79 Bible Verses About Having Faith

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Having Faith
  1. 1 Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, na udhahiri wa mambo yasiyoonekana. 2 Maana baba zetu wa kale walipongezwa kwa haya.

    3 Kwa imani tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, vitu vyote vinavyoonekana havikuumbwa kutoka kwa vitu vinavyoonekana.

    4 Kwa imani Abeli alimtolea Mungu dhabihu bora zaidi kuliko Kaini. Kwa imani alishuhudiwa kuwa mwenye haki, Mungu mwenyewe akazishuhudia sadaka zake. Kwa imani bado ananena ingawa amekufa.

    5 Kwa imani Enoki alitwaliwa kutoka maisha haya, kiasi kwamba hakuonja mauti. Hakuonekana, kwa sababu Mungu alikuwa amemchukua. Kwa kuwa kabla hajatwaliwa alikuwa ameshuhudiwa kuwa ni mtu aliyempendeza Mungu. 6 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa maana yeyote anayemjia Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na ya kuwa huwapa thawabu wale wamtafutao kwa bidii.

    7 Kwa imani, Noa alipoonywa na Mungu kuhusu mambo ambayo hayajaonekana bado, kwa kumcha Mungu alitengeneza safina ili kuokoa jamaa yake. Kwa imani yake aliuhukumu ulimwengu na akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani.

    8 Kwa imani Abrahamu, alipoitwa aende mahali ambapo Mungu angempa baadaye kuwa urithi, alitii na akaenda, ingawa hakujua anakokwenda. 9 Kwa imani alifanya maskani yake katika nchi ya ahadi kama mgeni katika nchi ya kigeni; aliishi katika mahema, kama Isaki na Yakobo walivyofanya, waliokuwa pia warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. 10 Kwa maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi ya kudumu ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.

    11 Kwa imani Abrahamu, ingawa alikuwa mzee wa umri, naye Sara mwenyewe aliyekuwa tasa, alipokea uwezo wa kuwa baba kwa sababu alimhesabu Mungu aliyemwahidi kuwa mwaminifu na kwamba angetimiza ahadi yake. 12 Hivyo kutokana na huyu huyu ambaye alikuwa sawa na mfu, wakazaliwa wazao wengi kama nyota za mbinguni na kama mchanga wa pwani usiohesabika.

    13 Watu hawa wote wakafa katika imani bila kuzipokea zile ahadi, lakini waliziona kwa mbali na kuzishangilia. Nao walikubali kwamba walikuwa wageni na wasiokuwa na maskani hapa duniani. 14 Watu wasemao mambo kama haya, wanaonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe. 15 Kwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangalipata nafasi ya kurudi huko. 16 Lakini badala yake walitamani nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandaa mji kwa ajili yao.

    17 Kwa imani Abrahamu, alipojaribiwa na Mungu, alimtoa Isaki kuwa dhabihu. Yeye aliyekuwa amezipokea ahadi za Mungu alikuwa tayari kumtoa mwanawe, aliyekuwa mwanawe pekee awe dhabihu. 18 Ingawa Mungu alikuwa amemwambia Abrahamu, “Uzao wako utahesabiwa kupitia kwa Isaki,” 19 Abrahamu alihesabu kuwa Mungu angaliweza kumfufua Isaki kutoka kwa wafu. Na kwa kusema kwa mfano, alimpata tena Isaki kutoka kwa wafu.

    20 Kwa imani Isaki alimbariki Yakobo na Esau kuhusu maisha yao ya baadaye.

    21 Kwa imani Yakobo alipokuwa anakufa, alimbariki kila mmoja wa mtoto wa Yosefu, akamwabudu Mungu akiwa ameegemea juu ya kichwa cha fimbo yake.

    22 Kwa imani, Yosefu alipokaribia mwisho wa maisha yake, alinena habari za kutoka kwa wana wa Israeli huko Misri na akatoa maagizo kuhusu mifupa yake.

    23 Kwa imani, wazazi wa Mose walimficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa, kwa sababu waliona kuwa si mtoto wa kawaida, wala hawakuiogopa amri ya mfalme.

    24 Kwa imani, Mose alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. 25 Akachagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha kwa anasa za dhambi kwa kitambo kidogo tu. 26 Aliona kushutumiwa kwa ajili ya Kristo ni utajiri mkubwa zaidi kuliko hazina za Misri, maana alikuwa anatazamia kupata thawabu baadaye.

  2. 6 Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’ ” (yaani ili kumleta Kristo chini) 7 “au ‘Ni nani atashuka kwenda kuzimu?’ ” (yaani ili kumleta Kristo kutoka kwa wafu.) 8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, lile neno la imani tunalolihubiri. 9 Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. 10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu. 11 Kama yasemavyo Maandiko, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.” 12 Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. 13 Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.”

    14 Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? 15 Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri habari njema!”

    16 Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” 17 Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo. 18 Lakini nauliza: Je, wao hawakusikia? Naam, wamesikia, kwa maana:

    “Sauti yao imeenea duniani pote,

    nayo maneno yao yameenea

    hadi miisho ya ulimwengu.”

  3. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

  4. 2 Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3 kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. 4 Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu chochote. 5 Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa. 6 Lakini anapoomba, lazima aamini wala asiwe na shaka, kwa sababu mtu aliye na shaka ni kama wimbi la bahari, lililochukuliwa na upepo na kutupwa huku na huku. 7 Mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapata kitu chochote kutoka kwa Bwana. 8 Yeye ni mtu mwenye nia mbili, mwenye kusitasita katika njia zake zote.

  5. 14 Kama vile Mose alivyomwinua yule nyoka kule jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu. 15 Ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele.

    16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa. 18 Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. 19 Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu. 20 Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe. 21 Lakini yule aishiye kwa ukweli huja kwenye nuru, ili ionekane wazi kwamba matendo yake yametendeka katika Mungu.”

  6. 21 Yesu akawajibu, “Amin, nawaambia, kama mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ngʼoka, ukatupwe baharini,’ litafanyika. 22 Yoyote mtakayoyaomba mkisali na mkiamini, mtayapokea.”

  7. 14 Walipowafikia wale wanafunzi wengine, wakawakuta wamezungukwa na umati mkubwa wa watu na baadhi ya walimu wa sheria wakibishana nao. 15 Mara wale watu walipomwona Yesu, wakastaajabu sana, wakamkimbilia ili kumsalimu.

    16 Akawauliza wanafunzi wake, “Mnabishana nao kuhusu nini?”

    17 Mtu mmoja miongoni mwa ule umati wa watu akajibu, “Mwalimu, nilimleta kwako mwanangu ambaye ana pepo mchafu anayemfanya asiweze kuongea. 18 Kila mara huyo pepo mchafu ampagaapo mwanangu, humwangusha chini na kumfanya atokwe povu mdomoni na kusaga meno, kisha mwili wake hukauka. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”

    19 Yesu akawaambia, “Enyi kizazi kisicho na imani! Nitakuwa pamoja nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni mvulana kwangu.”

    20 Nao wakamleta yule mvulana. Yule pepo mchafu alipomwona Yesu, mara akamtia yule mvulana kifafa, akaanguka, akagaagaa chini huku akitokwa na povu kinywani.

    21 Yesu akamuuliza baba yake, “Mwanao amekuwa katika hali hii tangu lini?”

    Akamjibu, “Tangu utoto wake. 22 Mara kwa mara huyo pepo mchafu amekuwa akimwangusha kwenye moto au kwenye maji ili kumwangamiza. Lakini kama unaweza kufanya jambo lolote, tafadhali tuhurumie utusaidie.”

