58 Bible Verses About Gratefulness

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Gratefulness
  1. 15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.

  2. 15 Angalieni kuwa mtu asimlipe mwenzake maovu kwa maovu, bali siku zote tafuteni kutendeana mema ninyi kwa ninyi na kwa watu wote.

    16 Furahini siku zote; 17 ombeni bila kukoma; 18 shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.

  3. 15 Kwa hiyo angalieni sana jinsi mnavyoenenda, si kama watu wasio na hekima, bali kama wenye hekima, 16 mkiukomboa wakati, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu. 17 Kwa hiyo msiwe wajinga, bali mpate kujua nini mapenzi ya Bwana. 18 Pia msilewe kwa mvinyo, ambamo ndani yake mna upotovu, bali mjazwe Roho. 19 Msemezane ninyi kwa ninyi kwa zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, mkimwimbia na kumsifu Bwana mioyoni mwenu, 20 siku zote mkimshukuru Mungu Baba kwa kila jambo katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

    21 Nyenyekeaneni ninyi kwa ninyi kwa heshima kwa ajili ya Kristo.

  4. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

    8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo.

  5. 10 Yeye ampaye mpanzi mbegu kwa ajili ya kupanda na mkate kuwa chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu. 11 Mtatajirishwa kwa kila namna ili mpate kuwa wakarimu kila wakati, na kupitia kwetu, ukarimu wenu utamletea Mungu shukrani.

    12 Huduma hii mnayofanya si tu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watakatifu, bali huzidi sana kwa shukrani nyingi apewazo Mungu. 13 Kwa sababu ya huduma ambayo mmejithibitisha wenyewe, watu watamtukuza Mungu kwa ajili ya utiifu ufuatanao na ukiri wenu wa Injili ya Kristo, na kwa ukarimu wenu wa kushiriki pamoja nao na pia wengine wote. 14 Nao katika maombi yao kwenu mioyo yao itawaonea shauku kwa sababu ya neema ipitayo kiasi mliyopewa na Mungu. 15 Ashukuriwe Mungu kwa karama yake isiyoelezeka.

  6. 6 Hivyo basi, kama vile mlivyompokea Kristo Yesu kuwa Bwana, endeleeni kukaa ndani yake, 7 mkiwa na mizizi, na mmejengwa ndani yake, mkiimarishwa katika imani kama mlivyofundishwa, na kufurika kwa wingi wa shukrani.

  7. 1 Njooni, tumwimbie Bwana kwa furaha;

    tumfanyie kelele za shangwe

    Mwamba wa wokovu wetu.

    2 Tuje mbele zake kwa shukrani,

    tumtukuze kwa vinanda na nyimbo.

    3 Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu,

    mfalme mkuu juu ya miungu yote.

  8. Zaburi ya Daudi.

    1 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.

    Vyote vilivyomo ndani yangu

    vilihimidi jina lake takatifu.

    2 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,

    wala usisahau wema wake wote,

    3 akusamehe dhambi zako zote,

    akuponya magonjwa yako yote,

    4 aukomboa uhai wako na kaburi,

    akuvika taji ya upendo na huruma,

    5 atosheleza mahitaji yako kwa vitu vyema,

    ili ujana wako uhuishwe kama wa tai.

  9. 18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao, 19 kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao. 20 Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.

    21 Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza.

  10. 3 Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu.

    Yeye ndiye alituumba, sisi tu mali yake;

    sisi tu watu wake,

    kondoo wa malisho yake.

    4 Ingieni malangoni mwake kwa shukrani

    na katika nyua zake kwa kusifu,

    mshukuruni yeye na kulisifu jina lake.

    5 Kwa maana Bwana ni mwema

    na upendo wake wadumu milele;

    uaminifu wake unadumu kwa vizazi vyote.

  11. KITABU CHA TANO

    1 Mshukuruni Bwana, kwa kuwa yeye ni mwema,

    upendo wake wadumu milele.

