anayemfanya asiweze kuongea. 18 Kila mara huyo pepo mchafu ampagaapo mwanangu, humwangusha chini na kumfanya atokwe povu mdomoni na kusaga meno, kisha mwili wake hukauka. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”

    19 Yesu akawaambia, “Enyi kizazi kisicho na imani! Nitakuwa pamoja nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni mvulana kwangu.”

    20 Nao wakamleta yule mvulana. Yule pepo mchafu alipomwona Yesu, mara akamtia yule mvulana kifafa, akaanguka, akagaagaa chini huku akitokwa na povu kinywani.

    21 Yesu akamuuliza baba yake, “Mwanao amekuwa katika hali hii tangu lini?”

    Akamjibu, “Tangu utoto wake. 22 Mara kwa mara huyo pepo mchafu amekuwa akimwangusha kwenye moto au kwenye maji ili kumwangamiza. Lakini kama unaweza kufanya jambo lolote, tafadhali tuhurumie utusaidie.”

    23 Yesu akamwambia, “Kama ukiweza kuamini, yote yawezekana kwake yeye aaminiye.”

    24 Mara baba yake yule mvulana akapiga kelele akisema, “Ninaamini. Nisaidie kutokuamini kwangu!” 25 Yesu alipoona kwamba umati wa watu unakusanyika pamoja mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akimwambia, “Wewe pepo bubu na kiziwi, nakuamuru umtoke, wala usimwingie tena!”

    26 Yule pepo mchafu akiisha kupiga kelele, akamtia kifafa kwa nguvu, na akamtoka. Yule mvulana alikuwa kama maiti, hivyo watu wengi wakasema, “Amekufa.” 27 Lakini Yesu akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama.

    28 Baada ya Yesu kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamuuliza wakiwa peke yao, “Mbona sisi hatukuweza kumtoa huyo pepo mchafu?”

    29 Yesu akawajibu, “Hali hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa kuomba na kufunga.”

  31. 1 Siku moja Petro na Yohana walikuwa wanapanda kwenda Hekaluni kusali yapata saa tisa alasiri. 2 Basi palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa kiwete tangu kuzaliwa. Alichukuliwa na kuwekwa kwenye lango la Hekalu liitwalo Zuri, kila siku ili aombe msaada kwa watu wanaoingia Hekaluni. 3 Huyu mtu alipowaona Petro na Yohana wakikaribia kuingia Hekaluni, akawaomba wampe sadaka. 4 Wakamkazia macho, kisha Petro akamwambia, “Tutazame sisi.” 5 Hivyo yule mtu akawatazama, akitazamia kupata kitu kutoka kwao.

    6 Ndipo Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!” 7 Petro akamshika yule mtu kwa mkono wa kuume akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikapata nguvu. 8 Akaruka juu na kusimama, akaanza kutembea. Kisha akaingia Hekaluni pamoja na Petro na Yohana, huku akitembea na kurukaruka na kumsifu Mungu. 9 Watu wote walipomwona akitembea na kumsifu Mungu, 10 wakamtambua kuwa ni yule mtu aliyekuwa akiketi nje ya Hekalu penye lango liitwalo Zuri akiomba msaada, nao wakajawa na mshangao, wakastaajabu juu ya yale yaliyomtukia.

  32. 8 Lakini Elima yule mchawi (hii ndiyo maana ya jina lake), aliwapinga Barnaba na Sauli na kujaribu kumpotosha yule mkuu wa kile kisiwa aiache imani. 9 Ndipo Sauli, ambaye pia aliitwa Paulo, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akamkazia macho Elima huyo mchawi, 10 akamwambia, “Ewe mwana wa ibilisi, wewe ni adui wa kila kilicho haki! Umejaa kila aina ya udanganyifu na ulaghai. Je, hutaacha kuzipotosha njia za Bwana zilizonyooka? 11 Nawe sasa sikiliza, mkono wa Bwana u dhidi yako. Utakuwa kipofu, wala hutaona jua kwa muda.”

    Mara ukungu na giza vikamfunika, naye akaenda huku na huko akitafuta mtu wa kumshika mkono ili amwonyeshe njia. 12 Yule mkuu wa kile kisiwa alipoona yaliyotukia, akaamini kwa sababu alistaajabishwa na mafundisho kuhusu Bwana.

  33. 6 Ndipo Bwana akapeleka nyoka wenye sumu katikati yao; wakawauma watu, nao Waisraeli wengi wakafa. 7 Watu wakamjia Mose na kusema, “Tumetenda dhambi wakati tuliponena dhidi ya Bwana na dhidi yako. Mwombe Bwana ili atuondolee hawa nyoka.” Hivyo Mose akawaombea hao watu.

    8 Bwana akamwambia Mose, “Tengeneza nyoka wa shaba na umweke juu ya mti; yeyote aliyeumwa na nyoka anaweza kumtazama na akaishi tena.” 9 Kwa hiyo Mose akatengeneza nyoka wa shaba na kumweka juu ya mti. Kisha wakati mtu yeyote aliumwa na nyoka, naye akamtazama yule nyoka wa shaba, aliishi.

  34. 3 Siku iyo hiyo, mtu wa Mungu akatoa ishara: “Hii ndiyo ishara Bwana aliyotangaza: Madhabahu haya yatapasuka na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.”

    4 Mfalme Yeroboamu aliposikia kile mtu wa Mungu alichosema, alipopiga kelele dhidi ya madhabahu huko Betheli, akanyoosha mkono wake kutoka madhabahuni na kusema, “Mkamate!” Lakini mkono aliokuwa ameunyoosha kumwelekea yule mtu ukasinyaa na kubaki hapo hapo, kiasi kwamba hakuweza kuurudisha. 5 Pia, madhabahu yalipasuka na majivu yakamwagika sawasawa na ishara iliyotolewa na mtu wa Mungu kwa neno la Bwana.

    6 Kisha mfalme akamwambia mtu wa Mungu, “Niombee kwa Bwana Mungu wako ili mkono wangu upate kupona.” Kwa hiyo mtu wa Mungu akamwombea kwa Bwana, nao mkono wa mfalme ukapona na kuwa kama ulivyokuwa hapo kwanza.

