67 Bible Verses About Forgiveness of Sins
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
9 “Hivi basi, ndivyo iwapasavyo kuomba:
“ ‘Baba yetu uliye mbinguni,
Jina lako litukuzwe.
10 Ufalme wako uje.
Mapenzi yako yafanyike
hapa duniani kama huko mbinguni.
11 Utupatie riziki yetu
ya kila siku.
12 Utusamehe deni zetu,
kama sisi nasi tulivyokwisha
kuwasamehe wadeni wetu.
13 Usitutie majaribuni,
bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu
[kwa kuwa Ufalme ni wako, na nguvu,
na utukufu, hata milele. Amen].’
14 Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. 15 Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.
-
5 Huu ndio ujumbe tuliosikia kutoka kwake na kuwatangazia ninyi: kwamba Mungu ni nuru na ndani yake hamna giza lolote. 6 Kama tukisema kwamba twashirikiana naye huku tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatutendi lililo kweli. 7 Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo nuruni, twashirikiana sisi kwa sisi na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.
8 Kama tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu. 9 Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutoka kwenye udhalimu wote. 10 Kama tukisema hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo na neno lake halimo ndani yetu.
-
37 Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”
38 Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. 39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu, na kwa wote walio mbali, na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”
-
25 Nanyi kila msimamapo kusali, sameheni mkiwa na neno na mtu, ili naye Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu. [ 26 Lakini kama ninyi msiposamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]”
-
7 Ndani yake tunao ukombozi kwa njia ya damu yake, yaani, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake 8 aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote. 9 Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Kristo, 10 ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani, kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Kristo.
-
12 Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi.
-
Zaburi ya Daudi. Funzo.
1 Heri mtu yule ambaye amesamehewa makosa yake,
ambaye dhambi zake zimefunikwa.
2 Heri mtu yule ambaye Bwana
hamhesabii dhambi,
na ambaye rohoni mwake
hamna udanganyifu.
3 Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa
kwa kulia kwa maumivu makali mchana kutwa.
4 Usiku na mchana
mkono wako ulinilemea,
nguvu zangu zilinyonywa
kama vile katika joto la kiangazi.
5 Kisha nilikujulisha dhambi yangu
wala sikuficha uovu wangu.
Nilisema, “Nitaungama
makosa yangu kwa Bwana.”
Ndipo uliponisamehe
hatia ya dhambi yangu.
-
3 Kwa hiyo, jilindeni.
“Kama ndugu yako akikukosea mwonye, naye akitubu, msamehe. 4 Kama akikukosea mara saba kwa siku moja na mara saba kwa siku moja akaja kwako akisema, ‘Ninatubu,’ msamehe.”
5 Mitume wake wakamwambia Bwana, “Tuongezee imani.”
-
33 Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walipomsulubisha Yesu pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wake wa kushoto. 34 Yesu akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura.
-
37 “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msilaumu, nanyi hamtalaumiwa. Sameheni, nanyi mtasamehewa.
-
8 Bwana ni mwingi wa huruma na mwenye neema;
si mwepesi wa hasira, bali amejaa upendo.
9 Yeye hatalaumu siku zote,
wala haweki hasira yake milele,
10 yeye hatutendei kulingana na dhambi zetu
wala hatupatilizi kwa kadiri ya maovu yetu.
11 Kama vile mbingu zilivyo juu ya dunia sana,
ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha;
12 kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
ndivyo Mungu alivyoziweka dhambi zetu mbali nasi.
13 Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake,
ndivyo Bwana anavyowahurumia wale wanaomcha;
14 kwa kuwa anajua tulivyoumbwa,
anakumbuka kwamba sisi tu mavumbi.
-
21 Lakini sasa, haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Sheria na Manabii wanaishuhudia. 22 Haki hii itokayo kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote wamwaminio. Kwa maana hapo hakuna tofauti, 23 kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, 24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu. 25 Yeye ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonyesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa. 26 Alifanya hivyo ili kuonyesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.
-
16 jiosheni na mkajitakase.
Yaondoeni matendo yenu maovu
mbele zangu!
