39 Bible Verses About God's Wisdom

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About God's Wisdom
  1. 13 Heri mtu yule aonaye hekima,

    mtu yule apataye ufahamu,

    14 kwa maana hekima ana faida kuliko fedha

    na mapato yake ni bora kuliko ya dhahabu safi.

    15 Hekima ana thamani kuliko marijani;

    hakuna chochote unachokitamani

    kinachoweza kulinganishwa naye.

    16 Maisha marefu yako katika mkono wake wa kuume;

    katika mkono wake wa kushoto

    kuna utajiri na heshima.

    17 Njia zake zinapendeza,

    mapito yake yote ni amani.

    18 Yeye ni mti wa uzima kwa wale wanaomkumbatia;

    wale wamshikao watabarikiwa.

    19 Kwa hekima Bwana aliiweka misingi ya dunia,

    kwa ufahamu aliziweka mbingu mahali pake;

    20 kwa maarifa yake vilindi viligawanywa,

    nayo mawingu yanadondosha umande.

    21 Mwanangu, hifadhi maamuzi mema na busara,

    usiache vitoke machoni pako;

    22 ndipo vitakapokuwa uzima nafsini mwako

    na pambo la neema shingoni mwako.

    23 Kisha utaenda katika njia yako salama,

    wala mguu wako hautajikwaa;

    24 ulalapo, hautaogopa;

    ulalapo usingizi wako utakuwa mtamu.

    25 Usiogope maafa ya ghafula

    au maangamizi yanayowapata waovu,

    26 kwa kuwa Bwana atakuwa tumaini lako

    na kuepusha mguu wako kunaswa katika mtego.

  2. 18 Kwa maana ujumbe wa msalaba kwa wale wanaopotea ni upuzi, lakini kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. 19 Kwa maana imeandikwa:

    “Nitaiharibu hekima ya wenye hekima,

    na kubatilisha akili ya wenye akili.”

    20 Yuko wapi mwenye hekima? Yuko wapi msomi? Yuko wapi mwanafalsafa wa nyakati hizi? Je, Mungu hakufanya hekima ya ulimwengu huu kuwa upumbavu? 21 Kwa kuwa katika hekima ya Mungu, ulimwengu kwa hekima yake haukumjua yeye, ilimpendeza Mungu kuwaokoa wale walioamini kwa upuzi wa lile neno lililohubiriwa. 22 Wayahudi wanadai ishara za miujiza na Wayunani wanatafuta hekima. 23 Lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa: yeye kwa Wayahudi ni kikwazo na kwa Wayunani ni upuzi. 24 Lakini kwa wale ambao Mungu amewaita, Wayahudi na pia Wayunani, Kristo ndiye nguvu ya Mungu na pia hekima ya Mungu. 25 Kwa maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi kuliko hekima ya wanadamu, nao udhaifu wa Mungu una nguvu kuliko nguvu ya wanadamu.

    26 Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika jamaa zenye vyeo. 27 Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima, Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu. 28 Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko, 29 ili mtu yeyote asijisifu mbele zake. 30 Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanyika kwetu hekima itokayo kwa Mungu, yaani haki, na utakatifu na ukombozi. 31 Hivyo, kama ilivyoandikwa: “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.”

  3. 13 Ni nani aliye na hekima na ufahamu miongoni mwenu? Basi na aionyeshe hiyo kwa maisha yake mema na kwa matendo yake yaliyotendwa kwa unyenyekevu utokanao na hekima. 14 Lakini ikiwa mna wivu na ni wenye chuki na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu kwa ajili ya hayo wala msiikatae kweli. 15 Hekima ya namna hiyo haishuki kutoka mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyo ya kiroho, na ya kishetani. 16 Kwa maana panapokuwa na wivu na ubinafsi, ndipo penye machafuko na uovu wa kila namna.

    17 Lakini hekima itokayo mbinguni kwanza ni safi, kisha inapenda amani, tena ni ya upole, iliyo tayari kusikiliza wengine kwa unyenyekevu, iliyojaa huruma na matunda mema, isiyopendelea mtu, tena isiyokuwa na unafiki. 18 Mavuno ya haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.

