91 Bible Verses About Preaching

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Preaching
  1. 1 Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake, kwamba: 2 Hubiri Neno; kuwa tayari wakati ufaao na wakati usiofaa; karipia, kemea na utie moyo kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri. 3 Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima. Badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe, watajikusanyia idadi kubwa ya walimu wapate kuwaambia yale ambayo masikio yao yanayowasha yanatamani kuyasikia. 4 Watakataa kusikiliza kweli na kuzigeukia hadithi za uongo. 5 Kwa habari yako wewe, vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiza wajibu wote wa huduma yako.

  2. 21 Kwa kuwa katika hekima ya Mungu, ulimwengu kwa hekima yake haukumjua yeye, ilimpendeza Mungu kuwaokoa wale walioamini kwa upuzi wa lile neno lililohubiriwa. 22 Wayahudi wanadai ishara za miujiza na Wayunani wanatafuta hekima. 23 Lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa: yeye kwa Wayahudi ni kikwazo na kwa Wayunani ni upuzi. 24 Lakini kwa wale ambao Mungu amewaita, Wayahudi na pia Wayunani, Kristo ndiye nguvu ya Mungu na pia hekima ya Mungu. 25 Kwa maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi kuliko hekima ya wanadamu, nao udhaifu wa Mungu una nguvu kuliko nguvu ya wanadamu.

  3. 18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”

  4. 13 Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.”

    14 Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? 15 Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri habari njema!”

  5. 4 Kwa hiyo wale waliotawanyika wakalihubiri neno la Mungu kila mahali walipokwenda. 5 Filipo akateremkia mji mmoja wa Samaria akawahubiria habari za Kristo 6 Watu walipomsikia Filipo na kuona ishara na miujiza aliyofanya, wakasikiliza kwa bidii yale aliyosema. 7 Pepo wachafu wakawa wakiwatoka watu wengi huku wakipiga kelele na wengi waliopooza na viwete wakaponywa. 8 Hivyo pakawa na furaha kuu katika mji huo.

    9 Basi mtu mmoja jina lake Simoni alikuwa amefanya uchawi kwa muda mrefu katika mji huo akiwashangaza watu wote wa Samaria. Alijitapa kwamba yeye ni mtu mkuu, 10 nao watu wote wakubwa kwa wadogo wakamsikiliza na kumaka, wakisema “Mtu huyu ndiye uweza wa Mungu ujulikanao kama ‘Uweza Mkuu.’ ” 11 Wakamfuata kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake. 12 Lakini watu walipomwamini Filipo alipohubiri habari njema za Ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, wakabatizwa wanaume na wanawake. 13 Simoni naye akaamini na akabatizwa. Akamfuata Filipo kila mahali, akistaajabishwa na ishara kuu na miujiza aliyoiona.

  6. 1 Ndugu zangu nilipokuja kwenu, sikuja na maneno ya ushawishi wala hekima ya hali ya juu nilipowahubiria siri ya Mungu. 2 Kwa kuwa niliamua kutokujua kitu chochote wakati nikiwa nanyi isipokuwa Yesu Kristo aliyesulubiwa. 3 Mimi nilikuja kwenu nikiwa dhaifu na mwenye hofu na kwa kutetemeka sana. 4 Kuhubiri kwangu na ujumbe wangu haukuwa kwa hekima na maneno ya ushawishi bali kwa madhihirisho ya nguvu za Roho 5 ili imani yenu isiwe imejengwa katika hekima ya wanadamu bali katika nguvu za Mungu.

  7. 15 Akawaambia, “Enendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. 16 Yeyote aaminiye na kubatizwa ataokoka. Lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa. 17 Nazo ishara hizi zitafuatana na wanaoamini: Kwa Jina langu watatoa pepo wachafu; watasema kwa lugha mpya; 18 watashika nyoka kwa mikono yao; na hata wakinywa kitu chochote cha kuua, hakitawadhuru kamwe; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona.”

    19 Baada ya Bwana Yesu kusema nao, alichukuliwa juu mbinguni na kuketi mkono wa kuume wa Mungu.

  8. 1 Yesu kisha akawaita wale kumi na wawili pamoja, akawapa mamlaka na uwezo wa kutoa pepo wachafu wote na kuponya magonjwa yote, 2 kisha akawatuma waende wakahubiri Ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa. 3 Akawaagiza akisema, “Msichukue chochote safarini: sio fimbo, wala mkoba, wala mkate, wala fedha, hata msichukue kanzu ya ziada. 4 Katika nyumba yoyote mwingiayo, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo. 5 Kama watu wasipowakaribisha, mnapoondoka katika mji wao, kungʼuteni mavumbi kutoka kwenye miguu yenu ili kuwa ushuhuda dhidi yao.” 6 Hivyo wale wanafunzi wakaondoka wakaenda kutoka kijiji hadi kijiji, wakihubiri habari njema na kuponya wagonjwa kila mahali.

  9. 33 Basi ikiwa yeye ametukuzwa kwa mkono wa kuume wa Mungu, amepokea kutoka kwa Baba ahadi ya Roho Mtakatifu, naye amemimina kile mnachoona sasa na kusikia. 34 Kwa kuwa Daudi hakupaa kwenda mbinguni, lakini anasema,

    “ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:

    “Keti mkono wangu wa kuume,

    35 hadi nitakapowaweka adui zako

    chini ya miguu yako.” ’

    36 “Kwa hiyo Israeli wote na wajue jambo hili kwa uhakika kwamba: Mungu amemfanya huyu Yesu, ambaye ninyi mlimsulubisha, kuwa Bwana na Kristo.”

    37 Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”

    38 Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. 39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu, na kwa wote walio mbali, na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”

    40 Petro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.” 41 Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa na siku ile waliongezeka watu wapatao 3,000.

  10. 1 Ndugu zangu, kwa kuwa ninyi wenyewe mnajua ya kwamba kuja kwetu kwenu hakukuwa bure, 2 kama vile mjuavyo, tulikuwa tumeteswa na kutukanwa huko Filipi, lakini hata hivyo, kwa msaada wa Mungu wetu, tulikuwa na ujasiri wa kuwaambia Injili ya Mungu ingawa kulikuwa na upinzani mkubwa. 3 Kwa maana himizo letu halikutokana na hila wala nia mbaya au udanganyifu. 4 Kinyume chake, tulinena kama watu tuliokubaliwa na Mungu tukakabidhiwa Injili. Sisi hatujaribu kuwapendeza wanadamu bali kumpendeza Mungu, yeye ayachunguzaye mawazo ya ndani sana ya mioyo yetu. 5 Kama mjuavyo, hatukuja kwenu kwa maneno ya kujipendekeza au maneno yasiyo ya kweli ili kuficha tamaa mbaya: Mungu ndiye shahidi yetu. 6 Wala hatukuwa tunatafuta sifa kutoka kwa wanadamu, wala kutoka kwenu au kwa mtu mwingine awaye yote.

    Kama mitume wa Kristo tungaliweza kuwa mzigo kwenu, 7 lakini tulikuwa wapole katikati yenu, kama mama anayewatunza watoto wake wadogo. 8 Tuliwapenda sana kiasi kwamba tulifurahia kushirikiana nanyi, si Injili ya Mungu tu, bali hata maisha yetu, kwa sababu mlikuwa wa thamani mno kwetu. 9 Ndugu zetu, mnakumbuka juhudi yetu na taabu yetu. Tulifanya kazi usiku na mchana, ili tusimlemee mtu yeyote wa kwenu wakati tulipokuwa tunawahubiria Injili ya Mungu.

    10 Ninyi wenyewe ni mashahidi na Mungu pia, jinsi tulivyokuwa watakatifu, wenye haki na wasio na lawama miongoni mwenu ninyi mlioamini. 11 Maana mnajua kwamba tuliwatendea kila mmoja wenu kama vile baba awatendeavyo watoto wake. 12 Tuliwatia moyo, tuliwafariji na kuwahimiza kuishi maisha yampendezayo Mungu, anayewaita katika Ufalme na utukufu wake.

  11. 17 Kwa maana Kristo hakunituma ili kubatiza bali kuhubiri Injili; sio kwa maneno ya hekima ya kibinadamu, ili msalaba wa Kristo usije ukakosa nguvu yake.

    18 Kwa maana ujumbe wa msalaba kwa wale wanaopotea ni upuzi, lakini kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.

  12. 14 Baada ya Yohana kukamatwa na kutiwa gerezani, Yesu aliingia Galilaya akaanza kuhubiri habari njema ya Mungu, 15 akisema, “Wakati umewadia, Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema.”

    16 Yesu alipokuwa akitembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona Simoni na Andrea nduguye wakizitupa nyavu zao baharini, kwa kuwa wao walikuwa wavuvi. 17 Yesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.” 18 Mara wakaacha nyavu zao, wakamfuata.

    19 Alipokwenda mbele kidogo, akamwona Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa kwenye mashua yao wakizitengeneza nyavu zao.

  13. 15 Ndiyo sababu ninatamani sana kuihubiri Injili kwenu pia ninyi mlioko Rumi.

    16 Mimi siionei haya Injili ya Kristo kwa maana ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, kwanza kwa Myahudi na kwa Myunani pia. 17 Kwa maana katika Injili haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa, haki ile iliyo kwa njia ya imani hadi imani. Kama ilivyoandikwa: “Mwenye haki ataishi kwa imani.”

  14. 12 Mtu yeyote asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe kielelezo kizuri kwa waumini katika usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi. 13 Fanya bidii kusoma Maandiko hadharani, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja. 14 Usiache kutumia kipawa kilicho ndani yako, ambacho ulipewa kwa neno la unabii wakati wazee walikuwekea mikono.

    15 Uwe na bidii katika mambo haya; ujitolee kwa ajili ya mambo haya kikamilifu, ili kila mtu aone kuendelea kwako. 16 Jilinde sana nafsi yako na mafundisho yako. Dumu katika hayo, kwa maana kwa kufanya hivyo, utajiokoa wewe mwenyewe pamoja na wale wanaokusikia.

  15. 1 Wakasafiri kupitia Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambako kulikuwa na sinagogi la Wayahudi. 2 Kama desturi yake, Paulo aliingia ndani ya sinagogi, na kwa muda wa Sabato tatu akawa anahojiana nao kutoka kwenye Maandiko, 3 akidhihirisha wazi na kuthibitisha kwamba ilikuwa lazima Kristo ateswe na afufuke kutoka kwa wafu. Akasema, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake, ndiye Kristo.” 4 Baadhi ya Wayahudi wakasadiki, wakaungana na Paulo na Sila, wakiwepo idadi kubwa ya Wayunani waliomcha Mungu na wanawake wengi mashuhuri.

  16. 36 Ninyi mnajua ule ujumbe uliotumwa kwa Israeli, ukitangaza habari njema za amani kwa Yesu Kristo. Yeye ni Bwana wa wote. 37 Mnajua yale yaliyotukia katika Uyahudi wote kuanzia Galilaya baada ya mahubiri ya Yohana Mbatizaji: 38 Jinsi Mungu alivyomtia Yesu wa Nazareti mafuta katika Roho Mtakatifu na jinsi alivyokwenda huku na huko akitenda mema na kuponya wote waliokuwa wameonewa na nguvu za ibilisi, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye.

    39 “Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyoyafanya katika Uyahudi na Yerusalemu. Wakamuua kwa kumtundika msalabani. 40 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu siku ya tatu na akamwezesha kuonekana na watu. 41 Hakuonekana kwa watu wote, lakini kwetu sisi tuliochaguliwa na Mungu kuwa mashahidi, ambao tulikula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. 42 Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote na kushuhudia kwamba ndiye alitiwa mafuta na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu.

  17. 1 Roho wa Bwana Mwenyezi yu juu yangu,

    kwa sababu Bwana amenitia mafuta

    kuwahubiria maskini habari njema.

    Amenituma kuwaganga waliovunjika moyo,

    kuwatangazia mateka uhuru wao,

    na hao waliofungwa

    habari za kufunguliwa kwao;

    2 kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,

    na siku ya kisasi ya Mungu wetu,

    kuwafariji wote waombolezao,

    3 na kuwapa mahitaji

    wale wanaohuzunika katika Sayuni,

    ili kuwapa taji ya uzuri badala ya majivu,

    mafuta ya furaha badala ya maombolezo,

    vazi la sifa badala ya roho ya kukata tamaa.

    Nao wataitwa mialoni ya haki,

    pando la Bwana,

    ili kuonyesha utukufu wake.

  18. 35 Lakini Paulo na Barnaba walibaki Antiokia ambako wao pamoja na wengine wengi walifundisha na kuhubiri neno la Bwana.

    Safari Ya Pili Ya Paulo Kueneza Injili

    36 Baada ya muda, Paulo akamwambia Barnaba, “Turudi tukawatembelee ndugu katika miji yote tuliyohubiri neno la Bwana tuone jinsi wanavyoendelea.”

  19. 11 Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, 12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa 13 mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo.

    14 Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. 15 Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo. 16 Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.

  20. 30 Kwa miaka miwili mizima Paulo alikaa huko kwa nyumba aliyokuwa amepanga. Akawakaribisha wote waliokwenda kumwona. 31 Akahubiri Ufalme wa Mungu na kufundisha mambo yale yaliyomhusu Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri wote na bila kizuizi chochote.

  21. 1 Siku hizo Yohana Mbatizaji alikuja akihubiri katika nyika ya Uyahudi, akisema, 2 “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.” 3 Huyu ndiye yule aliyenenwa habari zake na nabii Isaya aliposema:

    “Sauti ya mtu aliaye huko nyikani,

    ‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana,

    yanyoosheni mapito yake.’ ”

    4 Basi Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia, akiwa na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. 5 Watu walikuwa wakimwendea kutoka Yerusalemu, Uyahudi yote na nchi zote za kandokando ya Mto Yordani. 6 Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.

  22. 23 Yesu akapita katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu. 24 Kwa hiyo sifa zake zikaenea sehemu zote za Shamu, nao watu wakamletea wote waliokuwa na magonjwa mbalimbali na maumivu, waliopagawa na pepo wachafu, wenye kifafa na waliopooza, naye akawaponya. 25 Makutano makubwa ya watu yakawa yanamjia kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Uyahudi na kutoka ngʼambo ya Mto Yordani.

  23. 8 Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.”

  24. 25 “Nami sasa najua ya kuwa hakuna hata mmoja miongoni mwenu ambaye nimemhubiria Ufalme wa Mungu katika kwenda kwangu huku na huko, atakayeniona uso tena. 26 Kwa hiyo nawatangazia leo, sina hatia ya damu ya mtu awaye yote. 27 Kwa kuwa sikusita kuwatangazia mapenzi yote ya Mungu.

  25. 1 Basi ndugu zangu nataka niwakumbushe kuhusu Injili niliyowahubiria, mkaipokea na ambayo katika hiyo mmesimama. 2 Kwa Injili hii mnaokolewa mkishikilia kwa uthabiti neno nililowahubiria ninyi. La sivyo, mmeamini katika ubatili.

    3 Kwa maana yale niliyopokea ndiyo niliyowapa ninyi, kama yenye umuhimu wa kwanza: Kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yasemavyo Maandiko, 4 ya kuwa alizikwa na alifufuliwa siku ya tatu, kama yasemavyo Maandiko, 5 na kwamba alimtokea Kefa, kisha akawatokea wale kumi na wawili. 6 Baadaye akawatokea wale ndugu waumini zaidi ya 500 kwa pamoja, ambao wengi wao bado wako hai, ingawa wengine wamelala. 7 Ndipo akamtokea Yakobo na kisha mitume wote. 8 Mwisho wa wote, akanitokea mimi pia, ambaye ni kama aliyezaliwa si kwa wakati wake.

  26. 6 Nami nikasema, “Aa, Bwana Mwenyezi, sijui kusema, kwani mimi ni mtoto mdogo tu.”

    7 Lakini Bwana akaniambia, “Usiseme, ‘Mimi ni mtoto mdogo tu.’ Utaenda popote nitakapokutuma na kunena lolote nitakalokuagiza. 8 Usiwaogope, kwa maana niko pamoja nawe nikuokoe,” asema Bwana.

    9 Kisha Bwana akaunyoosha mkono wake na kugusa kinywa changu, akaniambia, “Sasa nimeyaweka maneno yangu kinywani mwako. 10 Tazama, leo nimekuweka juu ya mataifa na falme ili kungʼoa na kubomoa, kuharibu na kuangamiza, kujenga na kupanda.”

  27. 5 Hawa kumi na wawili, Yesu aliwatuma akawaagiza: “Msiende miongoni mwa watu wa Mataifa, wala msiingie mji wowote wa Wasamaria. 6 Lakini afadhali mshike njia kuwaendea kondoo wa nyumba ya Israeli waliopotea. 7 Wakati mnapokwenda, hubirini mkisema, ‘Ufalme wa Mbinguni umekaribia.’

  28. 29 Sasa, Bwana angalia vitisho vyao na utuwezeshe sisi watumishi wako kulinena neno lako kwa ujasiri mkuu. 30 Nyoosha mkono wako ili kuponya wagonjwa na kutenda ishara na miujiza kwa jina la Mwanao mtakatifu Yesu.”

    31 Walipokwisha kuomba, mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.

    32 Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. 33 Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. 34 Wala hapakuwepo mtu yeyote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, 35 wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.

    36 Yosefu, Mlawi kutoka Kipro, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake Mwana wa Faraja), 37 aliuza shamba alilokuwa nalo, akaleta hizo fedha alizopata na kuziweka miguuni pa mitume.

