75 Bible Verses About Strength and Courage
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
5 Hakuna mtu yeyote atakayeweza kushindana na wewe siku zote za maisha yako. Kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe, sitakuacha wala sitakupungukia.
6 “Uwe hodari na shujaa, kwa sababu wewe ndiwe utakayewaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa. 7 Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. 8 Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”
-
6 Kuweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu anakwenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.”
7 Kisha Mose akamwita Yoshua na akamwambia mbele ya Israeli wote, “Uwe imara na moyo wa ushujaa, kwa kuwa ni lazima uende na watu hawa katika nchi ile Bwana aliyowaapia baba zao kuwapa, nawe ni lazima uwagawie kama urithi wao. 8 Bwana mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.”
-
8 “Lakini wewe, ee Israeli, mtumishi wangu,
Yakobo, niliyemchagua,
ninyi wazao wa Abrahamu rafiki yangu,
9 nilikuchukua toka miisho ya dunia,
nilikuita kutoka pembe zake za mbali.
Nilisema, ‘Wewe ni mtumishi wangu’;
nimekuchagua, wala sikukukataa.
10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;
usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.
Nitakutia nguvu na kukusaidia;
nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.
11 “Wote walioona hasira dhidi yako
hakika wataaibika na kutahayarika,
wale wakupingao
watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia.
12 Ingawa utawatafuta adui zako,
hutawaona.
Wale wanaopigana vita dhidi yako
watakuwa kama vile si kitu kabisa.
13 Kwa maana Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,
nikushikaye mkono wako wa kuume
na kukuambia, Usiwe na hofu,
nitakusaidia.
14 Usiogope, ee Yakobo uliye mdudu,
ee Israeli uliye mdogo,
kwa kuwa Mimi mwenyewe nitakusaidia,” asema Bwana,
Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
-
28 Je wewe, hufahamu?
Je wewe, hujasikia?
Bwana ni Mungu wa milele,
Muumba wa miisho ya dunia.
Hatachoka wala kulegea,
wala hakuna hata mmoja
awezaye kuupima ufahamu wake.
29 Huwapa nguvu waliolegea
na huongeza nguvu za wadhaifu.
30 Hata vijana huchoka na kulegea,
nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,
31 bali wale wamtumainio Bwana
atafanya upya nguvu zao.
Watapaa juu kwa mbawa kama tai;
watapiga mbio wala hawatachoka,
watatembea kwa miguu wala hawatazimia.
-
10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi. 12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 13 Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara.
-
7 Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. 8 Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.
-
5 Kwa kuwa siku ya shida,
atanihifadhi salama katika maskani yake,
atanificha uvulini mwa hema yake
na kuniweka juu kwenye mwamba.
6 Kisha kichwa changu kitainuliwa
juu ya adui zangu wanaonizunguka.
Katika maskani yake nitatoa dhabihu kwa kelele za shangwe;
nitamwimbia Bwana na kumsifu.
7 Isikie sauti yangu nikuitapo, Ee Bwana,
unihurumie na unijibu.
8 Moyo wangu unasema kuhusu wewe,
“Utafute uso wake!”
Uso wako, Bwana “Nitautafuta.”
9 Usinifiche uso wako,
usimkatae mtumishi wako kwa hasira;
wewe umekuwa msaada wangu.
Usinikatae wala usiniache,
Ee Mungu Mwokozi wangu.
10 Hata kama baba yangu na mama wakiniacha,
Bwana atanipokea.
11 Nifundishe njia yako, Ee Bwana,
niongoze katika njia iliyonyooka
kwa sababu ya watesi wangu.
12 Usiniachilie kwa nia za adui zangu,
kwa maana mashahidi wa uongo
wameinuka dhidi yangu,
wakipumua ujeuri.
13 Nami bado nina tumaini hili:
nitauona wema wa Bwana
katika nchi ya walio hai.
14 Mngojee Bwana,
uwe hodari na mwenye moyo mkuu,
nawe, umngojee Bwana.
-
13 Kesheni, simameni imara katika imani, fanyeni kiume, kuweni mashujaa kuweni hodari. 14 Fanyeni kila kitu katika upendo.
-
11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
-
7 Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.
-
Zaburi ya Daudi.
1 Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
nimhofu nani?
2 Waovu watakaposogea dhidi yangu
ili wanile nyama yangu,
adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia,
watajikwaa na kuanguka.
3 Hata jeshi linizunguke pande zote,
moyo wangu hautaogopa;
hata vita vitokee dhidi yangu,
hata hapo nitakuwa na ujasiri.
-
24 Kuweni hodari na mjipe moyo,
ninyi nyote mnaomtumaini Bwana.
-
20 Daudi pia akamwambia Solomoni mwanawe, “Uwe hodari na moyo mkuu, ukafanye kazi hii. Usiogope wala usifadhaike, kwa maana Bwana aliye Mungu, Mungu wangu yu pamoja nawe. Hatakuacha wala hatakupungukia mpaka kazi hii yote kwa ajili ya utumishi wa Hekalu la Bwana itakapokamilika.
-
11 “Sasa, mwanangu, Bwana awe pamoja nawe, nawe uwe na mafanikio upate kuijenga nyumba ya Bwana Mungu wako, kama alivyosema utafanya. 12 Bwana na akupe hekima na ufahamu wakati atakuweka juu ya Israeli, ili uweze kuishika sheria ya Bwana Mungu wako. 13 Ndipo utakapofanikiwa, ikiwa utakuwa na bidii kutii amri na sheria Bwana alizompa Mose kwa ajili ya Israeli. Uwe hodari na ushujaa. Usiogope wala usikate tamaa.
-
6 Akaweka maafisa wa jeshi juu ya watu, wakawakutanisha mbele yake katika uwanja kwenye lango la mji, naye akawatia moyo kwa maneno haya: 7 “Kuweni hodari na wenye moyo mkuu. Msiogope, msifadhaike wala msikate tamaa kwa sababu ya mfalme wa Ashuru na hili jeshi kubwa lililo pamoja naye, kwa kuwa aliye pamoja nasi ni mkuu kuliko aliye pamoja naye. 8 Kwake uko mkono wa mwili tu, bali kwetu yuko Bwana Mungu wetu kutusaidia na kutupigania vita vyetu.” Nao watu wakatiwa moyo kutokana na maneno aliyowaambia Hezekia mfalme wa Yuda.
-
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Mtindo wa alamothi.
1 Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,
msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
2 Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa
nayo milima ikiangukia moyoni mwa bahari.
3 Hata kama maji yake yatanguruma na kuumuka,
milima nayo ikitetemeka kwa mawimbi yake.
-
1 Ndipo Mose na Waisraeli wakamwimbia Bwana wimbo huu:
“Nitamwimbia Bwana,
kwa kuwa ametukuzwa sana.
Farasi na mpanda farasi
amewatosa baharini.
2 Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu;
amekuwa wokovu wangu.
Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu,
Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.
3 Bwana ni shujaa wa vita;
Bwana ndilo jina lake.
-
2 Hakika Mungu ni wokovu wangu;
nitamtumaini wala sitaogopa.
Bwana, Bwana, ni nguvu zangu na wimbo wangu;
amekuwa wokovu wangu.”
-
33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”
-
26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27 Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.
28 “Mlinisikia nikisema, ‘Ninakwenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngelinipenda mngelifurahi kwa kuwa naenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuniliko mimi. 29 Nimewaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini. 30 Sitasema nanyi zaidi, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu anakuja, naye hana kitu kwangu, 31 lakini ulimwengu upate kujua kuwa ninampenda Baba, nami hufanya vile Baba alivyoniamuru.
“Haya inukeni; twendeni zetu.
