80 Bible Verses About Scripture

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Scripture
  1. 14 Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani, 15 na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. 16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, 17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.

  2. 7 Sheria ya Bwana ni kamilifu,

    ikihuisha nafsi.

    Shuhuda za Bwana ni za kuaminika,

    zikimpa mjinga hekima.

    8 Maagizo ya Bwana ni kamili,

    nayo hufurahisha moyo.

    Amri za Bwana huangaza,

    zatia nuru machoni.

    9 Kumcha Bwana ni utakatifu,

    nako kwadumu milele.

    Amri za Bwana ni za hakika,

    nazo zina haki.

    10 Ni za thamani kuliko dhahabu,

    kuliko dhahabu iliyo safi sana,

    ni tamu kuliko asali,

    kuliko asali kutoka kwenye sega.

    11 Kwa hizo mtumishi wako anaonywa,

    katika kuzishika kuna thawabu kubwa.

    12 Ni nani awezaye kutambua makosa yake?

    Nisamehe makosa yangu nisiyoyajua.

    13 Mlinde mtumishi wako na dhambi za makusudi,

    nazo zisinitawale.

    Ndipo nitakapokuwa sina lawama,

    wala sitakuwa na hatia ya kosa kubwa.

  3. 21 Kwa hiyo, ondoleeni mbali uchafu wote na uovu ambao umezidi kuwa mwingi, mkalipokee kwa unyenyekevu lile Neno lililopandwa ndani yenu ambalo laweza kuokoa nafsi zenu.

    22 Basi kuweni watendaji wa Neno wala msiwe wasikiaji tu, huku mkijidanganya nafsi zenu. 23 Kwa maana kama mtu ni msikiaji tu wa Neno wala hatendi kile linachosema, yeye ni kama mtu ajitazamaye uso wake kwenye kioo 24 na baada ya kujiona alivyo, huenda zake na mara husahau jinsi alivyo. 25 Lakini yeye anayeangalia kwa bidii katika sheria kamilifu, ile iletayo uhuru, naye akaendelea kufanya hivyo bila kusahau alichosikia, bali akalitenda, atabarikiwa katika kile anachofanya.

  4. 4 Kwa maana kila kitu kilichoandikwa zamani, kiliandikwa kutufundisha, ili kwamba kwa saburi na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini.

  5. 6 Kwa hiyo inabaki kuwa wazi kwa wengine kuingia, nao wale wa kwanza waliopokea Injili walishindwa kuingia kwa sababu ya kutokutii. 7 Kwa hiyo Mungu ameweka siku nyingine, akaiita Leo, akisema kwa kinywa cha Daudi baadaye sana, kwa maneno yaliyotangulia kunenwa:

    “Leo, kama mkiisikia sauti yake,

    msiifanye mioyo yenu migumu.”

    8 Kwa maana kama Yoshua alikuwa amewapa raha, Mungu hangesema tena baadaye kuhusu siku nyingine. 9 Kwa hiyo basi, imebaki raha ya Sabato kwa ajili ya watu wa Mungu; 10 kwa kuwa kila mmoja aingiaye katika raha ya Mungu pia hupumzika kutoka kazi zake mwenyewe, kama vile Mungu alivyopumzika kutoka kazi zake. 11 Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha hiyo, ili kwamba asiwepo yeyote atakayeanguka kwa kufuata mfano wao wa kutokutii.

    12 Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu. Lina makali kuliko upanga wowote wenye makali kuwili, hivyo linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. 13 Wala hakuna kiumbe chochote kilichofichika machoni pa Mungu. Kila kitu kimefunuliwa na kiko wazi machoni pake yeye ambaye kwake ni lazima tutatoa hesabu.

  6. 10 Usiku ule ule, wale ndugu walioamini wakawapeleka Paulo na Sila waende zao Beroya. Walipowasili huko wakaenda kwenye sinagogi la Wayahudi. 11 Hawa Waberoya walikuwa waungwana zaidi kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa waliupokea ule ujumbe kwa shauku kubwa na kuyachunguza Maandiko kila siku ili kuona kama yale Paulo aliyosema yalikuwa kweli.

  7. KITABU CHA KWANZA

    1 Heri mtu yule ambaye

    haendi katika shauri la watu waovu,

    wala hasimami katika njia ya wenye dhambi,

    au kuketi katika baraza la wenye mizaha.

    2 Bali huifurahia sheria ya Bwana,

    naye huitafakari hiyo sheria usiku na mchana.

    3 Mtu huyo ni kama mti uliopandwa

    kando ya vijito vya maji,

    ambao huzaa matunda kwa majira yake

    na majani yake hayanyauki.

    Lolote afanyalo hufanikiwa.

  8. 44 Akawaambia, “Haya ndiyo yale niliyowaambia nilipokuwa bado niko pamoja nanyi, kwamba yote yaliyoandikwa kunihusu mimi katika Sheria ya Mose, Manabii na Zaburi hayana budi kutimizwa.”

    45 Ndipo akafungua fahamu zao ili waweze kuyaelewa Maandiko. 46 Akawaambia, “Haya ndiyo yaliyoandikwa: Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu. 47 Toba na msamaha wa dhambi zitatangaziwa mataifa yote kupitia jina lake kuanzia Yerusalemu.

