57 Bible Verses About Satan

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Satan
  1. 3 Kisha ishara nyingine ikaonekana mbinguni: Likaonekana joka kubwa jekundu lenye vichwa saba na pembe kumi na taji saba katika vichwa vyake. 4 Mkia wake ukakokota theluthi ya nyota zote angani na kuziangusha katika nchi. Ndipo lile joka likasimama mbele ya yule mwanamke aliyekuwa karibu kuzaa ili lipate kumla huyo mtoto mara tu atakapozaliwa. 5 Yule mwanamke akazaa mtoto mwanaume, atakayeyatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya utawala ya chuma. Lakini huyo mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu kwenye kiti chake cha enzi. 6 Yule mwanamke akakimbilia jangwani, ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali ili apate kutunzwa huko kwa muda wa siku 1,260.

    7 Basi palikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na hilo joka, nalo joka pamoja na malaika zake likapigana nao. 8 Lakini joka na malaika zake wakashindwa, na hapakuwa tena na nafasi yao huko mbinguni. 9 Lile joka kuu likatupwa chini, yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani, aupotoshaye ulimwengu wote. Akatupwa chini duniani, yeye pamoja na malaika zake.

  2. 10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za ibilisi. 12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 13 Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara. 14 Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15 nayo miguu yenu ifungiwe utayari tuupatao kwa Injili ya amani. 16 Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

  3. 1 Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, akiwa ameshika ufunguo wa lile Shimo na mnyororo mkubwa mkononi mwake. 2 Akalishika lile joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ndiye ibilisi au Shetani, naye akamfunga kwa muda wa miaka 1,000. 3 Akamtupa katika lile Shimo, akamfunga humo na kulitia lakiri, ili kumzuia asiendelee kudanganya mataifa mpaka hiyo miaka 1,000 itimie. Baada ya hayo lazima afunguliwe kwa muda mfupi.

    4 Kisha nikaona viti vya enzi vilivyokuwa vimekaliwa na hao waliopewa mamlaka ya kuhukumu, na nikaona roho za wale waliokatwa vichwa kwa sababu ya ushuhuda wa Yesu na kwa sababu ya neno la Mungu. Hawakuwa wamemsujudu huyo mnyama wala sanamu yake wala hawakupokea ile chapa yake kwenye vipaji vya nyuso zao au kwenye mikono yao. Wakawa hai na kutawala pamoja na Kristo miaka 1,000. 5 (Wafu waliosalia hawakufufuka mpaka ilipotimia hiyo miaka 1,000.) Huu ndio ufufuo wa kwanza. 6 Waliobarikiwa na walio watakatifu ni wale walio na sehemu katika ufufuo wa kwanza. Hao mauti ya pili haina nguvu juu yao, bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye kwa muda wa miaka 1,000.

    7 Hiyo miaka 1,000 itakapotimia, Shetani atafunguliwa kutoka kifungoni mwake, 8 naye atatoka ili kuyadanganya mataifa yaliyopo katika pembe nne za dunia, yaani, Gogu na Magogu apate kuwakusanya tayari kwa vita. Idadi yao ni kama mchanga ulioko pwani. 9 Nao walitembea katika eneo lote la dunia, wakaizunguka kambi ya watakatifu na ule mji unaopendwa. Lakini moto ukashuka kutoka mbinguni na kuwateketeza. 10 Naye ibilisi aliyewadanganya akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti walikokuwa wametupwa yule mnyama na yule nabii wa uongo. Watateswa humo usiku na mchana, milele na milele.

  4. 8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza. 9 Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.

    10 Nanyi mkiisha kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Kristo, yeye mwenyewe atawarejesha na kuwatia nguvu, akiwaimarisha na kuwathibitisha.

  5. 6 Siku moja wana wa Mungu walikwenda kujionyesha mbele za Bwana. Shetani naye akaja pamoja nao. 7 Bwana akamwambia Shetani, “Umetoka wapi?”

    Shetani akamjibu Bwana, “Natoka kuzunguka pote duniani, nikitembea huku na huko humo.”

    8 Ndipo Bwana akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Hakuna mtu mwingine duniani aliye kama yeye, asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu, na kuepukana na uovu.”

