101 Bible Verses About Evil

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Evil
  1. 10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi. 12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 13 Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara. 14 Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15 nayo miguu yenu ifungiwe utayari tuupatao kwa Injili ya amani. 16 Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17 Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho, ambao ni Neno la Mungu. 18 Mkiomba kwa Roho siku zote katika sala zote na maombi, mkikesha kila wakati mkiwaombea watakatifu wote.

    19 Niombeeni na mimi pia, ili kila nifunguapo kinywa changu, nipewe maneno ya kusema, niweze kutangaza siri ya Injili kwa ujasiri, 20 ambayo mimi ni balozi wake katika vifungo. Ombeni ili nipate kuhubiri kwa ujasiri kama inipasavyo.

  2. 20 Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. 21 Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, 22 tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu. 23 Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.”

  3. 12 Mtu mbaya sana na mlaghai,

    ambaye huzungukazunguka

    na maneno ya upotovu,

    13 ambaye anakonyeza kwa jicho lake,

    anayetoa ishara kwa miguu yake

    na kuashiria kwa vidole vyake,

    14 ambaye hupanga ubaya

    kwa udanganyifu moyoni mwake:

    daima huchochea fitina.

    15 Kwa hiyo maafa yatamkumba ghafula;

    ataangamizwa mara, pasipo msaada.

    16 Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana,

    naam, viko saba vilivyo chukizo kwake:

    17 macho ya kiburi,

    ulimi udanganyao,

    mikono imwagayo damu isiyo na hatia,

    18 moyo uwazao mipango miovu,

    miguu iliyo myepesi kukimbilia uovu,

    19 shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo,

    na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu.

  4. 7 Basi palikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na hilo joka, nalo joka pamoja na malaika zake likapigana nao. 8 Lakini joka na malaika zake wakashindwa, na hapakuwa tena na nafasi yao huko mbinguni. 9 Lile joka kuu likatupwa chini, yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani, aupotoshaye ulimwengu wote. Akatupwa chini duniani, yeye pamoja na malaika zake.

    10 Kisha nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema:

    “Sasa wokovu na uweza na Ufalme wa Mungu wetu umekuja

    na mamlaka ya Kristo wake.

    Kwa kuwa ametupwa chini

    mshtaki wa ndugu zetu,

    anayewashtaki mbele za Mungu

    usiku na mchana.

    11 Nao wakamshinda

    kwa damu ya Mwana-Kondoo

    na kwa neno la ushuhuda wao.

    Wala wao hawakuyapenda maisha yao

    hata kufa.

    12 Kwa hiyo, furahini ninyi mbingu

    na wote wakaao humo!

    Lakini ole wenu nchi na bahari,

    kwa maana huyo ibilisi ameshuka kwenu,

    akiwa amejaa ghadhabu,

    kwa sababu anajua ya kuwa

    muda wake ni mfupi!”

  5. 20 Badala yake:

    “Kama adui yako ana njaa, mlishe;

    kama ana kiu, mpe kinywaji.

    Kwa kufanya hivyo,

    unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.”

    21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.

  6. 34 Enyi uzao wa nyoka! Mnawezaje kunena mambo mema, wakati ninyi ni waovu? Kwa maana kinywa cha mtu huyanena yale yaliyoujaza moyo wake. 35 Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka hazina ya mambo mema yaliyohifadhiwa ndani yake, naye mtu mwovu hutoa yaliyo maovu kutoka hazina ya mambo maovu yaliyohifadhiwa ndani yake.

  7. 9 Upendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema.

  8. 26 Kwa sababu hii, Mungu aliwaacha wavunjiane heshima kwa kufuata tamaa zao za aibu. Hata wanawake wao wakabadili matumizi ya asili ya miili yao wakaitumia isivyokusudiwa. 27 Vivyo hivyo wanaume pia wakiacha matumizi ya asili ya wanawake wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wakafanyiana matendo ya aibu na wanaume wengine nao wakapata katika maisha yao adhabu iliyowastahili kwa ajili ya upotovu wao.

    28 Nao kwa kuwa hawakuona umuhimu wa kudumisha ufahamu wa Mungu, yeye akawaachilia wafuate akili za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa. 29 Wakiwa wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji, 30 wasingiziaji, wanaomchukia Mungu, wajeuri, wenye kiburi na majivuno, wenye hila, wasiotii wazazi wao, 31 wajinga, wasioamini, wasio na huruma na wakatili. 32 Ingawa wanafahamu sheria ya haki ya Mungu kwamba watu wanaofanya mambo kama hayo wanastahili mauti, si kwamba wanaendelea kutenda hayo tu, bali pia wanakubaliana na wale wanaoyatenda.

  9. 13 Mtu anapojaribiwa asiseme, “Ninajaribiwa na Mungu.” Kwa maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu wala yeye hamjaribu mtu yeyote. 14 Lakini kila mtu hujaribiwa wakati anapovutwa na kudanganywa na tamaa zake mwenyewe zilizo mbaya. 15 Basi ile tamaa mbaya ikishachukua mimba, huzaa dhambi, nayo ile dhambi ikikomaa, huzaa mauti.

  10. 38 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’ 39 Lakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu. Lakini kama mtu akikupiga kwenye shavu la kuume, mgeuzie na la pili pia. 40 Kama mtu akitaka kukushtaki na kuchukua joho lako, mwachie achukue na koti pia. 41 Kama mtu akikulazimisha kwenda maili moja, nenda naye maili mbili. 42 Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa.

    43 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’ 44 Lakini ninawaambia: Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi, 45 ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. 46 Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo? 47 Nanyi kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu, hawafanyi hivyo? 48 Kwa hiyo kuweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

  11. 13 Kumcha Bwana ni kuchukia uovu;

    ninachukia kiburi na majivuno,

    tabia mbaya na mazungumzo potovu.

  12. 14 Tafuteni mema, wala si mabaya,

    ili mpate kuishi.

    Ndipo Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote atakuwa pamoja nanyi,

    kama msemavyo yupo nanyi.

    15 Yachukieni maovu, yapendeni mema;

    dumisheni haki mahakamani.

    Yamkini Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote

    atawahurumia mabaki ya Yosefu.

  13. 13 Usitutie majaribuni,

    bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu

    [kwa kuwa Ufalme ni wako, na nguvu,

    na utukufu, hata milele. Amen].’

  14. 21 Jaribuni kila kitu. Yashikeni yaliyo mema. 22 Jiepusheni na uovu wa kila namna.

  15. 5 Vivyo hivyo ulimi ni kiungo kidogo sana katika mwili, lakini hujivuna majivuno makuu. Fikirini jinsi moto mdogo unavyoweza kuteketeza msitu mkubwa! 6 Ulimi pia ni moto, ndio ulimwengu wa uovu kati ya viungo vya mwili. Ulimi huutia mwili wote wa mtu unajisi na kuuwasha moto mfumo mzima wa maisha yake, nao wenyewe huchomwa moto wa jehanamu.

    7 Kwa maana kila aina ya wanyama, ndege, wanyama watambaao na viumbe vya baharini vinafugika na vimefugwa na binadamu, 8 lakini hakuna mtu awezaye kuufuga ulimi. Ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti.

    9 Kwa ulimi tunamhimidi Bwana, yaani Baba yetu, na kwa huo twawalaani watu walioumbwa kwa mfano wa Mungu. 10 Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haistahili kuwa hivyo.

  16. 5 Bwana akaona jinsi uovu wa mwanadamu ulivyokuwa mkubwa duniani, na ya kuwa kila mwelekeo wa mawazo ya moyo wake wakati wote ulikuwa mbaya tu. 6 Bwana akasikitika kwamba alimuumba mwanadamu duniani, moyo wa Mungu ukajaa masikitiko. 7 Kwa hiyo Bwana akasema, “Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemuumba kutoka kwenye uso wa dunia, wanadamu na wanyama, pamoja na viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Kwa maana nasikitika kuwaumba.”

  17. 20 Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe. 21 Lakini yule aishiye kwa ukweli huja kwenye nuru, ili ionekane wazi kwamba matendo yake yametendeka katika Mungu.”

  18. 29 Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao. 30 Wala msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwake mlitiwa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi. 31 Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu. 32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

  19. 23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.

  20. 10 Wale wanaompenda Bwana na wauchukie uovu,

    kwa maana yeye hulinda maisha ya waaminifu wake

    na kuwaokoa kutoka mkononi mwa mwovu.

  21. 1 Ole kwa wale wapangao uovu,

    kwa wale wafanyao shauri la hila vitandani mwao!

    Kunapopambazuka wanalitimiza

    kwa sababu uko katika uwezo wao kutekeleza.

  22. 1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini ambao Bwana Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati kweli Mungu alisema, ‘Kamwe msile matunda ya mti wowote wa bustanini’?”

    2 Mwanamke akamjibu nyoka, “Tunaweza kula matunda ya miti iliyoko bustanini, 3 lakini Mungu alisema, ‘Kamwe msile tunda la mti ulio katikati ya bustani, wala kuugusa, la sivyo mtakufa.’ ”

    4 Lakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa. 5 Kwa maana Mungu anajua ya kuwa wakati mtakapoyala, macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”

  23. 10 Kesho yake roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikaja kwa nguvu juu ya Sauli. Alikuwa akitabiri nyumbani mwake, wakati Daudi alikuwa akipiga kinubi, kama alivyozoea. Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake; 11 akautupa kwa nguvu, akijiambia mwenyewe, “Nitamchoma kwa mkuki abaki hapo ukutani.” Lakini Daudi akamkwepa mara mbili.

  24. 17 Vivyo hivyo, mti mwema huzaa matunda mazuri, na mti mbaya huzaa matunda mabaya. 18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. 19 Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. 20 Hivyo, mtawatambua kwa matunda yao.