  4. 5 Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa. 6 Lakini anapoomba, lazima aamini wala asiwe na shaka, kwa sababu mtu aliye na shaka ni kama wimbi la bahari, lililochukuliwa na upepo na kutupwa huku na huku. 7 Mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapata kitu chochote kutoka kwa Bwana. 8 Yeye ni mtu mwenye nia mbili, mwenye kusitasita katika njia zake zote.

  5. 19 Wakati wa usiku lile fumbo lilifunuliwa kwa Danieli katika maono. Ndipo Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni, 20 na akasema:

    “Lihimidiwe jina la Mungu milele na milele;

    hekima na uweza ni vyake.

    21 Yeye hubadili nyakati na majira;

    huwaweka wafalme na kuwaondoa.

    Huwapa hekima wenye hekima,

    na maarifa wenye ufahamu.

    22 Hufunua siri na mambo yaliyofichika;

    anajua yale yaliyo gizani,

    nayo nuru hukaa kwake.

    23 Ninakushukuru na kukuhimidi,

    Ee Mungu wa baba zangu:

    Umenipa hekima na uwezo,

    umenijulisha kile tulichokuomba,

    umetujulisha ndoto ya mfalme.”

  6. 30 Kama vile ninyi wakati fulani mlivyokuwa waasi kwa Mungu lakini sasa mmepata rehema kwa sababu ya kutokutii kwao, 31 hivyo nao Waisraeli wamekuwa waasi ili kwamba wao nao sasa waweze kupata rehema kwa ajili ya rehema za Mungu kwenu. 32 Kwa maana Mungu amewafunga wanadamu wote kwenye kuasi ili apate kuwarehemu wote.

    33 Tazama jinsi kilivyo kina cha utajiri

    wa hekima na maarifa ya Mungu!

    Tazama jinsi ambavyo hukumu zake hazichunguziki,

    na ambavyo njia zake zisivyotafutikana!

    34 “Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Bwana?

    Au ni nani ambaye amekuwa mshauri wake?”

    35 “Au ni nani aliyempa chochote

    ili arudishiwe?”

    36 Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, viko kwake na kwa ajili yake.

    Utukufu ni wake milele! Amen.

  7. 1 Mwanangu, kama utayakubali maneno yangu

    na kuyaweka akiba maagizo yangu ndani mwako,

    2 kutega sikio lako kwenye hekima

    na kuweka moyo wako katika ufahamu,

    3 na kama ukiita busara

    na kuita kwa sauti ufahamu,

    4 na kama utaitafuta kama fedha

    na kuitafuta sana kama hazina iliyofichwa,

    5 ndipo utakapoelewa kumcha Bwana

    na kupata maarifa ya Mungu.

    6 Kwa maana Bwana hutoa hekima,

    na kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.

    7 Anahifadhi ushindi kwa ajili ya mwadilifu,

    yeye ni ngao kwa wale wasio na lawama,

    8 kwa kuwa hulinda mwenendo wa mwenye haki

    na kuhifadhi njia ya waaminifu wake.

    9 Ndipo utafahamu lipi lililo kweli na haki

    na sawa: yaani kila njia nzuri.

    10 Kwa maana hekima itaingia moyoni mwako,

    nayo maarifa yataifurahisha nafsi yako.

    11 Busara itakuhifadhi

    na ufahamu utakulinda.

    12 Hekima itakuokoa kutoka njia za waovu,

    kutoka kwa watu ambao maneno yao yamepotoka,

    13 wale waachao mapito yaliyonyooka

    wakatembea katika njia za giza,

    14 wale wapendao kutenda mabaya

    na kufurahia upotovu wa ubaya,

    15 ambao mapito yao yamepotoka

    na ambao ni wapotovu katika njia zao.

  8. 8 Usimkemee mwenye mzaha la sivyo atakuchukia;

    mkemee mwenye hekima naye atakupenda.

