35 Bible Verses About Loneliness

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Loneliness
  1. 18 Bwana Mungu akasema, “Si vyema huyu mtu awe peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.”

    19 Basi Bwana Mungu alikuwa amefanyiza kutoka ardhi wanyama wote wa porini na ndege wote wa angani. Akawaleta kwa huyu mtu aone atawaitaje, nalo jina lolote alilokiita kila kiumbe hai, likawa ndilo jina lake. 20 Hivyo Adamu akawapa majina wanyama wote wa kufugwa, ndege wa angani, na wanyama wote wa porini.

    Lakini kwa Adamu hakupatikana msaidizi wa kumfaa. 21 Hivyo Bwana Mungu akamfanya Adamu kulala usingizi mzito, naye alipokuwa amelala akachukua moja ya mbavu zake, akapafunika mahali pale kwa nyama. 22 Kisha Bwana Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwenye ule ubavu aliouchukua kutoka kwa huyo mwanaume, akamleta huyo mwanamke kwa huyo mwanaume.

    23 Huyo mwanaume akasema,

    “Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu

    na nyama ya nyama yangu,

    ataitwa ‘mwanamke,’

    kwa kuwa alitolewa katika mwanaume.”

    24 Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.

  2. 5 Baba wa yatima, mtetezi wa wajane,

    ni Mungu katika makao yake matakatifu.

    6 Mungu huwaweka wapweke katika jamaa,

    huwaongoza wafungwa wakiimba,

    bali waasi huishi katika nchi kame.

  3. 5 Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,

    “Kamwe sitakuacha,

    wala sitakupungukia.”

    6 Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,

    “Bwana ni msaada wangu; sitaogopa.

    Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”

  4. 35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga? 36 Kama ilivyoandikwa:

    “Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;

    tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.”

    37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

  5. 15 Macho yangu humwelekea Bwana daima,

    kwa kuwa yeye peke yake ndiye ataitoa

    miguu yangu kutoka mtego.

    16 Nigeukie na unihurumie,

    kwa maana mimi ni mpweke na mwenye kuteseka.

    17 Shida za moyo wangu zimeongezeka,

    niokoe katika dhiki yangu.

    18 Uangalie mateso na shida zangu

    na uniondolee dhambi zangu zote.

    19 Tazama adui zangu walivyo wengi,

    pia uone jinsi wanavyonichukia vikali!

    20 Uyalinde maisha yangu na uniokoe,

    usiniache niaibike,

    kwa maana nimekukimbilia wewe.

    21 Uadilifu na uaminifu vinilinde,

    kwa sababu tumaini langu ni kwako.

  6. 15 “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu. 16 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele. 17 Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye anakaa ndani yenu. 18 Sitawaacha ninyi yatima, naja kwenu.

  7. 9 Usinifiche uso wako,

    usimkatae mtumishi wako kwa hasira;

    wewe umekuwa msaada wangu.

    Usinikatae wala usiniache,

    Ee Mungu Mwokozi wangu.

    10 Hata kama baba yangu na mama wakiniacha,

    Bwana atanipokea.

  8. 18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”

  9. 33 Ilipofika saa sita, giza liliifunika nchi yote hadi saa tisa. 34 Mnamo saa tisa, Yesu akapaza sauti, akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”)

  10. 16 Katika utetezi wangu wa mara ya kwanza, hakuna hata mmoja aliyeniunga mkono, bali kila mmoja aliniacha. Namwomba Mungu wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. 17 Lakini Bwana alisimama upande wangu akanitia nguvu, ili kupitia kwangu lile Neno lihubiriwe kwa ukamilifu, watu wote Mataifa wapate kulisikia. Mimi niliokolewa kutoka kinywa cha simba. 18 Bwana ataniokoa katika kila shambulio baya na kunileta salama katika Ufalme wake wa mbinguni. Atukuzwe yeye milele na milele. Amen.

  11. 10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;

    usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.

    Nitakutia nguvu na kukusaidia;

    nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.

  12. 7 Tena nikaona kitu kingine kilicho ubatili chini ya jua:

    8 Kulikuwepo mwanadamu aliye peke yake,

    hakuwa na mwana wala ndugu.

