48 Bible Verses About False Prophets

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About False Prophets
  1. 15 “Jihadharini na manabii wa uongo, wanaowajia wakiwa wamevaa mavazi ya kondoo, lakini ndani ni mbwa mwitu wakali. 16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je, watu huchuma zabibu kwenye miiba, au tini kwenye michongoma? 17 Vivyo hivyo, mti mwema huzaa matunda mazuri, na mti mbaya huzaa matunda mabaya. 18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. 19 Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. 20 Hivyo, mtawatambua kwa matunda yao.

    21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22 Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’ 23 Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’

    24 “Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. 25 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, na upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba. Lakini haikuanguka; kwa sababu msingi wake ulikuwa kwenye mwamba. 26 Naye kila anayesikia haya maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. 27 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.”

  2. 13 “Miongoni mwa manabii wa Samaria

    nililiona jambo la kuchukiza:

    Walitabiri kwa Baali

    na kuwapotosha Israeli watu wangu.

    14 Nako miongoni mwa manabii wa Yerusalemu

    nimeona jambo baya sana:

    Wanafanya uzinzi

    na kuenenda katika uongo.

    Wanatia nguvu mikono ya watenda mabaya,

    kwa ajili hiyo hakuna yeyote

    anayeachana na uovu wake.

    Wote wako kama Sodoma kwangu;

    watu na Yerusalemu wako kama Gomora.”

    15 Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo kuhusu manabii:

    “Nitawafanya wale chakula kichungu

    na kunywa maji yaliyotiwa sumu,

    kwa sababu kutokana na manabii wa Yerusalemu

    kutokumcha Mungu kumeenea katika nchi yote.”

    16 Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo:

    “Msisikilize wanachowatabiria manabii,

    wanawajaza matumaini ya uongo.

    Wanasema maono kutoka akili zao wenyewe,

    hayatoki katika kinywa cha Bwana.

    17 Huendelea kuwaambia wale wanaonidharau mimi,

    ‘Bwana asema: Mtakuwa na amani.’

    Kwa wale wote wafuatao ugumu wa mioyo yao,

    wao husema, ‘Hakuna dhara litakalowapata.’

    18 Lakini ni yupi miongoni mwao aliyesimama katika baraza la Bwana

    ili kuona au kusikia neno lake?

    Ni nani aliyesikiliza

    na kusikia neno lake?

  3. 1 Lakini pia waliinuka manabii wa uongo miongoni mwa watu, kama vile watakavyokuwako walimu wa uongo miongoni mwenu. Wataingiza mafundisho yasiyopatana na kweli kwa siri, hata kumkana Bwana wa pekee aliyewanunua, na hivyo kujiletea wenyewe maangamizi ya haraka. 2 Hata hivyo, wengi watafuata njia zao za ufisadi, na kwa ajili yao njia ya kweli itatukanwa. 3 Nao katika tamaa zao mbaya, walimu hawa watajipatia faida kwenu kwa hadithi walizotunga wenyewe. Lakini hukumu imekwisha kutangazwa dhidi yao tangu zamani, wala uangamivu wao haujalala usingizi.

    4 Kwa maana, kama Mungu hakuwasamehe malaika walipotenda dhambi, bali aliwatupa kuzimu katika vifungo vya giza wakae humo mpaka ije hukumu; 5 kama hakuusamehe ulimwengu wa kale alipoleta gharika juu ya watu wale wasiomcha Mungu, bali akamhifadhi Noa, mhubiri wa haki, pamoja na watu wengine saba; 6 kama aliihukumu miji ya Sodoma na Gomora kwa kuiteketeza kwa moto ikawa majivu, na kuifanya kuwa kielelezo kwa yale yatakayowapata wale wasiomcha Mungu; 7 na kama alimwokoa Loti, mtu mwenye haki, ambaye alihuzunishwa na maisha machafu ya watu wapotovu 8 (kwa sababu yale matendo mapotovu aliyoyaona na kuyasikia huyo mtu mwenye haki alipoishi miongoni mwao yalimhuzunisha siku baada ya siku): 9 ikiwa hivyo ndivyo, basi Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa wamchao Mungu kutoka majaribu, na kuwaweka waasi katika adhabu hadi siku ya hukumu. 10 Hii ni hakika hasa kwa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kudharau mamlaka.