    9 Mfundishe mtu mwenye hekima

    naye atakuwa na hekima zaidi;

    mfundishe mtu mwadilifu

    naye atazidi kufundishika.

    10 “Kumcha Bwana ndicho chanzo cha hekima,

    na kumjua Aliye Mtakatifu ni ufahamu.

    11 Kwa maana kwa msaada wangu

    siku zako zitakuwa nyingi,

    na miaka itaongezwa katika maisha yako.

    12 Kama wewe una hekima, hekima yako itakupa tuzo;

    kama wewe ni mtu wa mzaha,

    wewe mwenyewe ndiwe utateseka.”

  9. 1 Mithali za Solomoni mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli:

    2 Kwa kupata hekima na nidhamu;

    kwa kufahamu maneno ya busara;

    3 kwa kujipatia nidhamu na busara,

    kufanya lililo sawa, haki na bila kupendelea;

    4 huwapa busara wajinga,

    maarifa na akili kwa vijana;

    5 wenye hekima na wasikilize nao waongeze elimu yao,

    wenye kupambanua na wapate mwongozo;

    6 kwa kufahamu mithali na mifano,

    misemo na vitendawili vya wenye hekima.

    7 Kumcha Bwana ndicho chanzo cha maarifa,

    lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu.

  10. 24 Wakati mkulima alimapo ili apande,

    je, hulima siku zote?

    Je, huendelea kubomoa ardhi

    na kusawazisha udongo?

    25 Akiisha kusawazisha shamba,

    je, hatapanyi mbegu za bizari na kutawanya jira?

    Je, hapandi ngano katika sehemu yake,

    shayiri katika eneo lake,

    na nafaka nyingine katika shamba lake?

    26 Mungu wake humwelekeza

    na kumfundisha njia iliyo sahihi.

    27 Iliki haipurwi kwa nyundo,

    wala gurudumu la gari halivingirishwi juu ya jira;

    iliki hupurwa kwa fimbo,

    na jira kwa ufito.

    28 Nafaka lazima isagwe ili kutengeneza mkate,

    kwa hiyo mtu haendelei kuipura daima.

    Ingawa huendesha magurudumu ya gari lake la kupuria juu yake,

    farasi wake hawasagi.

    29 Haya yote pia hutoka kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote,

    mwenye mashauri ya ajabu, na anayepita wote kwa hekima.

  11. 1 Nataka mjue jinsi ninavyojitaabisha kwa ajili yenu na kwa ajili ya wale walioko Laodikia, na pia kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona mimi binafsi. 2 Kusudi langu ni watiwe moyo na kuunganishwa katika upendo, ili wapate ule utajiri wa ufahamu mkamilifu, ili waijue siri ya Mungu, yaani, Kristo mwenyewe, 3 ambaye ndani yake kumefichwa hazina zote za hekima na maarifa.

  12. 18 Msijidanganye. Kama mtu yeyote miongoni mwenu akidhani kuwa ana hekima kwa viwango vya dunia hii, inampasa awe mjinga ili apate kuwa na hekima. 19 Kwa maana hekima ya ulimwengu huu ni upuzi mbele za Mungu. Kama ilivyoandikwa: “Mungu huwanasa wenye hekima katika hila yao,” 20 tena, “Bwana anajua kwamba mawazo ya wenye hekima ni ubatili.” 21 Hivyo basi, mtu asijivune kuhusu wanadamu! Vitu vyote ni vyenu, 22 ikiwa ni Paulo au Apolo au Kefa au dunia au uzima au mauti, au wakati uliopo au wakati ujao, haya yote ni yenu 23 na ninyi ni wa Kristo, naye Kristo ni wa Mungu.

  13. 16 Ni bora kiasi gani kupata hekima kuliko dhahabu,

    kuchagua ufahamu kuliko fedha!