    7 Mfalme akamwambia yule mtu wa Mungu, “Twende nyumbani kwangu upate chakula, nami nitakupa zawadi.”

  35. 14 Yesu alipoingia nyumbani kwa Petro, alimkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, akiwa ana homa. 15 Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, naye akainuka na kuanza kumhudumia.

    16 Jioni ile, wakamletea watu wengi waliopagawa na pepo wachafu, naye akawatoa wale pepo wachafu kwa neno lake, na kuwaponya wagonjwa wote. 17 Haya yalifanyika ili litimie lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kwamba:

    “Mwenyewe alitwaa udhaifu wetu

    na alichukua magonjwa yetu.”

  36. 16 Inua fimbo yako na unyooshe mkono wako juu ya bahari ili kuyagawa maji, hivyo kwamba Waisraeli wapate kupita mahali pakavu baharini. 17 Nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu kusudi waingie baharini wakiwafuatia. Nami nitajipatia utukufu kupitia Farao pamoja na jeshi lake lote, kupitia magari yake ya vita na wapanda farasi wake. 18 Nao Wamisri watajua kwamba Mimi ndimi Bwana nitakapojipatia utukufu kupitia Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake.”

    19 Ndipo malaika wa Mungu, aliyekuwa akisafiri mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akakaa nyuma yao. Pia ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao na kusimama nyuma, 20 ikakaa kati ya majeshi ya Misri na Israeli. Usiku kucha wingu likaleta giza upande mmoja na nuru kwa upande mwingine, kwa hiyo hakuna aliyemkaribia mwenzake usiku kucha.

    21 Ndipo Mose akanyoosha mkono wake juu ya bahari, naye Bwana akayasukuma maji ya bahari nyuma kwa upepo mkali wa mashariki usiku ule wote na kupafanya nchi kavu. Maji yakagawanyika, 22 nao Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, maji yakiwa ukuta upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto.

    23 Wamisri wakawafuatia ndani ya bahari, pamoja na farasi wote wa Farao, magari ya vita na wapanda farasi. 24 Karibia mapambazuko, Bwana akaliangalia jeshi la Wamisri kutoka ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha. 25 Mungu akayaondoa magurudumu ya magari yao, kwa hivyo wakayaendesha kwa shida. Nao Wamisri wakasema, “Tuachane na Waisraeli! Bwana anawapigania dhidi ya Misri.”

    26 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Nyoosha mkono wako juu ya bahari ili maji yarudiane yawafunike Wamisri, magari yao ya vita na wapanda farasi wao.” 27 Mose akanyoosha mkono wake juu ya bahari, wakati wa mapambazuko bahari ikarudiana na kuwa kama kawaida. Wamisri wakajaribu kuyakimbia maji, lakini Bwana akawasukumia ndani ya bahari. 28 Maji yakarudiana na kuyafunika magari ya vita na wapanda farasi pamoja na jeshi lote la Farao lililokuwa limewafuata Waisraeli ndani ya bahari. Hakuna hata mmoja wao aliyenusurika.

    29 Lakini Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, ukiwepo ukuta wa maji upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto. 30 Siku ile Bwana akawaokoa Waisraeli kutoka mikononi mwa Wamisri, nao Waisraeli wakawaona Wamisri wamelala ufuoni mwa bahari wakiwa wamekufa. 31 Basi Waisraeli walipoona uwezo mkubwa Bwana aliodhihirisha dhidi ya Wamisri, watu wakamwogopa Bwana na wakaweka tumaini lao kwake na kwa Mose mtumishi wake.

  37. 6 Kisha Eliya akamwambia, “Kaa hapa. Bwana amenituma kwenda Yordani.”

    Naye akamjibu, “Kwa hakika kama Bwana aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wote wawili wakaendelea pamoja.

    7 Wana hamsini wa manabii wakaenda na kusimama kwa mbali, kuelekea mahali ambapo Eliya na Elisha walikuwa wamesimama kando ya Mto Yordani. 8 Eliya akachukua vazi lake, akalisokota na kupiga nalo maji. Maji yakagawanyika upande wa kuume na upande wa kushoto, nao wawili wakavuka pakavu.

    9 Walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, “Niambie, nikufanyie nini kabla sijaondolewa kutoka kwako?”

    Elisha akajibu, “Naomba nirithi sehemu maradufu ya roho yako.”

    10 Eliya akasema, “Umeomba jambo gumu. Lakini kama utaniona wakati ninapoondolewa kutoka kwako litakuwa lako. La sivyo, hautalipata.”

    11 Walipokuwa wakitembea pamoja na kuzungumza, ghafula gari la moto na farasi wa moto vilitokea na kuwatenganisha wao wawili, naye Eliya akapanda mbinguni katika upepo wa kisulisuli. 12 Elisha aliona hili, naye akapaza sauti, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya Israeli na wapanda farasi wake!” Naye Elisha hakumwona tena. Kisha akazishika nguo zake mwenyewe na kuzirarua.

    13 Akaliokota lile vazi lililoanguka kutoka kwa Eliya, kisha akarudi na kusimama ukingoni mwa Yordani. 14 Ndipo akalichukua lile vazi ambalo lilikuwa limeanguka kutoka kwa Eliya, naye akayapiga yale maji nalo. Akauliza, “Yuko wapi sasa Bwana, Mungu wa Eliya?” Elisha alipoyapiga maji, yakagawanyika kulia na kushoto, naye akavuka.

  38. 1 Yesu aliposhuka kutoka mlimani, makutano makubwa ya watu yakamfuata. 2 Mtu mmoja mwenye ukoma akaja na kupiga magoti mbele yake, akasema, “Bwana, kama ukitaka, unaweza kunitakasa.”

    3 Yesu akanyoosha mkono wake akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Mara yule mtu akatakasika ukoma wake. 4 Kisha Yesu akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote. Lakini nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na utoe sadaka aliyoamuru Mose, ili kuwa ushuhuda kwao.”

  39. 13 Simoni naye akaamini na akabatizwa. Akamfuata Filipo kila mahali, akistaajabishwa na ishara kuu na miujiza aliyoiona.

  40. 10 Elisha akamtuma mjumbe kumwambia, “Nenda uoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itapona, nawe utatakasika.”