    23 Yesu akamwambia, “Kama ukiweza kuamini, yote yawezekana kwake yeye aaminiye.”

    24 Mara baba yake yule mvulana akapiga kelele akisema, “Ninaamini. Nisaidie kutokuamini kwangu!” 25 Yesu alipoona kwamba umati wa watu unakusanyika pamoja mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akimwambia, “Wewe pepo bubu na kiziwi, nakuamuru umtoke, wala usimwingie tena!”

    26 Yule pepo mchafu akiisha kupiga kelele, akamtia kifafa kwa nguvu, na akamtoka. Yule mvulana alikuwa kama maiti, hivyo watu wengi wakasema, “Amekufa.” 27 Lakini Yesu akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama.

    28 Baada ya Yesu kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamuuliza wakiwa peke yao, “Mbona sisi hatukuweza kumtoa huyo pepo mchafu?”

    29 Yesu akawajibu, “Hali hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa kuomba na kufunga.”

  8. 22 Yesu akawajibu, “Mwaminini Mungu. 23 Amin, nawaambia, mtu yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ngʼoka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, atatimiziwa. 24 Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote mtakayoyaomba mkisali, aminini ya kwamba mmeyapokea, nayo yatakuwa yenu.

  9. 16 Mimi siionei haya Injili ya Kristo kwa maana ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, kwanza kwa Myahudi na kwa Myunani pia. 17 Kwa maana katika Injili haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa, haki ile iliyo kwa njia ya imani hadi imani. Kama ilivyoandikwa: “Mwenye haki ataishi kwa imani.”

    18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao, 19 kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao. 20 Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.

    21 Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza. 22 Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga 23 na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizofanywa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vitambaavyo.

    24 Kwa hiyo, Mungu akawaacha wazifuate tamaa mbaya za mioyo yao katika uasherati, hata wakavunjiana heshima miili yao wao kwa wao. 25 Kwa sababu waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakaabudu na kutumikia kiumbe badala ya Muumba, ahimidiwaye milele! Amen.

    26 Kwa sababu hii, Mungu aliwaacha wavunjiane heshima kwa kufuata tamaa zao za aibu. Hata wanawake wao wakabadili matumizi ya asili ya miili yao wakaitumia isivyokusudiwa. 27 Vivyo hivyo wanaume pia wakiacha matumizi ya asili ya wanawake wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wakafanyiana matendo ya aibu na wanaume wengine nao wakapata katika maisha yao adhabu iliyowastahili kwa ajili ya upotovu wao.

    28 Nao kwa kuwa hawakuona umuhimu wa kudumisha ufahamu wa Mungu, yeye akawaachilia wafuate akili za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa. 29 Wakiwa wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji, 30 wasingiziaji, wanaomchukia Mungu, wajeuri, wenye kiburi na majivuno, wenye hila, wasiotii wazazi wao, 31 wajinga, wasioamini, wasio na huruma na wakatili.

  10. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2 ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

    6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. 7 Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.

    9 Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake! 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. 11 Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kupitia kwake tumepata upatanisho.

  11. 21 Lakini sasa, haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Sheria na Manabii wanaishuhudia. 22 Haki hii itokayo kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote wamwaminio. Kwa maana hapo hakuna tofauti, 23 kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, 24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu. 25 Yeye ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonyesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa. 26 Alifanya hivyo ili kuonyesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.

    27 Basi, kujivuna kuko wapi? Kumewekwa mbali. Kwa sheria gani? Je, ni kwa ile ya matendo? La hasha, bali kwa ile sheria ya imani. 28 Kwa maana twaona kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kwa njia ya imani wala si kwa matendo ya sheria. 29 Je, Mungu ni Mungu wa Wayahudi peke yao? Je, yeye si Mungu wa watu wa Mataifa pia? Naam, yeye ni Mungu wa watu wa Mataifa pia. 30 Basi kwa kuwa tuna Mungu mmoja tu, atawahesabia haki wale waliotahiriwa kwa imani na wale wasiotahiriwa kwa imani iyo hiyo.

  12. 3 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa rehema zake kuu ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima kupitia kwa kufufuka kwa Yesu Kristo kutoka kwa wafu, 4 ili tuupate urithi usioharibika, usio na uchafu, ule usionyauka: uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu, 5 ninyi ambao mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani, hadi uje ule wokovu ulio tayari kufunuliwa nyakati za mwisho. 6 Katika hili mnafurahi sana, ingawa sasa kwa kitambo kidogo mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna nyingi. 7 Haya yamewajia ili kwamba imani yenu, iliyo ya thamani kuliko dhahabu ipoteayo, ingawa hujaribiwa kwa moto, ionekane kuwa halisi na imalizie katika sifa, utukufu na heshima wakati Yesu Kristo atadhihirishwa. 8 Ingawa hamjamwona, mnampenda; tena ingawa sasa hammwoni, mnamwamini na kujawa na furaha isiyoneneka yenye utukufu usioelezeka. 9 Maana mnaupokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu.

  13. 14 Walipofika penye umati wa watu, mtu mmoja akamjia Yesu na kupiga magoti mbele yake, akasema, 15 “Bwana, mhurumie mwanangu. Yeye ana kifafa na anateseka sana. Mara kwa mara huanguka kwenye moto au kwenye maji. 16 Nilimleta kwa wanafunzi wako, lakini hawakuweza kumponya.”

    17 Yesu akajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni mvulana hapa kwangu.” 18 Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akamtoka yule kijana, naye akapona saa ile ile.

    19 Kisha wanafunzi wakamwendea Yesu wakiwa peke yao, wakamuuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?”

    20 Akawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu ndogo. Ninawaambia kweli, mkiwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mtauambia mlima huu, ‘Ondoka hapa uende pale,’ nao utaondoka. Wala hakutakuwa na jambo lisilowezekana kwenu. [ 21 Lakini hali kama hii haitoki ila kwa kuomba na kufunga.]”

  14. 24 Lakini Tomaso, aliyeitwa Didimasi, yaani Pacha, mmoja wa wale kumi na wawili, hakuwa pamoja nao Yesu alipokuja. 25 Hivyo wale wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana.”

    Lakini yeye akawaambia, “Nisipoona zile alama za misumari mikononi mwake, na kuweka kidole changu kwenye hizo alama za misumari na mkono wangu ubavuni mwake, sitaamini.”

    26 Baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwa tena pamoja ndani ya nyumba, naye Tomaso alikuwa pamoja nao. Ndipo Yesu akaja milango ikiwa imefungwa na kusimama katikati yao akasema, “Amani iwe nanyi.” 27 Kisha akamwambia Tomaso, “Weka kidole chako hapa na uone mikono yangu, nyoosha mkono wako uguse ubavuni mwangu. Usiwe na shaka, bali uamini tu.”

    28 Tomaso akamwambia, “Bwana wangu na Mungu wangu!”

    29 Yesu akamwambia, “Umeamini kwa kuwa umeniona? Wamebarikiwa wale ambao hawajaona lakini wameamini.”

    30 Yesu alifanya miujiza mingine mingi mbele za wanafunzi wake, ambayo haikuandikwa katika kitabu hiki. 31 Lakini haya yameandikwa ili mweze kuamini ya kuwa Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu, na kwa kumwamini mpate uzima katika jina lake.

  15. 10 Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.

    11 Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole. 12 Pigana vile vita vizuri vya imani. Shika uzima wa milele ambao ndio ulioitiwa ulipokiri ule ukiri mzuri mbele ya mashahidi wengi.

