105 Bible Verses About The Holy Spirit
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
1 Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu, wale ambao hawaenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho. 2 Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima katika Kristo Yesu imeniweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti. 3 Kwa maana kile ambacho sheria haikuwa na uwezo wa kufanya, kwa vile ilivyokuwa dhaifu katika mwili, Mungu kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe kwa mfano wa mwanadamu mwenye mwili ulio wa dhambi na kwa ajili ya dhambi, yeye aliihukumu dhambi katika mwili, 4 ili kwamba haki ipatikanayo kwa sheria itimizwe ndani yetu sisi, ambao hatuenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho.
5 Kwa maana wale wanaoishi kwa kuufuata mwili huziweka nia zao katika vitu vya mwili, lakini wale wanaoishi kwa kufuata Roho, huziweka nia zao katika mambo ya Roho. 6 Kwa maana kuwa na nia ya mwili ni mauti, bali kuwa na nia inayoongozwa na Roho ni uzima na amani. 7 Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui na Mungu, kwa maana haiitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. 8 Wale wanaotawaliwa na mwili, hawawezi kumpendeza Mungu.
9 Lakini ninyi, hamtawaliwi na mwili, bali na Roho, ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu. Mtu yeyote ambaye hana Roho wa Kristo, yeye si wa Kristo. 10 Lakini kama Kristo anakaa ndani yenu, miili yenu imekufa kwa sababu ya dhambi, lakini roho zenu zi hai kwa sababu ya haki. 11 Nanyi ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu kutoka kwa wafu ataihuisha pia miili yenu ambayo hufa, kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu.
-
9 Lakini ni kama ilivyoandikwa:
“Hakuna jicho limepata kuona,
wala sikio limepata kusikia,
wala hayakuingia moyoni wowote,
yale Mungu amewaandalia
wale wampendao”:
10 Lakini mambo haya Mungu ametufunulia kwa Roho wake.
Roho huchunguza kila kitu, hata mambo ya ndani sana ya Mungu. 11 Kwa maana ni nani anayejua mawazo ya mtu isipokuwa roho iliyo ndani ya huyo mtu? Vivyo hivyo hakuna mtu ajuaye mawazo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu. 12 Basi hatukupokea roho ya dunia bali Roho atokaye kwa Mungu, ili tuweze kuelewa kile kipawa ambacho Mungu ametupatia bure. 13 Haya ndiyo tusemayo, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya wanadamu bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua kweli za kiroho kwa maneno ya kiroho. 14 Mtu ambaye hana Roho hawezi kupokea mambo yatokayo kwa Roho wa Mungu, kwa kuwa ni upuzi kwake, naye hawezi kuyaelewa kwa sababu hayo yanaeleweka tu kwa upambanuzi wa rohoni. 15 Mtu wa kiroho hubainisha mambo yote, lakini yeye mwenyewe habainishwi na mtu yeyote.
16 “Kwa maana ni nani aliyefahamu mawazo ya Bwana
ili apate kumfundisha?”
Lakini sisi tunayo mawazo ya Kristo.
-
13 Atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza awatie katika kweli yote. Yeye hatanena kwa ajili yake mwenyewe, bali atanena yale yote atakayosikia, naye atawaonyesha mambo yajayo. 14 Atanitukuza mimi, kwa maana atayachukua yaliyo yangu na kuwajulisha ninyi. 15 Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu. Ndiyo maana nimesema Roho atachukua yaliyo yangu na kuwajulisha ninyi.
-
15 “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu. 16 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele. 17 Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye anakaa ndani yenu. 18 Sitawaacha ninyi yatima, naja kwenu. 19 Bado kitambo kidogo ulimwengu hautaniona tena, ila ninyi mtaniona, kwa kuwa mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai.
-
25 “Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi. 26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
-
3 Kwa hiyo nawaambieni ya kuwa hakuna mtu anayeongozwa na Roho wa Mungu anayeweza kusema, “Yesu na alaaniwe.” Pia hakuna mtu awezaye kusema, “Yesu ni Bwana,” isipokuwa ameongozwa na Roho Mtakatifu.
4 Kuna aina mbalimbali za karama, lakini Roho ni yule yule. 5 Kuna huduma za aina mbalimbali, lakini Bwana ni yule yule. 6 Kisha kuna tofauti za kutenda kazi, lakini ni Mungu yule yule atendaye kazi zote kwa watu wote.
7 Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote. 8 Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo. 9 Mtu mwingine imani kwa huyo Roho na mwingine karama za kuponya kwa huyo Roho mmoja. 10 Kwa mwingine matendo ya miujiza, kwa mwingine unabii kwa mwingine kupambanua roho, kwa mwingine aina mbalimbali za lugha, na kwa mwingine bado, tafsiri za lugha. 11 Haya yote hufanywa na huyo huyo Roho mmoja, Roho naye humgawia kila mtu, kama apendavyo.
-
14 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio watoto wa Mungu. 15 Kwa maana hamkupokea roho ya utumwa iwaleteayo tena hofu, bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambaye kwa yeye twalia, “Abba, yaani, Baba,” 16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kwamba sisi tu watoto wa Mungu. 17 Hivyo, ikiwa sisi ni watoto, basi tu warithi, warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo, naam, tukiteswa pamoja naye tupate pia kutukuzwa pamoja naye.
