70 Bible Verses About The Sabbath
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
8 Ikumbuke siku ya Sabato, uitakase. 9 Kwa siku sita utafanya kazi na kutenda shughuli zako zote, 10 lakini siku ya saba ni Sabato kwa Bwana Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wako wa kiume au wa kike, wala wanyama wako, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. 11 Kwa kuwa kwa siku sita, Bwana aliumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo, lakini akapumzika siku ya saba. Kwa hiyo Bwana akaibariki siku ya Sabato na kuifanya takatifu.
-
1 Kwa hiyo mbingu na dunia zikakamilika, pamoja na vyote vilivyomo.
2 Katika siku ya saba Mungu alikuwa amekamilisha kazi aliyokuwa akiifanya, hivyo siku ya saba akapumzika kutoka kazi zake zote. 3 Mungu akaibariki siku ya saba akaifanya takatifu, kwa sababu katika siku hiyo alipumzika kutoka kazi zote za kuumba alizokuwa amefanya.
-
12 Kisha Bwana akamwambia Mose, 13 “Waambie Waisraeli, ‘Ninyi ni lazima mzishike Sabato zangu. Hii itakuwa ni ishara kati yangu na ninyi kwa ajili ya vizazi vijavyo, ili mpate kujua kwamba Mimi Ndimi Bwana, niwafanyaye ninyi watakatifu.
14 “ ‘Mtaishika Sabato, kwa sababu ni takatifu kwenu. Yeyote atakayeinajisi lazima auawe, yeyote atakayefanya kazi siku hiyo lazima akafie mbali na watu wake. 15 Kwa siku sita, mtafanya kazi, lakini siku ya saba ni Sabato ya kupumzika, takatifu kwa Bwana. Yeyote afanyaye kazi yoyote siku ya Sabato ni lazima auawe. 16 Waisraeli wataishika Sabato, kuiadhimisha kwa vizazi vijavyo kuwa Agano la milele. 17 Itakuwa ishara kati yangu na Waisraeli milele, kwa kuwa kwa muda wa siku sita Bwana aliumba mbingu na dunia, na siku ya saba akaacha kufanya kazi, akapumzika.’ ”
-
6 Hivyo basi, kama vile mlivyompokea Kristo Yesu kuwa Bwana, endeleeni kukaa ndani yake, 7 mkiwa na mizizi, na mmejengwa ndani yake, mkiimarishwa katika imani kama mlivyofundishwa, na kufurika kwa wingi wa shukrani.
8 Angalieni mtu yeyote asiwafanye ninyi mateka kwa elimu batili na madanganyo matupu yanayotegemea mapokeo ya wanadamu na mafundisho ya ulimwengu badala ya Kristo.
9 Maana ukamilifu wote wa Uungu umo ndani ya Kristo katika umbile la mwili wa kibinadamu, 10 nanyi mmepewa ukamilifu ndani ya Kristo, ambaye ndiye mkuu juu ya kila enzi na kila mamlaka. 11 Katika Kristo pia mlitahiriwa kwa kutengwa mbali na asili ya dhambi, si kwa tohara inayofanywa kwa mikono ya wanadamu, bali kwa ile tohara iliyofanywa na Kristo, 12 mkiwa mmezikwa pamoja naye katika ubatizo, na kufufuliwa pamoja naye kwa njia ya imani yenu katika uweza wa Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu.
13 Mlipokuwa wafu katika dhambi zenu na kutokutahiriwa katika asili yenu ya dhambi, Mungu aliwafanya mwe hai pamoja na Kristo. Alitusamehe dhambi zetu zote, 14 akiisha kuifuta ile hati yenye mashtaka yaliyokuwa yanatukabili, pamoja na maagizo yake. Aliiondoa isiwepo tena, akiigongomea kwenye msalaba wake. 15 Mungu akiisha kuzivua enzi na mamlaka, alizifanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuziburura kwa ujasiri, akizishinda katika msalaba wa Kristo.
16 Kwa hiyo mtu asiwahukumu ninyi kuhusu vyakula au vinywaji, au kuhusu kuadhimisha sikukuu za dini, au Sikukuu za Mwezi Mwandamo au siku ya Sabato. 17 Hizi zilikuwa kivuli cha mambo ambayo yangekuja, lakini ile iliyo halisi imo ndani ya Kristo. 18 Mtu yeyote asiwaondolee thawabu yenu kwa kusisitiza kunyenyekea kwake na kuabudu malaika. Mtu kama huyo hudumu katika maono yake, akijivuna bila sababu katika mawazo ya kibinadamu. 19 Yeye amepoteza ushirikiano na Kichwa, ambaye kutoka kwake mwili wote unalishwa na kushikamanishwa pamoja kwa viungo na mishipa, nao hukua kwa ukuaji utokao kwa Mungu.
20 Kwa kuwa mlikufa pamoja na Kristo, mkayaacha yale mafundisho ya msingi ya ulimwengu huu, kwa nini bado mnaishi kama ninyi ni wa ulimwengu? Kwa nini mnajitia chini ya amri: 21 “Msishike! Msionje! Msiguse!”? 22 Haya yote mwisho wake ni kuharibika yanapotumiwa, kwa sababu msingi wake ni katika maagizo na mafundisho ya wanadamu. 23 Kwa kweli amri kama hizo huonekana kama zina hekima, katika namna za ibada walizojitungia wenyewe, na unyenyekevu wa uongo na kuutawala mwili kwa ukali, lakini hayafai kitu katika kuzuia tamaa za mwili.
-
15 Siku hizo nikaona watu katika Yuda wakikanyaga mashinikizo ya divai siku ya Sabato na kuleta nafaka wakiwapakiza punda, pamoja na divai, zabibu, tini na aina nyingine za mizigo. Nao walikuwa wakileta haya yote Yerusalemu siku ya Sabato. Kwa hiyo niliwaonya dhidi ya kuuza vyakula siku hiyo. 16 Watu kutoka Tiro waliokuwa wakiishi Yerusalemu walileta samaki na aina nyingi za bidhaa na kuziuza Yerusalemu siku ya Sabato kwa watu wa Yuda. 17 Niliwakemea wakuu wa Yuda na kuwaambia, “Ni uovu gani huu mnaofanya wa kuinajisi siku ya Sabato? 18 Je, baba zenu hawakufanya mambo kama haya, hata wakamsababisha Mungu wetu kuleta maafa haya yote juu yetu na juu ya mji huu? Sasa bado mnazidi kuchochea ghadhabu yake dhidi ya Israeli kwa kuinajisi Sabato.”