    11 Lakini Naamani akaondoka akiwa amekasirika, akasema, “Hakika nilidhani kwamba angetoka nje, asimame na kuliitia jina la Bwana Mungu wake, na kuweka mkono wake juu ya mahali pagonjwa, aniponye ukoma wangu. 12 Je, Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora zaidi kuliko mito yoyote ya Israeli? Je, nisingeweza kuoga ndani ya hiyo mito na kutakasika?” Basi akageuka na kuondoka kwa hasira kuu.

    13 Watumishi wa Naamani wakamwendea na kumwambia, “Baba yangu, kama huyo nabii angekuambia kufanya jambo lililo kubwa, je, usingelifanya? Je, si zaidi sana basi, anapokuambia, ‘Oga na utakasike!’ ” 14 Hivyo akashuka na kujizamisha ndani ya Yordani mara saba, kama vile huyo mtu wa Mungu alivyokuwa amemwambia, nayo nyama ya mwili wake ikapona na kutakasika kama ya mwili wa mvulana mdogo.

  41. 20 Wale watu walipofika kwa Yesu wakamwambia, “Yohana Mbatizaji ametutuma tukuulize, ‘Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?’ ”

    21 Wakati huo huo, Yesu aliwaponya wengi waliokuwa na magonjwa, maradhi na pepo wachafu, na pia akawafungua vipofu wengi macho wakapata kuona. 22 Hivyo akawajibu wale wajumbe, “Rudini mkamwambie Yohana yote mnayoyaona na kuyasikia: Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa habari njema.

  42. 47 Yesu alipokuwa bado anazungumza, umati mkubwa wa watu ukaja. Uliongozwa na Yuda, ambaye alikuwa mmoja wa wale wanafunzi Kumi na Wawili. Akamkaribia Yesu ili ambusu. 48 Lakini Yesu akamwambia, “Yuda, je, unamsaliti Mwana wa Adamu kwa busu?”

    49 Wafuasi wa Yesu walipoona yale yaliyokuwa yanakaribia kutokea, wakasema, “Bwana, tuwakatekate kwa panga zetu?” 50 Mmoja wao akampiga mtumishi wa kuhani mkuu kwa upanga, akamkata sikio la kuume.

    51 Lakini Yesu akasema, “Acheni!” Akaligusa lile sikio la yule mtu na kumponya.

  43. 1 Yesu alipokuwa akipita, akamwona mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa. 2 Wanafunzi wake wakamuuliza, “Rabi, ni nani aliyetenda dhambi, ni huyu mtu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?”

    3 Yesu akawajibu, “Huyu mtu wala wazazi wake hawakutenda dhambi. Alizaliwa kipofu ili kazi za Mungu zidhihirishwe katika maisha yake. 4 Yanipasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenituma wakati bado ni mchana, kwa kuwa usiku waja ambapo hakuna mtu awezaye kufanya kazi. 5 Wakati niko ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.”

    6 Baada ya kusema haya, akatema mate ardhini, akatengeneza tope kwa mate na kumpaka yule mtu kipofu machoni. 7 Kisha akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.” (Siloamu maana yake ni aliyetumwa.) Ndipo yule kipofu akaenda, akanawa, naye akarudi akiwa anaona.

  44. 23 Yesu akapita katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu. 24 Kwa hiyo sifa zake zikaenea sehemu zote za Shamu, nao watu wakamletea wote waliokuwa na magonjwa mbalimbali na maumivu, waliopagawa na pepo wachafu, wenye kifafa na waliopooza, naye akawaponya. 25 Makutano makubwa ya watu yakawa yanamjia kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Uyahudi na kutoka ngʼambo ya Mto Yordani.

  45. 38 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamwambia, “Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako.”

    39 Lakini yeye akawajibu, “Kizazi kiovu na cha uzinzi kinaomba ishara! Lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ishara ya nabii Yona. 40 Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ndani ya tumbo la nyangumi kwa siku tatu, usiku na mchana, vivyo hivyo Mwana wa Adamu atakuwa katika moyo wa nchi siku tatu, usiku na mchana. 41 Siku ya hukumu watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu; kwa maana wao walitubu waliposikia mahubiri ya Yona. Na tazama, hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona. 42 Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kukihukumu kizazi hiki. Kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Solomoni. Na hapa yupo aliye mkuu kuliko Solomoni.”

  46. 29 Yesu akaondoka na kwenda kando ya Bahari ya Galilaya. Kisha akapanda mlimani, akaketi huko. 30 Umati mkubwa wa watu ukamjia, wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; naye akawaponya. 31 Hao watu wakashangaa walipoona bubu wakisema, vilema wakipona, viwete wakitembea na vipofu wakiona, wakamtukuza Mungu wa Israeli.

  47. 16 Ilipofika jioni, wanafunzi wake waliteremka kwenda baharini. 17 Wakaingia kwenye mashua, wakaanza kuvuka bahari kwenda Kapernaumu. Wakati huu kulikuwa tayari giza na Yesu alikuwa hajajumuika nao. 18 Bahari ikachafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma. 19 Wanafunzi walipokuwa wamekwenda mwendo wa karibu maili tatu au nne, walimwona Yesu akitembea juu ya maji akikaribia mashua, nao wakaogopa sana. 20 Lakini Yesu akawaambia, “Ni mimi. Msiogope.” 21 Ndipo wakamkaribisha kwa furaha ndani ya mashua, na mara wakafika ufuoni walikokuwa wakienda.

  48. 32 Sasa uliza kuhusu siku za zamani, zamani kabla ya wakati wako, tangu siku ile Mungu alipomuumba mtu juu ya nchi, uliza kutoka mwisho mmoja wa mbingu mpaka mwisho mwingine wa mbingu. Je, kumepata kutokea jambo jingine lililo kubwa kama hili, au kuna jambo jingine kama hilo limepata kusikiwa? 33 Je, kuna watu wengine wowote waliosikia sauti ya Mungu ikizungumza kwenye moto, kama mlivyosikia, nao wakaishi? 34 Je, kuna mungu yeyote amepata kujaribu mwenyewe kuchukua taifa moja kutoka taifa lingine, kwa mapigo, kwa ishara za miujiza na maajabu, kwa vita, kwa mkono wenye nguvu na mkono ulionyooshwa au kwa matendo makuu ya kutisha, kama yale ambayo Bwana Mungu wenu aliyofanya kwa ajili yenu huko Misri mbele ya macho yenu?