-
26 “Lakini atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, yaani, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi. 27 Ninyi nanyi itawapasa kushuhudia kwa sababu mmekuwa pamoja nami tangu mwanzo.
-
10 Lakini waliasi,
na kumhuzunisha Roho Mtakatifu wake.
Hivyo aligeuka na kuwa adui yao,
na yeye mwenyewe akapigana dhidi yao.
11 Ndipo watu wake wakazikumbuka siku zilizopita,
siku za Mose na watu wake:
yuko wapi yeye aliyewaleta kupitia katikati ya bahari,
pamoja na wachungaji wa kundi lake?
Yuko wapi yule aliyeweka
Roho wake Mtakatifu katikati yao,
12 aliyetuma mkono wake uliotukuka wenye nguvu
kuwa katika mkono wa kuume wa Mose,
aliyegawa maji ya bahari mbele yao,
ili kujipatia jina milele,
13 aliyewaongoza kupitia kwenye vilindi?
Kama farasi katika nchi iliyo wazi,
wao hawakujikwaa,
14 kama ngʼombe washukao bondeni kwenye malisho,
walipewa pumziko na Roho wa Bwana.
Hivi ndivyo ulivyowaongoza watu wako
ili kujipatia mwenyewe jina tukufu.
-
1 Roho wa Bwana Mwenyezi yu juu yangu,
kwa sababu Bwana amenitia mafuta
kuwahubiria maskini habari njema.
Amenituma kuwaganga waliovunjika moyo,
kuwatangazia mateka uhuru wao,
na hao waliofungwa
habari za kufunguliwa kwao;
2 kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,
na siku ya kisasi ya Mungu wetu,
kuwafariji wote waombolezao,
3 na kuwapa mahitaji
wale wanaohuzunika katika Sayuni,
ili kuwapa taji ya uzuri badala ya majivu,
mafuta ya furaha badala ya maombolezo,
vazi la sifa badala ya roho ya kukata tamaa.
Nao wataitwa mialoni ya haki,
pando la Bwana,
ili kuonyesha utukufu wake.
-
4 Wakati mmoja alipokuwa pamoja nao, aliwapa amri hii, “Msitoke Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba, ambayo mmenisikia nikisema habari zake. 5 Yohana aliwabatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”
6 Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamuuliza Yesu, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?”
7 Yesu akawaambia, “Si juu yenu kujua nyakati na majira ambayo Baba ameyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. 8 Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.”
-
44 Wakati Petro alikuwa akisema maneno haya, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wakisikiliza ule ujumbe. 45 Wale wa tohara walioamini waliokuja na Petro walishangaa kwa kuona kuwa kipawa cha Roho Mtakatifu kimemwagwa juu ya watu wa Mataifa. 46 Kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha mpya na kumwadhimisha Mungu.
Ndipo Petro akasema, 47 “Je, kuna mtu yeyote anayeweza kuzuia watu hawa wasibatizwe kwa maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea.” 48 Kwa hiyo akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Wakamsihi Petro akae nao kwa siku chache.
-
1 Chipukizi litatokea kutoka shina la Yese,
kutoka mizizi yake Tawi litazaa tunda.
2 Roho wa Bwana atakaa juu yake,
Roho wa hekima na wa ufahamu,
Roho wa shauri na wa uweza,
Roho wa maarifa na wa kumcha Bwana
-
2 Walipokuwa wakimwabudu Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, “Nitengeeni Sauli na Barnaba kwa kazi ile maalum niliyowaitia.” 3 Ndipo baada ya kufunga na kuomba, wakawawekea mikono yao na wakawatuma waende zao.
4 Hivyo, wakiwa wametumwa na Roho Mtakatifu, wakashuka kwenda Seleukia na kutoka huko wakasafiri baharini mpaka kisiwa cha Kipro. 5 Walipowasili katika mji wa Salami, wakahubiri neno la Mungu katika sinagogi la Wayahudi. Pia walikuwa na Yohana Marko kuwa msaidizi wao.
-
1 Siku ya Pentekoste ilipowadia, waamini wote walikuwa mahali pamoja. 2 Ghafula sauti kama mvumo mkubwa wa upepo mkali uliotoka mbinguni ukaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi. 3 Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kukaa juu ya kila mmoja wao. 4 Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia.
-
25 Nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi, nitawatakasa kutoka uchafu wenu wote na kutoka sanamu zenu zote. 26 Nitawapa moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu, nitaondoa ndani yenu moyo wenu wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama. 27 Nami nitaweka Roho yangu ndani yenu na kuwafanya ninyi mfuate amri zangu na kuwafanya kuwa waangalifu kuzishika sheria zangu. 28 Mtaishi katika nchi niliyowapa baba zenu, ninyi mtakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wenu.
-
7 Lakini nawaambia kweli, yafaa mimi niondoke, kwa kuwa nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu, lakini nikienda nitamtuma kwenu. 8 Naye atakapokuja, atauthibitishia ulimwengu kuhusu dhambi, haki na hukumu. 9 Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi, 10 kwa habari ya haki, kwa sababu ninakwenda kwa Baba, nanyi hamtaniona tena, 11 kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.
