84 Bible Verses About Knowing God

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Knowing God
  1. 1 Baada ya Yesu kusema haya, alitazama kuelekea mbinguni akawaombea na kusema:

    “Baba, saa imewadia. Umtukuze Mwanao, ili Mwanao apate kukutukuza wewe. 2 Kwa kuwa umempa mamlaka juu ya wote wenye mwili ili awape uzima wa milele wale uliompa. 3 Nao uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe uliye Mungu wa pekee, wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma. 4 Nimekutukuza wewe duniani kwa kuitimiza ile kazi uliyonipa niifanye. 5 Hivyo sasa, Baba, unitukuze mbele zako kwa ule utukufu niliokuwa nao pamoja na wewe kabla ulimwengu haujakuwepo.

  2. 7 Wapendwa, tupendane, kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu. Kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. 8 Yeye asiyependa hamjui Mungu, kwa sababu Mungu ni pendo. 9 Hivi ndivyo Mungu alivyoonyesha pendo lake kwetu: Mungu alimtuma Mwanawe wa pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kupitia kwake. 10 Hili ndilo pendo: si kwamba tulimpenda Mungu, bali yeye alitupenda, akamtuma Mwanawe, ili yeye awe dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu. 11 Marafiki wapendwa, kama Mungu alivyotupenda sisi, imetupasa na sisi kupendana. 12 Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote. Lakini tukipendana, Mungu anakaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu.

  3. 1 Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.

  4. 18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao, 19 kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao. 20 Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.

    21 Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza. 22 Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga 23 na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizofanywa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vitambaavyo.

    24 Kwa hiyo, Mungu akawaacha wazifuate tamaa mbaya za mioyo yao katika uasherati, hata wakavunjiana heshima miili yao wao kwa wao. 25 Kwa sababu waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakaabudu na kutumikia kiumbe badala ya Muumba, ahimidiwaye milele! Amen.

  5. 9 Kwa sababu hii, tangu siku ile tuliposikia habari zenu, hatujakoma kuomba kwa ajili yenu na kumsihi Mungu awajaze ninyi maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote ya kiroho na ufahamu. 10 Nasi tunaomba haya ili mpate kuishi maisha yanayostahili mbele za Bwana, na mpate kumpendeza kwa kila namna: mkizaa matunda kwa kila kazi njema, mkikua katika kumjua Mungu, 11 mkiwa mmetiwa nguvu kwa uwezo wote kwa kadiri ya nguvu yake yenye utukufu, ili mpate kuwa na wingi wa saburi na uvumilivu. Nanyi kwa furaha 12 mkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru. 13 Kwa maana ametuokoa kutoka ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa, 14 ambaye katika yeye tunao ukombozi, yaani msamaha wa dhambi.

  6. 33 Tazama jinsi kilivyo kina cha utajiri

    wa hekima na maarifa ya Mungu!

    Tazama jinsi ambavyo hukumu zake hazichunguziki,

    na ambavyo njia zake zisivyotafutikana!

    34 “Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Bwana?

    Au ni nani ambaye amekuwa mshauri wake?”

    35 “Au ni nani aliyempa chochote

    ili arudishiwe?”

    36 Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, viko kwake na kwa ajili yake.

    Utukufu ni wake milele! Amen.

  7. 14 Kwa sababu hii nampigia Baba magoti, 15 ambaye ubaba wote wa kila jamaa za mbinguni na za duniani unatokana naye. 16 Namwomba Mungu awaimarishe kwa kuwatia nguvu mioyo yenu kwa njia ya Roho wake kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, 17 ili kwamba, Kristo apate kukaa mioyoni mwenu kwa njia ya imani. Nami ninaomba kwamba ninyi mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo, 18 mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Kristo, 19 na kujua upendo huu unaopita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu.

    20 Basi kwa yeye awezaye kutenda mambo ya ajabu yasiyopimika kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya uweza wake ule utendao kazi ndani yetu, 21 yeye atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu kwa vizazi vyote, milele na milele. Amen.