    Kwa ushupavu na kwa kiburi, watu hawa hawaogopi kunena mabaya dhidi ya viumbe vya mbinguni. 11 Lakini hata malaika, ingawa wana nguvu na uwezo zaidi, hawaleti mashtaka mabaya dhidi ya viumbe kama hao mbele za Bwana. 12 Lakini watu hawa hukufuru katika mambo wasiyoyafahamu. Wao ni kama wanyama wasio na akili, viumbe wanaotawaliwa na hisia za mwili, waliozaliwa ili wakamatwe na kuchinjwa. Hawa nao kama wanyama wataangamizwa pia.

    13 Watalipwa madhara kwa ajili ya madhara waliyowatendea wengine. Huhesabu kuwa ni fahari kufanya karamu za ulevi na ulafi mchana peupe. Wao ni mawaa na dosari, wakijifurahisha katika anasa zao wanaposhiriki katika karamu zenu. 14 Wakiwa na macho yaliyojaa uzinzi, kamwe hawaachi kutenda dhambi. Huwashawishi wale wasio imara. Wao ni hodari kwa kutamani; ni wana wa laana! 15 Wameiacha njia iliyonyooka, wakapotoka na kuifuata njia ya Balaamu mwana wa Beori aliyependa mshahara wa uovu. 16 Lakini kwa ajili ya uovu wake, alikemewa na punda, mnyama asiyejua kusema, akaongea akitumia sauti ya mwanadamu na kuzuia wazimu wa huyo nabii.

    17 Watu hawa ni chemchemi zisizo na maji, na ukungu upeperushwao na tufani. Giza nene limewekwa tayari kwa ajili yao. 18 Kwa maana wao hunena maneno makuu mno ya kiburi cha bure, na kwa kuvutia tamaa mbaya za asili ya mwili, huwashawishi watu ambao ndipo tu wamejiondoa miongoni mwa wale wanaoishi katika ufisadi. 19 Huwaahidi uhuru hao waliowanasa, wakati wao wenyewe ni watumwa wa ufisadi: kwa maana mtu ni mtumwa wa kitu chochote kinachomtawala. 20 Kama wameukimbia upotovu wa dunia kwa kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo, kisha wakanaswa tena humo na kushindwa, hali yao ya mwisho ni mbaya zaidi kuliko ile ya kwanza. 21 Ingelikuwa afadhali kwao kama wasingeliijua kamwe njia ya haki, kuliko kuijua kisha wakaiacha ile amri takatifu waliyokabidhiwa. 22 Imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli isemayo: “Mbwa huyarudia matapiko yake mwenyewe,” tena, “Nguruwe aliyeoshwa hurudi kugaagaa matopeni.”

  4. 18 Nitawainulia nabii kama wewe kutoka miongoni mwa ndugu zao; nitaweka maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia kila kitu nitakachomwamuru. 19 Kama mtu yeyote hatasikiliza maneno yangu ambayo huyo nabii atayasema kwa Jina langu, mimi mwenyewe nitamwajibisha. 20 Lakini nabii ambaye atathubutu kusema kwa Jina langu kitu chochote ambacho sikumwamuru akiseme, au nabii ambaye husema kwa jina la miungu mingine ni lazima auawe.”

    21 Mnaweza kuulizana wenyewe, “Tutawezaje kujua wakati ujumbe haukusemwa na Bwana?” 22 Ikiwa kile nabii anachotangaza kwa jina la Bwana hakikutokea au kutimia, huo ni ujumbe ambao Bwana hakusema. Nabii huyo amesema kwa ujuaji. Msimwogope huyo.

  5. 1 Wapendwa, msiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho mwone kama zimetoka kwa Mungu, kwa sababu manabii wengi wa uongo wametokea ulimwenguni. 2 Hivi ndivyo mnavyoweza kutambua Roho wa Mungu: Kila roho inayokubali kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatoka kwa Mungu. 3 Lakini kila roho ambayo haimkubali Yesu haitoki kwa Mungu. Hii ndiyo roho ya mpinga Kristo, ambayo mmesikia kwamba inakuja na sasa tayari iko ulimwenguni.