    35 Mlionyeshwa mambo haya ili mpate kujua kuwa Bwana ndiye Mungu; hakuna mwingine ila yeye. 36 Kutoka mbinguni amewasikizisha sauti yake ili kuwaadilisha. Hapa duniani aliwaonyesha moto wake mkubwa, nanyi mlisikia maneno yake kutoka kwenye ule moto.

  49. 19 Watu wa mji wakamwambia Elisha, “Tazama, bwana wetu, mahali mji huu ulipojengwa ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo, lakini maji yake ni mabaya, na nchi haizai.”

    20 Akasema, “Nileteeni bakuli mpya, mweke chumvi ndani yake.” Kwa hiyo wakamletea.

    21 Kisha akaenda kwenye chemchemi na kuitupa ile chumvi ndani yake, akisema, “Hili ndilo asemalo Bwana: ‘Nimeyaponya maji haya. Kamwe hayatasababisha mauti tena wala kutozaa.’ ” 22 Nayo yale maji yakaponywa mpaka leo, sawasawa na neno la Elisha alilokuwa amesema.

  50. 5 Mmoja wao alipokuwa anakata mti, shoka lilitumbukia kwenye maji. Akalia, “Ee bwana wangu, shoka lilikuwa la kuazima!”

    6 Mtu wa Mungu akauliza, “Je, liliangukia wapi?” Alipomwonyesha mahali penyewe, Elisha akakata kijiti na kukitupa mahali pale, nalo shoka likaelea. 7 Akasema, “Lichukue.” Kisha yule mtu akanyoosha mkono wake, akalichukua.

  51. 18 Wakati adui waliposhuka kumwelekea, Elisha akamwomba Bwana: “Wapige watu hawa kwa upofu.” Basi Mungu akawapiga kwa upofu, kama Elisha alivyoomba.

    19 Elisha akawaambia, “Hii sio njia yenyewe, na huu sio huo mji. Nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa huyo mtu mnayemtafuta.” Naye akawapeleka Samaria.

    20 Baada ya kuingia mjini, Elisha akasema, “Bwana, yafungue macho ya watu hawa ili wapate kuona.” Ndipo Bwana akayafungua macho yao, na walipotazama, kumbe hapo ndipo walipojikuta, ndani ya Samaria.

    21 Wakati mfalme wa Israeli alipowaona, akamuuliza Elisha, “Je, baba yangu, niwaue?”

    22 Naye akajibu, “Usiwaue. Je, utawaua watu uliowateka kwa upanga wako mwenyewe na upinde wako? Wape chakula na maji ili wapate kula na kunywa, na kisha wamrudie bwana wao.” 23 Basi akawaandalia karamu kubwa, na baada ya kula na kunywa, akawaaga nao wakarudi kwa bwana wao. Hivyo, vikosi kutoka Aramu vikakoma kuvamia nchi ya Israeli.

  52. 20 Elisha akafa, nao wakamzika.

    Vikosi vya Wamoabu vilikuwa vinashambulia nchi kwa vita kila mwaka wakati wa vuli. 21 Ikawa Waisraeli fulani walipokuwa wanamzika mtu, ghafula wakaona kikosi cha washambuliaji, basi wakaitupa ile maiti ya yule mtu ndani ya kaburi la Elisha. Wakati ile maiti ilipogusa mifupa ya Elisha, yule mtu akafufuka na kusimama kwa miguu yake.

  53. 36 Wakauacha ule umati wa watu, na wakamchukua vile alivyokuwa kwenye mashua. Palikuwa pia na mashua nyingine nyingi pamoja naye. 37 Kukawa na dhoruba kali, nayo mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikawa karibu kujaa maji. 38 Yesu alikuwa katika shetri, akiwa analala juu ya mto. Wanafunzi wake wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, hujali kama tunazama?”

    39 Akaamka, akaukemea ule upepo, akayaambia yale mawimbi, “Uwe kimya! Tulia!” Ule upepo ukatulia, kukawa shwari kabisa.

    40 Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa hivyo? Je, bado hamna imani?”

    41 Nao wakawa wameogopa sana, wakaulizana, “Ni nani huyu ambaye hata upepo na mawimbi vinamtii?”

  54. 2 Huyu alimjia Yesu usiku akamwambia, “Rabi, tunajua kuwa wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, kwa maana hakuna mtu awezaye kufanya miujiza hii uifanyayo wewe, kama Mungu hayuko pamoja naye.”

  55. 15 Hata wakawa wanawaleta wagonjwa na kuwalaza kwenye magodoro na kwenye vitanda barabarani ili yamkini Petro akipita kivuli chake kiwaguse baadhi yao. 16 Pia watu wakakusanyika kutoka miji iliyokuwa karibu na Yerusalemu, wakileta wagonjwa na watu walioteswa na pepo wachafu. Hao wote wakaponywa.

  56. 28 Ndipo Mose akasema, “Hivi ndivyo mtakavyojua kuwa Bwana amenituma kufanya mambo haya, na kwamba halikuwa wazo langu. 29 Ikiwa watu hawa watakufa kifo cha kawaida na kupatwa na yale ya kawaida yanayowapata wanadamu, basi Bwana hakunituma mimi. 30 Lakini ikiwa Bwana ataleta jambo jipya kabisa, ardhi ikifunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na kila kitu kilicho mali yao, nao washuke chini kaburini wakiwa hai, ndipo mtafahamu kuwa watu hawa wamemdharau Bwana.”

    31 Mara Mose alipomaliza kusema haya yote, ardhi iliyokuwa chini yao ikapasuka, 32 nchi ikafunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na jamaa zao, na watu wote wa Kora na mali zao zote. 33 Wakashuka chini kaburini wakiwa hai, pamoja na kila kitu walichokuwa nacho; nchi ikajifunika juu yao, nao wakaangamia wakatoweka kutoka kusanyiko. 34 Kutoka kilio chao, Waisraeli wote waliowazunguka walikimbia, wakipaza sauti, “Nchi inatumeza na sisi pia!”

