43 Bible Verses About Husbands

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Husbands
  1. 25 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Kristo alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake 26 kusudi alifanye takatifu, akilitakasa kwa kuliosha kwa maji katika Neno lake, 27 apate kujiletea Kanisa tukufu lisilo na doa wala kunyanzi au waa lolote, bali takatifu na lisilo na hatia. 28 Vivyo hivyo imewapasa waume kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.

  2. 7 Vivyo hivyo ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, nanyi wapeni heshima mkitambua ya kuwa wao ni wenzi walio dhaifu, na kama warithi pamoja nanyi wa kipawa cha neema cha uzima, ili kusiwepo na chochote cha kuzuia maombi yenu.

  3. 12 Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi. 14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.

    15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.

    18 Ninyi wake, watiini waume zenu, kama inavyostahili katika Bwana.

    19 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, wala msiwe na uchungu dhidi yao.

    20 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote, kwa maana hivi ndivyo inavyompendeza Bwana.

  4. 21 Hivyo Bwana Mungu akamfanya Adamu kulala usingizi mzito, naye alipokuwa amelala akachukua moja ya mbavu zake, akapafunika mahali pale kwa nyama. 22 Kisha Bwana Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwenye ule ubavu aliouchukua kutoka kwa huyo mwanaume, akamleta huyo mwanamke kwa huyo mwanaume.

    23 Huyo mwanaume akasema,

    “Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu

    na nyama ya nyama yangu,

    ataitwa ‘mwanamke,’

    kwa kuwa alitolewa katika mwanaume.”

    24 Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.

    25 Adamu na mkewe wote wawili walikuwa uchi, wala hawakuona aibu.

  5. 4 Akawajibu, “Je, hamkusoma kwamba hapo mwanzo Muumba aliwaumba mwanaume na mwanamke, 5 naye akasema, ‘Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja’? 6 Hivyo si wawili tena, bali mwili mmoja. Kwa hiyo alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”

    7 Wakamuuliza, “Kwa nini basi Mose aliagiza mtu kumpa mkewe hati ya talaka na kumwacha?”

    8 Yesu akawajibu, “Mose aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu mwanzo haikuwa hivyo. 9 Mimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa sababu ya uasherati naye akaoa mke mwingine, anazini. Naye amwoaye yule mwanamke aliyeachwa pia anazini.”

  6. 1 Basi kuhusu mambo yale mliyoyaandika: Ni vyema mwanaume asimguse mwanamke. 2 Lakini ili kuepuka zinaa, kila mwanaume na awe na mke wake mwenyewe na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe. 3 Mume atimize wajibu wake wa ndoa kwa mkewe, naye vivyo hivyo mke kwa mumewe. 4 Mwanamke hana mamlaka juu ya mwili wake bali mumewe, wala mume hana mamlaka juu ya mwili wake bali mkewe. 5 Msinyimane, isipokuwa mmekubaliana kufanya hivyo kwa muda fulani ili mweze kujitoa kwa maombi, kisha mrudiane tena ili Shetani asije akapata nafasi ya kuwajaribu kwa sababu ya kutokuwa na kiasi.

  7. 13 Kitu kingine mnachokifanya: Mnaifurikisha madhabahu ya Bwana kwa machozi. Mnalia na kuugua kwa sababu yeye haziangalii tena sadaka zenu wala hazikubali kwa furaha kutoka mikononi mwenu. 14 Mnauliza, “Kwa nini?” Ni kwa sababu Bwana ni shahidi kati yako na mke wa ujana wako, kwa sababu umevunja uaminifu naye, ingawa yeye ni mwenzako, mke wa agano lako la ndoa.

    15 Je, Bwana hakuwafanya wao kuwa mmoja? Katika mwili na katika roho wao ni wa Mungu. Kwa nini wawe mmoja? Kwa sababu Mungu alikuwa akitafuta mzao mwenye kumcha Mungu. Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, mtu asivunje uaminifu kwa mke wa ujana wake.

    16 “Ninachukia kuachana,” asema Bwana, Mungu wa Israeli, “pia nachukia mtu anayejivika jeuri kama vazi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

    Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, wala msije mkavunja uaminifu.

  8. 1 Igeni mfano wangu, kama ninavyouiga mfano wa Kristo.

    2 Ninawasifu kwa kuwa mnanikumbuka katika kila jambo na kwa kushika mafundisho niliyowapa.

    3 Napenda mfahamu kwamba kichwa cha kila mwanaume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanaume, nacho kichwa cha Kristo ni Mungu.

  9. 26 Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.”

    27 Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,

    kwa mfano wa Mungu alimuumba;

    mwanaume na mwanamke aliwaumba.

    28 Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”

  10. 7 Laiti watu wangekuwa kama mimi nilivyo. Lakini kila mtu amepewa kipawa chake kutoka kwa Mungu, mmoja ana kipawa cha namna hii na mwingine ana cha namna ile.

    8 Kwa wale wasiooa na kwa wajane, nasema hivi, ingekuwa vizuri wasioe. 9 Lakini kama hawawezi kujizuia, basi waoe na kuolewa, kwa maana ni afadhali kuoa au kuolewa kuliko kuwaka tamaa.

    10 Kwa wale waliooana nawapa amri (si mimi ila ni Bwana): Mke asitengane na mumewe. 11 Lakini akitengana, ni lazima akae bila kuolewa, ama sivyo apatane tena na mumewe. Wala mume asimpe mkewe talaka.

    12 Lakini kwa wengine nasema (si Bwana ila ni mimi): Kama ndugu ana mke asiyeamini, naye huyo mke anakubali kuishi pamoja naye, basi asimwache. 13 Naye mwanamke aaminiye kama ameolewa na mwanaume asiyeamini na huyo mume anakubali kuishi naye, basi huyo mwanamke asimwache. 14 Kwa maana huyo mume asiyeamini anatakaswa kupitia mkewe, naye mke asiyeamini anatakaswa kupitia mumewe anayeamini. Kama isingalikuwa hivyo watoto wenu wangalikuwa si safi, lakini ilivyo sasa wao ni watakatifu.

  11. 5 Kwa maana Muumba wako ndiye mume wako,

    Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake,

    yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli ni Mkombozi wako,

    yeye anaitwa Mungu wa dunia yote.

    6 Bwana atakuita urudi

    kana kwamba ulikuwa mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni;

    kama mke aliyeolewa bado angali kijana

    na kukataliwa,” asema Mungu wako.

  12. 1 Endeleeni kupendana kama ndugu. 2 Msisahau kuwakaribisha wageni, kwa kuwa kwa kufanya hivyo, watu wengine waliwakaribisha malaika pasipo kujua. 3 Wakumbukeni wale waliofungwa gerezani kana kwamba ninyi mmefungwa pamoja nao. Pia wakumbukeni wale wanaotendewa vibaya, kana kwamba ni ninyi wenyewe mnateswa.

    4 Ndoa na iheshimiwe na watu wote, nayo malazi yawe safi, kwa kuwa Mungu atawahukumu wazinzi na waasherati wote. 5 Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,

    “Kamwe sitakuacha,

    wala sitakupungukia.”

    6 Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,

    “Bwana ni msaada wangu; sitaogopa.

    Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”

  13. 31 “Pia ilinenwa kwamba, ‘Mtu yeyote amwachaye mkewe sharti ampe hati ya talaka.’ 32 Lakini mimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa kosa la uasherati, amfanya mkewe kuwa mzinzi. Na yeyote amwoaye yule mwanamke aliyeachwa, anazini.

  14. 9 Wawili ni afadhali kuliko mmoja,

    kwa sababu wana malipo mazuri kwa kazi yao:

    10 Kama mmoja akianguka,

    mwenzake atamwinua.

    Lakini ni jambo la kuhuzunisha

    kwa mtu yule aangukaye

    naye hana wa kumwinua!

    11 Pia, kama wawili wakilala pamoja

    watapashana joto.

    Lakini ni vipi mtu aweza

    kujipasha joto mwenyewe?

    12 Ingawa mtu mmoja aweza kushindwa,

    watu wawili wanaweza

    kumkabili adui na kumshinda.

    Kamba ya nyuzi tatu

    haikatiki kwa urahisi.

  15. 18 Basi Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi: Maria mama yake alikuwa ameposwa na Yosefu, lakini kabla hawajakutana kimwili, Maria alionekana kuwa na mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 19 Kwa kuwa Yosefu, mwanaume aliyekuwa amemposa alikuwa mtu mwadilifu, hakutaka kumwaibisha Maria hadharani, aliazimu kumwacha kwa siri.

    20 Lakini mara alipoazimu kufanya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto na kusema, “Yosefu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu.

  16. 15 Kunywa maji kutoka kwenye kisima chako mwenyewe,

    maji yanayotiririka kutoka kwenye kisima chako mwenyewe.

    16 Je, chemchemi zako zifurike katika barabara za mji

    na vijito vyako vya maji viwanjani?

    17 Na viwe vyako mwenyewe,

    kamwe visishirikishwe wageni.

    18 Chemchemi yako na ibarikiwe

    na umfurahie mke wa ujana wako.

    19 Kulungu jike apendaye, kulungu mzuri:

    matiti yake na yakutosheleze siku zote,

    nawe utekwe daima na upendo wake.

  17. 4 Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. 5 Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. 6 Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. 7 Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.

    8 Upendo haushindwi kamwe. Lakini ukiwepo unabii, utakoma; zikiwepo lugha, zitakoma; yakiwepo maarifa, yatapita.

  18. 8 Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini.

  19. 5 Kama mtu ameoa karibuni, kamwe asipelekwe vitani au kupewa wajibu mwingine wowote. Kwa mwaka mmoja atakuwa huru kubaki nyumbani ili amfurahishe mke aliyemwoa.

  20. 22 Apataye mke apata kitu chema

    naye ajipatia kibali kwa Bwana.

  21. 2 Kwa mfano, mwanamke aliyeolewa amefungwa kwa mumewe wakati akiwa hai, lakini yule mume akifa, yule mwanamke amefunguliwa kutoka sheria ya ndoa. 3 Hivyo basi, kama huyo mwanamke ataolewa na mwanaume mwingine wakati mumewe akiwa bado yuko hai, ataitwa mzinzi. Lakini kama mumewe akifa, mwanamke huyo hafungwi tena na sheria ya ndoa, naye akiolewa na mtu mwingine haitwi mzinzi.

  22. 8 Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi.

  23. 2 Nikaona Mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe.

  24. 16 Kwa mwanamke akasema,

    “Nitakuzidishia sana utungu wakati wa kuzaa kwako;

    kwa utungu utazaa watoto.

    Tamaa yako itakuwa kwa mumeo

    naye atakutawala.”

  25. 14 “Rudini, enyi watu msio waaminifu, kwa kuwa mimi ni mume wenu,” asema Bwana. “Nitawachagua ninyi, mmoja kutoka kwenye mji, na wawili kutoka kwenye ukoo, nami nitawaleta Sayuni.

  26. 27 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Usizini.’ 28 Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.

  27. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

  28. 2 Ninawaonea wivu, wivu wa Kimungu, kwa kuwa mimi niliwaposea mume mmoja, ili niwalete kwa Kristo kama mabikira safi.

  29. 4 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana.

  30. 9 Furahia maisha na mke wako, umpendaye, siku zote za maisha ya ubatili uliyopewa na Mungu chini ya jua, siku zote za ubatili. Kwa maana hili ndilo fungu lako katika maisha na katika kazi yako ya taabu chini ya jua.

  31. 19 Nitakuposa uwe wangu milele;

    nitakuposa kwa uadilifu na haki,

    kwa upendo na huruma.

    20 Nitakuposa kwa uaminifu,

    nawe utamkubali Bwana.

    21 “Katika siku ile nitajibu,”

    asema Bwana,

    “nitajibu kwa anga,

    nazo anga zitajibu kwa nchi;

    22 nayo nchi itajibu kwa nafaka,

    divai mpya na mafuta,

    navyo vitajibu kwa Yezreeli.

    23 Nitampanda katika nchi kwa ajili yangu mwenyewe;

    nami nitaonyesha pendo langu kwake

    yule ambaye nilimwita, ‘Si mpenzi wangu.’

    Nitawaambia wale walioitwa, ‘Sio watu wangu,’

    ‘Ninyi ni watu wangu’;

    nao watasema, ‘Wewe ndiwe Mungu wangu.’ ”

  32. 6 Lakini tangu mwanzo wa uumbaji, ‘Mungu aliwaumba mwanaume na mwanamke. 7 Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja.’ 8 Kwa hiyo hawatakuwa wawili tena, bali mwili mmoja. 9 Basi, alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”

    10 Walipokuwa tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamuuliza kuhusu jambo hili. 11 Akawajibu, “Mtu yeyote amwachaye mkewe na kuoa mke mwingine, anazini naye. 12 Naye mwanamke amwachaye mumewe na kuolewa na mume mwingine, anazini.”

  33. 1 Basi, mimi niliye mfungwa wa Bwana, nawasihi mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa. 2 Kwa unyenyekevu wote na upole, mkiwa wavumilivu, mkichukuliana kwa upendo. 3 Jitahidini kudumisha umoja wa Roho katika kifungo cha amani.

  34. 8 Enda nami kutoka Lebanoni, bibi arusi wangu,

    enda nami kutoka Lebanoni.

    Shuka kutoka ncha ya Amana,

    kutoka juu ya Seniri, kilele cha Hermoni,

    kutoka mapango ya simba

    na kutoka mlima wapendapo kukaa chui.

    9 Umeiba moyo wangu, dada yangu, bibi arusi wangu;

    umeiba moyo wangu

    kwa mtazamo mmoja wa macho yako,

    kwa kito kimoja cha mkufu wako.

    10 Tazama jinsi pendo lako linavyofurahisha,

    dada yangu, bibi arusi wangu!

    Pendo lako linafurahisha aje zaidi ya divai,

    na harufu ya manukato yako zaidi ya kikolezo chochote!

    11 Midomo yako inadondosha utamu kama sega la asali,

    bibi arusi wangu;

    maziwa na asali viko chini ya ulimi wako.

    Harufu nzuri ya mavazi yako ni kama ile ya Lebanoni.

    12 Wewe ni bustani iliyofungwa, dada yangu,

    bibi arusi wangu;

    wewe ni chanzo cha maji kilichozungushiwa kabisa,

    chemchemi yangu peke yangu.

  35. 18 “Mtu yeyote amwachaye mkewe na kumwoa mwanamke mwingine anazini, naye mwanaume amwoaye mwanamke aliyetalikiwa anazini.

  36. 2 Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha, 3 asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha. 4 Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia.

  37. 14 Usizini.

  38. 1 Bwana akaniambia, “Nenda, ukaonyeshe upendo wako kwa mke wako tena, ingawa amependwa na mwingine naye ni mzinzi. Mpende kama Bwana apendavyo Waisraeli, ingawa wanageukia miungu mingine na kupenda mikate mitamu ya zabibu kavu iliyowekwa wakfu.”

    2 Basi nilimnunua huyo mwanamke kwa shekeli kumi na tano za fedha, pia kwa kiasi kama cha homeri moja na nusu ya shayiri. 3 Kisha nilimwambia, “Utaishi nami kwa siku nyingi, hupaswi kuwa kahaba au kuwa na uhusiano wa karibu na mtu yeyote, nami nitaishi na wewe.”

  39. 1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini ambao Bwana Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati kweli Mungu alisema, ‘Kamwe msile matunda ya mti wowote wa bustanini’?”

    2 Mwanamke akamjibu nyoka, “Tunaweza kula matunda ya miti iliyoko bustanini, 3 lakini Mungu alisema, ‘Kamwe msile tunda la mti ulio katikati ya bustani, wala kuugusa, la sivyo mtakufa.’ ”

    4 Lakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa. 5 Kwa maana Mungu anajua ya kuwa wakati mtakapoyala, macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”

    6 Mwanamke alipoona ya kuwa tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula na la kupendeza macho, tena linatamanika kwa kujipatia hekima, basi akachuma katika matunda yake, akala, pia akampa mumewe, aliyekuwa pamoja naye, naye akala.

  40. 22 Ikiwa mwanaume atakutwa akizini na mke wa mtu mwingine, wote wawili, mwanaume na mwanamke aliyezini naye, lazima wauawe. Lazima mwondoe uovu katika Israeli.

  41. 7 Ndipo Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiwe huyo mtu! Hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Nilikupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli, nilikuokoa kutokana na mkono wa Sauli. 8 Nilikupa nyumba ya bwana wako na wake za bwana wako mikononi mwako. Nikakupa nyumba ya Israeli na Yuda. Kama haya yote yalikuwa madogo sana, ningekupa hata zaidi. 9 Kwa nini ulilidharau neno la Bwana kwa kufanya lililo ovu machoni pake? Ulimuua Uria, Mhiti kwa upanga na kumchukua mke wake awe mkeo. Ulimuua kwa upanga wa Waamoni. 10 Basi kwa hiyo, upanga hautaondoka nyumbani mwako kamwe kwa sababu ulinidharau mimi na kumchukua mke wa Uria, Mhiti kuwa mkeo.’

  42. 10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine.

  43. 12 Shemasi awe mume wa mke mmoja na inampasa aweze kusimamia watoto wake na watu wa nyumbani mwake vyema.