    9 Shetani akamjibu Bwana, “Je, Ayubu anamcha Mungu bure? 10 Je, wewe hukumjengea boma pande zote yeye na wa nyumbani mwake pamoja na kila kitu alicho nacho? Kazi za mikono yake umezibariki na hivyo makundi yake ya kondoo na mbuzi pamoja na ya wanyama yameenea katika nchi nzima. 11 Lakini nyoosha mkono wako na kupiga kila kitu alicho nacho, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.”

    12 Bwana akamwambia Shetani, “Vema sana, kwa hiyo, kila kitu alicho nacho kiko mikononi mwako, lakini juu ya huyo mtu mwenyewe usimguse hata kwa kidole.”

    Ndipo Shetani akatoka mbele za Bwana.

  6. 7 Watoto wapendwa, mtu yeyote asiwadanganye. Kila mtu atendaye haki ana haki, kama yeye alivyo na haki. 8 Yeye atendaye dhambi ni wa ibilisi, kwa sababu ibilisi amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili aziangamize kazi za ibilisi. 9 Yeyote aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wa Mungu wakaa ndani yake, wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa na Mungu. 10 Kwa jinsi hii tunaweza kujua dhahiri watoto wa Mungu na pia watoto wa ibilisi. Yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.

    11 Hili ndilo neno mlilolisikia tangu mwanzo: Kwamba imetupasa tupendane sisi kwa sisi. 12 Msiwe kama Kaini aliyekuwa wa yule mwovu akamuua ndugu yake. Basi kwa nini alimuua? Ni kwa sababu matendo yake Kaini yalikuwa mabaya na ya ndugu yake yalikuwa ya haki.

  7. 42 Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda, kwa maana nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, ila yeye alinituma. 43 Kwa nini hamwelewi ninayowaambia? Ni kwa sababu hamwezi kusikia nisemacho. 44 Ninyi ni watoto wa baba yenu ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli maana hamna kweli ndani yake. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo. 45 Lakini kwa sababu nimewaambia kweli hamkuniamini! 46 Je, kuna yeyote miongoni mwenu awezaye kunithibitisha kuwa mwenye dhambi? Kama nawaambia yaliyo kweli, mbona hamniamini? 47 Yeye atokaye kwa Mungu husikia kile Mungu asemacho. Sababu ya ninyi kutosikia ni kwa kuwa hamtokani na Mungu.”

  8. 12 Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni,

    ewe nyota ya asubuhi, mwana wa mapambazuko!

    Umetupwa chini duniani,

    wewe uliyepata kuangusha mataifa!

    13 Ulisema moyoni mwako,

    “Nitapanda juu hadi mbinguni,

    nitakiinua kiti changu cha enzi

    juu ya nyota za Mungu,

    nitaketi nimetawazwa

    juu ya mlima wa kusanyiko,

    kwenye vimo vya juu sana vya Mlima Mtakatifu.

    14 Nitapaa juu kupita mawingu,

    nitajifanya kama Yeye Aliye Juu Sana.”

    15 Lakini umeshushwa chini hadi kuzimu,

    hadi kwenye vina vya shimo.

  9. 1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini ambao Bwana Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati kweli Mungu alisema, ‘Kamwe msile matunda ya mti wowote wa bustanini’?”

    2 Mwanamke akamjibu nyoka, “Tunaweza kula matunda ya miti iliyoko bustanini, 3 lakini Mungu alisema, ‘Kamwe msile tunda la mti ulio katikati ya bustani, wala kuugusa, la sivyo mtakufa.’ ”

    4 Lakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa. 5 Kwa maana Mungu anajua ya kuwa wakati mtakapoyala, macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”

  10. 7 Basi mtiini Mungu. Mpingeni ibilisi, naye atawakimbia. 8 Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu ninyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu ninyi wenye nia mbili. 9 Huzunikeni, ombolezeni na kulia. Kicheko chenu na kigeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa huzuni. 10 Jinyenyekezeni mbele za Bwana, naye atawainua.

  11. 41 “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake.

  12. 24 Lakini Mafarisayo waliposikia jambo hili wakasema, “Mtu huyu anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo wachafu.”

