34 Bible Verses About Confession

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Confession
  1. 13 Je, mtu yeyote miongoni mwenu amepatwa na taabu? Basi inampasa aombe. Je, kuna yeyote mwenye furaha? Basi na aimbe nyimbo za kusifu. 14 Je, kuna yeyote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Basi inampasa awaite wazee wa kanisa wamwombee na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana. 15 Kule kuomba kwa imani kutamwokoa huyo mgonjwa, naye Bwana atamwinua na kama ametenda dhambi, atasamehewa. 16 Kwa hiyo ungamianeni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu tena yanafaa sana.

    17 Eliya alikuwa mwanadamu kama sisi. Akaomba kwa bidii kwamba mvua isinyeshe, nayo haikunyesha juu ya nchi kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita. 18 Kisha akaomba tena, nazo mbingu zikatoa mvua nayo ardhi ikatoa mazao yake.

    19 Ndugu zangu, yeyote miongoni mwenu akipotoka na kuicha kweli, naye akarejezwa na mtu mwingine, 20 hamna budi kujua kwamba yeyote amrejezaye mwenye dhambi kutoka upotovu wake, ataiokoa roho ya huyo mwenye dhambi kutoka mauti na kusitiri wingi wa dhambi.

  2. 6 Kama tukisema kwamba twashirikiana naye huku tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatutendi lililo kweli. 7 Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo nuruni, twashirikiana sisi kwa sisi na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.

    8 Kama tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu. 9 Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutoka kwenye udhalimu wote. 10 Kama tukisema hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo na neno lake halimo ndani yetu.

  3. 9 Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine: 10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. 11 Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. 12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’

    13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’

    14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”

  4. 2 Heri mtu yule ambaye Bwana

    hamhesabii dhambi,

    na ambaye rohoni mwake

    hamna udanganyifu.

    3 Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa

    kwa kulia kwa maumivu makali mchana kutwa.

    4 Usiku na mchana

    mkono wako ulinilemea,

    nguvu zangu zilinyonywa

    kama vile katika joto la kiangazi.

    5 Kisha nilikujulisha dhambi yangu

    wala sikuficha uovu wangu.

    Nilisema, “Nitaungama

    makosa yangu kwa Bwana.”

    Ndipo uliponisamehe

    hatia ya dhambi yangu.

    6 Kwa hiyo kila mtu mcha Mungu akuombe

    wakati unapopatikana,

    hakika maji makuu yatakapofurika

    hayatamfikia yeye.

  5. 3 Kwa hiyo, jilindeni.

    “Kama ndugu yako akikukosea mwonye, naye akitubu, msamehe. 4 Kama akikukosea mara saba kwa siku moja na mara saba kwa siku moja akaja kwako akisema, ‘Ninatubu,’ msamehe.”

  6. 13 Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa,

    bali yeyote aziungamaye na kuziacha hupata rehema.

    14 Amebarikiwa mtu ambaye siku zote humcha Bwana,

    bali yeye afanyaye moyo wake kuwa mgumu

    huangukia kwenye taabu.

  7. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Baada ya kukemewa na nabii Nathani kwa kuzini na Bathsheba.

    1 Ee Mungu, unihurumie,

    kwa kadiri ya upendo wako usiokoma,

    kwa kadiri ya huruma yako kuu,

    uyafute makosa yangu.

    2 Unioshe na uovu wangu wote

    na unitakase dhambi yangu.

    3 Kwa maana ninajua makosa yangu,

    na dhambi yangu iko mbele yangu daima.

    4 Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi

    na kufanya yaliyo mabaya machoni pako,

    ili uthibitike kuwa wa kweli unenapo,

    na kuwa na haki utoapo hukumu.

    5 Hakika mimi nilizaliwa mwenye dhambi,

    mwenye dhambi tangu nilipotungwa mimba kwa mama yangu.

  8. 32 “Kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, mimi nami nitamkiri yeye mbele za Baba yangu aliye mbinguni. 33 Lakini yeyote atakayenikana mimi mbele ya watu, mimi nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.”

  9. 18 Wengi wa wale waliokuwa wameamini wakati huu wakaja na kutubu waziwazi kuhusu matendo yao maovu. 19 Idadi kubwa ya wale waliofanya mambo ya uganga wakaleta vitabu vyao na kuviteketeza kwa moto hadharani. Walipofanya hesabu ya thamani ya vitabu vilivyoteketezwa ilikuwa drakma 50,000 za fedha.

  10. 5 “ ‘Wakati mtu yeyote atakapokuwa na hatia katika mojawapo ya haya, lazima akiri ni kwa njia gani ametenda dhambi,

  11. 40 “ ‘Lakini kama watatubu dhambi zao na dhambi za baba zao, udanganyifu wao dhidi yangu na uadui wao kwangu, 41 ambao ulinifanya niwe na uadui nao hata nikawapeleka katika nchi ya adui zao, wakati mioyo yao isiyotahiriwa itanyenyekea na kutubu dhambi yao, 42 nami nitakumbuka agano langu na Yakobo, na agano langu na Isaki, na agano langu na Abrahamu, nami nitaikumbuka nchi.

  12. 6 Lakini yeye hutupatia neema zaidi. Hii ndiyo sababu Andiko husema:

    “Mungu huwapinga wenye kiburi,

    lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

    7 Basi mtiini Mungu. Mpingeni ibilisi, naye atawakimbia. 8 Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu ninyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu ninyi wenye nia mbili. 9 Huzunikeni, ombolezeni na kulia. Kicheko chenu na kigeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa huzuni. 10 Jinyenyekezeni mbele za Bwana, naye atawainua.

  13. 6 Lakini, ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Ndipo akamwambia yule aliyepooza, “Inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.” 7 Yule mtu akasimama, akaenda nyumbani kwake. 8 Makutano walipoyaona haya, wakajawa na hofu ya Mungu, wakamtukuza Mungu ambaye alikuwa ametoa mamlaka kama haya kwa wanadamu.

  14. 20 “Aroni atakapokuwa amemaliza kufanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu, Hema la Kukutania na madhabahu, atamleta mbele yule mbuzi aliye hai. 21 Aroni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha mbuzi aliye hai na kuungama juu yake uovu wote na uasi wa Waisraeli, yaani dhambi zao zote, ili kuziweka juu ya kichwa cha huyo mbuzi. Atamwachia huyo mbuzi akimbilie jangwani kwa uangalizi wa mtu aliyepewa wajibu huo. 22 Yule mbuzi atachukua juu yake dhambi zao zote mpaka mahali pasipo na watu; naye yule mtu atamwachia akimbilie jangwani.

  15. 11 Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha hiyo, ili kwamba asiwepo yeyote atakayeanguka kwa kufuata mfano wao wa kutokutii.

    12 Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu. Lina makali kuliko upanga wowote wenye makali kuwili, hivyo linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. 13 Wala hakuna kiumbe chochote kilichofichika machoni pa Mungu. Kila kitu kimefunuliwa na kiko wazi machoni pake yeye ambaye kwake ni lazima tutatoa hesabu.

    14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi.

  16. 5 Bwana akamwambia Mose, 6 “Waambie Waisraeli, ‘Wakati mwanaume au mwanamke akimkosea mwenzake kwa njia yoyote, na kwa hivyo akawa si mwaminifu kwa Bwana, mtu huyo ana hatia, 7 na ni lazima atubu dhambi aliyoifanya. Ni lazima atoe malipo kamili kwa ajili ya kosa lake, aongeze sehemu ya tano juu ya malipo hayo na kutoa yote kwa mtu aliyemkosea.

  17. 17 “Lakini alipozingatia moyoni mwake, akasema, ‘Ni watumishi wangapi walioajiriwa na baba yangu ambao wana chakula cha kuwatosha na kusaza, bali mimi hapa nakufa kwa njaa! 18 Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimetenda dhambi mbele za Mungu na mbele yako. 19 Sistahili tena kuitwa mwanao; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.’ 20 Basi akaondoka, akaenda kwa baba yake.

    “Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu.

    21 “Yule mwana akamwambia baba yake, ‘Baba, nimekosa mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwanao tena.’

  18. 22 Kwa hiyo tubu kwa uovu huu wako na umwombe Bwana. Yamkini aweza kukusamehe mawazo uliyo nayo moyoni mwako. 23 Kwa maana ninaona kwamba wewe umejawa na uchungu na ni mfungwa wa dhambi.”

    24 Ndipo Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Bwana, ili hayo mliyosema lolote yasinitukie.”

  19. 9 lakini sasa nina furaha, si kwa sababu mlihuzunika, bali kwa kuwa huzuni hiyo iliwafanya mtubu. Kwa maana mlihuzunishwa kama Mungu alivyokusudia watu wahuzunike na hivyo sisi hatukuwadhuru kwa njia yoyote.