19 Wakati vivuli vya jioni vilipoangukia juu ya malango ya Yerusalemu kabla ya Sabato, niliamuru milango ifungwe, wala isifunguliwe mpaka Sabato iishe. Nikawaweka baadhi ya watu wangu mwenyewe kwenye malango ili pasiwepo mzigo utakaoingizwa ndani siku ya Sabato. 20 Mara moja au mbili wachuuzi na wauzaji wa bidhaa za aina zote walilala usiku nje ya mji wa Yerusalemu. 21 Lakini niliwaonya na kuwaambia, “Kwa nini mnalala karibu na ukuta? Kama mkifanya hivi tena, nitawaadhibu.” Kuanzia wakati ule hawakuja tena siku ya Sabato. 22 Kisha nikawaamuru Walawi kujitakasa na kwenda kulinda malango ili kutunza Sabato iwe takatifu.
Ee Mungu wangu, unikumbuke kwa ajili ya hili pia, nawe unionyeshe wema wako sawasawa na upendo wako mkuu.
-
23 Siku moja ya Sabato, Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wakipita katikati ya mashamba ya nafaka. Walipokuwa wakitembea, wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke. 24 Mafarisayo wakamwambia, “Tazama, mbona wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato?”
25 Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma kamwe alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walikuwa na njaa, wakahitaji chakula? 26 Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu, wakati Abiathari alikuwa kuhani mkuu, akaila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani peke yao. Naye pia akawapa wenzake.”
27 Kisha Yesu akawaambia, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, lakini si mwanadamu kwa ajili ya Sabato. 28 Hivyo, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”
-
1 Wakati huo Yesu alipitia kwenye mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wanafunzi wake walikuwa na njaa, nao wakaanza kuvunja masuke ya nafaka na kuyala. 2 Lakini Mafarisayo walipoona jambo hili, wakamwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato.”
3 Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alichofanya Daudi na wenzake walipokuwa na njaa? 4 Aliingia katika nyumba ya Mungu, akala mikate iliyowekwa wakfu, yeye na wenzake, jambo ambalo halikuwa halali kwao kufanya, isipokuwa makuhani peke yao. 5 Au hamjasoma katika Sheria kwamba siku ya Sabato makuhani huvunja sheria ya Sabato Hekaluni lakini hawahesabiwi kuwa na hatia? 6 Nawaambia wazi kwamba, yeye aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa. 7 Kama mngekuwa mmejua maana ya maneno haya, ‘Nataka rehema, wala si dhabihu,’ msingewalaumu watu wasio na hatia, 8 kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”
9 Yesu akaondoka mahali hapo, akaingia ndani ya sinagogi lao, 10 na huko alikuwepo mtu aliyepooza mkono. Wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu, wakamuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?”
11 Yesu akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu, mwenye kondoo wake ambaye huyo kondoo akitumbukia shimoni siku ya Sabato hatamtoa? 12 Mtu ana thamani kubwa kuliko kondoo. Kwa hiyo ni halali kutenda mema siku ya Sabato.”
13 Ndipo akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa ukawa mzima kama ule mwingine. 14 Lakini Mafarisayo wakatoka nje, wakafanya shauri baya juu ya Yesu jinsi watakavyoweza kumuua.
-
18 Nao walipopima katika pishi, yule aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa. Kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji.
19 Kisha Mose akawaambia, “Mtu yeyote asibakize chochote mpaka asubuhi.”
20 Hata hivyo, wengine hawakuzingatia aliyosema Mose, wakahifadhi kiasi fulani mpaka asubuhi, lakini kile alichohifadhi kikajaa mabuu na kuanza kunuka. Kwa hiyo Mose akawakasirikia.
21 Kila asubuhi, kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji na jua lilipokuwa kali, iliyeyuka. 22 Siku ya sita, wakakusanya mara mbili, kiasi cha pishi mbili kwa kila mtu, nao viongozi wa jumuiya wakaja kumwarifu Mose. 23 Mose akawaambia, “Hivi ndivyo alivyoagiza Bwana: ‘Kesho itakuwa siku ya mapumziko, Sabato takatifu kwa Bwana. Kwa hiyo okeni kile mnachotaka kuoka na mchemshe kile mnachotaka kuchemsha. Hifadhini chochote kinachobaki na mkiweke mpaka asubuhi.’ ”
24 Kwa hiyo wakavihifadhi mpaka asubuhi, kama Mose alivyoagiza, na havikunuka wala kuwa na mabuu. 25 Mose akawaambia, “Kuleni leo, kwa sababu leo ni Sabato kwa Bwana. Hamtapata chochote juu ya nchi leo. 26 Kwa siku sita mtakusanya, lakini siku ya saba, yaani Sabato, hakutakuwepo chochote.”
27 Hata hivyo, baadhi ya watu wakatoka kwenda kukusanya siku ya saba, lakini hawakupata chochote. 28 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Je, mtaacha kushika maagizo na maelekezo yangu mpaka lini? 29 Fahamuni kuwa Bwana amewapa ninyi Sabato, ndiyo sababu katika siku ya sita amewapa mikate ya siku mbili. Kila mmoja inampasa kukaa pale alipo katika siku ya saba. Hata mmoja haruhusiwi kutoka.” 30 Kwa hiyo watu wakapumzika siku ya saba.