    4 Watoto wapendwa, ninyi mmetokana na Mungu, nanyi mmewashinda kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika ulimwengu. 5 Wao wanatokana na ulimwengu na kwa hiyo hunena yaliyo ya ulimwengu, hivyo ulimwengu huwasikiliza. 6 Sisi twatokana na Mungu na yeyote anayemjua Mungu hutusikiliza, lakini asiyetokana na Mungu hatusikilizi. Hivi ndivyo tunavyoweza kutambua Roho wa Kweli na roho ya upotovu.

  6. 13 Lakini nikasema, “Aa, Bwana Mwenyezi, manabii wanaendelea kuwaambia, ‘Hamtaona upanga wala kukabiliwa na njaa. Naam, nitawapa amani ya kudumu mahali hapa.’ ”

    14 Ndipo Bwana akaniambia, “Manabii wanatabiri uongo kwa jina langu. Sikuwatuma, wala sikuwaweka, wala sikusema nao. Wanawatabiria maono ya uongo, maaguzi, maono ya sanamu zisizofaa kitu, na madanganyo ya mawazo yao wenyewe. 15 Kwa hiyo, hili ndilo Bwana asemalo kuhusu manabii wanaotabiri kwa jina langu: Mimi sikuwatuma, lakini wanasema, ‘Hakuna upanga wala njaa itakayoigusa nchi hii.’ Manabii hao hao watakufa kwa upanga na njaa. 16 Nao watu hao wanaowatabiria watatupwa nje katika barabara za Yerusalemu kwa sababu ya njaa na upanga. Hapatakuwepo yeyote wa kuwazika wao au wake zao, wana wao au binti zao. Nitawamwagia maafa wanayostahili.

  7. 1 Kama nabii, au yule anayetabiri kwa njia ya ndoto, akijitokeza miongoni mwenu na akawatangazia ishara ya miujiza na ajabu, 2 ikiwa ishara au ajabu ya aliyozungumza ikatokea, naye akasema, “Na tufuate miungu mingine” (miungu ambayo hamjaifahamu) “na tuiabudu,” 3 kamwe msiyasikilize maneno ya nabii wala mwota ndoto huyo. Bwana Mungu wenu anawajaribu kuangalia kama mnampenda kwa moyo wenu wote na kwa roho yenu yote. 4 Ni Bwana Mungu wenu ambaye mnapaswa kumfuata tena ni yeye mnapaswa kumheshimu. Shikeni maagizo yake na kumtii, mtumikieni na kushikamana naye. 5 Huyo nabii au mwota ndoto lazima auawe, kwa sababu amehubiri uasi dhidi ya Bwana Mungu wenu, ambaye aliwatoa kutoka nchi ya Misri na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa; amejaribu kuwageuza kutoka njia ambayo Bwana Mungu wenu aliwaagiza mfuate. Ni lazima mwondoe uovu miongoni mwenu.

  8. 3 Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamjia faraghani, wakamuuliza, “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, nayo dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia ni gani?”

    4 Yesu akawajibu, “Jihadharini, mtu yeyote asiwadanganye. 5 Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye Kristo,’ nao watawadanganya wengi. 6 Mtasikia habari za vita na matetesi ya vita. Angalieni msitishike, kwa maana haya hayana budi kutukia. Lakini ule mwisho bado. 7 Taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. 8 Haya yote yatakuwa ndio mwanzo wa utungu.

    9 “Ndipo mtasalitiwa, ili mteswe na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote kwa ajili yangu. 10 Wakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana. 11 Watatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi. 12 Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu upendo wa watu wengi utapoa, 13 lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa.

  9. 28 Jilindeni nafsi zenu na mlilinde lile kundi lote ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi wake. Lichungeni kanisa lake Mungu alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. 29 Najua kwamba baada yangu kuondoka, mbwa mwitu wakali watakuja katikati yenu ambao hawatalihurumia kundi. 30 Hata kutoka miongoni mwenu watainuka watu na kuupotosha ukweli ili wawavute wanafunzi wawafuate. 31 Hivyo jilindeni! Kumbukeni kwamba kwa miaka mitatu sikuacha kamwe kuwaonya kila mmoja kwa machozi usiku na mchana.

