66 Bible Verses About Women
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
10 Mke mwenye sifa nzuri, ni nani awezaye kumpata?
Yeye ni wa thamani sana kuliko marijani.
11 Mume wake anamwamini kikamilifu
wala hakosi kitu chochote cha thamani.
12 Humtendea mumewe mema, wala si mabaya,
siku zote za maisha yake.
13 Huchagua sufu na kitani
naye hufanya kazi kwa mikono yenye bidii.
14 Yeye ni kama meli za biashara
akileta chakula chake kutoka mbali.
15 Yeye huamka kungali bado giza
huwapa jamaa yake chakula
na mafungu kwa watumishi wake wa kike.
16 Huangalia shamba na kulinunua,
kutokana na mapato yake hupanda shamba la mizabibu.
17 Hufanya kazi zake kwa nguvu,
mikono yake ina nguvu kwa ajili ya kazi zake.
18 Huona kwamba biashara yake ina faida,
wala taa yake haizimiki usiku.
19 Huweka mikono yake kwenye pia,
navyo vidole vyake hushikilia kijiti chenye uzi.
20 Huwanyooshea maskini mikono yake
na kuwakunjulia wahitaji vitanga vyake.
21 Theluji ishukapo, hana hofu kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake,
kwa maana wote wamevikwa nguo za kutia joto.
22 Hutengeneza mazulia ya urembo ya kufunika kitanda chake,
yeye huvaa kitani safi na urujuani.
23 Mume wake anaheshimiwa kwenye lango la mji,
aketipo miongoni mwa wazee wa nchi.
24 Hutengeneza mavazi ya kitani na kuyauza,
naye huwauzia wafanyabiashara mishipi.
25 Amevikwa nguvu na heshima,
anaweza kucheka bila kuwa na hofu kwa siku zijazo.
26 Huzungumza kwa hekima
na mafundisho ya kuaminika yapo ulimini mwake.
27 Huangalia mambo ya nyumbani mwake
wala hali chakula cha uvivu.
28 Watoto wake huamka na kumwita aliyebarikiwa,
mumewe pia humsifu, akisema:
29 “Wanawake wengi hufanya vitu vyenye sifa nzuri,
lakini wewe umewapita wote.”
30 Kujipamba ili kuvutia ni udanganyifu na uzuri unapita upesi,
bali mwanamke anayemcha Bwana atasifiwa.
31 Mpe thawabu anayostahili,
nazo kazi zake na zimletee sifa kwenye lango la mji.
-
8 Nataka kila mahali wanaume wasali wakiinua mikono mitakatifu pasipo hasira wala kugombana.
9 Vivyo hivyo nataka wanawake wajipambe kwa adabu na kwa heshima katika mavazi yanayostahili, si kwa kusuka nywele, kuvalia dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa, 10 bali kwa matendo mazuri kama iwapasavyo wanawake wanaokiri kuwa wanamcha Mungu.
11 Mwanamke na ajifunze kwa utulivu na kwa utiifu wote. 12 Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha au kuwa na mamlaka juu ya mwanaume. Mwanamke inampasa kukaa kimya. 13 Kwa maana Adamu aliumbwa kwanza, kisha Eva. 14 Wala si Adamu aliyedanganywa, bali ni mwanamke aliyedanganywa akawa mkosaji. 15 Lakini mwanamke ataokolewa kwa kuzaa kwake, kama wakiendelea kudumu katika imani, upendo na utakatifu, pamoja na kuwa na kiasi.
-
1 Kadhalika enyi wake, watiini waume zenu, ili kama kunao wasioamini lile neno, wapate kuvutwa na mwenendo wa wake zao pasipo neno, 2 kwa kuuona utakatifu na uchaji wa Mungu katika maisha yenu. 3 Kujipamba kwenu kusiwe kwa nje tu, kama vile kusuka nywele, kuvalia vitu vilivyofanyizwa kwa dhahabu na kwa mavazi. 4 Badala yake, kujipamba kwenu kuwe katika utu wenu wa moyoni, yaani uzuri usioharibika wa roho ya upole na utulivu, ambayo ni ya thamani sana machoni pa Mungu. 5 Kwa kuwa hivi ndivyo walivyokuwa wakijipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu. Wao walikuwa ni watiifu kwa waume zao, 6 kama Sara alivyomtii mumewe Abrahamu, hata akamwita bwana. Ninyi ni watoto wa Sara kama mkitenda yaliyo mema, bila kuogopa jambo lolote.
7 Vivyo hivyo ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, nanyi wapeni heshima mkitambua ya kuwa wao ni wenzi walio dhaifu, na kama warithi pamoja nanyi wa kipawa cha neema cha uzima, ili kusiwepo na chochote cha kuzuia maombi yenu.
-
21 Nyenyekeaneni ninyi kwa ninyi kwa heshima kwa ajili ya Kristo.
22 Ninyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana. 23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe kama vile Kristo alivyo kichwa cha Kanisa, ambalo ni mwili wake, naye Kristo ni Mwokozi wake. 24 Basi, kama vile Kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo na wake nao imewapasa kuwatii waume zao kwa kila jambo.