-
14 Lakini akili zao zilipumbazwa, kwa maana mpaka leo utaji ule ule hufunika wakati Agano la Kale linasomwa. Huo utaji haujaondolewa, kwa maana ni katika Kristo peke yake unaondolewa. 15 Hata leo Sheria ya Mose inaposomwa, utaji hufunika mioyo yao. 16 Lakini wakati wowote mtu anapomgeukia Bwana, utaji unaondolewa. 17 Basi Bwana ndiye Roho. Mahali alipo Roho wa Bwana hapo pana uhuru. 18 Nasi sote, tukiwa na nyuso zisizotiwa utaji tunadhihirisha utukufu wa Bwana, kama kwenye kioo. Nasi tunabadilishwa ili tufanane naye, toka utukufu hadi utukufu mkuu zaidi, utokao kwa Bwana, ambaye ndiye Roho.
-
26 Vivyo hivyo, Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa sababu hatujui kuomba ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa uchungu usioweza kutamkwa. 27 Naye Mungu aichunguzaye mioyo, anaijua nia ya Roho, kwa sababu Roho huwaombea watakatifu sawasawa na mapenzi ya Mungu.
-
1 Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia. 2 Wakati huu dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya maji.
-
15 “Nami nilipoanza kusema, Roho Mtakatifu akashuka juu yao kama vile alivyotushukia sisi hapo mwanzo. 16 Nami nikakumbuka neno la Bwana alivyosema, ‘Yohana alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’ 17 Basi ikiwa Mungu aliwapa hawa watu kipawa kile kile alichotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani hata nifikirie kuwa ningeweza kumpinga Mungu?”
18 Waliposikia haya hawakuwa na la kupinga zaidi. Nao wakamwadhimisha Mungu wakisema, “Basi, Mungu amewapa hata watu wa Mataifa toba iletayo uzima wa milele.”
-
14 Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” 15 Kama mkiumana na kutafunana, angalieni, msije mkaangamizana.
16 Kwa hiyo nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. 17 Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka.
-
22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria. 24 Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake. 25 Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho. 26 Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.
-
29 Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao. 30 Wala msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwake mlitiwa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi. 31 Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu. 32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.
-
7 Niende wapi nijiepushe na Roho yako?
Niende wapi niukimbie uso wako?
8 Kama nikienda juu mbinguni, wewe uko huko;
nikifanya vilindi kuwa kitanda changu,
wewe uko huko.
9 Kama nikipanda juu ya mbawa za mapambazuko,
kama nikikaa pande za mbali za bahari,
10 hata huko mkono wako utaniongoza,
mkono wako wa kuume utanishika kwa uthabiti.
-
13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
-
1 Ninyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaroga? Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele yenu kwamba amesulubiwa. 2 Nataka nijifunze neno moja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa kushika sheria, au kwa kuyaamini yale mliyosikia? 3 Je, ninyi ni wajinga kiasi hicho? Baada ya kuanza kwa Roho, je, sasa mwataka kumalizia katika mwili? 4 Je, mlipata mateso kiasi hicho bure? Ni kama kweli yalikuwa bure! 5 Je, Mungu huwapa Roho wake na kufanya miujiza katikati yenu kwa sababu mnatii sheria, au kwa sababu mnaamini kile mlichosikia?
-
6 Paulo pamoja na wenzake wakasafiri sehemu za Frigia na Galatia, kwa kuwa Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kulihubiri neno huko Asia. 7 Walipofika mpaka wa Misia, wakajaribu kuingia Bithinia lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu. 8 Kwa hiyo wakapita Misia, wakafika Troa. 9 Wakati wa usiku Paulo akaona maono, mtu wa Makedonia amesimama akimsihi, “Vuka uje huku Makedonia utusaidie.” 10 Baada ya Paulo kuona maono haya, tulijiandaa kwa haraka kuondoka kwenda Makedonia tukiwa tumesadiki kuwa Mungu alikuwa ametuita kuhubiri habari njema huko.
-
9 Ndipo aliponiambia, “Utabirie upepo, tabiri, mwanadamu na uuambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Njoo kutoka pande nne, ee pumzi, nawe upulizie pumzi ndani ya hawa waliouawa, ili wapate kuishi.’ ” 10 Hivyo nikatabiri kama alivyoniamuru, nayo pumzi ikawaingia, wakawa hai na wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno.
11 Ndipo akaniambia: “Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli. Nao wanasema, ‘Mifupa yetu imekauka na tumaini letu limetoweka, tumekatiliwa mbali.’ 12 Hivyo watabirie na uwaambie: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Enyi watu wangu, nitayafunua makaburi yenu na kuwatoa ndani yake, nami nitawarudisha tena katika nchi ya Israeli. 13 Ndipo ninyi watu wangu, mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu na kuwatoa humo. 14 Nitatia Roho yangu ndani yenu nanyi mtaishi, nami nitawakalisha katika nchi yenu wenyewe. Ndipo mtakapojua kwamba Mimi Bwana nimenena, nami nitalitenda, asema Bwana!’ ”
-
19 Lakini watakapowapeleka humo, msisumbuke kufikiria mtakalosema, kwa maana mtapewa la kusema wakati huo. 20 Kwa sababu si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho wa Baba yenu atakayekuwa akinena kupitia kwenu.