    25 Yesu alijua walichokuwa wakiwaza, hivyo akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Hali kadhalika kila mji au watu wa nyumba moja waliogawanyika dhidi yao wenyewe hawawezi kusimama. 26 Kama Shetani akimtoa Shetani, atakuwa amegawanyika yeye mwenyewe. Basi ufalme wake utawezaje kusimama? 27 Nami kama natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, watu wenu je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu. 28 Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa Roho wa Mungu, basi Ufalme wa Mungu umekuja juu yenu.

    29 “Au tena, mtu awezaje kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Akishamfunga, ndipo hakika anaweza kuteka nyara mali zake.

  13. 12 Nami nitaendelea kufanya lile ninalofanya sasa ili nisiwape nafasi wale ambao wanatafuta nafasi ya kuhesabiwa kuwa sawa na sisi katika mambo wanayojisifia.

    13 Watu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Kristo. 14 Wala hii si ajabu, kwa kuwa hata Shetani mwenyewe hujigeuza aonekane kama malaika wa nuru. 15 Kwa hiyo basi si ajabu, kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili.

  14. 17 Wale sabini na wawili wakarudi kwa furaha, na kusema, “Bwana, hata pepo wachafu wanatutii kwa jina lako.”

    18 Yesu akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme wa radi.

  15. 30 Yesu akawaambia, “Sauti hii imesikika kwa faida yenu, wala si kwa faida yangu. 31 Sasa ni saa ya hukumu kwa ajili ya ulimwengu huu, sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.

  16. 1 Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, akiwa amesimama mbele ya malaika wa Bwana, naye Shetani amesimama upande wake wa kuume ili amshtaki. 2 Bwana akamwambia Shetani, “Bwana akukemee Shetani! Bwana, ambaye ameichagua Yerusalemu, akukemee! Je, mtu huyu siyo kijinga kinachowaka kilichonyakuliwa kwenye moto?”

    3 Wakati huu, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu alipokuwa amesimama mbele ya malaika. 4 Malaika akawaambia wale waliokuwa wamesimama mbele yake, “Mvueni hizo nguo zake chafu.”

    Kisha akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeiondoa dhambi yako, nami nitakuvika mavazi ya kitajiri.”

    5 Kisha nikasema, “Mvike kilemba kilicho safi kichwani mwake.” Kwa hiyo wakamvika kilemba safi kichwani na kumvika yale mavazi mengine, wakati malaika wa Bwana akiwa amesimama karibu.

  17. 1 Shetani akainuka dhidi ya Israeli na kumshawishi Daudi ahesabu watu wa Israeli. 2 Kwa hiyo Daudi akamwambia Yoabu na majemadari wa jeshi, “Nendeni mkawahesabu Waisraeli kuanzia Beer-Sheba mpaka Dani. Kisha nileteeni taarifa ili kwamba niweze kufahamu wako wangapi.”

  18. 31 Yesu akasema, “Simoni, Simoni, sikiliza, Shetani ameomba kuwapepeta ninyi wote kama ngano. 32 Lakini nimekuombea wewe Simoni ili imani yako isishindwe, nawe ukiisha kunirudia, uwaimarishe ndugu zako.”

    33 Petro akajibu, “Bwana, niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani na hata kifoni.”

    34 Yesu akamjibu, “Ninakuambia Petro, kabla jogoo hajawika usiku wa leo, utakana mara tatu kwamba hunijui mimi.”

  19. 6 Nao malaika ambao hawakulinda nafasi zao, lakini wakayaacha makao yao, hawa amewaweka katika giza, wakiwa wamefungwa kwa minyororo ya milele kwa ajili ya hukumu Siku ile kuu. 7 Vivyo hivyo, Sodoma na Gomora na pia ile miji iliyokuwa kandokando, ambayo kwa jinsi moja na hao, walijifurahisha kwa uasherati na kufuata tamaa za mwili zisizo za asili, waliwekwa wawe mfano kwa kuadhibiwa katika moto wa milele.

    8 Vivyo hivyo, hawa waotao ndoto huutia mwili unajisi, hukataa kuwa chini ya mamlaka na kunena mabaya juu ya wenye mamlaka. 9 Lakini hata malaika mkuu Mikaeli alipokuwa anashindana na ibilisi juu ya mwili wa Mose, hakuthubutu kumlaumu, bali alimwambia, “Bwana na akukemee!”

  20. 13 Ndipo Bwana Mungu akamuuliza mwanamke, “Ni nini hili ambalo umelifanya?” Mwanamke akajibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”

    14 Hivyo Bwana Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hili,

    “Umelaaniwa kuliko wanyama wote

    wa kufugwa na wa porini!

    Utatambaa kwa tumbo lako

    na kula mavumbi

    siku zote za maisha yako.

    15 Nami nitaweka uadui

    kati yako na huyo mwanamke,

    na kati ya uzao wako na wake,

    yeye atakuponda kichwa,

    nawe utamuuma kisigino.”

  21. 13 Kwa maana ametuokoa kutoka ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa, 14 ambaye katika yeye tunao ukombozi, yaani msamaha wa dhambi.

    15 Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16 Kwake yeye vitu vyote vilivyoko mbinguni na juu ya nchi viliumbwa: vitu vinavyoonekana na visivyoonekana, viwe ni viti vya enzi au falme, au wenye mamlaka au watawala; vitu vyote viliumbwa na yeye na kwa ajili yake. 17 Yeye alikuwepo kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja.

  22. 14 Basi kwa kuwa watoto wana nyama na damu, yeye pia alishiriki katika ubinadamu wao, ili kwa kifo chake, apate kumwangamiza huyo mwenye nguvu za mauti, yaani ibilisi, 15 na kuwaweka huru wale waliokuwa utumwani maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa mauti.

  23. 8 Kwa mara nyingine, ibilisi akamchukua Yesu mpaka kwenye kilele cha mlima mrefu na kumwonyesha falme zote za dunia na fahari zake, 9 kisha akamwambia, “Nitakupa hivi vyote kama ukinisujudia na kuniabudu.”

    10 Yesu akamwambia, “Ondoka mbele yangu, Shetani! Kwa maana imeandikwa, ‘Mwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’ ”

    11 Ndipo ibilisi akamwacha, nao malaika wakaja na kumhudumia.

  24. 21 Tangu wakati huo, Yesu alianza kuwaeleza wanafunzi wake kwamba hana budi kwenda Yerusalemu na kupata mateso mengi mikononi mwa wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa sheria, na kwamba itampasa auawe lakini siku ya tatu kufufuliwa.

    22 Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea akisema, “Haiwezekani, Bwana! Jambo hili kamwe halitakupata!”

    23 Lakini Yesu akageuka na kumwambia Petro, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

  25. 17 Ndugu zangu, nawasihi mjihadhari na kujiepusha na wale watu waletao matengano na kuweka vikwazo mbele yenu dhidi ya mafundisho mliyojifunza. 18 Kwa maana watu kama hao hawamtumikii Bwana Kristo, bali wanatumikia tamaa zao wenyewe. Kwa kutumia maneno laini na ya kubembeleza, hupotosha mioyo ya watu wajinga. 19 Kila mtu amesikia juu ya utii wenu, nami nimejawa na furaha tele kwa ajili yenu. Lakini nataka mwe na hekima katika mambo mema na bila hatia katika mambo maovu.

    20 Mungu wa amani atamponda Shetani chini ya miguu yenu upesi.

    Neema ya Bwana wetu Yesu iwe nanyi. Amen.

  26. 3 Bwana akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Hakuna mtu mwingine duniani aliye kama yeye, mtu asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Naye bado anadumisha uadilifu wake, ingawa ulinichochea dhidi yake, ili nimwangamize pasipo sababu.”

    4 Shetani akamjibu Bwana, “Ngozi kwa ngozi! Mwanadamu atatoa vyote alivyo navyo kwa ajili ya uhai wake. 5 Lakini nyoosha mkono wako na kuipiga nyama yake na mifupa yake, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.”

    6 Bwana akamwambia Shetani, “Vema sana, kwa hiyo, yeye yumo mikononi mwako, lakini lazima umwachie uhai wake.”

    7 Basi Shetani akatoka mbele za Bwana naye akampiga Ayubu kwa majipu mabaya tangu nyayo za miguu yake hadi utosi wa kichwa.

