34 Bible Verses About Food

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Food
  1. 32 Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, si Mose aliyewapa mikate kutoka mbinguni, bali Baba yangu ndiye anawapa mkate wa kweli kutoka mbinguni. 33 Kwa maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”

    34 Wakamwambia, “Bwana, kuanzia sasa tupatie huo mkate siku zote.”

    35 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uzima. Yeye ajaye kwangu, hataona njaa kamwe na yeye aniaminiye, hataona kiu kamwe.

  2. 23 “Vitu vyote ni halali,” lakini si vitu vyote vilivyo na faida. “Vitu vyote ni halali,” lakini si vyote vinavyojenga. 24 Mtu yeyote asitafute yaliyo yake mwenyewe, bali kila mtu atafute yale yanayowafaa wengine.

    25 Kuleni chochote kinachouzwa sokoni, bila kuuliza swali lolote kwa ajili ya dhamiri. 26 Kwa maana, “Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana.”

    27 Kama ukikaribishwa chakula na mtu asiyeamini nawe ukikubali kwenda, kula kila kitu kitakachowekwa mbele yako bila kuuliza maswali kwa ajili ya dhamiri. 28 Lakini kama mtu yeyote akikuambia, “Hiki kimetolewa kafara kwa sanamu,” basi usikile kwa ajili ya huyo aliyekuambia na kwa ajili ya dhamiri. 29 Nina maana dhamiri ya huyo aliyekuambia, wala si kwa ajili ya dhamiri yako. Lakini kwa nini uhuru wangu uhukumiwe na dhamiri ya mtu mwingine? 30 Kama nikila kwa shukrani, kwa nini nashutumiwa kwa kile ambacho kwa hicho ninamshukuru Mungu?

    31 Basi, lolote mfanyalo, kama ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu. 32 Msiwe kikwazo kwa mtu yeyote, wawe Wayahudi au Wayunani, au kwa kanisa la Mungu, 33 kama hata mimi ninavyojaribu kumpendeza kila mtu kwa kila namna. Kwa maana sitafuti mema kwa ajili yangu mwenyewe bali kwa ajili ya wengi, ili waweze kuokolewa.

  3. 29 Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote, na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa chakula chenu. 30 Nao wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani, na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi: yaani kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo.

  4. 27 Daudi alipofika Mahanaimu, Shobi mwana wa Nahashi kutoka Raba ya Waamoni, Makiri mwana wa Amieli kutoka Lo-Debari, na Barzilai Mgileadi kutoka Rogelimu 28 wakaleta matandiko ya kitandani, mabakuli na vyombo vya mfinyanzi. Walileta pia ngano na shayiri, unga na bisi, maharagwe na kunde, 29 asali na maziwa yaliyoganda, kondoo na jibini kutoka kwenye maziwa ya ngʼombe kwa ajili ya Daudi na watu wake ili wale. Kwa maana walisema, “Watu wameona njaa, tena wamechoka na wamepata kiu huko jangwani.”

  5. 2 Wanyama wote wa duniani, ndege wote wa angani, kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi, na samaki wote wa baharini wamekabidhiwa mikononi mwenu, nao watawaogopa na kuwahofu. 3 Kila kitu chenye uhai kiendacho kitakuwa chakula chenu. Kama vile nilivyowapa mimea mbalimbali, sasa nawapa kila kitu.

    4 “Lakini kamwe msile nyama ambayo bado ina damu ya uhai wake, kwa maana damu ni uhai. 5 Hakika damu ya uhai wenu nitaidai. Nitaidai kutoka kwa kila mnyama. Kutoka kwa kila mwanadamu pia nitaidai kwa ajili ya uhai wa mtu mwenzake.

  6. 4 Lakini Yesu akajibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’ ”

  7. 25 “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini au mtakunywa nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi?

  8. 27 Msishughulikie chakula kiharibikacho, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana wa Adamu atawapa. Yeye ndiye ambaye Mungu Baba amemtia muhuri.”