  8. 1 Mwanangu, kama utayakubali maneno yangu

    na kuyaweka akiba maagizo yangu ndani mwako,

    2 kutega sikio lako kwenye hekima

    na kuweka moyo wako katika ufahamu,

    3 na kama ukiita busara

    na kuita kwa sauti ufahamu,

    4 na kama utaitafuta kama fedha

    na kuitafuta sana kama hazina iliyofichwa,

    5 ndipo utakapoelewa kumcha Bwana

    na kupata maarifa ya Mungu.

    6 Kwa maana Bwana hutoa hekima,

    na kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.

  9. 8 Zamani, mlipokuwa hammjui Mungu, mlikuwa watumwa wa viumbe ambavyo kwa asili si Mungu. 9 Lakini sasa kwa kuwa mmemjua Mungu, au zaidi mmejulikana na Mungu, inakuwaje mnarejea tena katika zile kanuni za kwanza zenye udhaifu na upungufu? Mnataka ziwafanye tena watumwa?

  10. 25 Wakati huo Yesu alisema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. 26 Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.

    27 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu: Hakuna mtu amjuaye Mwana ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.

    28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

  11. 6 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu.

  12. 17 Basi Mfalme wa milele, asiye na mwisho, asiyeonekana, aliye Mungu pekee, apewe heshima na utukufu milele na milele. Amen.

  13. 31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia. 34 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.

  14. 14 Kama vile Mose alivyomwinua yule nyoka kule jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu. 15 Ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele.

    16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa. 18 Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. 19 Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu.

  15. 1 Nataka mjue jinsi ninavyojitaabisha kwa ajili yenu na kwa ajili ya wale walioko Laodikia, na pia kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona mimi binafsi. 2 Kusudi langu ni watiwe moyo na kuunganishwa katika upendo, ili wapate ule utajiri wa ufahamu mkamilifu, ili waijue siri ya Mungu, yaani, Kristo mwenyewe, 3 ambaye ndani yake kumefichwa hazina zote za hekima na maarifa. 4 Nawaambia mambo haya ili mtu yeyote asiwadanganye kwa maneno ya kuwashawishi. 5 Kwa kuwa ingawa mimi siko pamoja nanyi kimwili, lakini niko pamoja nanyi kiroho, nami nafurahi kuuona utaratibu wenu na jinsi uthabiti wa imani yenu katika Kristo ulivyo.

  16. 43 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’ 44 Lakini ninawaambia: Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi, 45 ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. 46 Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo? 47 Nanyi kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu, hawafanyi hivyo? 48 Kwa hiyo kuweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

  17. 1 Hatimaye, ndugu, tuliwaomba na kuwasihi katika Bwana Yesu kwamba, kama mlivyojifunza kutoka kwetu jinsi iwapasavyo kuishi ili kumpendeza Mungu, kama vile mnavyoishi, imewapasa mzidi sana kufanya hivyo. 2 Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa mamlaka ya Bwana Yesu.

    3 Mapenzi ya Mungu ni kwamba ninyi mtakaswe, ili kwamba mjiepushe na zinaa, 4 ili kwamba kila mmoja wenu ajifunze kuutawala mwili wake mwenyewe katika utakatifu na heshima, 5 si kwa tamaa mbaya kama watu wa Mataifa wasiomjua Mungu. 6 Katika jambo hili mtu asimkosee ndugu yake wala kumlaghai. Kwa kuwa Bwana ni mlipiza kisasi katika mambo haya yote, kama vile tulivyokwisha kuwaambia mapema na kuwaonya vikali. 7 Kwa maana Mungu hakutuitia uchafu, bali utakatifu. 8 Kwa hiyo, mtu yeyote anayekataa mafundisho haya hamkatai mwanadamu, bali anamkataa Mungu anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu.

  18. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

    1 Ee Bwana, umenichunguza

    na kunijua.

    2 Unajua ninapoketi na ninapoinuka;

    unatambua mawazo yangu tokea mbali.

    3 Unafahamu kutoka kwangu na kulala kwangu;

    unaelewa njia zangu zote.

    4 Kabla neno halijafika katika ulimi wangu,

    wewe walijua kikamilifu, Ee Bwana.

    5 Umenizunguka nyuma na mbele;

    umeweka mkono wako juu yangu.

    6 Maarifa haya ni ya ajabu mno kwangu,

    ni ya juu sana kwangu kuyafikia.

    7 Niende wapi nijiepushe na Roho yako?

    Niende wapi niukimbie uso wako?