Acheni kutenda mabaya,
17 jifunzeni kutenda mema!
Tafuteni haki,
watieni moyo walioonewa.
Teteeni shauri la yatima,
wateteeni wajane.
18 “Njooni basi tuhojiane,”
asema Bwana.
“Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu,
zitakuwa nyeupe kama theluji;
ingawa ni nyekundu sana kama damu,
zitakuwa nyeupe kama sufu.
19 Kama mkikubali na kutii,
mtakula mema ya nchi,
20 lakini kama mkikataa na kuasi,
mtaangamizwa kwa upanga.”
Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena.
-
18 Ni nani Mungu kama wewe,
ambaye anaachilia dhambi
na kusamehe makosa
ya mabaki ya urithi wake?
Wewe huwi na hasira milele,
bali unafurahia kuonyesha rehema.
19 Utatuhurumia tena,
utazikanyaga dhambi zetu
chini ya nyayo zako,
na kutupa maovu yetu yote
katika vilindi vya bahari.
20 Utakuwa wa kweli kwa Yakobo,
nawe utamwonyesha Abrahamu rehema,
kama ulivyowaahidi kwa kiapo baba zetu
siku za kale.
-
21 Ndipo Petro akamjia Yesu na kumuuliza, “Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Je, hata mara saba?”
22 Yesu akamjibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.
23 “Kwa hiyo Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme aliyetaka kufanya hesabu zake za fedha na watumishi wake. 24 Alipoanza kufanya hesabu zake, mtu mmoja aliyekuwa anadaiwa talanta 10,000, aliletwa kwake. 25 Kwa kuwa alikuwa hawezi kulipa deni hilo, bwana wake akaamuru kwamba auzwe, yeye, mkewe, watoto wake na vyote alivyokuwa navyo, ili lile deni lipate kulipwa.
26 “Yule mtumishi akampigia magoti, akamsihi yule bwana akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’ 27 Yule bwana wa huyo mtumishi akamwonea huruma, akafuta deni lake lote, akamwacha aende zake.
28 “Lakini yule mtumishi alipokuwa anatoka nje, akakutana na mtumishi mwenzake aliyekuwa amemkopesha dinari mia moja. Akamkamata, akamkaba koo akimwambia, ‘Nilipe kile ninachokudai!’
29 “Yule mtumishi mwenzake akapiga magoti akamsihi akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’
30 “Lakini akakataa. Badala yake, alienda akamtupa gerezani hata atakapolipa hilo deni. 31 Watumishi wenzake walipoona haya yaliyotukia wakaudhika sana, nao wakaenda na kumwambia bwana wao kila kitu kilichokuwa kimetukia.
32 “Yule bwana akamwita yule mtumishi akamwambia, ‘Wewe mtumishi mwovu! Mimi nilikusamehe deni lako lote uliponisihi. 33 Je, haikukupasa kumhurumia mtumishi mwenzako kama mimi nilivyokuhurumia wewe?’ 34 Kwa hasira, yule bwana wake akamtia yule mtumishi mikononi mwa askari wa gereza ili ateswe mpaka atakapolipa yote aliyokuwa anadaiwa.
35 “Hivi ndivyo Baba yangu wa mbinguni atakavyomfanyia kila mmoja wenu ikiwa hatamsamehe ndugu yake kutoka moyoni mwake.”
-
25 “Mimi, naam mimi, ndimi nizifutaye dhambi zako,
kwa ajili yangu mwenyewe,
wala sizikumbuki dhambi zako tena.
26 Tafakari mambo yaliyopita,
njoo na tuhojiane,
leta shauri lako uweze kupewa haki yako.
-
6 Mtafuteni Bwana maadamu anapatikana;
mwiteni maadamu yu karibu.
7 Mtu mwovu na aiache njia yake,
na mtu mbaya na ayaache mawazo yake.
Yeye na amrudie Bwana, naye atamrehemu,
arudi kwa Mungu wetu, kwa kuwa atamsamehe bure kabisa.
