59 Bible Verses About Peace

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Peace
  1. 1 Kwa hiyo, ndugu zangu, ninaowapenda na ambao ninawaonea shauku, ninyi mlio furaha yangu na taji yangu, hivi ndivyo iwapasavyo kusimama imara katika Bwana, ninyi wapenzi wangu.

    2 Nawasihi Euodia na Sintike wawe na nia moja katika Bwana. 3 Naam, nakusihi wewe pia, mwenzangu mwaminifu, uwasaidie hawa wanawake, kwa sababu walijitaabisha katika kazi ya Injili pamoja nami bega kwa bega, wakiwa pamoja na Klementi na watendakazi wenzangu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima.

    4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! 5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

    8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo. 9 Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.

  2. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2 ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

  3. 13 Lakini sasa katika Kristo Yesu, ninyi ambao hapo kwanza mlikuwa mbali na Mungu, sasa mmeletwa karibu kwa njia ya damu ya Kristo.

    14 Kwa maana yeye mwenyewe ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi tuliokuwa wawili, yaani, Wayahudi na watu wa Mataifa, tuwe wamoja kwa kuvunja kizuizi na kubomoa ule ukuta wa uadui uliokuwa kati yetu, 15 kwa kuibatilisha ile sheria pamoja na amri zake na maagizo yake alipoutoa mwili wake, ili apate kufanya ndani yake mtu mmoja mpya badala ya hao wawili, hivyo akifanya amani, 16 naye katika mwili huu mmoja awapatanishe wote wawili na Mungu kupitia msalaba, ili kwa huo msalaba akaangamiza uadui wao. 17 Alikuja na kuhubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali na pia akahubiri amani kwao waliokuwa karibu. 18 Kwa maana kwa kupitia kwake, sisi sote tunaweza kumkaribia Baba katika Roho mmoja.

  4. 23 Yesu akamjibu, “Mtu yeyote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake. 24 Mtu yeyote asiyenipenda hayashiki maneno yangu na maneno niliyowapa si yangu bali ni ya Baba aliyenituma.

    25 “Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi. 26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27 Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.

  5. 16 Kwa hiyo nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. 17 Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka. 18 Lakini kama mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria.

    19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

    22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria. 24 Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake. 25 Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho.

  6. 17 Kwa maana Ufalme wa Mungu si kula na kunywa, bali ni haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu. 18 Kwa sababu mtu yeyote anayemtumikia Kristo kwa jinsi hii, anampendeza Mungu na kukubaliwa na wanadamu.

    19 Kwa hiyo na tufanye bidii kutafuta yale yaletayo amani na kujengana sisi kwa sisi.

  7. 1 Katika siku ile, wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda:

    Tuna mji ulio na nguvu,

    Mungu huufanya wokovu kuwa kuta zake na maboma yake.

    2 Fungua malango ili taifa lenye haki lipate kuingia,

    taifa lile lidumishalo imani.

    3 Utamlinda katika amani kamilifu

    yeye ambaye moyo wake ni thabiti

    kwa sababu anakutumaini wewe.

    4 Mtumaini Bwana milele,

    kwa kuwa Bwana, Bwana, ni Mwamba wa milele.

  8. 31 Yesu akawajibu, “Je, sasa mnaamini? 32 Saa inakuja, naam, imekwisha kuwadia, mtakapotawanyika kila mmoja kwenda nyumbani kwake na kuniacha peke yangu. Lakini mimi siko peke yangu kwa sababu Baba yu pamoja nami. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

  9. 165 Wanaopenda sheria yako wana amani tele,

    wala hakuna kitu kinachoweza kuwakwaza.

    166 Ee Bwana, ninangojea wokovu wako,

    nami ninafuata amri zako,

    167 Ninazitii sheria zako,

    kwa sababu ninazipenda mno.

    168 Nimetii mausia yako na sheria zako,

    kwa kuwa njia zangu zote zinajulikana kwako.

  10. 12 Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi. 14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.

    15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu.