-
26 Mwili na moyo wangu vyaweza kushindwa,
bali Mungu ni nguvu ya moyo wangu
na fungu langu milele.
-
5 Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,
“Kamwe sitakuacha,
wala sitakupungukia.”
6 Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,
“Bwana ni msaada wangu; sitaogopa.
Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”
-
14 Kwa sababu hii nampigia Baba magoti, 15 ambaye ubaba wote wa kila jamaa za mbinguni na za duniani unatokana naye. 16 Namwomba Mungu awaimarishe kwa kuwatia nguvu mioyo yenu kwa njia ya Roho wake kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, 17 ili kwamba, Kristo apate kukaa mioyoni mwenu kwa njia ya imani. Nami ninaomba kwamba ninyi mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo, 18 mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Kristo, 19 na kujua upendo huu unaopita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu.
20 Basi kwa yeye awezaye kutenda mambo ya ajabu yasiyopimika kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya uweza wake ule utendao kazi ndani yetu, 21 yeye atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu kwa vizazi vyote, milele na milele. Amen.
-
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Njiwa mkimya wa mbali.” Utenzi wa Daudi. Baada ya kukamatwa na Wafilisti huko Gathi.
1 Ee Mungu unihurumie, maana watu wananifuatia vikali;
mchana kutwa wanazidisha mashambulizi yao.
2 Wasingiziaji wangu wananifuatia mchana kutwa,
wengi wananishambulia kwa kiburi chao.
3 Wakati ninapoogopa,
nitakutumaini wewe.
4 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,
katika Mungu ninatumaini; sitaogopa.
Mwanadamu apatikanaye na kufa,
atanitenda nini?
-
18 Tena yule aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa na kunitia nguvu. 19 Akasema, “Ee mtu upendwaye sana, usiogope. Amani iwe kwako! Uwe na nguvu sasa; jipe nguvu.”
Alipozungumza nami, nilipata nguvu, nikasema, “Nena, bwana wangu, kwa kuwa umenipa nguvu.”
20 Kwa hiyo akasema, “Je, unajua kwa nini nimekujia? Sasa hivi nitarudi kupigana dhidi ya mkuu wa Uajemi, nami nikienda, mkuu wa Uyunani atakuja. 21 Lakini kwanza nitakuambia kile kilichoandikwa katika Kitabu cha Kweli. (Hakuna hata mmoja anayenisaidia dhidi yao isipokuwa Mikaeli, mkuu wenu.
-
6 Kwa hiyo siku zote tunalo tumaini, hata ingawa tunajua kwamba wakati tukiwa katika mwili huu, tuko mbali na Bwana, 7 kwa maana twaenenda kwa imani wala si kwa kuona. 8 Naam, tunalo tumaini na ingekuwa bora zaidi kuuacha mwili huu na kwenda kukaa na Bwana.
-
24 Walipokuwa wamewaleta hawa wafalme kwa Yoshua, akawaita watu wote wa Israeli, na kuwaambia majemadari wa vita waliokwenda pamoja naye, “Njooni hapa mweke nyayo zenu juu ya shingo za hawa wafalme.” Basi wakaja wakaweka nyayo zao shingoni.
25 Yoshua akawaambia, “Msiogope, wala msivunjike moyo. Kuweni hodari na wenye ushujaa. Hili ndilo Bwana atakalowatendea adui zenu wote mnaokwenda kupigana nao.”
-
8 Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda.
9 Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa;
waambieni matendo yake yote ya ajabu.
10 Lishangilieni jina lake takatifu;
mioyo ya wale wamtafutao Bwana na ifurahi.
11 Mtafuteni Bwana na nguvu zake;
utafuteni uso wake siku zote.
12 Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya,
miujiza yake na hukumu alizozitamka,
13 enyi wazao wa Israeli mtumishi wake,
enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
-
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi mtumishi wa Bwana aliyomwimbia Bwana wakati Bwana alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na pia mkononi mwa Sauli. Alisema hivi:
1 Nakupenda wewe, Ee Bwana,
nguvu yangu.