  29. 15 Jitahidi kujionyesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtendakazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli. 16 Jiepushe na maneno mabaya, yasiyo na maana, yasiyo ya utauwa, kwa maana hayo huzidi kuwatosa watu katika kukosa heshima kwa Mungu.

  30. 17 Tangu wakati huo, Yesu alianza kuhubiri akisema: “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.”

  31. 9 “Hivi basi, ndivyo iwapasavyo kuomba:

    “ ‘Baba yetu uliye mbinguni,

    Jina lako litukuzwe.

    10 Ufalme wako uje.

    Mapenzi yako yafanyike

    hapa duniani kama huko mbinguni.

    11 Utupatie riziki yetu

    ya kila siku.

    12 Utusamehe deni zetu,

    kama sisi nasi tulivyokwisha

    kuwasamehe wadeni wetu.

    13 Usitutie majaribuni,

    bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu

    [kwa kuwa Ufalme ni wako, na nguvu,

    na utukufu, hata milele. Amen].’

    14 Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. 15 Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

    16 “Mnapofunga, msiwe wenye huzuni kama wafanyavyo wanafiki. Maana wao hukunja nyuso zao ili kuwaonyesha wengine kwamba wamefunga. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupata thawabu yao kamilifu. 17 Lakini mnapofunga, jipakeni mafuta kichwani na kunawa nyuso zenu 18 ili kufunga kwenu kusionekane na watu wengine ila Baba yenu aketiye mahali pa siri; naye Baba yenu aonaye sirini atawapa thawabu yenu kwa wazi.

    19 “Msijiwekee hazina duniani, mahali ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi huvunja na kuiba. 20 Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba. 21 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.

  32. 1 Baada ya Yesu kumaliza kutoa maagizo kwa wanafunzi wake kumi na wawili, aliondoka hapo akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.

    2 Yohana aliposikia akiwa gerezani mambo ambayo Kristo alikuwa akiyafanya, aliwatuma wanafunzi wake 3 ili wakamuulize, “Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?”

    4 Yesu akajibu, “Rudini mkamwambie Yohana yale mnayosikia na kuyaona: 5 Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema.

  33. 18 “Roho wa Bwana yu juu yangu,

    kwa sababu amenitia mafuta

    kuwahubiria maskini habari njema.

    Amenituma kuwatangazia wafungwa

    kufunguliwa kwao,

    na vipofu kupata kuona tena,

    kuwaweka huru wanaoonewa,

    19 na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika.”

  34. 43 Lakini yeye akawaambia, “Imenipasa kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa maana kwa kusudi hili nilitumwa.” 44 Naye aliendelea kuhubiri katika masinagogi ya Uyahudi.

  35. 20 Papo hapo akaanza kuhubiri kwenye masinagogi kwamba “Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu” 21 Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa na kuuliza, “Huyu si yule mtu aliyesababisha maangamizi makuu huko Yerusalemu miongoni mwa watu waliolitaja jina hili? Naye si amekuja hapa kwa kusudi la kuwakamata na kuwapeleka wakiwa wafungwa mbele ya viongozi wa makuhani?” 22 Sauli akazidi kuwa hodari na kuwashangaza Wayahudi walioishi Dameski kwa kuthibitisha kuwa Yesu ndiye Kristo.

  36. 4 Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja, 5 vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. 6 Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani. 7 Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe, 8 kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha.

    9 Upendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema. 10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine. 11 Msiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana. 12 Kuweni na furaha katika tumaini, katika dhiki kuweni na saburi, dumuni katika maombi. 13 Changieni katika mahitaji ya watakatifu, wakaribisheni wageni.

  37. 1 Kwa hiyo, ndugu zangu, ninaowapenda na ambao ninawaonea shauku, ninyi mlio furaha yangu na taji yangu, hivi ndivyo iwapasavyo kusimama imara katika Bwana, ninyi wapenzi wangu.

    2 Nawasihi Euodia na Sintike wawe na nia moja katika Bwana. 3 Naam, nakusihi wewe pia, mwenzangu mwaminifu, uwasaidie hawa wanawake, kwa sababu walijitaabisha katika kazi ya Injili pamoja nami bega kwa bega, wakiwa pamoja na Klementi na watendakazi wenzangu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima.

    4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! 5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

    8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo. 9 Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.

  38. 14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.

    15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.

    18 Ninyi wake, watiini waume zenu, kama inavyostahili katika Bwana.

    19 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, wala msiwe na uchungu dhidi yao.

    20 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote, kwa maana hivi ndivyo inavyompendeza Bwana.

    21 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

  39. 7 Akawaita wale kumi na wawili, akawatuma wawili wawili, na kuwapa mamlaka kutoa pepo wachafu.

    8 Akawaagiza akisema, “Msichukue chochote kwa ajili ya safari isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kwenye mikanda yenu. 9 Vaeni viatu, lakini msivae nguo ya ziada.” 10 Akawaambia, “Mkiingia kwenye nyumba yoyote, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo. 11 Kama mahali popote hawatawakaribisha wala kuwasikiliza, mtakapoondoka huko, kungʼuteni mavumbi kutoka kwenye miguu yenu ili kuwa ushuhuda dhidi yao.”

    12 Kwa hiyo wakatoka na kuhubiri kwamba inawapasa watu kutubu na kuacha dhambi.

  40. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa. 18 Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. 19 Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu. 20 Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe. 21 Lakini yule aishiye kwa ukweli huja kwenye nuru, ili ionekane wazi kwamba matendo yake yametendeka katika Mungu.”

  41. 42 Kila siku, Hekaluni na nyumba kwa nyumba, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema kwamba Yesu ndiye Kristo.

  42. 21 Wakahubiri habari njema katika mji huo na kupata wanafunzi wengi. Kisha wakarudi Listra, Ikonio na Antiokia, 22 wakiwaimarisha wanafunzi na kuwatia moyo waendelee kudumu katika imani. Wakawaonya wakisema, “Imetupasa kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa kupitia katika taabu nyingi.”

  43. 10 Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo na neema yake kwangu haikuwa kitu bure. Bali nilizidi sana kufanya kazi kuliko mitume wote, lakini haikuwa mimi, bali ni ile neema ya Mungu iliyokuwa pamoja nami. 11 Hivyo basi, kama ilikuwa mimi au wao, hili ndilo tunalohubiri, na hili ndilo mliloamini.

    12 Basi kama tumehubiri ya kwamba Kristo alifufuliwa kutoka kwa wafu, mbona baadhi yenu mnasema hakuna ufufuo wa wafu? 13 Lakini kama hakuna ufufuo wa wafu, basi hata Kristo hakufufuliwa. 14 Tena ikiwa Kristo hakufufuliwa kutoka kwa wafu, kuhubiri kwetu kumekuwa ni bure na imani yenu ni batili.

  44. 35 Yesu akazunguka katika miji yote na vijiji vyote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi. 36 Alipoona makutano, aliwahurumia kwa sababu walikuwa wanasumbuka bila msaada, kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. 37 Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache. 38 Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watendakazi katika shamba lake la mavuno.”

  45. 20 Kisha wanafunzi wake wakatoka, wakahubiri kila mahali, naye Bwana akatenda kazi pamoja nao na kulithibitisha neno lake kwa ishara zilizofuatana nalo.]

  46. 1 Baada ya haya Yesu alikwenda, akawa anazunguka katika miji na vijiji akihubiri habari njema za Ufalme wa Mungu. Wale wanafunzi wake kumi na wawili walikuwa pamoja naye,

  47. 8 Petro, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akajibu, “Enyi watawala na wazee wa watu, 9 kama leo tukihojiwa kwa habari ya mambo mema aliyotendewa yule kiwete na kuulizwa jinsi alivyoponywa, 10 ijulikane kwenu nyote na kwa watu wote wa Israeli kwamba: Ni kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulubisha lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama mbele yenu akiwa mzima kabisa. 11 Huyu ndiye

    “ ‘jiwe ambalo ninyi wajenzi mlilikataa,

    ambalo limekuwa jiwe kuu la pembeni.’

    12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”

    13 Wale viongozi na wazee walipoona ujasiri wa Petro na Yohana na kujua ya kuwa walikuwa watu wa kawaida, wasio na elimu, walishangaa sana, wakatambua kwamba hawa watu walikuwa na Yesu. 14 Lakini kwa kuwa walikuwa wanamwona yule kiwete aliyeponywa amesimama pale pamoja nao, hawakuweza kusema lolote kuwapinga.

  48. 4 Kila Sabato Paulo alikuwa akihojiana nao katika sinagogi, akijitahidi kuwashawishi Wayahudi na Wayunani.

    5 Sila na Timotheo walipowasili kutoka Makedonia, walimkuta Paulo akiwa amejitolea muda wake wote katika kuhubiri, akiwashuhudia Wayahudi kwamba Yesu ndiye Kristo 6 Wayahudi walipompinga Paulo na kukufuru, yeye aliyakungʼuta mavazi yake, akawaambia, “Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu! Mimi sina hatia, nimetimiza wajibu wangu. Kuanzia sasa nitawaendea watu wa Mataifa.”

  49. 16 Lakini ninapohubiri Injili siwezi kujisifu maana ninalazimika kuhubiri. Ole wangu nisipoihubiri Injili! 17 Nikihubiri kwa hiari, ninayo thawabu. Lakini kama si kwa hiari, basi ninachofanya ni kutekeleza tu uwakili niliowekewa. 18 Basi je, thawabu yangu ni nini? Thawabu yangu ni hii: Ya kwamba katika kuhubiri Injili niitoe bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili.

  50. 5 Kwa maana hatujihubiri sisi wenyewe ila tunamhubiri Yesu Kristo kuwa ni Bwana na sisi ni watumishi wenu kwa ajili ya Yesu.

  51. 6 Nashangaa kwamba mnamwacha upesi hivyo yeye aliyewaita kwa neema ya Kristo na kuifuata Injili nyingine, 7 ambayo kwa kweli si Injili kamwe, ila kwa dhahiri kuna watu wanaowachanganya na wanaotaka kuipotosha Injili ya Kristo. 8 Lakini hata ikiwa sisi au malaika atokaye mbinguni akihubiri Injili nyingine tofauti na ile tuliyowahubiria sisi, basi mtu huyo alaaniwe milele! 9 Kama vile tulivyokwisha kusema kabla, sasa nasema tena, ikiwa mtu yeyote atawahubiria Injili kinyume na ile mliyoipokea na alaaniwe milele!

    10 Je, sasa mimi ninatafuta kukubaliwa na wanadamu au kukubaliwa na Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa bado najaribu kuwapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumishi wa Kristo.

  52. 6 Kwa sababu hii nakukumbusha uchochee ile karama ya Mungu, iliyowekwa ndani yako nilipokuwekea mikono yangu. 7 Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.

    8 Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu, 9 ambaye alituokoa na kutuita katika mwito mtakatifu: si kwa kadiri ya matendo yetu mema bali kwa sababu ya kusudi lake mwenyewe na neema yake. Neema hii tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele. 10 Lakini sasa imefunuliwa kwa kudhihirishwa kwake Mwokozi wetu, Kristo Yesu, ambaye amebatilisha mauti na kuleta uzima na kutokufa kwa njia ya Injili. 11 Nami nimewekwa kuwa mhubiri, mtume na mwalimu wa Injili hii.

  53. 16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, 17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.

  54. 45 Ndipo akafungua fahamu zao ili waweze kuyaelewa Maandiko. 46 Akawaambia, “Haya ndiyo yaliyoandikwa: Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu. 47 Toba na msamaha wa dhambi zitatangaziwa mataifa yote kupitia jina lake kuanzia Yerusalemu. 48 Ninyi ni mashahidi wa mambo haya.

    49 “Tazama nitawatumia ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini hadi mtakapovikwa uwezo utokao juu.”

  55. 1 Wakati Petro na Yohana walipokuwa wakisema na watu, makuhani, mkuu wa walinzi wa Hekalu na Masadukayo wakawajia, 2 huku wakiwa wamekasirika sana kwa sababu mitume walikuwa wanawafundisha watu na kuhubiri kwamba kuna ufufuo wa wafu ndani ya Yesu. 3 Wakawakamata Petro na Yohana na kuwatia gerezani mpaka kesho yake kwa kuwa ilikuwa jioni. 4 Lakini wengi waliosikia lile neno waliamini, idadi yao ilikuwa yapata wanaume 5,000.

    5 Kesho yake, viongozi wa Kiyahudi, wazee na walimu wa sheria wakakusanyika Yerusalemu. 6 Walikuwepo kuhani mkuu Anasi, Kayafa, Yohana, Iskanda, na wengi wa jamaa ya kuhani mkuu.

  56. 14 Vivyo hivyo, Bwana ameamuru kwamba wale wanaohubiri Injili wapate riziki yao kutokana na Injili.

  57. 5 Sababu ya mimi kukuacha huko Krete ni ili uweke utaratibu mambo yale yaliyosalia na kuwaweka wazee wa kanisa katika kila mji, kama nilivyokuagiza. 6 Mzee wa kanisa asiwe na lawama, awe mume wa mke mmoja, mtu ambaye watoto wake ni waaminio na wala hawashtakiwi kwa ufisadi. 7 Kwa kuwa mwangalizi, kama wakili wa Mungu, imempasa kuwa mtu asiye na lawama, asiwe mwenye majivuno au mwepesi wa hasira, wala mlevi, wala asiwe mtu mwenye tamaa ya mapato yasiyo ya halali. 8 Bali awe mkarimu, anayependa mema, mwenye kiasi, mwenye haki, mwadilifu, mnyofu, mtakatifu na mwenye kuitawala nafsi yake. 9 Inampasa alishike kwa uthabiti lile neno la imani kama lilivyofundishwa, kusudi aweze kuwaonya wengine kwa mafundisho manyofu na kuwakanusha wale wanaopingana nayo.

    10 Kwa maana wako wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, hasa wale wa kikundi cha tohara. 11 Hao ni lazima wanyamazishwe, kwa sababu wanaharibu watu wa nyumba nzima wakifundisha mambo yasiyowapasa kufundisha. Wanafanya hivyo kwa ajili ya kujipatia mapato ya udanganyifu.

  58. 1 Ndugu zangu, msiwe walimu wengi, kwa maana mnafahamu kwamba sisi tufundishao tutahukumiwa vikali zaidi.

  59. 1 Hata kama nitasema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa kengele inayolialia au toazi livumalo. 2 Ningekuwa na karama ya unabii na kujua siri zote na maarifa yote, hata kama nina imani kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, mimi si kitu. 3 Kama nikitoa mali yote niliyo nayo na kama nikijitolea mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo, hainifaidi kitu.

    4 Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. 5 Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. 6 Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. 7 Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.

    8 Upendo haushindwi kamwe. Lakini ukiwepo unabii, utakoma; zikiwepo lugha, zitakoma; yakiwepo maarifa, yatapita.

  60. 17 Alikuja na kuhubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali na pia akahubiri amani kwao waliokuwa karibu.

  61. 9 Kwa sababu hii, tangu siku ile tuliposikia habari zenu, hatujakoma kuomba kwa ajili yenu na kumsihi Mungu awajaze ninyi maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote ya kiroho na ufahamu. 10 Nasi tunaomba haya ili mpate kuishi maisha yanayostahili mbele za Bwana, na mpate kumpendeza kwa kila namna: mkizaa matunda kwa kila kazi njema, mkikua katika kumjua Mungu, 11 mkiwa mmetiwa nguvu kwa uwezo wote kwa kadiri ya nguvu yake yenye utukufu, ili mpate kuwa na wingi wa saburi na uvumilivu. Nanyi kwa furaha 12 mkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru. 13 Kwa maana ametuokoa kutoka ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa, 14 ambaye katika yeye tunao ukombozi, yaani msamaha wa dhambi.

    15 Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16 Kwake yeye vitu vyote vilivyoko mbinguni na juu ya nchi viliumbwa: vitu vinavyoonekana na visivyoonekana, viwe ni viti vya enzi au falme, au wenye mamlaka au watawala; vitu vyote viliumbwa na yeye na kwa ajili yake. 17 Yeye alikuwepo kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja.

  62. 28 Yeye ndiye tunayemtangaza, tukimwonya kila mtu na kumfundisha kila mtu kwa hekima yote ili tuweze kumleta kila mmoja akiwa amekamilika katika Kristo. 29 Kwa ajili ya jambo hili, ninajitaabisha, nikijitahidi kwa kadiri ya nguvu zake ambazo hutenda kazi ndani yangu kwa uweza mwingi.

  63. 1 Hili ni neno la kuaminiwa, kwamba mtu akitamani kazi ya uangalizi, atamani kazi nzuri. 2 Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha, 3 asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha. 4 Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia. 5 (Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kanisa la Mungu?)

  64. 2 Nayo mambo yale uliyonisikia nikiyasema mbele ya mashahidi wengi, uwakabidhi watu waaminifu watakaoweza kuwafundisha watu wengine vilevile.

  65. 1 Neno la Bwana lilimjia Yona mwana wa Amitai: 2 “Nenda katika mji mkubwa wa Ninawi ukahubiri juu yake, kwa sababu uovu wake umekuja juu mbele zangu.”

    3 Lakini Yona alimkimbia Bwana na kuelekea Tarshishi. Alishuka mpaka Yafa, ambapo alikuta meli iliyokuwa imepangwa kuelekea bandari ile. Baada ya kulipa nauli, akapanda melini na kuelekea Tarshishi ili kumkimbia Bwana.

  66. 2 Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:

    “Tazama, nitamtuma mjumbe wangu mbele yako,

    atakayetengeneza njia mbele yako”:

    3 “sauti ya mtu aliaye nyikani.

    ‘Itengenezeni njia ya Bwana,

    yanyoosheni mapito yake.’ ”

    4 Yohana alikuja, akibatiza huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi. 5 Watu kutoka Uyahudi wote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea. Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.

  67. 3 Akaenda katika nchi yote kandokando ya Mto Yordani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi. 4 Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:

    “Sauti ya mtu aliaye nyikani,

    ‘Itengenezeni njia ya Bwana,

    yanyoosheni mapito yake.

    5 Kila bonde litajazwa,

    kila mlima na kilima vitashushwa.

    Njia zilizopinda zitanyooshwa,

    na zilizoparuza zitasawazishwa.

    6 Nao watu wote watauona

    wokovu wa Mungu.’ ”

  68. 19 Tubuni basi mkamgeukie Mungu, dhambi zenu zifutwe, ili zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwepo kwake Bwana, 20 naye apate kumtuma Kristo, ambaye ameteuliwa kwa ajili yenu, yaani Yesu. 21 Ilimpasa mbingu zimpokee mpaka wakati wa kufanywa upya kila kitu, kama Mungu alivyoahidi zamani kupitia kwa vinywa vya manabii wake watakatifu.

  69. 18 Kisha wakawaita tena ndani na kuwaamuru wasiseme wala kufundisha kamwe kwa hili jina la Yesu.

    19 Lakini Petro na Yohana wakajibu, “Amueni ninyi wenyewe iwapo ni haki mbele za Mungu kuwatii ninyi kuliko kumtii Mungu. 20 Lakini sisi hatuwezi kuacha kusema yale tuliyoyaona na kuyasikia.”

  70. Mateso Na Kuenea Kwa Injili

    1 Basi ikawa katika siku hizo, wakati idadi ya wanafunzi ilipokuwa ikiongezeka sana, palitokea manungʼuniko kati ya Wayahudi wa Kiyunani, dhidi ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahaulika katika mgawanyo wa chakula wa kila siku. 2 Wale mitume kumi na wawili wakakusanya wanafunzi wote pamoja wakasema, “Haitakuwa vyema sisi kuacha huduma ya neno la Mungu ili kuhudumu mezani. 3 Kwa hiyo ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, watu wenye sifa njema, waliojawa na Roho Mtakatifu na hekima, ambao tunaweza kuwakabidhi kazi hii, 4 nasi tutatumia muda wetu kuomba na huduma ya neno.”

    5 Yale waliyosema yakawapendeza watu wote, nao wakamchagua Stefano (mtu aliyejawa na imani na Roho Mtakatifu) pamoja na Filipo, Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena na Nikolao, mwongofu kutoka Antiokia.

  71. Safari Ya Kwanza Ya Paulo Kueneza Injili

    1 Katika kanisa huko Antiokia ya Shamu walikuwako manabii na walimu, yaani: Barnaba, Simeoni aitwaye Nigeri, Lukio Mkirene, Manaeni aliyekuwa amelelewa pamoja na Mfalme Herode Agripa, na Sauli. 2 Walipokuwa wakimwabudu Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, “Nitengeeni Sauli na Barnaba kwa kazi ile maalum niliyowaitia.” 3 Ndipo baada ya kufunga na kuomba, wakawawekea mikono yao na wakawatuma waende zao.

    4 Hivyo, wakiwa wametumwa na Roho Mtakatifu, wakashuka kwenda Seleukia na kutoka huko wakasafiri baharini mpaka kisiwa cha Kipro. 5 Walipowasili katika mji wa Salami, wakahubiri neno la Mungu katika sinagogi la Wayahudi. Pia walikuwa na Yohana Marko kuwa msaidizi wao.

  72. 17 Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo.

  73. 1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.

  74. 24 Je, hamjui kwamba katika mashindano ya mbio wote wanaoshindana hukimbia, lakini ni mmoja wao tu apewaye tuzo? Kwa hiyo kimbieni katika mashindano kwa jinsi ambavyo mtapata tuzo.

    25 Kila mmoja anayeshiriki katika mashindano hufanya mazoezi makali. Wao hufanya hivyo ili wapokee taji isiyodumu, lakini sisi tunafanya hivyo ili kupata taji idumuyo milele. 26 Kwa hiyo mimi sikimbii kama mtu akimbiaye bila lengo, sipigani kama mtu anayepiga hewa, 27 la, bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha ili nikiisha kuwahubiria wengine, mimi nisiwe mtu wa kukataliwa.

  75. 8 Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi. 9 Kuweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manungʼuniko. 10 Kila mmoja na atumie kipawa chochote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu. 11 Yeyote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Yeyote ahudumuye hana budi kuhudumu kwa nguvu zile anazopewa na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kwa njia ya Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye milele na milele. Amen.

  76. 10 Mose akamwambia Bwana, “Ee Bwana, kamwe sijapata kuwa msemaji kwa ufasaha wakati uliopita wala tangu ulipoanza kuzungumza na mtumishi wako. Ulimi wangu ni mzito kuzungumza.”

    11 Bwana akamwambia, “Ni nani aliyempa mwanadamu kinywa? Ni nani aliyemfanya mtu kuwa kiziwi au bubu? Ni nani anayempa mtu kuona au upofu? Je, si mimi, Bwana? 12 Sasa nenda, nitakusaidia kusema, nami nitakufundisha jambo la kusema.”

  77. 27 Wakiisha kuwaleta mitume wakawaamuru kusimama mbele ya baraza ili kuhani mkuu awahoji. 28 “Tuliwaonya kwa nguvu msifundishe kwa jina hili, lakini ninyi mmeijaza Yerusalemu yote mafundisho yenu na tena mmekusudia kuleta damu ya mtu huyu juu yetu.”

    29 Petro na wale mitume wengine wakajibu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.

  78. 9 Je, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wahanithi, wala walawiti, 10 wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyangʼanyi hawataurithi Ufalme wa Mungu. 11 Baadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Yesu Kristo na katika Roho wa Mungu wetu.

  79. 24 Lakini kama mtu asiyeamini au asiyeelewa akiingia wakati kila mtu anatoa unabii, ataaminishwa na watu wote kuwa yeye ni mwenye dhambi na kuhukumiwa na wote, 25 nazo siri za moyo wake zitawekwa wazi. Kwa hiyo ataanguka chini na kumwabudu Mungu akikiri, “Kweli Mungu yuko katikati yenu!”

    26 Basi tuseme nini ndugu zangu? Mnapokutana pamoja, kila mmoja ana wimbo, au neno la mafundisho, au ufunuo, lugha mpya au atatafsiri. Mambo yote yatendeke kwa ajili ya kulijenga kanisa. 27 Kama mtu yeyote akinena kwa lugha, basi waseme watu wawili au watatu si zaidi, mmoja baada ya mwingine na lazima awepo mtu wa kutafsiri. 28 Lakini kama hakuna mtu wa kutafsiri, hao watu na wanyamaze kimya kanisani na wanene na nafsi zao wenyewe na Mungu.

    29 Manabii wawili au watatu wanene na wengine wapime yale yasemwayo. 30 Kama mtu yeyote aliyeketi karibu, akipata ufunuo, basi yule wa kwanza na anyamaze. 31 Kwa maana wote mnaweza kutoa unabii, mmoja baada ya mwingine, ili kila mtu apate kufundishwa na kutiwa moyo.

  80. 15 Ni kweli kwamba wengine wanamhubiri Kristo kutokana na wivu na kwa kutaka kushindana, lakini wengine wanamhubiri Kristo kwa nia njema. 16 Hawa wa mwisho wanamhubiri Kristo kwa moyo wa upendo, wakifahamu kwamba nimo humu gerezani kwa ajili ya kuitetea Injili. 17 Hao wa kwanza wanamtangaza Kristo kutokana na tamaa zao wenyewe wala si kwa moyo mweupe, bali wanakusudia kuongeza mateso yangu katika huku kufungwa kwangu. 18 Lakini inadhuru nini? Jambo la muhimu ni kwamba kwa kila njia, ikiwa ni kwa nia mbaya au njema, Kristo anahubiriwa. Nami kwa ajili ya jambo hilo ninafurahi.

    Naam, nami nitaendelea kufurahi,

  81. 23 Tushike kwa uthabiti lile tumaini la ukiri wetu bila kuyumbayumba, kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu. 24 Tuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema. 25 Wala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi, bali tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.

    26 Kama tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi. 27 Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao, utakaowaangamiza adui za Mungu. 28 Yeyote aliyeikataa sheria ya Mose alikufa pasipo huruma kwa ushahidi wa watu wawili au watatu. 29 Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani anayostahili kupewa mtu aliyemkanyaga Mwana wa Mungu chini ya nyayo zake, yeye aliyeifanya damu ya Agano iliyomtakasa kuwa kitu najisi na kumtendea maovu Roho wa neema? 30 Kwa kuwa tunamjua yeye aliyesema, “Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza.” Tena asema, “Bwana atawahukumu watu wake.” 31 Ni jambo la kutisha kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai.

  82. 5 kama hakuusamehe ulimwengu wa kale alipoleta gharika juu ya watu wale wasiomcha Mungu, bali akamhifadhi Noa, mhubiri wa haki, pamoja na watu wengine saba;

  83. 5 Huu ndio ujumbe tuliosikia kutoka kwake na kuwatangazia ninyi: kwamba Mungu ni nuru na ndani yake hamna giza lolote. 6 Kama tukisema kwamba twashirikiana naye huku tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatutendi lililo kweli. 7 Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo nuruni, twashirikiana sisi kwa sisi na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.

    8 Kama tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu. 9 Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutoka kwenye udhalimu wote. 10 Kama tukisema hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo na neno lake halimo ndani yetu.

  84. 6 “Uwe hodari na shujaa, kwa sababu wewe ndiwe utakayewaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa. 7 Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. 8 Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”

  85. 14 Amosi akamjibu Amazia, “Mimi sikuwa nabii wala mwana wa nabii, lakini nilikuwa mchungaji wa kondoo na mtunza mikuyu. 15 Lakini Bwana akanitoa kutoka kuchunga kondoo na kuniambia, ‘Nenda, ukawatabirie watu wangu Israeli.’

  86. 14 Injili ya Ufalme itahubiriwa ulimwenguni kote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Ndipo mwisho utakapokuja.

  87. 38 Alipokuwa akifundisha, Yesu alisema, “Jihadharini na walimu wa sheria. Wao hupenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa kwa heshima masokoni. 39 Pia wao hupenda kukaa kwenye viti vya mbele katika masinagogi, na kupewa nafasi za heshima katika karamu. 40 Wao hula nyumba za wajane, na ili waonekane kuwa wema wanasali sala ndefu. Watu kama hawa watapata hukumu iliyo kuu sana.”

    41 Kisha Yesu akaketi mkabala na sehemu ambapo sadaka zilikuwa zinawekwa na kuangalia umati wa watu wakiweka fedha zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. Matajiri wengi wakaweka kiasi kikubwa cha fedha. 42 Lakini mjane mmoja maskini akaja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba zenye thamani ya senti mbili.

    43 Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka katika sanduku la hazina zaidi ya watu wengine wote. 44 Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali zao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake, akaweka kila kitu alichokuwa nacho, hata kile alichohitaji ili kuishi.”

  88. 60 Yesu akamwambia, “Waache wafu wawazike wafu wao, bali wewe nenda ukautangaze Ufalme wa Mungu.”

  89. 9 Mungu ambaye mmeitwa naye ili mwe na ushirika na Mwanawe Yesu Kristo, Bwana wetu ni mwaminifu.

    10 Nawasihi ndugu zangu, katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi, ili pasiwepo na matengano katikati yenu na kwamba mwe na umoja kikamilifu katika nia na katika kusudi.

  90. 1 Igeni mfano wangu, kama ninavyouiga mfano wa Kristo.

    2 Ninawasifu kwa kuwa mnanikumbuka katika kila jambo na kwa kushika mafundisho niliyowapa.

  91. 1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, 2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. 3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.