  9. 8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, lile neno la imani tunalolihubiri. 9 Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. 10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu. 11 Kama yasemavyo Maandiko, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.” 12 Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. 13 Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.”

    14 Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? 15 Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri habari njema!”

    16 Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” 17 Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo.

  10. 19 Kwa hiyo, ndugu zangu, kwa kuwa tunao ujasiri wa kupaingia Patakatifu pa Patakatifu kwa damu ya Yesu, 20 kwa njia mpya iliyo hai tuliyofunguliwa kwa ajili yetu kupitia kwenye lile pazia, yaani, mwili wake, 21 basi kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu juu ya nyumba ya Mungu, 22 sisi na tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu kwa imani timilifu, mioyo yetu ikiwa imenyunyizwa damu ya Kristo na kuwa safi kutokana na dhamiri mbaya nayo miili yetu ikiwa imeoshwa kwa maji safi. 23 Tushike kwa uthabiti lile tumaini la ukiri wetu bila kuyumbayumba, kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu. 24 Tuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema. 25 Wala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi, bali tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.

    26 Kama tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi. 27 Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao, utakaowaangamiza adui za Mungu. 28 Yeyote aliyeikataa sheria ya Mose alikufa pasipo huruma kwa ushahidi wa watu wawili au watatu. 29 Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani anayostahili kupewa mtu aliyemkanyaga Mwana wa Mungu chini ya nyayo zake, yeye aliyeifanya damu ya Agano iliyomtakasa kuwa kitu najisi na kumtendea maovu Roho wa neema? 30 Kwa kuwa tunamjua yeye aliyesema, “Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza.” Tena asema, “Bwana atawahukumu watu wake.” 31 Ni jambo la kutisha kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai.

    32 Kumbukeni siku zile za kwanza, ambazo mkiisha kutiwa nuru mlistahimili mashindano makali ya maumivu. 33 Wakati mwingine mlitukanwa na kuteswa hadharani; wakati mwingine mlikuwa radhi kuungana na wale waliofanyiwa hivyo. 34 Mliwahurumia wale waliokuwa kifungoni, mkikubali kwa furaha kunyangʼanywa mali zenu kwa maana mlijua kwamba mnayo mali iliyo bora zaidi idumuyo.

    35 Kwa hiyo msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kubwa mno. 36 Inawapasa kuvumilia ili mkiisha kufanya mapenzi ya Mungu mpate kile alichoahidi.

  11. 130 Kuingia kwa maneno yako kunaleta nuru,

    kunampa mjinga ufahamu.

  12. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.

  13. 17 Uwatakase kwa ile kweli, neno lako ndilo kweli.

  14. 19 Nasi tunalo pia neno la hakika zaidi la unabii, ambalo mtafanya vyema mkiliangalia kwa bidii, kama vile nuru inavyongʼaa gizani, hadi kupambazuka na nyota ya asubuhi izuke mioyoni mwenu. 20 Zaidi ya yote, yawapasa mjue kwamba hakuna unabii katika Maandiko uliofasiriwa kama alivyopenda nabii mwenyewe. 21 Kwa maana unabii haukuja kamwe kwa mapenzi ya mwanadamu, bali watu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

  15. 17 “Msidhani kwamba nimekuja kufuta Sheria au Manabii; sikuja kuondoa bali kutimiza. 18 Kwa maana, amin nawaambia, mpaka mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yoyote kutoka kwenye Sheria, mpaka kila kitu kiwe kimetimia. 19 Kwa hiyo, yeyote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, lakini yeyote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika Ufalme wa Mbinguni.

  16. 28 Tomaso akamwambia, “Bwana wangu na Mungu wangu!”

    29 Yesu akamwambia, “Umeamini kwa kuwa umeniona? Wamebarikiwa wale ambao hawajaona lakini wameamini.”

    30 Yesu alifanya miujiza mingine mingi mbele za wanafunzi wake, ambayo haikuandikwa katika kitabu hiki. 31 Lakini haya yameandikwa ili mweze kuamini ya kuwa Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu, na kwa kumwamini mpate uzima katika jina lake.

  17. 1 Basi ndugu zangu nataka niwakumbushe kuhusu Injili niliyowahubiria, mkaipokea na ambayo katika hiyo mmesimama. 2 Kwa Injili hii mnaokolewa mkishikilia kwa uthabiti neno nililowahubiria ninyi. La sivyo, mmeamini katika ubatili.

    3 Kwa maana yale niliyopokea ndiyo niliyowapa ninyi, kama yenye umuhimu wa kwanza: Kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yasemavyo Maandiko, 4 ya kuwa alizikwa na alifufuliwa siku ya tatu, kama yasemavyo Maandiko, 5 na kwamba alimtokea Kefa, kisha akawatokea wale kumi na wawili. 6 Baadaye akawatokea wale ndugu waumini zaidi ya 500 kwa pamoja, ambao wengi wao bado wako hai, ingawa wengine wamelala. 7 Ndipo akamtokea Yakobo na kisha mitume wote. 8 Mwisho wa wote, akanitokea mimi pia, ambaye ni kama aliyezaliwa si kwa wakati wake.