8 “Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu,
wala njia zenu si njia zangu,”
asema Bwana.
9 “Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia,
ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu
na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.
-
13 Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa,
bali yeyote aziungamaye na kuziacha hupata rehema.
-
13 Je, mtu yeyote miongoni mwenu amepatwa na taabu? Basi inampasa aombe. Je, kuna yeyote mwenye furaha? Basi na aimbe nyimbo za kusifu. 14 Je, kuna yeyote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Basi inampasa awaite wazee wa kanisa wamwombee na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana. 15 Kule kuomba kwa imani kutamwokoa huyo mgonjwa, naye Bwana atamwinua na kama ametenda dhambi, atasamehewa. 16 Kwa hiyo ungamianeni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu tena yanafaa sana.
17 Eliya alikuwa mwanadamu kama sisi. Akaomba kwa bidii kwamba mvua isinyeshe, nayo haikunyesha juu ya nchi kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita.
-
19 Tubuni basi mkamgeukie Mungu, dhambi zenu zifutwe, ili zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwepo kwake Bwana, 20 naye apate kumtuma Kristo, ambaye ameteuliwa kwa ajili yenu, yaani Yesu.
-
38 “Kwa hiyo ndugu zangu, nataka ninyi mjue kwamba kwa kupitia huyu Yesu msamaha wa dhambi unatangazwa kwenu. 39 Kwa kupitia yeye, kila mtu amwaminiye anahesabiwa haki kwa kila kitu ambacho asingeweza kuhesabiwa haki kwa sheria ya Mose.
-
10 Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli
baada ya siku zile, asema Bwana.
Nitaziweka sheria zangu katika nia zao
na kuziandika mioyoni mwao.
Nitakuwa Mungu wao,
nao watakuwa watu wangu.
11 Mtu hatamfundisha tena jirani yake,
wala mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘Mjue Bwana,’
kwa sababu wote watanijua mimi,
tangu aliye mdogo kabisa kwao, hadi aliye mkuu sana.
12 Kwa sababu nitasamehe uovu wao,
wala sitazikumbuka dhambi zao tena!”
-
3 Kama wewe, Ee Bwana, ungeweka kumbukumbu ya dhambi,
Ee Bwana, ni nani angeliweza kusimama?
4 Lakini kwako kuna msamaha,
kwa hiyo wewe unaogopwa.
-
9 Yeye anayesamehe kosa hudumisha upendo,
bali yeyote arudiaye jambo hutenganisha marafiki wa karibu.
-
2 Akawaambia, “Mnapoomba, semeni:
“ ‘Baba yetu (uliye mbinguni),
jina lako litukuzwe,
ufalme wako uje.
(Mapenzi yako yafanyike
hapa duniani kama huko mbinguni.)
3 Utupatie kila siku riziki yetu.
4 Utusamehe dhambi zetu,
kwa kuwa na sisi huwasamehe wote wanaotukosea.
Wala usitutie majaribuni
(bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu).’ ”
-
1 Watoto wangu wapendwa, nawaandikia haya ili msitende dhambi. Lakini kama mtu yeyote akitenda dhambi, tunaye Mwombezi kwa Baba: ndiye Yesu Kristo, Mwenye Haki. 2 Yeye ndiye dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu, wala si kwa ajili ya dhambi zetu tu, bali pia kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote.
-
27 Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, “Nyweni nyote katika kikombe hiki. 28 Hii ndiyo damu yangu ya Agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.
-
16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.
-
30 Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu. 31 Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.”
-
16 “Hili ndilo Agano nitakalofanya nao
baada ya siku hizo, asema Bwana.
Nitaziweka sheria zangu mioyoni mwao,
na kuziandika katika nia zao.”
17 Kisha aongeza kusema:
“Dhambi zao na kutokutii kwao
sitakumbuka tena.”
18 Basi haya yakiisha kusamehewa, hakuna tena dhabihu yoyote inayotolewa kwa ajili ya dhambi.
-
14 kama watu wangu, wanaoitwa kwa Jina langu, watajinyenyekesha na kuomba na kuutafuta uso wangu na kuacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi yao na nitaiponya nchi yao.
-
9 Bwana Mungu wetu ni mwenye rehema na anayesamehe, hata ingawa tumefanya uasi dhidi yake.
-
43 Manabii wote walishuhudia juu yake kwamba kila mtu amwaminiye hupokea msamaha wa dhambi katika Jina lake.”
-
17 “Basi sasa nguvu za Bwana na zionekane, sawasawa na vile ulivyosema: 18 ‘Bwana si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo na mwenye kusamehe dhambi na uasi. Lakini haachi kumwadhibu mwenye hatia, huadhibu watoto kwa ajili ya dhambi ya baba zao hata kizazi cha tatu na cha nne.’ 19 Kwa kadiri ya upendo wako mkuu, usamehe dhambi ya watu hawa, kama vile ulivyowasamehe tangu wakati walitoka Misri mpaka sasa.”
20 Bwana akajibu, “Nimewasamehe kama ulivyoomba. 21 Hata hivyo, kwa hakika kama niishivyo, na kwa hakika kama utukufu wa Bwana uijazavyo dunia yote, 22 hakuna hata mmoja wa watu hawa ambao waliuona utukufu wangu na ishara za miujiza niliyotenda huko Misri na huko jangwani, lakini ambaye hakunitii na akanijaribu mara hizi kumi, 23 hakuna hata mmoja wao atakayeona nchi niliyowaahidi baba zao kwa kiapo. Hakuna hata mmoja ambaye amenidharau atakayeiona.
-
5 Kisha Bwana akashuka katika wingu akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina lake, Bwana. 6 Bwana akapita mbele ya Mose, akitangaza, “Bwana, Bwana, Mungu mwenye huruma na neema, asiye mwepesi wa hasira, mwingi wa upendo na uaminifu, 7 akidumisha upendo kwa maelfu, pia akisamehe uovu, uasi na dhambi. Lakini haachi kuadhibu mwenye hatia; huwaadhibu watoto na watoto wao kwa ajili ya dhambi ya baba zao hata katika kizazi cha tatu na cha nne.”
8 Mara Mose akasujudu na kuabudu. 9 Mose akasema, “Ee Bwana, kama nimepata kibali mbele zako, basi Bwana uende pamoja nasi. Ingawa watu hawa ni wenye shingo ngumu, samehe uovu wetu na dhambi yetu, tuchukue kuwa urithi wako.”
-
5 Ee Bwana, wewe ni mwema na mwenye kusamehe,
umejaa upendo kwa wote wakuitao.
-
4 Yohana alikuja, akibatiza huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi. 5 Watu kutoka Uyahudi wote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea. Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.
-
59 Walipokuwa wakimpiga mawe, Stefano aliomba, “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” 60 Kisha akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii.” Baada ya kusema hayo, akalala.
-
20 Yesu alipoiona imani yao, akamwambia yule mgonjwa, “Rafiki, dhambi zako zimesamehewa.”
21 Mafarisayo na wale walimu wa sheria wakaanza kuuliza, “Ni nani mtu huyu anayesema maneno ya kukufuru? Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”
-
11 Katika Kristo pia mlitahiriwa kwa kutengwa mbali na asili ya dhambi, si kwa tohara inayofanywa kwa mikono ya wanadamu, bali kwa ile tohara iliyofanywa na Kristo, 12 mkiwa mmezikwa pamoja naye katika ubatizo, na kufufuliwa pamoja naye kwa njia ya imani yenu katika uweza wa Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu.
13 Mlipokuwa wafu katika dhambi zenu na kutokutahiriwa katika asili yenu ya dhambi, Mungu aliwafanya mwe hai pamoja na Kristo. Alitusamehe dhambi zetu zote, 14 akiisha kuifuta ile hati yenye mashtaka yaliyokuwa yanatukabili, pamoja na maagizo yake. Aliiondoa isiwepo tena, akiigongomea kwenye msalaba wake. 15 Mungu akiisha kuzivua enzi na mamlaka, alizifanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuziburura kwa ujasiri, akizishinda katika msalaba wa Kristo.
-
10 “Mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli uwaambie, ‘Hili ndilo mnalosema: “Makosa yetu na dhambi zetu zimetulemea, nasi tunadhoofika kwa sababu ya hayo. Tutawezaje basi kuishi?” ’ 11 Waambie, ‘Hakika kama mimi niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, sifurahii kifo cha watu waovu, bali kwamba wageuke kutoka njia zao mbaya wapate kuishi. Geukeni! Geukeni kutoka njia zenu mbaya! Kwa nini mkafe, ee nyumba ya Israeli?’
12 “Kwa hiyo, mwanadamu, waambie watu wako, ‘Haki ya mtu mwenye haki haitamwokoa wakati anapoacha kutii, wala uovu wa mtu mwovu hautamsababisha yeye kuanguka anapotubu na kuacha uovu. Mtu mwenye haki, kama akitenda dhambi, hataishi kwa sababu ya uadilifu wake wa awali.’ 13 Kama nikimwambia mtu mwenye haki kwamba hakika utaishi, lakini akategemea hiyo haki yake na kutenda uovu, hakuna tendo lolote la haki alilotenda litakalokumbukwa, atakufa kwa ajili ya uovu alioutenda. 14 Nami kama nikimwambia mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ kisha akageuka kutoka dhambi yake na kufanya lile lililo haki na sawa, 15 kama akirudisha kile alichochukua rehani kwa ajili ya deni, akarudisha alichoiba na kufuata amri zile ziletazo uzima, wala hafanyi uovu, hakika ataishi, hatakufa. 16 Hakuna dhambi yoyote aliyoitenda itakayokumbukwa juu yake. Ametenda lile lililo haki na sawa, hakika ataishi.
-
17 “Lakini alipozingatia moyoni mwake, akasema, ‘Ni watumishi wangapi walioajiriwa na baba yangu ambao wana chakula cha kuwatosha na kusaza, bali mimi hapa nakufa kwa njaa! 18 Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimetenda dhambi mbele za Mungu na mbele yako. 19 Sistahili tena kuitwa mwanao; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.’ 20 Basi akaondoka, akaenda kwa baba yake.
“Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu.
21 “Yule mwana akamwambia baba yake, ‘Baba, nimekosa mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwanao tena.’
22 “Lakini baba yake akawaambia watumishi, ‘Leteni upesi joho lililo bora sana, tieni pete kidoleni mwake na viatu miguuni mwake. 23 Leteni ndama aliyenona, mkamchinje ili tuwe na karamu, tule na kufurahi. 24 Kwa maana huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yu hai tena; alikuwa amepotea na sasa amepatikana!’ Nao wakaanza kufanya tafrija.
-
46 Akawaambia, “Haya ndiyo yaliyoandikwa: Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu. 47 Toba na msamaha wa dhambi zitatangaziwa mataifa yote kupitia jina lake kuanzia Yerusalemu. 48 Ninyi ni mashahidi wa mambo haya.
49 “Tazama nitawatumia ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini hadi mtakapovikwa uwezo utokao juu.”
-
15 “Nikauliza, ‘Ni nani wewe, Bwana?’
“Naye Bwana akajibu, ‘Ni Mimi Yesu unayemtesa. 16 Sasa inuka usimame kwa miguu yako. Nimekutokea ili nikuteue uwe mtumishi na shahidi wa mambo ambayo umeyaona, na yale nitakayokuonyesha. 17 Nitakuokoa kutoka kwa watu wako na watu wa Mataifa ambao ninakutuma kwao, 18 uyafumbue macho yao ili wageuke kutoka gizani waingie nuruni, na kutoka kwenye nguvu za Shetani wamgeukie Mungu, ili wapate msamaha wa dhambi na sehemu miongoni mwa wale waliotakaswa kwa kuniamini mimi.’
-
23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.
-
22 Kwa kweli sheria hudai kwamba, karibu kila kitu kitakaswe kwa damu, wala pasipo kumwaga damu, hakuna msamaha wa dhambi.
-
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Baada ya kukemewa na nabii Nathani kwa kuzini na Bathsheba.
1 Ee Mungu, unihurumie,
kwa kadiri ya upendo wako usiokoma,
kwa kadiri ya huruma yako kuu,
uyafute makosa yangu.
2 Unioshe na uovu wangu wote
na unitakase dhambi yangu.
3 Kwa maana ninajua makosa yangu,
na dhambi yangu iko mbele yangu daima.
4 Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi
na kufanya yaliyo mabaya machoni pako,
ili uthibitike kuwa wa kweli unenapo,
na kuwa na haki utoapo hukumu.
5 Hakika mimi nilizaliwa mwenye dhambi,
mwenye dhambi tangu nilipotungwa mimba kwa mama yangu.
-
1 Katika mwaka ule Mfalme Uzia alikufa, nilimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu na kilichotukuzwa sana, nalo pindo la joho lake likajaza Hekalu. 2 Juu yake walikuwepo maserafi, kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Kwa mabawa mawili walifunika nyuso zao, kwa mengine mawili walifunika miguu yao, na kwa mawili walikuwa wakiruka. 3 Nao walikuwa wakiitana kila mmoja na mwenzake:
“Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu
ni Bwana Mwenye Nguvu Zote;
dunia yote imejaa utukufu wake.”
4 Kwa sauti zao, miimo ya milango na vizingiti vilitikisika, nalo Hekalu likajaa moshi.
5 Ndipo nikalia, “Ole wangu! Nimeangamia! Kwa kuwa mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninaishi katikati ya watu wenye midomo michafu, nayo macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana Mwenye Nguvu Zote.”
6 Ndipo mmoja wa wale maserafi akaruka kunijia akiwa na kaa la moto linalowaka mkononi mwake, ambalo alikuwa amelichukua kwa koleo kutoka madhabahuni. 7 Akanigusa nalo kinywa changu na kusema, “Tazama, hili limegusa midomo yako, uovu wako umeondolewa, nayo dhambi yako imesamehewa.”
-
7 Heri wenye huruma,
maana hao watapata rehema.
-
21 “Mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiue. Yeyote atakayeua atapaswa hukumu.’ 22 Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote atakayemkasirikia ndugu yake, atapaswa hukumu. Tena, yeyote atakayemwambia ndugu yake, ‘Raka,’ atapaswa kujibu kwa Baraza la Wayahudi. Lakini yeyote atakayesema ‘Wewe mpumbavu!’ atapaswa hukumu ya moto wa jehanamu.
23 “Kwa hiyo, kama unatoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako ana kitu dhidi yako, 24 iache sadaka yako hapo mbele ya madhabahu. Enda kwanza ukapatane na ndugu yako; kisha urudi na ukatoe sadaka yako.
-
2 Wakati huo huo wakamletea mtu aliyepooza, akiwa amelazwa kwenye mkeka. Yesu alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, jipe moyo mkuu. Dhambi zako zimesamehewa.”
3 Kwa ajili ya jambo hili, baadhi ya walimu wa sheria wakasema mioyoni mwao, “Huyu mtu anakufuru!”
4 Lakini Yesu akiyafahamu mawazo yao, akawaambia, “Kwa nini mnawaza maovu mioyoni mwenu? 5 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’? 6 Lakini, ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Ndipo akamwambia yule aliyepooza, “Inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.”
-
12 “Mwaonaje? Ikiwa mtu ana kondoo mia moja, na mmoja wao akapotea, je, hatawaacha wale tisini na tisa vilimani na kwenda kumtafuta huyo mmoja aliyepotea? 13 Naye akishampata, amin, nawaambia, hufurahi zaidi kwa ajili ya huyo kondoo mmoja kuliko wale tisini na tisa ambao hawakupotea. 14 Vivyo hivyo, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmojawapo wa hawa wadogo apotee.
15 “Kama ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonyeshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Kama akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako. 16 Lakini kama hatakusikiliza, nenda na mtu mwingine mmoja au wawili ili kila neno lithibitishwe kwa ushahidi wa mashahidi wawili au watatu. 17 Kama akikataa kuwasikiliza hao, liambie kanisa. Naye kama akikataa hata kulisikiliza kanisa, basi awe kwenu kama mtu asiyeamini au mtoza ushuru.
18 “Amin, nawaambia, lolote mtakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote mtakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.
-
47 Kwa hiyo, nakuambia, dhambi zake zilizokuwa nyingi zimesamehewa, kwani ameonyesha upendo mwingi. Lakini yule aliyesamehewa kidogo, hupenda kidogo.”
48 Kisha akamwambia yule mwanamke, “Dhambi zako zimesamehewa.”
-
29 Siku iliyofuata, Yohana alimwona Yesu akimjia akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu!
-
1 Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu, wale ambao hawaenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho. 2 Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima katika Kristo Yesu imeniweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti. 3 Kwa maana kile ambacho sheria haikuwa na uwezo wa kufanya, kwa vile ilivyokuwa dhaifu katika mwili, Mungu kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe kwa mfano wa mwanadamu mwenye mwili ulio wa dhambi na kwa ajili ya dhambi, yeye aliihukumu dhambi katika mwili, 4 ili kwamba haki ipatikanayo kwa sheria itimizwe ndani yetu sisi, ambao hatuenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho.
-
8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, lile neno la imani tunalolihubiri. 9 Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. 10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu.
-
9 Je, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wahanithi, wala walawiti, 10 wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyangʼanyi hawataurithi Ufalme wa Mungu. 11 Baadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Yesu Kristo na katika Roho wa Mungu wetu.
-
16 Sasa basi, mbona unakawia? Inuka, ukabatizwe na dhambi zako zikasafishwe, ukiliita Jina lake.’
-
8 Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi.
-
12 Nawaandikia ninyi, watoto wadogo,
kwa sababu dhambi zenu
zimesamehewa kwa ajili ya Jina lake.
-
13 Ndipo Daudi akamjibu Nathani, “Nimefanya dhambi dhidi ya Bwana.”
Nathani akamjibu, “Bwana amekuondolea dhambi yako. Hutakufa.
-
12 Nenda, ukatangaze ujumbe huu kuelekea kaskazini:
“ ‘Rudi, Israeli usiye mwaminifu,’ asema Bwana,
‘sitakutazama tena kwa uso uliokunjamana,
kwa kuwa mimi ni mwenye huruma,’ asema Bwana,
‘Sitashika hasira yangu milele.
-
21 Yesu akawaambia tena, “Amani iwe nanyi! Kama vile Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawatuma ninyi.” 22 Naye alipokwisha kusema haya, akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. 23 Mkimwondolea mtu yeyote dhambi zake, zitaondolewa, na yeyote msiyemwondolea dhambi zake, hazitaondolewa.”
-
18 Wengi wa wale waliokuwa wameamini wakati huu wakaja na kutubu waziwazi kuhusu matendo yao maovu.
-
6 Adhabu hii aliyopewa na wengi inamtosha. 7 Basi sasa badala yake, inawapasa kumsamehe na kumfariji, ili asigubikwe na huzuni kupita kiasi. 8 Kwa hiyo, nawasihi, mpate kuuthibitisha tena upendo wenu kwa ajili yake. 9 Sababu ya kuwaandikia ni kuona kama mngeweza kushinda hilo jaribio na kutii katika kila jambo. 10 Kama ninyi mkimsamehe mtu yeyote, mimi pia nimemsamehe. Kile nilichosamehe, kama kulikuwa na kitu chochote cha kusamehe, nimekwisha kusamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu, 11 ili Shetani asitushinde. Kwa maana hatuachi kuzijua hila zake.
-
10 Kwa maana huzuni ya kimungu huleta toba iletayo wokovu na wala haina majuto. Lakini huzuni ya kidunia husababisha mauti.
-
29 Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao. 30 Wala msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwake mlitiwa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi. 31 Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu. 32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.
Shows Read in context, Share and Copy.