    8 Kama nikienda juu mbinguni, wewe uko huko;

    nikifanya vilindi kuwa kitanda changu,

    wewe uko huko.

  19. 32 Kwa udanganyifu atapotosha wale walionajisi agano, lakini watu wanaomjua Mungu wao watampinga kwa uthabiti.

  20. 25 “Baba Mwenye Haki, ingawa ulimwengu haukujui, mimi ninakujua, nao wanajua ya kuwa umenituma. 26 Nimefanya jina lako lijulikane kwao nami nitaendelea kufanya lijulikane, ili kwamba upendo ule unaonipenda mimi uwe ndani yao na mimi mwenyewe nipate kuwa ndani yao.”

  21. 23 Hili ndilo asemalo Bwana:

    “Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake,

    au mwenye nguvu ajisifu katika nguvu zake,

    wala tajiri ajisifu katika utajiri wake,

    24 lakini yeye ajisifuye, na ajisifu kwa sababu hili:

    kwamba ananifahamu na kunijua mimi,

    kwamba mimi ndimi Bwana, nitendaye wema,

    hukumu na haki duniani,

    kwa kuwa napendezwa na haya,”

    asema Bwana.

  22. 6 Lakini miongoni mwa watu waliokomaa twanena hekima, wala si hekima ya ulimwengu huu au ya watawala wa dunia hii wanaobatilika. 7 Sisi tunanena hekima ya Mungu ambayo ni siri, tena iliyofichika, ambayo Mungu aliikusudia kabla ya ulimwengu kuwepo, kwa ajili ya utukufu wetu. 8 Hakuna hata mtawala mmoja wa nyakati hizi aliyeelewa jambo hili. Kwa maana kama wangelielewa, wasingemsulubisha Bwana wa utukufu. 9 Lakini ni kama ilivyoandikwa:

    “Hakuna jicho limepata kuona,

    wala sikio limepata kusikia,

    wala hayakuingia moyoni wowote,

    yale Mungu amewaandalia

    wale wampendao”:

    10 Lakini mambo haya Mungu ametufunulia kwa Roho wake.

    Roho huchunguza kila kitu, hata mambo ya ndani sana ya Mungu. 11 Kwa maana ni nani anayejua mawazo ya mtu isipokuwa roho iliyo ndani ya huyo mtu? Vivyo hivyo hakuna mtu ajuaye mawazo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu. 12 Basi hatukupokea roho ya dunia bali Roho atokaye kwa Mungu, ili tuweze kuelewa kile kipawa ambacho Mungu ametupatia bure. 13 Haya ndiyo tusemayo, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya wanadamu bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua kweli za kiroho kwa maneno ya kiroho. 14 Mtu ambaye hana Roho hawezi kupokea mambo yatokayo kwa Roho wa Mungu, kwa kuwa ni upuzi kwake, naye hawezi kuyaelewa kwa sababu hayo yanaeleweka tu kwa upambanuzi wa rohoni. 15 Mtu wa kiroho hubainisha mambo yote, lakini yeye mwenyewe habainishwi na mtu yeyote.

    16 “Kwa maana ni nani aliyefahamu mawazo ya Bwana

    ili apate kumfundisha?”

    Lakini sisi tunayo mawazo ya Kristo.

  23. 15 Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.

  24. 1 Watoto wangu wapendwa, nawaandikia haya ili msitende dhambi. Lakini kama mtu yeyote akitenda dhambi, tunaye Mwombezi kwa Baba: ndiye Yesu Kristo, Mwenye Haki. 2 Yeye ndiye dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu, wala si kwa ajili ya dhambi zetu tu, bali pia kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote.

    3 Basi katika hili twajua ya kuwa tumemjua, tukizishika amri zake. 4 Mtu yeyote asemaye kuwa, “Ninamjua,” lakini hazishiki amri zake, ni mwongo, wala ndani ya mtu huyo hamna kweli. 5 Lakini mtu yeyote anayelitii neno lake, upendo wa Mungu umekamilika ndani yake kweli kweli. Katika hili twajua kuwa tumo ndani yake. 6 Yeyote anayesema anakaa ndani yake hana budi kuenenda kama Yesu alivyoenenda.