  11. 12 Yeyote kati yenu anayependa uzima

    na kutamani kuziona siku nyingi njema,

    13 basi auzuie ulimi wake na mabaya,

    na midomo yake kutokana na kusema uongo.

    14 Aache uovu, atende mema,

    aitafute amani na kuifuatilia.

  12. 16 Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge. Wala msiwe watu wenye kujivuna kwamba mnajua kila kitu.

    17 Msimlipe mtu yeyote ovu kwa ovu. Jitahidini ili mtende yaliyo mema machoni pa watu wote. 18 Kama ikiwezekana, kwa upande wenu kaeni kwa amani na watu wote. 19 Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Ni juu yangu kulipiza kisasi, nitalipiza,” asema Bwana. 20 Badala yake:

    “Kama adui yako ana njaa, mlishe;

    kama ana kiu, mpe kinywaji.

    Kwa kufanya hivyo,

    unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.”

    21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.

  13. 6 Kwa maana, kwa ajili yetu mtoto amezaliwa,

    tumepewa mtoto mwanaume,

    nao utawala utakuwa mabegani mwake.

    Naye ataitwa

    Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu,

    Baba wa Milele, Mfalme wa Amani.

    7 Kuongezeka kwa utawala wake na amani

    hakutakuwa na mwisho.

    Atatawala katika kiti cha enzi cha Daudi

    na juu ya ufalme wake,

    akiuthibitisha na kuutegemeza

    kwa haki na kwa adili,

    tangu wakati huo na hata milele.

    Wivu wa Bwana Mwenye Nguvu Zote

    utatimiza haya.

  14. 6 Kwa maana kuwa na nia ya mwili ni mauti, bali kuwa na nia inayoongozwa na Roho ni uzima na amani. 7 Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui na Mungu, kwa maana haiitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. 8 Wale wanaotawaliwa na mwili, hawawezi kumpendeza Mungu.

    9 Lakini ninyi, hamtawaliwi na mwili, bali na Roho, ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu. Mtu yeyote ambaye hana Roho wa Kristo, yeye si wa Kristo.

  15. 13 Ni nani aliye na hekima na ufahamu miongoni mwenu? Basi na aionyeshe hiyo kwa maisha yake mema na kwa matendo yake yaliyotendwa kwa unyenyekevu utokanao na hekima. 14 Lakini ikiwa mna wivu na ni wenye chuki na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu kwa ajili ya hayo wala msiikatae kweli. 15 Hekima ya namna hiyo haishuki kutoka mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyo ya kiroho, na ya kishetani. 16 Kwa maana panapokuwa na wivu na ubinafsi, ndipo penye machafuko na uovu wa kila namna.

    17 Lakini hekima itokayo mbinguni kwanza ni safi, kisha inapenda amani, tena ni ya upole, iliyo tayari kusikiliza wengine kwa unyenyekevu, iliyojaa huruma na matunda mema, isiyopendelea mtu, tena isiyokuwa na unafiki. 18 Mavuno ya haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.

  16. 11 Hatimaye, ndugu zangu, kwaherini. Kuweni wakamilifu, mkafarijike, kuweni wa nia moja, kaeni kwa amani. Naye Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi.

  17. 9 Heri walio wapatanishi,

    maana hao wataitwa wana wa Mungu.

  18. 19 Ikawa jioni ya ile siku ya kwanza ya juma, wanafunzi wake walikuwa pamoja, milango ikiwa imefungwa kwa kuwaogopa Wayahudi. Naye Yesu aliwatokea, akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!” 20 Baada ya kusema haya, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Wanafunzi wake wakafurahi sana walipomwona Bwana.

    21 Yesu akawaambia tena, “Amani iwe nanyi! Kama vile Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawatuma ninyi.” 22 Naye alipokwisha kusema haya, akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu.

  19. 16 Basi, Bwana wa amani mwenyewe awapeni amani nyakati zote na kwa kila njia. Bwana awe nanyi nyote.

