17 Bible Verses About The Lord's Supper
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
26 Walipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu.”
27 Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, “Nyweni nyote katika kikombe hiki. 28 Hii ndiyo damu yangu ya Agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. 29 Lakini ninawaambia, tangu sasa sitakunywa tena katika uzao huu wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya pamoja nanyi katika Ufalme wa Baba yangu.”
-
14 Wakati ulipowadia, Yesu akaketi mezani pamoja na wale mitume wake. 15 Kisha akawaambia, “Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu. 16 Kwa maana, nawaambia, sitaila tena Pasaka mpaka itakapotimizwa katika Ufalme wa Mungu.”
17 Akiisha kukichukua kikombe, akashukuru, akasema, “Chukueni hiki mnywe wote. 18 Kwa maana nawaambia tangu sasa sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi Ufalme wa Mungu utakapokuja.”
19 Kisha akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa, akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”
20 Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, imwagikayo kwa ajili yenu.
-
14 Kwa hiyo wapenzi wangu, zikimbieni ibada za sanamu. 15 Nasema watu wenye ufahamu, amueni wenyewe kuhusu haya niyasemayo. 16 Je, kikombe cha baraka ambacho tunakibariki, si ushirika katika damu ya Kristo? Mkate tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? 17 Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa kuwa wote twashiriki mkate mmoja.
18 Waangalieni watu wa Israeli: Je, wale wote walao dhabihu si ni wale watendao kazi madhabahuni? 19 Je, nina maana kwamba kafara iliyotolewa kwa sanamu ni kitu chenye maana yoyote? Au kwamba sanamu ni kitu chenye maana yoyote? 20 La hasha! Lakini kafara za watu wasiomjua Mungu hutolewa kwa mashetani, wala si kwa Mungu. Nami sitaki ninyi mwe na ushirika na mashetani. 21 Hamwezi kunywa katika kikombe cha Bwana na cha mashetani pia. Hamwezi kuwa na sehemu katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani pia. 22 Je, tunataka kuamsha wivu wa Bwana? Je, sisi tuna nguvu kuliko yeye?
-
22 Walipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni mle; huu ndio mwili wangu.”
23 Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, nao wote wakanywa kutoka humo.
24 Akawaambia, “Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. 25 Amin, nawaambia, sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya katika Ufalme wa Mungu.”
26 Walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka wakaenda Mlima wa Mizeituni.
-
42 Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali. 43 Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume. 44 Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika. 45 Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake. 46 Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe, 47 wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa wale waliokuwa wakiokolewa.
-
17 Basi katika maagizo yafuatayo, siwezi kuwasifu, kwa sababu mkutanikapo si kwa ajili ya faida bali kwa hasara. 18 Kwanza, mnapokutana kama kanisa, nasikia kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwenu, nami kwa kiasi fulani nasadiki kuwa ndivyo ilivyo. 19 Bila shaka lazima pawe na tofauti miongoni mwenu ili kuonyesha ni nani anayekubaliwa na Mungu. 20 Mkutanikapo pamoja si chakula cha Bwana mnachokula, 21 kwa kuwa mnapokula, kila mmoja wenu anakula bila kuwangoja wengine. Mmoja hukaa njaa na mwingine analewa. 22 Je, hamna nyumbani kwenu ambako mnaweza kula na kunywa? Au mnalidharau kanisa la Mungu na kuwadhalilisha wale wasio na kitu? Niwaambie nini? Je, niwasifu juu ya jambo hili? La, hasha!
23 Kwa maana mimi nilipokea kutoka kwa Bwana yale niliyowapa ninyi, kwamba Bwana Yesu, usiku ule aliposalitiwa, alitwaa mkate, 24 naye akiisha kushukuru, akaumega, akasema, “Huu ndio mwili wangu, uliotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” 25 Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu. Fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.” 26 Maana kila mlapo mkate huu na kunywea kikombe hiki, mnatangaza mauti ya Bwana mpaka ajapo.
27 Kwa hiyo, mtu yeyote alaye mkate huo au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa na hatia ya dhambi juu ya mwili na damu ya Bwana. 28 Inampasa mtu ajichunguze mwenyewe, kabla ya kula mkate na kukinywea kikombe. 29 Kwa maana mtu yeyote alaye na kunywa pasipo kuutambua mwili wa Bwana, hula na kunywa hukumu juu yake mwenyewe. 30 Hii ndiyo sababu wengi miongoni mwenu ni wagonjwa na dhaifu na wengine wenu hata wamekufa. 31 Lakini kama tungejichunguza wenyewe tusingehukumiwa. 32 Tunapohukumiwa na Bwana, tunaadibishwa ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu.
33 Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo pamoja ili kula, mngojane. 34 Kama mtu akiwa na njaa, ale nyumbani kwake ili mkutanapo pamoja msije mkahukumiwa.
Nami nitakapokuja nitawapa maelekezo zaidi.
-
7 Siku ya kwanza ya juma tulikutana pamoja kwa ajili ya kumega mkate. Paulo akaongea na watu, naye kwa kuwa alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliendelea kuongea mpaka usiku wa manane.
-
53 Hivyo Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, msipoula mwili wa Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. 54 Mtu yeyote aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, anao uzima wa milele. Nami nitamfufua siku ya mwisho. 55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli. 56 Yeyote alaye mwili wangu na kunywa damu yangu, atakaa ndani yangu nami nitakaa ndani yake. 57 Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, na kama nami ninavyoishi kwa sababu ya Baba, hivyo anilaye mimi ataishi kwa sababu yangu. 58 Huu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, si kama ule mkate baba zenu waliokula nao wakafa. Lakini yeye aulaye mkate huu ataishi milele.” 59 Yesu alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika sinagogi huko Kapernaumu.
-
47 Amin, amin nawaambia, yeye anayeamini anao uzima wa milele. 48 Mimi ni mkate wa uzima. 49 Baba zenu walikula mana jangwani, lakini wakafa. 50 Lakini hapa kuna mkate utokao mbinguni, ambao mtu yeyote akiula, hatakufa. 51 Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni. Mtu yeyote akiula mkate huu, ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu, ambao nitautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.”
-
9 Ndipo malaika akaniambia, “Andika: ‘Wamebarikiwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo!’ ” Naye akaongeza kusema, “Haya ndiyo maneno ya kweli ya Mungu.”
-
23 Yesu akamjibu, “Mtu yeyote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake.
-
21 Ndipo Mose akawaita wazee wote wa Israeli na kuwaambia, “Nendeni mara moja mkachague wanyama kwa ajili ya jamaa zenu, mkachinje mwana-kondoo wa Pasaka. 22 Chukueni kitawi cha hisopo, kichovyeni kwenye damu iliyopo kwenye sinia na kuipaka baadhi ya hiyo damu kwenye vizingiti na kwenye miimo yote miwili ya milango. Mtu yeyote asitoke nje ya mlango wa nyumba yake mpaka asubuhi. 23 Bwana apitapo katika nchi yote kuwapiga Wamisri, ataiona damu juu ya vizingiti na kwenye miimo ya milango, naye atapita juu, wala hatamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwapiga ninyi.
24 “Shikeni maagizo haya yawe kanuni ya kudumu kwenu na kwa ajili ya wazao wenu. 25 Mtakapoingia katika nchi Bwana atakayowapa kama alivyoahidi, shikeni desturi hii. 26 Watoto wenu watakapowauliza, ‘Sikukuu hii ina maana gani kwenu?’ 27 Basi waambieni, ‘Hii ni dhabihu ya Pasaka kwa Bwana, ambaye alipita juu ya nyumba za Waisraeli katika nchi ya Misri na hakudhuru nyumba zetu alipowapiga Wamisri.’ ” Ndipo watu wa Israeli waliposujudu na kuabudu. 28 Waisraeli wakafanya kama vile Bwana alivyomwagiza Mose na Aroni.
-
17 Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wanafunzi walimjia Yesu wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?”
18 Akajibu, “Nendeni kwa mtu fulani huko mjini, mkamwambie, ‘Mwalimu asema hivi: Saa yangu imekaribia. Nitaiadhimisha Pasaka pamoja na wanafunzi wangu katika nyumba yako.’ ” 19 Hivyo wanafunzi wakafanya kama vile Yesu alivyokuwa amewaelekeza, nao wakaandaa Pasaka.
-
7 Ondoeni chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu, kama vile mlivyo. Kwa maana Kristo, Mwana-Kondoo wetu wa Pasaka amekwisha tolewa kuwa dhabihu. 8 Kwa hiyo, tusiiadhimishe sikukuu hii, kwa chachu ya zamani, chachu ya nia mbaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu, ndio weupe wa moyo na kweli.
-
32 Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, si Mose aliyewapa mikate kutoka mbinguni, bali Baba yangu ndiye anawapa mkate wa kweli kutoka mbinguni. 33 Kwa maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”
-
1 Igeni mfano wangu, kama ninavyouiga mfano wa Kristo.
-
8 Lakini Mungu aliona kosa kwa watu, naye akasema:
“Siku zinakuja, asema Bwana,
nitakapofanya agano jipya
na nyumba ya Israeli
na nyumba ya Yuda.
9 Agano langu halitakuwa kama lile
nililofanya na baba zao
nilipowashika mkono
kuwaongoza watoke nchi ya Misri,
kwa sababu hawakuendelea kuwa waaminifu katika agano langu,
nami nikawaacha,
asema Bwana.
10 Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli
baada ya siku zile, asema Bwana.
Nitaziweka sheria zangu katika nia zao
na kuziandika mioyoni mwao.
Nitakuwa Mungu wao,
nao watakuwa watu wangu.
11 Mtu hatamfundisha tena jirani yake,
wala mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘Mjue Bwana,’
kwa sababu wote watanijua mimi,
tangu aliye mdogo kabisa kwao, hadi aliye mkuu sana.
12 Kwa sababu nitasamehe uovu wao,
wala sitazikumbuka dhambi zao tena!”
13 Kwa kuliita agano hili “jipya,” Mungu amefanya lile agano la kwanza kuwa kuukuu; nacho kitu kinachoanza kuchakaa na kuwa kikuukuu kiko karibu kutoweka.
Shows Read in context, Share and Copy.