    9 Kwa maana mimi ndiye mdogo kuliko mitume wote, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu nililitesa kanisa la Mungu. 10 Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo na neema yake kwangu haikuwa kitu bure. Bali nilizidi sana kufanya kazi kuliko mitume wote, lakini haikuwa mimi, bali ni ile neema ya Mungu iliyokuwa pamoja nami. 11 Hivyo basi, kama ilikuwa mimi au wao, hili ndilo tunalohubiri, na hili ndilo mliloamini.

  18. 22 Basi kwa kuwa mmejitakasa nafsi zenu kwa kuitii ile kweli hata mkawa na upendo wa ndugu usio na unafiki, basi pendaneni kwa dhati kutoka moyoni. 23 Kwa maana mmezaliwa upya, si kwa mbegu ile iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika, kupitia kwa neno la Mungu lililo hai na linalodumu milele. 24 Maana,

    “Wanadamu wote ni kama majani,

    nao utukufu wao ni kama maua ya kondeni;

    majani hunyauka na maua huanguka,

    25 lakini neno la Bwana ladumu milele.”

    Hili ndilo neno lililohubiriwa kwenu.

  19. 7 Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. 8 Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi.

  20. 104 Ninapata ufahamu kutoka mausia yako,

    kwa hiyo ninachukia kila njia ya upotovu.

    105 Neno lako ni taa ya miguu yangu

    na mwanga katika njia yangu.

  21. 27 Ikawa Yesu alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katikati ya ule umati wa watu akapaza sauti akasema, “Limebarikiwa tumbo lililokuzaa na matiti uliyonyonya!”

    28 Yesu akajibu, “Wamebarikiwa zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulitii.”

  22. 39 Ninyi mnachunguza Maandiko mkidhani ya kuwa ndani yake mna uzima wa milele, maandiko haya ndiyo yanayonishuhudia Mimi. 40 Lakini mnakataa kuja kwangu ili mpate uzima.

  23. 1 Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume na kutengwa kwa ajili ya Injili ya Mungu, 2 Injili ambayo Mungu alitangulia kuiahidi kwa vinywa vya manabii wake katika Maandiko Matakatifu, 3 yaani, Injili inayomhusu Mwanawe, yeye ambaye kwa uzao wa mwili alikuwa mzao wa Daudi, 4 na ambaye kwa uwezo wa Roho wa utakatifu alidhihirishwa kuwa Mwana wa Mungu kwa ufufuo wake kutoka kwa wafu, yaani, Yesu Kristo, Bwana wetu. 5 Kwa kupitia kwake na kwa ajili ya Jina lake, tumepokea neema na utume ili kuwaita watu miongoni mwa watu wa mataifa yote, waje kwenye utii utokanao na imani. 6 Ninyi nyote pia mko miongoni mwa watu walioitwa ili mpate kuwa mali ya Yesu Kristo.

  24. 24 Basi akaja Efeso Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mwenyeji wa Iskanderia. Yeye alikuwa na elimu kubwa, pia alikuwa hodari katika Maandiko. 25 Alikuwa amefundishwa katika njia ya Bwana, naye alikuwa na bidii katika roho, akafundisha kwa usahihi juu ya Yesu, ingawa alijua tu ubatizo wa Yohana. 26 Apolo alianza kunena kwa ujasiri mkubwa katika sinagogi. Lakini Prisila na Akila walipomsikia, walimchukua kando na kumweleza njia ya Mungu kwa ufasaha zaidi.

    27 Naye Apolo alipotaka kwenda Akaya, ndugu wa Efeso walimtia moyo, wakawaandikia wanafunzi huko ili wamkaribishe. Alipofika huko, aliwasaidia sana wale ambao, kwa neema ya Mungu, walikuwa wameamini. 28 Kwa uwezo mkubwa aliwakanusha hadharani Wayahudi waliokuwa wakipinga, akionyesha kwa njia ya Maandiko kwamba Yesu ndiye Kristo.

  25. 9 Lakini ni kama ilivyoandikwa:

    “Hakuna jicho limepata kuona,

    wala sikio limepata kusikia,

    wala hayakuingia moyoni wowote,

    yale Mungu amewaandalia

    wale wampendao”:

    10 Lakini mambo haya Mungu ametufunulia kwa Roho wake.

    Roho huchunguza kila kitu, hata mambo ya ndani sana ya Mungu. 11 Kwa maana ni nani anayejua mawazo ya mtu isipokuwa roho iliyo ndani ya huyo mtu? Vivyo hivyo hakuna mtu ajuaye mawazo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu. 12 Basi hatukupokea roho ya dunia bali Roho atokaye kwa Mungu, ili tuweze kuelewa kile kipawa ambacho Mungu ametupatia bure. 13 Haya ndiyo tusemayo, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya wanadamu bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua kweli za kiroho kwa maneno ya kiroho.

  26. 1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, 2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. 3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.

    5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:

    6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,

    hakuona kule kuwa sawa na Mungu

    kuwa kitu cha kushikilia,

    7 bali alijifanya si kitu,

    akachukua hali hasa na mtumwa,

    naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.

    8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,

    alijinyenyekeza, akatii hata mauti:

    naam, mauti ya msalaba!

    9 Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana,

    na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina,

    10 ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe,

    la vitu vya mbinguni, na vya duniani,

    na vya chini ya nchi,

    11 na kila ulimi ukiri ya kwamba

    Yesu Kristo ni Bwana,

    kwa utukufu wa Mungu Baba.