  16. 13 Kwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Abrahamu au kwa wazao wake kwa njia ya sheria bali kwa njia ya haki ipatikanayo kwa imani. 14 Kwa maana ikiwa wale waishio kwa sheria ndio warithi, imani haina thamani na ahadi haifai kitu, 15 kwa sababu sheria huleta ghadhabu. Mahali ambapo hakuna sheria hakuna makosa.

    16 Kwa hiyo, ahadi huja kwa njia ya imani, ili iwe ni kwa neema, na itolewe kwa wazao wa Abrahamu, si kwa wale walio wa sheria peke yao, bali pia kwa wale walio wa imani ya Abrahamu. Yeye ndiye baba yetu sisi sote. 17 Kama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Yeye ni baba yetu mbele za Mungu, ambaye yeye alimwamini, yule Mungu anaye fufua waliokufa, na kuvitaja vile vitu ambavyo haviko kana kwamba vimekwisha kuwako.

    18 Akitarajia yasiyoweza kutarajiwa, Abrahamu akaamini, akawa baba wa mataifa mengi, kama alivyoahidiwa kwamba, “Uzao wako utakuwa mwingi mno.” 19 Abrahamu hakuwa dhaifu katika imani hata alipofikiri juu ya mwili wake, ambao ulikuwa kama uliokufa, kwani umri wake ulikuwa unakaribia miaka mia moja, au alipofikiri juu ya ufu wa tumbo la Sara. 20 Lakini Abrahamu hakusitasita kwa kutokuamini ahadi ya Mungu, bali alitiwa nguvu katika imani yake na kumpa Mungu utukufu, 21 akiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi. 22 Hii ndio sababu, “ilihesabiwa kwake kuwa haki.” 23 Maneno haya “ilihesabiwa kwake kuwa haki,” hayakuandikwa kwa ajili yake peke yake, 24 bali kwa ajili yetu sisi pia ambao Mungu atatupa haki, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu kutoka kwa wafu. 25 Alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, naye alifufuliwa kutoka mauti ili tuhesabiwe haki.

  17. 5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote

    wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

    6 katika njia zako zote mkiri yeye,

    naye atayanyoosha mapito yako.

    7 Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe;

    mche Bwana ukajiepushe na uovu.

  18. 5 Basi Mungu ndiye alitufanya kwa ajili ya jambo lilo hilo naye ametupa Roho Mtakatifu kuwa amana, akituhakikishia ahadi ya kile kijacho.

    6 Kwa hiyo siku zote tunalo tumaini, hata ingawa tunajua kwamba wakati tukiwa katika mwili huu, tuko mbali na Bwana, 7 kwa maana twaenenda kwa imani wala si kwa kuona.

  19. 1 Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na kongwa la utumwa.

    2 Sikilizeni! Mimi, Paulo, nawaambieni kwamba kama mkikubali kutahiriwa, basi Kristo hatawafaidia chochote. 3 Namshuhudia tena kila mtu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika sheria yote. 4 Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kwa njia ya sheria mmetengwa na Kristo, mko mbali na neema ya Mungu. 5 Kwa maana, kwa njia ya Roho kwa imani, tunangojea kwa shauku tumaini la haki. 6 Kwa maana ndani ya Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuleti tofauti, bali lililo muhimu ni imani itendayo kazi kwa njia ya upendo.

  20. 3 Kwa hiyo, jilindeni.

    “Kama ndugu yako akikukosea mwonye, naye akitubu, msamehe. 4 Kama akikukosea mara saba kwa siku moja na mara saba kwa siku moja akaja kwako akisema, ‘Ninatubu,’ msamehe.”

    5 Mitume wake wakamwambia Bwana, “Tuongezee imani.”

    6 Bwana akawajibu, “Kama mkiwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu, ‘Ngʼoka ukaote baharini,’ nao ungewatii.

  21. 5 Yale waliyosema yakawapendeza watu wote, nao wakamchagua Stefano (mtu aliyejawa na imani na Roho Mtakatifu) pamoja na Filipo, Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena na Nikolao, mwongofu kutoka Antiokia. 6 Wakawaleta watu hawa mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono juu yao.

    7 Neno la Mungu likazidi kuenea. Idadi ya wanafunzi ikazidi kuongezeka sana katika Yerusalemu hata makuhani wengi wakaitii ile imani.

    8 Stefano, akiwa amejaa neema na nguvu za Mungu, alifanya ishara na miujiza mikubwa miongoni mwa watu. 9 Hata hivyo, ukainuka upinzani wa watu wa Sinagogi la Watu Huru (kama lilivyokuwa linaitwa), la Wayahudi wa Kirene na wa Iskanderia, na wengine kutoka Kilikia na Asia. Watu hawa wakaanza kupingana na Stefano. 10 Lakini hawakuweza kushindana na hekima yake wala huyo Roho ambaye alisema kwake.

  22. 14 Ndugu zangu, yafaa nini ikiwa mtu atadai kuwa anayo imani lakini hana matendo? Je, imani kama hiyo yaweza kumwokoa? 15 Ikiwa ndugu yako au dada hana mavazi wala chakula, 16 mmoja wenu akamwambia, “Enenda zako kwa amani, ukaote moto na kushiba,” pasipo kumpatia yale mahitaji ya mwili aliyopungukiwa, yafaa nini? 17 Vivyo hivyo, imani peke yake kama haikuambatana na matendo, imekufa.

    18 Lakini mtu mwingine atasema, “Wewe unayo imani; mimi ninayo matendo.”

    Nionyeshe imani yako pasipo matendo nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo. 19 Unaamini kwamba kuna Mungu mmoja. Vyema! Hata mashetani yanaamini hivyo na kutetemeka.

    20 Ewe mpumbavu! Je, wataka kujua kwamba imani bila matendo haifai kitu? 21 Je, Abrahamu baba yetu hakuhesabiwa haki kwa kile alichotenda, alipomtoa mwanawe Isaki madhabahuni? 22 Unaona jinsi ambavyo imani yake na matendo yake vilikuwa vinatenda kazi pamoja, nayo imani yake ikakamilishwa na kile alichotenda. 23 Kwa njia hiyo yakatimizwa yale Maandiko yasemayo, “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki,” naye akaitwa rafiki wa Mungu. 24 Mnaona ya kwamba mtu huhesabiwa haki kwa yale anayotenda wala si kwa imani peke yake.

    25 Vivyo hivyo, hata Rahabu, yule kahaba, hakuhesabiwa haki kwa yale aliyotenda alipowapokea wale wapelelezi na kuwaambia waende njia nyingine? 26 Kama vile ambavyo mwili pasipo roho umekufa, kadhalika nayo imani pasipo matendo imekufa.

  23. 1 Roho asema waziwazi kwamba katika siku za mwisho baadhi ya watu wataiacha imani na kufuata roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani. 2 Mafundisho kama hayo huja kupitia kwa waongo ambao ni wanafiki, hali dhamiri zao zikiungua kwa kuchomwa moto. 3 Wao huwakataza watu wasioe na kuwaagiza wajiepushe na vyakula fulani, ambavyo Mungu aliviumba ili vipokewe kwa shukrani na wale wanaoamini na kuijua kweli. 4 Kwa maana kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, wala hakuna kitu chochote cha kukataliwa kama kikipokewa kwa shukrani, 5 kwa sababu kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.

