32 Bible Verses About Fasting

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Fasting
  1. 16 “Mnapofunga, msiwe wenye huzuni kama wafanyavyo wanafiki. Maana wao hukunja nyuso zao ili kuwaonyesha wengine kwamba wamefunga. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupata thawabu yao kamilifu. 17 Lakini mnapofunga, jipakeni mafuta kichwani na kunawa nyuso zenu 18 ili kufunga kwenu kusionekane na watu wengine ila Baba yenu aketiye mahali pa siri; naye Baba yenu aonaye sirini atawapa thawabu yenu kwa wazi.

  2. Safari Ya Kwanza Ya Paulo Kueneza Injili

    1 Katika kanisa huko Antiokia ya Shamu walikuwako manabii na walimu, yaani: Barnaba, Simeoni aitwaye Nigeri, Lukio Mkirene, Manaeni aliyekuwa amelelewa pamoja na Mfalme Herode Agripa, na Sauli. 2 Walipokuwa wakimwabudu Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, “Nitengeeni Sauli na Barnaba kwa kazi ile maalum niliyowaitia.” 3 Ndipo baada ya kufunga na kuomba, wakawawekea mikono yao na wakawatuma waende zao.

    4 Hivyo, wakiwa wametumwa na Roho Mtakatifu, wakashuka kwenda Seleukia na kutoka huko wakasafiri baharini mpaka kisiwa cha Kipro.

  3. 3 Wao husema, ‘Mbona tumefunga, nawe hujaona?

    Mbona tumejinyenyekeza, nawe huangalii?’

    “Lakini katika siku ya kufunga kwenu, mnafanya mnavyotaka

    na kuwadhulumu wafanyakazi wenu wote.

    4 Kufunga kwenu huishia kwenye magomvi na mapigano,

    na kupigana ninyi kwa ninyi kwa ngumi za uovu.

    Hamwezi kufunga kama mnavyofanya leo

    na kutazamia sauti zenu kusikiwa huko juu.

    5 Je, hii ndiyo aina ya mfungo niliouchagua,

    siku moja tu ya mtu kujinyenyekeza?

    Je, ni kwa kuinamisha kichwa chini kama tete,

    na kwa kujilaza juu ya nguo ya gunia na majivu?

    Je, huo ndio mnaouita mfungo,

    siku iliyokubalika kwa Bwana?

    6 “Je, hii si ndiyo aina ya mfungo niliyoichagua:

    kufungua minyororo ya udhalimu,

    na kufungua kamba za nira,

    kuwaweka huru walioonewa,

    na kuvunja kila nira?

    7 Je, sio kushirikiana chakula chako na wenye njaa

    na kuwapatia maskini wasiokuwa na makao hifadhi,

    unapomwona aliye uchi, umvike,

    wala si kumkimbia mtu wa nyama na damu yako mwenyewe?

    8 Ndipo nuru yako itajitokeza kama mapambazuko

    na uponyaji wako utatokea upesi;

    ndipo haki yako itakapokutangulia mbele yako,

    na utukufu wa Bwana utakuwa mlinzi nyuma yako.

    9 Ndipo utaita, naye Bwana atajibu,

    utalia kuomba msaada,

    naye atasema: Mimi hapa.

    “Kama ukiiondoa nira ya udhalimu,

    na kunyoosha kidole na kuzungumza maovu,

    10 nanyi kama mkimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi zenu

    na kutosheleza mahitaji ya walioonewa,

    ndipo nuru yenu itakapongʼaa gizani,

    nao usiku wenu utakuwa kama adhuhuri.

    11 Bwana atakuongoza siku zote,

    atayatosheleza mahitaji yako katika nchi kame,

    naye ataitia nguvu mifupa yako.

    Utakuwa kama bustani iliyonyweshwa vizuri,

    kama chemchemi ambayo maji yake hayakauki kamwe.

    12 Watu wako watajenga tena magofu ya zamani

    na kuinua misingi ya kale;

    utaitwa Mwenye Kukarabati Kuta Zilizobomoka,

    Mwenye Kurejeza Barabara za Makao.