  14. 1 Ndugu zangu nilipokuja kwenu, sikuja na maneno ya ushawishi wala hekima ya hali ya juu nilipowahubiria siri ya Mungu. 2 Kwa kuwa niliamua kutokujua kitu chochote wakati nikiwa nanyi isipokuwa Yesu Kristo aliyesulubiwa. 3 Mimi nilikuja kwenu nikiwa dhaifu na mwenye hofu na kwa kutetemeka sana. 4 Kuhubiri kwangu na ujumbe wangu haukuwa kwa hekima na maneno ya ushawishi bali kwa madhihirisho ya nguvu za Roho 5 ili imani yenu isiwe imejengwa katika hekima ya wanadamu bali katika nguvu za Mungu.

    6 Lakini miongoni mwa watu waliokomaa twanena hekima, wala si hekima ya ulimwengu huu au ya watawala wa dunia hii wanaobatilika. 7 Sisi tunanena hekima ya Mungu ambayo ni siri, tena iliyofichika, ambayo Mungu aliikusudia kabla ya ulimwengu kuwepo, kwa ajili ya utukufu wetu. 8 Hakuna hata mtawala mmoja wa nyakati hizi aliyeelewa jambo hili. Kwa maana kama wangelielewa, wasingemsulubisha Bwana wa utukufu. 9 Lakini ni kama ilivyoandikwa:

    “Hakuna jicho limepata kuona,

    wala sikio limepata kusikia,

    wala hayakuingia moyoni wowote,

    yale Mungu amewaandalia

    wale wampendao”:

    10 Lakini mambo haya Mungu ametufunulia kwa Roho wake.

    Roho huchunguza kila kitu, hata mambo ya ndani sana ya Mungu. 11 Kwa maana ni nani anayejua mawazo ya mtu isipokuwa roho iliyo ndani ya huyo mtu? Vivyo hivyo hakuna mtu ajuaye mawazo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu. 12 Basi hatukupokea roho ya dunia bali Roho atokaye kwa Mungu, ili tuweze kuelewa kile kipawa ambacho Mungu ametupatia bure. 13 Haya ndiyo tusemayo, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya wanadamu bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua kweli za kiroho kwa maneno ya kiroho. 14 Mtu ambaye hana Roho hawezi kupokea mambo yatokayo kwa Roho wa Mungu, kwa kuwa ni upuzi kwake, naye hawezi kuyaelewa kwa sababu hayo yanaeleweka tu kwa upambanuzi wa rohoni. 15 Mtu wa kiroho hubainisha mambo yote, lakini yeye mwenyewe habainishwi na mtu yeyote.

    16 “Kwa maana ni nani aliyefahamu mawazo ya Bwana

    ili apate kumfundisha?”

    Lakini sisi tunayo mawazo ya Kristo.

  15. Sehemu Ya Nne: Mungu Anazungumza

    1 Kisha Bwana akamjibu Ayubu kutoka upepo wa kisulisuli. Akasema:

    2 “Nani huyu atiaye mashauri yangu giza

    kwa maneno yasiyo na maarifa?

    3 Jikaze kama mwanaume;

    nitakuuliza swali,

    nawe unijibu.

    4 “Ulikuwa wapi nilipoweka misingi ya dunia?

    Niambie, kama unafahamu.

    5 Ni nani aliyeweka alama vipimo vyake?

    Hakika wewe unajua!

    Ni nani aliyenyoosha kamba ya kupimia juu yake?

    6 Je, misingi yake iliwekwa juu ya nini,

    au ni nani aliyeweka jiwe la pembeni,

    7 wakati nyota za asubuhi zilipoimba pamoja,

    na malaika wote walipokuwa wakipiga kelele kwa furaha?

    8 “Ni nani aliyeifungia bahari milango

    ilipopasuka kutoka tumbo,

    9 nilipoyafanya mawingu kuwa vazi lake,

    na kuyafungia katika giza nene,

    10 nilipoamuru mipaka yake,

    na kuiweka milango yake na makomeo mahali pake,

    11 niliposema, ‘Unaweza kufika mpaka hapa wala si zaidi;

    hapa ndipo mawimbi yako yenye kiburi yatakapokomea’?