    6 Kama ukiwakumbusha ndugu mambo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, uliyelelewa katika kweli ya imani na yale mafundisho mazuri uliyoyafuata. 7 Usijishughulishe kamwe na hadithi za kipagani na masimulizi ya uongo ya wanawake wazee; badala yake, jizoeze kuwa mtauwa. 8 Kwa maana mazoezi ya mwili yana faida kwa sehemu, lakini utauwa una faida katika mambo yote, yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa na ya ule ujao.

  24. 4 Kwa maana kila aliyezaliwa na Mungu huushinda ulimwengu. Huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, yaani, hiyo imani yetu. 5 Ni nani yule aushindaye ulimwengu? Ni yule tu aaminiye kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.

  25. 40 Basi Yesu aliporudi, umati mkubwa wa watu ukampokea kwa furaha, kwani walikuwa wakimngojea. 41 Kisha mtu mmoja, jina lake Yairo, aliyekuwa kiongozi wa sinagogi, akaja na kuanguka miguuni mwa Yesu, akimwomba afike nyumbani kwake, 42 kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa anakufa.

    Yesu alipokuwa akienda, umati wa watu ukamsonga sana. 43 Katika umati huo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa na tatizo la kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Tena alikuwa amegharimia yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya matibabu, wala hakuna yeyote aliyeweza kumponya. 44 Huyo mwanamke akaja kwa nyuma ya Yesu na kugusa upindo wa vazi lake. Mara kutokwa damu kwake kukakoma.

    45 Yesu akauliza, “Ni nani aliyenigusa?”

    Watu wote walipokana, Petro akasema, “Bwana, huu umati wa watu unakusonga na kukusukuma kila upande.”

    46 Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, kwa maana nimetambua kuwa nguvu zimenitoka.”

    47 Yule mwanamke alipofahamu ya kuwa hawezi kuendelea kujificha, alikuja akitetemeka, akaanguka miguuni mwa Yesu. Akaeleza mbele ya watu wote kwa nini alimgusa na jinsi alivyoponywa mara. 48 Basi Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.”

    49 Yesu alipokuwa bado anasema, akaja mtumishi kutoka nyumbani kwa Yairo, yule kiongozi wa sinagogi, kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Usiendelee kumsumbua Mwalimu.”

    50 Yesu aliposikia jambo hili, akamwambia Yairo, “Usiogope. Amini tu, naye binti yako atapona.”

    51 Walipofika nyumbani kwa Yairo, hakumruhusu mtu yeyote aingie ndani naye isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, pamoja na baba na mama wa yule binti. 52 Wakati ule ule watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili ya huyo binti. Yesu akawaambia, “Acheni kulia. Huyu binti hajafa, ila amelala.”

    53 Wao wakamcheka kwa dharau, wakijua kuwa amekwisha kufa. 54 Yesu akamshika yule binti mkono na kuita, “Binti, amka!” 55 Roho yake ikamrudia, naye akainuka mara moja. Akaamuru apewe kitu cha kula. 56 Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote juu ya yale yaliyotukia.

  26. 36 Yeyote anayemwamini Mwana ana uzima wa milele, lakini yeye asiyemwamini Mwana hatauona uzima, bali ghadhabu ya Mungu itakuwa juu yake.”

  27. 37 Siku ile ya mwisho ya Sikukuu, siku ile kuu, wakati Yesu akiwa amesimama huko, akapaza sauti yake akasema, “Kama mtu yeyote anaona kiu na aje kwangu anywe. 38 Yeyote aniaminiye mimi, kama Maandiko yasemavyo, vijito vya maji ya uzima vitatiririka ndani mwake.” 39 Yesu aliposema haya alimaanisha Roho Mtakatifu ambaye wote waliomwamini wangempokea, kwani mpaka wakati huo, Roho alikuwa hajatolewa, kwa kuwa Yesu alikuwa bado hajatukuzwa.

  28. 20 Nimesulubiwa pamoja na Kristo, wala si mimi tena ninayeishi, bali Kristo ndiye aishiye ndani yangu. Uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani ya Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu.

  29. 7 Nimevipiga vita vizuri, mashindano nimeyamaliza, imani nimeilinda. 8 Sasa nimewekewa taji ya haki ambayo Bwana, mwamuzi wa haki, atanitunukia siku ile: wala si mimi tu, bali pia wote ambao wamengoja kwa shauku kudhihirishwa kwake.

  30. 20 Lakini ninyi wapendwa, jijengeni katika imani yenu iliyo takatifu sana tena ombeni katika Roho Mtakatifu. 21 Jilindeni katika upendo wa Mungu mkitazamia kwa furaha rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo ili awalete katika uzima wa milele.

  31. 10 Huyo Neno alikuwako ulimwenguni na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua. 11 Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea. 12 Bali wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake. 13 Hawa ndio wasiozaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali kwa mapenzi ya Mungu.

  32. 8 Filipo akamwambia, “Bwana, tuonyeshe Baba yako yatosha.”

    9 Yesu akamjibu, “Filipo, nimekaa nanyi muda huu wote hata usinijue? Mtu yeyote aliyeniona mimi, amemwona Baba. Sasa wawezaje kusema, ‘Tuonyeshe Baba’? 10 Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambia siyasemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba akaaye ndani yangu ndiye atendaye hizi kazi. 11 Nisadiki mimi kwamba niko ndani ya Baba na Baba yuko ndani yangu, la sivyo, niaminini kwa sababu ya zile kazi nizitendazo. 12 Amin, amin nawaambia, yeyote aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo yeye atazifanya, naam na kubwa kuliko hizi atazifanya, kwa sababu mimi ninakwenda kwa Baba. 13 Nanyi mkiomba lolote kwa Jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba apate kutukuzwa katika Mwana. 14 Kama mkiniomba lolote kwa Jina langu nitalifanya.

    15 “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu. 16 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele. 17 Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye anakaa ndani yenu.

  33. 25 Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. 26 Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka. 27 Yule mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza iko wazi, akachomoa upanga wake akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wote wametoroka. 28 Lakini Paulo akapiga kelele kwa sauti kubwa, akasema, “Usijidhuru kwa maana sisi sote tuko hapa!”

    29 Yule askari wa gereza akaagiza taa ziletwe, akaingia ndani ya kile chumba cha gereza, akapiga magoti akitetemeka mbele ya Paulo na Sila. 30 Kisha akawaleta nje akisema, “Bwana zangu, nifanye nini nipate kuokoka?”

    31 Wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu Kristo, nawe utaokoka, pamoja na watu wa nyumbani mwako.” 32 Wakamwambia neno la Bwana yeye pamoja na wote waliokuwako nyumbani mwake. 33 Wakati ule ule, yule mkuu wa gereza akawachukua, akawaosha majeraha yao, kisha akabatizwa yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake bila kuchelewa. 34 Akawapandisha nyumbani mwake akawaandalia chakula, yeye pamoja na nyumba yake yote wakafurahi sana kwa kuwa sasa walikuwa wamemwamini Mungu.

  34. 21 Wakahubiri habari njema katika mji huo na kupata wanafunzi wengi. Kisha wakarudi Listra, Ikonio na Antiokia, 22 wakiwaimarisha wanafunzi na kuwatia moyo waendelee kudumu katika imani. Wakawaonya wakisema, “Imetupasa kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa kupitia katika taabu nyingi.”

  35. 13 Kesheni, simameni imara katika imani, fanyeni kiume, kuweni mashujaa kuweni hodari.

  36. 15 “Sisi wenyewe ni Wayahudi kwa kuzaliwa na si watu wenye dhambi kama watu wa Mataifa, 16 bado tunajua ya kwamba mtu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria bali kwa njia ya imani katika Yesu Kristo. Hivyo sisi pia, tumemwamini Kristo Yesu ili tupate kuhesabiwa haki kwa njia ya imani katika Kristo, wala si kwa matendo ya sheria, kwa sababu kwa kushika sheria hakuna hata mtu mmoja atakayehesabiwa haki.