  4. 21 Kando ya Mto Ahava, hapo nilitangaza kufunga, ili tujinyenyekeshe mbele za Mungu wetu na kumwomba kwa ajili ya kutujalia safari ya amani sisi na watoto wetu, pamoja na mali zetu zote. 22 Niliona aibu kumwomba mfalme askari na wapanda farasi wa kutulinda njiani kutokana na adui zetu, kwa sababu tulikwisha kumwambia mfalme, “Mkono wa neema wa Mungu wetu uko juu ya kila mmoja anayemtafuta, lakini hasira yake kubwa ni dhidi ya wote wamwachao.” 23 Kwa hiyo tulifunga na kumwomba Mungu wetu kuhusu jambo hili, naye akajibu maombi yetu.

  5. 9 Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine: 10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. 11 Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. 12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’

    13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’

    14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”

  6. 14 Wanafunzi wa Yohana Mbatizaji wakaja na kumuuliza Yesu, “Imekuwaje kwamba sisi na Mafarisayo tunafunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?”

    15 Yesu akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wawezaje kuomboleza wakati angali pamoja nao? Wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Hapo ndipo watakapofunga.

    16 “Hakuna mtu anayeshonea kiraka kipya kwenye nguo iliyochakaa, kwa maana kile kiraka kitachanika kutoka kwenye hiyo nguo, nayo hiyo nguo itachanika zaidi. 17 Wala watu hawaweki divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Kama wakifanya hivyo, viriba vitapasuka nayo divai itamwagika, navyo viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya, na hivyo divai na viriba huwa salama.”

  7. 13 Lakini walipokuwa wagonjwa, nilivaa nguo ya gunia

    na nikajinyenyekesha kwa kufunga.

    Maombi yangu yaliponirudia bila kujibiwa,

    14 niliendelea kuomboleza

    kama vile wao ni rafiki au ndugu.

    Niliinamisha kichwa chini kwa huzuni

    kama ninayemwombolezea mama yangu.

  8. 12 “Hata sasa,” asema Bwana,

    “nirudieni kwa mioyo yenu yote,

    kwa kufunga, kwa kulia na kuomboleza.”

    13 Rarueni mioyo yenu

    na siyo mavazi yenu.

    Mrudieni Bwana, Mungu wenu,

    kwa maana yeye ndiye mwenye neema

    na mwingi wa huruma,

    si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo,

    huona huruma, hujizuia kuleta maafa.

    14 Ni nani ajuaye? Yeye aweza kugeuka na kuwa na huruma

    na kuacha baraka nyuma yake:

    sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji

    kwa ajili ya Bwana Mungu wenu.

    15 Pigeni tarumbeta katika Sayuni,

    tangazeni saumu takatifu,

    liiteni kusanyiko takatifu.

    16 Wakusanyeni watu,

    wekeni wakfu kusanyiko;

    waleteni pamoja wazee,

    wakusanyeni watoto,

    wale wanyonyao maziwa.

    Bwana arusi na atoke chumbani mwake

    na bibi arusi naye atoke katika chumba chake.

  9. 1 Kisha Yesu akaongozwa na Roho Mtakatifu kwenda nyikani ili akajaribiwe na ibilisi. 2 Baada ya kufunga siku arobaini usiku na mchana, hatimaye akaona njaa. 3 Mjaribu akamjia na kumwambia, “Ikiwa wewe ndiye Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate.”

    4 Lakini Yesu akajibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’ ”

  10. 1 Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Dario mwana wa Ahasuero (mzaliwa wa Umedi), ambaye alifanywa mtawala juu ya ufalme wa Babeli, 2 katika mwaka wa kwanza wa utawala wake, mimi Danieli nilielewa kutokana na Maandiko, kulingana na neno la Bwana alilopewa nabii Yeremia, kwamba ukiwa wa Yerusalemu ungetimizwa kwa miaka sabini. 3 Kwa hiyo nikamgeukia Bwana Mungu na kumsihi katika maombi na dua, katika kufunga, na kuvaa nguo ya gunia na kujipaka majivu.

    4 Nikamwomba Bwana Mungu wangu na kutubu:

    “Ee Bwana, Mungu mkuu na unayetisha, anayeshika agano lake la upendo kwao wanaompenda na kutii maagizo yake, 5 tumetenda dhambi na kufanya mabaya. Tumekuwa waovu na tumeasi; tumegeuka mbali na maagizo yako na sheria zako. 6 Hatukuwasikiliza watumishi wako manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, wakuu wetu, baba zetu, na watu wote wa nchi.