    35 Moto ukaja kutoka kwa Bwana, ukawateketeza wale watu 250 waliokuwa wakifukiza uvumba.

  57. 7 Bwana akamwambia Mose, 8 “Chukua ile fimbo, na wewe na ndugu yako Aroni mkusanye kusanyiko pamoja. Nena na ule mwamba mbele ya macho yao, nao utatoa maji yake. Utatoa maji kutoka huo mwamba kwa ajili ya jumuiya ili wao na mifugo yao waweze kunywa.”

    9 Kwa hiyo Mose akaichukua hiyo fimbo kutoka pale ilipokuwa mbele za Bwana kama alivyomwagiza. 10 Mose na Aroni wakakusanya kusanyiko pamoja mbele ya huo mwamba, naye Mose akawaambia, “Sikilizeni, enyi waasi. Je, ni lazima tuwatoleeni maji kutoka mwamba huu?” 11 Ndipo Mose akainua mkono wake na kuupiga mwamba mara mbili kwa fimbo yake. Maji yakabubujika, nayo jumuiya na mifugo yao wakanywa.

  58. 13 Mara tu nyayo za makuhani walichukualo Sanduku la Bwana, Bwana wa dunia yote, zitakapokanyaga ndani ya Mto Yordani, maji hayo yatiririkayo kutoka juu yatatindika na kusimama kama chuguu.”

    14 Basi, watu walipovunja kambi ili kuvuka Yordani, makuhani wakiwa wamebeba Sanduku la Agano waliwatangulia. 15 Wakati huu ulikuwa wakati wa mavuno, nao Mto Yordani ulikuwa umefurika hadi kwenye kingo zake. Ilikuwa kawaida ya Yordani kufurika nyakati zote za mavuno. Mara tu makuhani wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Agano walipofika mtoni na nyayo zao kuzama ndani ya yale maji, 16 maji hayo yaliyotiririka kutoka upande wa juu yaliacha kutiririka yakasimama kama chuguu mbali kabisa nao, kwenye mji ulioitwa Adamu kwenye eneo la Sarethani, wakati yale maji yaliyokuwa yanatiririka kuingia kwenye Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), yalitindika kabisa. Hivyo watu wakavuka kukabili Yeriko.

    17 Wale makuhani waliobeba Sanduku la Agano la Bwana, wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Mto Yordani, wakati Waisraeli wote wakiwa wanapita hadi taifa lote likaisha kuvuka mahali pakavu.

  59. 13 Eliya akamwambia, “Usiogope. Nenda nyumbani ukafanye kama ulivyosema. Lakini kwanza unitengenezee mimi mkate mdogo kutoka vile ulivyo navyo kisha uniletee na ndipo utayarishe chochote kwa ajili yako na mwanao. 14 Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Lile gudulia la unga halitakwisha wala ile chupa ya mafuta haitakauka hadi siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi.’ ”

    15 Akaondoka na kufanya kama Eliya alivyomwambia. Kwa hiyo kukawa na chakula kila siku kwa ajili ya Eliya, yule mwanamke na jamaa yake. 16 Kwa kuwa lile gudulia la unga halikwisha na ile chupa ya mafuta haikukauka, sawasawa na lile neno la Bwana alilosema Eliya.

  60. 20 Ndipo Ahabu akatuma ujumbe katika Israeli yote na kuwakusanya manabii hao juu ya mlima Karmeli. 21 Eliya akasimama mbele ya watu na kusema, “Mtasitasita katika mawazo mawili hadi lini? Ikiwa Bwana ndiye Mungu, mfuateni yeye; lakini ikiwa Baali ni Mungu, basi mfuateni yeye.”

    Lakini watu hawakusema kitu.

    22 Kisha Eliya akawaambia, “Ni mimi peke yangu nabii wa Bwana aliyebaki, lakini Baali ana manabii mia nne na hamsini. 23 Leteni mafahali wawili. Wao na wajichagulie mmoja, wamkate vipande vipande na waweke juu ya kuni lakini wasiiwashie moto. Nitamwandaa huyo fahali mwingine na kumweka juu ya kuni lakini sitawasha moto. 24 Kisha mliitie jina la mungu wenu, nami nitaliitia jina la Bwana Mungu yule ambaye atajibu kwa moto, huyo ndiye Mungu.”

    Kisha watu wote wakasema, “Hilo unalosema ni jema.”

    25 Eliya akawaambia manabii wa Baali, “Chagueni mmoja kati ya hawa mafahali na mwe wa kwanza kumwandaa, kwa kuwa ninyi mko wengi sana. Liitieni jina la mungu wenu, lakini msiwashe moto.” 26 Kwa hiyo wakamchukua yule fahali waliyepewa, nao wakamwandaa.

    Kisha wakaliitia jina la Baali kutoka asubuhi hadi adhuhuri, wakapiga kelele, “Ee Baali, utujibu!” Lakini hapakuwa na jibu; hakuna aliyejibu. Nao wakacheza kuizunguka madhabahu waliyoijenga.

    27 Wakati wa adhuhuri, Eliya akaanza kuwadhihaki, akisema, “Pigeni kelele zaidi! Hakika yeye ni mungu! Labda amezama katika mawazo mazito, au ana shughuli nyingi, au amesafiri. Labda amelala usingizi mzito, naye ni lazima aamshwe.” 28 Kwa hiyo wakapiga kelele zaidi na kama ilivyokuwa desturi yao wakajichanja wenyewe kwa visu na vyembe, mpaka damu ikachuruzika. 29 Adhuhuri ikapita, nao wakaendelea na utabiri wao wa kiwazimu mpaka wakati wa dhabihu ya jioni. Lakini hapakuwa na jibu, hakuna aliyejibu, hakuna aliyeangalia.

    30 Kisha Eliya akawaambia watu wote, “Sogeeni karibu nami.” Watu wote wakamkaribia, naye akakarabati madhabahu ya Bwana, ambayo ilikuwa imevunjwa. 31 Eliya akachukua mawe kumi na mawili, moja kwa ajili ya kila kabila la wana wa Yakobo, ambaye neno la Bwana lilimjia, likisema, “Jina lako litakuwa Israeli.” 32 Kwa mawe hayo, akajenga madhabahu katika jina la Bwana, na akachimba handaki kuizunguka, ukubwa wa kutosha vipimo viwili vya mbegu. 33 Akapanga kuni, akamkata yule fahali vipande vipande na kuvipanga juu ya kuni. Kisha akawaambia, “Jazeni mapipa manne maji na kuyamwaga juu ya sadaka ya kuteketezwa na juu ya kuni.”