  25. 13 Tunajua kwamba twakaa ndani yake na yeye ndani yetu, kwa sababu ametupa sisi sehemu ya Roho wake. 14 Nasi tumeona na kushuhudia kwamba Baba amemtuma Mwanawe ili awe Mwokozi wa ulimwengu. 15 Kila akiriye kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, basi Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu. 16 Hivyo nasi twajua na kulitumainia pendo la Mungu alilo nalo kwa ajili yetu.

    Mungu ni Upendo. Kila akaaye katika upendo hukaa ndani ya Mungu na Mungu hukaa ndani yake. 17 Kwa njia hii, pendo hukamilishwa miongoni mwetu ili tupate kuwa na ujasiri katika siku ya hukumu, kwa sababu kama alivyo ndivyo tulivyo sisi katika ulimwengu huu. 18 Katika pendo hakuna hofu. Lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa sababu hofu inahusika na adhabu. Kila mwenye hofu hakukamilika katika pendo.

    19 Twampenda yeye kwa sababu yeye alitupenda kwanza. 20 Ikiwa mtu atasema, “Nampenda Mungu,” lakini anamchukia ndugu yake, yeye ni mwongo. Kwa maana kila mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, atampendaje Mungu asiyemuona? 21 Naye ametupa amri hii: Yeyote anayempenda Mungu lazima pia ampende ndugu yake.

  26. 5 Kisha Bwana akashuka katika wingu akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina lake, Bwana. 6 Bwana akapita mbele ya Mose, akitangaza, “Bwana, Bwana, Mungu mwenye huruma na neema, asiye mwepesi wa hasira, mwingi wa upendo na uaminifu, 7 akidumisha upendo kwa maelfu, pia akisamehe uovu, uasi na dhambi. Lakini haachi kuadhibu mwenye hatia; huwaadhibu watoto na watoto wao kwa ajili ya dhambi ya baba zao hata katika kizazi cha tatu na cha nne.”

  27. 29 Mambo ya siri ni ya Bwana Mungu wetu, bali yaliyofunuliwa ni yetu na watoto wetu milele, ili tuweze kuyafanya maneno yote ya sheria hii.

  28. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ndiye mchungaji wangu,

    sitapungukiwa na kitu.

    2 Hunilaza katika malisho

    ya majani mabichi,

    kando ya maji matulivu huniongoza,

    3 hunihuisha nafsi yangu.

    Huniongoza katika njia za haki

    kwa ajili ya jina lake.

  29. 10 “Kumcha Bwana ndicho chanzo cha hekima,

    na kumjua Aliye Mtakatifu ni ufahamu.

  30. 6 Mtafuteni Bwana maadamu anapatikana;

    mwiteni maadamu yu karibu.

    7 Mtu mwovu na aiache njia yake,

    na mtu mbaya na ayaache mawazo yake.

    Yeye na amrudie Bwana, naye atamrehemu,

    arudi kwa Mungu wetu, kwa kuwa atamsamehe bure kabisa.

    8 “Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu,

    wala njia zenu si njia zangu,”

    asema Bwana.

    9 “Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia,

    ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu

    na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.

  31. 11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. 12 Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.

  32. 18 Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote, ila ni Mungu Mwana pekee, aliye kifuani mwa Baba ndiye ambaye amemdhihirisha.

  33. 19 Ndipo wakamuuliza, “Huyo Baba yako yuko wapi?”

    Yesu akawajibu, “Ninyi hamnifahamu mimi ni nani, wala hammfahamu Baba yangu. Kama mngenifahamu mimi, mngemfahamu na Baba yangu.”

  34. 15 Kwa wale walio safi, kila kitu ni safi kwao. Lakini kwa wale waliopotoka na wasioamini, hakuna chochote kilicho safi. Kwa kweli nia zao na dhamiri zao zimepotoka. 16 Wanadai kumjua Mungu, lakini kwa matendo yao wanamkana. Hao watu ni chukizo, wasiotii, wasiofaa kwa jambo lolote jema.

  35. 20 Nasi pia twajua ya kwamba Mwana wa Mungu amekuja, naye ametupa sisi ufahamu ili tupate kumjua yeye aliye Kweli. Nasi tumo ndani yake yeye aliye Kweli, yaani, ndani ya Yesu Kristo Mwanawe. Yeye ndiye Mungu wa kweli na uzima wa milele.