    2 Waliokombolewa wa Bwana na waseme hivi,

    wale aliowaokoa kutoka mkono wa adui,

    3 wale aliowakusanya kutoka nchi mbalimbali,

    kutoka mashariki na magharibi,

    kutoka kaskazini na kusini.

  12. 56 Uchungu wa mauti ni dhambi na nguvu ya dhambi ni sheria. 57 Lakini ashukuriwe Mungu, yeye atupaye ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.

    58 Kwa hiyo, ndugu zangu wapenzi, simameni imara, msitikisike, mzidi sana katika kuitenda kazi ya Bwana, kwa maana mnajua ya kuwa, kazi yenu katika Bwana si bure.

  13. 17 Kila kitolewacho kilicho chema na kilicho kamili, hutoka juu, na hushuka kutoka kwa Baba wa mianga, ambaye kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka.

  14. 14 Kwa kuwa hapa hatuna mji udumuo, bali tunautafuta ule ujao.

    15 Basi kwa njia ya Yesu, tuzidi kumtolea Mungu dhabihu ya sifa, yaani matunda ya midomo inayolikiri Jina lake. 16 Na msiache kutenda mema na kushirikiana vile vitu mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu.

  15. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa muth-labeni. Zaburi ya Daudi.

    1 Ee Bwana, nitakutukuza kwa moyo wangu wote,

    nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu.

    2 Nitafurahi na kushangilia ndani yako.

    Nitaliimbia sifa jina lako, Ewe Uliye Juu Sana.

  16. 15 Haya yote ni kwa faida yenu, ili kwamba neema ile inavyowafikia watu wengi zaidi na zaidi, ipate kusababisha shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu.

    16 Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku.

  17. 2 Dumuni sana katika maombi, mkikesha katika hayo pamoja na kushukuru.

  18. 25 Angalieni, msije mkamkataa yeye anenaye. Ikiwa wao hawakuepuka adhabu walipomkataa yeye aliyewaonya hapa duniani, sisi je, tutaokokaje tusipomsikiliza yeye anayetuonya kutoka mbinguni? 26 Wakati ule sauti yake ilitetemesha dunia, lakini sasa ameahidi, “Kwa mara moja tena nitatetemesha si nchi tu bali na mbingu pia.”

    27 Maneno haya “kwa mara moja tena” yanaonyesha kuondoshwa kwa vile vitu vinavyoweza kutetemeshwa, yaani vile vitu vilivyoumbwa, kwa kusudi vile tu visivyoweza kutetemeshwa vibaki.

    28 Kwa hiyo, kwa kuwa tunapokea ufalme ambao hauwezi kutetemeshwa, basi na tuwe na shukrani, na hivyo tumwabudu Mungu kwa namna inayompendeza, kwa unyenyekevu na uchaji, 29 kwa kuwa “Mungu wetu ni moto ulao.”

  19. 30 Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,

    nami nitamtukuza kwa kumtolea shukrani.

    31 Hili litampendeza Bwana kuliko ngʼombe dume,

    zaidi ya fahali akiwa na pembe na kwato zake.

    32 Maskini wataona na kufurahi:

    ninyi mnaomtafuta Mungu, mioyo yenu na iishi!

  20. 14 Lakini Mungu ashukuriwe, yeye ambaye siku zote hutufanya tuandamane kwa ushindi tukiwa ndani ya Kristo. Naye kupitia kwetu hueneza kila mahali harufu nzuri ya kumjua yeye. 15 Kwa maana sisi kwa Mungu ni harufu nzuri ya manukato ya Kristo miongoni mwa wale wanaookolewa na kwa wale wanaopotea. 16 Kwa wale wanaopotea, sisi ni harufu ya mauti iletayo mauti; lakini kwa wale wanaookolewa, sisi ni harufu nzuri iletayo uzima. Ni nani awezaye mambo hayo?

  21. 34 Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema;

    upendo wake wadumu milele.

  22. 1 Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema.

    Fadhili zake zadumu milele.

    2 Mshukuruni Mungu wa miungu.

    Fadhili zake zadumu milele.

    3 Mshukuruni Bwana wa mabwana:

    Fadhili zake zadumu milele.

