67 Bible Verses About Money
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
19 “Msijiwekee hazina duniani, mahali ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi huvunja na kuiba. 20 Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba. 21 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.
22 “Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni nyofu, mwili wako wote utajaa nuru. 23 Lakini kama jicho lako ni ovu, mwili wako wote utajawa na giza. Kwa hiyo basi, kama nuru iliyomo ndani yako ni giza, hilo ni giza kuu namna gani!
24 “Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.
25 “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini au mtakunywa nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? 26 Waangalieni ndege wa angani; wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wa thamani zaidi kuliko hao ndege?
-
6 Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa. 7 Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu chochote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu. 8 Lakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo. 9 Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka huanguka kwenye majaribu, na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi. 10 Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.
-
17 Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. 18 Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. 19 Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.
-
27 Vyema basi, ingekupasa kuweka fedha yangu kwa watoa riba, ili nirudipo, nichukue ile iliyo yangu na faida yake.
-
10 “Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, pia ni mwaminifu hata katika mambo makubwa, naye mtu ambaye si mwaminifu katika mambo madogo pia si mwaminifu katika mambo makubwa. 11 Ikiwa hamkuwa waaminifu katika mali ya kidunia, ni nani atakayewaaminia mali ya kweli? 12 Nanyi kama hamkuwa waaminifu na mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?
13 “Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.”
-
5 Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,
“Kamwe sitakuacha,
wala sitakupungukia.”
6 Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,
“Bwana ni msaada wangu; sitaogopa.
Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”
-
10 Yeyote apendaye fedha kamwe
hatosheki na fedha;
yeyote apendaye utajiri kamwe
hatosheki na kipato chake.
Hili nalo pia ni ubatili.
11 Mali ikiongezeka, ndivyo walaji
wanavyoongezeka.
Hii nayo inamfaidia nini mwenye mali
isipokuwa ni kushibisha macho yake?
12 Usingizi wa kibarua ni mtamu,
awe amekula kidogo au kingi,
lakini wingi wa mali
humnyima tajiri usingizi.
13 Nimeshaona uovu mzito chini ya jua:
Utajiri uliolimbikizwa kwa kujinyima
na kuleta madhara kwa mwenye mali,
14 au utajiri uliopotea kwa bahati mbaya,
hivyo kwamba wakati akiwa na mwana
hakuna chochote kilichobaki kwa ajili yake.
-
11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
-
1 Basi sikilizeni, ninyi matajiri, lieni na kuomboleza kwa ajili ya hali mbaya sana inayowajia. 2 Utajiri wenu umeoza na mavazi yenu yameliwa na nondo. 3 Dhahabu yenu na fedha yenu vimeliwa na kutu. Kutu yake itashuhudia dhidi yenu nayo itaila miili yenu kama vile moto. Mmejiwekea hazina kwa ajili ya siku za mwisho. 4 Angalieni! Ule ujira wa vibarua waliolima mashamba yenu mliouzuia kwa hila unapiga kelele dhidi yenu na vilio vya wavunaji vimefika masikioni mwa Bwana Mwenye Nguvu Zote. 5 Mmeishi duniani kwa anasa na kwa starehe, mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa. 6 Mmewahukumu na kuwaua watu wenye haki, waliokuwa hawapingani nanyi.
-
11 Fedha isiyo ya halali hupungua,
bali yeye akusanyaye fedha kidogo kidogo huongezeka.
12 Kilichotarajiwa kikikawia kuja moyo huugua,
bali tumaini lililotimizwa ni mti wa uzima.
-
31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia. 34 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.
-
15 Ndipo Yesu akawaambia, “Jihadharini! Jilindeni na aina zote za choyo. Kwa maana maisha ya mtu hayatokani na wingi wa mali alizo nazo.”
-
6 Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu. 7 Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. 8 Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema.
-
41 Kisha Yesu akaketi mkabala na sehemu ambapo sadaka zilikuwa zinawekwa na kuangalia umati wa watu wakiweka fedha zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. Matajiri wengi wakaweka kiasi kikubwa cha fedha. 42 Lakini mjane mmoja maskini akaja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba zenye thamani ya senti mbili.
43 Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka katika sanduku la hazina zaidi ya watu wengine wote. 44 Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali zao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake, akaweka kila kitu alichokuwa nacho, hata kile alichohitaji ili kuishi.”
-
7 Mlipeni kila mtu kile mnachodaiwa. Kama mnadaiwa kodi lipeni kodi, kama ni ushuru, lipeni ushuru, astahiliye hofu, mhofu, astahiliye heshima, mheshimu.
8 Msidaiwe kitu na mtu yeyote, isipokuwa kupendana, kwa maana yeye ampendaye mwenzake, ameitimiza sheria.
-
9 Mheshimu Bwana kwa mali zako na
kwa malimbuko ya mazao yako yote;
10 ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika,
viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya.
-
24 Baada ya Yesu na wanafunzi wake kufika Kapernaumu, wakusanya kodi ya Hekalu wakamjia Petro na kumuuliza, “Je, Mwalimu wenu halipi kodi ya Hekalu?”
25 Petro akajibu, “Ndiyo, yeye hulipa.” Petro aliporudi nyumbani, Yesu akawa wa kwanza kulizungumzia, akamuuliza, “Unaonaje Simoni? Wafalme wa dunia hupokea ushuru na kodi kutoka kwa nani? Je, ni kutoka kwa watoto wao au kutoka kwa watu wengine?”
26 Petro akamjibu, “Kutoka kwa watu wengine.” Yesu akamwambia, “Kwa hiyo watoto wao wamesamehewa. 27 Lakini ili tusije tukawaudhi, nenda baharini ukatupe ndoana. Mchukue samaki wa kwanza utakayemvua. Fungua kinywa chake nawe utakuta humo fedha, ichukue ukalipe kodi yako na yangu.”
-
4 Usijitaabishe ili kuupata utajiri,
uwe na hekima kuonyesha kujizuia.
5 Kufumba na kufumbua utajiri hutoweka,
huwa kama umepata mabawa ghafula,
ukaruka na kutoweka angani kama tai.
-
19 Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu.
-
32 Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. 33 Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. 34 Wala hapakuwepo mtu yeyote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, 35 wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.
-
17 Yesu alipokuwa anaondoka, mtu mmoja akamkimbilia, akapiga magoti mbele yake, akamuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
18 Yesu akamwambia, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake. 19 Unazijua amri: ‘Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, usidanganye, waheshimu baba yako na mama yako.’ ”
20 Akamjibu, “Mwalimu, amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”
21 Yesu akamtazama na kumpenda, akamwambia, “Umepungukiwa na kitu kimoja. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho uwape maskini hizo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
22 Yule mtu aliposikia hayo, akasikitika sana. Akaondoka kwa huzuni kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
23 Yesu akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, “Itakuwa vigumu sana kwa wenye mali kuingia katika Ufalme wa Mungu!”
24 Wanafunzi wake wakashangazwa sana na maneno hayo. Lakini Yesu akawaambia tena, “Wanangu, tazama jinsi ilivyo vigumu kwa wale wanaotumainia mali kuingia katika Ufalme wa Mungu. 25 Ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”
-
28 “Ni nani miongoni mwenu ambaye kama anataka kujenga nyumba, hakai kwanza chini na kufanya makisio ya gharama aone kama ana fedha za kutosha kukamilisha? 29 La sivyo, akiisha kuweka msingi, naye akiwa hana uwezo wa kuikamilisha, wote waionao wataanza kumdhihaki, 30 wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga lakini hakuweza kukamilisha.’
-
28 Yeyote ategemeaye utajiri wake ataanguka,
bali mwenye haki atastawi kama jani bichi.
-
19 Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele,
bali yule afuataye mambo ya upuzi atakuwa na umaskini wa kumtosha.
20 Mtu mwaminifu atabarikiwa sana,
bali yeye atamaniye kupata utajiri kwa haraka
hataacha kuadhibiwa.
21 Kuonyesha upendeleo si vizuri,
hata hivyo mtu atafanya kosa kwa kipande cha mkate.
-
12 Yesu akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. 13 Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyangʼanyi.”
-
1 Heri kuchagua jina jema kuliko utajiri mwingi,
kuheshimiwa ni bora kuliko fedha au dhahabu.
2 Tajiri na maskini wanafanana kwa hili:
Bwana ni Muumba wao wote.
-
24 Yeye amwibiaye babaye au mamaye
na kusema, “Si kosa,”
yeye ni mwenzi wa yule aharibuye.
-
10 Leteni zaka kamili ghalani, ili kuwe na chakula katika nyumba yangu. Nijaribuni katika hili,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, “nanyi mwone kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni na kuwamwagieni baraka nyingi mpaka mkose nafasi ya kutosha.
-
1 “Angalieni msitende wema wenu mbele ya watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni.
2 “Hivyo mnapowapa wahitaji, msipige panda mbele yenu kama wafanyavyo wanafiki katika masinagogi na mitaani, ili wasifiwe na watu. Amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao. 3 Lakini ninyi mtoapo sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa kushoto usijue mkono wako wa kuume unachofanya, 4 ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo Baba yako wa mbinguni, yeye aonaye sirini atakupa thawabu kwa wazi.
-
18 Simoni alipoona kuwa watu wanapokea Roho Mtakatifu mitume walipoweka mikono juu yao, akataka kuwapa fedha 19 akisema, “Nipeni na mimi uwezo huu ili kila mtu nitakayeweka mikono yangu juu yake apate kupokea Roho Mtakatifu.”
20 Petro akamjibu, “Fedha yako na iangamie pamoja nawe, kwa sababu ulidhani unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha!
-
21 Waovu hukopa na hawalipi,
bali wenye haki hutoa kwa ukarimu.
22 Wale wanaobarikiwa na Bwana watairithi nchi,
bali wale anaowalaani watakatiliwa mbali.
-
4 Mikono mivivu hufanya mtu kuwa maskini
lakini mikono yenye bidii huleta utajiri.
-
4 Utajiri haufaidi kitu katika siku ya ghadhabu,
bali haki huokoa kutoka mautini.
-
23 Hili ndilo asemalo Bwana:
“Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake,
au mwenye nguvu ajisifu katika nguvu zake,
wala tajiri ajisifu katika utajiri wake,
24 lakini yeye ajisifuye, na ajisifu kwa sababu hili:
kwamba ananifahamu na kunijua mimi,
kwamba mimi ndimi Bwana, nitendaye wema,
hukumu na haki duniani,
kwa kuwa napendezwa na haya,”
asema Bwana.
-
9 Msichukue dhahabu, wala fedha, wala shaba kwenye vifuko vyenu.
-
32 “Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi Ufalme. 33 Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwizi hakaribii wala nondo haharibu. 34 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo moyo wako utakapokuwa pia.
-
35 Katika kila jambo nimewaonyesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii imetupasa kuwasaidia wadhaifu, mkikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe jinsi alivyosema, ‘Ni heri kutoa kuliko kupokea.’ ”
-
25 “Kama ukimkopesha mmojawapo wa watu wangu fedha ambaye ni mhitaji, usiwe kama mtu mkopesha fedha; usimtoze riba.
-
27 Mtu mwenye tamaa huletea jamaa yake taabu,
bali yeye achukiaye rushwa ataishi.
-
20 Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?”
21 Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”
Basi Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”
-
38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”
-
2 Siku ya kwanza ya kila juma, kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha, kulingana na mapato yake na fedha hizo aziweke akiba, ili nitakapokuja pasiwe na lazima ya kufanya mchango.
-
14 Zile mbegu zilizoanguka kwenye miiba ni mfano wa wale wanaosikia, lakini wanapoendelea husongwa na masumbufu ya maisha haya, utajiri na anasa, nao hawakui.
-
23 Kazi zote zinazofanywa kwa bidii huleta faida,
bali mazungumzo matupu huelekea umaskini tu.
-
5 Mipango ya mwenye bidii huelekeza kwenye faida,
kama vile kwa hakika pupa huelekeza kwenye umaskini.
-
22 Mtu mchoyo ana tamaa ya kupata utajiri,
naye hana habari kuwa umaskini unamngojea.
-
7 “Ninakuomba vitu viwili, Ee Bwana;
usininyime kabla sijafa:
8 Uutenge mbali nami udanganyifu na uongo;
usinipe umaskini wala utajiri,
bali unipe chakula cha kunitosha kila siku.
9 Nisije nikawa na vingi vya kuzidi nikakukana
na kusema, ‘Bwana ni nani?’
Au nisije nikawa maskini nikaiba,
nami nikaliaibisha jina la Mungu wangu.
-
6 Ndipo Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!”
-
5 Kwa habari ya mambo haya mjue hakika kwamba: Msherati, wala mtu mwovu, wala mwenye tamaa mbaya, mtu kama huyo ni mwabudu sanamu, kamwe hataurithi Ufalme wa Kristo na wa Mungu.
-
15 Msiupende ulimwengu wala mambo yaliyo ulimwenguni. Kama mtu yeyote akiupenda ulimwengu, upendo wa Baba haumo ndani yake. 16 Kwa maana kila kitu kilichomo ulimwenguni, yaani tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima, havitokani na Baba bali hutokana na ulimwengu. 17 Nao ulimwengu unapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu milele.
-
16 Kisha akawaambia mfano huu: “Shamba la mtu mmoja tajiri lilizaa sana. 17 Akawaza moyoni mwake, ‘Nifanye nini? Sina mahali pa kuhifadhi mavuno yangu.’
18 “Ndipo huyo tajiri akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu za nafaka na kujenga nyingine kubwa zaidi na huko nitayahifadhi mavuno yangu yote na vitu vyangu. 19 Nami nitaiambia nafsi yangu, “Nafsi, unavyo vitu vingi vizuri ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi. Pumzika; kula, unywe, ufurahi.” ’
20 “Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe! Usiku huu uhai wako unatakiwa. Sasa hivyo vitu ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani?’