    Hapakuwa na mwisho wa kazi yake,

    hata hivyo macho yake

    hayakutosheka na utajiri wake.

    Aliuliza, “Ninajitaabisha hivi kwa ajili ya nani,

    nami kwa nini ninajinyima kufurahia?”

    Hili pia ni ubatili,

    ni shughuli yenye taabu!

    9 Wawili ni afadhali kuliko mmoja,

    kwa sababu wana malipo mazuri kwa kazi yao:

    10 Kama mmoja akianguka,

    mwenzake atamwinua.

    Lakini ni jambo la kuhuzunisha

    kwa mtu yule aangukaye

    naye hana wa kumwinua!

    11 Pia, kama wawili wakilala pamoja

    watapashana joto.

    Lakini ni vipi mtu aweza

    kujipasha joto mwenyewe?

    12 Ingawa mtu mmoja aweza kushindwa,

    watu wawili wanaweza

    kumkabili adui na kumshinda.

    Kamba ya nyuzi tatu

    haikatiki kwa urahisi.

  13. 28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

  14. 4 Hata kama nikipita katikati

    ya bonde la uvuli wa mauti,

    sitaogopa mabaya,

    kwa maana wewe upo pamoja nami;

    fimbo yako na mkongojo wako

    vyanifariji.

    5 Waandaa meza mbele yangu

    machoni pa adui zangu.

    Umenipaka mafuta kichwani pangu,

    kikombe changu kinafurika.

    6 Hakika wema na upendo vitanifuata

    siku zote za maisha yangu,

    nami nitakaa nyumbani mwa Bwana

    milele.

  15. 31 Yesu akawajibu, “Je, sasa mnaamini? 32 Saa inakuja, naam, imekwisha kuwadia, mtakapotawanyika kila mmoja kwenda nyumbani kwake na kuniacha peke yangu. Lakini mimi siko peke yangu kwa sababu Baba yu pamoja nami. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

  16. 6 Kuweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu anakwenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.”

  17. 3 Alidharauliwa na kukataliwa na wanadamu,

    mtu wa huzuni nyingi, ajuaye mateso.

    Kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,

    alidharauliwa, wala hatukumhesabu kuwa kitu.

    4 Hakika alichukua udhaifu wetu

    na akajitwika huzuni zetu,

    hata hivyo tulidhania kuwa amepigwa na Mungu,

    akapigwa sana naye, na kuteswa.

    5 Lakini alitobolewa kwa ajili ya makosa yetu,

    alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu;

    adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake,

    na kwa majeraha yake sisi tumepona.

    6 Sisi sote, kama kondoo, tumepotea,

    kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe,

    naye Bwana aliweka juu yake

    maovu yetu sisi sote.

  18. 35 Alfajiri na mapema sana kulipokuwa bado kuna giza, Yesu akaamka, akaondoka, akaenda mahali pa faragha ili kuomba.

  19. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”

  20. 24 Mtu mwenye marafiki wengi wanaweza kumharibu,

    bali yuko rafiki aambatanaye na mtu kwa karibu kuliko ndugu.

  21. 15 “Je, mama aweza kumsahau mtoto

    aliyeko matitini mwake akinyonya,

    wala asiwe na huruma

    juu ya mtoto aliyemzaa?

    Ingawa anaweza kusahau,

    mimi sitakusahau wewe!

    16 Tazama, nimekuchora kama muhuri

    katika vitanga vya mikono yangu,

    kuta zako zi mbele yangu daima.

  22. 8 Bwana mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.”

  23. 4 Kamba za mauti zilinizunguka,

    mafuriko ya maangamizi yalinilemea.

    5 Kamba za kuzimu zilinizunguka,

    mitego ya mauti ilinikabili.

    6 Katika shida yangu nalimwita Bwana,

    nilimlilia Mungu wangu anisaidie.

    Kutoka hekaluni mwake alisikia sauti yangu,

    kilio changu kikafika mbele zake,

    masikioni mwake.

  24. 23 Hata hivyo niko pamoja nawe siku zote,

    umenishika mkono wangu wa kuume.

    24 Unaniongoza kwa shauri lako,

    hatimaye utaniingiza katika utukufu.

    25 Nani niliye naye mbinguni ila wewe?

    Dunia haina chochote ninachokitamani ila wewe.

    26 Mwili na moyo wangu vyaweza kushindwa,

    bali Mungu ni nguvu ya moyo wangu

    na fungu langu milele.

  25. 1 Kisha Yesu akaongozwa na Roho Mtakatifu kwenda nyikani ili akajaribiwe na ibilisi. 2 Baada ya kufunga siku arobaini usiku na mchana, hatimaye akaona njaa.

  26. 14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

  27. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa utenzi wa “Kulungu wa Alfajiri.” Zaburi ya Daudi.

    1 Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?

    Kwa nini uko mbali hivyo kuniokoa?

    Mbali hivyo na maneno ya kuugua kwangu?

    2 Ee Mungu wangu, ninalia mchana, lakini hunijibu,

    hata usiku, sinyamazi.

  28. 7 Niende wapi nijiepushe na Roho yako?

    Niende wapi niukimbie uso wako?

    8 Kama nikienda juu mbinguni, wewe uko huko;

    nikifanya vilindi kuwa kitanda changu,

    wewe uko huko.

    9 Kama nikipanda juu ya mbawa za mapambazuko,

    kama nikikaa pande za mbali za bahari,

    10 hata huko mkono wako utaniongoza,

    mkono wako wa kuume utanishika kwa uthabiti.

  29. 4 Tazama kuume kwangu na uone,

    hakuna hata mmoja anayejihusisha nami.

    Sina kimbilio,

    hakuna anayejali maisha yangu.

  30. 16 Maneno yako yalipokuja, niliyala;

    yakawa shangwe yangu

    na furaha ya moyo wangu,

    kwa kuwa nimeitwa kwa jina lako,

    Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote.

    17 Kamwe sikuketi katika kundi la wafanyao sherehe,

    wala kamwe sikujifurahisha pamoja nao;

    niliketi peke yangu kwa sababu mkono wako ulikuwa juu yangu,

    na wewe ulikuwa umenijaza hasira.

  31. 3 Waheshimu wanawake wajane ambao ni wajane kweli kweli. 4 Kama mjane ana watoto ama wajukuu, hawa inawapasa awali ya yote wajifunze kutimiza wajibu wao wa kumcha Mungu katika matendo kwa kuwatunza wale wa jamaa zao wenyewe, na hivyo wawarudishie wema waliowatendea wazazi wao, kwa kuwa hivi ndivyo impendezavyo Mungu. 5 Mwanamke ambaye ni mjane kweli kweli, yaani, yeye aliyebaki peke yake huweka tumaini lake kwa Mungu naye hudumu katika maombi usiku na mchana akimwomba Mungu ili amsaidie. 6 Lakini mjane aishiye kwa anasa amekufa, ingawa anaishi.

  32. 17 Wenye haki hulia, naye Bwana huwasikia,

    huwaokoa katika taabu zao zote.

    18 Bwana yu karibu na waliovunjika moyo,

    na huwaokoa waliopondeka roho.

  33. 11 Rafiki na wenzangu wananikwepa

    kwa sababu ya majeraha yangu;

    majirani zangu wanakaa mbali nami.

  34. 28 Je wewe, hufahamu?

    Je wewe, hujasikia?

    Bwana ni Mungu wa milele,

    Muumba wa miisho ya dunia.

    Hatachoka wala kulegea,

    wala hakuna hata mmoja

    awezaye kuupima ufahamu wake.

    29 Huwapa nguvu waliolegea

    na huongeza nguvu za wadhaifu.

    30 Hata vijana huchoka na kulegea,

    nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,

    31 bali wale wamtumainio Bwana

    atafanya upya nguvu zao.

    Watapaa juu kwa mbawa kama tai;

    watapiga mbio wala hawatachoka,

    watatembea kwa miguu wala hawatazimia.

  35. 20 Kwa kuwa wanapokusanyika pamoja watu wawili au watatu kwa Jina langu, mimi niko papo hapo pamoja nao.”