-
13 “Kama ukitunza miguu yako isivunje Sabato,
na kutokufanya kama vile upendavyo katika siku yangu takatifu,
kama ukiita Sabato siku ya furaha
na siku takatifu ya Bwana ya kuheshimiwa,
kama utaiheshimu kwa kutoenenda
katika njia zako mwenyewe,
na kutokufanya yakupendezayo
au kusema maneno ya upuzi,
14 ndipo utakapojipatia furaha yako katika Bwana,
nami nitakufanya upande juu ya miinuko ya nchi
na kusherehekea urithi wa Yakobo baba yako.”
Kinywa cha Bwana kimenena haya.
-
22 Mitume na wazee pamoja na kanisa lote, wakaamua kuwachagua baadhi ya watu wao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Wakamchagua Yuda aitwaye Barsaba pamoja na Sila, watu wawili waliokuwa viongozi miongoni mwa ndugu. 23 Wakatumwa na barua ifuatayo:
Sisi mitume na wazee, ndugu zenu,
Kwa ndugu Mataifa mlioamini mlioko Antiokia, Shamu na Kilikia:
Salamu.
24 Tumesikia kwamba kuna baadhi ya watu waliokuja huko kutoka kwetu bila ruhusa yetu na kuwasumbua, wakiyataabisha mawazo yenu. 25 Hivyo tumekubaliana wote kuwachagua baadhi ya watu na kuwatuma kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo, 26 watu ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. 27 Kwa hiyo tunawatuma Yuda na Sila, kuthibitisha kwa maneno ya mdomo mambo haya tunayowaandikia. 28 Kwa maana imempendeza Roho Mtakatifu na sisi tusiwatwike mzigo wowote mkubwa zaidi ya mambo haya yafuatayo ambayo ni ya lazima: 29 Kwamba mjiepushe na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na mjiepushe na uasherati. Mkiyaepuka mambo haya, mtakuwa mmefanya vyema.
Kwaherini.
30 Hivyo wakaagwa, wakashuka kwenda Antiokia. Baada ya kulikusanya kanisa pamoja, wakawapa ile barua. 31 Nao hao watu wakiisha kuisoma, wakafurahishwa sana kwa ujumbe wake wa kutia moyo. 32 Yuda na Sila, ambao wenyewe walikuwa manabii, wakanena maneno mengi ya kuwatia moyo na kuwajenga katika imani wale ndugu walioamini. 33 Baada ya kukaa huko Antiokia kwa muda, wakaagwa kwa amani na wale ndugu ili waende kwa wale waliowatuma. [ 34 Lakini Sila bado akaendelea kukaa huko.] 35 Lakini Paulo na Barnaba walibaki Antiokia ambako wao pamoja na wengine wengi walifundisha na kuhubiri neno la Bwana.
-
12 Adhimisha siku ya Sabato na kuiweka takatifu, kama Bwana Mungu wako alivyokuagiza. 13 Kwa siku sita utafanya kazi na kutenda shughuli zako zote. 14 Lakini siku ya Saba ni Sabato kwa Bwana, Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wa kiume au mtumishi wa kike, wala ngʼombe wako, punda wako au mnyama wako yeyote, wala mgeni aliyeko malangoni mwako, ili kwamba mtumishi wako wa kiume na wa kike wapate kupumzika kama wewe. 15 Kumbuka mlikuwa watumwa huko Misri, na Bwana Mungu wenu aliwatoa huko kwa mkono wenye nguvu na kwa mkono ulionyooshwa. Kwa hiyo Bwana Mungu wako amekuagiza kuiadhimisha siku ya Sabato.
-
20 Waambie, ‘Sikieni neno la Bwana, enyi wafalme wa Yuda, nanyi watu wote wa Yuda, na kila mmoja aishiye Yerusalemu apitaye katika malango haya. 21 Hili ndilo asemalo Bwana: Jihadharini msije mkabeba mzigo siku ya Sabato, wala kuingiza mzigo kupitia malango ya Yerusalemu. 22 Msitoe mizigo nje ya nyumba zenu wala kufanya kazi yoyote wakati wa Sabato, lakini itakaseni siku ya Sabato, kama nilivyowaamuru baba zenu. 23 Hata hivyo hawakusikiliza wala kujali, walishupaza shingo zao, na hawakutaka kusikia wala kukubali adhabu. 24 Lakini mkiwa waangalifu kunitii, asema Bwana, nanyi msipoleta mzigo wowote kupitia malango ya mji huu wakati wa Sabato, lakini mkaitakasa siku ya Sabato kwa kutofanya kazi siku hiyo, 25 ndipo wafalme wakaao juu ya kiti cha enzi cha Daudi wataingia kupitia malango ya mji huu, pamoja na maafisa wao. Wao na maafisa wao watakuja wakiwa wamepanda magari na farasi, wakiandamana na watu wa Yuda na wale waishio Yerusalemu, nao mji huu utakaliwa na watu daima. 26 Watu watakuja kutoka miji ya Yuda na vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu, kutoka nchi ya Benyamini na chini ya vilima vya magharibi, kutoka nchi ya vilima na Negebu, wakileta sadaka za kuteketezwa na dhabihu, sadaka za nafaka, uvumba na sadaka za shukrani kwenye nyumba ya Bwana. 27 Lakini ikiwa hamtanitii mimi kwa kuitakasa Sabato na kwa kutochukua mzigo wowote mnapoingia katika malango ya Yerusalemu wakati wa Sabato, basi nitawasha moto usiozimika katika malango ya Yerusalemu utakaoteketeza ngome zake.’ ”
-
2 Amebarikiwa mtu yule atendaye hili,
mtu yule alishikaye kwa uthabiti,
yeye ashikaye Sabato bila kuinajisi,
auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote.”
3 Usimwache mgeni aambatanaye na Bwana aseme,
“Hakika Bwana atanitenga na watu wake.”
Usimwache towashi yeyote alalamike akisema,
“Mimi ni mti mkavu tu.”
4 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana:
“Kwa matowashi washikao Sabato zangu,
ambao huchagua kile kinachonipendeza
na kulishika sana agano langu:
5 hao nitawapa ndani ya Hekalu langu na kuta zake
kumbukumbu na jina bora
kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike:
nitawapa jina lidumulo milele,
ambalo halitakatiliwa mbali.