    32 “Sasa nawakabidhi kwa Mungu na kwa neno la neema yake, linaloweza kuwajenga na kuwapa ninyi urithi miongoni mwa wote ambao wametakaswa.

  10. 13 Watu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Kristo. 14 Wala hii si ajabu, kwa kuwa hata Shetani mwenyewe hujigeuza aonekane kama malaika wa nuru. 15 Kwa hiyo basi si ajabu, kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili.

  11. 25 “Nimesikia wanayoyasema manabii, hao wanaotabiri uongo kwa jina langu. Wanasema, ‘Nimeota ndoto! Nimeota ndoto!’ 26 Mambo haya yataendelea mpaka lini ndani ya mioyo ya hawa manabii wa uongo, ambao hutabiri maono ya uongo ya akili zao wenyewe? 27 Wanadhani ndoto wanazoambiana wao kwa wao zitawafanya watu wangu walisahau jina langu, kama baba zao walivyolisahau jina langu kwa kumwabudu Baali. 28 Mwache nabii aliye na ndoto aseme ndoto yake, lakini yule aliye na neno langu na aliseme kwa uaminifu. Kwa maana jani kavu lina uhusiano gani na ngano?” asema Bwana. 29 “Je, neno langu si kama moto,” asema Bwana, “na kama nyundo ivunjayo mwamba vipande vipande?

    30 “Kwa hiyo, niko kinyume na manabii wanaoibiana maneno kana kwamba ni yangu,” asema Bwana. 31 “Naam, mimi niko kinyume na manabii wanaotikisa ndimi zao wenyewe na kusema, ‘Bwana asema.’ 32 Kweli, niko kinyume na hao wanaotabiri ndoto za uongo,” asema Bwana. “Wanazisimulia na kuwapotosha watu wangu kwa uongo wao bila kujali, lakini sikuwatuma wala sikuwaamuru. Hawawafaidi watu hawa hata kidogo,” asema Bwana.

  12. 23 Wakati huo kama mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo huyu hapa!’ Au, ‘Kristo yuko kule,’ msisadiki. 24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa. 25 Angalieni, nimekwisha kuwaambia mapema.

    26 “Kwa hiyo mtu yeyote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki. 27 Kwa maana kama vile umeme utokeavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 28 Kwa maana popote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai.

  13. 3 Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima. Badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe, watajikusanyia idadi kubwa ya walimu wapate kuwaambia yale ambayo masikio yao yanayowasha yanatamani kuyasikia. 4 Watakataa kusikiliza kweli na kuzigeukia hadithi za uongo.

  14. 11 Kisha nikamwona mnyama mwingine, akipanda juu kutoka dunia. Alikuwa na pembe mbili kama mwana-kondoo, lakini akanena kama joka. 12 Akatumia mamlaka yote ya yule mnyama wa kwanza kwa niaba yake, naye akawafanya wote wakaao duniani kumwabudu yule mnyama wa kwanza, ambaye jeraha lake la mauti lilipona. 13 Naye akafanya ishara kuu na za ajabu, hata kusababisha moto kushuka toka mbinguni kuja duniani watu wakiona waziwazi. 14 Kwa sababu ya zile ishara alizokuwa amepewa uwezo wa kuzifanya kwa niaba ya yule mnyama wa kwanza, akawadanganya wakaao duniani. Akawaamuru wasimamishe sanamu kwa heshima ya yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini akaishi. 15 Akapewa uwezo wa kuipa pumzi ile sanamu ya yule mnyama wa kwanza, ili iweze kusema na kuwasababisha wale wote waliokataa kuiabudu hiyo sanamu kuuawa.

  15. 6 Nashangaa kwamba mnamwacha upesi hivyo yeye aliyewaita kwa neema ya Kristo na kuifuata Injili nyingine, 7 ambayo kwa kweli si Injili kamwe, ila kwa dhahiri kuna watu wanaowachanganya na wanaotaka kuipotosha Injili ya Kristo. 8 Lakini hata ikiwa sisi au malaika atokaye mbinguni akihubiri Injili nyingine tofauti na ile tuliyowahubiria sisi, basi mtu huyo alaaniwe milele! 9 Kama vile tulivyokwisha kusema kabla, sasa nasema tena, ikiwa mtu yeyote atawahubiria Injili kinyume na ile mliyoipokea na alaaniwe milele!