  20. 19 Kwa kuwa ilimpendeza Mungu kwamba utimilifu wake wote ukae ndani yake, 20 na kwa njia yake aweze kuvipatanisha vitu vyote na yeye mwenyewe, viwe ni vitu vilivyo duniani au vilivyo mbinguni, kwa kufanya amani kwa damu yake, iliyomwagika msalabani.

    21 Hapo kwanza mlikuwa mmetengana na Mungu, na mlikuwa adui zake katika nia zenu kwa sababu ya mienendo yenu mibaya. 22 Lakini sasa Mungu amewapatanisha ninyi kwa njia ya mwili wa Kristo kupitia mauti, ili awalete mbele zake mkiwa watakatifu, bila dosari wala lawama,

  21. 8 Hatimaye, ninyi nyote kuweni na nia moja, wenye kuhurumiana, mkipendana kama ndugu, na mwe wasikitivu na wanyenyekevu. 9 Msilipe ovu kwa ovu, au jeuri kwa jeuri, bali barikini, kwa maana hili ndilo mliloitiwa ili mpate kurithi baraka. 10 Kwa maana,

    “Yeyote apendaye uzima

    na kuona siku njema,

    basi auzuie ulimi wake usinene mabaya,

    na midomo yake isiseme hila.

    11 Mtu huyo lazima aache uovu, akatende mema;

    lazima aitafute amani na kuifuatilia sana.

    12 Kwa maana macho ya Bwana

    huwaelekea wenye haki,

    na masikio yake yako makini

    kusikiliza maombi yao.

    Bali uso wa Bwana uko kinyume

    na watendao maovu.”

  22. 8 Nitajilaza chini na kulala kwa amani,

    kwa kuwa wewe peke yako, Ee Bwana,

    waniwezesha kukaa kwa salama.

  23. 13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

  24. 10 Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama nawaletea habari njema za furaha itakayokuwa kwa watu wote. 11 Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. 12 Hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori ya kulia ngʼombe.”

    13 Ghafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema,

    14 “Atukuzwe Mungu juu mbinguni,

    na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”

  25. 11 Bwana huwapa watu wake nguvu;

    Bwana huwabariki watu wake kwa kuwapa amani.

  26. 14 Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo utakatifu, ambao bila kuwa nao hakuna mtu atakayemwona Bwana. 15 Angalieni sana mtu yeyote asiikose neema ya Mungu na kwamba shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo. 16 Angalieni miongoni mwenu asiwepo mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, ambaye kwa ajili ya mlo mmoja aliuza haki ya uzaliwa wake wa kwanza. 17 Baadaye kama mnavyofahamu, alipotaka kurithi ile baraka, alikataliwa, maana hakupata nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi.

  27. 24 “ ‘ “Bwana akubariki

    na kukulinda;

    25 Bwana akuangazie nuru ya uso wake

    na kukufadhili;

    26 Bwana akugeuzie uso wake

    na kukupa amani.” ’

  28. 26 Basi tuseme nini ndugu zangu? Mnapokutana pamoja, kila mmoja ana wimbo, au neno la mafundisho, au ufunuo, lugha mpya au atatafsiri. Mambo yote yatendeke kwa ajili ya kulijenga kanisa. 27 Kama mtu yeyote akinena kwa lugha, basi waseme watu wawili au watatu si zaidi, mmoja baada ya mwingine na lazima awepo mtu wa kutafsiri. 28 Lakini kama hakuna mtu wa kutafsiri, hao watu na wanyamaze kimya kanisani na wanene na nafsi zao wenyewe na Mungu.

    29 Manabii wawili au watatu wanene na wengine wapime yale yasemwayo. 30 Kama mtu yeyote aliyeketi karibu, akipata ufunuo, basi yule wa kwanza na anyamaze. 31 Kwa maana wote mnaweza kutoa unabii, mmoja baada ya mwingine, ili kila mtu apate kufundishwa na kutiwa moyo. 32 Roho za manabii huwatii manabii. 33 Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko bali ni Mungu wa amani.