    12 “Umepata kuiamrisha asubuhi ipambazuke,

    au kuyaonyesha mapambazuko mahali pake,

    13 yapate kushika miisho ya dunia,

    na kuwakungʼuta waovu waliomo?

    14 Dunia hubadilika kama udongo wa mfinyanzi chini ya lakiri;

    sura yake hukaa kama ile ya vazi.

    15 Waovu huzuiliwa nuru yao,

    nao mkono wao ulioinuliwa huvunjwa.

    16 “Je, umepata kufika kwenye chemchemi za bahari?

    Au kutembea mahali pa ndani pa vilindi?

    17 Umewahi kuonyeshwa malango ya mauti?

    Umewahi kuiona milango ya uvuli wa mauti?

    18 Je, wewe unafahamu ukubwa wa dunia?

    Niambie kama unajua haya yote.

    19 “Njia ya kufika kwenye makao ya nuru ni ipi?

    Nako maskani mwa giza ni wapi?

    20 Je, unaweza kuvirudisha kwenye makao yake?

    Unajua njia za kufika maskani mwake?

    21 Hakika unajua, kwa kuwa ulikuwa umeshazaliwa!

    Kwani umeishi miaka mingi!

    22 “Je, umeshawahi kuingia katika ghala za theluji,

    au kuona ghala za mvua ya mawe,

    23 ambazo nimeziweka akiba kwa ajili ya wakati wa taabu,

    na kwa ajili ya wakati wa vita na mapigano?

    24 Ni ipi njia iendayo mahali umeme wa radi unapotawanyiwa,

    au mahali upepo wa mashariki unaposambaziwa juu ya dunia?

    25 Ni nani aliyepasua mifereji kwa ajili ya maji mengi ya mvua yaendayo kasi

    na njia ya umeme wa radi,

    26 ili kusababisha mvua kunyeshea mahali pasipokaliwa na mtu,

    jangwa lisilo na yeyote ndani yake,

    27 ili kuitosheleza nchi ya ukiwa na jangwa,

    na majani yaanze kumea ndani yake?

    28 Je, mvua ina baba?

    Ni nani baba azaaye matone ya umande?

    29 Barafu inatoka tumbo la nani?

    Ni nani azaaye ukungu kutoka mbinguni,

    30 wakati maji yawapo magumu kama jiwe,

    wakati uso wa vilindi vya maji unapoganda?

    31 “Je, waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia?

    Waweza kulegeza kamba za Orioni?

    32 Waweza kuyaongoza makundi ya nyota kwa majira yake,

    au kuongoza Dubu na watoto wake?

    33 Je, unajua sheria zinazotawala mbingu?

    Waweza kuweka utawala wa Mungu duniani?

    34 “Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni,

    na kujifunika mwenyewe na gharika ya maji?

    35 Je, wewe hutuma umeme wa radi kwenye njia zake?

    Je, hutoa taarifa kwako kukuambia, ‘Sisi tuko hapa’?

    36 Ni nani aliyeujalia moyo hekima

    au kuzipa akili ufahamu?

    37 Nani mwenye hekima ya kuyahesabu mawingu?

    Ni nani awezaye kuinamisha magudulia ya mbinguni

    38 wakati mavumbi yawapo magumu,

    na mabonge ya udongo kushikamana pamoja?

    39 “Je, utamwindia simba jike mawindo,

    na kuwashibisha simba wenye njaa

    40 wakati wao wamejikunyata mapangoni mwao,

    au wakivizia kichakani?

    41 Ni nani ampaye kunguru chakula

    wakati makinda yake yanamlilia Mungu,

    yakizungukazunguka kwa ajili ya kukosa chakula?

  16. 15 Kwa hiyo angalieni sana jinsi mnavyoenenda, si kama watu wasio na hekima, bali kama wenye hekima, 16 mkiukomboa wakati, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu. 17 Kwa hiyo msiwe wajinga, bali mpate kujua nini mapenzi ya Bwana.