6 Wageni wanaoambatana na Bwana
ili kumtumikia,
kulipenda jina la Bwana,
na kumwabudu yeye,
wote washikao Sabato bila kuinajisi
na ambao hushika sana agano langu:
7 hawa nitawaleta kwenye mlima wangu mtakatifu
na kuwapa furaha ndani ya nyumba yangu ya sala.
Sadaka zao za kuteketeza na dhabihu zao
zitakubalika juu ya madhabahu yangu;
kwa maana nyumba yangu itaitwa
nyumba ya sala kwa mataifa yote.”
-
1 Bwana akamwambia Mose, 2 “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Hizi ndizo sikukuu zangu zilizoamriwa, sikukuu zilizoamriwa za Bwana, ambazo mtazitangaza kuwa makusanyiko matakatifu.
3 “ ‘Kuna siku sita mnazoweza kufanya kazi, lakini siku ya saba ni Sabato ya kupumzika, siku ya kusanyiko takatifu. Hamtafanya kazi yoyote. Popote mnapoishi, ni Sabato kwa Bwana.
-
11 Nikawapa amri zangu na kuwajulisha sheria zangu, kwa kuwa mtu anayezitii ataishi kwa hizo. 12 Pia niliwapa Sabato zangu kama ishara kati yangu nao, ili wapate kujua kuwa Mimi Bwana niliwafanya kuwa watakatifu.
13 “ ‘Lakini watu wa Israeli waliniasi Mimi jangwani. Hawakufuata amri zangu, bali walikataa sheria zangu, ingawa mtu yule anayezitii ataishi kwa hizo sheria, nao walizinajisi Sabato zangu kabisa. Hivyo nilisema ningemwaga ghadhabu yangu juu yao na kuwaangamiza huko jangwani. 14 Lakini kwa ajili ya Jina langu nikafanya kile ambacho kitalifanya Jina langu lisitiwe unajisi machoni mwa mataifa ambao mbele yao nilikuwa nimewatoa Waisraeli.
-
32 Waisraeli walipokuwa jangwani, mtu mmoja alikutwa akikusanya kuni siku ya Sabato. 33 Wale waliomkuta akikusanya kuni wakamleta kwa Mose, Aroni na kusanyiko lote, 34 nao wakamweka kifungoni, kwa sababu haikufahamika kwa wazi kwamba afanyiwe nini. 35 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Huyo mtu ni lazima afe. Kusanyiko lote lazima limpige mawe nje ya kambi.” 36 Hivyo kusanyiko likamtoa nje ya kambi na kumpiga mawe hadi akafa, kama Bwana alivyomwamuru Mose.
-
1 Mose akakusanya jumuiya yote ya Waisraeli na kuwaambia, “Haya ndiyo mambo ambayo Bwana amewaamuru ninyi mfanye: 2 Kwa siku sita, mtafanya kazi, lakini siku ya saba itakuwa takatifu kwenu, Sabato ya kupumzika kwa Bwana. Yeyote atakayefanya kazi yoyote siku hiyo ni lazima auawe. 3 Msiwashe moto mahali popote katika makazi yenu siku ya Sabato.”
-
16 Yesu akaenda Nazareti, alipolelewa, na siku ya Sabato alikwenda katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome, 17 naye akapewa kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na kukuta mahali palipoandikwa:
18 “Roho wa Bwana yu juu yangu,
kwa sababu amenitia mafuta
kuwahubiria maskini habari njema.
Amenituma kuwatangazia wafungwa
kufunguliwa kwao,
na vipofu kupata kuona tena,
kuwaweka huru wanaoonewa,
19 na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika.”
20 Kisha akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi na akaketi. Watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. 21 Ndipo akaanza kwa kuwaambia, “Leo Andiko hili limetimia mkiwa mnasikia.”
-
50 Basi kulikuwa na mtu mmoja mwema na mwenye haki, jina lake Yosefu. Yeye alikuwa mjumbe wa Baraza la Wayahudi, 51 lakini yeye hakuwa amekubaliana na maamuzi na vitendo vya viongozi wenzake. Huyu alikuwa mwenyeji wa Arimathaya huko Uyahudi, naye alikuwa anaungojea Ufalme wa Mungu kwa matarajio makubwa. 52 Yosefu alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. 53 Akaushusha kutoka msalabani, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi, na kuuweka katika kaburi lililochongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limezikiwa mtu mwingine bado. 54 Ilikuwa Siku ya Maandalizi, nayo Sabato ilikuwa karibu kuanza.
55 Wale wanawake waliokuwa wamekuja pamoja na Yesu wakimfuata kutoka Galilaya wakamfuata Yosefu, wakaliona kaburi na jinsi mwili wa Yesu ulivyolazwa. 56 Kisha wakarudi nyumbani, wakaandaa manukato na marhamu ya kuupaka huo mwili. Lakini wakapumzika siku ya Sabato kama ilivyoamriwa.
-
1 Ikawa siku moja ya Sabato Yesu alikuwa akipita katika mashamba ya nafaka, nao wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke ya nafaka, wakayafikicha kwa mikono yao na kula punje zake. 2 Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya mambo yasiyo halali kufanywa siku ya Sabato?”
3 Yesu akawajibu, “Je, ninyi hamjasoma kamwe alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walikuwa na njaa? 4 Aliingia ndani ya nyumba ya Mungu, akaichukua na kuila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani peke yao. Naye pia akawapa wenzake.” 5 Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”
6 Ikawa siku nyingine ya Sabato, Yesu aliingia ndani ya sinagogi na akawa anafundisha. Huko palikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umepooza. 7 Mafarisayo na walimu wa sheria walikuwa wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu. Kwa hivyo wakawa wanamwangalia sana ili waone kama ataponya katika siku ya Sabato. 8 Lakini Yesu alijua mawazo yao, hivyo akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka usimame mbele ya watu wote.” Hivyo yule mtu akainuka, akasimama mbele yao wote.
9 Ndipo Yesu akawaambia wale walimu wa sheria na Mafarisayo, “Nawauliza ninyi, ni lipi lililo halali siku ya Sabato? Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuyaangamiza?”