    Kama ilivyo katika makusanyiko yote ya watakatifu,

  29. 1 Basi, mimi niliye mfungwa wa Bwana, nawasihi mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa. 2 Kwa unyenyekevu wote na upole, mkiwa wavumilivu, mkichukuliana kwa upendo. 3 Jitahidini kudumisha umoja wa Roho katika kifungo cha amani. 4 Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja. 5 Tena kuna Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja, 6 Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote, katika yote na ndani ya yote.

  30. 23 Mungu mwenyewe, Mungu wa amani, awatakase ninyi kabisa. Nanyi mhifadhiwe roho zenu, nafsi zenu na miili yenu, bila kuwa na lawama katika Bwana wetu Yesu Kristo. 24 Yeye aliyewaita ni mwaminifu naye atafanya hayo.

  31. 3 “ ‘Ikiwa mtafuata amri zangu na kuwa waangalifu kutii maagizo yangu, 4 nitawanyeshea mvua katika majira yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, na miti ya mashambani itazaa matunda yake. 5 Kupura nafaka kwenu kutaendelea mpaka wakati wa kuvuna zabibu. Pia kuvuna zabibu kutaendelea mpaka wakati wa kupanda mbegu, nanyi mtakula na kushiba, na mtaishi salama katika nchi yenu.

    6 “ ‘Nitawapa amani katika nchi, mpate kulala pasipo kutiwa hofu na yeyote. Nitawaondoa wanyama wakali watoke kwenye nchi, nao upanga hautapita katika nchi yenu.

  32. 18 Nimeziona njia zake, lakini nitamponya,

    nitamwongoza na kumrudishia upya faraja,

    19 nikiumba sifa midomoni ya waombolezaji

    katika Israeli.

    Amani, amani, kwa wale walio mbali

    na kwa wale walio karibu,”

    asema Bwana. “Nami nitawaponya.”

    20 Bali waovu ni kama bahari ichafukayo,

    ambayo haiwezi kutulia,

    mawimbi yake hutupa takataka na matope.

    21 Mungu wangu asema,

    “Hakuna amani kwa waovu.”

  33. 20 Basi Mungu wa amani, ambaye kwa damu ya Agano la milele alimleta tena kutoka kwa wafu Bwana wetu Yesu, yule Mchungaji Mkuu wa kondoo, 21 awafanye ninyi wakamilifu mkiwa mmekamilishwa katika kila jambo jema ili mpate kutenda mapenzi yake, naye atende ndani yetu kile kinachompendeza machoni Pake, kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye utukufu una yeye milele na milele. Amen.

  34. 13 Heri mtu yule aonaye hekima,

    mtu yule apataye ufahamu,

    14 kwa maana hekima ana faida kuliko fedha

    na mapato yake ni bora kuliko ya dhahabu safi.

    15 Hekima ana thamani kuliko marijani;

    hakuna chochote unachokitamani

    kinachoweza kulinganishwa naye.

    16 Maisha marefu yako katika mkono wake wa kuume;

    katika mkono wake wa kushoto

    kuna utajiri na heshima.

    17 Njia zake zinapendeza,

    mapito yake yote ni amani.

    18 Yeye ni mti wa uzima kwa wale wanaomkumbatia;

    wale wamshikao watabarikiwa.

  35. 22 “Hakuna amani kwa waovu,” asema Bwana.

  36. 10 Ijapotikisika milima, na vilima viondolewe,

    hata hivyo upendo wangu usiokoma kwenu hautatikisika,

    wala agano langu la amani halitaondolewa,”

    asema Bwana, mwenye huruma juu yenu.

  37. 50 “Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake utaifanyaje ili iweze kukolea tena? Mwe na chumvi ndani yenu, mkaishi kwa amani, kila mmoja na mwenzake.”

  38. 20 Mungu wa amani atamponda Shetani chini ya miguu yenu upesi.

    Neema ya Bwana wetu Yesu iwe nanyi. Amen.

  39. 34 “Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga. 35 Kwa maana nimekuja kumfitini

    “ ‘mtu na babaye,

    binti na mamaye,

    mkwe na mama mkwe wake;

    36 nao adui za mtu watakuwa

    ni wale watu wa nyumbani kwake.’