  11. 1 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi, Danieli (ambaye aliitwa Belteshaza) alipewa ufunuo. Ujumbe wake ulikuwa kweli, nao ulihusu vita vikubwa. Ufahamu wa ujumbe ulimjia katika maono.

    2 Wakati huo, mimi Danieli nikaomboleza kwa majuma matatu. 3 Sikula chakula kizuri; nyama wala divai havikugusa midomo yangu; nami sikujipaka mafuta kamwe mpaka majuma matatu yalipotimia.

    4 Kwenye siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilipokuwa nimesimama kwenye ukingo wa mto mkubwa Hidekeli, 5 nikatazama juu, na mbele yangu alikuwepo mtu aliyevaa mavazi ya kitani na mshipi wa dhahabu safi kutoka ufazi kiunoni mwake. 6 Mwili wake ulikuwa kama kito cha zabarajadi safi, uso wake kama umeme wa radi, macho yake kama mwali wa moto, mikono yake na miguu yake kama mngʼao wa shaba iliyosuguliwa sana, nayo sauti yake kama ya umati mkubwa wa watu.

  12. 36 Tena alikuwako Hekaluni nabii mmoja mwanamke, jina lake Ana binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa mzee sana; naye alikuwa ameolewa na kuishi na mume kwa miaka saba tu, kisha mumewe akafa. 37 Hivyo alikuwa mjane na umri wake ulikuwa miaka themanini na minne. Yeye hakuondoka humo Hekaluni usiku wala mchana, bali alikuwa akimwabudu Mungu, akifunga na kuomba. 38 Wakati huo huo, Ana alikuja akaanza kusifu, akimshukuru Mungu na kusema habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wakitarajia ukombozi wa Yerusalemu.

  13. 21 Wakahubiri habari njema katika mji huo na kupata wanafunzi wengi. Kisha wakarudi Listra, Ikonio na Antiokia, 22 wakiwaimarisha wanafunzi na kuwatia moyo waendelee kudumu katika imani. Wakawaonya wakisema, “Imetupasa kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa kupitia katika taabu nyingi.” 23 Nao baada ya kuwateua wazee katika kila kanisa, kwa kufunga na kuomba wakawakabidhi kwa Bwana waliyemwamini.

  14. 33 Wakamwambia Yesu, “Wanafunzi wa Yohana na wa Mafarisayo mara kwa mara hufunga na kuomba, lakini wanafunzi wako wanaendelea kula na kunywa.”

    34 Yesu akawajibu, “Je, mnaweza kuwafanya wageni wa bwana arusi kufunga wakati yuko pamoja nao? 35 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Hapo ndipo watakapofunga.”

    36 Yesu akawapa mfano huu, akawaambia: “Hakuna mtu achanaye kiraka kutoka kwenye nguo mpya na kukishonea kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, atakuwa amechana nguo mpya, na kile kiraka hakitalingana na ile nguo iliyochakaa. 37 Hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, hiyo divai mpya itavipasua hivyo viriba, nayo yote itamwagika. 38 Divai mpya lazima iwekwe kwenye viriba vipya.

  15. 1 Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi ule ule, Waisraeli walikusanyika pamoja, wakifunga na kuvaa nguo za gunia na kujitia mavumbi vichwani mwao. 2 Wale wa uzao wa Israeli walijitenga na wageni wote. Wakasimama mahali pao, na kuungama dhambi zao na uovu wa baba zao. 3 Wakasimama pale walipokuwa, wakasoma kutoka kwenye kile Kitabu cha Sheria ya Bwana Mungu wao kwa muda wa robo siku, na wakatumia robo nyingine kwa kuungama dhambi na kumwabudu Bwana Mungu wao.

  16. 28 Mose alikuwa huko pamoja na Bwana kwa siku arobaini usiku na mchana bila kula chakula wala kunywa maji. Naye akaandika juu ya vibao maneno ya Agano, yaani zile Amri Kumi.

    29 Mose alipoteremka kutoka Mlima Sinai akiwa na vile vibao viwili vya Ushuhuda mikononi mwake, hakujua kuwa uso wake ulikuwa ukingʼaa, kwa sababu alikuwa amezungumza na Bwana.