25 Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Kristo alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake
-
3 Napenda mfahamu kwamba kichwa cha kila mwanaume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanaume, nacho kichwa cha Kristo ni Mungu. 4 Kila mwanaume anayeomba au kutoa unabii akiwa amefunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake. 5 Naye kila mwanamke anayeomba au kutoa unabii pasipo kufunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake, kwani ni sawa na yeye aliyenyoa nywele. 6 Kama mwanamke hatajifunika kichwa chake, basi inampasa kunyoa nywele zake. Lakini kama ni aibu kwa mwanamke kukata au kunyoa nywele zake, basi afunike kichwa chake. 7 Haimpasi mwanaume kufunika kichwa chake kwa kuwa yeye ni mfano wa Mungu na utukufu wa Mungu, lakini mwanamke ni utukufu wa mwanaume. 8 Kwa maana mwanaume hakutoka kwa mwanamke, bali mwanamke alitoka kwa mwanaume. 9 Wala mwanaume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanaume. 10 Kwa sababu hii na kwa sababu ya malaika, inampasa mwanamke awe na ishara ya mamlaka juu yake.
11 Lakini katika Bwana, mwanamke hajitegemei pasipo mwanaume na mwanaume hajitegemei pasipo mwanamke. 12 Kama vile mwanamke alivyoumbwa kutoka kwa mwanaume, vivyo hivyo mwanaume huzaliwa na mwanamke. Lakini vitu vyote vyatoka kwa Mungu.
-
1 Inakupasa kufundisha itikadi sahihi. 2 Wafundishe wazee kuwa na kiasi, wastahivu, wenye busara na wanyofu katika imani, upendo na saburi.
3 Vivyo hivyo, wafundishe wanawake wazee kuwa na mwenendo wa utakatifu, wala wasiwe wasingiziaji au walevi, bali wafundishe yale yaliyo mema, 4 ili waweze kuwafundisha wanawake vijana kuwa na kiasi, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao, 5 wawe waaminifu, watakatifu, wakitunza vyema nyumba zao, wema, watiifu kwa waume zao, ili mtu yeyote asije akalikufuru neno la Mungu.
-
18 Bwana Mungu akasema, “Si vyema huyu mtu awe peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.”
19 Basi Bwana Mungu alikuwa amefanyiza kutoka ardhi wanyama wote wa porini na ndege wote wa angani. Akawaleta kwa huyu mtu aone atawaitaje, nalo jina lolote alilokiita kila kiumbe hai, likawa ndilo jina lake. 20 Hivyo Adamu akawapa majina wanyama wote wa kufugwa, ndege wa angani, na wanyama wote wa porini.
Lakini kwa Adamu hakupatikana msaidizi wa kumfaa. 21 Hivyo Bwana Mungu akamfanya Adamu kulala usingizi mzito, naye alipokuwa amelala akachukua moja ya mbavu zake, akapafunika mahali pale kwa nyama. 22 Kisha Bwana Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwenye ule ubavu aliouchukua kutoka kwa huyo mwanaume, akamleta huyo mwanamke kwa huyo mwanaume.
23 Huyo mwanaume akasema,
“Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu
na nyama ya nyama yangu,
ataitwa ‘mwanamke,’
kwa kuwa alitolewa katika mwanaume.”
24 Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.
25 Adamu na mkewe wote wawili walikuwa uchi, wala hawakuona aibu.
-
36 Tena alikuwako Hekaluni nabii mmoja mwanamke, jina lake Ana binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa mzee sana; naye alikuwa ameolewa na kuishi na mume kwa miaka saba tu, kisha mumewe akafa. 37 Hivyo alikuwa mjane na umri wake ulikuwa miaka themanini na minne. Yeye hakuondoka humo Hekaluni usiku wala mchana, bali alikuwa akimwabudu Mungu, akifunga na kuomba. 38 Wakati huo huo, Ana alikuja akaanza kusifu, akimshukuru Mungu na kusema habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wakitarajia ukombozi wa Yerusalemu.
-
34 wanawake wanapaswa kuwa kimya kanisani. Hawaruhusiwi kusema, bali wanyenyekee kama sheria isemavyo. 35 Kama wakitaka kuuliza kuhusu jambo lolote, wawaulize waume zao nyumbani. Kwa maana ni aibu kwa mwanamke kuzungumza kanisani.
-
13 Siku ya Sabato tukaenda nje ya lango la mji kando ya mto, mahali ambapo tulitarajia tungepata mahali pa kufanyia maombi. Tukaketi, tukaanza kuongea na baadhi ya wanawake waliokuwa wamekusanyika huko. 14 Mmoja wa wale wanawake waliotusikiliza aliitwa Lidia, mfanyabiashara wa nguo za zambarau, mwenyeji wa mji wa Thiatira, aliyekuwa mcha Mungu. Bwana akaufungua moyo wake akaupokea ujumbe wa Paulo. 15 Basi alipokwisha kubatizwa yeye na watu wa nyumba yake, alitukaribisha nyumbani kwake akisema, “Kama mmeona kweli mimi nimemwamini Bwana, karibuni mkae nyumbani mwangu.” Naye akatushawishi.
-
1 Napenda kumtambulisha kwenu dada yetu Foibe, mtumishi katika kanisa la Kenkrea. 2 Naomba mpokeeni katika Bwana ipasavyo watakatifu na kumpa msaada wowote atakaohitaji kutoka kwenu, kwa maana yeye amekuwa msaada kwa watu wengi, mimi nikiwa miongoni mwao.