    12 Kwa hiyo, wapenzi wangu, kama vile ambavyo mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwepo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka, 13 kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema.

    14 Fanyeni mambo yote bila kunungʼunika wala kushindana, 15 ili msiwe na lawama wala hatia, bali mwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka, ambacho ndani yake ninyi mnangʼaa kama mianga ulimwenguni. 16 Mkilishika neno la uzima, ili nipate kuona fahari siku ya Kristo kwamba sikupiga mbio wala kujitaabisha bure.

  27. 14 Kwa sababu hii, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo haya, fanyeni bidii ili awakute katika amani, bila mawaa wala dosari. 15 Hesabuni uvumilivu wa Bwana kuwa ni wokovu, kama vile ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima ile aliyopewa na Mungu. 16 Huandika vivyo hivyo katika nyaraka zake zote, akizungumzia ndani yake mambo haya. Katika nyaraka zake kuna mambo mengine ambayo ni vigumu kuyaelewa, ambayo watu wajinga na wasio thabiti huyapotosha kwa maangamizi yao wenyewe, kama wapotoshavyo pia Maandiko mengine.

  28. 50 Faraja yangu katika mateso yangu ni hii:

    Ahadi yako inahifadhi maisha yangu.

    51 Wenye majivuno wamenisimanga bila kuchoka,

    hata hivyo sitaiacha sheria yako.

  29. 140 Ahadi zako zimejaribiwa kikamilifu,

    mtumishi wako anazipenda.

    141 Ingawa ni mdogo na ninadharauliwa,

    sisahau mausia yako.

    142 Haki yako ni ya milele,

    na sheria yako ni kweli.

    143 Shida na dhiki zimenipata,

    lakini amri zako ni furaha yangu.

  30. 6 Sauti husema, “Piga kelele.”

    Nami nikasema, “Nipige kelele gani?”

    “Wanadamu wote ni kama majani,

    nao utukufu wao wote

    ni kama maua ya kondeni.

    7 Majani hunyauka na maua huanguka,

    kwa sababu pumzi ya Bwana huyapuliza.

    Hakika wanadamu ni majani.

    8 Majani hunyauka na maua huanguka,

    lakini neno la Mungu wetu ladumu milele.”

  31. 28 Je wewe, hufahamu?

    Je wewe, hujasikia?

    Bwana ni Mungu wa milele,

    Muumba wa miisho ya dunia.

    Hatachoka wala kulegea,

    wala hakuna hata mmoja

    awezaye kuupima ufahamu wake.

    29 Huwapa nguvu waliolegea

    na huongeza nguvu za wadhaifu.

    30 Hata vijana huchoka na kulegea,

    nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,

    31 bali wale wamtumainio Bwana

    atafanya upya nguvu zao.

    Watapaa juu kwa mbawa kama tai;

    watapiga mbio wala hawatachoka,

    watatembea kwa miguu wala hawatazimia.

  32. 37 Siku ile ya mwisho ya Sikukuu, siku ile kuu, wakati Yesu akiwa amesimama huko, akapaza sauti yake akasema, “Kama mtu yeyote anaona kiu na aje kwangu anywe. 38 Yeyote aniaminiye mimi, kama Maandiko yasemavyo, vijito vya maji ya uzima vitatiririka ndani mwake.”

  33. 1 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli na Baba yangu ndiye mkulima. 2 Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata, nalo kila tawi lizaalo, hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi. 3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililonena nanyi. 4 Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda lisipokaa ndani ya mzabibu, vivyo hivyo ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kuzaa matunda.

    5 “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lolote. 6 Mtu yeyote asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi kama hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea. 7 Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo, nanyi mtatendewa. 8 Kwa hiyo Baba yangu hutukuzwa, kwa vile mzaavyo matunda mengi, nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.

  34. 11 Mambo haya yaagize na kuyafundisha. 12 Mtu yeyote asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe kielelezo kizuri kwa waumini katika usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi. 13 Fanya bidii kusoma Maandiko hadharani, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja. 14 Usiache kutumia kipawa kilicho ndani yako, ambacho ulipewa kwa neno la unabii wakati wazee walikuwekea mikono.

    15 Uwe na bidii katika mambo haya; ujitolee kwa ajili ya mambo haya kikamilifu, ili kila mtu aone kuendelea kwako. 16 Jilinde sana nafsi yako na mafundisho yako. Dumu katika hayo, kwa maana kwa kufanya hivyo, utajiokoa wewe mwenyewe pamoja na wale wanaokusikia.

  35. 9 Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu walio milki ya Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu. 10 Mwanzo ninyi mlikuwa si taifa, lakini sasa ninyi ni taifa la Mungu. Mwanzo mlikuwa hamjapata rehema, lakini sasa mmepata rehema.

    11 Wapenzi, ninawasihi, mkiwa kama wageni na wapitaji hapa ulimwenguni, epukeni tamaa mbaya za mwili ambazo hupigana vita na roho zenu. 12 Kuweni na mwenendo mzuri mbele ya watu wasiomjua Mungu, ili kama wanawasingizia kuwa watenda mabaya, wayaone matendo yenu mema nao wamtukuze Mungu siku atakapokuja kwetu.