  16. 3 Ikiwa mtu yeyote atafundisha mafundisho mapotovu wala hakubaliani na mafundisho manyofu ya Bwana wetu Yesu Kristo na yale ya utauwa, 4 huyo amejivuna wala hajui kitu chochote. Yeye amejaa tamaa ya mabishano na ugomvi kuhusu maneno ambavyo matokeo yake ni wivu na mapigano, maneno ya ukorofi, shuku mbaya, 5 na kuzozana kusikokoma kati ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, na ambao hudhani kwamba utauwa ni njia ya kupata faida.

    6 Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa.

  17. 19 Wakati watu wanapowaambia ninyi kutafuta ushauri kwa waaguzi na wenye kuongea na mizimu, ambao hunongʼona na kunungʼunika, je, watu wasingeuliza kwa Mungu wao? Kwa nini watake shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai? 20 Kwa sheria na kwa ushuhuda! Kama hawatasema sawasawa na neno hili, hawana mwanga wa mapambazuko.

  18. 17 Ndugu zangu, nawasihi mjihadhari na kujiepusha na wale watu waletao matengano na kuweka vikwazo mbele yenu dhidi ya mafundisho mliyojifunza. 18 Kwa maana watu kama hao hawamtumikii Bwana Kristo, bali wanatumikia tamaa zao wenyewe. Kwa kutumia maneno laini na ya kubembeleza, hupotosha mioyo ya watu wajinga.

  19. 11 Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, 12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa 13 mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo.

    14 Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. 15 Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo. 16 Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.

  20. 1 Roho asema waziwazi kwamba katika siku za mwisho baadhi ya watu wataiacha imani na kufuata roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani. 2 Mafundisho kama hayo huja kupitia kwa waongo ambao ni wanafiki, hali dhamiri zao zikiungua kwa kuchomwa moto. 3 Wao huwakataza watu wasioe na kuwaagiza wajiepushe na vyakula fulani, ambavyo Mungu aliviumba ili vipokewe kwa shukrani na wale wanaoamini na kuijua kweli.

  21. 30 “Jambo la kutisha na kushtusha

    limetokea katika nchi hii:

    31 Manabii wanatabiri uongo,

    makuhani wanatawala kwa mamlaka yao wenyewe,

    nao watu wangu wanapenda hivyo.

    Lakini mtafanya nini mwisho wake?

  22. 3 Kama nilivyokusihi wakati nilipokwenda Makedonia, endelea kubaki Efeso, ili kwamba upate kuwaagiza watu wasiendelee kufundisha mafundisho ya uongo 4 wala wasitoe muda wao kwa hadithi za kubuniwa na orodha za majina ya vizazi visivyo na mwisho, ambazo huchochea mabishano badala ya mpango wa Mungu utokanao na imani. 5 Kusudi la maagizo haya ni upendo utokao katika moyo safi, dhamiri njema na imani ya kweli. 6 Watu wengine wamepotoka kutoka haya na kugeukia majadiliano yasiyo na maana kwa kuwa, 7 wanataka kuwa walimu wa sheria, lakini hawajui mambo yale wanayosema wala hayo wanayoyatumainia kwa uthabiti.

  23. 16 Jiepushe na maneno mabaya, yasiyo na maana, yasiyo ya utauwa, kwa maana hayo huzidi kuwatosa watu katika kukosa heshima kwa Mungu. 17 Mafundisho yao yataenea kama kidonda kisichopona. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto 18 ambao wameiacha kweli, wakisema kwamba ufufuo wa wafu umekwisha kuwako, nao huharibu imani ya baadhi ya watu. 19 Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, ukiwa na muhuri wenye maandishi haya: “Bwana anawajua walio wake”; tena, “Kila alitajaye jina la Bwana, na auache uovu.”

  24. 20 “Hata hivyo, nina neno dhidi yako: Unamvumilia yule mwanamke Yezebeli ambaye anajiita nabii, lakini anawafundisha na kuwapotosha watumishi wangu ili wafanye uasherati na kula vyakula vilivyotolewa kafara kwa sanamu.