3 Wasalimuni Prisila na Akila, watumishi wenzangu katika Kristo Yesu. 4 Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu; wala si mimi tu ninayewashukuru bali pia makanisa yote ya watu wa Mataifa.
-
23 Kabla imani hii haijaja tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ile imani ifunuliwe. 24 Hivyo, sheria ilikuwa kiongozi kutufikisha kwa Kristo, ili tupate kuhesabiwa haki kwa imani. 25 Lakini sasa kwa kuwa ile imani imekuja, hatusimamiwi tena na sheria.
26 Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani. 27 Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo. 28 Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu. 29 Nanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.
-
2 Nawasihi Euodia na Sintike wawe na nia moja katika Bwana. 3 Naam, nakusihi wewe pia, mwenzangu mwaminifu, uwasaidie hawa wanawake, kwa sababu walijitaabisha katika kazi ya Injili pamoja nami bega kwa bega, wakiwa pamoja na Klementi na watendakazi wenzangu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima.
-
20 Kisha Miriamu yule nabii mke, ndugu yake Aroni, akachukua matari mkononi mwake na wanawake wote wakamfuata na matari yao wakicheza. 21 Miriamu akawaimbia:
“Mwimbieni Bwana,
kwa maana ametukuka sana.
Farasi na mpanda farasi
amewatosa baharini.”
-
55 Walikuwako wanawake huko wakiangalia kwa mbali. Hawa walikuwa wamemfuata Yesu tangu Galilaya ili kushughulikia mahitaji yake. 56 Miongoni mwao walikuwepo Maria Magdalene, na Maria mama yao Yakobo na Yosefu, na mama yao wana wa Zebedayo.
-
9 Mjane yeyote asiwekwe kwenye orodha ya wajane isipokuwa awe ametimiza umri wa miaka sitini, na ambaye alikuwa mke wa mume mmoja, 10 awe ameshuhudiwa kwa matendo yake mema, aliyewalea watoto wake vizuri, aliye mkarimu, aliyewanawisha watakatifu miguu, aliyewasaidia wenye shida na aliyejitolea kwa ajili ya matendo mema ya kila namna.
11 Lakini kwa habari za wajane vijana usiwaweke kwenye orodha hiyo, maana tamaa zao za kimaumbile zikizidi kule kujitoa kwao kwa Kristo, watataka kuolewa tena. 12 Nao kwa njia hiyo watajiletea hukumu kwa kukiuka ahadi yao ya kwanza. 13 Zaidi ya hayo, wajane kama hao huwa na tabia ya uvivu wakizurura nyumba kwa nyumba, wala hawawi wavivu tu, bali pia huwa wasengenyaji, wajiingizao katika mambo yasiyowahusu na kusema mambo yasiyowapasa kusema. 14 Hivyo nawashauri wajane vijana waolewe, wazae watoto na wasimamie nyumba zao, wasije wakampa adui nafasi ya kutushutumu. 15 Kwa maana kwa kweli wajane wengine wamepotoka ili kumfuata Shetani.
16 Lakini kama mwanamke yeyote aaminiye ana wajane katika jamaa yake, inampasa awasaidie wala si kuwaacha wakililemea kanisa, ili kanisa liweze kuwasaidia wale ambao ni wajane kweli kweli.
-
38 Ikawa Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakienda Yerusalemu, akaingia kwenye kijiji kimoja ambapo mwanamke mmoja aliyeitwa Martha alimkaribisha nyumbani kwake. 39 Martha alikuwa na mdogo wake aliyeitwa Maria, ambaye aliketi chini miguuni mwa Bwana akisikiliza yale aliyokuwa akisema. 40 Lakini Martha alikuwa akihangaika na maandalizi yote yaliyokuwa yafanyike. Martha akaja kwa Yesu na kumuuliza, “Bwana, hujali kwamba ndugu yangu ameniachia kazi zote mwenyewe? Basi mwambie anisaidie.”
41 Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, mbona unasumbuka na kuhangaika na mengi? 42 Lakini kunahitajika kitu kimoja tu. Maria amechagua kile kilicho bora, wala hakuna mtu atakayemwondolea.”
-
3 Yesu alikuwa Bethania nyumbani kwa Simoni aliyekuwa na ukoma. Wakati alipokuwa ameketi mezani akila chakula cha jioni, mwanamke mmoja aliingia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa. Akaivunja hiyo chupa, akamiminia hayo manukato kichwani mwa Yesu.
4 Baadhi ya watu waliokuwepo pale walikuwa wakisemezana wao kwa wao, “Upotevu huu wote ni wa nini? 5 Mafuta haya yangeweza kuuzwa kwa zaidi ya dinari 300, na fedha hizo wakapewa maskini.” Wakamkemea vikali huyo mwanamke.
6 Lakini Yesu akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Mwacheni! Yeye amenitendea jambo zuri sana. 7 Maskini mtakuwa nao siku zote na mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaotaka. Lakini mimi hamtakuwa nami siku zote. 8 Huyu mwanamke amenitendea lile aliloweza. Ameumiminia mwili wangu manukato ili kuniandaa kwa maziko yangu. 9 Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.”