  27. 1 Wapendwa, msiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho mwone kama zimetoka kwa Mungu, kwa sababu manabii wengi wa uongo wametokea ulimwenguni. 2 Hivi ndivyo mnavyoweza kutambua Roho wa Mungu: Kila roho inayokubali kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatoka kwa Mungu. 3 Lakini kila roho ambayo haimkubali Yesu haitoki kwa Mungu. Hii ndiyo roho ya mpinga Kristo, ambayo mmesikia kwamba inakuja na sasa tayari iko ulimwenguni.

    4 Watoto wapendwa, ninyi mmetokana na Mungu, nanyi mmewashinda kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika ulimwengu. 5 Wao wanatokana na ulimwengu na kwa hiyo hunena yaliyo ya ulimwengu, hivyo ulimwengu huwasikiliza.

  28. 37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

  29. 13 Hakuna jaribu lolote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu; hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kutokea ili mweze kustahimili.

  30. 1 Hili ni neno la kuaminiwa, kwamba mtu akitamani kazi ya uangalizi, atamani kazi nzuri. 2 Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha, 3 asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha. 4 Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia. 5 (Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kanisa la Mungu?) 6 Asiwe mtu aliyeokoka karibuni asije akajivuna na kuangukia kwenye hukumu ile ile ya ibilisi. 7 Inampasa pia awe na sifa njema kwa watu walio nje, ili asije akalaumiwa na kuanguka kwenye mtego wa ibilisi.

  31. 7 Lakini nawaambia kweli, yafaa mimi niondoke, kwa kuwa nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu, lakini nikienda nitamtuma kwenu. 8 Naye atakapokuja, atauthibitishia ulimwengu kuhusu dhambi, haki na hukumu. 9 Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi, 10 kwa habari ya haki, kwa sababu ninakwenda kwa Baba, nanyi hamtaniona tena, 11 kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.

  32. 20 Lakini ninyi, hivyo sivyo mlivyojifunza Kristo. 21 Kama hivyo ndivyo ilivyo, ninyi mmemsikia, tena mmefundishwa naye, vile kweli ilivyo katika Yesu. 22 Mlifundishwa kuuvua mwenendo wenu wa zamani, utu wenu wa kale, ulioharibiwa na tamaa zake za udanganyifu, 23 ili mfanywe upya roho na nia zenu, 24 mkajivike utu mpya, ulioumbwa sawasawa na mfano wa Mungu katika haki yote na utakatifu.

    25 Kwa hiyo kila mmoja wenu avue uongo na kuambiana kweli mtu na jirani yake, kwa maana sisi sote tu viungo vya mwili mmoja. 26 Mkikasirika, msitende dhambi, wala jua lisichwe mkiwa bado mmekasirika, 27 wala msimpe ibilisi nafasi.

  33. 7 Maana ile nguvu ya siri ya uasi tayari inatenda kazi, lakini yule anayeizuia ataendelea kufanya hivyo mpaka atakapoondolewa. 8 Hapo ndipo yule mwasi atafunuliwa, ambaye Bwana Yesu atamteketeza kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kabisa kwa utukufu wa kuja kwake. 9 Kuja kwa yule mwasi kutaonekana kana kwamba ni kutenda kazi kwake Shetani ambaye hutumia nguvu zote, ishara, maajabu ya uongo, 10 na kila aina ya uovu kwa wale wanaoangamia kwa sababu walikataa kuipenda kweli wapate kuokolewa.

  34. 14 Hivyo nawashauri wajane vijana waolewe, wazae watoto na wasimamie nyumba zao, wasije wakampa adui nafasi ya kutushutumu. 15 Kwa maana kwa kweli wajane wengine wamepotoka ili kumfuata Shetani.

  35. 1 Wakati huu Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa imekaribia. 2 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwa wanatafuta njia ya kumuua Yesu, kwa sababu waliwaogopa watu. 3 Shetani akamwingia Yuda, aliyeitwa Iskariote, mmoja wa wale Kumi na Wawili. 4 Yuda akaenda kwa viongozi wa makuhani na kwa maafisa wa walinzi wa Hekalu, akazungumza nao jinsi ambavyo angeweza kumsaliti Yesu. 5 Wakafurahi na wakakubaliana kumpa fedha. 6 Naye akakubali, akaanza kutafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Yesu kwao, wakati ambapo hakuna umati wa watu.

  36. 3 Petro akamuuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? 4 Je, kabla hujauza hicho kiwanja si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, fedha ulizopata si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu bali Mungu.”