    10 Kwa maana huzuni ya kimungu huleta toba iletayo wokovu na wala haina majuto. Lakini huzuni ya kidunia husababisha mauti. 11 Tazameni jinsi huzuni hii ya kimungu ilivyoleta faida ndani yenu: bidii mliyo nayo, juhudi mliyofanya kujitetea, uchungu wenu, hofu yenu, upendo wenu, shauku yenu na jinsi mlivyokuwa tayari kutoa adhabu inayostahili. Kwa kila njia mmejithibitisha kuwa safi katika jambo hilo.

  20. 24 Ndipo Sauli akamwambia Samweli, “Nimetenda dhambi. Nimevunja amri ya Bwana na maagizo yako. Niliwaogopa watu na kwa hiyo nikafanya walivyotaka.

  21. 13 Ndipo Daudi akamjibu Nathani, “Nimefanya dhambi dhidi ya Bwana.”

    Nathani akamjibu, “Bwana amekuondolea dhambi yako. Hutakufa.

  22. 1 Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi ule ule, Waisraeli walikusanyika pamoja, wakifunga na kuvaa nguo za gunia na kujitia mavumbi vichwani mwao. 2 Wale wa uzao wa Israeli walijitenga na wageni wote. Wakasimama mahali pao, na kuungama dhambi zao na uovu wa baba zao. 3 Wakasimama pale walipokuwa, wakasoma kutoka kwenye kile Kitabu cha Sheria ya Bwana Mungu wao kwa muda wa robo siku, na wakatumia robo nyingine kwa kuungama dhambi na kumwabudu Bwana Mungu wao.

  23. 19 Tubuni basi mkamgeukie Mungu, dhambi zenu zifutwe, ili zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwepo kwake Bwana, 20 naye apate kumtuma Kristo, ambaye ameteuliwa kwa ajili yenu, yaani Yesu.

  24. 24 “Wakati watu wako Israeli watakapokuwa wameshindwa na adui kwa sababu ya dhambi walizofanya dhidi yako, watakapokugeukia na kulikiri jina lako, wakiomba na kufanya dua kwako katika Hekalu hili, 25 basi usikie kutoka mbinguni, ukasamehe dhambi ya watu wako Israeli na kuwarudisha katika nchi uliyowapa baba zao.

    26 “Wakati mbingu zitakapokuwa zimefungwa kusiwe na mvua kwa sababu watu wako wametenda dhambi dhidi yako, watakapoomba kuelekea mahali hapa na kulikiri jina lako nao wakageuka kutoka dhambi zao kwa sababu umewaadhibu, 27 basi usikie kutoka mbinguni na usamehe dhambi ya watumishi wako, watu wako Israeli. Wafundishe njia sahihi ya kuishi na ukanyeshe mvua juu ya nchi uliyowapa watu wako kuwa urithi.

  25. 15 “Kama ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonyeshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Kama akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako.

  26. 1 Watoto wangu wapendwa, nawaandikia haya ili msitende dhambi. Lakini kama mtu yeyote akitenda dhambi, tunaye Mwombezi kwa Baba: ndiye Yesu Kristo, Mwenye Haki. 2 Yeye ndiye dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu, wala si kwa ajili ya dhambi zetu tu, bali pia kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote.

  27. 19 Ndipo Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, mtukuze Bwana, Mungu wa Israeli, nawe ukiri kwake. Niambie ni nini ulichotenda; usinifiche.”

  28. 1 Wakati Ezra alipokuwa anaomba na kuungama, huku akilia na kujitupa chini mbele ya nyumba ya Mungu, umati mkubwa wa Waisraeli, wanaume, wanawake na watoto walikusanyika kumzunguka. Nao pia wakalia sana.

  29. 12 Ni nani awezaye kutambua makosa yake?

    Nisamehe makosa yangu nisiyoyajua.

  30. 23 “Kwa hiyo, kama unatoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako ana kitu dhidi yako, 24 iache sadaka yako hapo mbele ya madhabahu. Enda kwanza ukapatane na ndugu yako; kisha urudi na ukatoe sadaka yako.

  31. 12 Utusamehe deni zetu,

    kama sisi nasi tulivyokwisha

    kuwasamehe wadeni wetu.

  32. 19 Nitakupa funguo za Ufalme wa mbinguni, na lolote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa Mbinguni, nalo lolote utakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.”

  33. 8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, lile neno la imani tunalolihubiri. 9 Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. 10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu. 11 Kama yasemavyo Maandiko, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.” 12 Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. 13 Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.”

  34. 1 Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejesheni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa. 2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo.