53 Bible Verses About Kids

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Kids
  1. 1 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, kwa kuwa hili ni jema. 2 “Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi, 3 “upate baraka na uishi siku nyingi duniani.”

    4 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana.

  2. 3 Wana ni urithi utokao kwa Bwana,

    watoto ni zawadi kutoka kwake.

    4 Kama mishale mikononi mwa shujaa

    ndivyo walivyo wana awazaao mtu katika ujana wake.

    5 Heri mtu ambaye podo lake

    limejazwa nao.

    Hawataaibishwa wanaposhindana

    na adui zao langoni.

  3. 1 Wakati huo, wanafunzi wakamjia Yesu na kumuuliza, “Je, nani aliye mkuu kuliko wote katika Ufalme wa Mbinguni?”

    2 Yesu akamwita mtoto mdogo na kumsimamisha katikati yao. 3 Naye akasema: “Amin, nawaambia, msipookoka na kuwa kama watoto wadogo, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni. 4 Kwa hiyo mtu yeyote anyenyekeaye kama huyu mtoto, ndiye aliye mkuu kuliko wote katika Ufalme wa Mbinguni.

    5 “Yeyote amkaribishaye mtoto mdogo kama huyu kwa Jina langu, anikaribisha mimi. 6 Lakini kama mtu yeyote akimsababisha mmojawapo wa hawa wadogo wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa katika kilindi cha bahari.

  4. 13 Watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wake wakawakemea. 14 Yesu alipoona yaliyokuwa yakitukia, akachukizwa. Akawaambia wanafunzi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa. 15 Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.” 16 Akawachukua watoto mikononi mwake, akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.

  5. 13 Kisha watoto wadogo wakaletwa kwa Yesu ili aweke mikono yake juu yao na awaombee. Lakini wanafunzi wake wakawakemea wale waliowaleta.

    14 Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mbinguni ni wa wale walio kama hawa.” 15 Naye akaweka mikono yake juu yao, na akaondoka huko.

  6. 6 Mfundishe mtoto njia impasayo kuiendea,

    naye hataiacha hata akiwa mzee.

  7. 20 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote, kwa maana hivi ndivyo inavyompendeza Bwana.

    21 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

  8. 33 Basi wakafika Kapernaumu na baada ya kuingia nyumbani akawauliza, “Mlikuwa mnabishana nini kule njiani?” 34 Lakini hawakumjibu, kwa sababu njiani walikuwa wakibishana kuhusu nani miongoni mwao alikuwa mkuu zaidi ya wote.

    35 Akaketi chini, akawaita wote kumi na wawili, akawaambia: “Kama mtu yeyote akitaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa wa mwisho na mtumishi wa wote.”

    36 Kisha akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha katikati yao. Akamkumbatia, akawaambia, 37 “Mtu yeyote amkaribishaye mmoja wa hawa watoto wadogo kwa Jina langu, anikaribisha mimi. Naye anikaribishaye mimi, amkaribisha Baba yangu aliyenituma.”

  9. 8 Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako,

    wala usiyaache mafundisho ya mama yako.

    9 Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako,

    na mkufu wa kuipamba shingo yako.

  10. 5 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. 6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. 7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo. 8 Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako. 9 Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.

  11. 14 Vipofu na vilema wakamwendea kule Hekaluni, naye akawaponya. 15 Lakini viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walipoona mambo ya ajabu aliyofanya na kuwasikia watoto wakishangilia katika eneo la Hekalu wakisema, “Hosana Mwana wa Daudi,” walikasirika.

    16 Wakamuuliza Yesu, “Je, unasikia hayo hawa wanayosema?”

    Akawajibu, “Naam; kwani hamkusoma,

    “ ‘Midomoni mwa watoto wachanga na wanyonyao

    umeamuru sifa’?”

  12. 12 Waheshimu baba yako na mama yako, ili upate kuishi siku nyingi katika nchi anayokupa Bwana Mungu wako.

  13. 7 Vumilieni taabu kwa ajili ya kufunzwa adabu. Mungu anawatendea ninyi kama watoto wake, kwa maana ni mtoto yupi asiyeadibishwa na mzazi wake? 8 Kama hakuna kuadibishwa (ambalo ni fungu la watoto wote), basi ninyi ni watoto wa haramu wala si watoto halali. 9 Tena, sisi sote tunao baba wa kimwili, waliotuadibisha nasi tukawaheshimu kwa ajili ya hilo. Je, si inatupasa kujinyenyekeza zaidi kwa Baba wa roho zetu ili tuishi? 10 Baba zetu walituadibisha kwa kitambo kidogo kama wao wenyewe walivyoona vyema, lakini Mungu hutuadibisha kwa faida yetu ili tupate kushiriki utakatifu wake. 11 Kuadibishwa wakati wowote hakuonekani kuwa kitu cha kufurahisha bali chenye maumivu kinapotekelezwa. Lakini baadaye huzaa matunda ya haki na amani kwa wale waliofunzwa nayo.

  14. 11 Kama nikisema, “Hakika giza litanificha

    na nuru inayonizunguka iwe usiku,”

    12 hata giza halitakuwa giza kwako,

    usiku utangʼaa kama mchana,

    kwa kuwa giza ni kama nuru kwako.

    13 Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani;

    uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu.

    14 Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa

    kwa namna ya ajabu na ya kutisha;

    kazi zako ni za ajabu,

    ninajua hayo kikamilifu.

    15 Umbile langu halikufichika kwako,

    nilipoumbwa mahali pa siri.

    Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi,

    16 macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika.

    Siku zangu zote ulizonipangia

    ziliandikwa katika kitabu chako

    kabla haijakuwepo hata moja.

  15. 15 Pia, watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wachanga ili awaguse. Wanafunzi wake walipoona hivyo, wakawakemea. 16 Lakini Yesu akawaita wale watoto waje kwake, akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa. 17 Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”

  16. 15 Upumbavu umefungwa ndani ya moyo wa mtoto,

    bali fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali naye.

  17. 17 Mrudi mwanao, naye atakupa amani,

    atakufurahisha nafsi yako.

  18. 46 Kukazuka mabishano miongoni mwa wanafunzi kuhusu ni nani miongoni mwao atakayekuwa mkuu kuliko wote. 47 Lakini Yesu akayatambua mawazo yao, naye akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha kando yake. 48 Kisha akawaambia, “Yeyote amkaribishaye mtoto huyu mdogo kwa Jina langu, anikaribisha mimi, na yeyote atakayenikaribisha mimi, atakuwa amemkaribisha yeye aliyenituma. Kwa maana yeye aliye mdogo miongoni mwenu, ndiye aliye mkuu kuliko wote.”

  19. 15 Fimbo ya maonyo hutia hekima,

    bali mtoto aliyeachiwa bila maonyo

    humwaibisha mama yake.

  20. 24 Yeye aizuiaye fimbo yake hampendi mwanawe,

    bali yeye ampendaye

    huwa mwangalifu kumwadibisha.

  21. 15 “Yeyote amshambuliaye baba yake au mama yake ni lazima auawe.

    16 “Yeyote amtekaye nyara mwingine akamuuza au akamweka kwake, akikamatwa ni lazima auawe.

    17 “Yeyote atakayemlaani baba yake au mama yake ni lazima auawe.

  22. 6 Wana wa wana ni taji la wazee,

    nao wazazi ni fahari ya watoto wao.

  23. 11 Njooni, watoto wangu, mnisikilize,

    nitawafundisha kumcha Bwana.

  24. 5 Mpumbavu hubeza maonyo ya baba yake,

    bali yeyote akubaliye maonyo huonyesha busara.

  25. 32 “Basi sasa wanangu, nisikilizeni;

    heri wale wanaozishika njia zangu.

    33 Sikilizeni mafundisho yangu mwe na hekima;

    msiyapuuze.

  26. 11 Hata mtoto hujulikana kwa matendo yake,

    kama tabia yake ni safi na adili.

    12 Masikio yasikiayo na macho yaonayo,

    Bwana ndiye alivifanya vyote viwili.

  27. 16 Waheshimu baba yako na mama yako, kama Bwana Mungu wako alivyokuagiza, ili siku zako zipate kuwa nyingi na kufanikiwa katika nchi Bwana Mungu wako anayokupa.

  28. 1 Sikilizeni wanangu, mafundisho ya baba yenu;

    sikilizeni kwa makini na mpate ufahamu.

    2 Ninawapa mafundisho ya maana,

    kwa hiyo msiyaache mafundisho yangu.

    3 Nilipokuwa mvulana mdogo katika nyumba ya baba yangu,

    ningali mchanga na mtoto pekee kwa mama yangu,

    4 baba alinifundisha akisema,

    “Yashike maneno yangu yote kwa moyo wako wote;

    yashike maagizo yangu na wewe utaishi.

    5 Pata hekima, pata ufahamu;

    usiyasahau maneno yangu wala usiyaache.

    6 Usimwache hekima naye atakuweka salama;

    mpende, naye atakulinda.

    7 Hekima ni bora kuliko vitu vyote; kwa hiyo jipe hekima.

    Hata ikikugharimu vyote ulivyo navyo, pata ufahamu.

  29. 1 Kwa hiyo, wekeni mbali nanyi uovu wote na udanganyifu wote, unafiki, wivu na masingizio ya kila namna. 2 Kama watoto wachanga, waliozaliwa sasa, yatamanini maziwa ya kiroho yasiyochanganywa na kitu kingine chochote, ili kwa hayo mpate kukua katika wokovu, 3 ikiwa kweli mmeonja ya kwamba Bwana ni mwema.

  30. 5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote

    wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

    6 katika njia zako zote mkiri yeye,

    naye atayanyoosha mapito yako.

  31. 13 Usimnyime mtoto adhabu,

    ukimwadhibu kwa fimbo, hatakufa.

    14 Mwadhibu kwa fimbo

    na kuiokoa nafsi yake kutoka mautini.

  32. 5 Vivyo hivyo, ninyi mlio vijana watiini wazee. Nanyi nyote imewapasa kujivika unyenyekevu kila mtu kwa mwenzake, kwa kuwa,

    “Mungu huwapinga wenye kiburi,

    lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

  33. 3 Ilinifurahisha sana baadhi ya ndugu walipokuja na kutueleza juu ya uaminifu wako katika kweli na jinsi unavyoendelea kuenenda katika hiyo kweli. 4 Sina furaha kubwa kuliko hii, kusikia kwamba watoto wangu wanaenenda katika kweli.

  34. 14 Bwana na awawezeshe kuongezeka,

    ninyi na watoto wenu.

  35. 3 Mke wako atakuwa kama mzabibu uzaao

    ndani ya nyumba yako;

    wana wako watakuwa kama machipukizi ya mizeituni

    kuizunguka meza yako.

  36. 7 “Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango. 8 Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.

    9 “Au ni nani miongoni mwenu ambaye mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe? 10 Au mwanawe akimwomba samaki atampa nyoka? 11 Ikiwa ninyi basi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa vitu vizuri wale wamwombao?

  37. 30 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’

  38. 11 “Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba samaki, atampa nyoka badala yake? 12 Au mtoto akimwomba yai atampa nge? 13 Basi ikiwa ninyi mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wale wamwombao!”

  39. 1 Kwa hiyo, mfuateni Mungu kama watoto wapendwao, 2 mkiishi maisha ya upendo, kama vile Kristo alivyotupenda sisi akajitoa kwa ajili yetu kuwa sadaka yenye harufu nzuri na dhabihu kwa Mungu.

  40. 1 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao, kwa kuwa nimeufanya moyo wake kuwa mgumu na mioyo ya maafisa wake ili kwamba nipate kutenda ishara hizi zangu za ajabu miongoni mwao 2 ili upate kuwaeleza watoto wako na wajukuu wako jinsi nilivyowatendea Wamisri kwa ukali na jinsi nilivyofanya ishara zangu miongoni mwao, nanyi mpate kujua kuwa Mimi ndimi Bwana.”

  41. 9 “ ‘Ikiwa mtu yeyote atamlaani baba yake au mama yake, lazima auawe. Amemlaani baba yake au mama yake, nayo damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe.

  42. 20 Mwanangu, zishike amri za baba yako,

    wala usiyaache mafundisho ya mama yako.

  43. 1 Mithali za Solomoni:

    Mwana mwenye hekima

    huleta furaha kwa baba yake,

    lakini mwana mpumbavu

    huleta huzuni kwa mama yake.

  44. 20 Mwana mwenye hekima huleta furaha kwa baba yake,

    bali mtu mpumbavu humdharau mama yake.

  45. 18 Mrudi mwanao, kwa maana katika hiyo kuna tumaini,

    usiwe mshirika katika mauti yake.

  46. 24 Baba wa mwenye haki ana furaha kubwa,

    naye aliye na mwana mwenye hekima humfurahia.

  47. 1 Mkumbuke Muumba wako

    siku za ujana wako,

    kabla hazijaja siku za taabu,

    wala haijakaribia miaka utakaposema,

    “Mimi sifurahii hiyo”:

  48. 42 “Kama mtu yeyote akimsababisha mmojawapo wa wadogo hawa wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa baharini.

  49. 21 Mwanamke anapokuwa na utungu wa kuzaa huwa na maumivu kwa sababu saa yake imewadia. Lakini mtoto akiisha kuzaliwa, yule mwanamke husahau maumivu hayo kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtoto ulimwenguni.

  50. 11 Nilipokuwa mtoto, nilisema kama mtoto, niliwaza kama mtoto, nilifikiri kama mtoto. Nilipokuwa mtu mzima niliacha mambo ya kitoto.

  51. 20 Ndugu zangu, msiwe kama watoto katika kufikiri kwenu, afadhali kuhusu uovu mwe kama watoto wachanga, lakini katika kufikiri kwenu, mwe watu wazima.

  52. 26 Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani. 27 Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo.

  53. 4 Kama mjane ana watoto ama wajukuu, hawa inawapasa awali ya yote wajifunze kutimiza wajibu wao wa kumcha Mungu katika matendo kwa kuwatunza wale wa jamaa zao wenyewe, na hivyo wawarudishie wema waliowatendea wazazi wao, kwa kuwa hivi ndivyo impendezavyo Mungu.