  17. 15 Kwa sababu hii, tangu niliposikia juu ya imani yenu katika Bwana Yesu na upendo wenu kwa watakatifu wote, 16 sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, nikiwakumbuka katika maombi yangu. 17 Nazidi kumwomba Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awajalieni ninyi roho ya hekima na ya ufunuo, ili mpate kumjua zaidi. 18 Ninaomba pia kwamba macho ya mioyo yenu yatiwe nuru ili mpate kujua tumaini mliloitiwa, utajiri wa urithi wa utukufu wake kwa watakatifu 19 na uweza wake mkuu usiolinganishwa kwa ajili yetu sisi tuaminio. Uweza huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na ile nguvu kuu mno 20 aliyoitumia katika Kristo alipomfufua kutoka kwa wafu, na akamketisha mkono wake wa kuume huko mbinguni, 21 juu sana kuliko falme zote na mamlaka, enzi na milki, na juu ya kila jina litajwalo, si katika ulimwengu huu tu, bali katika ule ujao pia. 22 Naye Mungu ameweka vitu vyote viwe chini ya miguu yake na amemfanya yeye awe kichwa cha vitu vyote kwa ajili ya Kanisa, 23 ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake yeye aliye yote katika yote.

  18. 24 Ee Bwana, jinsi matendo yako yalivyo mengi!

    Kwa hekima ulizifanya zote,

    dunia imejaa viumbe vyako.

    25 Pale kuna bahari, kubwa na yenye nafasi tele,

    imejaa viumbe visivyo na idadi,

    vitu vyenye uhai vikubwa na vidogo.

    26 Huko meli huenda na kurudi,

    pia Lewiathani, uliyemuumba acheze ndani yake.

  19. 12 Ni nani aliyepima maji ya bahari

    kwenye konzi ya mkono wake,

    au kuzipima mbingu kwa shibiri yake?

    Ni nani aliyeyashika mavumbi ya dunia katika kikapu,

    au kupima milima kwenye kipimio

    na vilima kwenye mizani?

    13 Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Bwana,

    au kumfundisha akiwa kama mshauri wake?

    14 Ni nani ambaye Bwana ametaka shauri kwake ili kumwelimisha,

    naye ni nani aliyemfundisha njia iliyo sawa?

    Ni nani aliyemfundisha maarifa

    au kumwonyesha mapito ya ufahamu?

  20. 9 “Nawe Solomoni mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa kujitoa kwa moyo wote na kwa nia ya kumkubali, kwa maana Bwana huuchunguza kila moyo na kujua kila kusudi la kila fikira. Ukimtafuta, ataonekana kwako; bali kama ukimwacha, yeye atakukataa milele.

  21. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

    1 Ee Bwana, umenichunguza

    na kunijua.

    2 Unajua ninapoketi na ninapoinuka;

    unatambua mawazo yangu tokea mbali.

    3 Unafahamu kutoka kwangu na kulala kwangu;

    unaelewa njia zangu zote.

    4 Kabla neno halijafika katika ulimi wangu,

    wewe walijua kikamilifu, Ee Bwana.

    5 Umenizunguka nyuma na mbele;

    umeweka mkono wako juu yangu.

    6 Maarifa haya ni ya ajabu mno kwangu,

    ni ya juu sana kwangu kuyafikia.

  22. 28 Je wewe, hufahamu?

    Je wewe, hujasikia?

    Bwana ni Mungu wa milele,

    Muumba wa miisho ya dunia.

    Hatachoka wala kulegea,

    wala hakuna hata mmoja

    awezaye kuupima ufahamu wake.

  23. 12 Lakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake,

    akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake,

    na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake.

  24. 7 Usiku ule Mungu akamtokea Solomoni na kumwambia, “Omba lolote utakalo nikupe.”