-
32 Kisha Yohana akatoa ushuhuda huu: “Nilimwona Roho akishuka kutoka mbinguni kama hua, akakaa juu yake. 33 Mimi nisingemtambua, lakini yeye aliyenituma nibatize kwa maji alikuwa ameniambia, ‘Yule mtu utakayemwona Roho akimshukia na kukaa juu yake, huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu.’ 34 Mimi mwenyewe nimeona jambo hili na ninashuhudia kuwa huyu ndiye Mwana wa Mungu.”
-
9 Hata hivyo, ukainuka upinzani wa watu wa Sinagogi la Watu Huru (kama lilivyokuwa linaitwa), la Wayahudi wa Kirene na wa Iskanderia, na wengine kutoka Kilikia na Asia. Watu hawa wakaanza kupingana na Stefano. 10 Lakini hawakuweza kushindana na hekima yake wala huyo Roho ambaye alisema kwake.
-
17 Kwa maana Ufalme wa Mungu si kula na kunywa, bali ni haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu.
-
6 Kwa sababu ninyi ni watoto wa Mungu, Mungu amemtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, anayelia, “Abba, Baba.”
-
1 Haya ni maneno ya mwisho ya Daudi:
“Neno la Daudi mwana wa Yese,
neno la mtu aliyeinuliwa na Aliye Juu Sana,
mtu aliyepakwa mafuta na Mungu wa Yakobo,
mwimbaji wa nyimbo wa Israeli:
2 “Roho wa Bwana alinena kupitia kwangu,
neno lake lilikuwa ulimini mwangu.
-
31 Walipokwisha kuomba, mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.
-
10 Kwa habari ya wokovu huu, wale manabii waliosema kuhusu neema ambayo ingewajia ninyi, walitafuta kwa bidii na kwa uangalifu mkubwa, 11 wakijaribu kujua ni wakati upi na katika mazingira gani ambayo Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao alionyesha, alipotabiri kuhusu mateso ya Kristo na utukufu ule ambao ungefuata. 12 Walidhihirishiwa kwamba walikuwa hawajihudumii wao wenyewe, bali waliwahudumia ninyi, waliponena kuhusu mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiria ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Hata malaika wanatamani kuyafahamu mambo haya.
-
19 Nasi tunalo pia neno la hakika zaidi la unabii, ambalo mtafanya vyema mkiliangalia kwa bidii, kama vile nuru inavyongʼaa gizani, hadi kupambazuka na nyota ya asubuhi izuke mioyoni mwenu. 20 Zaidi ya yote, yawapasa mjue kwamba hakuna unabii katika Maandiko uliofasiriwa kama alivyopenda nabii mwenyewe. 21 Kwa maana unabii haukuja kamwe kwa mapenzi ya mwanadamu, bali watu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.
-
6 Roho wa Bwana atakuja juu yako kwa nguvu, nawe utatoa unabii pamoja nao; nawe utageuzwa kuwa mtu wa tofauti. 7 Mara ishara hizi zitakapotimizwa, fanya lolote mkono wako upasao kufanya, kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe.
-
4 Roho wa Mungu ameniumba;
pumzi ya Mwenyezi hunipa uhai.
-
16 Naye Yesu alipokwisha kubatizwa, mara alipotoka ndani ya maji, ghafula mbingu zikafunguka, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua na kutulia juu yake.
-
11 Mtakapokamatwa na kushtakiwa, msisumbuke awali kuhusu mtakalosema. Semeni tu lolote mtakalopewa wakati huo, kwa kuwa si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho Mtakatifu.
-
34 Ndipo Petro akafungua kinywa chake akasema, “Mungu hana upendeleo, 35 Lakini katika kila taifa, kila mtu amchaye na kutenda yaliyo haki hukubaliwa naye. 36 Ninyi mnajua ule ujumbe uliotumwa kwa Israeli, ukitangaza habari njema za amani kwa Yesu Kristo. Yeye ni Bwana wa wote. 37 Mnajua yale yaliyotukia katika Uyahudi wote kuanzia Galilaya baada ya mahubiri ya Yohana Mbatizaji: 38 Jinsi Mungu alivyomtia Yesu wa Nazareti mafuta katika Roho Mtakatifu na jinsi alivyokwenda huku na huko akitenda mema na kuponya wote waliokuwa wameonewa na nguvu za ibilisi, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye.
-
13 Ninyi pia mliingia ndani ya Kristo mliposikia Neno la kweli, Injili ya wokovu wenu. Mkiisha kuamini, ndani yake mlitiwa muhuri, yaani, Roho Mtakatifu mliyeahidiwa, 14 yeye ambaye ni amana yetu akituhakikishia urithi wetu hadi ukombozi wa wale walio milki ya Mungu kwa sifa ya utukufu wake.
-
2 Siku zote tunamshukuru Mungu kwa ajili yenu ninyi nyote, tukiwataja kwenye maombi yetu daima. 3 Tunaikumbuka daima kazi yenu ya imani mbele za Mungu aliye Baba yetu, taabu yenu katika upendo na saburi yenu ya tumaini katika Bwana wetu Yesu Kristo.
4 Ndugu zetu mpendwao na Mungu, kwa kuwa tunajua kwamba Mungu amewachagua, 5 kwa sababu ujumbe wetu wa Injili haukuja kwenu kwa maneno matupu bali pia ulidhihirishwa katika nguvu na katika Roho Mtakatifu, tena ukiwa na uthibitisho kamili, kama vile ninyi wenyewe mnavyojua jinsi tulivyoenenda katikati yenu kwa ajili yenu.