10 Akawatazama watu wote waliokuwepo, kisha akamwambia yule aliyepooza mkono, “Nyoosha mkono wako!” Akaunyoosha na mkono wake ukaponywa kabisa. 11 Wale wakuu wakakasirika sana, wakashauriana wao kwa wao ni nini watakachomtendea Yesu.
-
9 “ ‘Siku ya Sabato, utatoa sadaka ya wana-kondoo wawili wa mwaka mmoja wasiokuwa na dosari pamoja na sadaka yake ya kinywaji na sadaka ya nafaka yenye uzito wa sehemu mbili za kumi za efa za unga laini uliochanganywa na mafuta. 10 Hii ni sadaka ya kuteketezwa itakayotolewa kwa ajili ya kila Sabato, pamoja na sadaka ya kawaida ya kuteketezwa na sadaka yake ya kinywaji.
-
1 Basi kuhusu changizo kwa ajili ya watakatifu: Kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia, fanyeni vivyo hivyo. 2 Siku ya kwanza ya kila juma, kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha, kulingana na mapato yake na fedha hizo aziweke akiba, ili nitakapokuja pasiwe na lazima ya kufanya mchango.
-
19 Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, fuateni amri zangu tena kuweni waangalifu kushika sheria zangu. 20 Zitakaseni Sabato zangu ili ziwe ishara kati yangu nanyi. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”
21 “ ‘Lakini watoto hao wakaniasi: Hawakufuata amri zangu, wala hawakuwa waangalifu kushika sheria zangu, ingawa mtu anayezitii anaishi kwa hizo sheria, nao wakazinajisi Sabato zangu. Hivyo nikasema ningemwaga ghadhabu yangu juu yao na kutimiza hasira yangu dhidi yao huko jangwani.
-
8 Kwa maana kama Yoshua alikuwa amewapa raha, Mungu hangesema tena baadaye kuhusu siku nyingine. 9 Kwa hiyo basi, imebaki raha ya Sabato kwa ajili ya watu wa Mungu; 10 kwa kuwa kila mmoja aingiaye katika raha ya Mungu pia hupumzika kutoka kazi zake mwenyewe, kama vile Mungu alivyopumzika kutoka kazi zake. 11 Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha hiyo, ili kwamba asiwepo yeyote atakayeanguka kwa kufuata mfano wao wa kutokutii.
-
42 Paulo na Barnaba walipokuwa wakitoka nje ya sinagogi, watu wakawaomba wazungumze tena mambo hayo Sabato iliyofuata. 43 Baada ya kusanyiko la Sinagogi kutawanyika, wengi wa Wayahudi na waongofu wa dini ya Kiyahudi wakawafuata Paulo na Barnaba, wakazungumza nao na kuwahimiza wadumu katika neema ya Mungu.
44 Sabato iliyofuata, karibu watu wote wa mji walikuja kusikiliza neno la Bwana.
-
1 Mkaribisheni yeye ambaye imani yake ni dhaifu, lakini si kwa kugombana na kubishana juu ya mawazo yake. 2 Mtu mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu, lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula mboga tu. 3 Yeye alaye kila kitu asimdharau yeye asiyekula. Wala yeye asiyekula kila kitu asimhukumu yule alaye kila kitu, kwa maana Mungu amemkubali. 4 Wewe ni nani hata umhukumu mtumishi wa mtu mwingine? Kwa bwana wake tu anasimama au kuanguka. Naye atasimama kwa sababu Bwana anaweza kumsimamisha.
5 Mtu mmoja anaitukuza siku fulani kuwa ni bora kuliko nyingine, na mwingine anaona kuwa siku zote ni sawa. Basi kila mmoja awe na hakika na yale anayoamini. 6 Yeye anayehesabu siku moja kuwa takatifu kuliko nyingine, hufanya hivyo kwa kumheshimu Bwana. Naye alaye nyama hula kwa Bwana, kwa maana humshukuru Mungu, naye akataaye kula nyama hufanya hivyo kwa Bwana na humshukuru Mungu. 7 Kwa kuwa hakuna hata mmoja wetu anayeishi kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna hata mmoja wetu afaye kwa ajili yake mwenyewe. 8 Kama tunaishi, tunaishi kwa Bwana, nasi pia tukifa tunakufa kwa Bwana. Kwa hiyo basi, kama tukiishi au kama tukifa, sisi ni mali ya Bwana.
-
1 Ikawa siku moja Yesu alipokuwa amekwenda kula chakula kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo siku ya Sabato, watu walikuwa wakimchunguza kwa bidii. 2 Papo hapo mbele yake palikuwa na mtu mmoja mwenye ugonjwa wa kuvimba mwili. 3 Yesu akawauliza wale Mafarisayo na walimu wa sheria, “Je, ni halali kuponya watu siku ya Sabato au la?” 4 Wakakaa kimya. Hivyo Yesu akamshika yule mgonjwa mkono na kumponya, akamruhusu aende zake.
5 Kisha akawauliza, “Kama mmoja wenu angekuwa na mtoto au ngʼombe wake aliyetumbukia katika kisima siku ya Sabato, je, hamtamvuta mara moja na kumtoa?” 6 Nao hawakuwa na la kusema.
-
14 Kutoka Perga wakaendelea hadi Antiokia ya Pisidia. Siku ya Sabato wakaingia ndani ya sinagogi, wakaketi. 15 Baada ya Sheria ya Mose na Kitabu cha Manabii kusomwa, viongozi wa sinagogi wakawatumia ujumbe wakisema, “Ndugu, kama mna neno la kuwafariji watu hawa, tafadhali lisemeni.”
-
13 Siku ya Sabato tukaenda nje ya lango la mji kando ya mto, mahali ambapo tulitarajia tungepata mahali pa kufanyia maombi. Tukaketi, tukaanza kuongea na baadhi ya wanawake waliokuwa wamekusanyika huko. 14 Mmoja wa wale wanawake waliotusikiliza aliitwa Lidia, mfanyabiashara wa nguo za zambarau, mwenyeji wa mji wa Thiatira, aliyekuwa mcha Mungu. Bwana akaufungua moyo wake akaupokea ujumbe wa Paulo.