  37. 1 Kwa hivyo tulipokuwa hatuwezi kuvumilia zaidi, tuliamua tubaki Athene peke yetu. 2 Tukamtuma Timotheo ambaye ni ndugu yetu na mtumishi mwenzetu wa Mungu katika kuieneza Injili ya Kristo, aje kuwaimarisha na kuwatia moyo katika imani yenu, 3 ili mtu yeyote asifadhaishwe na mateso haya. Mnajua vyema kwamba tumewekewa hayo mateso. 4 Kwa kweli, tulipokuwa pamoja nanyi tuliwaambia mara kwa mara kwamba tutateswa na imekuwa hivyo kama mjuavyo. 5 Kwa sababu hii nilipokuwa siwezi kuvumilia zaidi, nilimtuma mtu ili nipate habari za imani yenu. Niliogopa kwamba kwa njia fulani yule mjaribu asiwe amewajaribu, nasi tukawa tumejitaabisha bure.

  38. 27 Kwa imani Mose aliondoka Misri bila kuogopa ghadhabu ya mfalme. Alivumilia kwa sababu alimwona yeye asiyeonekana kwa macho. 28 Kwa imani akaadhimisha Pasaka na kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wazaliwa wa Israeli.

    29 Kwa imani, watu walivuka Bahari ya Shamu kama vile juu ya nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo, walitoswa ndani ya maji.

    30 Kwa imani kuta za Yeriko zilianguka, baada ya watu kuzizunguka kwa siku saba.

    31 Kwa imani, Rahabu, yule kahaba, hakuangamizwa pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi.

    32 Basi niseme nini zaidi? Sina wakati wa kusema habari za Gideoni, Baraka, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samweli na manabii, 33 ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitekeleza haki, na wakapokea ahadi za Mungu; walifunga vinywa vya simba, 34 wakazima makali ya miali ya moto, na wakaepuka kuuawa kwa upanga; udhaifu wao uligeuka kuwa nguvu; pia walikuwa hodari vitani na kuyafukuza majeshi ya wageni. 35 Wanawake walipokea watu wao waliokuwa wamekufa, wakafufuliwa. Lakini wengine waliteswa, nao wakakataa kufunguliwa, ili wapate ufufuo ulio bora zaidi. 36 Wengine walidhihakiwa na kupigwa, hata walifungwa minyororo na kutiwa gerezani. 37 Walipigwa kwa mawe; walipasuliwa vipande viwili kwa msumeno; waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na mbuzi, wakiwa maskini, wakiteswa na kutendwa mabaya, 38 watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao. Walizunguka majangwani na milimani, katika mapango na katika mahandaki ardhini.

    39 Hawa wote walishuhudiwa vyema kwa sababu ya imani yao, lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea yale yaliyoahidiwa. 40 Kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea kitu kilicho bora zaidi ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.

  39. 51 Yesu akamuuliza, “Unataka nikufanyie nini?”

    Yule kipofu akajibu, “Mwalimu, nataka kuona.”

    52 Yesu akamwambia, “Nenda zako, imani yako imekuponya.” Mara akapata kuona, akamfuata Yesu njiani.

  40. 25 Yesu akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, hata akifa atakuwa anaishi 26 na yeyote aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je, unasadiki haya?”

    27 Martha akamwambia, “Ndiyo Bwana, ninaamini ya kuwa wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yeye ajaye ulimwenguni.”

  41. 4 Kuhubiri kwangu na ujumbe wangu haukuwa kwa hekima na maneno ya ushawishi bali kwa madhihirisho ya nguvu za Roho 5 ili imani yenu isiwe imejengwa katika hekima ya wanadamu bali katika nguvu za Mungu.

  42. 10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi. 12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 13 Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara. 14 Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15 nayo miguu yenu ifungiwe utayari tuupatao kwa Injili ya amani. 16 Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17 Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho, ambao ni Neno la Mungu. 18 Mkiomba kwa Roho siku zote katika sala zote na maombi, mkikesha kila wakati mkiwaombea watakatifu wote.

    19 Niombeeni na mimi pia, ili kila nifunguapo kinywa changu, nipewe maneno ya kusema, niweze kutangaza siri ya Injili kwa ujasiri, 20 ambayo mimi ni balozi wake katika vifungo. Ombeni ili nipate kuhubiri kwa ujasiri kama inipasavyo.

  43. 19 Kwa hiyo, ndugu zangu, kwa kuwa tunao ujasiri wa kupaingia Patakatifu pa Patakatifu kwa damu ya Yesu, 20 kwa njia mpya iliyo hai tuliyofunguliwa kwa ajili yetu kupitia kwenye lile pazia, yaani, mwili wake, 21 basi kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu juu ya nyumba ya Mungu, 22 sisi na tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu kwa imani timilifu, mioyo yetu ikiwa imenyunyizwa damu ya Kristo na kuwa safi kutokana na dhamiri mbaya nayo miili yetu ikiwa imeoshwa kwa maji safi. 23 Tushike kwa uthabiti lile tumaini la ukiri wetu bila kuyumbayumba, kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu. 24 Tuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema. 25 Wala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi, bali tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.

  44. 1 Basi ndugu zangu, kuhusu karama za rohoni, sitaki mkose kufahamu. 2 Mnajua kwamba mlipokuwa watu wasiomjua Mungu, kwa njia moja au ingine mlishawishika na kupotoshwa mkielekezwa kwa sanamu zisizonena. 3 Kwa hiyo nawaambieni ya kuwa hakuna mtu anayeongozwa na Roho wa Mungu anayeweza kusema, “Yesu na alaaniwe.” Pia hakuna mtu awezaye kusema, “Yesu ni Bwana,” isipokuwa ameongozwa na Roho Mtakatifu.

    4 Kuna aina mbalimbali za karama, lakini Roho ni yule yule. 5 Kuna huduma za aina mbalimbali, lakini Bwana ni yule yule. 6 Kisha kuna tofauti za kutenda kazi, lakini ni Mungu yule yule atendaye kazi zote kwa watu wote.

    7 Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote. 8 Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo. 9 Mtu mwingine imani kwa huyo Roho na mwingine karama za kuponya kwa huyo Roho mmoja. 10 Kwa mwingine matendo ya miujiza, kwa mwingine unabii kwa mwingine kupambanua roho, kwa mwingine aina mbalimbali za lugha, na kwa mwingine bado, tafsiri za lugha. 11 Haya yote hufanywa na huyo huyo Roho mmoja, Roho naye humgawia kila mtu, kama apendavyo.

  45. 16 Kwa hiyo nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. 17 Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka. 18 Lakini kama mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria.

    19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

    22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria. 24 Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake. 25 Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho.

  46. 1 Kwa sababu hii, kwa kuwa tumezungukwa na wingu kubwa namna hii la mashahidi, basi na tuweke kando kila kitu kinachotuzuia na ile dhambi inayotuzinga kwa urahisi, nasi tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa kwa ajili yetu. 2 Basi na tumtazame sana Yesu mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu, yeye ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake alistahimili msalaba, bila kujali aibu ya huo msalaba, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. 3 Mtafakarini sana yeye aliyestahimili upinzani mkuu namna hii kutoka kwa watu wenye dhambi, ili kwamba msije mkachoka na kukata tamaa.