-
36 Huko Yafa palikuwa na mwanafunzi jina lake Tabitha (ambalo kwa Kiyunani ni Dorkasi). Huyu alikuwa mkarimu sana, akitenda mema na kuwasaidia maskini. 37 Wakati huo akaugua, akafa na wakiisha kuuosha mwili wake wakauweka katika chumba cha ghorofani. 38 Kwa kuwa Yafa hapakuwa mbali sana na Lida, wanafunzi waliposikia kwamba Petro yuko huko waliwatuma watu wawili kwake ili kumwomba, “Tafadhali njoo huku pasipo kukawia.”
39 Kwa hiyo Petro akainuka akaenda nao, naye alipowasili, wakampeleka hadi kwenye chumba cha ghorofani alipokuwa amelazwa. Wajane wengi walisimama karibu naye wakilia na kuonyesha majoho na nguo nyingine ambazo Dorkasi alikuwa amewashonea alipokuwa pamoja nao.
40 Petro akawatoa wote nje ya kile chumba, kisha akapiga magoti akaomba, akaugeukia ule mwili akasema, “Tabitha, inuka.” Akafumbua macho yake na alipomwona Petro, akaketi. 41 Petro akamshika mkono akamwinua, ndipo akawaita wale watakatifu na wajane akamkabidhi kwao akiwa hai. 42 Habari hizi zikajulikana sehemu zote za Yafa na watu wengi wakamwamini Bwana.
-
16 Kwa mwanamke akasema,
“Nitakuzidishia sana utungu wakati wa kuzaa kwako;
kwa utungu utazaa watoto.
Tamaa yako itakuwa kwa mumeo
naye atakutawala.”
-
4 Mke mwenye tabia nzuri ni taji ya mumewe,
bali aaibishaye ni kama uozo
katika mifupa ya mumewe.
-
21 Yesu aliondoka mahali pale, akaenda sehemu za Tiro na Sidoni. 22 Mwanamke mmoja Mkanaani aliyeishi sehemu jirani na hizo akaja kwake akilia, akasema, “Nihurumie, Ee Bwana, Mwana wa Daudi! Binti yangu amepagawa na pepo mchafu, na anateseka sana.”
23 Lakini Yesu hakumjibu neno. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea na kumsihi sana, wakisema, “Mwambie aende zake, kwa maana anaendelea kutupigia kelele.”
24 Yesu akajibu, “Nimetumwa tu kwa ajili ya kondoo wa Israeli waliopotea.”
25 Lakini yule mwanamke akaja, akapiga magoti mbele ya Yesu, akasema, “Bwana, nisaidie!”
26 Yesu akajibu, “Si haki kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”
27 Yule mwanamke akajibu, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka kwenye meza za bwana zao.”
28 Ndipo Yesu akamwambia, “Mwanamke, imani yako ni kubwa! Iwe kwako kama unavyotaka.” Naye binti yake akapona tangu saa ile.
-
37 Naye mwanamke mmoja kwenye ule mji, ambaye alikuwa mwenye dhambi, alipojua kwamba Yesu alikuwa akila chakula nyumbani kwa yule Farisayo, akaleta chupa ya marhamu yenye manukato. 38 Yule mwanamke akasimama nyuma ya miguu ya Yesu akilia. Akailowanisha miguu yake kwa machozi yake, kisha akaifuta kwa nywele zake, akaibusu na kuimiminia manukato.
-
18 Ninyi wake, watiini waume zenu, kama inavyostahili katika Bwana.
-
8 Vivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali. 9 Inawapasa kushikamana sana na ile siri ya imani kwa dhamiri safi. 10 Ni lazima wapimwe kwanza; kisha kama hakuna neno dhidi yao, basi na waruhusiwe kuhudumu kama mashemasi.
11 Vivyo hivyo, wake zao wawe wanawake wanaostahili heshima, wasio wasingiziaji, bali wawe na kiasi na waaminifu katika kila jambo.
12 Shemasi awe mume wa mke mmoja na inampasa aweze kusimamia watoto wake na watu wa nyumbani mwake vyema. 13 Wale ambao wamehudumu vyema katika huduma ya ushemasi hujipatia msimamo bora na ujasiri mkubwa katika imani yao ndani ya Kristo Yesu.
-
18 Lakini Samweli alikuwa akihudumu mbele za Bwana, kijana akivaa kisibau cha kitani. 19 Kila mwaka mama yake alimshonea joho dogo na kumchukulia wakati alipokwea pamoja na mumewe kutoa dhabihu ya mwaka. 20 Eli alikuwa akiwabariki Elikana na mkewe, akisema, “Bwana na akupe watoto kwa mwanamke huyu ili kuchukua nafasi ya yule aliyekuwa amemwomba na akamtoa kwa Bwana.” Kisha wakawa wanakwenda nyumbani. 21 Bwana akawa mwenye neema kwa Hana, naye akapata mimba akazaa wana watatu na binti wawili. Wakati huo, kijana Samweli akaendelea kukua mbele za Bwana.
-
1 Siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alikwenda Bethania mahali ambako Lazaro aliyekuwa amefufuliwa na Yesu alikuwa anaishi. 2 Wakaandaa karamu kwa heshima ya Yesu. Martha akawahudumia wakati Lazaro alikuwa miongoni mwa waliokaa mezani pamoja na Yesu. 3 Kisha Maria akachukua chupa ya painti moja yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa, akayamimina miguuni mwa Yesu na kuifuta kwa nywele zake. Nyumba nzima ikajaa harufu nzuri ya manukato.