    13 Kwa ajili ya Bwana, tiini kila mamlaka iliyowekwa na wanadamu: Kwa mfalme kwani ndiye aliye na mamlaka ya juu zaidi, 14 au kwa maafisa aliowaweka, kwa kuwa mfalme amewatuma ili kuwaadhibu wale wanaokosa, na kuwapongeza wale watendao mema. 15 Kwa maana ni mapenzi ya Mungu kwamba kwa kutenda mema mnyamazishe maneno ya kijinga ya watu wapumbavu.

  36. 18 Namwonya kila mtu asikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki: Mtu yeyote akiongeza humo chochote, Mungu atamwongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. 19 Kama mtu yeyote akipunguza humo chochote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.

  37. 28 Sasa basi, siku ya ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba, kwa kuwa wote walikuwa wamemwoa huyo mwanamke?”

    29 Yesu akawajibu, “Mwapotoka kwa sababu hamjui Maandiko wala uweza wa Mungu. 30 Wakati wa ufufuo, watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni. 31 Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjasoma kile Mungu alichowaambia, kwamba, 32 ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo’? Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.”

    33 Ule umati wa watu uliposikia hayo, ulishangaa sana kwa mafundisho yake.

  38. 13 Nasi pia tunamshukuru Mungu bila kukoma kwa sababu mlipolipokea neno la Mungu mlilosikia kutoka kwetu, hamkulipokea kama neno la wanadamu, bali mlilipokea kama lilivyo hasa, neno la Mungu, litendalo kazi ndani yenu ninyi mnaoamini.

  39. 15 Jitahidi kujionyesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtendakazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli. 16 Jiepushe na maneno mabaya, yasiyo na maana, yasiyo ya utauwa, kwa maana hayo huzidi kuwatosa watu katika kukosa heshima kwa Mungu. 17 Mafundisho yao yataenea kama kidonda kisichopona. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto 18 ambao wameiacha kweli, wakisema kwamba ufufuo wa wafu umekwisha kuwako, nao huharibu imani ya baadhi ya watu.

  40. 1 Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake, kwamba: 2 Hubiri Neno; kuwa tayari wakati ufaao na wakati usiofaa; karipia, kemea na utie moyo kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri. 3 Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima. Badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe, watajikusanyia idadi kubwa ya walimu wapate kuwaambia yale ambayo masikio yao yanayowasha yanatamani kuyasikia. 4 Watakataa kusikiliza kweli na kuzigeukia hadithi za uongo. 5 Kwa habari yako wewe, vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiza wajibu wote wa huduma yako.

  41. 9 Kijana aifanye njia yake kuwa safi jinsi gani?

    Ni kwa kutii, akilifuata neno lako.

  42. 34 Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia. 35 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

  43. 10 Je, hamjasoma Andiko hili:

    “ ‘Jiwe walilolikataa waashi

    limekuwa jiwe kuu la pembeni;

  44. 27 Naye akianzia na Sheria ya Mose na Manabii wote, akawafafanulia jinsi Maandiko yalivyosema kumhusu yeye.

  45. 1 Siku hiyo, Kitabu cha Mose kilisomwa kwa sauti kuu, na watu wote wakasikia. Humo ilionekana imeandikwa kwamba hakuna Mwamoni wala Mmoabu atakayeruhusiwa katika kusanyiko la watu wa Mungu, 2 kwa sababu hawakuwalaki Waisraeli kwa chakula na maji. Badala yake walimwajiri Balaamu kuwalaani (lakini hata hivyo Mungu wetu aligeuza laana kuwa baraka). 3 Watu waliposikia sheria hii, waliwatenga watu wote wasio Waisraeli waliokuwa wa uzao wa kigeni.

  46. 8 “Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu,

    wala njia zenu si njia zangu,”

    asema Bwana.

    9 “Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia,

    ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu

    na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.

    10 Kama vile mvua na theluji

    ishukavyo kutoka mbinguni,

    nayo hairudi tena huko

    bila kunywesha dunia

    na kuichipusha na kuistawisha,

    hivyo hutoa mbegu kwa mpanzi

    na mkate kwa mlaji,

    11 ndivyo lilivyo neno langu lile litokalo kinywani mwangu:

    Halitanirudia tupu,

    bali litatimiliza lile nililokusudia

    na litafanikiwa katika kusudi lile nililolituma.

  47. 18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”

  48. 13 Atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza awatie katika kweli yote. Yeye hatanena kwa ajili yake mwenyewe, bali atanena yale yote atakayosikia, naye atawaonyesha mambo yajayo.

  49. 15 Katika siku hizo Petro akasimama katikati ya waumini (jumla yao wote walikuwa watu wapatao 120), akasema, 16 “Ndugu zangu, ilibidi Andiko litimie ambalo Roho Mtakatifu alitabiri kupitia kwa Daudi kumhusu Yuda aliyewaongoza wale waliomkamata Yesu. 17 Yuda alikuwa mmoja wetu, kwa maana na yeye alichaguliwa ashiriki katika huduma hii.”

  50. 4 Sikia, ee Israeli: Bwana Mungu wako, Bwana ni mmoja. 5 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. 6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. 7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo. 8 Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako. 9 Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.

  51. 160 Maneno yako yote ni kweli,

    sheria zako zote za haki ni za milele.