-
4 Kila Sabato Paulo alikuwa akihojiana nao katika sinagogi, akijitahidi kuwashawishi Wayahudi na Wayunani.
5 Sila na Timotheo walipowasili kutoka Makedonia, walimkuta Paulo akiwa amejitolea muda wake wote katika kuhubiri, akiwashuhudia Wayahudi kwamba Yesu ndiye Kristo 6 Wayahudi walipompinga Paulo na kukufuru, yeye aliyakungʼuta mavazi yake, akawaambia, “Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu! Mimi sina hatia, nimetimiza wajibu wangu. Kuanzia sasa nitawaendea watu wa Mataifa.”
-
5 Akawaamuru akisema, “Hivi ndivyo iwapasavyo kufanya: Ninyi ambao mko makundi matatu mnaoingia zamu siku ya Sabato, theluthi yenu inayolinda jumba la kifalme, 6 theluthi nyingine Lango la Suri, na theluthi nyingine lango lililo nyuma ya walinzi, ambao hupeana zamu kulinda Hekalu, 7 nanyi ambao mko katika makundi mengine mawili ambao kwa kawaida hupumzika Sabato, wote mtalinda Hekalu kwa ajili ya mfalme. 8 Jipangeni kumzunguka mfalme, kila mtu akiwa na silaha yake mkononi. Yeyote anayesogelea safu zenu lazima auawe. Kaeni karibu na mfalme popote aendapo.”
9 Wakuu wa vikosi vya mamia wakafanya kama vile kuhani Yehoyada aliagiza. Kila mmoja akawachukua watu wake, wale waliokuwa wakiingia zamu siku ya Sabato na wale waliokuwa wakienda mapumziko, nao wakaja kwa kuhani Yehoyada.
-
10 Basi Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo siku ya Sabato. 11 Wakati huo huo akaja mwanamke mmoja aliyekuwa na pepo mchafu, naye alikuwa amepinda mgongo kwa muda wa miaka kumi na minane, wala alikuwa hawezi kunyooka wima. 12 Yesu alipomwona, akamwita, akamwambia, “Mwanamke, uwe huru, umepona ugonjwa wako.” 13 Yesu alipomwekea mikono yake, mara akasimama wima akaanza kumtukuza Mungu.
14 Lakini kiongozi wa sinagogi akakasirika kwa sababu Yesu alikuwa ameponya mtu siku ya Sabato. Akaambia ule umati wa watu, “Kuna siku sita ambazo watu wanapaswa kufanya kazi. Katika siku hizo, njooni mponywe, lakini si katika siku ya Sabato.”
15 Lakini Bwana akamjibu, “Enyi wanafiki! Je, kila mmoja wenu hamfungulii ngʼombe wake au punda wake kutoka zizini akampeleka kumnywesha maji siku ya Sabato? 16 Je, huyu mwanamke, ambaye ni binti wa Abrahamu, aliyeteswa na Shetani akiwa amemfunga kwa miaka yote hii kumi na minane, hakustahili kufunguliwa kutoka kifungo hicho siku ya Sabato?”
17 Aliposema haya, wapinzani wake wakaaibika, lakini watu wakafurahi kwa ajili ya mambo ya ajabu aliyoyafanya.
-
1 Wakasafiri kupitia Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambako kulikuwa na sinagogi la Wayahudi. 2 Kama desturi yake, Paulo aliingia ndani ya sinagogi, na kwa muda wa Sabato tatu akawa anahojiana nao kutoka kwenye Maandiko, 3 akidhihirisha wazi na kuthibitisha kwamba ilikuwa lazima Kristo ateswe na afufuke kutoka kwa wafu. Akasema, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake, ndiye Kristo.”
-
1 Yesu akaingia tena ndani ya sinagogi, na huko palikuwa na mtu aliyepooza mkono. 2 Wakawa wanamwangalia waone kama atamponya siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshtaki. 3 Yesu akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Njoo hapa mbele ya watu wote.”
4 Kisha Yesu akawauliza, “Je, ni lipi lililo halali siku ya Sabato: Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao wakanyamaza kimya.
5 Yesu akawatazama pande zote kwa hasira, akahuzunika sana kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa kabisa! 6 Kisha Mafarisayo wakatoka nje, nao wakaanza kufanya shauri la kumuua Yesu wakiwa na Maherode.
-
13 Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana!
Uvumba wenu ni chukizo kwangu.
Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada:
siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu.
-
22 “Kama vile mbingu mpya na nchi mpya ninazozifanya zitakavyodumu mbele zangu,” asema Bwana, “ndivyo jina lenu na wazao wenu watakavyodumu. 23 Kutoka Mwezi Mpya hata mwingine, na kutoka Sabato hadi nyingine, wanadamu wote watakuja na kusujudu mbele zangu,” asema Bwana.
-
8 Mikate hii itawekwa mbele za Bwana kila wakati, Sabato baada ya Sabato, kwa niaba ya Waisraeli, kuwa Agano la kudumu. 9 Hii ni mali ya Aroni na wanawe, watakaoila katika mahali patakatifu, kwa sababu ni sehemu takatifu sana ya fungu lao la kawaida la sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa kuteketezwa kwa moto.”
-
8 Mmedharau vitu vyangu vitakatifu na kuzinajisi Sabato zangu.
-
12 “Kwa siku sita fanya kazi zako, lakini siku ya saba usifanye kazi, ili maksai wako na punda wako wapate kupumzika, naye mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwako, pamoja na mgeni, wapate kustarehe.
-
21 “Kwa siku sita utafanya kazi, lakini siku ya saba utapumzika, hata ikiwa ni majira ya kulima au ya kuvuna lazima upumzike.
-
23 Mume wake akamuuliza, “Kwa nini uende kwake leo? Leo si mwandamo wa mwezi, wala si Sabato.”
Mwanamke akasema, “Yote ni sawa.”