    4 Kwake yeye pekee atendaye maajabu makuu,

    Fadhili zake zadumu milele.

    5 Ambaye kwa ufahamu wake aliziumba mbingu,

    Fadhili zake zadumu milele.

    6 Ambaye aliitandaza dunia juu ya maji,

    Fadhili zake zadumu milele.

    7 Ambaye aliumba mianga mikubwa,

    Fadhili zake zadumu milele.

    8 Jua litawale mchana,

    Fadhili zake zadumu milele.

    9 Mwezi na nyota vitawale usiku,

    Fadhili zake zadumu milele.

    10 Kwake yeye aliyemuua mzaliwa wa kwanza wa Misri,

    Fadhili zake zadumu milele.

    11 Na kuwatoa Israeli katikati yao,

    Fadhili zake zadumu milele.

    12 Kwa mkono wenye nguvu ulionyooshwa,

    Fadhili zake zadumu milele.

    13 Kwake yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu,

    Fadhili zake zadumu milele.

    14 Na kuwapitisha Israeli katikati yake,

    Fadhili zake zadumu milele.

    15 Lakini alimfagia Farao na jeshi lake katika Bahari ya Shamu,

    Fadhili zake zadumu milele.

    16 Kwake yeye aliyewaongoza watu wake katika jangwa,

    Fadhili zake zadumu milele.

    17 Ambaye aliwapiga wafalme wenye nguvu,

    Fadhili zake zadumu milele.

    18 Naye aliwaua wafalme wenye nguvu,

    Fadhili zake zadumu milele.

    19 Sihoni mfalme wa Waamori,

    Fadhili zake zadumu milele.

    20 Ogu mfalme wa Bashani,

    Fadhili zake zadumu milele.

    21 Akatoa nchi yao kuwa urithi,

    Fadhili zake zadumu milele.

    22 Urithi kwa Israeli mtumishi wake,

    Fadhili zake zadumu milele.

    23 Aliyetukumbuka katika unyonge wetu,

    Fadhili zake zadumu milele.

    24 Alituweka huru toka adui zetu,

    Fadhili zake zadumu milele.

    25 Ambaye humpa chakula kila kiumbe.

    Fadhili zake zadumu milele.

    26 Mshukuruni Mungu wa mbinguni,

    Fadhili zake zadumu milele.

  23. Zaburi. Wimbo wa siku ya Sabato.

    1 Ni vyema kumshukuru Bwana

    na kuliimbia jina lako, Ee Uliye Juu Sana,

    2 kuutangaza upendo wako asubuhi,

    na uaminifu wako wakati wa usiku,

    3 kwa zeze yenye nyuzi kumi

    na kwa sauti ya kinubi.

    4 Ee Bwana, kwa kuwa matendo yako yamenifurahisha,

    nitaziimba kwa shangwe kazi za mikono yako.

  24. 15 Kwa sababu hii, tangu niliposikia juu ya imani yenu katika Bwana Yesu na upendo wenu kwa watakatifu wote, 16 sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, nikiwakumbuka katika maombi yangu. 17 Nazidi kumwomba Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awajalieni ninyi roho ya hekima na ya ufunuo, ili mpate kumjua zaidi. 18 Ninaomba pia kwamba macho ya mioyo yenu yatiwe nuru ili mpate kujua tumaini mliloitiwa, utajiri wa urithi wa utukufu wake kwa watakatifu 19 na uweza wake mkuu usiolinganishwa kwa ajili yetu sisi tuaminio. Uweza huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na ile nguvu kuu mno 20 aliyoitumia katika Kristo alipomfufua kutoka kwa wafu, na akamketisha mkono wake wa kuume huko mbinguni, 21 juu sana kuliko falme zote na mamlaka, enzi na milki, na juu ya kila jina litajwalo, si katika ulimwengu huu tu, bali katika ule ujao pia. 22 Naye Mungu ameweka vitu vyote viwe chini ya miguu yake na amemfanya yeye awe kichwa cha vitu vyote kwa ajili ya Kanisa, 23 ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake yeye aliye yote katika yote.