4 Ndipo Yuda Iskariote mwana wa Simoni, mmoja wa wale wanafunzi ambaye ndiye angemsaliti Yesu, akasema, 5 “Kwa nini manukato haya hayakuuzwa kwa dinari 300 na fedha hizo wakapewa maskini?” 6 Yuda alisema hivi si kwa kuwa aliwajali maskini, bali kwa kuwa alikuwa mwizi, kwani ndiye alikuwa akitunza mfuko wa fedha akawa anaiba kile kilichowekwa humo.
7 Yesu akasema, “Mwacheni. Aliyanunua manukato hayo ili ayaweke kwa ajili ya siku ya maziko yangu. 8 Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.”
-
1 Alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma, kulipokuwa kungali giza bado, Maria Magdalene alikwenda kaburini na kukuta lile jiwe limeondolewa penye ingilio. 2 Hivyo akaja akikimbia kwa Simoni Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, na kusema, “Wamemwondoa Bwana kaburini, na hatujui walikomweka!”
-
17 “ ‘Katika siku za mwisho, asema Mungu,
nitamimina Roho wangu
juu ya wote wenye mwili.
Wana wenu na binti zenu watatabiri,
vijana wenu wataona maono,
na wazee wenu wataota ndoto.
18 Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake,
katika siku zile nitamimina Roho wangu,
nao watatabiri.
19 Nami nitaonyesha maajabu juu mbinguni,
na ishara chini duniani:
damu, moto, na mawimbi ya moshi.
20 Jua litakuwa giza
na mwezi utakuwa mwekundu kama damu,
kabla ya kuja siku ile kuu ya Bwana
iliyo tukufu.
21 Na kila mtu atakayeliitia
jina la Bwana, ataokolewa.’
-
15 Ikawa kabla hajamaliza kuomba, Rebeka akatokea akiwa na mtungi begani mwake. Alikuwa binti wa Bethueli. Bethueli alikuwa mwana wa Milka aliyekuwa mke wa Nahori ndugu wa Abrahamu. 16 Huyu msichana alikuwa mzuri sana wa sura, bikira, ambaye hakuna mtu aliyekuwa amekutana naye kimwili. Aliteremka kisimani, akajaza mtungi wake akapanda juu.
17 Ndipo yule mtumishi akaharakisha kukutana naye akamwambia, “Tafadhali nipe maji kidogo katika mtungi wako.”
18 Yule msichana akasema, “Kunywa, bwana wangu.” Akashusha kwa haraka mtungi mkononi mwake na akampa, akanywa.
19 Baada ya kumpa yule mtumishi yale maji, akamwambia, “Nitateka maji kwa ajili ya ngamia zako pia mpaka wote watosheke.” 20 Akafanya haraka kumimina maji kwenye birika ya kunyweshea wanyama, akakimbia kisimani kuteka maji mengine na akateka ya kuwatosha ngamia wake wote.
-
5 Haimpasi mwanamke kuvaa nguo za kiume wala mwanaume kuvaa nguo za kike, kwa maana Bwana Mungu wenu anachukia yeyote ambaye hufanya hivi.
-
8 Siku moja Elisha akaenda Shunemu. Huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo, ambaye alimsisitiza Elisha aje kula chakula. Kwa hiyo kila mara alipitia pale, akaingia humo ili ale. 9 Akamwambia mumewe, “Ninajua kwamba huyu mtu ambaye anakuja kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu. 10 Tutengeneze chumba kidogo juu darini na tuweke ndani yake kitanda na meza, kiti na taa kwa ajili yake. Kisha anaweza kukaa humo kila mara akija kwetu.”
-
20 Wakati huo huo, mwanamke mmoja, ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, akaja nyuma ya Yesu, akagusa upindo wa vazi lake, 21 kwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikigusa tu vazi lake, nitaponywa.”
22 Yesu akageuka, naye alipomwona akamwambia, “Binti, jipe moyo mkuu, imani yako imekuponya.” Naye yule mwanamke akapona kuanzia saa ile ile.
-
47 Maria Magdalene na Maria mamaye Yose walipaona mahali pale alipolazwa.
-
15 Naomi akamwambia, “Tazama, mwenzako anarejea kwa watu wake na kwa miungu yake. Rudi pamoja naye.”
16 Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakokwenda nami nitakwenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. 17 Pale utakapofia nami nitafia hapo, na papo hapo nitazikwa. Bwana na aniadhibu vikali, kama kitu kingine chochote kitanitenga nawe isipokuwa kifo.” 18 Naomi alipotambua kwamba Ruthu amenuia kufuatana naye, hakuendelea kumsihi tena.
-
1 Mwanangu, sikiliza kwa makini hekima yangu,
sikiliza vizuri maneno yangu ya busara,
2 ili uweze kutunza busara
na midomo yako ihifadhi maarifa.
3 Kwa maana midomo ya mwanamke kahaba
hudondoza asali,
na maneno ya kinywa chake
ni laini kuliko mafuta;
4 lakini mwisho wake ni mchungu kama nyongo,
mkali kama upanga ukatao kuwili.
5 Miguu yake hushuka kuelekea kwenye kifo;
hatua zake huelekea moja kwa moja kaburini.
6 Yeye hafikiri juu ya njia ya uzima;
njia zake zimepotoka, lakini yeye hajui.