-
11 “Watakapowapeleka katika masinagogi, na mbele ya watawala na wenye mamlaka, msiwe na wasiwasi kuhusu namna mtakavyojitetea au mtakavyosema. 12 Kwa maana Roho Mtakatifu atawafundisha wakati huo huo mnachopaswa kusema.”
-
37 Siku ile ya mwisho ya Sikukuu, siku ile kuu, wakati Yesu akiwa amesimama huko, akapaza sauti yake akasema, “Kama mtu yeyote anaona kiu na aje kwangu anywe. 38 Yeyote aniaminiye mimi, kama Maandiko yasemavyo, vijito vya maji ya uzima vitatiririka ndani mwake.” 39 Yesu aliposema haya alimaanisha Roho Mtakatifu ambaye wote waliomwamini wangempokea, kwani mpaka wakati huo, Roho alikuwa hajatolewa, kwa kuwa Yesu alikuwa bado hajatukuzwa.
-
5 Waliposikia haya, wakabatizwa katika jina la Bwana Yesu. 6 Paulo alipoweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akawashukia, nao wakanena kwa lugha mpya na kutabiri.
-
18 “Roho wa Bwana yu juu yangu,
kwa sababu amenitia mafuta
kuwahubiria maskini habari njema.
Amenituma kuwatangazia wafungwa
kufunguliwa kwao,
na vipofu kupata kuona tena,
kuwaweka huru wanaoonewa,
19 na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika.”
20 Kisha akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi na akaketi. Watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. 21 Ndipo akaanza kwa kuwaambia, “Leo Andiko hili limetimia mkiwa mnasikia.”
-
31 Ndipo kanisa katika Uyahudi wote, Galilaya na Samaria likafurahia wakati wa amani. Likatiwa nguvu, na kwa faraja ya Roho Mtakatifu, idadi yake ikazidi kuongezeka, na likaendelea kudumu katika kumcha Bwana.
-
28 Kwa maana imempendeza Roho Mtakatifu na sisi tusiwatwike mzigo wowote mkubwa zaidi ya mambo haya yafuatayo ambayo ni ya lazima: 29 Kwamba mjiepushe na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na mjiepushe na uasherati. Mkiyaepuka mambo haya, mtakuwa mmefanya vyema.
Kwaherini.
-
3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.
-
1 Ndipo Bwana akamwambia Mose, 2 “Tazama, nimemchagua Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, 3 nami nimemjaza Roho wa Mungu, pamoja na ustadi, uwezo na ujuzi katika aina zote za ufundi, 4 ili kubuni michoro ya kupendeza katika ufundi wa dhahabu, fedha na shaba, 5 kuchonga vito na kuvitia mahali, kufanya ufundi kwa mbao, na kujishughulisha na aina zote za ufundi. 6 Tena nimemteua Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, ili kumsaidia. Pia mafundi wote nimewapa ustadi wa kutengeneza kila kitu nilichokuamuru wewe:
-
10 Walipofika Gibea, akakutana na kundi la manabii. Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akajiunga nao katika kutoa unabii kwao.
-
13 Basi Samweli akachukua ile pembe ya mafuta na kumtia mafuta mbele ya ndugu zake, kuanzia siku ile na kuendelea Roho wa Bwana akaja juu ya Daudi kwa nguvu. Kisha Samweli akaenda zake Rama.
14 Basi Roho wa Bwana alikuwa ameondoka kwa Sauli, nayo roho mbaya ikaachiwa nafasi na Bwana ili imtese.
-
21 Wakati huo Yesu akashangilia katika Roho Mtakatifu, akasema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.
-
8 Petro, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akajibu, “Enyi watawala na wazee wa watu, 9 kama leo tukihojiwa kwa habari ya mambo mema aliyotendewa yule kiwete na kuulizwa jinsi alivyoponywa, 10 ijulikane kwenu nyote na kwa watu wote wa Israeli kwamba: Ni kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulubisha lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama mbele yenu akiwa mzima kabisa. 11 Huyu ndiye
“ ‘jiwe ambalo ninyi wajenzi mlilikataa,
ambalo limekuwa jiwe kuu la pembeni.’
12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”
-
28 “Hata itakuwa, baada ya hayo,
nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili.
Wana wenu na binti zenu watatabiri,
wazee wenu wataota ndoto,
na vijana wenu wataona maono.
29 Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake,
katika siku zile nitamimina Roho wangu.
30 Nami nitaonyesha maajabu katika mbingu
na duniani:
damu, moto na mawimbi ya moshi.
31 Jua litageuzwa kuwa giza
na mwezi kuwa mwekundu kama damu,
kabla ya kuja siku ya Bwana
ile kuu na ya kutisha.
32 Na kila mtu atakayeliitia
jina la Bwana ataokolewa.
Kwa maana juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu
kutakuwepo wokovu,
kama Bwana alivyosema,
miongoni mwa walionusurika
ambao Bwana awaita.
-
21 Baada ya watu wote kubatizwa, Yesu naye akabatizwa. Naye alipokuwa akiomba, mbingu zilifunguka. 22 Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa umbo kama la hua, nayo sauti kutoka mbinguni ikasema: “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.”
-
5 Yesu akamwambia, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu yeyote anayeweza kuingia Ufalme wa Mungu kama hajazaliwa kwa maji na kwa Roho. 6 Mwili huzaa mwili, lakini Roho huzaa roho. 7 Kwa hiyo usishangae ninapokuambia huna budi ‘kuzaliwa mara ya pili.’ 8 Upepo huvuma popote upendapo. Mvumo wake unausikia lakini huwezi ukafahamu utokako wala uendako. Ndivyo ilivyo kwa kila mtu aliyezaliwa na Roho.”
-
16 La, hili ni jambo lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema:
17 “ ‘Katika siku za mwisho, asema Mungu,
nitamimina Roho wangu
juu ya wote wenye mwili.
Wana wenu na binti zenu watatabiri,
vijana wenu wataona maono,
na wazee wenu wataota ndoto.
18 Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake,
katika siku zile nitamimina Roho wangu,
nao watatabiri.
-
15 Kwa hiyo angalieni sana jinsi mnavyoenenda, si kama watu wasio na hekima, bali kama wenye hekima, 16 mkiukomboa wakati, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu. 17 Kwa hiyo msiwe wajinga, bali mpate kujua nini mapenzi ya Bwana. 18 Pia msilewe kwa mvinyo, ambamo ndani yake mna upotovu, bali mjazwe Roho. 19 Msemezane ninyi kwa ninyi kwa zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, mkimwimbia na kumsifu Bwana mioyoni mwenu, 20 siku zote mkimshukuru Mungu Baba kwa kila jambo katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo.
-
27 Nanyi, upako mlioupata kutoka kwake unakaa ndani yenu, wala ninyi hamna haja ya mtu yeyote kuwafundisha. Lakini kama vile upako wake unavyowafundisha kuhusu mambo yote nayo ni kweli wala si uongo, basi kama ulivyowafundisha kaeni ndani yake.
-
9 Basi Yoshua mwana wa Nuni alijazwa roho ya hekima kwa sababu Mose alikuwa ameweka mikono yake juu yake. Kwa hiyo Waisraeli wakamsikiliza na wakafanya yale ambayo Bwana alikuwa amemwagiza Mose.
-
20 Uliwapa Roho wako mwema ili kuwafundisha. Hukuwanyima mana yako vinywani mwao, nawe ukawapa maji kwa ajili ya kiu yao.
-
1 “Huyu hapa mtumishi wangu, ninayemtegemeza,
mteule wangu, ambaye ninapendezwa naye;
nitaweka Roho yangu juu yake,
naye ataleta haki kwa mataifa.
-
21 “Kwa habari yangu mimi, hili ndilo agano langu nao,” asema Bwana. “Roho wangu, aliye juu yenu, na maneno yangu ambayo nimeyaweka katika vinywa vyenu, havitaondoka vinywani mwenu, wala kutoka vinywani mwa watoto wenu, wala kutoka vinywani mwa wazao wao, kuanzia sasa na hata milele,” asema Bwana.
-
10 Yesu alipokuwa akitoka ndani ya maji, aliona mbingu zikifunguka na Roho akishuka juu yake kama hua.
-
25 Basi alikuwako huko Yerusalemu mtu mmoja jina lake Simeoni, ambaye alikuwa mwenye haki na mcha Mungu, akitarajia faraja ya Israeli, na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. 26 Roho Mtakatifu alikuwa amemfunulia kuwa hatakufa kabla hajamwona Kristo wa Bwana. 27 Simeoni, akiwa ameongozwa na Roho Mtakatifu, alikwenda Hekaluni. Wazazi walipomleta mtoto Yesu ili kumfanyia kama ilivyokuwa desturi ya Sheria, 28 ndipo Simeoni akampokea mtoto mikononi mwake na kumsifu Mungu, akisema:
29 “Bwana Mwenyezi, kama ulivyoahidi,
sasa wamruhusu mtumishi wako
aende zake kwa amani.
30 Kwa maana macho yangu yameuona wokovu wako,
31 ulioweka tayari machoni pa watu wote,
32 nuru kwa ajili ya ufunuo kwa watu wa Mataifa
na kwa ajili ya utukufu kwa watu wako Israeli.”
-
29 Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye lile gari ukae karibu nalo.”
-
10 Roho wa Bwana akaja juu yake, hivyo akawa mwamuzi wa Israeli, akaenda vitani. Bwana akamtia Kushan-Rishathaimu mfalme wa Aramu mikononi mwa Othnieli, naye akamshinda.
-
1 Petro, mtume wa Yesu Kristo:
Kwa wateule wa Mungu, wageni katika ulimwengu, waliotawanyika kote katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia. 2 Ni ninyi ambao mlichaguliwa tangu mwanzo na Mungu Baba kulingana na alivyotangulia kuwajua, kupitia kwa kazi ya utakaso wa Roho, katika utiifu kwa Yesu Kristo na kunyunyiziwa damu yake:
Neema na amani ziwe kwenu kwa wingi.
-
16 Je, hamjui ya kwamba ninyi wenyewe ni hekalu la Mungu na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?
-
35 Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu.
-
33 Basi ikiwa yeye ametukuzwa kwa mkono wa kuume wa Mungu, amepokea kutoka kwa Baba ahadi ya Roho Mtakatifu, naye amemimina kile mnachoona sasa na kusikia.
-
8 Lakini kuhusu mimi, nimejazwa nguvu,
nimejazwa Roho wa Bwana,
haki na uweza,
kumtangazia Yakobo kosa lake,
na Israeli dhambi yake.
-
45 Ndipo akafungua fahamu zao ili waweze kuyaelewa Maandiko. 46 Akawaambia, “Haya ndiyo yaliyoandikwa: Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu. 47 Toba na msamaha wa dhambi zitatangaziwa mataifa yote kupitia jina lake kuanzia Yerusalemu. 48 Ninyi ni mashahidi wa mambo haya.
49 “Tazama nitawatumia ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini hadi mtakapovikwa uwezo utokao juu.”
-
34 Yeye aliyetumwa na Mungu husema maneno ya Mungu, kwa kuwa Mungu humtoa Roho pasipo kipimo.
-
63 Roho ndiye atiaye uzima, mwili haufai kitu. Maneno haya niliyowaambia ni Roho tena ni uzima.
-
3 Kwa hiyo ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, watu wenye sifa njema, waliojawa na Roho Mtakatifu na hekima, ambao tunaweza kuwakabidhi kazi hii, 4 nasi tutatumia muda wetu kuomba na huduma ya neno.”
5 Yale waliyosema yakawapendeza watu wote, nao wakamchagua Stefano (mtu aliyejawa na imani na Roho Mtakatifu) pamoja na Filipo, Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena na Nikolao, mwongofu kutoka Antiokia.
-
6 Huyu ndiye alikuja kwa maji na damu, yaani, Yesu Kristo. Hakuja kwa maji peke yake, bali kwa maji na damu. Naye Roho ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli. 7 Kwa maana wako watatu washuhudiao[ mbinguni: hao ni Baba, Neno na Roho Mtakatifu. Hawa watatu ni umoja. 8 Pia wako mashahidi watatu duniani]: Roho, Maji na Damu; hawa watatu wanakubaliana katika umoja. 9 Kama tunaukubali ushuhuda wa wanadamu, basi ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi, kwa kuwa huu ndio ushuhuda wa Mungu kwamba amemshuhudia Mwanawe. 10 Kila mtu amwaminiye Mwana wa Mungu anao huu ushuhuda moyoni mwake. Kila mtu asiyemwamini Mungu amemfanya yeye kuwa mwongo, kwa sababu hakuamini ushuhuda Mungu alioutoa kuhusu Mwanawe.
-
3 Petro akamuuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? 4 Je, kabla hujauza hicho kiwanja si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, fedha ulizopata si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu bali Mungu.”
-
14 Neema ya Bwana Yesu Kristo, na upendo wa Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote. Amen.
-
14 Kisha Yesu akarudi mpaka Galilaya, akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, nazo habari zake zikaenea katika sehemu zote za nchi za kandokando. 15 Akaanza kufundisha kwenye masinagogi yao, na kila mmoja akamsifu.
-
18 Ikimbieni zinaa. Dhambi zingine zote atendazo mtu ziko nje ya mwili wake, lakini yeye aziniye hutenda dhambi ndani ya mwili wake mwenyewe. 19 Je, hamjui ya kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe, 20 kwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu.
-
16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, 17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.
-
7 Kwa hiyo, kama Roho Mtakatifu asemavyo:
“Leo, kama mkiisikia sauti yake,
8 msiifanye mioyo yenu migumu,
kama mlivyofanya katika uasi,
wakati ule wa kujaribiwa jangwani,
9 ambapo baba zenu walinijaribu na kunipima
ingawa kwa miaka arobaini
walikuwa wameyaona matendo yangu.
10 Hiyo ndiyo sababu nilikasirikia kizazi kile,
nami nikasema, ‘Siku zote mioyo yao imepotoka,
nao hawajazijua njia zangu.’
11 Hivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu,
‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’ ”
-
14 kwa sababu kwa dhabihu moja amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wote wanaotakaswa.
15 Pia Roho Mtakatifu anatushuhudia kuhusu jambo hili. Kwanza anasema:
16 “Hili ndilo Agano nitakalofanya nao
baada ya siku hizo, asema Bwana.
Nitaziweka sheria zangu mioyoni mwao,
na kuziandika katika nia zao.”
17 Kisha aongeza kusema:
“Dhambi zao na kutokutii kwao
sitakumbuka tena.”
-
18 Kwa kuwa waliwaambia, “Siku za mwisho kutakuwa na watu wenye kudhihaki, watakaofuata tamaa zao wenyewe za upotovu.” 19 Hawa ndio watu wanaowagawa ninyi, wafuatao tamaa zao za asili, wala hawana Roho.
20 Lakini ninyi wapendwa, jijengeni katika imani yenu iliyo takatifu sana tena ombeni katika Roho Mtakatifu. 21 Jilindeni katika upendo wa Mungu mkitazamia kwa furaha rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo ili awalete katika uzima wa milele.
-
7 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa haki ya kula matunda toka kwa mti wa uzima, ambao uko katika paradiso ya Mungu.