  25. 9 Lakini mimi, kwa wimbo wa shukrani,

    nitakutolea dhabihu.

    Lile nililowekea nadhiri nitalitimiza.

    Wokovu watoka kwa Bwana.”

  26. 3 Ndugu, imetubidi kumshukuru Mungu kwa ajili yenu siku zote, kama ulivyo wajibu wetu, kwa sababu imani yenu inakua zaidi na zaidi na upendo wa kila mmoja wenu alio nao kwa mwenzake unazidi kuongezeka. 4 Ndiyo sababu miongoni mwa makanisa ya Mungu, tunajivuna kuhusu saburi yenu na imani mliyo nayo katika mateso yote na dhiki mnazostahimili.

  27. 16 Nao wale wazee ishirini na wanne, waliokuwa wameketi mbele za Mungu, kwenye viti vyao vya enzi, wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, 17 wakisema:

    “Tunakushukuru, Bwana Mungu Mwenyezi,

    uliyeko na uliyekuwako,

    kwa kuwa umetwaa uweza wako mkuu

    na ukaanza kutawala.

  28. 41 Kwa hiyo wakaliondoa lile jiwe kutoka kaburini. Yesu akainua macho yake juu akasema, “Baba, ninakushukuru kwa kuwa wanisikia. 42 Ninajua ya kuwa wewe hunisikia siku zote, lakini nimesema haya kwa ajili ya umati huu uliosimama hapa, ili wapate kuamini ya kuwa wewe umenituma.”

  29. 1 Yakobo, mtumwa wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo:

    Kwa makabila kumi na mawili yaliyotawanyika ulimwenguni:

    Salamu.

    2 Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3 kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. 4 Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu chochote.

  30. 6 Bwana asifiwe,

    kwa maana amesikia kilio changu

    nikimwomba anihurumie.

    7 Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu,

    moyo wangu umemtumaini yeye,

    nami nimesaidiwa.

    Moyo wangu unarukaruka kwa furaha

    nami nitamshukuru kwa wimbo.

  31. 23 Ninakushukuru na kukuhimidi,

    Ee Mungu wa baba zangu:

    Umenipa hekima na uwezo,

    umenijulisha kile tulichokuomba,

    umetujulisha ndoto ya mfalme.”

  32. 11 Yesu alipokuwa njiani akienda Yerusalemu, alipitia mpakani mwa Samaria na Galilaya. 12 Alipokuwa akiingia kwenye kijiji kimoja, watu kumi waliokuwa na ukoma wakakutana naye. Wakasimama mbali, 13 wakapaza sauti, wakasema, “Yesu, Bwana, tuhurumie!”

    14 Alipowaona akawaambia, “Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani.” Nao walipokuwa njiani wakienda, wakatakasika.

    15 Mmoja wao alipoona kwamba amepona, akarudi kwa Yesu, akimsifu Mungu kwa sauti kuu. 16 Akajitupa miguuni mwa Yesu akamshukuru. Yeye alikuwa Msamaria.

    17 Yesu akauliza, “Je, hawakutakaswa wote kumi? Wako wapi wale wengine tisa? 18 Hakuna hata mmoja aliyeonekana kurudi ili kumshukuru Mungu isipokuwa huyu mgeni?” 19 Yesu akamwambia, “Inuka na uende zako, imani yako imekuponya.”

  33. 47 “Bwana yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu!

    Atukuzwe Mungu,

    Mwamba, Mwokozi wangu!

    48 Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi,

    ayawekaye mataifa chini yangu,

    49 aniwekaye huru toka kwa adui zangu.

    Uliniinua juu ya adui zangu;

    uliniokoa toka kwa watu wajeuri.

    50 Kwa hiyo nitakusifu, Ee Bwana,

    katikati ya mataifa;

    nitaliimbia sifa jina lako.

    51 Humpa mfalme wake ushindi mkuu;

    huonyesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake,

    kwa Daudi na wazao wake milele.”

  34. 1 Msifuni Bwana.

    Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema;

    upendo wake wadumu milele.

  35. 21 Hata hivyo najikumbusha neno hili

    na kwa hiyo ninalo tumaini.

    22 Kwa sababu ya upendo mkuu wa Bwana, hatuangamii,

    kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe.

    23 Ni mpya kila asubuhi,

    uaminifu wako ni mkuu.

    24 Nimeiambia nafsi yangu, “Bwana ni fungu langu,

    kwa hiyo nitamngojea.”

    25 Bwana ni mwema kwa wale ambao tumaini lao ni kwake,

    kwa yule ambaye humtafuta;

  36. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.

  37. 8 Kwanza kabisa, namshukuru Mungu wangu kwa njia ya Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inatangazwa duniani kote.

  38. 3 Ninamshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo ninyi. 4 Katika maombi yangu yote daima nimekuwa nikiwaombea ninyi nyote kwa furaha, 5 kwa sababu ya kushiriki kwenu katika kueneza Injili, tangu siku ya kwanza hadi leo. 6 Nina hakika kwamba yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu, ataiendeleza na kuikamilisha hata siku ya Kristo Yesu.

  39. 1 Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake,

    wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda.

    2 Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa,

    waambieni matendo yake yote ya ajabu.

    3 Lishangilieni jina lake takatifu,

    mioyo ya wale wamtafutao Bwana na ifurahi.

  40. 24 Hii ndiyo siku Bwana aliyoifanya,

    tushangilie na kufurahi ndani yake.

  41. 28 Wewe ni Mungu wangu, nitakushukuru,

    wewe ni Mungu wangu, nitakutukuza.

    29 Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema;

    upendo wake wadumu milele.

  42. 1 Napenda kumtambulisha kwenu dada yetu Foibe, mtumishi katika kanisa la Kenkrea. 2 Naomba mpokeeni katika Bwana ipasavyo watakatifu na kumpa msaada wowote atakaohitaji kutoka kwenu, kwa maana yeye amekuwa msaada kwa watu wengi, mimi nikiwa miongoni mwao.

    3 Wasalimuni Prisila na Akila, watumishi wenzangu katika Kristo Yesu. 4 Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu; wala si mimi tu ninayewashukuru bali pia makanisa yote ya watu wa Mataifa.

  43. 11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

  44. 12 Utajiri na heshima vyatoka kwako;

    wewe ndiwe utawalaye vitu vyote.

    Mikononi mwako kuna nguvu na uweza

    ili kuinua na kuwapa wote nguvu,

    13 Sasa, Mungu wetu, tunakushukuru

    na kulisifu Jina lako tukufu.

    14 “Lakini mimi ni nani, nao watu wangu ni nani, hata tuweze kukutolea kwa ukarimu namna hii? Vitu vyote vyatoka kwako, nasi tumekutolea tu vile vitokavyo mkononi mwako.

  45. 17 Nitamshukuru Bwana kwa ajili ya haki yake,

    na nitaliimbia sifa jina la Bwana Aliye Juu Sana.

  46. 18 Nami nitakushukuru mbele ya kusanyiko kubwa,

    nitakusifu katikati ya watu wengi.

  47. 14 Toa sadaka za shukrani kwa Mungu,

    timiza nadhiri zako kwake Yeye Aliye Juu Sana,

    15 na uniite siku ya taabu;

    nami nitakuokoa, nawe utanitukuza.”

  48. 6 Nitakutolea dhabihu za hiari;

    Ee Bwana, nitalisifu jina lako

    kwa kuwa ni vyema.

    7 Kwa maana ameniokoa katika shida zangu zote,

    na macho yangu yamewatazama adui zangu kwa ushindi.

  49. 21 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma,

    na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu.

    22 Na watoe dhabihu za kushukuru,

    na wasimulie matendo yake kwa nyimbo za furaha.

  50. 62 Usiku wa manane ninaamka kukushukuru

    kwa sababu ya sheria zako za haki.

  51. 17 Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. 18 Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. 19 Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.

  52. 4 Siku zote ninamshukuru Mungu ninapokukumbuka katika maombi yangu, 5 kwa sababu ninasikia juu ya imani yako katika Bwana Yesu na upendo wako kwa watakatifu wote. 6 Naomba utiwe nguvu katika kuishuhudia imani yako, ili upate kuwa na ufahamu mkamilifu juu ya kila kitu chema tulicho nacho ndani ya Kristo. 7 Upendo wako umenifurahisha mno na kunitia moyo, kwa sababu wewe ndugu, umeiburudisha mioyo ya watakatifu.

  53. 8 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma,

    na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu,

    9 kwa maana yeye humtosheleza mwenye kiu,

    na kumshibisha mwenye njaa kwa vitu vyema.

  54. Wimbo wa kwenda juu.

    1 Bwana alipowarejeza mateka Sayuni,

    tulikuwa kama watu walioota ndoto.

    2 Vinywa vyetu vilijaa kicheko,

    ndimi zetu zilijaa nyimbo za shangwe.

    Ndipo iliposemwa miongoni mwa mataifa,

    “Bwana amewatendea mambo makuu.”

    3 Bwana ametutendea mambo makuu,

    nasi tumejaa furaha.

  55. Zaburi ya Daudi.

    1 Nitakusifu wewe, Ee Bwana, kwa moyo wangu wote,

    mbele ya “miungu” nitaimba sifa zako.

    2 Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu,

    nami nitalisifu jina lako

    kwa ajili ya upendo wako

    na uaminifu,

    kwa kuwa umelikuza jina lako na neno lako

    juu ya vitu vyote.

    3 Nilipoita, ulinijibu;

    ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari.

    4 Wafalme wote wa dunia wakusifu wewe Ee Bwana,

    wakati wanaposikia maneno ya kinywa chako.

    5 Wao na waimbe kuhusu njia za Bwana,

    kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu.

  56. 30 Kama nikila kwa shukrani, kwa nini nashutumiwa kwa kile ambacho kwa hicho ninamshukuru Mungu?

    31 Basi, lolote mfanyalo, kama ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.

  57. 12 Namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu, kwa sababu aliniona mwaminifu, akaniteua kwa kazi yake. 13 Ingawa wakati fulani nilikuwa mwenye kukufuru, mtesaji na mwenye jeuri, lakini nilipata rehema kwa sababu nilitenda hivyo kwa kutojua na kutoamini kwangu. 14 Neema ya Bwana wetu ilimiminwa juu yangu kwa wingi, ikiambatana na imani na upendo ulio katika Kristo Yesu.

    15 Msemo huu ni wa kweli na unaostahili kukubalika, usemao kwamba: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, ambao mimi ndiye niliye mbaya kuliko wote. 16 Lakini kwa sababu hiyo nilipata rehema, ili katika mimi, niliyekuwa mwenye dhambi kuliko wote, Kristo Yesu apate kuonyesha uvumilivu wake usio na kikomo, ili niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini na wapate uzima wa milele. 17 Basi Mfalme wa milele, asiye na mwisho, asiyeonekana, aliye Mungu pekee, apewe heshima na utukufu milele na milele. Amen.

  58. 3 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa rehema zake kuu ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima kupitia kwa kufufuka kwa Yesu Kristo kutoka kwa wafu, 4 ili tuupate urithi usioharibika, usio na uchafu, ule usionyauka: uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu, 5 ninyi ambao mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani, hadi uje ule wokovu ulio tayari kufunuliwa nyakati za mwisho. 6 Katika hili mnafurahi sana, ingawa sasa kwa kitambo kidogo mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna nyingi. 7 Haya yamewajia ili kwamba imani yenu, iliyo ya thamani kuliko dhahabu ipoteayo, ingawa hujaribiwa kwa moto, ionekane kuwa halisi na imalizie katika sifa, utukufu na heshima wakati Yesu Kristo atadhihirishwa. 8 Ingawa hamjamwona, mnampenda; tena ingawa sasa hammwoni, mnamwamini na kujawa na furaha isiyoneneka yenye utukufu usioelezeka. 9 Maana mnaupokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu.