28 Bible Verses About Christmas
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
4 Hivyo Yosefu akapanda kutoka mji wa Nazareti ulioko Galilaya kwenda Uyahudi, mpaka Bethlehemu, mji wa Daudi, kwa sababu yeye alikuwa wa ukoo na wa nyumba ya Daudi. 5 Alikwenda huko kujiandikisha pamoja na Maria, ambaye alikuwa amemposa naye alikuwa mjamzito. 6 Wakiwa Bethlehemu, wakati wa Maria wa kujifungua ukawa umetimia, 7 naye akamzaa mwanawe, kifungua mimba. Akamfunika nguo za kitoto na kumlaza katika hori ya kulia ngʼombe, kwa sababu hapakuwa na nafasi katika nyumba ya wageni.
8 Katika eneo lile walikuwako wachungaji waliokuwa wakikaa mashambani, wakilinda makundi yao ya kondoo usiku. 9 Ghafula tazama, malaika wa Bwana akawatokea, nao utukufu wa Bwana ukawangʼaria kotekote, wakaingiwa na hofu. 10 Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama nawaletea habari njema za furaha itakayokuwa kwa watu wote. 11 Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. 12 Hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori ya kulia ngʼombe.”
13 Ghafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema,
14 “Atukuzwe Mungu juu mbinguni,
na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”
15 Hao malaika walipokwisha kuondoka na kwenda zao mbinguni, wale wachungaji wakasemezana wao kwa wao, “Twendeni Bethlehemu tukaone mambo haya ya ajabu yaliyotukia, ambayo Bwana ametuambia habari zake.”
16 Hivyo wakaenda haraka Bethlehemu, wakawakuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga akiwa amelala katika hori la kulia ngʼombe. 17 Walipomwona yule mtoto, wakawaeleza yale waliyokuwa wameambiwa kuhusu huyo mtoto. 18 Nao wote waliosikia habari hizi wakastaajabia yale waliyoambiwa na wale wachungaji wa kondoo. 19 Lakini Maria akayaweka mambo haya yote moyoni mwake na kuyatafakari. 20 Wale wachungaji wakarudi, huku wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa ajili ya mambo yote waliyokuwa wameambiwa na kuyaona.
-
18 Basi Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi: Maria mama yake alikuwa ameposwa na Yosefu, lakini kabla hawajakutana kimwili, Maria alionekana kuwa na mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 19 Kwa kuwa Yosefu, mwanaume aliyekuwa amemposa alikuwa mtu mwadilifu, hakutaka kumwaibisha Maria hadharani, aliazimu kumwacha kwa siri.
20 Lakini mara alipoazimu kufanya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto na kusema, “Yosefu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 21 Naye atamzaa mwana, nawe utamwita Jina lake Yesu, kwa maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake kutoka dhambi zao.”
22 Haya yote yalitukia ili litimie lile Bwana alilokuwa amenena kupitia nabii, akisema: 23 “Tazama, bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, nao watamwita Jina lake Imanueli”: maana yake, “Mungu pamoja nasi.”
24 Yosefu alipoamka kutoka usingizini, akafanya kama vile alivyoagizwa na malaika wa Bwana, akamchukua Maria kuwa mke wake. 25 Lakini hawakukutana kimwili mpaka Maria alipojifungua mwanawe kifungua mimba akamwita Jina lake Yesu.
-
14 Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara: Bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, na ataitwa Imanueli. 15 Atakula jibini na asali atakapokuwa ameweza kukataa mabaya na kuchagua mema.
-
6 Kwa maana, kwa ajili yetu mtoto amezaliwa,
tumepewa mtoto mwanaume,
nao utawala utakuwa mabegani mwake.
Naye ataitwa
Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu,
Baba wa Milele, Mfalme wa Amani.
7 Kuongezeka kwa utawala wake na amani
hakutakuwa na mwisho.
Atatawala katika kiti cha enzi cha Daudi
na juu ya ufalme wake,
akiuthibitisha na kuutegemeza
kwa haki na kwa adili,
tangu wakati huo na hata milele.
Wivu wa Bwana Mwenye Nguvu Zote
utatimiza haya.
-
16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa. 18 Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. 19 Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu. 20 Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe. 21 Lakini yule aishiye kwa ukweli huja kwenye nuru, ili ionekane wazi kwamba matendo yake yametendeka katika Mungu.”
-
1 Baada ya Yesu kuzaliwa katika mji wa Bethlehemu huko Uyahudi, wakati wa utawala wa Mfalme Herode, wataalamu wa mambo ya nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu 2 wakiuliza, “Yuko wapi huyo aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota yake ikitokea mashariki, nasi tumekuja kumwabudu.”
3 Mfalme Herode aliposikia jambo hili aliingiwa na hofu sana pamoja na watu wote wa Yerusalemu. 4 Herode akawaita pamoja viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, akawauliza ni mahali gani ambapo Kristo angezaliwa. 5 Nao wakamwambia, “Katika Bethlehemu ya Uyahudi, kwa maana hivyo ndivyo ilivyoandikwa na nabii:
6 “ ‘Nawe, Bethlehemu, katika nchi ya Yuda,
wewe si mdogo miongoni
mwa watawala wa Yuda;
kwa maana kutoka kwako atakuja mtawala
atakayekuwa mchungaji
wa watu wangu Israeli.’ ”
7 Ndipo Herode akawaita wale wataalamu wa nyota kwa siri na kutaka kujua kutoka kwao uhakika kamili wa wakati ile nyota ilionekana. 8 Kisha akawatuma waende Bethlehemu akiwaambia, “Nendeni mkamtafute kwa bidii huyo mtoto. Nanyi mara mtakapomwona, mniletee habari ili na mimi niweze kwenda kumwabudu.”
9 Baada ya kumsikia mfalme, wale wataalamu wa nyota wakaenda zao, nayo ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, nao wakaifuata mpaka iliposimama mahali pale alipokuwa mtoto. 10 Walipoiona ile nyota wakajawa na furaha kubwa mno. 11 Walipoingia ndani ya ile nyumba, wakamwona mtoto pamoja na Maria mama yake, wakamsujudu na kumwabudu yule mtoto Yesu. Ndipo wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane. 12 Nao wakiisha kuonywa katika ndoto wasirudi kwa Herode, wakarudi kwenda katika nchi yao kwa njia nyingine.
-
26 Mwezi wa sita baada ya Elizabeti kupata mimba, Mungu alimtuma malaika Gabrieli aende Galilaya katika mji wa Nazareti, 27 kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu mmoja jina lake Yosefu wa nyumba ya Daudi. Jina la huyu mwanamwali bikira ni Maria. 28 Naye malaika akaja kwake akamwambia: “Salamu, wewe uliyebarikiwa, Bwana yu pamoja nawe!”
29 Maria akafadhaishwa sana na maneno haya, akajiuliza moyoni, “Salamu hii ni ya namna gani?” 30 Ndipo malaika akamwambia, “Usiogope, Maria, umepata kibali kwa Mungu. 31 Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanaume na utamwita jina lake Yesu. 32 Yeye atakuwa mkuu, naye ataitwa Mwana wa Aliye Juu Sana. Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake. 33 Ataimiliki nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”
34 Maria akamuuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?”
35 Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu. 36 Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake, na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa. 37 Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.”
38 Maria akasema, “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana. Na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka, akamwacha.
-
1 Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2 Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu.
3 Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa. 4 Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima na huo uzima ulikuwa nuru ya watu. 5 Nuru hungʼaa gizani nalo giza halikuishinda.
6 Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. 7 Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kwa kupitia kwake watu wote waweze kuamini. 8 Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru. 9 Kwamba nuru halisi, imwangaziayo kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni.
10 Huyo Neno alikuwako ulimwenguni na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua. 11 Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea. 12 Bali wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake. 13 Hawa ndio wasiozaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali kwa mapenzi ya Mungu.
14 Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli.
15 Yohana alishuhudia habari zake, akapaza sauti, akisema, “Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuniliko mimi, kwa kuwa alikuwepo kabla yangu.’ ” 16 Kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema juu ya neema. 17 Kwa kuwa sheria ilitolewa kwa mkono wa Mose, lakini neema na kweli imekuja kupitia Yesu Kristo. 18 Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote, ila ni Mungu Mwana pekee, aliye kifuani mwa Baba ndiye ambaye amemdhihirisha.
-
1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, 2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. 3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.
5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:
6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,
hakuona kule kuwa sawa na Mungu
kuwa kitu cha kushikilia,
7 bali alijifanya si kitu,
akachukua hali hasa na mtumwa,
naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.
8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,
alijinyenyekeza, akatii hata mauti:
naam, mauti ya msalaba!
9 Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana,
na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina,
10 ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe,
la vitu vya mbinguni, na vya duniani,
na vya chini ya nchi,
11 na kila ulimi ukiri ya kwamba
Yesu Kristo ni Bwana,
kwa utukufu wa Mungu Baba.
-
15 Ashukuriwe Mungu kwa karama yake isiyoelezeka.
-
23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.
-
13 Walipokwisha kwenda zao, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto akamwambia, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapowaambia, kwa maana Herode anataka kumtafuta huyu mtoto ili amuue.”
14 Kisha Yosefu akaondoka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake wakati wa usiku, nao wakaenda Misri 15 ambako walikaa mpaka Herode alipofariki. Hili lilifanyika ili litimie lile lililonenwa na Bwana kwa kinywa cha nabii kusema: “Nilimwita mwanangu kutoka Misri.”
16 Herode alipongʼamua kwamba wale wataalamu wa nyota wamemshinda kwa akili, alikasirika sana, naye akatoa amri ya kuwaua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili kurudi chini katika mji wa Bethlehemu na sehemu zote za jirani, kufuatana na ule muda alioambiwa na wale wataalamu wa nyota. 17 Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia.
18 “Sauti ilisikika huko Rama,
maombolezo na kilio kikubwa,
Raheli akilia kwa ajili ya wanawe,
akikataa kufarijiwa,
kwa sababu hawako tena.”
-
1 Chipukizi litatokea kutoka shina la Yese,
kutoka mizizi yake Tawi litazaa tunda.
2 Roho wa Bwana atakaa juu yake,
Roho wa hekima na wa ufahamu,
Roho wa shauri na wa uweza,
Roho wa maarifa na wa kumcha Bwana
-
9 Shangilia sana, ee Binti Sayuni!
Piga kelele, Binti Yerusalemu!
Tazama, Mfalme wako anakuja kwako,
ni mwenye haki, naye ana wokovu,
ni mpole, naye amepanda punda,
mwana-punda, mtoto wa punda.
-
11 Huu ndio ushuhuda: kwamba Mungu ametupa uzima wa milele, nao huo uzima umo katika Mwanawe.
-
22 Moyo wenye furaha ni dawa nzuri,
bali roho iliyopondeka hukausha mifupa.
-
27 Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.
-
5 Bwana asema, “Siku zinakuja,
nitakapomwinulia Daudi Tawi lenye haki,
Mfalme atakayetawala kwa hekima,
na kutenda lililo haki na sawa katika nchi.
-
14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.
15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu.
-
5 Yule mwanamke akazaa mtoto mwanaume, atakayeyatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya utawala ya chuma. Lakini huyo mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu kwenye kiti chake cha enzi.
-
38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”
-
27 Akajibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote’; tena, ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ ”
-
24 Kuna mtu atoaye kwa ukarimu, hata hivyo hupata zaidi,
mwingine huzuia, lakini huwa maskini.
25 Mtu mkarimu atastawi;
yeye awaburudishaye wengine
ataburudishwa mwenyewe.
-
25 “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini au mtakunywa nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? 26 Waangalieni ndege wa angani; wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wa thamani zaidi kuliko hao ndege? 27 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake?
28 “Nanyi kwa nini mnajitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi. 29 Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. 30 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba? 31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia. 34 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.
-
29 Siku iliyofuata, Yohana alimwona Yesu akimjia akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu!
-
29 kwa maana akishawapa watu karama, Mungu haziondoi, wala wito wake.
-
9 Upendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema. 10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine. 11 Msiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana. 12 Kuweni na furaha katika tumaini, katika dhiki kuweni na saburi, dumuni katika maombi. 13 Changieni katika mahitaji ya watakatifu, wakaribisheni wageni.
14 Wabarikini wale wanaowatesa, barikini wala msilaani. 15 Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao. 16 Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge. Wala msiwe watu wenye kujivuna kwamba mnajua kila kitu.
17 Msimlipe mtu yeyote ovu kwa ovu. Jitahidini ili mtende yaliyo mema machoni pa watu wote. 18 Kama ikiwezekana, kwa upande wenu kaeni kwa amani na watu wote. 19 Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Ni juu yangu kulipiza kisasi, nitalipiza,” asema Bwana. 20 Badala yake:
“Kama adui yako ana njaa, mlishe;
kama ana kiu, mpe kinywaji.
Kwa kufanya hivyo,
unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.”
21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.
-
4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini!
Shows Read in context, Share and Copy.