-
38 Hivyo Farao akawauliza, “Je tunaweza kumpata yeyote kama mtu huyu, ambaye Roho wa Mungu yumo ndani yake?”
39 Ndipo Farao akamwambia Yosefu, “Maadamu Mungu amekufunulia yote haya, hakuna mwingine yeyote mwenye akili na hekima kama wewe.
-
25 Yesu alijua walichokuwa wakiwaza, hivyo akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Hali kadhalika kila mji au watu wa nyumba moja waliogawanyika dhidi yao wenyewe hawawezi kusimama. 26 Kama Shetani akimtoa Shetani, atakuwa amegawanyika yeye mwenyewe. Basi ufalme wake utawezaje kusimama? 27 Nami kama natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, watu wenu je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu. 28 Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa Roho wa Mungu, basi Ufalme wa Mungu umekuja juu yenu.
29 “Au tena, mtu awezaje kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Akishamfunga, ndipo hakika anaweza kuteka nyara mali zake.
-
14 Kwa sababu hii nampigia Baba magoti, 15 ambaye ubaba wote wa kila jamaa za mbinguni na za duniani unatokana naye. 16 Namwomba Mungu awaimarishe kwa kuwatia nguvu mioyo yenu kwa njia ya Roho wake kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, 17 ili kwamba, Kristo apate kukaa mioyoni mwenu kwa njia ya imani. Nami ninaomba kwamba ninyi mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo, 18 mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Kristo, 19 na kujua upendo huu unaopita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu.
-
24 Wale wote wanaozishika amri zake hukaa ndani yake na yeye ndani yao. Hivi ndivyo tunavyojua kwamba anakaa ndani yetu. Nasi twajua hili kwa njia ya Roho yule aliyetupa.
-
3 Ndipo Bwana akasema, “Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye ni wa kufa, siku zake zitakuwa miaka 120.”
-
6 Kwa neno la Bwana mbingu ziliumbwa,
jeshi lao la angani kwa pumzi ya kinywa chake.
-
16 “Nikaribieni na msikilize hili:
“Tangu tangazo la kwanza sikusema kwa siri;
wakati litokeapo, nitakuwako hapo.”
Sasa Bwana Mwenyezi amenituma,
kwa Roho wake.
17 Hili ndilo asemalo Bwana,
Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli:
“Mimi ni Bwana, Mungu wako,
nikufundishaye ili upate faida,
nikuongozaye katika njia ikupasayo kuiendea.
-
11 “Mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba. Lakini nyuma yangu anakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuvichukua viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 12 Pepeto lake liko mkononi mwake, naye atasafisha sakafu yake ya kupuria, na kuikusanya ngano ghalani na kuyateketeza makapi kwa moto usiozimika.”
-
15 Lakini Yesu alipoyatambua mawazo yao, akaondoka mahali hapo. Watu wengi wakamfuata, naye akawaponya wagonjwa wao wote, 16 akiwakataza wasiseme yeye ni nani. 17 Hii ilikuwa ili litimie lile neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kusema:
18 “Tazama mtumishi wangu niliyemchagua,
mpendwa wangu, ninayependezwa naye.
Nitaweka Roho wangu juu yake,
naye atatangaza haki kwa mataifa.
-
16 Yohana akawajibu akawaambia, “Mimi nawabatiza kwa maji. Lakini atakuja aliye na nguvu kuniliko mimi, ambaye sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 17 Pepeto lake liko mkononi, tayari kusafisha sakafu yake ya kupuria na kuikusanya ngano ghalani, lakini makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.”
-
21 Yesu akawaambia tena, “Amani iwe nanyi! Kama vile Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawatuma ninyi.” 22 Naye alipokwisha kusema haya, akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. 23 Mkimwondolea mtu yeyote dhambi zake, zitaondolewa, na yeyote msiyemwondolea dhambi zake, hazitaondolewa.”
-
18 Kwa maana sitathubutu kusema kitu chochote zaidi ya kile ambacho Kristo amefanya kwa kunitumia mimi katika kuwaongoza watu wa Mataifa wamtii Mungu kwa yale niliyosema na kufanya, 19 kwa nguvu za ishara na miujiza, kwa uweza wa Roho wa Mungu, hivyo kuanzia Yerusalemu hadi maeneo yote ya kandokando yake mpaka Iliriko, nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa ukamilifu. 20 Hivyo ni nia yangu kuhubiri Habari Njema, si pale ambapo Kristo amekwisha kujulikana, ili nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine.
-
3 Mimi nilikuja kwenu nikiwa dhaifu na mwenye hofu na kwa kutetemeka sana. 4 Kuhubiri kwangu na ujumbe wangu haukuwa kwa hekima na maneno ya ushawishi bali kwa madhihirisho ya nguvu za Roho 5 ili imani yenu isiwe imejengwa katika hekima ya wanadamu bali katika nguvu za Mungu.
-
21 Basi ni Mungu atufanyaye sisi pamoja nanyi kusimama imara katika Kristo. Ametutia mafuta 22 kwa kututia muhuri wake na kutupa Roho wake mioyoni mwetu kuwa rehani kwa ajili ya kututhibitishia kile kijacho.
-
13 Tunajua kwamba twakaa ndani yake na yeye ndani yetu, kwa sababu ametupa sisi sehemu ya Roho wake.
Shows Read in context, Share and Copy.