    34 Akawaambia, “Fanyeni hivyo tena.” Nao wakafanya hivyo tena.

    Akaagiza, “Fanyeni kwa mara ya tatu.” Nao wakafanya hivyo kwa mara ya tatu. 35 Maji yakatiririka kuizunguka madhabahu na hata kujaza lile handaki.

    36 Wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, nabii Eliya akasogea mbele na kuomba, akisema: “Ee Bwana, Mungu wa Abrahamu, na Isaki na Israeli, ijulikane leo kwamba wewe ndiye Mungu katika Israeli na ya kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. 37 Unijibu mimi, Ee Bwana, nijibu mimi, ili watu hawa wajue kwamba wewe, Ee Bwana, ndiwe Mungu, na kwamba unaigeuza mioyo yao ikurudie tena.”

    38 Kisha moto wa Bwana ukashuka na kuiteketeza ile dhabihu, zile kuni, yale mawe, ule udongo, na pia kuramba yale maji yaliyokuwa ndani ya handaki.

    39 Wakati watu wote walipoona hili, wakaanguka kifudifudi na kulia, “Bwana: yeye ndiye Mungu! Bwana: yeye ndiye Mungu!”

    40 Kisha Eliya akawaamuru, “Wakamateni hao manabii wa Baali. Msimwache hata mmoja atoroke!” Wakawakamata, naye Eliya akawaleta mpaka Bonde la Kishoni na kuwachinja huko.

  61. 9 Ndipo mfalme akamtuma mkuu mmoja wa kikosi pamoja na kikosi chake cha askari hamsini kwa nabii Eliya. Yule mkuu wa kikosi akamwendea Eliya, aliyekuwa ameketi juu ya kilima, na kumwambia, “Mtu wa Mungu, mfalme anasema, ‘Shuka chini!’ ”

    10 Eliya akamjibu yule mkuu wa kikosi, “Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni ukuteketeze wewe na watu wako hamsini!” Ndipo moto ukashuka kutoka mbinguni na kuwateketeza yule mkuu wa kikosi pamoja na watu wake.

    11 Aliposikia hili, mfalme akatuma kwa Eliya mkuu wa kikosi mwingine na askari wake hamsini. Yule mkuu wa kikosi akamwambia Eliya, “Mtu wa Mungu, hili ndilo asemalo mfalme, ‘Shuka chini mara moja!’ ”

    12 Eliya akajibu, “Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni ukuteketeze wewe na watu wako hamsini!” Ndipo moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza yeye na watu wake hamsini.

  62. 9 Isaya akajibu, “Hii ndiyo ishara ya Bwana kwako kwamba Bwana atafanya kile alichoahidi: Je, kivuli kiende hatua kumi mbele, au kivuli kirudi nyuma hatua kumi?”

    10 Hezekia akasema, “Ni jambo rahisi kwa kivuli kutangulia mbele hatua kumi, kuliko kukifanya kirudi nyuma hatua kumi.”

    11 Ndipo nabii Isaya akamwita Bwana, naye Bwana akakifanya kivuli kurudi nyuma hatua kumi ambazo kilikuwa kimeshuka kwenye ngazi ya Ahazi.

  63. 20 Ndipo Yesu akaanza kushutumu miji ambamo alifanya miujiza yake mingi kuliko kwingine, kwa maana watu wake hawakutubu. 21 “Ole wako, Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa maana kama miujiza iliyofanyika kwenu, ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu. 22 Lakini nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi. 23 Nawe Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa mpaka kuzimu. Miujiza iliyofanyika kwako ingefanyika huko Sodoma, mji huo ungalikuwepo hadi leo. 24 Lakini nakuambia kwamba, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ya hukumu kuliko wewe.”

  64. 22 Wakafika Bethsaida na baadhi ya watu wakamleta mtu mmoja kipofu wakamsihi Yesu amguse. 23 Yesu akamshika mkono huyo kipofu akampeleka nje ya kijiji. Baada ya kuyatemea mate macho ya yule kipofu na kumwekea mikono, Yesu akamuuliza, “Unaona chochote?”

    24 Yule kipofu akaangalia, akasema, “Ninaona watu, wanaonekana kama miti inayotembea.”

    25 Yesu akamwekea tena mikono machoni. Kisha macho yake yakafunguka, kuona kwake kukarejea naye akaona kila kitu dhahiri. 26 Yesu akamuaga aende nyumbani kwake, akimwambia, “Hata kijijini usiingie.”

  65. 11 Baadaye kidogo, Yesu alikwenda katika mji mmoja ulioitwa Naini. Nao wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu walikwenda pamoja naye. 12 Alipokaribia lango la mji, alikutana na watu waliokuwa wamebeba maiti wakitoka nje ya mji. Huyu aliyekufa alikuwa mwana pekee wa mwanamke mjane. Umati mkubwa wa watu wa mji ule ulikuwa pamoja na huyo mwanamke. 13 Bwana Yesu alipomwona yule mjane, moyo wake ulimhurumia, akamwambia, “Usilie.”

    14 Kisha akasogea mbele akaligusa lile jeneza na wale waliokuwa wamelibeba wakasimama kimya. Akasema, “Kijana, nakuambia inuka.” 15 Yule aliyekuwa amekufa akaketi akaanza kuongea, naye Yesu akamkabidhi kwa mama yake.

    16 Watu wote wakajawa na hofu ya Mungu, nao wakamtukuza Mungu wakisema, “Nabii mkuu ametokea miongoni mwetu, Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.”

  66. 12 Ilipokaribia jioni, wale mitume kumi na wawili wakaenda kwa Yesu na kumwambia, “Waage makutano ili waende vijijini jirani na mashambani, ili wapate chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tuko nyikani.”

    13 Yesu akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.”

    Nao wakajibu, “Hatuna zaidi ya mikate mitano na samaki wawili. Labda twende tukanunue chakula cha kuwatosha watu hawa wote.” 14 Walikuwako wanaume wapatao 5,000.

    Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Waketisheni katika makundi ya watu hamsini hamsini.” 15 Wanafunzi wakafanya hivyo, wakawaketisha wote. 16 Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akavibariki na kuvimega. Kisha akawapa wanafunzi ili wawagawie watu. 17 Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili.

  67. 1 Ikawa siku moja Yesu alipokuwa amekwenda kula chakula kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo siku ya Sabato, watu walikuwa wakimchunguza kwa bidii. 2 Papo hapo mbele yake palikuwa na mtu mmoja mwenye ugonjwa wa kuvimba mwili. 3 Yesu akawauliza wale Mafarisayo na walimu wa sheria, “Je, ni halali kuponya watu siku ya Sabato au la?” 4 Wakakaa kimya. Hivyo Yesu akamshika yule mgonjwa mkono na kumponya, akamruhusu aende zake.

    5 Kisha akawauliza, “Kama mmoja wenu angekuwa na mtoto au ngʼombe wake aliyetumbukia katika kisima siku ya Sabato, je, hamtamvuta mara moja na kumtoa?” 6 Nao hawakuwa na la kusema.

  68. 19 “Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, ambaye aliishi kwa anasa kila siku. 20 Hapo penye mlango wake aliishi maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima. 21 Huyo Lazaro alitamani kujishibisha kwa makombo yaliyoanguka kutoka mezani kwa yule tajiri. Hata mbwa walikuwa wakija na kuramba vidonda vyake.

    22 “Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Abrahamu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa. 23 Kule kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Abrahamu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa karibu yake. 24 Hivyo yule tajiri akamwita, ‘Baba Abrahamu, nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu.’

    25 “Lakini Abrahamu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu. 26 Zaidi ya hayo, kati yetu na ninyi huko kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu yeyote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu.’

    27 “Akasema, ‘Basi, nakuomba, umtume Lazaro aende nyumbani kwa baba yangu, 28 maana ninao ndugu watano. Awaonye, ili wasije nao wakafika mahali hapa pa mateso.’

    29 “Abrahamu akamjibu, ‘Ndugu zako wana Maandiko ya Mose na Manabii, wawasikilize hao.’

    30 “Yule tajiri akasema, ‘Hapana, baba Abrahamu, lakini mtu kutoka kwa wafu akiwaendea, watatubu.’

    31 “Abrahamu akamwambia, ‘Kama wasipowasikiliza Mose na Manabii, hawataweza kushawishika hata kama mtu akifufuka kutoka kwa wafu.’ ”

  69. 47 Kwa hiyo viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakaita mkutano wa baraza.

    Wakaulizana, “Tufanyeje? Huyu mtu anafanya ishara nyingi. 48 Kama tukimwacha aendelee hivi, kila mtu atamwamini, nao Warumi watakuja na kupaharibu mahali petu patakatifu na taifa letu.”

  70. 12 Malaika wa sita akamimina bakuli lake kwenye mto mkubwa Frati, maji yake yakakauka ili kutayarisha njia kwa ajili ya wafalme watokao Mashariki. 13 Kisha nikaona roho wachafu watatu waliofanana na vyura wakitoka katika kinywa cha lile joka na katika kinywa cha yule mnyama na katika kinywa cha yule nabii wa uongo. 14 Hizo ndizo roho za pepo wachafu zitendazo miujiza. Nazo huwaendea wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya tayari kwa ajili ya vita katika siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.

    15 “Tazama, naja kama mwizi! Amebarikiwa yeye akeshaye na kuziweka tayari nguo zake ili asiende uchi na kuonekana aibu yake.”

    16 Ndipo wakawakusanya wafalme pamoja mahali paitwapo Armagedoni kwa Kiebrania.

  71. 10 Kisha Bwana akasema, “Hakika nitakurudia tena majira kama haya mwakani na Sara mkeo atakuwa ana mwana.”

    Sara alikuwa akiwasikiliza kwenye ingilio la hema, lililokuwa nyuma yake. 11 Abrahamu na Sara walikuwa wazee tena waliosogea miaka, naye Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. 12 Hivyo Sara akacheka kimoyomoyo alipokuwa akiwaza, “Baada ya mimi kuwa mkongwe hivi na bwana wangu amezeeka, je, nitaweza kufurahia jambo hili?”

    13 Ndipo Bwana akamwambia Abrahamu, “Kwa nini Sara amecheka na kusema, ‘Kweli nitazaa mtoto nami sasa ni mzee?’ 14 Je, kuna jambo lolote gumu lisilowezekana kwa Bwana? Nitakurudia mwakani majira kama haya, naye Sara atakuwa na mwana.”

  72. 29 Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakiondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu ulimfuata. 30 Vipofu wawili walikuwa wameketi kando ya barabara. Waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapita, wakapiga kelele wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie!”

    31 Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze, lakini wao wakazidi kupaza sauti, wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie.”

    32 Yesu akasimama na kuwaita, akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”

    33 Wakamjibu, “Bwana, tunataka kuona.”

    34 Yesu akawahurumia na kuwagusa macho yao. Mara macho yao yakapata kuona, nao wakamfuata.

  73. 9 Kijana mmoja jina lake Eutiko, alikuwa amekaa dirishani, wakati Paulo alipokuwa akihubiri kwa muda mrefu, alipatwa na usingizi mzito, akaanguka kutoka ghorofa ya tatu, wakamwinua akiwa amekufa. 10 Paulo akashuka chini, akajitupa juu yake na kumkumbatia, akasema, “Msishtuke, uzima wake bado umo ndani yake.” 11 Kisha Paulo akapanda tena ghorofani, akamega mkate na kula. Baada ya kuongea mpaka mapambazuko, akaondoka. 12 Watu wakamrudisha yule kijana nyumbani akiwa hai nao wakafarijika sana.

  74. 22 Lakini waganga wa Misri kwa kutumia siri ya uganga wao wakafanya vivyo hivyo, nao moyo wa Farao ukawa mgumu, hakuwasikiliza Mose na Aroni, kama vile Bwana alivyokuwa amesema.

  75. 5 Hivyo akafanya kile alichoambiwa na Bwana. Akaenda katika Kijito cha Kerithi, mashariki ya Yordani na akakaa huko. 6 Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi na mkate na nyama jioni, naye akanywa maji kutoka kile kijito.

  76. 2 Elisha akamjibu, “Nitawezaje kukusaidia? Niambie, una nini ndani ya nyumba yako?”

    Akasema, “Mtumishi wako hana kitu chochote kabisa, isipokuwa mafuta kidogo.”

    3 Elisha akasema, “Zunguka kwa majirani zako wote ukaombe vyombo vitupu. Usiombe vichache. 4 Kisha ingia ndani na ujifungie mlango, wewe na wanao. Mimina mafuta kwenye vyombo vyote, na kila kimoja kinapojaa, kiweke kando.”

    5 Yule mjane akaondoka na kujifungia ndani, yeye na wanawe. Wao wakamletea vyombo, naye akaendelea kumimina mafuta. 6 Vyombo vyote vilipojaa, akamwambia mwanawe, “Niletee chombo kingine.”

    Lakini mwanawe akajibu, “Hakuna chombo kingine kilichobaki.” Basi mafuta yakakoma kutiririka.

    7 Yule mwanamke akaenda akamwambia yule mtu wa Mungu, naye mtu wa Mungu akasema, “Nenda ukayauze hayo mafuta ulipe madeni yako. Wewe na wanao mnaweza kuishi kwa kile kinachosalia.”

  77. 14 Wewe ndiwe Mungu utendaye miujiza,

    umeonyesha uwezo wako katikati ya mataifa.

  78. 58 Naye hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao.

  79. 40 Mtu mmoja mwenye ukoma alimjia Yesu, akamwomba akipiga magoti, akamwambia, “Ukitaka, waweza kunitakasa.”

    41 Yesu, akiwa amejawa na huruma, akanyoosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka. Takasika!” 42 Mara ukoma ukamtoka, naye akatakasika. 43 Baada ya Yesu kumwonya vikali, akamruhusu aende zake 44 akimwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote habari hizi, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na ukatoe sadaka alizoagiza Mose kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.” 45 Lakini yule mtu akaenda akaanza kutangaza habari za kuponywa kwake waziwazi. Kwa hiyo, Yesu hakuweza tena kuingia katika miji waziwazi lakini alikaa sehemu zisizo na watu. Hata hivyo watu wakamfuata huko kutoka kila upande.

  80. 34 Maria akamuuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?”

    35 Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu. 36 Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake, na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa. 37 Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.”

  81. 28 Mungu ameweka katika kanisa, kwanza mitume, pili manabii, tatu walimu, kisha watenda miujiza, pia karama za kuponya, karama za kusaidiana, karama za uongozi, aina mbalimbali za lugha. 29 Je, wote ni mitume? Je, wote ni manabii? Je, wote ni walimu? Je, wote wanatenda miujiza? 30 Je, wote wana karama ya kuponya? Je, wote hunena kwa lugha mpya? Je, wote wanatafsiri? 31 Basi tamanini sana karama zilizo kuu.

    Nami nitawaonyesha njia iliyo bora zaidi.

  82. 5 Je, Mungu huwapa Roho wake na kufanya miujiza katikati yenu kwa sababu mnatii sheria, au kwa sababu mnaamini kile mlichosikia?

  83. 12 Katika siku ile ambayo Bwana aliwapeana Waamori kwa Israeli, Yoshua akanena na Bwana akiwa mbele ya Waisraeli akasema:

    “Wewe jua, simama juu ya Gibeoni,

    wewe mwezi, tulia juu ya Bonde la Aiyaloni.”

    13 Hivyo jua likasimama,

    nao mwezi ukatulia,

    hadi taifa hilo lilipokwisha

    kujilipizia kisasi kwa adui wake,

    kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Yashari.

    Jua likasimama kimya katikati ya mbingu, likachelewa kuzama muda wa siku moja nzima. 14 Haijakuwepo siku nyingine kama hiyo kabla au baada, siku ambayo Bwana alimsikiliza mwanadamu. Hakika Bwana alikuwa akiwapigania Israeli.

  84. 16 “Sasa basi, simameni kimya mkaone jambo hili kubwa ambalo Bwana anakwenda kulifanya mbele ya macho yenu! 17 Je, sasa si mavuno ya ngano? Nitamwomba Bwana ili alete ngurumo na mvua. Nanyi mtatambua jambo hili lilivyo baya mlilolifanya mbele za macho ya Bwana mlipoomba mfalme.”

    18 Kisha Samweli akamwomba Bwana, na siku ile ile Bwana akatuma ngurumo na mvua. Hivyo watu wote wakamwogopa sana Bwana na Samweli.

  85. 24 Baada ya Yesu na wanafunzi wake kufika Kapernaumu, wakusanya kodi ya Hekalu wakamjia Petro na kumuuliza, “Je, Mwalimu wenu halipi kodi ya Hekalu?”

    25 Petro akajibu, “Ndiyo, yeye hulipa.” Petro aliporudi nyumbani, Yesu akawa wa kwanza kulizungumzia, akamuuliza, “Unaonaje Simoni? Wafalme wa dunia hupokea ushuru na kodi kutoka kwa nani? Je, ni kutoka kwa watoto wao au kutoka kwa watu wengine?”

    26 Petro akamjibu, “Kutoka kwa watu wengine.” Yesu akamwambia, “Kwa hiyo watoto wao wamesamehewa. 27 Lakini ili tusije tukawaudhi, nenda baharini ukatupe ndoana. Mchukue samaki wa kwanza utakayemvua. Fungua kinywa chake nawe utakuta humo fedha, ichukue ukalipe kodi yako na yangu.”

  86. 29 Umati wa watu ulipokuwa unazidi kuongezeka, Yesu akaendelea kusema, “Hiki ni kizazi kiovu. Kinatafuta ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ya Yona.

  87. 17 Akawaacha, akatoka nje ya mji, akaenda hadi Bethania, akalala huko.

    18 Asubuhi na mapema, Yesu alipokuwa akirudi mjini, alikuwa na njaa. 19 Akauona mtini kando ya barabara, naye akaukaribia, lakini hakupata tunda lolote ila majani. Ndipo akauambia, “Wewe usizae matunda tena kamwe!” Papo hapo ule mtini ukanyauka.

    20 Wanafunzi wake walipoona jambo hili, wakashangaa, wakamuuliza, “Imekuwaje mtini huu kunyauka ghafula?”

    21 Yesu akawajibu, “Amin, nawaambia, kama mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ngʼoka, ukatupwe baharini,’ litafanyika. 22 Yoyote mtakayoyaomba mkisali na mkiamini, mtayapokea.”