  52. 47 “Mimi simhukumu mtu yeyote anayesikia maneno yangu na asiyatii, kwa maana sikuja kuuhukumu ulimwengu, bali kuuokoa. 48 Yuko amhukumuye yeye anikataaye mimi na kutokuyapokea maneno yangu, yaani, yale maneno niliyosema yenyewe yatamhukumu siku ya mwisho. 49 Kwa maana sisemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba aliyenituma aliniamuru ni nini cha kusema na jinsi ya kukisema. 50 Nami ninajua amri zake huongoza hadi kwenye uzima wa milele. Hivyo lolote nisemalo, ndilo lile Baba aliloniambia niseme.”

  53. 12 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi. 13 Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. 14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. 15 Siwaiti ninyi watumishi tena, kwa sababu watumishi hawajui bwana wao analofanya, bali nimewaita ninyi rafiki, kwa maana nimewajulisha mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu. 16 Si ninyi mlionichagua, bali mimi ndiye niliyewachagua ninyi na kuwaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kudumu. Ili nalo lolote mtakalomwomba Baba katika Jina langu, awape ninyi. 17 Amri yangu ndiyo hii: Mpendane.

    18 “Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba ulinichukia mimi kabla yenu. 19 Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungeliwapenda kama vile unavyowapenda walio wake. Kwa sababu ninyi si wa ulimwengu, lakini mimi nimewachagua kutoka ulimwengu, hii ndiyo sababu ulimwengu unawachukia.

  54. 6 Nashangaa kwamba mnamwacha upesi hivyo yeye aliyewaita kwa neema ya Kristo na kuifuata Injili nyingine, 7 ambayo kwa kweli si Injili kamwe, ila kwa dhahiri kuna watu wanaowachanganya na wanaotaka kuipotosha Injili ya Kristo. 8 Lakini hata ikiwa sisi au malaika atokaye mbinguni akihubiri Injili nyingine tofauti na ile tuliyowahubiria sisi, basi mtu huyo alaaniwe milele! 9 Kama vile tulivyokwisha kusema kabla, sasa nasema tena, ikiwa mtu yeyote atawahubiria Injili kinyume na ile mliyoipokea na alaaniwe milele!

    10 Je, sasa mimi ninatafuta kukubaliwa na wanadamu au kukubaliwa na Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa bado najaribu kuwapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumishi wa Kristo.

    11 Ndugu zangu, nataka mjue kwamba Injili niliyowahubiria haikutokana na wanadamu. 12 Kwa maana mimi sikuipokea hiyo Injili kutoka kwa mwanadamu, wala sikufundishwa na mtu, bali niliipata kwa ufunuo kutoka kwa Yesu Kristo.

  55. 11 Huu ndio ushuhuda: kwamba Mungu ametupa uzima wa milele, nao huo uzima umo katika Mwanawe. 12 Aliye naye Mwana wa Mungu anao uzima, yeye asiye na Mwana wa Mungu hana uzima.

    13 Nawaandikia mambo haya ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu ili mpate kujua ya kuwa mnao uzima wa milele. 14 Huu ndio ujasiri tulio nao tunapomkaribia Mungu, kwamba kama tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. 15 Nasi kama tunajua atusikia, lolote tuombalo, tunajua ya kwamba tumekwisha kupata zile haja tulizomwomba.

  56. 12 Sijaziacha amri zilizotoka midomoni mwake;

    nimeyathamini maneno ya kinywa chake kuliko chakula changu cha kila siku.

  57. 97 Aha! Tazama, sheria yako naipenda mno ajabu.

    Ninaitafakari mchana kutwa.

    98 Amri zako zimenipa hekima zaidi kuliko adui zangu,

    kwa kuwa nimezishika daima.

    99 Nina akili zaidi kuliko walimu wangu wote,

    kwa kuwa ninatafakari juu ya sheria zako.

  58. 1 Kisha Yesu akaongozwa na Roho Mtakatifu kwenda nyikani ili akajaribiwe na ibilisi. 2 Baada ya kufunga siku arobaini usiku na mchana, hatimaye akaona njaa. 3 Mjaribu akamjia na kumwambia, “Ikiwa wewe ndiye Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate.”

    4 Lakini Yesu akajibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’ ”

    5 Ndipo ibilisi akamchukua Yesu mpaka mji mtakatifu na kumweka juu ya mnara mrefu wa Hekalu, 6 akamwambia, “Kama wewe ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini. Kwa kuwa imeandikwa:

    “ ‘Atakuagizia malaika zake,

    nao watakuchukua mikononi mwao

    ili usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’ ”

    7 Yesu akamjibu, “Pia imeandikwa: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’ ”

    8 Kwa mara nyingine, ibilisi akamchukua Yesu mpaka kwenye kilele cha mlima mrefu na kumwonyesha falme zote za dunia na fahari zake, 9 kisha akamwambia, “Nitakupa hivi vyote kama ukinisujudia na kuniabudu.”

    10 Yesu akamwambia, “Ondoka mbele yangu, Shetani! Kwa maana imeandikwa, ‘Mwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’ ”

    11 Ndipo ibilisi akamwacha, nao malaika wakaja na kumhudumia.

  59. 28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

  60. 5 “Kila neno la Mungu ni kamilifu;

    yeye ni ngao kwa wale wanaomkimbilia.