-
1 Mwanamke mwenye hekima huijenga nyumba yake,
bali mpumbavu huibomoa nyumba yake
kwa mikono yake mwenyewe.
-
22 Apataye mke apata kitu chema
naye ajipatia kibali kwa Bwana.
-
27 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Usizini.’ 28 Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. 29 Jicho lako la kuume likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima ukatupwa jehanamu. 30 Kama mkono wako wa kuume ukikusababisha kutenda dhambi, ukate, uutupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe jehanamu.
31 “Pia ilinenwa kwamba, ‘Mtu yeyote amwachaye mkewe sharti ampe hati ya talaka.’ 32 Lakini mimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa kosa la uasherati, amfanya mkewe kuwa mzinzi. Na yeyote amwoaye yule mwanamke aliyeachwa, anazini.
-
41 Kisha Yesu akaketi mkabala na sehemu ambapo sadaka zilikuwa zinawekwa na kuangalia umati wa watu wakiweka fedha zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. Matajiri wengi wakaweka kiasi kikubwa cha fedha. 42 Lakini mjane mmoja maskini akaja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba zenye thamani ya senti mbili.
43 Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka katika sanduku la hazina zaidi ya watu wengine wote. 44 Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali zao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake, akaweka kila kitu alichokuwa nacho, hata kile alichohitaji ili kuishi.”
-
41 Naye Elizabeti aliposikia salamu ya Maria, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akaruka. Elizabeti akajazwa na Roho Mtakatifu, 42 akapaza sauti kwa nguvu akasema, “Umebarikiwa wewe miongoni mwa wanawake, naye mtoto utakayemzaa amebarikiwa. 43 Lakini ni kwa nini mimi nimepata upendeleo kiasi hiki, hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? 44 Mara tu niliposikia sauti ya salamu yako, mtoto aliyeko tumboni mwangu aliruka kwa furaha. 45 Amebarikiwa yeye aliyeamini kwamba lile Bwana alilomwambia litatimizwa.”
-
25 Wakati huo huo karibu na msalaba wa Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada wa mamaye, na Maria mke wa Klopa, na Maria Magdalene. 26 Yesu alipomwona mama yake mahali pale pamoja na yule mwanafunzi aliyempenda wamesimama karibu, akamwambia mama yake, “Mwanamke, huyo hapo ndiye mwanao,” 27 kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Nawe huyo hapo ndiye mama yako.” Tangu wakati huo yule mwanafunzi akamchukua mama yake Yesu nyumbani kwake.
-
12 Waheshimu baba yako na mama yako, ili upate kuishi siku nyingi katika nchi anayokupa Bwana Mungu wako.
-
18 Mtoto akakua, naye siku moja akamwendea baba yake, ambaye alikuwa pamoja na wavunaji. 19 Akamwambia baba yake, “Kichwa changu! Kichwa changu!”
Baba yake akamwambia mtumishi, “Mchukue umpeleke kwa mama yake.” 20 Baada ya mtumishi kumbeba na kumpeleka kwa mama yake, mtoto akaketi mapajani mwa mama yake mpaka adhuhuri, kisha akafa. 21 Mama akampandisha na kumlaza juu ya kitanda cha yule mtu wa Mungu, kisha akafunga mlango, akatoka nje.
22 Akamwita mume wake na kusema, “Tafadhali mtume mmoja miongoni mwa mtumishi pamoja na punda ili niweze kwenda kwa mtu wa Mungu haraka na kurudi.”
-
15 Kisha Esta alituma jibu hili kwa Mordekai: 16 “Nenda, kusanya pamoja Wayahudi wote walioko Shushani, nanyi mfunge kwa ajili yangu. Msile wala kunywa kwa siku tatu, usiku na mchana. Mimi na wajakazi wangu tutafunga kama mnavyofanya. Baada ya kufanyika hili, nitakwenda kwa mfalme, hata ingawa ni kinyume cha sheria. Ikiwa ni kuangamia na niangamie.”
-
16 Mwanamke mwenye moyo wa huruma hupata heshima,
bali wanaume wakorofi hupata mali tu.
-
18 Katika siku ile Bwana atawanyangʼanya uzuri wao: bangili, tepe za kichwani, mikufu yenye alama za mwezi mwandamo, 19 vipuli, vikuku, shela, 20 vilemba, mikufu ya vifundo vya miguu, mshipi, chupa za manukato na hirizi, 21 pete zenye muhuri, pete za puani, 22 majoho mazuri, mitandio, mavazi, kifuko cha kutilia fedha, 23 vioo, mavazi ya kitani, taji na shali.
24 Badala ya harufu ya manukato kutakuwa na uvundo;
badala ya mishipi, ni kamba;
badala ya nywele zilizotengenezwa vizuri, ni upara;
badala ya mavazi mazuri, ni nguo za magunia;
badala ya uzuri, ni alama ya aibu kwa chuma cha moto.
-
28 “Nanyi kwa nini mnajitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi. 29 Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua.
-
12 Alipokaribia lango la mji, alikutana na watu waliokuwa wamebeba maiti wakitoka nje ya mji. Huyu aliyekufa alikuwa mwana pekee wa mwanamke mjane. Umati mkubwa wa watu wa mji ule ulikuwa pamoja na huyo mwanamke. 13 Bwana Yesu alipomwona yule mjane, moyo wake ulimhurumia, akamwambia, “Usilie.”