    4 Katika kushindana kwenu dhidi ya dhambi, bado hamjapigana kiasi cha kumwaga damu yenu. 5 Nanyi mmesahau yale maneno ya kuwaonya yanayowataja ninyi kuwa wana, yakisema:

    “Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana,

    wala usikate tamaa akikukemea,

    6 kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao,

    na humwadhibu kila mmoja

    anayemkubali kuwa mwana.”

    7 Vumilieni taabu kwa ajili ya kufunzwa adabu. Mungu anawatendea ninyi kama watoto wake, kwa maana ni mtoto yupi asiyeadibishwa na mzazi wake? 8 Kama hakuna kuadibishwa (ambalo ni fungu la watoto wote), basi ninyi ni watoto wa haramu wala si watoto halali. 9 Tena, sisi sote tunao baba wa kimwili, waliotuadibisha nasi tukawaheshimu kwa ajili ya hilo. Je, si inatupasa kujinyenyekeza zaidi kwa Baba wa roho zetu ili tuishi? 10 Baba zetu walituadibisha kwa kitambo kidogo kama wao wenyewe walivyoona vyema, lakini Mungu hutuadibisha kwa faida yetu ili tupate kushiriki utakatifu wake. 11 Kuadibishwa wakati wowote hakuonekani kuwa kitu cha kufurahisha bali chenye maumivu kinapotekelezwa. Lakini baadaye huzaa matunda ya haki na amani kwa wale waliofunzwa nayo.

    12 Kwa hiyo, itieni nguvu mikono yenu iliyo dhaifu na magoti yenu yaliyolegea. 13 Sawazisheni mapito ya miguu yenu, ili kitu kilicho kiwete kisidhoofishwe bali kiponywe.

    14 Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo utakatifu, ambao bila kuwa nao hakuna mtu atakayemwona Bwana. 15 Angalieni sana mtu yeyote asiikose neema ya Mungu na kwamba shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo. 16 Angalieni miongoni mwenu asiwepo mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, ambaye kwa ajili ya mlo mmoja aliuza haki ya uzaliwa wake wa kwanza. 17 Baadaye kama mnavyofahamu, alipotaka kurithi ile baraka, alikataliwa, maana hakupata nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi.

  47. 1 Yuda, mtumwa wa Yesu Kristo na nduguye Yakobo:

    Kwa wale walioitwa, wapendwa katika Mungu Baba na kuhifadhiwa salama ndani ya Yesu Kristo:

    2 Rehema, amani na upendo viwe kwenu kwa wingi.

    3 Wapendwa, ingawa nilikuwa ninatamani sana kuwaandikia kuhusu wokovu ambao tunaushiriki sisi sote, niliona imenipasa kuwaandikia na kuwasihi kwamba mwitetee imani iliyokabidhiwa watakatifu kwa nafasi moja itoshayo.

  48. 22 Mara Yesu akawaambia wanafunzi wake waingie kwenye mashua watangulie kwenda ngʼambo ya bahari, wakati yeye alikuwa akiwaaga wale makutano. 23 Baada ya kuwaaga, akaenda zake mlimani peke yake kuomba. Jioni ilipofika, Yesu alikuwa huko peke yake. 24 Wakati huo ile mashua ilikuwa mbali kutoka nchi kavu ikisukwasukwa na mawimbi, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho.

    25 Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea wanafunzi wake akiwa anatembea juu ya maji. 26 Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji, waliingiwa na hofu kuu, wakasema, “Ni mzimu.” Wakapiga yowe kwa kuogopa.

    27 Lakini mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope.”

    28 Petro akamjibu, “Bwana, ikiwa ni wewe, niambie nije kwako nikitembea juu ya maji.”

    29 Yesu akamwambia, “Njoo.”

    Basi Petro akatoka kwenye chombo, akatembea juu ya maji kumwelekea Yesu. 30 Lakini alipoona upepo mkali aliingiwa na hofu, naye akaanza kuzama, huku akipiga kelele, “Bwana, niokoe!”

    31 Mara Yesu akaunyoosha mkono wake na kumshika, akamwambia, “Wewe mwenye imani haba, kwa nini uliona shaka?”

    32 Nao walipoingia ndani ya mashua, upepo ukakoma. 33 Ndipo wote waliokuwa ndani ya ile mashua wakamwabudu Yesu, wakisema, “Hakika, wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”

  49. 3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa.

  50. 2 Ningekuwa na karama ya unabii na kujua siri zote na maarifa yote, hata kama nina imani kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, mimi si kitu.

  51. 14 Kwa sababu hii nampigia Baba magoti, 15 ambaye ubaba wote wa kila jamaa za mbinguni na za duniani unatokana naye. 16 Namwomba Mungu awaimarishe kwa kuwatia nguvu mioyo yenu kwa njia ya Roho wake kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, 17 ili kwamba, Kristo apate kukaa mioyoni mwenu kwa njia ya imani. Nami ninaomba kwamba ninyi mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo, 18 mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Kristo, 19 na kujua upendo huu unaopita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu.

    20 Basi kwa yeye awezaye kutenda mambo ya ajabu yasiyopimika kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya uweza wake ule utendao kazi ndani yetu, 21 yeye atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu kwa vizazi vyote, milele na milele. Amen.

  52. 1 Ndugu, kuhusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanyika kwetu pamoja mbele zake, tunawasihi, 2 msiyumbishwe kwa urahisi wala msitiwe wasiwasi na roho wala neno au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu, isemayo kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwako. 3 Mtu yeyote na asiwadanganye kwa namna yoyote kwa maana siku ile haitakuja mpaka uasi utokee kwanza, na yule mtu wa kuasi adhihirishwe, yule ambaye amehukumiwa kuangamizwa kabisa. 4 Yeye atapingana na kujitukuza juu ya kila kitu kiitwacho Mungu au kinachoabudiwa, ili kujiweka juu katika Hekalu la Mungu, akijitangaza mwenyewe kuwa ndiye Mungu.

    5 Je, hamkumbuki ya kwamba nilipokuwa pamoja nanyi niliwaambia mambo haya? 6 Nanyi sasa mnajua kinachomzuia, ili apate kudhihirishwa wakati wake utakapowadia. 7 Maana ile nguvu ya siri ya uasi tayari inatenda kazi, lakini yule anayeizuia ataendelea kufanya hivyo mpaka atakapoondolewa. 8 Hapo ndipo yule mwasi atafunuliwa, ambaye Bwana Yesu atamteketeza kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kabisa kwa utukufu wa kuja kwake. 9 Kuja kwa yule mwasi kutaonekana kana kwamba ni kutenda kazi kwake Shetani ambaye hutumia nguvu zote, ishara, maajabu ya uongo, 10 na kila aina ya uovu kwa wale wanaoangamia kwa sababu walikataa kuipenda kweli wapate kuokolewa. 11 Kwa sababu hii, Mungu ameruhusu watawaliwe na nguvu ya udanganyifu, ili waendelee kuamini uongo, 12 na wahukumiwe wote ambao hawakuiamini ile kweli, bali wamefurahia uovu.

    13 Lakini imetupasa sisi kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu, ndugu mpendwao na Bwana, kwa sababu Mungu aliwachagua ninyi tangu mwanzo ili mwokolewe kwa kutakaswa na Roho kwa kuiamini kweli. 14 Kwa kusudi hili Mungu aliwaita kwa njia ya kuhubiri kwetu Injili, ili mpate kushiriki katika utukufu wa Bwana Yesu Kristo. 15 Hivyo basi, ndugu wapendwa, simameni imara na myashike sana yale mafundisho tuliyowapa ikiwa ni kwa maneno ya kinywa au kwa barua.