  25. 1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, tabiri dhidi ya manabii wa Israeli wanaotabiri sasa. Waambie hao ambao hutabiri kutokana na mawazo yao wenyewe: ‘Sikia neno la Bwana! 3 Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ole wao manabii wapumbavu wafuatao roho yao wenyewe na wala hawajaona chochote! 4 Manabii wako, ee Israeli, ni kama mbweha katikati ya magofu. 5 Hamjakwea kwenda kuziba mahali palipobomoka katika ukuta ili kuukarabati kwa ajili ya nyumba ya Israeli, ili kwamba isimame imara kwenye vita katika siku ya Bwana. 6 Maono yao ni ya uongo na ubashiri wao ni wa udanganyifu. Wao husema, “Bwana amesema,” wakati Bwana hakuwatuma, bado wakitarajia maneno yao kutimizwa. 7 Je, hamjaona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu hapo msemapo, “Bwana asema,” lakini Mimi sijasema?

    8 “ ‘Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ya uongo wa maneno yenu na kwa madanganyo ya maono yenu, Mimi ni kinyume na ninyi, asema Bwana Mwenyezi. 9 Mkono wangu utakuwa dhidi ya manabii ambao huona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu. Hawatakuwa katika baraza la watu wangu au kuandikwa katika kumbukumbu ya nyumba ya Israeli wala hawataingia katika nchi ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mwenyezi.

    10 “ ‘Kwa sababu ni kweli wanapotosha watu wangu, wakisema, “Amani,” wakati ambapo hakuna amani, pia kwa sababu, wakati ukuta dhaifu unapojengwa, wanaufunika kwa kupaka chokaa, 11 kwa hiyo waambie hao wanaoupaka chokaa isiyokorogwa vyema kwamba ukuta huo utaanguka. Mvua kubwa ya mafuriko itanyesha, nami nitaleta mvua ya mawe inyeshe kwa nguvu, nao upepo wa dhoruba utavuma juu yake. 12 Wakati ukuta utakapoanguka, je, watu hawatawauliza, “Iko wapi chokaa mliyopaka ukuta?”

  26. 6 Walipokwisha kupita katika nchi zote hizo wakafika Pafo, ambapo walikutana na Myahudi mmoja mchawi aliyekuwa nabii wa uongo, jina lake Bar-Yesu. 7 Mtu huyu alikuwa pamoja na Sergio Paulo, mtu mwenye hekima aliyekuwa msaidizi wa mwakilishi wa mtawala wa kile kisiwa. Sergio Paulo akawaita Sauli na Barnaba akitaka kusikia neno la Mungu. 8 Lakini Elima yule mchawi (hii ndiyo maana ya jina lake), aliwapinga Barnaba na Sauli na kujaribu kumpotosha yule mkuu wa kile kisiwa aiache imani. 9 Ndipo Sauli, ambaye pia aliitwa Paulo, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akamkazia macho Elima huyo mchawi, 10 akamwambia, “Ewe mwana wa ibilisi, wewe ni adui wa kila kilicho haki! Umejaa kila aina ya udanganyifu na ulaghai. Je, hutaacha kuzipotosha njia za Bwana zilizonyooka? 11 Nawe sasa sikiliza, mkono wa Bwana u dhidi yako. Utakuwa kipofu, wala hutaona jua kwa muda.”

    Mara ukungu na giza vikamfunika, naye akaenda huku na huko akitafuta mtu wa kumshika mkono ili amwonyeshe njia. 12 Yule mkuu wa kile kisiwa alipoona yaliyotukia, akaamini kwa sababu alistaajabishwa na mafundisho kuhusu Bwana.

  27. 10 Naye ibilisi aliyewadanganya akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti walikokuwa wametupwa yule mnyama na yule nabii wa uongo. Watateswa humo usiku na mchana, milele na milele.

  28. 11 Inakuwaje mnashindwa kuelewa kwamba nilikuwa sisemi nanyi habari za mikate? Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.” 12 Ndipo wakaelewa kwamba alikuwa hasemi juu ya chachu ya kutengeneza mikate, bali juu ya mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.