2 Bwana ni mwamba wangu,
ngome yangu na mwokozi wangu,
Mungu wangu ni mwamba,
ambaye kwake ninakimbilia.
Yeye ni ngao yangu na pembe ya wokovu wangu,
ngome yangu.
-
7 Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu,
moyo wangu umemtumaini yeye,
nami nimesaidiwa.
Moyo wangu unarukaruka kwa furaha
nami nitamshukuru kwa wimbo.
8 Bwana ni nguvu ya watu wake,
ngome ya wokovu kwa mpakwa mafuta wake.
-
28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. 29 Maana wale Mungu aliowajua tangu mwanzo, pia aliwachagua tangu mwanzo, wapate kufanana na mfano wa Mwanawe, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. 30 Nao wale Mungu aliotangulia kuwachagua, akawaita, wale aliowaita pia akawahesabia haki, nao wale aliowahesabia haki, pia akawatukuza.
31 Tuseme nini basi kuhusu haya? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, ni nani awezaye kuwa kinyume chetu? 32 Ikiwa Mungu hakumhurumia Mwanawe, bali alimtoa kwa ajili yetu sote, atakosaje basi kutupatia vitu vyote kwa ukarimu pamoja naye?
-
10 Nehemia akasema, “Nendeni mkafurahie chakula kizuri na vinywaji vitamu, na mpeleke sehemu kwa wale ambao hawana chochote cha kula. Siku hii ni takatifu kwa Bwana. Msihuzunike, kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu.”
-
Zaburi ya Daudi.
1 Bwana ndiye mchungaji wangu,
sitapungukiwa na kitu.
2 Hunilaza katika malisho
ya majani mabichi,
kando ya maji matulivu huniongoza,
3 hunihuisha nafsi yangu.
Huniongoza katika njia za haki
kwa ajili ya jina lake.
4 Hata kama nikipita katikati
ya bonde la uvuli wa mauti,
sitaogopa mabaya,
kwa maana wewe upo pamoja nami;
fimbo yako na mkongojo wako
vyanifariji.
-
19 kwa maana ninajua kwamba kwa maombi yenu na kwa msaada unaotolewa na Roho wa Yesu Kristo, yale yaliyonipata mimi yatageuka kuwa wokovu wangu. 20 Ninatarajia kwa shauku kubwa na kutumaini kwamba sitaaibika kwa njia yoyote, bali nitakuwa na ujasiri wa kutosha ili sasa kama wakati mwingine wowote, Kristo atukuzwe katika mwili wangu, ikiwa ni kwa kuishi au kwa kufa. 21 Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.
-
11 Ukuu na uweza, ni vyako, Ee Bwana,
na utukufu na enzi na uzuri,
kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani
ni chako wewe.
Ee Bwana, ufalme ni wako;
umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote.
12 Utajiri na heshima vyatoka kwako;
wewe ndiwe utawalaye vitu vyote.
Mikononi mwako kuna nguvu na uweza
ili kuinua na kuwapa wote nguvu,
-
15 Ndugu wa huko Rumi waliposikia habari zetu, walikuja mpaka Soko la Apio na mahali paitwapo Mikahawa Mitatu kutulaki. Paulo alipowaona, alimshukuru Mungu akatiwa moyo.
-
13 Hakuna jaribu lolote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu; hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kutokea ili mweze kustahimili.
-
6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.
-
25 Mwishoni mwa siku arobaini wakarudi kutoka kuipeleleza nchi.
26 Wakarudi kwa Mose, Aroni na jumuiya yote ya Waisraeli huko Kadeshi kwenye Jangwa la Parani. Hapo ndipo walipotoa habari kwao na kwa kusanyiko lote na kuwaonyesha matunda ya hiyo nchi. 27 Wakampa Mose taarifa hii: “Tuliingia katika nchi uliyotutuma, nayo inatiririka maziwa na asali! Hili hapa tunda lake. 28 Lakini watu wanaoishi huko ni wenye nguvu, na miji yao ina ngome na ni mikubwa sana. Huko tuliona hata wazao wa Anaki. 29 Waamaleki wanaishi Negebu; Wahiti, Wayebusi na Waamori wanaishi katika nchi ya vilima; nao Wakanaani wanaishi karibu na bahari na kando ya Yordani.”
30 Kisha Kalebu akawanyamazisha watu mbele ya Mose na kusema, “Imetupasa kupanda na kuimiliki nchi, kwa maana hakika tunaweza kufanya hivyo.”
31 Lakini watu waliokuwa wamepanda pamoja naye wakasema, “Hatuwezi kuwashambulia wale watu; wana nguvu kutuliko sisi.” 32 Wakaeneza taarifa mbaya miongoni mwa Waisraeli kuhusu nchi waliyoipeleleza. Wakasema, “Nchi tuliyoipeleleza hula watu waishio ndani yake. Watu wote tuliowaona huko ni majitu. 33 Tuliwaona Wanefili huko (wazao wa Anaki wanatokana na Wanefili.) Tulijiona kama panzi machoni petu wenyewe, nao ndivyo walivyotuona.”
-
22 Hivyo Mose akaandika wimbo huu siku ile na akawafundisha Waisraeli.
23 Bwana akampa Yoshua mwana wa Nuni agizo hili: “Uwe hodari na shujaa, kwa kuwa utawaleta Waisraeli katika nchi niliyowaahidi kwa kiapo, nami mwenyewe nitakuwa pamoja nawe.”
-
16 Ndipo wakamjibu Yoshua, “Chochote ambacho umetuagiza tutafanya na popote utakapotutuma tutakwenda. 17 Kama vile tulivyomtii Mose kikamilifu, ndivyo tutakavyokutii wewe. Bwana Mungu wako na awe pamoja nawe tu kama vile alivyokuwa pamoja na Mose. 18 Yeyote atakayeasi neno lako na kuacha kuyatii maneno yako, au chochote utakachowaamuru, atauawa. Uwe imara na hodari tu!”
-
19 Bwana Mwenyezi ni nguvu yangu;
huifanya miguu yangu kama miguu ya ayala,
huniwezesha kupita juu ya vilima.
Kwa kiongozi wa uimbaji. Kwa vinanda vyangu vya nyuzi.
-
27 Lakini lolote litakalotukia, mwenende kama ipasavyo Injili ya Kristo, ili kwamba nikija na kuwaona au ikiwa sipo, nipate kusikia haya juu yenu: Kuwa mnasimama imara katika roho moja, mkiishindania imani ya Injili kwa umoja, 28 wala msitishwe na wale wanaowapinga. Hii ni ishara kwao kuwa wataangamia, lakini ninyi mtaokolewa, na hii ni kazi ya Mungu.
-
41 Wakati ule ule, yule Mfilisti, akiwa na mbeba ngao wake mbele yake, akaendelea kujongea karibu na Daudi. 42 Mfilisti akamwangalia Daudi kote na kumwona kuwa ni kijana tu, mwekundu na mzuri wa kupendeza, naye akamdharau. 43 Akamwambia Daudi, “Je, mimi ni mbwa, hata unanijia na fimbo?” Yule Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake. 44 Tena Mfilisti akamwambia, “Njoo hapa, nami nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni nyama yako.”
45 Daudi akamwambia yule Mfilisti. “Wewe unanijia na upanga, mkuki na fumo, lakini mimi ninakujia kwa jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa majeshi ya Israeli, ambaye wewe umemtukana. 46 Siku hii leo Bwana atakutia mkononi mwangu, nami nitakupiga na kukukata kichwa chako. Leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya jeshi la Wafilisti, nayo dunia yote itajua kuwa yuko Mungu katika Israeli. 47 Wale wote waliokusanyika hapa watajua kuwa Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; kwa kuwa vita ni vya Bwana, naye atawatia wote mikononi mwetu.”
-
1 Mtu mwovu hukimbia ingawa hakuna yeyote anayemfukuza,
bali wenye haki ni wajasiri kama simba.
-
18 Kisha wakawaita tena ndani na kuwaamuru wasiseme wala kufundisha kamwe kwa hili jina la Yesu.
19 Lakini Petro na Yohana wakajibu, “Amueni ninyi wenyewe iwapo ni haki mbele za Mungu kuwatii ninyi kuliko kumtii Mungu. 20 Lakini sisi hatuwezi kuacha kusema yale tuliyoyaona na kuyasikia.”
-
9 Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.
10 Nanyi mkiisha kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Kristo, yeye mwenyewe atawarejesha na kuwatia nguvu, akiwaimarisha na kuwathibitisha.
-
12 Ee Mungu wetu, je, wewe hutawahukumu? Kwa kuwa sisi hatuna uwezo wa kukabiliana na jeshi hili kubwa linalokuja kutushambulia. Sisi hatujui la kufanya, bali macho yetu yanakutazama wewe.”
13 Watu wote wa Yuda pamoja na wake zao, watoto wao na wadogo wao wakasimama pale mbele za Bwana.
14 Ndipo Roho wa Bwana akaja juu ya mtu mmoja jina lake Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, Mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi mzao wa Asafu alipokuwa amesimama katika kusanyiko.
15 Akasema: “Sikilizeni, enyi Yuda wote nanyi nyote mkaao Yerusalemu, nawe Mfalme Yehoshafati! Hili ndilo Bwana asemalo kwenu, ‘Msiogope wala msifadhaike kwa sababu ya jeshi hili kubwa. Kwa maana vita hivi si vyenu, bali ni vya Mungu. 16 Kesho shukeni kukabiliana nao. Watakwea kwa kupandia Genge la Sisi, nanyi mtawakuta mwisho wa bonde, kabla ya Jangwa la Yerueli. 17 Hamtahitaji kupigana vita hivi. Kaeni kwenye nafasi zenu, simameni imara na mkaone wokovu Bwana atakaowapatia, enyi Yuda na Yerusalemu. Msiogope, wala msifadhaike. Kesho tokeni mwende mkawakabili, naye Bwana atakuwa pamoja nanyi.’ ”
-
3 Nilipoita, ulinijibu;
ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari.
4 Wafalme wote wa dunia wakusifu wewe Ee Bwana,
wakati wanaposikia maneno ya kinywa chako.
-
16 Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, hatuhitaji kujitetea mbele zako kuhusu jambo hili. 17 Ikiwa tutatupwa ndani ya tanuru iwakayo moto, Mungu tunayemtumikia anaweza kutuokoa na moto, naye atatuokoa kutoka mkononi mwako, ee mfalme. 18 Lakini hata ikiwa hatatuokoa, ee mfalme, tunataka ufahamu kwamba, hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”
-
26 “Kwa hiyo msiwaogope hao, kwa maana hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna siri ambayo haitajulikana. 27 Ninalowaambia gizani, ninyi lisemeni mchana peupe. Na lile mnalosikia likinongʼonwa masikioni mwenu, lihubirini juu ya nyumba. 28 Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuua roho. Afadhali mwogopeni yeye awezaye kuiangamiza roho na mwili katika jehanamu. 29 Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti moja tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka chini pasipo Baba yenu kujua. 30 Hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. 31 Hivyo msiogope; kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.
-
5 Kesho yake, viongozi wa Kiyahudi, wazee na walimu wa sheria wakakusanyika Yerusalemu. 6 Walikuwepo kuhani mkuu Anasi, Kayafa, Yohana, Iskanda, na wengi wa jamaa ya kuhani mkuu. 7 Baada ya kuwasimamisha Petro na Yohana katikati yao, wakawauliza, “Ni kwa uwezo gani au kwa jina la nani mmefanya jambo hili?”
8 Petro, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akajibu, “Enyi watawala na wazee wa watu, 9 kama leo tukihojiwa kwa habari ya mambo mema aliyotendewa yule kiwete na kuulizwa jinsi alivyoponywa, 10 ijulikane kwenu nyote na kwa watu wote wa Israeli kwamba: Ni kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulubisha lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama mbele yenu akiwa mzima kabisa. 11 Huyu ndiye
“ ‘jiwe ambalo ninyi wajenzi mlilikataa,
ambalo limekuwa jiwe kuu la pembeni.’
12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”
-
11 Usiku uliofuata, Bwana akasimama karibu naye akamwambia, “Jipe moyo! Kama vile ulivyonishuhudia hapa Yerusalemu, hivyo imekupasa kunishuhudia huko Rumi pia.”
-
1 Siku zilipokaribia za Daudi kufa, akampa mwanawe Solomoni agizo.
2 Akasema, “Mimi ninakaribia kwenda njia ya dunia yote. Hivyo uwe hodari, jionyeshe kuwa mwanaume, 3 shika lile Bwana Mungu wako analokuagiza: Enenda katika njia zake, ushike maagizo na amri zake, sheria zake na kanuni zake, kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Mose, ili upate kustawi katika yote ufanyayo na popote uendako,
-
11 Bwana huwapa watu wake nguvu;
Bwana huwabariki watu wake kwa kuwapa amani.
-
17 “Ee Bwana Mwenyezi, umeumba mbingu na nchi kwa uwezo wako mkuu na kwa mkono ulionyooshwa. Hakuna jambo lililo gumu usiloliweza. 18 Wewe huonyesha upendo kwa maelfu, lakini huleta adhabu kwa ajili ya dhambi za baba mapajani mwa watoto wao baada yao. Ee Mungu mkuu na mwenye uweza, ambaye jina lako ni Bwana Mwenye Nguvu Zote, 19 makusudi yako ni makuu, na matendo yako ni yenye uwezo. Macho yako yanaona njia zote za wanadamu, nawe humlipa kila mmoja kulingana na mwenendo wake, na kama yanavyostahili matendo yake. 20 Ulitenda ishara za miujiza na maajabu huko Misri, na umeyaendeleza mpaka leo, katika Israeli na miongoni mwa wanadamu wote, nawe umejulikana na kufahamika hivyo mpaka leo. 21 Uliwatoa watu wako Israeli kutoka Misri kwa ishara na maajabu, kwa mkono wenye nguvu na ulionyooshwa na kwa matisho makuu. 22 Uliwapa nchi hii uliyokuwa umeapa kuwapa baba zao, nchi inayotiririka maziwa na asali.
-
22 Mara Yesu akawaambia wanafunzi wake waingie kwenye mashua watangulie kwenda ngʼambo ya bahari, wakati yeye alikuwa akiwaaga wale makutano. 23 Baada ya kuwaaga, akaenda zake mlimani peke yake kuomba. Jioni ilipofika, Yesu alikuwa huko peke yake. 24 Wakati huo ile mashua ilikuwa mbali kutoka nchi kavu ikisukwasukwa na mawimbi, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho.
25 Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea wanafunzi wake akiwa anatembea juu ya maji. 26 Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji, waliingiwa na hofu kuu, wakasema, “Ni mzimu.” Wakapiga yowe kwa kuogopa.
27 Lakini mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope.”
-
11 Yeyote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Yeyote ahudumuye hana budi kuhudumu kwa nguvu zile anazopewa na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kwa njia ya Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye milele na milele. Amen.
-
28 Nafsi yangu imechakazwa kwa huzuni,
uniimarishe sawasawa na neno lako.
-
10 Jina la Bwana ni ngome imara,
wenye haki huikimbilia na kuwa salama.
-
43 Yosefu wa Arimathaya, mtu aliyeheshimiwa katika Baraza, na ambaye alikuwa anautarajia Ufalme wa Mungu, akamwendea Pilato kwa ujasiri na kumwomba mwili wa Yesu.
-
17 Lakini Bwana alisimama upande wangu akanitia nguvu, ili kupitia kwangu lile Neno lihubiriwe kwa ukamilifu, watu wote Mataifa wapate kulisikia. Mimi niliokolewa kutoka kinywa cha simba.
-
6 “Kuweni hodari sana, kuweni waangalifu kutii yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Sheria ya Mose, pasipo kugeuka upande wa kuume au kushoto. 7 Msishirikiane na mataifa yaliyobakia katikati yenu, wala msiombe kwa majina ya miungu yao au kuapa kwayo. Msiitumikie wala kuisujudia. 8 Bali mtashikamana kwa uthabiti na Bwana, Mungu wenu, kama vile ambavyo mmefanya mpaka sasa.
-
14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.
-
13 Uwe hodari na tupigane kwa ujasiri kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu. Bwana atafanya lile lililo jema machoni pake.”
-
17 Wenye haki hulia, naye Bwana huwasikia,
huwaokoa katika taabu zao zote.
18 Bwana yu karibu na waliovunjika moyo,
na huwaokoa waliopondeka roho.
19 Mwenye haki ana mateso mengi,
lakini Bwana humwokoa nayo yote,
20 huhifadhi mifupa yake yote,
hata mmoja hautavunjika.
21 Ubaya utamuua mtu mwovu,
nao adui za mwenye haki watahukumiwa.
22 Bwana huwakomboa watumishi wake,
yeyote anayemkimbilia yeye
hatahukumiwa kamwe.
-
14 Bwana ni nguvu yangu na wimbo wangu,
yeye amefanyika wokovu wangu.
-
14 Je, ujasiri wako utadumu au mikono yako itakuwa na nguvu siku hiyo nitakapokushughulikia? Mimi Bwana nimesema na nitalifanya.
-
25 “Pamoja na jeshi kubwa atachochea nguvu zake na ushujaa wake dhidi ya mfalme wa Kusini. Mfalme wa Kusini atafanya vita na jeshi lenye nguvu sana, lakini hataweza kusimama kwa sababu ya kwa hila zilizofanywa dhidi yake.
-
35 Ee Mungu, wewe unatisha katika mahali patakatifu pako,
Mungu wa Israeli huwapa watu wake uwezo na nguvu.
Mungu Asifiwe!
-
6 Bwana yuko pamoja nami, sitaogopa.
Mwanadamu anaweza kunitenda nini?
-
10 Ukikata tamaa wakati wa taabu,
jinsi gani nguvu zako ni kidogo!
-
22 Sasa ninawasihi sana, jipeni moyo mkuu kwa kuwa hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza maisha yake, ila meli itaangamia. 23 Jana usiku, malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake na ambaye ninamwabudu alisimama karibu nami, 24 naye akasema, ‘Paulo usiogope, kwa kuwa ni lazima usimame mbele ya Kaisari, naye Mungu amekupa kwa neema uhai wa wote wanaosafiri pamoja nawe. 25 Hivyo jipeni moyo, enyi watu, kwa kuwa ninamwamini Mungu kwamba yatakuwa kama vile alivyoniambia.’ 26 Lakini hata hivyo meli yetu itakwama kwenye kisiwa fulani.”
-
16 Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. 17 Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi, 18 kwa sababu hatuangalii yale yanayoweza kuonekana bali yale yasiyoweza kuonekana. Kwa maana yale yanayoweza kuonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoweza kuonekana ni ya milele.
-
9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa.
Shows Read in context, Share and Copy.