    8 Solomoni akamjibu Mungu, “Umemwonyesha baba yangu Daudi fadhili nyingi, nawe umeniweka niwe mfalme mahali pake. 9 Sasa, Bwana Mungu, ahadi yako kwa baba yangu Daudi na ithibitike, kwa kuwa umenifanya mimi mfalme juu ya watu ambao ni wengi kama mavumbi ya nchi. 10 Nakuomba unipe mimi hekima na maarifa, ili niweze kuongoza watu hawa, kwa kuwa ni nani awezaye kutawala hawa watu wako walio wengi hivi?”

    11 Mungu akamwambia Solomoni, “Kwa kuwa jambo hili ndilo shauku ya moyo wako na hukuomba mali, utajiri au heshima, wala kifo kwa ajili ya adui zako, nawe kwa kuwa hukuomba maisha marefu, bali umeomba hekima na maarifa ili kuongoza watu wangu ambao nimekufanya uwe mfalme juu yao, 12 kwa hiyo utapewa hekima na maarifa. Tena nitakupa pia mali, utajiri na heshima, ambavyo hakuna mfalme yeyote aliyekuwepo kabla yako amewahi kuwa navyo, na hakuna yeyote baada yako atakayekuwa navyo.”

  25. 8 “Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu,

    wala njia zenu si njia zangu,”

    asema Bwana.

    9 “Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia,

    ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu

    na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.

  26. 8 Ingawa mimi ni mdogo kuliko aliye mdogo kabisa miongoni mwa watakatifu wote, nilipewa neema hii: ili niwahubirie watu wa Mataifa kuhusu utajiri usiopimika ulio ndani ya Kristo, 9 na kuweka wazi kwa kila mtu siri hii iliyokuwa imefichwa tangu zamani katika Mungu, aliyeumba vitu vyote. 10 Ili sasa kwa njia ya Kanisa, hekima yote ya Mungu ipate kujulikana kwa watawala na wenye mamlaka katika ulimwengu wa roho, 11 sawasawa na kusudi lake la milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.

  27. 5 Bwana wetu ni mkuu na mwenye uwezo mwingi,

    ufahamu wake hauna kikomo.

  28. 24 “Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. 25 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, na upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba. Lakini haikuanguka; kwa sababu msingi wake ulikuwa kwenye mwamba. 26 Naye kila anayesikia haya maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. 27 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.”

    28 Yesu alipomaliza kusema maneno haya, makutano ya watu wakashangazwa sana na mafundisho yake, 29 kwa sababu alifundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wao wa sheria.

  29. 7 “Sasa, Ee Bwana Mungu wangu, umemfanya mtumishi wako mfalme badala ya baba yangu Daudi. Lakini mimi ni mtoto mdogo tu, wala sijui jinsi ya kutekeleza wajibu wangu. 8 Mtumishi wako yuko hapa miongoni mwa watu uliowachagua: taifa kubwa, watu wengi wasioweza kuhesabika wala kutoa idadi yao. 9 Hivyo mpe mtumishi wako moyo wa ufahamu ili kutawala watu wako na kupambanua kati ya mema na mabaya. Kwa maana, ni nani awezaye kutawala watu wako hawa walio wengi hivi?”

    10 Bwana akapendezwa kwamba Solomoni ameliomba jambo hili. 11 Basi Mungu akamwambia, “Kwa kuwa umeomba neno hili na hukuomba maisha marefu au upate utajiri kwa nafsi yako, wala adui zako wafe, bali umeomba ufahamu katika kutoa haki, 12 nitafanya lile uliloomba. Nitakupa moyo wa hekima na wa ufahamu, kiasi kwamba hajakuwepo mtu mwingine kama wewe, wala kamwe hatakuwepo baada yako. 13 Zaidi ya hayo, nitakupa yale ambayo hukuomba, yaani utajiri na heshima, ili kwamba maisha yako yote hapatakuwa na mtu kama wewe miongoni mwa wafalme. 14 Nawe kama ukienenda katika njia zangu na kutii sheria na amri zangu kama baba yako Daudi alivyofanya, nitakupa maisha marefu.”