    21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22 Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’ 23 Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’

  25. 1 Kwa hiyo, wekeni mbali nanyi uovu wote na udanganyifu wote, unafiki, wivu na masingizio ya kila namna. 2 Kama watoto wachanga, waliozaliwa sasa, yatamanini maziwa ya kiroho yasiyochanganywa na kitu kingine chochote, ili kwa hayo mpate kukua katika wokovu, 3 ikiwa kweli mmeonja ya kwamba Bwana ni mwema.

  26. 14 Hivyo Bwana Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hili,

    “Umelaaniwa kuliko wanyama wote

    wa kufugwa na wa porini!

    Utatambaa kwa tumbo lako

    na kula mavumbi

    siku zote za maisha yako.

    15 Nami nitaweka uadui

    kati yako na huyo mwanamke,

    na kati ya uzao wako na wake,

    yeye atakuponda kichwa,

    nawe utamuuma kisigino.”

    16 Kwa mwanamke akasema,

    “Nitakuzidishia sana utungu wakati wa kuzaa kwako;

    kwa utungu utazaa watoto.

    Tamaa yako itakuwa kwa mumeo

    naye atakutawala.”

    17 Kwa Adamu akasema, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka kwenye mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’

    “Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako,

    kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo

    siku zote za maisha yako.

    18 Itazaa miiba na mibaruti kwa ajili yako,

    nawe utakula mimea ya shambani.

    19 Kwa jasho la uso wako

    utakula chakula chako

    hadi utakaporudi ardhini,

    kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo,

    kwa kuwa wewe u mavumbi

    na mavumbini wewe utarudi.”

  27. 14 Aache uovu, atende mema,

    aitafute amani na kuifuatilia.

  28. 16 Uso wa Bwana uko kinyume na watendao maovu,

    ili kufuta kumbukumbu lao duniani.

  29. 11 “Bali kwenu ninyi mnaomwacha Bwana

    na kuusahau mlima wangu mtakatifu,

    ninyi mnaoandaa meza kwa ajili ya Bahati,

    na kujaza mabakuli ya mvinyo uliochanganywa

    kwa ajili ya Ajali,

    12 nitawaagiza mfe kwa upanga,

    nanyi nyote mtainama chini ili kuchinjwa;

    kwa kuwa niliwaita lakini hamkuitika,

    nilisema lakini hamkusikiliza.

    Mlitenda maovu machoni pangu,

    nanyi mkachagua mambo yale yanayonichukiza.”

  30. 15 Petro akasema, “Tueleze maana ya huu mfano.”

    16 Yesu akawauliza, “Je, bado ninyi hamfahamu? 17 Je, hamwelewi kwamba chochote kiingiacho kinywani huenda tumboni, na hatimaye hutolewa nje kikiwa uchafu? 18 Lakini kitokacho kinywani hutoka moyoni, na hiki ndicho kimtiacho mtu unajisi. 19 Kwa maana ndani ya moyo hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na masingizio. 20 Haya ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.”

  31. 6 Kwa maana Mungu atamlipa kila mtu sawasawa na matendo yake. 7 Wale ambao kwa kuvumilia katika kutenda mema hutafuta utukufu, heshima na maisha yasiyoharibika, Mungu atawapa uzima wa milele. 8 Lakini kwa wale watafutao mambo yao wenyewe na wale wanaokataa kweli na kuzifuata njia mbaya, kutakuwa na ghadhabu na hasira ya Mungu. 9 Kutakuwa na taabu na dhiki kwa kila mmoja atendaye maovu, Myahudi kwanza na mtu wa Mataifa pia, 10 bali utukufu, heshima na amani kwa ajili ya kila mmoja atendaye mema, kwa Myahudi kwanza, kisha kwa mtu wa Mataifa. 11 Kwa maana Mungu hana upendeleo.

  32. 1 Kila mtu na atii mamlaka inayotawala, kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu, nazo mamlaka zilizopo zimewekwa na Mungu. 2 Kwa hiyo yeye anayeasi dhidi ya mamlaka inayotawala anaasi dhidi ya kile kilichowekwa na Mungu, nao wale wafanyao hivyo watajiletea hukumu juu yao wenyewe. 3 Kwa kuwa watawala hawawatishi watu wale wanaotenda mema bali wale wanaotenda mabaya. Je, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Basi tenda lile lililo jema naye atakusifu. 4 Kwa maana mwenye mamlaka ni mtumishi wa Mungu kwa ajili ya mema. Lakini kama ukitenda mabaya, basi ogopa, kwa kuwa hauinui upanga bila sababu. Yeye ni mtumishi wa Mungu, mjumbe wa Mungu wa kutekeleza adhabu juu ya watenda mabaya.

  33. 4 Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. 5 Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. 6 Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. 7 Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.

  34. 21 Bwana akasikia harufu nzuri ya kupendeza, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena ardhi kwa sababu ya mwanadamu, hata ingawa kila mwelekeo wa moyo wake ni mbaya tangu ujana. Kamwe sitaangamiza tena viumbe hai vyote kama nilivyofanya.

  35. Zaburi ya Daudi.

    1 Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu,

    wala usiwaonee wivu watendao mabaya,

    2 kwa maana kama majani watanyauka mara,

    kama mimea ya kijani watakufa mara.

    3 Mtumaini Bwana na utende yaliyo mema;

    Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama.

    4 Jifurahishe katika Bwana

    naye atakupa haja za moyo wako.

    5 Mkabidhi Bwana njia yako,

    mtumaini yeye, naye atatenda hili:

    6 Yeye atafanya haki yako ingʼae kama mapambazuko,

    na hukumu ya shauri lako kama jua la adhuhuri.

    7 Tulia mbele za Bwana

    na umngojee kwa uvumilivu;

    usisumbuke watu wanapofanikiwa katika njia zao,

    wanapotekeleza mipango yao miovu.

  36. 15 Siombi kwamba uwaondoe ulimwenguni, bali uwalinde dhidi ya yule mwovu.

  37. 15 Kwa hiyo angalieni sana jinsi mnavyoenenda, si kama watu wasio na hekima, bali kama wenye hekima, 16 mkiukomboa wakati, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu. 17 Kwa hiyo msiwe wajinga, bali mpate kujua nini mapenzi ya Bwana.

  38. 13 Ni nani aliye na hekima na ufahamu miongoni mwenu? Basi na aionyeshe hiyo kwa maisha yake mema na kwa matendo yake yaliyotendwa kwa unyenyekevu utokanao na hekima. 14 Lakini ikiwa mna wivu na ni wenye chuki na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu kwa ajili ya hayo wala msiikatae kweli. 15 Hekima ya namna hiyo haishuki kutoka mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyo ya kiroho, na ya kishetani. 16 Kwa maana panapokuwa na wivu na ubinafsi, ndipo penye machafuko na uovu wa kila namna.

    17 Lakini hekima itokayo mbinguni kwanza ni safi, kisha inapenda amani, tena ni ya upole, iliyo tayari kusikiliza wengine kwa unyenyekevu, iliyojaa huruma na matunda mema, isiyopendelea mtu, tena isiyokuwa na unafiki. 18 Mavuno ya haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.

  39. 9 Msilipe ovu kwa ovu, au jeuri kwa jeuri, bali barikini, kwa maana hili ndilo mliloitiwa ili mpate kurithi baraka. 10 Kwa maana,

    “Yeyote apendaye uzima

    na kuona siku njema,

    basi auzuie ulimi wake usinene mabaya,

    na midomo yake isiseme hila.

    11 Mtu huyo lazima aache uovu, akatende mema;

    lazima aitafute amani na kuifuatilia sana.

    12 Kwa maana macho ya Bwana

    huwaelekea wenye haki,

    na masikio yake yako makini

    kusikiliza maombi yao.

    Bali uso wa Bwana uko kinyume

    na watendao maovu.”

  40. 8 Yeye atendaye dhambi ni wa ibilisi, kwa sababu ibilisi amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili aziangamize kazi za ibilisi.

  41. 18 Tunajua ya kuwa yeye aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, bali aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hawezi kumdhuru. 19 Sisi twajua kuwa tu watoto wa Mungu na ya kwamba ulimwengu wote uko chini ya utawala wa yule mwovu.

  42. 14 Basi Roho wa Bwana alikuwa ameondoka kwa Sauli, nayo roho mbaya ikaachiwa nafasi na Bwana ili imtese.

    15 Watumishi wa Sauli wakamwambia, “Angalia, roho mbaya imeachiwa nafasi na Bwana nayo inakutesa. 16 Basi bwana wetu na aamuru watumishi wake walioko hapa kutafuta mtu ambaye anaweza kupiga kinubi. Atakipiga kinubi wakati roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikujiapo, nawe utajisikia vizuri.”

  43. 4 Hata kama nikipita katikati

    ya bonde la uvuli wa mauti,

    sitaogopa mabaya,

    kwa maana wewe upo pamoja nami;

    fimbo yako na mkongojo wako

    vyanifariji.

  44. 13 Ikiwa mtu atalipa baya kwa jema,

    kamwe ubaya hautaondoka katika nyumba yake.

  45. 20 Bila kuni moto huzimika;

    pasipo uchongezi ugomvi humalizika.

    21 Kama makaa juu ya makaa yanayowaka, na kama kuni kwenye moto,

    ndivyo alivyo mtu mgomvi kwa kuchochea ugomvi.

    22 Maneno ya mchongezi ni kama chakula kitamu;

    huingia sehemu za ndani sana za mtu.

    23 Kama rangi ingʼaayo iliyopakwa kwenye vyombo vya udongo

    ndivyo ilivyo midomo laini pamoja na moyo mbaya.

  46. 3 Huu ni ubaya ulio katika kila kitu kinachotendeka chini ya jua: Mwisho unaofanana huwapata wote. Zaidi ya hayo, mioyo ya watu, imejaa ubaya na kuna wazimu mioyoni mwao wangali hai, hatimaye huungana na waliokufa.

  47. 1 “Hakika siku inakuja, itawaka kama tanuru. Wote wenye kiburi na kila mtenda mabaya watakuwa mabua makavu, na siku ile inayokuja itawawasha moto,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. “Hakuna mzizi wala tawi litakalosalia kwao.