  36. 24 Mungu ni Roho na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

  37. 14 Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani, 15 na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. 16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, 17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.

  38. 16 Ndugu zangu wapendwa, msidanganyike. 17 Kila kitolewacho kilicho chema na kilicho kamili, hutoka juu, na hushuka kutoka kwa Baba wa mianga, ambaye kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka. 18 Kwa mapenzi yake mwenyewe alituzaa kwa neno la kweli, kusudi tuwe kama mazao ya kwanza katika viumbe vyake vyote.

  39. 1 Baadaye Mose na Aroni wakaenda kwa Farao, wakamwambia, “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Waruhusu watu wangu waende, ili waweze kunifanyia sikukuu huko jangwani.’ ”

    2 Farao akasema, “Huyo Bwana ni nani, hata nimtii na kuruhusu Israeli uende? Simjui huyo Bwana wala sitawaruhusu Israeli waende.”

  40. 8 Bwana ni mwema na mwenye adili,

    kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia zake.

  41. 33 “Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli

    baada ya siku zile,” asema Bwana.

    “Nitaweka sheria yangu katika nia zao,

    na kuiandika mioyoni mwao.

    Nitakuwa Mungu wao,

    nao watakuwa watu wangu.

    34 Mtu hatamfundisha tena jirani yake,

    wala mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘Mjue Bwana Mungu,’

    kwa sababu wote watanijua mimi,

    tangu aliye mdogo kabisa kwao, hadi aliye mkuu sana,”

    asema Bwana.

    “Kwa sababu nitasamehe uovu wao,

    wala sitazikumbuka dhambi zao tena.”

  42. 21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22 Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’ 23 Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’

  43. 21 Yeyote mwenye amri zangu na kuzishika ndiye anipendaye, naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”

  44. 1 Tazameni ni pendo kuu namna gani alilotupa Baba, kwamba sisi tuitwe wana wa Mungu! Na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. 2 Wapendwa, sasa tu wana wa Mungu, lakini bado haijadhihirika tutakavyokuwa, lakini twajua ya kwamba yeye atakapodhihirishwa, tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo.

  45. 14 Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli.

  46. 10 Mwizi huja ili aibe, kuua na kuangamiza. Mimi nimekuja ili wapate uzima kisha wawe nao tele.

  47. 1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.

  48. 5 Haya yote ni uthibitisho kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na kwa sababu hiyo ninyi mtahesabiwa kwamba mnastahili kuwa wa Ufalme wa Mungu, mnaoteswa kwa ajili wake. 6 Mungu ni mwenye haki: yeye atawalipa mateso wale wawatesao ninyi 7 na kuwapa ninyi mnaoteseka raha pamoja na sisi, wakati Bwana Yesu atakapodhihirishwa kutoka mbinguni katika mwali wa moto pamoja na malaika wake wenye nguvu. 8 Atawaadhibu wale wasiomjua Mungu na ambao hawakuitii Injili ya Bwana wetu Yesu. 9 Wataadhibiwa kwa uangamivu wa milele na kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa uweza wake, 10 siku hiyo atakapokuja kutukuzwa katika watakatifu wake na kustaajabiwa miongoni mwa wote walioamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwa hawa kwa sababu mliamini ushuhuda wetu kwenu.

    11 Kwa sababu hii, tunawaombea ninyi bila kukoma, ili Mungu apate kuwahesabu kuwa mnastahili wito wake na kwamba kwa uwezo wake apate kutimiza kila kusudi lenu jema na kila tendo linaloongozwa na imani yenu. 12 Tunaomba hivi ili Jina la Bwana wetu Yesu lipate kutukuzwa ndani yenu, nanyi ndani yake, kulingana na neema ya Mungu wetu na Bwana Yesu Kristo.

  49. 1 Awali ya yote, nasihi kwamba dua, sala, maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya watu wote: 2 kwa ajili ya wafalme na wale wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi kwa amani na utulivu, katika uchaji wote wa Mungu na utakatifu. 3 Jambo hili ni jema, tena linapendeza machoni pa Mungu Mwokozi wetu, 4 anayetaka watu wote waokolewe na wafikie kuijua kweli. 5 Kwa maana kuna Mungu mmoja na mpatanishi mmoja kati ya Mungu na wanadamu, yaani mwanadamu Kristo Yesu, 6 aliyejitoa mwenyewe kuwa fidia kwa ajili ya wanadamu wote: jambo hili lilishuhudiwa kwa wakati wake ufaao. 7 Nami kwa kusudi hili nimewekwa niwe mhubiri na mtume (nasema kweli katika Kristo wala sisemi uongo), mwalimu wa watu wa Mataifa katika imani na kweli.

  50. 12 Mose akamwambia Bwana, “Umekuwa ukiniambia, ‘Ongoza watu hawa,’ lakini hujanifahamisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Umesema, ‘Ninakujua wewe kwa jina lako, nawe umepata kibali mbele zangu.’ 13 Ikiwa umependezwa nami, nifundishe njia zako ili nipate kukujua, nami nizidi kupata kibali mbele zako. Kumbuka kuwa taifa hili ni watu wako.”

    14 Bwana akajibu, “Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.”

  51. 10 Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe,

    kwa maana wewe Bwana,

    hujawaacha kamwe wakutafutao.

  52. 10 “Tulieni, mjue ya kwamba mimi ndimi Mungu;

    nitatukuzwa katikati ya mataifa,

    nitatukuzwa katika dunia.”

  53. 5 Baba wa yatima, mtetezi wa wajane,

    ni Mungu katika makao yake matakatifu.

  54. 13 Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake,

    ndivyo Bwana anavyowahurumia wale wanaomcha;

  55. 2 Roho wa Bwana atakaa juu yake,

    Roho wa hekima na wa ufahamu,

    Roho wa shauri na wa uweza,

    Roho wa maarifa na wa kumcha Bwana

  56. 7 nitawapa moyo wa kunifahamu mimi, kwamba mimi ndimi Bwana. Watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, kwa maana watanirudia kwa moyo wao wote.

  57. 2 “Hili ndilo Bwana asemalo, yeye aliyeumba dunia, Bwana aliyeifanya na kuithibitisha, Bwana ndilo jina lake: 3 ‘Niite nami nitakuitika na kukuambia mambo makuu na yasiyochunguzika, usiyoyajua.’

  58. 23 Nami hivyo ndivyo nitakavyoonyesha ukuu wangu na utakatifu wangu, nami nitajijulisha mbele ya macho ya mataifa mengi. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.’

  59. 22 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake: “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. 23 Maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi. 24 Fikirini ndege! Wao hawapandi wala hawavuni, hawana ghala wala popote pa kuhifadhi nafaka; lakini Mungu huwalisha. Ninyi ni wa thamani zaidi kuliko ndege! 25 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake? 26 Kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini basi kuyasumbukia hayo mengine?

    27 “Angalieni maua jinsi yameavyo: Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. 28 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo, na kesho yanatupwa motoni, si atawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba! 29 Wala msisumbuke mioyoni mwenu mtakula nini au mtakunywa nini. Msiwe na wasiwasi juu ya haya. 30 Watu wa mataifa ya duniani husumbuka sana kuhusu vitu hivi vyote, lakini Baba yenu anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 31 Bali utafuteni Ufalme wa Mungu, na haya yote atawapa pia.

    32 “Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi Ufalme. 33 Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwizi hakaribii wala nondo haharibu. 34 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo moyo wako utakapokuwa pia.

  60. 3 Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa.

  61. 7 Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba pia. Tangu sasa, mnamjua Baba yangu, tena mmemwona.”

  62. 14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. 15 Siwaiti ninyi watumishi tena, kwa sababu watumishi hawajui bwana wao analofanya, bali nimewaita ninyi rafiki, kwa maana nimewajulisha mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu.

  63. 22 Ndipo Paulo akasimama katikati ya Areopago akasema, “Enyi watu wa Athene! Ninaona kwamba katika kila jambo ninyi ni watu wa dini sana. 23 Kwa kuwa nilipokuwa nikitembea mjini na kuangalia kwa bidii vitu vyenu vya kuabudiwa, niliona huko madhabahu moja iliyoandikwa: Kwa Mungu Asiyejulikana. Basi sasa kile ambacho mmekuwa mkikiabudu kama kisichojulikana, ndicho ninachowahubiria.