  17. 11 Ndipo Daudi pamoja na watu wote waliokuwa pamoja naye wakazishika nguo zao na kuzirarua. 12 Wakaomboleza, wakalia pia na kufunga mpaka jioni kwa ajili ya Sauli na Yonathani mwanawe, kwa ajili ya jeshi la Bwana na nyumba ya Israeli, kwa sababu wameanguka kwa upanga.

  18. 4 Mwanamke hana mamlaka juu ya mwili wake bali mumewe, wala mume hana mamlaka juu ya mwili wake bali mkewe. 5 Msinyimane, isipokuwa mmekubaliana kufanya hivyo kwa muda fulani ili mweze kujitoa kwa maombi, kisha mrudiane tena ili Shetani asije akapata nafasi ya kuwajaribu kwa sababu ya kutokuwa na kiasi.

  19. 16 Nilimleta kwa wanafunzi wako, lakini hawakuweza kumponya.”

    17 Yesu akajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni mvulana hapa kwangu.” 18 Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akamtoka yule kijana, naye akapona saa ile ile.

    19 Kisha wanafunzi wakamwendea Yesu wakiwa peke yao, wakamuuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?”

    20 Akawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu ndogo. Ninawaambia kweli, mkiwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mtauambia mlima huu, ‘Ondoka hapa uende pale,’ nao utaondoka. Wala hakutakuwa na jambo lisilowezekana kwenu. [ 21 Lakini hali kama hii haitoki ila kwa kuomba na kufunga.]”

  20. 5 Watu wa Ninawi wakamwamini Mungu, wakatangaza kufunga, watu wote kuanzia mkubwa sana hadi yule mdogo kabisa, wakavaa nguo za gunia.

    6 Habari zilipomfikia mfalme wa Ninawi, aliondoka kwenye kiti chake cha enzi, akavua majoho yake ya kifalme, akajifunika nguo ya gunia kisha akaketi chini mavumbini. 7 Ndipo akatoa tangazo katika Ninawi yote:

    “Kwa amri ya mfalme na wakuu wake:

    “Msiruhusu mtu yeyote au mnyama, makundi ya ngʼombe au wanyama wengine wafugwao, kuonja kitu chochote, msiwaruhusu kula wala kunywa. 8 Bali wanadamu na wanyama wafunikwe kwa nguo za gunia. Kila mmoja afanye hima kumwomba Mungu. Waziache njia zao mbaya na udhalimu ulio mikononi mwao. 9 Ni nani ajuaye? Huenda Mungu akaghairi kwa huruma yake akaacha hasira yake kali ili tusiangamie.”

    10 Mungu alipoona walivyofanya na jinsi walivyogeuka kutoka njia zao mbaya, akawa na huruma wala hakuleta maangamizi juu yao kama alivyokuwa ameonya.

  21. 4 Kisha neno la Bwana Mwenye Nguvu Zote likanijia kusema: 5 “Waulize watu wote wa nchi na makuhani, ‘Je, mlipofunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na wa saba kwa miaka sabini iliyopita, mlifunga kweli kwa ajili yangu? 6 Na mlipokuwa mkila na kunywa, je, hamkuwa mnasherehekea kwa ajili ya nafsi zenu?

  22. 15 Baada ya Nathani kurudi nyumbani kwake, Bwana akampiga yule mtoto ambaye mke wa Uria alikuwa amemzalia Daudi, akaugua. 16 Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto. Akafunga na akaingia ndani ya nyumba yake akawa siku zote analala sakafuni usiku kucha. 17 Wazee wa nyumbani mwake wakamwendea wakasimama karibu naye ili kumwamsha kutoka pale sakafuni, lakini akakataa, wala hakula chochote pamoja nao.

    18 Kunako siku ya saba yule mtoto akafa. Watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia kuwa mtoto amekufa, kwa maana walifikiri, “Wakati mtoto alipokuwa angali hai, tulizungumza na Daudi lakini hakutusikiliza. Tutawezaje kumwambia kwamba mtoto amekufa? Anaweza kufanya kitu cha kujidhuru.”

