43 Bible Verses About Discouragement

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Discouragement
  1. 28 Je wewe, hufahamu?

    Je wewe, hujasikia?

    Bwana ni Mungu wa milele,

    Muumba wa miisho ya dunia.

    Hatachoka wala kulegea,

    wala hakuna hata mmoja

    awezaye kuupima ufahamu wake.

    29 Huwapa nguvu waliolegea

    na huongeza nguvu za wadhaifu.

    30 Hata vijana huchoka na kulegea,

    nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,

    31 bali wale wamtumainio Bwana

    atafanya upya nguvu zao.

    Watapaa juu kwa mbawa kama tai;

    watapiga mbio wala hawatachoka,

    watatembea kwa miguu wala hawatazimia.

  2. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”

  3. 31 Tuseme nini basi kuhusu haya? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, ni nani awezaye kuwa kinyume chetu? 32 Ikiwa Mungu hakumhurumia Mwanawe, bali alimtoa kwa ajili yetu sote, atakosaje basi kutupatia vitu vyote kwa ukarimu pamoja naye? 33 Ni nani atakayewashtaki wale ambao Mungu amewateua? Ni Mungu mwenyewe ndiye mwenye kuwahesabia haki. 34 Ni nani basi atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu aliyekufa, naam, zaidi ya hayo, aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, yuko mkono wa kuume wa Mungu, naye pia anatuombea. 35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga? 36 Kama ilivyoandikwa:

    “Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;

    tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.”

    37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

  4. 1 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia. 2 Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Naenda kuwaandalia makao. 3 Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo.

  5. 6 Katika hili mnafurahi sana, ingawa sasa kwa kitambo kidogo mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna nyingi. 7 Haya yamewajia ili kwamba imani yenu, iliyo ya thamani kuliko dhahabu ipoteayo, ingawa hujaribiwa kwa moto, ionekane kuwa halisi na imalizie katika sifa, utukufu na heshima wakati Yesu Kristo atadhihirishwa. 8 Ingawa hamjamwona, mnampenda; tena ingawa sasa hammwoni, mnamwamini na kujawa na furaha isiyoneneka yenye utukufu usioelezeka. 9 Maana mnaupokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu.

  6. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

  7. 28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.

  8. 13 Hakuna jaribu lolote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu; hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kutokea ili mweze kustahimili.

  9. 21 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

  10. 9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa.

  11. 4 Waisraeli wakasafiri kutoka mlima Hori kupitia njia inayoelekea Bahari ya Shamu, kuizunguka Edomu. Lakini watu wakakosa uvumilivu njiani, 5 wakamnungʼunikia Mungu na Mose, wakisema, “Kwa nini umetupandisha kutoka Misri ili tufe jangwani? Hakuna mkate! Hakuna maji! Nasi tunachukia sana chakula hiki duni!”

  12. 10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;

    usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.

    Nitakutia nguvu na kukusaidia;

    nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.

    11 “Wote walioona hasira dhidi yako

    hakika wataaibika na kutahayarika,

    wale wakupingao

    watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia.

    12 Ingawa utawatafuta adui zako,

    hutawaona.

    Wale wanaopigana vita dhidi yako

    watakuwa kama vile si kitu kabisa.

    13 Kwa maana Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,

    nikushikaye mkono wako wa kuume

    na kukuambia, Usiwe na hofu,

    nitakusaidia.

    14 Usiogope, ee Yakobo uliye mdudu,

    ee Israeli uliye mdogo,

    kwa kuwa Mimi mwenyewe nitakusaidia,” asema Bwana,

    Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

  13. 3 Mwanzi uliopondeka hatauvunja,

    na utambi unaofuka moshi hatauzima.

    Kwa uaminifu ataleta haki,

    4 hatazimia roho wala kukata tamaa,

    mpaka atakaposimamisha haki juu ya dunia.

    Visiwa vitaweka tumaini lao katika sheria yake.”

  14. 29 Ndipo nikawaambia, “Msihofu, wala msiwaogope. 30 Bwana Mungu wenu anayewatangulia, atawapigania, kama alivyofanya kwa ajili yenu huko Misri, mbele ya macho yenu hasa, 31 na pia huko jangwani. Huko mliona jinsi Bwana Mungu wenu alivyowachukua, kama baba amchukuavyo mwanawe, katika njia yote mliyoiendea mpaka mkafika mahali hapa.”

  15. 8 Bwana mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.”

  16. 15 Akasema: “Sikilizeni, enyi Yuda wote nanyi nyote mkaao Yerusalemu, nawe Mfalme Yehoshafati! Hili ndilo Bwana asemalo kwenu, ‘Msiogope wala msifadhaike kwa sababu ya jeshi hili kubwa. Kwa maana vita hivi si vyenu, bali ni vya Mungu.

  17. 6 Mungu wangu.

    Nafsi yangu inasononeka ndani yangu;

    kwa hiyo nitakukumbuka

    kutoka nchi ya Yordani,

    katika vilele vya Hermoni,

    kutoka Mlima Mizari.

    7 Kilindi huita kilindi,

    katika ngurumo za maporomoko ya maji yako;

    mawimbi yako yote pamoja na viwimbi

    vimepita juu yangu.

    8 Mchana Bwana huelekeza upendo wake,

    usiku wimbo wake uko nami:

    maombi kwa Mungu wa uzima wangu.

    9 Ninamwambia Mungu Mwamba wangu,

    “Kwa nini umenisahau?

    Kwa nini niendelee kuomboleza,

    nikiwa nimeonewa na adui?”

    10 Mifupa yangu inateseka kwa maumivu makali

    adui zangu wanaponidhihaki,

    wakiniambia mchana kutwa,

    “Yuko wapi Mungu wako?”

    11 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka?

    Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu?

    Weka tumaini lako kwa Mungu,

    kwa sababu bado nitamsifu,

    Mwokozi wangu na Mungu wangu.

  18. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.

  19. 6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.

    8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza.

  20. 10 Kisha yule Mfilisti akasema, “Siku hii ya leo nayatukana majeshi ya Israeli! Nipeni mtu tupigane.” 11 Kwa kusikia maneno ya Wafilisti, Sauli na Waisraeli wote wakafadhaika na kuogopa.

  21. 7 “Kuweni hodari na wenye moyo mkuu. Msiogope, msifadhaike wala msikate tamaa kwa sababu ya mfalme wa Ashuru na hili jeshi kubwa lililo pamoja naye, kwa kuwa aliye pamoja nasi ni mkuu kuliko aliye pamoja naye.

  22. 9 Ee Bwana unihurumie, kwa kuwa niko kwenye shida;

    macho yangu yanafifia kwa huzuni,

    nafsi yangu na mwili wangu kwa sikitiko.

    10 Maisha yangu yamedhoofika kwa majonzi,

    naam, miaka yangu kwa kulia kwa maumivu makali;

    nguvu zangu zinaisha kwa ajili ya mateso,

    na mifupa yangu inachakaa.

    11 Kwa sababu ya adui zangu wote,

    nimedharauliwa kabisa na jirani zangu,

    hata kwa rafiki zangu nimekuwa tisho,

    wale wanionao barabarani hunikimbia.

    12 Nimesahaulika miongoni mwao kama mtu aliyekufa,

    nimekuwa kama chombo cha mfinyanzi kilichovunjika.

  23. 17 Wenye haki hulia, naye Bwana huwasikia,

    huwaokoa katika taabu zao zote.

    18 Bwana yu karibu na waliovunjika moyo,

    na huwaokoa waliopondeka roho.

    19 Mwenye haki ana mateso mengi,

    lakini Bwana humwokoa nayo yote,

  24. 22 Mtwike Bwana fadhaa zako,

    naye atakutegemeza,

    hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke.

  25. 16 Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. 17 Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi, 18 kwa sababu hatuangalii yale yanayoweza kuonekana bali yale yasiyoweza kuonekana. Kwa maana yale yanayoweza kuonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoweza kuonekana ni ya milele.

  26. 5 Kwa maana hata tulipoingia Makedonia, miili yetu haikuwa na raha. Tulisumbuliwa kila upande, kwa nje kulikuwa na mapigano na mioyoni mwetu tulikuwa na hofu. 6 Bali Mungu, yeye awafarijie wenye huzuni, alitufariji kwa kufika kwake Tito. 7 Lakini si kule kuja kwa Tito tu, bali pia kwa faraja mliyompa. Alitueleza jinsi mlivyonionea shauku, huzuni yenu kubwa na juhudi yenu kwa ajili yangu, ili kwamba furaha yangu ipate kuwa kubwa kuliko wakati wowote.

  27. 13 Kwa hiyo, nawaomba msikate tamaa kwa sababu ya mateso yangu kwa ajili yenu, hayo ni utukufu wenu.

  28. 4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! 5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

  29. 19 Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu.

  30. 8 Nami nitawaleta mpaka nchi niliyoapa kwa mkono ulioinuliwa kumpa Abrahamu, Isaki na Yakobo. Nitawapa iwe milki yenu. Mimi ndimi Bwana.’ ”

    9 Mose akawaarifu Waisraeli jambo hili, lakini hawakumsikiliza kwa sababu ya maumivu makuu ya moyoni na utumwa wa kikatili.

  31. 6 Kuweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu anakwenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.”

  32. 13 Nami bado nina tumaini hili:

    nitauona wema wa Bwana

    katika nchi ya walio hai.

    14 Mngojee Bwana,

    uwe hodari na mwenye moyo mkuu,

    nawe, umngojee Bwana.

  33. 3 Nilipoita, ulinijibu;

    ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari.

  34. 5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote

    wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

    6 katika njia zako zote mkiri yeye,

    naye atayanyoosha mapito yako.

  35. 1 Akiwa ndani ya tumbo la nyangumi, Yona alimwomba Bwana Mungu wake. 2 Akasema:

    “Katika shida yangu nalimwita Bwana,

    naye akanijibu.

    Kutoka kina cha kaburi niliomba msaada,

    nawe ukasikiliza kilio changu.

  36. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.

  37. 21 Wakahubiri habari njema katika mji huo na kupata wanafunzi wengi. Kisha wakarudi Listra, Ikonio na Antiokia, 22 wakiwaimarisha wanafunzi na kuwatia moyo waendelee kudumu katika imani. Wakawaonya wakisema, “Imetupasa kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa kupitia katika taabu nyingi.”

  38. 11 Ninatamani sana kuwaona ili nipate kuweka juu yenu karama za rohoni ili mwe imara, 12 au zaidi, ninyi pamoja nami tuweze kutiana moyo katika imani sisi kwa sisi.

  39. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.

  40. 13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

  41. 58 Kwa hiyo, ndugu zangu wapenzi, simameni imara, msitikisike, mzidi sana katika kuitenda kazi ya Bwana, kwa maana mnajua ya kuwa, kazi yenu katika Bwana si bure.

  42. 11 Kwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa.

  43. 3 Mtafakarini sana yeye aliyestahimili upinzani mkuu namna hii kutoka kwa watu wenye dhambi, ili kwamba msije mkachoka na kukata tamaa.