  29. 8 Angalieni mtu yeyote asiwafanye ninyi mateka kwa elimu batili na madanganyo matupu yanayotegemea mapokeo ya wanadamu na mafundisho ya ulimwengu badala ya Kristo.

  30. 8 Hapo ndipo yule mwasi atafunuliwa, ambaye Bwana Yesu atamteketeza kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kabisa kwa utukufu wa kuja kwake. 9 Kuja kwa yule mwasi kutaonekana kana kwamba ni kutenda kazi kwake Shetani ambaye hutumia nguvu zote, ishara, maajabu ya uongo, 10 na kila aina ya uovu kwa wale wanaoangamia kwa sababu walikataa kuipenda kweli wapate kuokolewa. 11 Kwa sababu hii, Mungu ameruhusu watawaliwe na nguvu ya udanganyifu, ili waendelee kuamini uongo, 12 na wahukumiwe wote ambao hawakuiamini ile kweli, bali wamefurahia uovu.

  31. 16 Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana: ‘Hivi karibuni nitakuondoa kutoka juu ya uso wa dunia. Mwaka huu utakufa, kwa sababu umetangaza uasi dhidi ya Bwana.’ ”

    17 Katika mwezi wa saba wa mwaka ule ule, nabii Hanania akafa.

  32. 8 Naam, hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: “Msikubali manabii na wabashiri walioko miongoni mwenu wawadanganye. Msisikilize ndoto ambazo mmewatia moyo kuota. 9 Wanawatabiria ninyi uongo kwa jina langu. Sikuwatuma,” asema Bwana.

  33. 28 Manabii wake wanapaka chokaa matendo haya kwa maono ya uongo na utabiri wa udanganyifu. Wanasema, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo,’ wakati Bwana hajasema.

  34. 5 Hili ndilo asemalo Bwana:

    “Kuhusu manabii wanaowapotosha watu wangu,

    mtu akiwalisha,

    wanatangaza ‘amani’;

    kama hakufanya hivyo,

    wanaandaa kupigana vita dhidi yake.

    6 Kwa hiyo usiku utawajieni, msiweze kuwa na maono,

    na giza, msiweze kubashiri.

    Jua litawachwea manabii hao,

    nao mchana utakuwa giza kwao.

    7 Waonaji wataaibika

    na waaguzi watafedheheka.

    Wote watafunika nyuso zao

    kwa sababu hakuna jibu litokalo kwa Mungu.”

  35. 2 “Katika siku hiyo, nitayakatilia mbali majina ya sanamu kutoka nchi, nayo hayatakumbukwa tena,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. “Nitaondoa manabii wao pamoja na roho ya uchafu katika nchi. 3 Ikiwa yupo yeyote atakayeendelea kutabiri, baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, ‘Ni lazima ufe, kwa sababu umesema uongo kwa jina la Bwana.’ Atakapotabiri, wazazi wake mwenyewe watampasua tumbo.

    4 “Katika siku hiyo, kila nabii ataaibika kwa maono ya unabii wake. Hatavaa vazi la kinabii la nywele ili apate kudanganya watu. 5 Atasema, ‘Mimi sio nabii. Mimi ni mkulima; ardhi imekuwa kazi yangu tangu ujana wangu.’ 6 Ikiwa mtu atamuuliza, ‘Majeraha haya yaliyo mwilini mwako ni ya nini?’ Atajibu, ‘Ni majeraha niliyoyapata katika nyumba ya rafiki zangu.’

  36. 22 Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara na maajabu ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule. 23 Hivyo jihadharini. Nimekwisha kuwaambia mambo haya yote mapema kabla hayajatukia.

  37. 2 Ninawaonea wivu, wivu wa Kimungu, kwa kuwa mimi niliwaposea mume mmoja, ili niwalete kwa Kristo kama mabikira safi. 3 Lakini nina hofu kuwa, kama vile Eva alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Kristo. 4 Kwa sababu kama mtu akija na kuwahubiria Yesu mwingine ambaye si yule tuliyemhubiri, au kama mkipokea roho mwingine ambaye si yule mliyempokea, au Injili tofauti na ile mliyoikubali, ninyi mnaitii kwa urahisi.