  23. 8 Kwa hiyo akainuka, akala na kunywa. Akiwa ametiwa nguvu na kile chakula, akasafiri siku arobaini usiku na mchana mpaka akafika Horebu, mlima wa Mungu.

  24. 2 Watu fulani wakaja wakamwambia Yehoshafati, “Jeshi kubwa linakuja dhidi yako kutoka Edomu tokea ngʼambo ile nyingine ya Bahari. Tayari liko Hasason-Tamari” (yaani En-Gedi). 3 Yehoshafati akaogopa, akaazimu kumtafuta Bwana, na akatangaza kwa Yuda wote kufunga. 4 Watu wa Yuda wakakusanyika pamoja ili kutafuta msaada kutoka kwa Bwana. Wakaja kutoka kila mji wa Yuda ili kumtafuta.

  25. 11 Kisha Bwana akaniambia, “Usiombe kwa ajili ya mafanikio ya watu hawa. 12 Ingawa wanafunga, sitasikiliza kilio chao; hata wakitoa dhabihu za kuteketezwa na dhabihu za nafaka, sitazikubali. Badala yake, nitawaangamiza kwa upanga, njaa na tauni.”

  26. 13 Vaeni nguo ya gunia, enyi makuhani, muomboleze;

    pigeni yowe, enyi mnaohudumu madhabahuni.

    Njooni, vaeni nguo ya gunia usiku kucha,

    enyi mnaohudumu mbele za Mungu wangu;

    kwa kuwa sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji

    zimezuiliwa kufika katika nyumba ya Mungu wenu.

    14 Tangazeni saumu takatifu;

    liiteni kusanyiko takatifu.

    Iteni wazee

    na wote waishio katika nchi

    waende katika nyumba ya Bwana Mungu wenu,

    wakamlilie Bwana.

  27. 8 Sauli akainuka kutoka pale chini na alipojaribu kufungua macho yake hakuweza kuona kitu chochote. Basi wakamshika mkono wakamwongoza mpaka Dameski. 9 Naye kwa muda wa siku tatu alikuwa kipofu naye hakula wala kunywa chochote.

    10 Huko Dameski alikuwepo mwanafunzi mmoja jina lake Anania. Bwana alimwita katika maono, “Anania!”

    Akajibu, “Mimi hapa Bwana.”

    11 Bwana akamwambia, “Ondoka uende katika barabara iitwayo Nyofu ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu kutoka Tarso, jina lake Sauli, kwa maana wakati huu anaomba, 12 katika maono amemwona mtu aitwaye Anania akija na kuweka mikono juu yake ili apate kuona tena.”

  28. 30 Kornelio akajibu, “Siku nne zilizopita, nilikuwa nyumbani nikisali saa kama hii, saa tisa alasiri. Ghafula mtu aliyevaa nguo zilizongʼaa akasimama mbele yangu, 31 akasema, ‘Kornelio, maombi yako yamesikiwa na sadaka zako kwa maskini zimekumbukwa mbele za Mungu.

  29. 18 Ndipo tena nikasujudu mbele za Bwana kwa siku arobaini usiku na mchana. Sikula mkate wala sikunywa maji, kwa sababu ya dhambi yote mliyoifanya, mkifanya lile lililo ovu mbele za Bwana na kumkasirisha.

  30. 33 Kabla ya mapambazuko, Paulo akawasihi watu wote wale chakula akisema, “Leo ni siku ya kumi na nne mmekuwa katika wasiwasi mkiwa mmefunga na bila kula chochote. 34 Kwa hiyo nawasihi mle chakula, kwa maana itawasaidia ili mweze kuishi. Kwa kuwa hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza unywele hata mmoja kutoka kichwani mwake.”

  31. 1 “Angalieni msitende wema wenu mbele ya watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni.

    2 “Hivyo mnapowapa wahitaji, msipige panda mbele yenu kama wafanyavyo wanafiki katika masinagogi na mitaani, ili wasifiwe na watu. Amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao. 3 Lakini ninyi mtoapo sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa kushoto usijue mkono wako wa kuume unachofanya, 4 ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo Baba yako wa mbinguni, yeye aonaye sirini atakupa thawabu kwa wazi.

  32. 24 Magoti yangu yamelegea kwa kufunga,

    mwili wangu umedhoofika na kukonda.