-
3 Siku za Sabato na za Mwezi mwandamo watu wote wa nchi wataabudu mbele za Bwana penye lile ingilio la ile njia.
-
15 “Hivyo mtakapoona lile ‘chukizo la uharibifu’ lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu (asomaye na afahamu), 16 basi wale walioko Uyahudi wakimbilie milimani. 17 Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke ili kuchukua chochote kutoka ndani ya nyumba. 18 Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake. 19 Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! 20 Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato. 21 Kwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa dunia mpaka sasa: wala haitakuwako tena kamwe. 22 Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna hata mtu mmoja ambaye angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, siku hizo zitafupizwa. 23 Wakati huo kama mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo huyu hapa!’ Au, ‘Kristo yuko kule,’ msisadiki. 24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa. 25 Angalieni, nimekwisha kuwaambia mapema.
26 “Kwa hiyo mtu yeyote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki. 27 Kwa maana kama vile umeme utokeavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
-
34 Ndipo nchi itafurahia Sabato zake muda wote ule itakapokuwa ukiwa, nanyi mkiwa katika nchi ya adui zenu. Ndipo nchi itapumzika na kufurahia Sabato zake. 35 Wakati wote nchi itakapobaki ukiwa, itapumzika na kufurahia Sabato zake ambazo haikuzipata mlipokuwa mnaishi humo.
-
11 Nitakomesha furaha na macheko yake yote:
sikukuu zake za mwaka,
sikukuu za Miandamo ya Mwezi,
siku zake za Sabato,
sikukuu zake zote zilizoamriwa.
-
30 “ ‘Shika Sabato zangu na kuheshimu mahali pangu patakatifu. Mimi ndimi Bwana.
-
17 “Msidhani kwamba nimekuja kufuta Sheria au Manabii; sikuja kuondoa bali kutimiza. 18 Kwa maana, amin nawaambia, mpaka mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yoyote kutoka kwenye Sheria, mpaka kila kitu kiwe kimetimia. 19 Kwa hiyo, yeyote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, lakini yeyote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika Ufalme wa Mbinguni.
-
27 “Siku ya kumi ya mwezi huu wa saba ni Siku ya Upatanisho. Mtafanya kusanyiko takatifu, mfunge, nanyi mtoe sadaka kwa Bwana ya kuteketezwa kwa moto. 28 Msifanye kazi siku hiyo, kwa sababu ni Siku ya Upatanisho, ambapo upatanisho unafanyika kwa ajili yenu mbele za Bwana Mungu wenu. 29 Mtu yeyote ambaye hatafunga siku hiyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake. 30 Mtu yeyote atakayefanya kazi siku hiyo nitamwangamiza kutoka miongoni mwa watu wake. 31 Hamtafanya kazi kamwe. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo popote mnapoishi. 32 Ni Sabato ya mapumziko kwenu ninyi, na lazima mfunge. Tangu jioni ya siku ya tisa ya mwezi hadi jioni inayofuata, mtaishika Sabato yenu.”
-
32 Baadhi ya ndugu zao wa ukoo wa Kohathi walikuwa viongozi wa kuandaa mikate ya Wonyesho kwa ajili ya kila Sabato, mikate iliyokuwa inawekwa mezani.
-
13 “Ulishuka katika Mlima Sinai, ukanena nao kutoka mbinguni. Uliwapa masharti na sheria zile ambazo ni za kweli na haki, pia amri na maagizo mazuri. 14 Uliwafahamisha Sabato yako takatifu na ukawapa amri, maagizo na sheria kupitia mtumishi wako Mose.
-
1 Baada ya Sabato, alfajiri mapema siku ya kwanza ya juma, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kulitazama kaburi.
-
19 Je, Mose hakuwapa ninyi sheria? Lakini hakuna hata mmoja wenu anayeishika hiyo sheria. Kwa nini mnataka kuniua?”
20 Ule umati wa watu ukamjibu, “Wewe una pepo mchafu! Ni nani anayetaka kukuua?”
21 Yesu akawajibu, “Nimefanya muujiza mmoja na nyote mkastaajabu. 22 Lakini kwa kuwa Mose aliwaamuru tohara (ingawa kwa kweli haikutoka kwa Mose bali kwa baba zenu wakuu), mnamtahiri mtoto hata siku ya Sabato. 23 Ikiwa mtoto aweza kutahiriwa siku ya Sabato kusudi sheria ya Mose isivunjwe, kwa nini mnanikasirikia kwa kumponya mtu mwili wake wote siku ya Sabato? 24 Acheni kuhukumu mambo kwa jinsi mnavyoona tu, bali hukumuni kwa haki.”
-
2 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Mtakapoingia katika nchi ninayowapa ninyi, nchi yenyewe ni lazima ishike Sabato kwa ajili ya Bwana. 3 Kwa miaka sita mtapanda mazao katika mashamba yenu, nanyi kwa miaka sita mtaikata mizabibu yenu matawi na kuvuna mazao yake. 4 Lakini mwaka wa saba nchi lazima iwe na Sabato ya mapumziko, Sabato kwa Bwana. Msipande mbegu katika mashamba yenu, wala msikate mizabibu yenu matawi. 5 Msivune na kuweka akiba kinachoota chenyewe, wala kuvuna na kusindika zabibu ambayo hamkuhudumia mashamba yake. Nchi lazima iwe na mwaka wa mapumziko. 6 Chochote nchi itoacho katika mwaka wa Sabato kitakuwa chakula chenu wenyewe, watumishi wenu wa kiume na wa kike, mfanyakazi aliyeajiriwa, na mkazi wa muda anayeishi miongoni mwenu,
-
3 “ ‘Kila mmoja wenu ni lazima amheshimu mama yake na baba yake, na pia ni lazima kuzishika Sabato zangu. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.
-
2 Ilipofika siku ya Sabato, akaanza kufundisha katika sinagogi, na wengi waliomsikia wakashangaa.
Nao wakauliza, “Mtu huyu ameyapata wapi mambo haya yote? Tazama ni hekima ya namna gani hii aliyopewa? Tazama matendo ya miujiza ayafanyayo kwa mikono yake!
-
31 Kisha Yesu akashuka kwenda Kapernaumu, mji wa Galilaya, na katika siku ya Sabato akawa anafundisha. 32 Wakashangazwa sana na mafundisho yake, maana maneno yake yalikuwa na mamlaka.
33 Ndani ya sinagogi palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu. Naye akapiga kelele kwa nguvu akisema, 34 “Tuache! Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”
35 Basi Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akisema, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!” Yule pepo mchafu akamwangusha yule mtu chini mbele yao wote, akatoka pasipo kumdhuru.
-
1 Kwa hiyo, kwa kuwa bado ahadi ya kuingia rahani iko wazi, tujihadhari ili hata mmoja wenu asije akaikosa. 2 Kwa maana sisi pia tumesikia Injili iliyohubiriwa kwetu, kama nao walivyosikia; lakini ujumbe ule waliousikia haukuwa na maana kwao, kwa sababu wale waliousikia hawakuuchanganya na imani. 3 Sasa sisi ambao tumeamini tunaingia katika ile raha, kama vile Mungu alivyosema,
“Kwa hiyo nikaapa katika hasira yangu,
‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’ ”
Lakini kazi yake ilikamilika tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 4 Kwa maana mahali fulani amezungumza kuhusu siku ya saba, akisema: “Katika siku ya saba Mungu alipumzika kutoka kazi zake zote.”
-
29 “Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu: Katika siku ya kumi ya mwezi wa saba ni lazima mfunge, wala msifanye kazi yoyote, iwe mzawa au mgeni anayeishi miongoni mwenu, 30 kwa sababu siku hii upatanisho utafanyika kwa ajili yenu ili kuwatakasa. Kisha mtakuwa safi mbele za Bwana kutokana na dhambi zenu zote. 31 Ni Sabato ya mapumziko, na lazima mfunge; ni agizo la kudumu.
-
2 “ ‘Zishikeni Sabato zangu na kuheshimu mahali patakatifu pangu. Mimi ndimi Bwana.
3 “ ‘Ikiwa mtafuata amri zangu na kuwa waangalifu kutii maagizo yangu, 4 nitawanyeshea mvua katika majira yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, na miti ya mashambani itazaa matunda yake.
-
6 Ameharibu maskani yake kama bustani,
ameharibu mahali pake pa mkutano.
Bwana amemfanya Sayuni kusahau
sikukuu zake zilizoamriwa na Sabato zake;
katika hasira yake kali amewadharau
mfalme na kuhani.
-
4 Sadaka ya kuteketezwa aletazo mkuu anayetawala kwa Bwana siku ya Sabato itakuwa ni wana-kondoo sita na kondoo dume mmoja, wote wasiwe na dosari. 5 Sadaka ya nafaka inayotolewa pamoja na huyo kondoo dume itakuwa efa moja na sadaka ya nafaka inayotolewa na hao wana-kondoo itakuwa kiasi apendacho mtu pamoja na hini ya mafuta kwa kila efa.
-
12 Ndipo waliporudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, uliokuwa karibu na Yerusalemu, umbali wa mwendo wa Sabato kutoka mjini.
-
27 Kwa sababu wakaao Yerusalemu na viongozi wao hawakumtambua wala kuelewa maneno ya manabii yasomwayo kila Sabato, bali waliyatimiza maneno hayo kwa kumhukumu yeye.
-
21 Kwa maana katika kila mji kwa vizazi vilivyopita, Mose amekuwa na wale wanaotangaza sheria yake kwa kuwa imekuwa ikisomwa kwa sauti kubwa katika masinagogi kila Sabato.”
-
14 Basi siku hiyo Yesu alipotengeneza tope na kuyafungua macho ya huyo mtu ilikuwa Sabato. 15 Mafarisayo nao wakaanza kumuuliza alivyopata kuponywa. Naye akawaambia, “Alinipaka tope kwenye macho yangu, nikanawa na sasa ninaona.”
16 Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Huyu mtu hatoki kwa Mungu, kwa sababu hashiki Sabato.”
Lakini wengine wakasema, “Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya miujiza kama hii?” Wakagawanyika.
-
8 Zamani, mlipokuwa hammjui Mungu, mlikuwa watumwa wa viumbe ambavyo kwa asili si Mungu. 9 Lakini sasa kwa kuwa mmemjua Mungu, au zaidi mmejulikana na Mungu, inakuwaje mnarejea tena katika zile kanuni za kwanza zenye udhaifu na upungufu? Mnataka ziwafanye tena watumwa? 10 Mnaadhimisha siku maalum, miezi, nyakati na miaka! 11 Nina hofu juu yenu, kwamba kazi niliyofanya kwa ajili yenu inaweza kuwa nimejitaabisha bure.
-
10 Kwa miaka arobaini nilikasirikia kizazi kile,
nikasema, “Hawa ni taifa ambalo mioyo yao imepotoka,
nao hawajazijua njia zangu.”
11 Hivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu,
“Kamwe hawataingia rahani mwangu.”
-
Zaburi ya Daudi.
1 Bwana ndiye mchungaji wangu,
sitapungukiwa na kitu.
2 Hunilaza katika malisho
ya majani mabichi,
kando ya maji matulivu huniongoza,
3 hunihuisha nafsi yangu.
Huniongoza katika njia za haki
kwa ajili ya jina lake.
-
1 Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na kongwa la utumwa.
2 Sikilizeni! Mimi, Paulo, nawaambieni kwamba kama mkikubali kutahiriwa, basi Kristo hatawafaidia chochote. 3 Namshuhudia tena kila mtu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika sheria yote. 4 Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kwa njia ya sheria mmetengwa na Kristo, mko mbali na neema ya Mungu.
-
16 Kwa hiyo Wayahudi wakaanza kumsumbua Yesu, kwa sababu alikuwa anafanya mambo kama hayo siku ya Sabato. 17 Yesu akawajibu, “Baba yangu anafanya kazi yake daima hata siku hii ya leo, nami pia ninafanya kazi.”
Shows Read in context, Share and Copy.