  40. 1 Awali ya yote, nasihi kwamba dua, sala, maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya watu wote: 2 kwa ajili ya wafalme na wale wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi kwa amani na utulivu, katika uchaji wote wa Mungu na utakatifu.

  41. 20 Upo udanganyifu katika mioyo

    ya wale ambao hupanga mabaya,

    bali kuna furaha kwa wale wanaoleta amani.

  42. 17 Hili ndilo asemalo Bwana,

    Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli:

    “Mimi ni Bwana, Mungu wako,

    nikufundishaye ili upate faida,

    nikuongozaye katika njia ikupasayo kuiendea.

    18 Laiti ungesikiliza kwa makini maagizo yangu,

    amani yako ingekuwa kama mto,

    haki yako kama mawimbi ya bahari.

  43. 22 Zikimbie tamaa mbaya za ujana, ufuate haki, imani, upendo na amani pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi. 23 Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa wajua ya kwamba hayo huzaa magomvi. 24 Tena haimpasi mtumishi wa Bwana kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu. 25 Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli, 26 ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake.

  44. 5 “Agano langu lilikuwa pamoja naye, agano la uhai na amani, nami nilimpa yote, ili aniche na kuniheshimu, naye akaniheshimu na kusimama akilicha Jina langu. 6 Fundisho la kweli lilikuwa kinywani mwake, wala hakuna uongo wowote uliopatikana katika midomo yake. Alitembea nami katika amani na unyofu, naye akawageuza wengi kutoka dhambini.

  45. 3 Alipoivunja ile lakiri ya pili, nikamsikia yule kiumbe wa pili mwenye uhai akisema, “Njoo!” 4 Ndipo akatokea farasi mwingine mwekundu sana. Yeye aliyempanda akapewa uwezo wa kuondoa amani duniani na kuwafanya watu wauane. Yeye akapewa upanga mkubwa.

    5 Mwana-kondoo alipoivunja ile lakiri ya tatu, nikamsikia yule kiumbe wa tatu mwenye uhai akisema, “Njoo!” Nikatazama, na mbele yangu alikuwepo farasi mweusi! Yeye aliyempanda alikuwa na mizani mkononi mwake. 6 Ndipo nikasikia kile kilichokuwa kama sauti katikati ya wale viumbe wanne wenye uhai ikisema, “Kipimo kimoja cha ngano kwa mshahara wa kibarua wa siku moja, na vipimo vitatu vya shayiri kwa mshahara wa kibarua cha siku moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!”

    7 Alipovunja ile lakiri ya nne, nikasikia sauti ya yule kiumbe wa nne mwenye uhai ikisema, “Njoo!” 8 Nikatazama, na hapo mbele yangu alikuwepo farasi mwenye rangi ya kijivujivu! Yeye aliyempanda aliitwa Mauti, naye Kuzimu alikuwa akimfuata nyuma yake kwa karibu. Wakapewa mamlaka juu ya robo ya dunia, kuua kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia.

  46. 1 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia. 2 Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Naenda kuwaandalia makao. 3 Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo.

  47. 15 Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri habari njema!”

  48. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ndiye mchungaji wangu,

    sitapungukiwa na kitu.

    2 Hunilaza katika malisho

    ya majani mabichi,

    kando ya maji matulivu huniongoza,

    3 hunihuisha nafsi yangu.

    Huniongoza katika njia za haki

    kwa ajili ya jina lake.

  49. 6 Mbwa mwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo,

    naye chui atalala pamoja na mbuzi,

    ndama, mwana simba na ngʼombe wa mwaka mmoja watakaa pamoja,

    naye mtoto mdogo atawaongoza.

    7 Ngʼombe na dubu watalisha pamoja,

    watoto wao watalala pamoja,

    na simba atakula majani makavu kama maksai.

    8 Mtoto mchanga atacheza karibu na shimo la nyoka,

    naye mtoto mdogo ataweka mkono wake

    kwenye kiota cha fira.

    9 Hawatadhuru wala kuharibu

    juu ya mlima wangu mtakatifu wote,

    kwa kuwa dunia itajawa na kumjua Bwana

    kama maji yajazavyo bahari.

  50. 9 Shangilia sana, ee Binti Sayuni!

    Piga kelele, Binti Yerusalemu!

    Tazama, Mfalme wako anakuja kwako,

    ni mwenye haki, naye ana wokovu,

    ni mpole, naye amepanda punda,

    mwana-punda, mtoto wa punda.

    10 Nitaondoa magari ya vita kutoka Efraimu

    na farasi wa vita kutoka Yerusalemu,

    nao upinde wa vita utavunjwa.

    Atatangaza amani kwa mataifa.

    Utawala wake utaenea kutoka bahari hadi bahari,

    na kutoka Mto Frati hadi mwisho wa dunia.

  51. 12 Mkiingia kwenye nyumba, itakieni amani. 13 Kama nyumba hiyo inastahili, amani yenu na iwe juu yake. La sivyo, amani yenu na iwarudie ninyi. 14 Kama mtu yeyote hatawakaribisha ninyi, wala kusikiliza maneno yenu, kungʼuteni mavumbi kutoka kwenye miguu yenu mtakapokuwa mnatoka kwenye nyumba hiyo au mji huo. 15 Amin, nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa miji ya Sodoma na Gomora kustahimili katika hukumu kuliko mji huo.

  52. 48 Kisha akamwambia yule mwanamke, “Dhambi zako zimesamehewa.”

    49 Lakini wale waliokuwa wameketi pamoja naye chakulani wakaanza kusemezana wao kwa wao, “Huyu ni nani ambaye hata anasamehe dhambi?”

    50 Yesu akamwambia yule mwanamke, “Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.”

  53. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa. 18 Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.

  54. 3 Neema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo,

  55. 2 Rehema, amani na upendo viwe kwenu kwa wingi.

  56. 11 “ ‘Haya ndiyo masharti kwa ajili ya sadaka ya amani ambayo mtu aweza kuileta kwa Bwana:

    12 “ ‘Ikiwa mtu atatoa sadaka ya amani kwa ajili ya kuonyesha shukrani, pamoja na sadaka hii ya shukrani, atatoa maandazi yasiyotiwa chachu yaliyochanganywa na mafuta, mikate myembamba isiyotiwa chachu iliyopakwa mafuta, maandazi ya unga laini uliokandwa vizuri na kuchanganywa na mafuta. 13 Pamoja na sadaka hii ya amani ya shukrani ataleta sadaka ya maandazi yaliyotengenezwa kwa chachu. 14 Ataleta moja ya kila aina ya andazi kama sadaka, matoleo kwa Bwana; hii ni ya kuhani anayenyunyiza damu ya sadaka ya amani. 15 Nyama ya sadaka ya amani kwa ajili ya shukrani lazima iliwe siku iyo hiyo inapotolewa; hutabakiza kitu chochote mpaka asubuhi.

  57. 2 Mataifa mengi yatakuja na kusema,

    “Njooni, twendeni mlimani mwa Bwana,

    kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo.

    Atatufundisha njia zake,

    ili tuweze kuenenda katika mapito yake.”

    Sheria itatoka Sayuni,

    neno la Bwana litatoka Yerusalemu.

    3 Atahukumu kati ya mataifa mengi,

    na ataamua migogoro ya mataifa

    yenye nguvu na yaliyo mbali.

    Watafua panga zao ziwe majembe,

    na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi.

    Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine,

    wala hawatajifunza vita tena.

    4 Kila mtu ataketi chini ya mzabibu wake

    na chini ya mtini wake,

    wala hakuna mtu atakayewaogopesha,

    kwa kuwa Bwana Mwenye Nguvu Zote amesema.

  58. 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake.

  59. 11 Kuadibishwa wakati wowote hakuonekani kuwa kitu cha kufurahisha bali chenye maumivu kinapotekelezwa. Lakini baadaye huzaa matunda ya haki na amani kwa wale waliofunzwa nayo.