    6 Usiongeze kwenye maneno yake,

    ama atakukemea na kukuthibitisha kuwa mwongo.

  61. 16 Angalieni katika gombo la Bwana na msome:

    Hakuna hata mmoja katika hawa atakayekosekana,

    hakuna hata mmoja atakayemkosa mwenzi wake.

    Kwa kuwa ni kinywa chake Mungu kimeagiza,

    na Roho wake atawakusanya pamoja.

  62. 42 Yesu akawaambia, “Je, hamjasoma katika Maandiko kwamba:

    “ ‘Jiwe walilolikataa waashi

    limekuwa jiwe kuu la pembeni.

    Bwana ndiye alitenda jambo hili,

    nalo ni la ajabu machoni petu’?

  63. 21 Ndipo akaanza kwa kuwaambia, “Leo Andiko hili limetimia mkiwa mnasikia.”

  64. 63 Roho ndiye atiaye uzima, mwili haufai kitu. Maneno haya niliyowaambia ni Roho tena ni uzima.

  65. 20 Wakati huo mtajua ya kuwa mimi niko ndani ya Baba na ninyi mko ndani yangu na mimi niko ndani yenu. 21 Yeyote mwenye amri zangu na kuzishika ndiye anipendaye, naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”

    22 Ndipo Yuda, siyo Iskariote, akamwambia, “Bwana, itakuwaje kwamba utajidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?”

    23 Yesu akamjibu, “Mtu yeyote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake. 24 Mtu yeyote asiyenipenda hayashiki maneno yangu na maneno niliyowapa si yangu bali ni ya Baba aliyenituma.

  66. 26 Basi malaika wa Bwana akamwambia Filipo, “Nenda upande wa kusini kwenye ile barabara itokayo Yerusalemu kuelekea Gaza ambayo ni jangwa.” 27 Hivyo akaondoka. Akiwa njiani akakutana na towashi wa Kushi, aliyekuwa afisa mkuu, mwenye mamlaka juu ya hazina zote za Kandake, Malkia wa Kushi. Huyu towashi alikuwa amekwenda Yerusalemu ili kuabudu, 28 naye akiwa njiani kurudi nyumbani alikuwa ameketi garini mwake akisoma kitabu cha nabii Isaya. 29 Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye lile gari ukae karibu nalo.”

    30 Ndipo Filipo akakimbilia lile gari na kumsikia yule mtu anasoma kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamuuliza, “Je, unaelewa hayo usomayo?”

    31 Yule towashi akasema, “Nitawezaje kuelewa mtu asiponifafanulia?” Hivyo akamkaribisha Filipo ili apande na kuketi pamoja naye.

    32 Huyu towashi alikuwa anasoma fungu hili la Maandiko:

    “Aliongozwa kama kondoo aendaye machinjoni,

    kama mwana-kondoo anyamazavyo

    mbele yake yule amkataye manyoya,

    hivyo hakufungua kinywa chake.

    33 Katika kufedheheshwa kwake alinyimwa haki yake.

    Nani awezaye kueleza juu ya kizazi chake?

    Kwa maana maisha yake yaliondolewa

    kutoka duniani.”

    34 Yule towashi akamuuliza Filipo, “Tafadhali niambie, nabii huyu anena habari zake mwenyewe au habari za mtu mwingine?” 35 Ndipo Filipo akaanza kutumia fungu lile la Maandiko, akamweleza habari njema za Yesu.

    36 Walipokuwa wakiendelea na safari wakafika mahali palipokuwa na maji, yule towashi akamuuliza Filipo, “Tazama, hapa kuna maji. Kitu gani kitanizuia nisibatizwe?” [ 37 Filipo akamwambia, “Kama ukiamini kwa moyo wako wote unaweza kubatizwa.” Akajibu, “Naamini kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu.”] 38 Naye akaamuru lile gari lisimamishwe. Wakateremka kwenye maji wote wawili, yule towashi na Filipo, naye Filipo akambatiza. 39 Nao walipopanda kutoka kwenye maji, ghafula Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, naye towashi hakumwona tena, lakini akaenda zake akifurahi. 40 Filipo akajikuta yuko Azoto, akasafiri akihubiri Injili katika miji yote mpaka alipofika Kaisaria.

  67. 17 Ndugu zangu, nawasihi mjihadhari na kujiepusha na wale watu waletao matengano na kuweka vikwazo mbele yenu dhidi ya mafundisho mliyojifunza. 18 Kwa maana watu kama hao hawamtumikii Bwana Kristo, bali wanatumikia tamaa zao wenyewe. Kwa kutumia maneno laini na ya kubembeleza, hupotosha mioyo ya watu wajinga.

  68. 11 Mambo haya yote yaliwapata wao ili yawe mifano kwa wengine, nayo yaliandikwa ili yatuonye sisi ambao mwisho wa nyakati umetufikia. 12 Hivyo, yeye ajidhaniaye amesimama, aangalie asianguke.

  69. 1 Zamani Mungu alisema na baba zetu kwa njia ya manabii mara nyingi na kwa njia mbalimbali, 2 lakini katika siku hizi za mwisho anasema nasi kwa njia ya Mwanawe, ambaye amemweka kuwa mrithi wa vitu vyote, na ambaye kupitia kwake aliuumba ulimwengu.