  48. 43 “Pepo mchafu amtokapo mtu, hutangatanga katika sehemu zisizo na maji akitafuta mahali pa kupumzika, lakini hapati. 44 Ndipo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba yangu nilikotoka.’ Naye arudipo huikuta ile nyumba ikiwa tupu, imefagiliwa na kupangwa vizuri. 45 Kisha huenda na kuwaleta pepo wachafu wengine saba wabaya kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo. Nayo hali ya mwisho ya yule mtu huwa ni mbaya kuliko ile ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kiovu.”

  49. 10 Hivyo wale walioajiriwa kwanza walipofika, walidhani watalipwa zaidi. Lakini kila mmoja wao pia alipokea dinari moja. 11 Walipoipokea, wakaanza kulalamika dhidi ya yule mwenye shamba, 12 wakisema, ‘Hawa watu walioajiriwa mwisho wamefanya kazi kwa muda wa saa moja tu, nawe umewafanya sawa na sisi ambao tumestahimili taabu na joto lote la mchana kutwa?’

    13 “Yule mwenye shamba akamjibu mmoja wao, ‘Rafiki, sijakudhulumu. Je, hukukubaliana nami kwa ujira wa kawaida wa dinari moja? 14 Chukua ujira wako na uende. Mimi nimeamua kumlipa huyu mtu aliyeajiriwa mwisho kama nilivyokupa wewe. 15 Je, sina haki yangu kufanya kile nitakacho na mali yangu mwenyewe? Au unaona wivu kwa kuwa nimekuwa mkarimu?’

    16 “Vivyo hivyo, wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”

  50. 45 “Ni nani basi aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake amemweka kusimamia watumishi wengine katika nyumba yake, ili awape chakula chao kwa wakati unaofaa? 46 Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo. 47 Amin, nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote. 48 Lakini kama huyo mtumishi ni mwovu, naye akasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu atakawia muda mrefu,’ 49 kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, na kula na kunywa pamoja na walevi. 50 Basi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. 51 Atamkata vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wanafiki, mahali ambako kutakuwa ni kulia na kusaga meno.

  51. 31 “Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti cha enzi cha utukufu wake. 32 Mataifa yote watakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi. 33 Atawaweka kondoo upande wake wa kuume, na mbuzi upande wake wa kushoto.

    34 “Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njooni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu; urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 35 Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, 36 nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’

    37 “Ndipo wale wenye haki watakapomjibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha? 38 Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha, au ukiwa uchi tukakuvika? 39 Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza, au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’

    40 “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’

    41 “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. 42 Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, 43 nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza, na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’

    44 “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’

    45 “Naye atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’

    46 “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”

  52. 23 Basi Yesu akawaita na kuzungumza nao kwa mifano akasema: “Shetani awezaje kumtoa Shetani? 24 Kama ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama. 25 Nayo nyumba kama ikigawanyika dhidi yake yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama. 26 Naye Shetani kama akijipinga mwenyewe na awe amegawanyika, hawezi kusimama bali mwisho wake umewadia. 27 Hakuna mtu yeyote awezaye kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu. Ndipo ataweza kuteka nyara mali zake. 28 Amin, nawaambia, dhambi zote na makufuru yote ya wanadamu watasamehewa. 29 Lakini yeyote anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa kamwe, atakuwa na hatia ya dhambi ya milele.”

    30 Yesu alisema hivi kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”

  53. 6 Majivuno yenu si mazuri. Je, hamjui ya kwamba chachu kidogo huchachusha donge zima la unga? 7 Ondoeni chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu, kama vile mlivyo. Kwa maana Kristo, Mwana-Kondoo wetu wa Pasaka amekwisha tolewa kuwa dhabihu.

  54. 14 Msifungiwe nira pamoja na watu wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa, kwa maana pana uhusiano gani kati ya haki na uovu? Au kuna ushirika gani kati ya nuru na giza? 15 Kuna mapatano gani kati ya Kristo na Beliari? Yeye aaminiye ana sehemu gani na yeye asiyeamini? 16 Kuna mapatano gani kati ya Hekalu la Mungu na sanamu? Kwa kuwa sisi tu Hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu alivyosema: “Nitakaa pamoja nao na kutembea katikati yao, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.”

    17 “Kwa hiyo tokeni miongoni mwao,

    mkatengwe nao,

    asema Bwana.

    Msiguse kitu chochote kilicho najisi,

    nami nitawakaribisha.”

    18 “Mimi nitakuwa Baba kwenu,

    nanyi mtakuwa wanangu na binti zangu,

    asema Bwana Mwenyezi.”

  55. 7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. 8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.

  56. 21 Kama hivyo ndivyo ilivyo, ninyi mmemsikia, tena mmefundishwa naye, vile kweli ilivyo katika Yesu. 22 Mlifundishwa kuuvua mwenendo wenu wa zamani, utu wenu wa kale, ulioharibiwa na tamaa zake za udanganyifu, 23 ili mfanywe upya roho na nia zenu, 24 mkajivike utu mpya, ulioumbwa sawasawa na mfano wa Mungu katika haki yote na utakatifu.