21 “Hivyo ndivyo ilivyo kwa wale wanaojiwekea mali lakini hawajitajirishi kwa Mungu.”
-
35 “ ‘Ikiwa mmoja wa wazawa wa nchi yako amekuwa maskini, naye akashindwa kujitegemeza mwenyewe katikati yako, msaidie kama vile ambavyo ungelimsaidia mgeni au kama mkazi wa muda, ili aweze kuendelea kuishi katikati yako. 36 Usichukue riba wala faida yoyote kutoka kwake, bali utamwogopa Mungu wako, ili mzawa wa nchi yako aweze kuendelea kuishi katikati yako. 37 Usimkopeshe fedha ili alipe na riba, wala usimuuzie chakula kwa faida.
-
13 Usiwe na mawe ya kupimia ya aina mbili katika mkoba wako, moja zito na jingine jepesi. 14 Usiwe na vipimo viwili tofauti katika nyumba yako, kimoja kikubwa, kingine kidogo. 15 Ni lazima uwe na uzito na vipimo sahihi na vya haki, ili upate kuishi maisha marefu katika nchi anayokupa Bwana Mungu wako.
-
6 Ewe mvivu, mwendee mchwa;
zitafakari njia zake ukapate hekima!
7 Kwa maana yeye hana msimamizi,
wala mwangalizi, au mtawala,
8 lakini hujiwekea akiba wakati wa kiangazi
na hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.
-
22 Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi,
bali mali ya wenye dhambi imehifadhiwa
kwa ajili ya wenye haki.
-
27 Yeye ampaye maskini
hatapungukiwa na kitu chochote,
bali yeye awafumbiaye maskini macho
hupata laana nyingi.
-
36 Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake?
-
14 Askari nao wakamuuliza, “Je, nasi inatupasa tufanye nini?”
Akawaambia, “Msimdhulumu mtu wala msimshtaki mtu kwa uongo, bali mridhike na mishahara yenu.”
-
32 “Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwapenda wale wawapendao. 33 Tena mkiwatendea mema wale tu wanaowatendea ninyi mema, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ hufanya vivyo hivyo. 34 Tena mnapowakopesha wale tu mnaotegemea wawalipe, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwakopesha ‘wenye dhambi’ wenzao wakitarajia kulipwa mali yao yote. 35 Lakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Sana, kwa sababu yeye ni mwema kwa watu wasio na shukrani na kwa wale waovu.
-
12 Kisha Yesu akamwambia yule aliyewaalika, “Uandaapo karamu ya chakula cha mchana au cha jioni, usialike rafiki zako au ndugu zako au jamaa zako au majirani zako walio matajiri tu. Ukifanya hivyo, wao nao wanaweza kukualika kwao, nawe ukawa umelipwa kile ulichofanya na kupata thawabu yako. 13 Bali ufanyapo karamu, waalike maskini, vilema na vipofu, 14 nawe utabarikiwa kwa sababu hawa hawana uwezo wa kukulipa. Mungu atakulipa wakati wa ufufuo wa wenye haki.”
-
6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.
-
24 Kuna mtu atoaye kwa ukarimu, hata hivyo hupata zaidi,
mwingine huzuia, lakini huwa maskini.
25 Mtu mkarimu atastawi;
yeye awaburudishaye wengine
ataburudishwa mwenyewe.
26 Watu humlaani mtu awanyimae watu nafaka,
bali baraka itamkalia kichwani kama taji
yeye aliye radhi kuiuza.
-
22 Bwana anachukia sana midomo idanganyayo,
bali hufurahia watu ambao ni wa kweli.
-
16 Ni bora kiasi gani kupata hekima kuliko dhahabu,
kuchagua ufahamu kuliko fedha!
-
9 Mtu mkarimu yeye mwenyewe atabarikiwa
kwa kuwa hushiriki chakula chake na maskini.
-
47 “Yule mtumishi anayefahamu vyema mapenzi ya bwana wake na asijiandae wala kufanya kama apendavyo bwana wake, atapigwa kwa mapigo mengi. 48 Lakini yeyote ambaye hakujua naye akafanya yale yastahiliyo kupigwa, atapigwa kidogo. Yeyote aliyepewa vitu vingi, atadaiwa vingi; na yeyote aliyekabidhiwa vingi, kwake vitatakiwa vingi.
-
17 Wazee wa kanisa wanaoongoza shughuli za kanisa vizuri wanastahili heshima mara mbili, hasa wale ambao kazi yao ni kuhubiri na kufundisha. 18 Kwa maana Maandiko husema, “Usimfunge maksai kinywa apurapo nafaka,” tena, “Mfanyakazi anastahili mshahara wake.”
Shows Read in context, Share and Copy.