    16 Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu, aliyetupenda na kwa neema yake akatupatia faraja ya milele na tumaini jema, 17 awafariji mioyo yenu na kuwaimarisha katika kila neno na tendo jema.

  53. 27 Lakini lolote litakalotukia, mwenende kama ipasavyo Injili ya Kristo, ili kwamba nikija na kuwaona au ikiwa sipo, nipate kusikia haya juu yenu: Kuwa mnasimama imara katika roho moja, mkiishindania imani ya Injili kwa umoja, 28 wala msitishwe na wale wanaowapinga. Hii ni ishara kwao kuwa wataangamia, lakini ninyi mtaokolewa, na hii ni kazi ya Mungu. 29 Kwa maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, bali pia kuteswa kwa ajili yake, 30 kwa kuwa mnashiriki mashindano yale yale mliyoyaona nikiwa nayo na ambayo hata sasa mnasikia kuwa bado ninayo.

  54. 5 Kwa kuwa ingawa mimi siko pamoja nanyi kimwili, lakini niko pamoja nanyi kiroho, nami nafurahi kuuona utaratibu wenu na jinsi uthabiti wa imani yenu katika Kristo ulivyo.

    6 Hivyo basi, kama vile mlivyompokea Kristo Yesu kuwa Bwana, endeleeni kukaa ndani yake, 7 mkiwa na mizizi, na mmejengwa ndani yake, mkiimarishwa katika imani kama mlivyofundishwa, na kufurika kwa wingi wa shukrani.

  55. 8 Lakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo.

  56. 12 Mtu yeyote asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe kielelezo kizuri kwa waumini katika usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi.

  57. 21 Yesu aliondoka mahali pale, akaenda sehemu za Tiro na Sidoni. 22 Mwanamke mmoja Mkanaani aliyeishi sehemu jirani na hizo akaja kwake akilia, akasema, “Nihurumie, Ee Bwana, Mwana wa Daudi! Binti yangu amepagawa na pepo mchafu, na anateseka sana.”

    23 Lakini Yesu hakumjibu neno. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea na kumsihi sana, wakisema, “Mwambie aende zake, kwa maana anaendelea kutupigia kelele.”

    24 Yesu akajibu, “Nimetumwa tu kwa ajili ya kondoo wa Israeli waliopotea.”

    25 Lakini yule mwanamke akaja, akapiga magoti mbele ya Yesu, akasema, “Bwana, nisaidie!”

    26 Yesu akajibu, “Si haki kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”

    27 Yule mwanamke akajibu, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka kwenye meza za bwana zao.”

    28 Ndipo Yesu akamwambia, “Mwanamke, imani yako ni kubwa! Iwe kwako kama unavyotaka.” Naye binti yake akapona tangu saa ile.

  58. 16 Yeyote aaminiye na kubatizwa ataokoka. Lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa.

  59. 35 Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu. 36 Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake, na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa. 37 Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.”

    38 Maria akasema, “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana. Na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka, akamwacha.

  60. 31 Yesu akasema, “Simoni, Simoni, sikiliza, Shetani ameomba kuwapepeta ninyi wote kama ngano. 32 Lakini nimekuombea wewe Simoni ili imani yako isishindwe, nawe ukiisha kunirudia, uwaimarishe ndugu zako.”

    33 Petro akajibu, “Bwana, niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani na hata kifoni.”

    34 Yesu akamjibu, “Ninakuambia Petro, kabla jogoo hajawika usiku wa leo, utakana mara tatu kwamba hunijui mimi.”

  61. 24 “Amin, amin nawaambia, yeyote anayesikia maneno yangu na kumwamini yeye aliyenituma, anao uzima wa milele, naye hatahukumiwa, bali amepita kutoka mautini, na kuingia uzimani.

  62. 6 Mitume na wazee wakakutana pamoja ili kufikiri jambo hili. 7 Baada ya majadiliano mengi, Petro akasimama na kusema, “Ndugu zangu, mnajua kwamba siku za kwanza Mungu alinichagua ili kwa midomo yangu watu wa Mataifa wapate kusikia ujumbe wa Injili na kuamini. 8 Mungu, yeye ajuaye mioyo, alionyesha kwamba anawakubali kwa kuwapa Roho Mtakatifu kama vile alivyotupa sisi. 9 Mungu hakutofautisha kati yetu na wao, bali alitakasa mioyo yao kwa imani. 10 Sasa basi, mbona mnataka kumjaribu Mungu kwa kuweka kongwa shingoni mwa wanafunzi ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulibeba? 11 Lakini sisi tunaamini ya kuwa tunaokolewa kwa neema ya Bwana Yesu Kristo, kama wao wanavyookolewa.”

    12 Kusanyiko lote likakaa kimya, wakawasikiliza Paulo na Barnaba wakieleza jinsi Mungu alivyowatumia kutenda ishara na maajabu kwa watu wa Mataifa.

  63. 1 Mkaribisheni yeye ambaye imani yake ni dhaifu, lakini si kwa kugombana na kubishana juu ya mawazo yake. 2 Mtu mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu, lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula mboga tu. 3 Yeye alaye kila kitu asimdharau yeye asiyekula. Wala yeye asiyekula kila kitu asimhukumu yule alaye kila kitu, kwa maana Mungu amemkubali. 4 Wewe ni nani hata umhukumu mtumishi wa mtu mwingine? Kwa bwana wake tu anasimama au kuanguka. Naye atasimama kwa sababu Bwana anaweza kumsimamisha.

  64. 26 Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani. 27 Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo.

  65. 7 Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, sasa nayahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. 8 Zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara tupu nikiyalinganisha na faida kubwa ipitayo kiasi cha kumjua Kristo Yesu Bwana wangu, ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote, nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Kristo. 9 Nami nionekane mbele zake bila kuwa na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu kwa njia ya imani. 10 Nataka nimjue Kristo na uweza wa kufufuka kwake na ushirika wa mateso yake, ili nifanane naye katika mauti yake, 11 ili kwa njia yoyote niweze kufikia ufufuo wa wafu.

  66. 14 Je, kuna yeyote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Basi inampasa awaite wazee wa kanisa wamwombee na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana. 15 Kule kuomba kwa imani kutamwokoa huyo mgonjwa, naye Bwana atamwinua na kama ametenda dhambi, atasamehewa.

  67. 6 Yoshua mwana wa Nuni na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwa watu wale waliokwenda kuipeleleza nchi, wakararua nguo zao, 7 wakasema na kusanyiko lote la Kiisraeli, wakawaambia, “Nchi tuliyopita katikati yake na kuipeleleza ni nzuri sana sana. 8 Ikiwa Bwana anapendezwa nasi, atatuongoza kuingia katika nchi ile, nchi itiririkayo maziwa na asali, naye atatupa nchi hiyo. 9 Ila tu msimwasi Bwana. Wala msiwaogope watu wa nchi hiyo, kwa sababu tutawameza. Ulinzi wao umeondoka, lakini Bwana yupo pamoja nasi. Msiwaogope.”

  68. 28 Alipoingia mle nyumbani wale vipofu wakamjia. Naye Yesu akawauliza, “Mnaamini kwamba ninaweza kufanya jambo hili?”

    Wakamjibu, “Ndiyo, Bwana.”

    29 Ndipo Yesu akagusa macho yao na kusema, “Iwe kwenu sawasawa na imani yenu.” 30 Macho yao yakafunguka. Yesu akawaonya vikali, akisema, “Angalieni mtu yeyote asijue kuhusu jambo hili.”