    25 Kwa hiyo kila mmoja wenu avue uongo na kuambiana kweli mtu na jirani yake, kwa maana sisi sote tu viungo vya mwili mmoja. 26 Mkikasirika, msitende dhambi, wala jua lisichwe mkiwa bado mmekasirika, 27 wala msimpe ibilisi nafasi.

  57. 1 Roho asema waziwazi kwamba katika siku za mwisho baadhi ya watu wataiacha imani na kufuata roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani. 2 Mafundisho kama hayo huja kupitia kwa waongo ambao ni wanafiki, hali dhamiri zao zikiungua kwa kuchomwa moto. 3 Wao huwakataza watu wasioe na kuwaagiza wajiepushe na vyakula fulani, ambavyo Mungu aliviumba ili vipokewe kwa shukrani na wale wanaoamini na kuijua kweli. 4 Kwa maana kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, wala hakuna kitu chochote cha kukataliwa kama kikipokewa kwa shukrani, 5 kwa sababu kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.

  58. 10 Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.

  59. 9 Jihadhari usijiwekee wazo hili ovu: “Mwaka wa saba, mwaka wa kufuta madeni umekaribia,” usije ukaonyesha nia mbaya kwa ndugu yako mhitaji na ukaacha kumpa chochote. Anaweza kumlalamikia Bwana dhidi yako nawe utakuwa umepatikana na hatia ya dhambi.

  60. 1 Baada ya Ehudi kufa, Waisraeli wakafanya tena maovu machoni pa Bwana. 2 Hivyo Bwana akawatia mikononi mwa Yabini, mfalme wa Kanaani, aliyetawala huko Hazori. Jemadari wa jeshi lake alikuwa Sisera, aliyeishi huko Haroshethi-Hagoyimu

  61. 23 Mungu akaruhusu roho mbaya kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu, nao watu wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa hila.

  62. 6 Siku moja wana wa Mungu walikwenda kujionyesha mbele za Bwana. Shetani naye akaja pamoja nao. 7 Bwana akamwambia Shetani, “Umetoka wapi?”

    Shetani akamjibu Bwana, “Natoka kuzunguka pote duniani, nikitembea huku na huko humo.”

    8 Ndipo Bwana akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Hakuna mtu mwingine duniani aliye kama yeye, asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu, na kuepukana na uovu.”

    9 Shetani akamjibu Bwana, “Je, Ayubu anamcha Mungu bure? 10 Je, wewe hukumjengea boma pande zote yeye na wa nyumbani mwake pamoja na kila kitu alicho nacho? Kazi za mikono yake umezibariki na hivyo makundi yake ya kondoo na mbuzi pamoja na ya wanyama yameenea katika nchi nzima. 11 Lakini nyoosha mkono wako na kupiga kila kitu alicho nacho, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.”

  63. 7 Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe;

    mche Bwana ukajiepushe na uovu.

    8 Hii itakuletea afya mwilini mwako,

    na mafuta kwenye mifupa yako.

  64. 27 Usigeuke kulia wala kushoto;

    epusha mguu wako na ubaya.

  65. 2 Hata hivyo yeye pia ana hekima na anaweza kuleta maafa,

    wala hayatangui maneno yake.

    Yeye atainuka dhidi ya nyumba ya mwovu,

    dhidi ya wale ambao huwasaidia watenda mabaya.

  66. 7 Miguu yao hukimbilia kwenye dhambi,

    ni myepesi kumwaga damu isiyo na hatia.

    Mawazo yao ni mawazo maovu;

    uharibifu na maangamizi huonekana katika njia zao.

    8 Hawajui njia ya amani,

    hakuna haki katika mapito yao.

    Wameyageuza kuwa njia za upotovu,

    hakuna apitaye njia hizo atakayeifahamu amani.

  67. 37 ‘Ndiyo’ yenu iwe ‘Ndiyo,’ na ‘Hapana’ yenu iwe ‘Hapana.’ Lolote zaidi ya hili latoka kwa yule mwovu.

  68. 23 Lakini kama jicho lako ni ovu, mwili wako wote utajawa na giza. Kwa hiyo basi, kama nuru iliyomo ndani yako ni giza, hilo ni giza kuu namna gani!

  69. 19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

  70. 15 Angalieni kuwa mtu asimlipe mwenzake maovu kwa maovu, bali siku zote tafuteni kutendeana mema ninyi kwa ninyi na kwa watu wote.

  71. 1 Waisraeli wakafanya tena yaliyo maovu mbele za Bwana, naye kwa miaka saba Bwana akawatia mikononi mwa Wamidiani.

  72. 7 Watu waovu huondolewa na kutoweka,

    bali nyumba ya mwenye haki husimama imara.

  73. 6 Usile chakula cha mtu mchoyo,

    usitamani vyakula vyake vitamu,

    7 kwa maana yeye ni aina ya mtu

    ambaye kila mara anafikiri juu ya gharama.

    Anakuambia, “Kula na kunywa,”

    lakini moyo wake hauko pamoja nawe.

    8 Utatapika kile kidogo ulichokula,

    nawe utakuwa umepoteza bure

    maneno yako ya kumsifu.

  74. 20 Ole wao wanaoita ubaya ni wema,

    na wema ni ubaya,

    wawekao giza badala ya nuru,

    na nuru badala ya giza,

    wawekao uchungu badala ya utamu,

    na utamu badala ya uchungu.

  75. 9 Kuhusu manabii:

    Moyo wangu umevunjika ndani yangu;

    mifupa yangu yote inatetemeka.

    Nimekuwa kama mtu aliyelewa,

    kama mtu aliyelemewa na divai,

    kwa sababu ya Bwana

    na maneno yake matakatifu.

    10 Nchi imejaa wazinzi;

    kwa sababu ya laana, nchi imekauka

    na malisho yaliyoko nyikani yamekauka.

    Mwenendo wa manabii ni mbaya

    na mamlaka yao si ya haki.

    11 “Nabii na kuhani wote si wacha Mungu;

    hata hekaluni mwangu ninaona uovu wao,”

    asema Bwana.

    12 “Kwa hiyo mapito yao yatakuwa utelezi,

    watafukuziwa mbali gizani

    na huko wataanguka.

    Nitaleta maafa juu yao

    katika mwaka wa kuadhibiwa kwao,”

    asema Bwana.

    13 “Miongoni mwa manabii wa Samaria

    nililiona jambo la kuchukiza:

    Walitabiri kwa Baali

    na kuwapotosha Israeli watu wangu.

    14 Nako miongoni mwa manabii wa Yerusalemu

    nimeona jambo baya sana:

    Wanafanya uzinzi

    na kuenenda katika uongo.

    Wanatia nguvu mikono ya watenda mabaya,

    kwa ajili hiyo hakuna yeyote

    anayeachana na uovu wake.

    Wote wako kama Sodoma kwangu;

    watu na Yerusalemu wako kama Gomora.”

  76. 11 “Heri ninyi watu watakapowashutumu, na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu. 12 Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo walivyowatesa manabii waliokuwa kabla yenu.

  77. 3 Petro akamuuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? 4 Je, kabla hujauza hicho kiwanja si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, fedha ulizopata si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu bali Mungu.”

  78. 8 Tunajua kwamba sheria ni njema ikiwa inatumika kwa halali kama ilivyokusudiwa. 9 Lakini tunajua ya kuwa sheria si kwa ajili ya wenye haki, bali kwa ajili ya wavunja sheria na waasi, kwa ajili ya wasiomcha Mungu na wenye dhambi, wasio watakatifu na wanaokufuru; kwa wale wawauao baba zao au mama zao, kwa wauaji, 10 kwa wazinzi na wahanithi, kwa wale wauzao watu, na kwa waongo na waapao kwa uongo, na kwa chochote kingine kilicho kinyume na mafundisho ya kweli, 11 ambayo yanakubaliana na Injili ya utukufu wa Mungu anayehimidiwa, ambayo mimi nimewekewa amana.

  79. 2 Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3 kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. 4 Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu chochote.

  80. 7 Yeye ashindaye atayarithi haya yote, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. 8 Lakini waoga, wasioamini, wachafu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, pamoja na waongo wote, mahali pao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”

  81. 13 Usiue.

    14 Usizini.

    15 Usiibe.

    16 Usimshuhudie jirani yako uongo.

    17 Usiitamani nyumba ya jirani yako. Usimtamani mke wa jirani yako, wala mtumishi wake wa kiume au wa kike, wala ngʼombe wake au punda wake, wala chochote kile alicho nacho jirani yako.”

  82. 12 Yeyote kati yenu anayependa uzima

    na kutamani kuziona siku nyingi njema,

    13 basi auzuie ulimi wake na mabaya,

    na midomo yake kutokana na kusema uongo.

  83. 9 Kwa maana waovu watakatiliwa mbali,

    bali wale wanaomtumaini Bwana watairithi nchi.

  84. 16 jiosheni na mkajitakase.

    Yaondoeni matendo yenu maovu

    mbele zangu!

    Acheni kutenda mabaya,

    17 jifunzeni kutenda mema!

    Tafuteni haki,

    watieni moyo walioonewa.

    Teteeni shauri la yatima,

    wateteeni wajane.

  85. 9 Moyo ni mdanganyifu kuliko vitu vyote,

    ni mwovu kupita kiasi.

    Ni nani awezaye kuujua?

    10 “Mimi Bwana huchunguza moyo

    na kuzijaribu nia,

    ili kumlipa mtu kwa kadiri ya mwenendo wake,

    kwa kadiri ya matendo yake yanavyostahili.”

  86. 1 Kisha Yesu akaongozwa na Roho Mtakatifu kwenda nyikani ili akajaribiwe na ibilisi.

  87. 39 Lakini yeye akawajibu, “Kizazi kiovu na cha uzinzi kinaomba ishara! Lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ishara ya nabii Yona.

  88. 23 Wakati huo huo katika sinagogi lao palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, 24 naye akapiga kelele akisema, “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”

    25 Lakini Yesu akamkemea, akamwambia, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!” 26 Yule pepo mchafu akamtikisatikisa huyo mtu kwa nguvu, kisha akamtoka akipiga kelele kwa sauti kubwa.

    27 Watu wote wakashangaa, hata wakaulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!”

  89. 13 Je, kile kilicho chema basi kilikuwa mauti kwangu? La, hasha! Lakini ili dhambi itambuliwe kuwa ni dhambi, ilileta mauti ndani yangu kupitia kile kilichokuwa chema, ili kwa njia ya amri dhambi izidi kuwa mbaya kupita kiasi.

    14 Kwa maana tunajua kwamba sheria ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kimwili nikiwa nimeuzwa kwenye utumwa wa dhambi. 15 Sielewi nitendalo, kwa maana lile ninalotaka kulitenda, silitendi, lakini ninatenda lile ninalolichukia. 16 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, ni kwamba ninakubali kuwa sheria ni njema. 17 Lakini, kwa kweli si mimi tena nitendaye lile nisilotaka bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. 18 Kwa maana ninafahamu kwamba hakuna jema lolote likaalo ndani yangu, yaani, katika asili yangu ya dhambi. Kwa kuwa nina shauku ya kutenda lililo jema, lakini siwezi kulitenda. 19 Sitendi lile jema nitakalo kutenda, bali lile baya nisilolitaka, ndilo nitendalo. 20 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, si mimi tena nifanyaye hivyo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.

  90. 20 La hasha! Lakini kafara za watu wasiomjua Mungu hutolewa kwa mashetani, wala si kwa Mungu. Nami sitaki ninyi mwe na ushirika na mashetani. 21 Hamwezi kunywa katika kikombe cha Bwana na cha mashetani pia. Hamwezi kuwa na sehemu katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani pia.

  91. 33 Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.”

  92. 1 Kwa habari zenu, mlikuwa wafu katika makosa na dhambi zenu, 2 ambazo mlizitenda mlipofuatisha namna ya ulimwengu huu na za yule mtawala wa ufalme wa anga, yule roho atendaye kazi sasa ndani ya wale wasiotii. 3 Sisi sote pia tuliishi katikati yao hapo zamani, tukitimiza tamaa za asili yetu ya dhambi na kufuata tamaa zake na mawazo yake. Nasi kwa asili tulikuwa wana wa ghadhabu, kama mtu mwingine yeyote. 4 Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema, 5 hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema. 6 Mungu alitufufua pamoja na Kristo na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu, 7 ili katika ule ulimwengu ujao apate kuonyesha wingi wa neema yake isiyopimika, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Kristo Yesu. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

  93. 11 Msishiriki matendo ya giza yasiyofaa, bali yafichueni. 12 Kwa maana ni aibu hata kutaja mambo yale ambayo wasiotii wanayafanya sirini.

  94. 18 Bwana ataniokoa katika kila shambulio baya na kunileta salama katika Ufalme wake wa mbinguni. Atukuzwe yeye milele na milele. Amen.

  95. 21 Kwa hiyo, ondoleeni mbali uchafu wote na uovu ambao umezidi kuwa mwingi, mkalipokee kwa unyenyekevu lile Neno lililopandwa ndani yenu ambalo laweza kuokoa nafsi zenu.

  96. 7 Basi mtiini Mungu. Mpingeni ibilisi, naye atawakimbia.

  97. 8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza.

  98. 11 Hili ndilo neno mlilolisikia tangu mwanzo: Kwamba imetupasa tupendane sisi kwa sisi. 12 Msiwe kama Kaini aliyekuwa wa yule mwovu akamuua ndugu yake. Basi kwa nini alimuua? Ni kwa sababu matendo yake Kaini yalikuwa mabaya na ya ndugu yake yalikuwa ya haki.

  99. 14 Usiuweke mguu wako katika njia ya waovu

    wala usitembee katika njia ya watu wabaya.

    15 Epukana nayo, usisafiri katika njia hiyo;

    achana nayo, na uelekee njia yako.

  100. 9 “Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Fanyeni hukumu za haki, onyesheni rehema na huruma ninyi kwa ninyi. 10 Msimwonee mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’

  101. 11 Lakini Petro alipofika Antiokia, mimi nilimpinga ana kwa ana kwa sababu alikuwa amekosea kwa wazi. 12 Kabla baadhi ya watu waliotoka kwa Yakobo hawajafika, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa. Lakini hao watu walipofika alianza kujiondoa na kujitenga na watu wa Mataifa kwa sababu aliwaogopa wale wa kundi la tohara. 13 Pia Wayahudi wengine waliungana naye katika unafiki huu, hata Barnaba naye akapotoshwa na unafiki wao.

    14 Nilipoona kwamba hawatendi sawasawa na kweli ya Injili, nilimwambia Petro mbele ya wote, “Wewe ni Myahudi, nawe unaishi kama mtu wa Mataifa na wala si kama Myahudi. Imekuwaje basi, mnawalazimisha watu wa Mataifa kufuata desturi za Kiyahudi?