  38. 20 Zaidi ya yote, yawapasa mjue kwamba hakuna unabii katika Maandiko uliofasiriwa kama alivyopenda nabii mwenyewe. 21 Kwa maana unabii haukuja kamwe kwa mapenzi ya mwanadamu, bali watu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

  39. 9 Mtu yeyote asiyedumu katika mafundisho ya Kristo, bali akayaacha, yeye hana Mungu. Yeyote anayedumu katika mafundisho ana Baba na Mwana pia. 10 Msimpokee mtu yeyote anayewajia ambaye hawaletei mafundisho haya, wala msimkaribishe nyumbani mwenu.

  40. 3 Wapendwa, ingawa nilikuwa ninatamani sana kuwaandikia kuhusu wokovu ambao tunaushiriki sisi sote, niliona imenipasa kuwaandikia na kuwasihi kwamba mwitetee imani iliyokabidhiwa watakatifu kwa nafasi moja itoshayo. 4 Kwa kuwa kuna watu waliojipenyeza kwa siri katikati yenu, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, waovu, wapotoshao neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi wakimkana yeye aliye Bwana wetu wa pekee, Bwana Yesu Kristo.

  41. 13 Kisha nikaona roho wachafu watatu waliofanana na vyura wakitoka katika kinywa cha lile joka na katika kinywa cha yule mnyama na katika kinywa cha yule nabii wa uongo. 14 Hizo ndizo roho za pepo wachafu zitendazo miujiza. Nazo huwaendea wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya tayari kwa ajili ya vita katika siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.

  42. 10 Siku moja nilikwenda nyumbani kwa Shemaya mwana wa Delaya, mwana wa Mehetabeli, ambaye alikuwa amefungwa ndani ya nyumba yake. Akasema, “Tukutane katika nyumba ya Mungu, ndani ya Hekalu, na tufunge milango ya Hekalu, kwa sababu watu wanakuja kukuua. Naam, wanakuja usiku kukuua.”

    11 Lakini nikasema, “Je, mtu kama mimi akimbie? Au mtu kama mimi aende Hekaluni kuokoa maisha yake? Sitakwenda!” 12 Nilitambua kwamba Mungu hakumtuma, bali alitabiri dhidi yangu kwa sababu Tobia na Sanbalati walikuwa wamemwajiri. 13 Alikuwa ameajiriwa kunitisha ili kwa kufanya jambo hili nitende dhambi, kisha waweze kuniharibia jina langu na kuniaibisha.

    14 Ee Mungu wangu, wakumbuke Tobia na Sanbalati kwa sababu ya yale waliyotenda. Pia kumbuka nabii mke Noadia na manabii wengine ambao wamekuwa wakijaribu kunitisha.

  43. 15 Wazee na watu mashuhuri ndio vichwa,

    nao manabii wanaofundisha uongo ndio mkia.

    16 Wale wanaowaongoza watu hawa wanawapotosha,

    nao wale wanaoongozwa wamepotoka.

  44. 11 Viongozi wake wanahukumu kwa rushwa,

    na makuhani wake wanafundisha kwa malipo,

    nao manabii wake wanatabiri kwa fedha.

    Hata hivyo wanamwegemea Bwana na kusema,

    “Je, Bwana si yumo miongoni mwetu?

    Hakuna maafa yatakayotupata.”

  45. 2 Sanamu huzungumza udanganyifu,

    waaguzi huona maono ya uongo;

    husimulia ndoto ambazo si za kweli,

    wanatoa faraja batili.

    Kwa hiyo watu wanatangatanga kama kondoo

    walioonewa kwa kukosa mchungaji.

  46. 6 Yesu akawaambia, “Jihadharini. Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ya Masadukayo.”

  47. 20 Lakini yule mnyama akakamatwa pamoja na huyo nabii wa uongo ambaye alikuwa amefanya ishara kwa niaba ya huyo mnyama, ambaye kwa ishara hizi aliwadanganya wale waliopokea chapa ya huyo mnyama na kuiabudu sanamu yake. Hawa wawili wakatupwa wakiwa hai ndani ya ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti.

  48. 13 “Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa,

    wote wana tamaa ya kupata faida zaidi;

    manabii na makuhani wanafanana,

    wote wanafanya udanganyifu.