14 Kisha akasogea mbele akaligusa lile jeneza na wale waliokuwa wamelibeba wakasimama kimya. Akasema, “Kijana, nakuambia inuka.” 15 Yule aliyekuwa amekufa akaketi akaanza kuongea, naye Yesu akamkabidhi kwa mama yake.
-
10 Basi Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo siku ya Sabato. 11 Wakati huo huo akaja mwanamke mmoja aliyekuwa na pepo mchafu, naye alikuwa amepinda mgongo kwa muda wa miaka kumi na minane, wala alikuwa hawezi kunyooka wima. 12 Yesu alipomwona, akamwita, akamwambia, “Mwanamke, uwe huru, umepona ugonjwa wako.” 13 Yesu alipomwekea mikono yake, mara akasimama wima akaanza kumtukuza Mungu.
14 Lakini kiongozi wa sinagogi akakasirika kwa sababu Yesu alikuwa ameponya mtu siku ya Sabato. Akaambia ule umati wa watu, “Kuna siku sita ambazo watu wanapaswa kufanya kazi. Katika siku hizo, njooni mponywe, lakini si katika siku ya Sabato.”
15 Lakini Bwana akamjibu, “Enyi wanafiki! Je, kila mmoja wenu hamfungulii ngʼombe wake au punda wake kutoka zizini akampeleka kumnywesha maji siku ya Sabato? 16 Je, huyu mwanamke, ambaye ni binti wa Abrahamu, aliyeteswa na Shetani akiwa amemfunga kwa miaka yote hii kumi na minane, hakustahili kufunguliwa kutoka kifungo hicho siku ya Sabato?”
17 Aliposema haya, wapinzani wake wakaaibika, lakini watu wakafurahi kwa ajili ya mambo ya ajabu aliyoyafanya.
-
Mateso Na Kuenea Kwa Injili
1 Basi ikawa katika siku hizo, wakati idadi ya wanafunzi ilipokuwa ikiongezeka sana, palitokea manungʼuniko kati ya Wayahudi wa Kiyunani, dhidi ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahaulika katika mgawanyo wa chakula wa kila siku.
-
2 Kwa mfano, mwanamke aliyeolewa amefungwa kwa mumewe wakati akiwa hai, lakini yule mume akifa, yule mwanamke amefunguliwa kutoka sheria ya ndoa. 3 Hivyo basi, kama huyo mwanamke ataolewa na mwanaume mwingine wakati mumewe akiwa bado yuko hai, ataitwa mzinzi. Lakini kama mumewe akifa, mwanamke huyo hafungwi tena na sheria ya ndoa, naye akiolewa na mtu mwingine haitwi mzinzi.
-
10 Kwa wale waliooana nawapa amri (si mimi ila ni Bwana): Mke asitengane na mumewe. 11 Lakini akitengana, ni lazima akae bila kuolewa, ama sivyo apatane tena na mumewe. Wala mume asimpe mkewe talaka.
12 Lakini kwa wengine nasema (si Bwana ila ni mimi): Kama ndugu ana mke asiyeamini, naye huyo mke anakubali kuishi pamoja naye, basi asimwache. 13 Naye mwanamke aaminiye kama ameolewa na mwanaume asiyeamini na huyo mume anakubali kuishi naye, basi huyo mwanamke asimwache. 14 Kwa maana huyo mume asiyeamini anatakaswa kupitia mkewe, naye mke asiyeamini anatakaswa kupitia mumewe anayeamini. Kama isingalikuwa hivyo watoto wenu wangalikuwa si safi, lakini ilivyo sasa wao ni watakatifu. 15 Lakini kama yule asiyeamini akijitenga, basi afanye hivyo. Katika hali kama hiyo mwanamke au mwanaume aaminiye hafungwi, kwa sababu Mungu ametuita tuishi kwa amani. 16 Wewe mke, unajuaje kama utamwokoa mumeo? Au wewe mume unajuaje kama utamwokoa mkeo?
-
36 Kama mtu yeyote anadhani kwamba hamtendei ilivyo sawa mwanamwali ambaye amemposa, naye akiwa umri wake unazidi kuendelea na mtu huyo anajisikia kwamba inampasa kuoa, afanye kama atakavyo. Yeye hatendi dhambi. Yawapasa waoane. 37 Lakini mwanaume ambaye ameamua moyoni mwake kutooa bila kulazimishwa na mtu yeyote, bali anaweza kuzitawala tamaa zake kutomwoa huyo mwanamwali, basi anafanya ipasavyo. 38 Hivyo basi, mwanaume amwoaye mwanamwali afanya vyema, lakini yeye asiyemwoa afanya vyema zaidi.
39 Mwanamke aliyeolewa amefungwa na sheria maadamu mumewe yu hai. Lakini mumewe akifa, basi mwanamke huyo yuko huru kuolewa na mume mwingine ampendaye, lakini lazima awe katika Bwana. 40 Lakini kwa maoni yangu, angekuwa na furaha zaidi akibaki alivyo. Nami nadhani pia nina Roho wa Mungu.
-
3 Lakini nina hofu kuwa, kama vile Eva alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Kristo.
-
1 Usimkemee mzee kwa ukali bali umshawishi kama vile angekuwa ni baba yako. Uwatendee vijana kama vile ndugu zako; 2 nao wanawake wazee uwatendee kama mama zako, na wanawake vijana kama dada zako, katika usafi wote.
-
1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini ambao Bwana Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati kweli Mungu alisema, ‘Kamwe msile matunda ya mti wowote wa bustanini’?”
2 Mwanamke akamjibu nyoka, “Tunaweza kula matunda ya miti iliyoko bustanini, 3 lakini Mungu alisema, ‘Kamwe msile tunda la mti ulio katikati ya bustani, wala kuugusa, la sivyo mtakufa.’ ”
4 Lakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa. 5 Kwa maana Mungu anajua ya kuwa wakati mtakapoyala, macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”
6 Mwanamke alipoona ya kuwa tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula na la kupendeza macho, tena linatamanika kwa kujipatia hekima, basi akachuma katika matunda yake, akala, pia akampa mumewe, aliyekuwa pamoja naye, naye akala.
-
13 Ndipo Bwana Mungu akamuuliza mwanamke, “Ni nini hili ambalo umelifanya?” Mwanamke akajibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”
-
17 Lea alikuwa na macho dhaifu, lakini Raheli alikuwa na umbo la kupendeza na mzuri wa sura.
-
1 Hata hivyo, Mfalme Solomoni akawapenda wanawake wengi wa kigeni zaidi, mbali na binti Farao: wanawake wa Wamoabu, Waamoni, Waedomu, Wasidoni na Wahiti. 2 Walitoka katika mataifa ambayo Bwana aliwaambia Waisraeli, “Msije mkaoana nao, kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu mgeukie miungu yao.” Hata hivyo, Solomoni akakaza kuwapenda. 3 Alikuwa na wake 700 mabinti wa uzao wa kifalme, na masuria 300, nao wake zake wakampotosha. 4 Kadiri Solomoni alivyozidi kuzeeka, wake zake wakaugeuza moyo wake kuelekea miungu mingine, na moyo wake haukujitolea kikamilifu kwa Bwana Mungu wake, kama ulivyokuwa moyo wa Daudi baba yake. 5 Solomoni akafuata Ashtorethi mungu mke wa Wasidoni, na Moleki mungu aliyekuwa chukizo la Waamoni. 6 Kwa hiyo Solomoni akafanya uovu machoni pa Bwana; hakumfuata Bwana kikamilifu kama alivyofanya Daudi baba yake.
7 Kwenye kilima mashariki mwa Yerusalemu, Solomoni akajenga mahali pa juu kwa ajili ya Kemoshi chukizo la Wamoabu, na kwa Moleki mungu chukizo la Waamoni. 8 Akafanya hivyo kwa wake zake wote wa kigeni, ambao walifukiza uvumba na kutoa dhabihu kwa miungu yao.
-
13 Mwana mpumbavu ni maangamizi ya babaye,
naye mke mgomvi ni kama kutonatona kusikoisha.
-
14 Nyumba na mali hurithiwa kutoka kwa wazazi,
bali mke mwenye busara hutoka kwa Bwana.
-
9 Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba,
kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi.
-
16 Bwana asema,
“Wanawake wa Sayuni wana kiburi,
wanatembea na shingo ndefu,
wakikonyeza kwa macho yao,
wanatembea kwa hatua za madaha,
wakiwa na mapambo ya njuga kwenye vifundo vya miguu yao.
17 Kwa hiyo Bwana ataleta majipu kwenye vichwa vya wanawake wa Sayuni;
Bwana atazifanya ngozi za vichwa vyao kuwa vipara.”
-
1 Basi kuhusu mambo yale mliyoyaandika: Ni vyema mwanaume asimguse mwanamke. 2 Lakini ili kuepuka zinaa, kila mwanaume na awe na mke wake mwenyewe na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe. 3 Mume atimize wajibu wake wa ndoa kwa mkewe, naye vivyo hivyo mke kwa mumewe. 4 Mwanamke hana mamlaka juu ya mwili wake bali mumewe, wala mume hana mamlaka juu ya mwili wake bali mkewe. 5 Msinyimane, isipokuwa mmekubaliana kufanya hivyo kwa muda fulani ili mweze kujitoa kwa maombi, kisha mrudiane tena ili Shetani asije akapata nafasi ya kuwajaribu kwa sababu ya kutokuwa na kiasi.
-
18 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika:
“Haya ndiyo maneno ya Mwana wa Mungu, ambaye macho yake ni kama mwali wa moto na ambaye miguu yake ni kama shaba iliyosuguliwa sana. 19 Nayajua matendo yako, upendo wako na imani yako, huduma na saburi yako na kwamba matendo yako ya sasa yamezidi yale ya kwanza.
20 “Hata hivyo, nina neno dhidi yako: Unamvumilia yule mwanamke Yezebeli ambaye anajiita nabii, lakini anawafundisha na kuwapotosha watumishi wangu ili wafanye uasherati na kula vyakula vilivyotolewa kafara kwa sanamu. 21 Nimempa muda ili atubu kwa ajili ya uasherati wake, lakini hataki. 22 Kwa hiyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso, na nitawafanya hao wanaozini naye kupata mateso makali wasipotubia njia zake. 23 Nami nitawaua watoto wake. Nayo makanisa yote yatajua kwamba Mimi ndiye nichunguzaye mioyo na nia, na kwamba nitamlipa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake.
Shows Read in context, Share and Copy.