  70. 11 Yeyote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Yeyote ahudumuye hana budi kuhudumu kwa nguvu zile anazopewa na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kwa njia ya Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye milele na milele. Amen.

  71. 1 watu wote wakakusanyika kama mtu mmoja kwenye uwanja mbele ya Lango la Maji. Wakamwambia Ezra mwandishi alete Kitabu cha Sheria ya Mose, ambacho Bwana aliamuru kwa ajili ya Israeli.

    2 Basi katika siku ya kwanza ya mwezi wa saba, kuhani Ezra akaleta Sheria mbele ya kusanyiko, ambamo walikuwamo wanaume, wanawake na watu wote walioweza kufahamu. 3 Akaisoma kwa sauti kubwa tangu mapambazuko mpaka adhuhuri, akiwa ameuelekea uwanja uliokuwa mbele ya Lango la Maji mbele ya wanaume, wanawake na wengine ambao waliweza kufahamu. Watu wote wakasikiliza kwa makini kile Kitabu cha Sheria.

    4 Mwandishi Ezra alikuwa amesimama juu ya jukwaa la miti lililojengwa kwa kusudi hilo. Karibu naye upande wa kuume alisimama Matithia, Shema, Anaya, Uria, Hilkia na Maaseya. Upande wake wa kushoto walikuwepo Pedaya, Mishaeli, Malkiya, Hashumu, Hashbadani, Zekaria na Meshulamu.

    5 Ezra akakifungua kile kitabu. Watu wote waliweza kumwona kwa sababu alikuwa amesimama juu zaidi, naye alipokifungua watu wote wakasimama. 6 Ezra akamsifu Bwana, Mungu mkuu, nao watu wote wakainua mikono yao na kuitikia, “Amen! Amen!” Kisha wakasujudu na kumwabudu Bwana hali nyuso zao zikigusa ardhi.

    7 Watu wakiwa wamesimama pale, Walawi wafuatao waliwafunza ile Sheria: Yeshua, Bani, Sherebia, Yamini, Akubu, Shabethai, Hodia, Maaseya, Kelita, Azaria, Yozabadi, Hanani na Pelaya. 8 Walisoma kutoka kile Kitabu cha Sheria ya Mungu, wakiifafanua na kuwapa maelezo ili watu waweze kufahamu kile kilichokuwa kikisomwa.

  72. 82 Macho yangu yamefifia, nikingoja ahadi yako;

    ninasema, “Utanifajiri lini?”

  73. 148 Sikufumba macho yangu usiku kucha,

    ili niweze kutafakari juu ya ahadi zako.

  74. 36 “Mwalimu, ni amri ipi katika Sheria iliyo kuu kuliko zote?”

    37 Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’ 38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. 39 Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ 40 Amri hizi mbili ndizo msingi wa Sheria na Manabii.”

    41 Wakati Mafarisayo walikuwa wamekusanyika pamoja, Yesu akawauliza, 42 “Mnaonaje kuhusu Kristo? Yeye ni mwana wa nani?”

    Wakamjibu, “Yeye ni mwana wa Daudi.”

    43 Akawaambia, “Inakuwaje basi kwamba Daudi, akinena kwa kuongozwa na Roho, anamwita Kristo ‘Bwana’? Kwa maana asema,

    44 “ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:

    “Keti mkono wangu wa kuume,

    hadi nitakapowaweka adui zako

    chini ya miguu yako.” ’

    45 Kama basi Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ awezaje kuwa mwanawe?” 46 Hakuna mtu aliyeweza kumjibu Yesu neno. Tena tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu kumuuliza tena maswali.

  75. 15 Akawaambia, “Enendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. 16 Yeyote aaminiye na kubatizwa ataokoka. Lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa.

  76. 22 Baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake wakakumbuka yale aliyokuwa amesema. Ndipo wakayaamini Maandiko na yale maneno Yesu aliyokuwa amesema.

  77. 1 Wakasafiri kupitia Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambako kulikuwa na sinagogi la Wayahudi. 2 Kama desturi yake, Paulo aliingia ndani ya sinagogi, na kwa muda wa Sabato tatu akawa anahojiana nao kutoka kwenye Maandiko, 3 akidhihirisha wazi na kuthibitisha kwamba ilikuwa lazima Kristo ateswe na afufuke kutoka kwa wafu. Akasema, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake, ndiye Kristo.” 4 Baadhi ya Wayahudi wakasadiki, wakaungana na Paulo na Sila, wakiwepo idadi kubwa ya Wayunani waliomcha Mungu na wanawake wengi mashuhuri.

  78. 11 Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, 12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa 13 mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo.

    14 Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. 15 Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo. 16 Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.

  79. 26 kusudi alifanye takatifu, akilitakasa kwa kuliosha kwa maji katika Neno lake,

  80. 3 Basi katika hili twajua ya kuwa tumemjua, tukizishika amri zake. 4 Mtu yeyote asemaye kuwa, “Ninamjua,” lakini hazishiki amri zake, ni mwongo, wala ndani ya mtu huyo hamna kweli. 5 Lakini mtu yeyote anayelitii neno lake, upendo wa Mungu umekamilika ndani yake kweli kweli. Katika hili twajua kuwa tumo ndani yake. 6 Yeyote anayesema anakaa ndani yake hana budi kuenenda kama Yesu alivyoenenda.