    24 “Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, yeye ndiye Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu. 25 Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji chochote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote. 26 Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi. 27 Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu. 28 ‘Kwa kuwa katika yeye tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni watoto wake.’

    29 “Kwa kuwa sisi ni watoto wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe, mfano uliotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu. 30 Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu. 31 Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.”

  64. 1 Ndugu zangu, shauku ya moyo wangu na maombi yangu kwa Mungu ni kwa ajili ya Waisraeli, kwamba waokolewe. 2 Kwa maana ninaweza nikashuhudia wazi kwamba wao wana juhudi kubwa kwa ajili ya Mungu, lakini juhudi yao haina maarifa. 3 Kwa kuwa hawakuijua haki itokayo kwa Mungu, wakatafuta kuweka haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu. 4 Kwa maana Kristo ni ukomo wa sheria ili kuwe na haki kwa kila mtu aaminiye.

  65. 20 Yuko wapi mwenye hekima? Yuko wapi msomi? Yuko wapi mwanafalsafa wa nyakati hizi? Je, Mungu hakufanya hekima ya ulimwengu huu kuwa upumbavu? 21 Kwa kuwa katika hekima ya Mungu, ulimwengu kwa hekima yake haukumjua yeye, ilimpendeza Mungu kuwaokoa wale walioamini kwa upuzi wa lile neno lililohubiriwa. 22 Wayahudi wanadai ishara za miujiza na Wayunani wanatafuta hekima. 23 Lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa: yeye kwa Wayahudi ni kikwazo na kwa Wayunani ni upuzi. 24 Lakini kwa wale ambao Mungu amewaita, Wayahudi na pia Wayunani, Kristo ndiye nguvu ya Mungu na pia hekima ya Mungu. 25 Kwa maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi kuliko hekima ya wanadamu, nao udhaifu wa Mungu una nguvu kuliko nguvu ya wanadamu.

  66. 12 Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu. Lina makali kuliko upanga wowote wenye makali kuwili, hivyo linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.

  67. 6 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa maana yeyote anayemjia Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na ya kuwa huwapa thawabu wale wamtafutao kwa bidii.

  68. 7 Watoto wapendwa, mtu yeyote asiwadanganye. Kila mtu atendaye haki ana haki, kama yeye alivyo na haki. 8 Yeye atendaye dhambi ni wa ibilisi, kwa sababu ibilisi amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili aziangamize kazi za ibilisi. 9 Yeyote aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wa Mungu wakaa ndani yake, wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa na Mungu. 10 Kwa jinsi hii tunaweza kujua dhahiri watoto wa Mungu na pia watoto wa ibilisi. Yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.

  69. 1 Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia.

  70. 5 Mjue basi ndani ya mioyo yenu kama mtu anavyomwadibisha mwanawe, ndivyo Bwana Mungu wako atawaadibisha ninyi.

  71. 7 Nitatangaza amri ya Bwana:

    Yeye aliniambia, “Wewe ni Mwanangu,

    leo mimi nimekuzaa.

  72. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

    1 Mbingu zinatangaza utukufu wa Mungu,

    anga zahubiri kazi ya mikono yake.

    2 Siku baada ya siku zinatoa habari,

    usiku baada ya usiku zinatangaza maarifa.

    3 Hakuna msemo wala lugha,

    ambapo sauti zao hazisikiki.

    4 Sauti yao imeenea duniani pote,

    nayo maneno yao yameenea

    hadi miisho ya ulimwengu.

    Katika mbingu amepiga hema kwa ajili ya jua,

    5 linafanana na bwana arusi

    akitoka chumbani mwake,

    kama shujaa afurahiavyo

    kukamilisha kushindana kwake.

    6 Huchomoza upande mmoja wa mbingu,

    na kufanya mzunguko wake

    hadi upande mwingine.

    Hakuna kilichojificha joto lake.

  73. 10 Hata kama baba yangu na mama wakiniacha,

    Bwana atanipokea.

  74. 26 Naye ataniita kwa sauti, ‘Wewe ni Baba yangu,

    Mungu wangu, Mwamba na Mwokozi wangu.’

  75. 11 Mwanangu, usiidharau adhabu ya Bwana

    na usichukie kukaripiwa naye,

    12 kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao,

    kama vile baba afanyavyo

    kwa mwana apendezwaye naye.

  76. 15 “Je, mama aweza kumsahau mtoto

    aliyeko matitini mwake akinyonya,

    wala asiwe na huruma

    juu ya mtoto aliyemzaa?

    Ingawa anaweza kusahau,

    mimi sitakusahau wewe!

  77. 5 Kwa maana Muumba wako ndiye mume wako,

    Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake,

    yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli ni Mkombozi wako,

    yeye anaitwa Mungu wa dunia yote.

  78. 14 “Rudini, enyi watu msio waaminifu, kwa kuwa mimi ni mume wenu,” asema Bwana. “Nitawachagua ninyi, mmoja kutoka kwenye mji, na wawili kutoka kwenye ukoo, nami nitawaleta Sayuni.

  79. 7 “Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango. 8 Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.

    9 “Au ni nani miongoni mwenu ambaye mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe? 10 Au mwanawe akimwomba samaki atampa nyoka? 11 Ikiwa ninyi basi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa vitu vizuri wale wamwombao?

  80. 11 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.

  81. 8 Filipo akamwambia, “Bwana, tuonyeshe Baba yako yatosha.”

    9 Yesu akamjibu, “Filipo, nimekaa nanyi muda huu wote hata usinijue? Mtu yeyote aliyeniona mimi, amemwona Baba. Sasa wawezaje kusema, ‘Tuonyeshe Baba’? 10 Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambia siyasemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba akaaye ndani yangu ndiye atendaye hizi kazi. 11 Nisadiki mimi kwamba niko ndani ya Baba na Baba yuko ndani yangu, la sivyo, niaminini kwa sababu ya zile kazi nizitendazo.

  82. 1 Sasa kuhusu chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu, tunajua kwamba “sisi sote tuna ujuzi.” Lakini ujuzi hujivuna, bali upendo hujenga. 2 Mtu yeyote anayedhani kwamba anajua kitu, bado hajui kama impasavyo kujua. 3 Lakini mtu ampendaye Mungu, hujulikana naye Mungu.

  83. 10 Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli

    baada ya siku zile, asema Bwana.

    Nitaziweka sheria zangu katika nia zao

    na kuziandika mioyoni mwao.

    Nitakuwa Mungu wao,

    nao watakuwa watu wangu.

    11 Mtu hatamfundisha tena jirani yake,

    wala mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘Mjue Bwana,’

    kwa sababu wote watanijua mimi,

    tangu aliye mdogo kabisa kwao, hadi aliye mkuu sana.

  84. 3 Mtafakarini sana yeye aliyestahimili upinzani mkuu namna hii kutoka kwa watu wenye dhambi, ili kwamba msije mkachoka na kukata tamaa.

    4 Katika kushindana kwenu dhidi ya dhambi, bado hamjapigana kiasi cha kumwaga damu yenu. 5 Nanyi mmesahau yale maneno ya kuwaonya yanayowataja ninyi kuwa wana, yakisema:

    “Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana,

    wala usikate tamaa akikukemea,

    6 kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao,

    na humwadhibu kila mmoja

    anayemkubali kuwa mwana.”

    7 Vumilieni taabu kwa ajili ya kufunzwa adabu. Mungu anawatendea ninyi kama watoto wake, kwa maana ni mtoto yupi asiyeadibishwa na mzazi wake? 8 Kama hakuna kuadibishwa (ambalo ni fungu la watoto wote), basi ninyi ni watoto wa haramu wala si watoto halali. 9 Tena, sisi sote tunao baba wa kimwili, waliotuadibisha nasi tukawaheshimu kwa ajili ya hilo. Je, si inatupasa kujinyenyekeza zaidi kwa Baba wa roho zetu ili tuishi? 10 Baba zetu walituadibisha kwa kitambo kidogo kama wao wenyewe walivyoona vyema, lakini Mungu hutuadibisha kwa faida yetu ili tupate kushiriki utakatifu wake. 11 Kuadibishwa wakati wowote hakuonekani kuwa kitu cha kufurahisha bali chenye maumivu kinapotekelezwa. Lakini baadaye huzaa matunda ya haki na amani kwa wale waliofunzwa nayo.