  37. 17 Lakini ndugu zetu, tulipotenganishwa nanyi kwa kitambo kidogo (ingawa kutengana huko kulikuwa kwa mwili tu, si kwa moyo), tulizidi kuwa na shauku kubwa kuwaona uso kwa uso. 18 Maana tulitaka kuja kwenu, hasa mimi Paulo, nilitaka kuja tena na tena, lakini Shetani akatuzuia.

  38. 9 Naijua dhiki yako na umaskini wako, lakini wewe ni tajiri! Nayajua masingizio ya wale wasemao kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali wao ni sinagogi la Shetani. 10 Usiogope mateso yatakayokupata. Nakuambia ibilisi atawatia baadhi yenu gerezani ili kuwajaribu, nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.

  39. 8 Lakini Elima yule mchawi (hii ndiyo maana ya jina lake), aliwapinga Barnaba na Sauli na kujaribu kumpotosha yule mkuu wa kile kisiwa aiache imani. 9 Ndipo Sauli, ambaye pia aliitwa Paulo, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akamkazia macho Elima huyo mchawi, 10 akamwambia, “Ewe mwana wa ibilisi, wewe ni adui wa kila kilicho haki! Umejaa kila aina ya udanganyifu na ulaghai. Je, hutaacha kuzipotosha njia za Bwana zilizonyooka?

  40. 22 Zikimbie tamaa mbaya za ujana, ufuate haki, imani, upendo na amani pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi. 23 Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa wajua ya kwamba hayo huzaa magomvi. 24 Tena haimpasi mtumishi wa Bwana kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu. 25 Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli, 26 ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake.

  41. 4 Kwa maana, kama Mungu hakuwasamehe malaika walipotenda dhambi, bali aliwatupa kuzimu katika vifungo vya giza wakae humo mpaka ije hukumu; 5 kama hakuusamehe ulimwengu wa kale alipoleta gharika juu ya watu wale wasiomcha Mungu, bali akamhifadhi Noa, mhubiri wa haki, pamoja na watu wengine saba; 6 kama aliihukumu miji ya Sodoma na Gomora kwa kuiteketeza kwa moto ikawa majivu, na kuifanya kuwa kielelezo kwa yale yatakayowapata wale wasiomcha Mungu; 7 na kama alimwokoa Loti, mtu mwenye haki, ambaye alihuzunishwa na maisha machafu ya watu wapotovu 8 (kwa sababu yale matendo mapotovu aliyoyaona na kuyasikia huyo mtu mwenye haki alipoishi miongoni mwao yalimhuzunisha siku baada ya siku): 9 ikiwa hivyo ndivyo, basi Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa wamchao Mungu kutoka majaribu, na kuwaweka waasi katika adhabu hadi siku ya hukumu. 10 Hii ni hakika hasa kwa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kudharau mamlaka.

    Kwa ushupavu na kwa kiburi, watu hawa hawaogopi kunena mabaya dhidi ya viumbe vya mbinguni.

  42. 18 Tunajua ya kuwa yeye aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, bali aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hawezi kumdhuru. 19 Sisi twajua kuwa tu watoto wa Mungu na ya kwamba ulimwengu wote uko chini ya utawala wa yule mwovu. 20 Nasi pia twajua ya kwamba Mwana wa Mungu amekuja, naye ametupa sisi ufahamu ili tupate kumjua yeye aliye Kweli. Nasi tumo ndani yake yeye aliye Kweli, yaani, ndani ya Yesu Kristo Mwanawe. Yeye ndiye Mungu wa kweli na uzima wa milele.

    21 Watoto wapendwa, jilindeni nafsi zenu kutokana na sanamu. Amen.

  43. 19 Mtu yeyote anaposikia neno la Ufalme naye asilielewe, yule mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake. Hii ndiyo ile mbegu iliyopandwa kando ya njia.

  44. 5 Ibilisi akampeleka hadi juu ya mlima mrefu akamwonyesha milki zote za dunia kwa mara moja. 6 Akamwambia, “Nitakupa mamlaka juu ya milki hizi na fahari zake zote, kwa maana zimekabidhiwa mkononi mwangu nami ninaweza kumpa yeyote ninayetaka. 7 Hivyo ikiwa utanisujudia na kuniabudu, vyote vitakuwa vyako.”

    8 Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mwabudu Bwana Mungu wako na umtumikie yeye peke yake.’ ”

  45. 4 Mwanamke hana mamlaka juu ya mwili wake bali mumewe, wala mume hana mamlaka juu ya mwili wake bali mkewe. 5 Msinyimane, isipokuwa mmekubaliana kufanya hivyo kwa muda fulani ili mweze kujitoa kwa maombi, kisha mrudiane tena ili Shetani asije akapata nafasi ya kuwajaribu kwa sababu ya kutokuwa na kiasi.

  46. 10 Kama ninyi mkimsamehe mtu yeyote, mimi pia nimemsamehe. Kile nilichosamehe, kama kulikuwa na kitu chochote cha kusamehe, nimekwisha kusamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu, 11 ili Shetani asitushinde. Kwa maana hatuachi kuzijua hila zake.

  47. 3 Lakini nina hofu kuwa, kama vile Eva alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Kristo.

  48. 22 Walimu wa sheria walioteremka kutoka Yerusalemu walisema, “Amepagawa na Beelzebuli! Anatoa pepo wachafu kwa kutumia mkuu wa pepo wachafu!”

    23 Basi Yesu akawaita na kuzungumza nao kwa mifano akasema: “Shetani awezaje kumtoa Shetani? 24 Kama ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama. 25 Nayo nyumba kama ikigawanyika dhidi yake yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama. 26 Naye Shetani kama akijipinga mwenyewe na awe amegawanyika, hawezi kusimama bali mwisho wake umewadia.

  49. 27 Mara tu baada ya kukipokea kile kipande cha mkate, Shetani akamwingia.

    Yesu akamwambia Yuda, “Lile unalotaka kulitenda litende haraka.”

  50. 15 Siombi kwamba uwaondoe ulimwenguni, bali uwalinde dhidi ya yule mwovu.

  51. 7 Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. 8 Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.

  52. 20 Lakini yule mnyama akakamatwa pamoja na huyo nabii wa uongo ambaye alikuwa amefanya ishara kwa niaba ya huyo mnyama, ambaye kwa ishara hizi aliwadanganya wale waliopokea chapa ya huyo mnyama na kuiabudu sanamu yake. Hawa wawili wakatupwa wakiwa hai ndani ya ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti.

  53. 8 Malaika wa pili akafuata akisema, “Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu, ule uliyafanya mataifa yote kulewa kwa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.”

    9 Malaika wa tatu akawafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Kama mtu yeyote anamwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa chapa yake kwenye kipaji chake cha uso au kwenye mkono wake, 10 yeye pia atakunywa mvinyo wa hasira kali ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake pasipo kuchanganywa na maji. Naye atateswa kwa moto uwakao na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo. 11 Nao moshi wa mateso yao hupanda juu milele na milele. Hakuna mapumziko, mchana wala usiku, kwa wale wamwabuduo huyo mnyama na sanamu yake, au kwa yeyote anayepokea chapa ya jina lake.” 12 Hapa ndipo penye wito wa subira na uvumilivu wa watakatifu; wale wanaozishika amri za Mungu na kudumu katika uaminifu kwa Yesu.

  54. 1 Kisha Yesu akaongozwa na Roho Mtakatifu kwenda nyikani ili akajaribiwe na ibilisi.

  55. 13 Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga kwa siku ishirini na moja. Ndipo Mikaeli, mmoja wa malaika wakuu, alikuja kunisaidia, kwa sababu nilikuwa nimezuiliwa huko na mfalme wa Uajemi.

  56. 15 Hawa ndio wale walio kando ya njia ambako neno lilipandwa. Walisikiapo neno, Shetani huja mara na kulinyakua lile neno lililopandwa ndani yao.

  57. 13 Mtu anapojaribiwa asiseme, “Ninajaribiwa na Mungu.” Kwa maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu wala yeye hamjaribu mtu yeyote. 14 Lakini kila mtu hujaribiwa wakati anapovutwa na kudanganywa na tamaa zake mwenyewe zilizo mbaya. 15 Basi ile tamaa mbaya ikishachukua mimba, huzaa dhambi, nayo ile dhambi ikikomaa, huzaa mauti.