  30. 28 Wakati Israeli yote iliposikia hukumu aliyotoa mfalme, wakamwogopa mfalme, kwa sababu waliona kuwa alikuwa na hekima kutoka kwa Mungu kwa kutoa haki.

  31. 22 “Je, yuko mtu yeyote awezaye kumfundisha Mungu maarifa,

    iwapo yeye ndiye ahukumuye hata walio juu ya wote?

  32. 7 Ni nani basi aliye kama mimi? Yeye na atangaze.

    Yeye atangaze na kuweka mbele yangu

    ni kitu gani kilichotokea tangu nilipoumba watu wangu wa kale,

    tena ni nini kitakachotokea:

    naam, yeye na atoe unabii ni nini kitakachokuja.

  33. 7 Ni nani ambaye haimpasi kukuheshimu wewe,

    Ee Mfalme wa mataifa?

    Hii ni stahili yako.

    Miongoni mwa watu wote wenye hekima

    katika mataifa na katika falme zao zote,

    hakuna aliye kama wewe.

  34. 12 Je, hekima haipatikani katikati ya wazee?

    Je, maisha marefu hayaleti ufahamu?

    13 “Hekima na nguvu ni vya Mungu;

    shauri na ufahamu ni vyake yeye.

  35. 14 Lakini kusudieni mioyoni mwenu msisumbuke awali kuhusu mtakalosema mbele ya mashtaka. 15 Kwa maana nitawapa maneno na hekima ambayo hakuna hata adui yenu mmoja atakayeweza kushindana nayo wala kuipinga.

  36. 29 Mungu akampa Solomoni hekima na akili kubwa, pia ufahamu mpana usiopimika kama mchanga ulioko pwani ya bahari. 30 Hekima ya Solomoni ilikuwa kubwa kuliko hekima ya watu wote wa Mashariki na kubwa kuliko hekima yote ya Misri. 31 Alikuwa na hekima kuliko kila mwandishi, akiwemo Ethani Mwezrahi: kuliko Hemani, Kalkoli na Darda, wana wa Maholi. Umaarufu wake ukaenea kwa mataifa yote yaliyomzunguka. 32 Akanena mithali 3,000 na nyimbo zake zilikuwa 1,005. 33 Akaelezea maisha ya mimea kuanzia mwerezi wa Lebanoni hadi hisopo iotayo ukutani. Pia akafundisha kuhusu wanyama na ndege, wanyama wenye damu baridi, wakiwemo samaki. 34 Watu wa mataifa yote wakaja kusikiliza hekima ya Solomoni, waliotumwa na wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamesikia juu ya hekima yake.

  37. 24 Kwake yeye awezaye kuwalinda ninyi msianguke na kuwaleta mbele za utukufu wake mkuu bila dosari na kwa furaha ipitayo kiasi: 25 kwake yeye Mungu pekee Mwokozi wetu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu, utukufu, ukuu, uweza na mamlaka ni vyake tangu milele, sasa na hata milele! Amen.

  38. 30 Hakuna hekima, wala akili, wala mpango

    unaoweza kufaulu dhidi ya Bwana.

  39. 12 Bwana atakapokuwa amemaliza kazi yake yote dhidi ya Mlima Sayuni na Yerusalemu, atasema, “Nitamwadhibu mfalme wa Ashuru kwa ajili ya majivuno ya ukaidi wa moyo wake na kutazama kwa macho yenye dharau.” 13 Kwa kuwa anasema:

    “ ‘Kwa nguvu za mkono wangu nimefanya hili,

    kwa hekima yangu, kwa sababu nina ufahamu.

    Niliondoa mipaka ya mataifa,

    niliteka nyara hazina zao,

    kama yeye aliye shujaa

    niliwatiisha wafalme wao.

    14 Kama mtu atiavyo mkono kwenye kiota,

    ndivyo mkono wangu ulivyochukua utajiri wa mataifa;

    kama watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa,

    ndivyo nilivyokusanya nchi zote;

    wala hakuna hata mmoja aliyepiga bawa

    au kufungua kinywa chake kutoa mlio.’ ”