  69. 28 Ndipo wakamuuliza, “Tufanye nini ili tupate kuitenda kazi ya Mungu?”

    29 Yesu akawajibu, “Kazi ya Mungu ndiyo hii: Mwaminini yeye aliyetumwa naye.”

  70. 1 Kwa hiyo, tukiachana na mafundisho yale ya awali kuhusu Kristo na tukisonga mbele ili tufikie utimilifu, sio kuweka tena msingi wa mafundisho ya kuzitubia kazi zisizo na uhai na imani katika Mungu, 2 mafundisho kuhusu aina za ubatizo, kuwekea watu mikono, ufufuo wa wafu, na hukumu ya milele. 3 Mungu akitujalia tutafanya hivyo.

    4 Kwa kuwa ni vigumu kwa wale ambao wakati fulani walishapata nuru, ambao walishaonja kipawa cha mbinguni, ambao wamekwisha kushiriki katika Roho Mtakatifu, 5 ambao wameonja uzuri wa Neno la Mungu na nguvu za wakati ujao, 6 kisha wakianguka, kuwarejesha tena katika toba. Kwa kuwa wanamsulubisha Mwana wa Mungu mara ya pili na kumdhalilisha hadharani, nayo ikawa hasara kwao.

    7 Ardhi ile ipokeayo mvua inyeshayo juu yake mara kwa mara hutoa mazao yanayowanufaisha wale ambao kwa ajili yao yalimwa, nayo nchi hiyo hupokea baraka kutoka kwa Mungu. 8 Lakini ardhi ikizaa miiba na mibaruti, haina thamani na iko hatarini ya kulaaniwa. Mwisho wake ni kuchomwa moto.

  71. 40 Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa hivyo? Je, bado hamna imani?”

    41 Nao wakawa wameogopa sana, wakaulizana, “Ni nani huyu ambaye hata upepo na mawimbi vinamtii?”

  72. 4 Umati mkubwa wa watu ulipokuwa ukija kwa Yesu kutoka kila mji, akawaambia mfano huu: 5 “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia; zikakanyagwa, nao ndege wa angani wakazila. 6 Mbegu nyingine zilianguka penye miamba, nazo zilipoota, hiyo mimea ikakauka kwa kukosa unyevu. 7 Nazo mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo ile miiba ikakua pamoja nazo, na kuisonga hiyo mimea. 8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri. Zikaota na kuzaa mara mia moja zaidi ya mbegu alizopanda.”

    Baada ya kusema haya, Yesu akapaza sauti, akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

    9 Wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano huo. 10 Naye akasema, “Ninyi mmepewa kufahamu siri za Ufalme wa Mungu, lakini kwa wengine nazungumza kwa mifano, ili,

    “ ‘ingawa wanatazama, wasione;

    ingawa wanasikiliza, wasielewe.’

    11 “Maana ya mfano huu ni hii: Mbegu ni neno la Mungu. 12 Zile zilizoanguka kando ya njia ni wale ambao husikia neno, naye ibilisi anakuja na kuliondoa neno kutoka mioyoni mwao, ili wasije wakaamini na kuokoka. 13 Zile mbegu zilizoanguka kwenye mwamba ni wale ambao hulipokea neno kwa furaha wanapolisikia, lakini hawana mizizi. Wanaamini kwa muda mfupi, lakini wakati wa kujaribiwa huiacha imani. 14 Zile mbegu zilizoanguka kwenye miiba ni mfano wa wale wanaosikia, lakini wanapoendelea husongwa na masumbufu ya maisha haya, utajiri na anasa, nao hawakui. 15 Lakini zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo mzuri ni mfano wa wale ambao hulisikia neno la Mungu na kulishika kwa moyo mnyofu wa utiifu, nao kwa kuvumilia kwingi huzaa matunda.

  73. 23 Lakini kama mtu ana shaka kuhusu kile anachokula, amehukumiwa, kwa sababu hakula kwa imani. Kwa kuwa chochote kinachofanywa pasipo imani ni dhambi.

  74. 3 Kama nilivyokusihi wakati nilipokwenda Makedonia, endelea kubaki Efeso, ili kwamba upate kuwaagiza watu wasiendelee kufundisha mafundisho ya uongo 4 wala wasitoe muda wao kwa hadithi za kubuniwa na orodha za majina ya vizazi visivyo na mwisho, ambazo huchochea mabishano badala ya mpango wa Mungu utokanao na imani. 5 Kusudi la maagizo haya ni upendo utokao katika moyo safi, dhamiri njema na imani ya kweli. 6 Watu wengine wamepotoka kutoka haya na kugeukia majadiliano yasiyo na maana kwa kuwa, 7 wanataka kuwa walimu wa sheria, lakini hawajui mambo yale wanayosema wala hayo wanayoyatumainia kwa uthabiti.

    8 Tunajua kwamba sheria ni njema ikiwa inatumika kwa halali kama ilivyokusudiwa. 9 Lakini tunajua ya kuwa sheria si kwa ajili ya wenye haki, bali kwa ajili ya wavunja sheria na waasi, kwa ajili ya wasiomcha Mungu na wenye dhambi, wasio watakatifu na wanaokufuru; kwa wale wawauao baba zao au mama zao, kwa wauaji, 10 kwa wazinzi na wahanithi, kwa wale wauzao watu, na kwa waongo na waapao kwa uongo, na kwa chochote kingine kilicho kinyume na mafundisho ya kweli, 11 ambayo yanakubaliana na Injili ya utukufu wa Mungu anayehimidiwa, ambayo mimi nimewekewa amana.

  75. 6 Bwana yuko pamoja nami, sitaogopa.

    Mwanadamu anaweza kunitenda nini?

    7 Bwana yuko pamoja nami,

    yeye ni msaidizi wangu.

    Nitawatazama adui zangu

    wakiwa wameshindwa.

    8 Ni bora kumkimbilia Bwana

    kuliko kumtumainia mwanadamu.

    9 Ni bora kumkimbilia Bwana

    kuliko kuwatumainia wakuu.

  76. 24 Niliwaambia kuwa mtakufa katika dhambi zenu, kwa maana msipoamini ya kwamba ‘Mimi Ndiye,’ mtakufa katika dhambi zenu.”

  77. 24 Kwa kuwa tuliokolewa kwa tumaini hili. Lakini kama kinachotumainiwa kikionekana hakiwi tumaini tena. Je, kuna mtu anayetumaini kupata kitu alicho nacho tayari? 25 Lakini tunapotumaini kupata kitu ambacho hatuna, basi twakingojea kwa saburi.

    26 Vivyo hivyo, Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa sababu hatujui kuomba ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa uchungu usioweza kutamkwa. 27 Naye Mungu aichunguzaye mioyo, anaijua nia ya Roho, kwa sababu Roho huwaombea watakatifu sawasawa na mapenzi ya Mungu.

    28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. 29 Maana wale Mungu aliowajua tangu mwanzo, pia aliwachagua tangu mwanzo, wapate kufanana na mfano wa Mwanawe, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.

  78. 5 Jichunguzeni wenyewe mwone kama mnaishi katika imani. Jipimeni wenyewe. Je, hamtambui ya kuwa Yesu Kristo yumo ndani yenu? Kama sivyo, basi, mmeshindwa kufikia kipimo hicho! 6 Natumaini mtaona kuwa sisi hatukushindwa.

  79. 10 Usiogope mateso yatakayokupata. Nakuambia ibilisi atawatia baadhi yenu gerezani ili kuwajaribu, nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.