  9. 13 Akamfanya apande sehemu zilizoinuka za nchi,

    akamlisha kwa mavuno ya mashamba.

    Akamlea kwa asali toka mwambani,

    na kwa mafuta kutoka mwamba mgumu,

    14 kwa jibini na maziwa kutoka makundi ya ngʼombe

    na kutoka makundi ya mbuzi,

    kwa mafuta ya wana-kondoo na mbuzi,

    kwa kondoo dume wazuri wa Bashani,

    na kwa ngano nzuri.

    Ukanywa damu ya zabibu inayotoa povu.

  10. 18 Akawajibu, “Je, hata nanyi hamwelewi? Je, hamfahamu kwamba kitu kimwingiacho mtu hakimtii unajisi? 19 Mtu akila kitu hakiingii moyoni mwake bali tumboni, na baadaye hutolewa nje ya mwili wake.” (Kwa kusema hivi, Yesu alivihalalisha vyakula vyote kuwa ni “safi.”)

    20 Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. 21 Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, 22 tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu. 23 Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.”

  11. 1 Mkaribisheni yeye ambaye imani yake ni dhaifu, lakini si kwa kugombana na kubishana juu ya mawazo yake. 2 Mtu mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu, lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula mboga tu. 3 Yeye alaye kila kitu asimdharau yeye asiyekula. Wala yeye asiyekula kila kitu asimhukumu yule alaye kila kitu, kwa maana Mungu amemkubali. 4 Wewe ni nani hata umhukumu mtumishi wa mtu mwingine? Kwa bwana wake tu anasimama au kuanguka. Naye atasimama kwa sababu Bwana anaweza kumsimamisha.

    5 Mtu mmoja anaitukuza siku fulani kuwa ni bora kuliko nyingine, na mwingine anaona kuwa siku zote ni sawa. Basi kila mmoja awe na hakika na yale anayoamini.

  12. 4 Kwa maana kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, wala hakuna kitu chochote cha kukataliwa kama kikipokewa kwa shukrani, 5 kwa sababu kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.

  13. 17 Wakati huo Yese akamwambia mwanawe Daudi, “Chukua hii efa ya bisi na hii mikate kumi kwa ajili ya ndugu zako uwapelekee upesi kambini mwao. 18 Chukua pamoja na hizi jibini kumi kwa jemadari wa kikosi chao. Ujue hali ya ndugu zako na uniletee taarifa za uhakika kutoka kwao.

  14. 31 Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wakimsihi, “Rabi, kula angalau chochote.”

    32 Lakini yeye akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkifahamu.”

    33 Basi wanafunzi wakaanza kuulizana, “Kuna mtu ambaye amemletea chakula?” 34 Lakini Yesu akawajibu, “Chakula changu ni kufanya mapenzi ya Mungu ambaye amenituma na kuikamilisha kazi yake.

  15. 12 “Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini si vitu vyote vyenye faida. “Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini sitatawaliwa na kitu chochote. 13 “Chakula ni cha tumbo, na tumbo ni la chakula”: lakini Mungu ataviangamiza vyote viwili. Mwili haukuumbwa kwa ajili ya zinaa bali kwa ajili ya Bwana na Bwana kwa ajili ya mwili.

  16. 7 Nenda, kula chakula chako kwa furaha, unywe divai yako kwa moyo wa shangwe, kwa maana sasa Mungu anakubali unachofanya.

  17. 1 Bwana akamtokea Abrahamu karibu na mialoni ya Mamre wakati alipokuwa ameketi kwenye ingilio la hema lake wakati wa adhuhuri. 2 Abrahamu akainua macho akaona watu watatu wamesimama karibu naye. Alipowaona, aliharakisha kutoka kwenye ingilio la hema lake kuwalaki na kuwasujudia hadi nchi.

    3 Akasema, “Kama nimepata kibali machoni penu, ee bwana wangu, usimpite mtumishi wako. 4 Acha yaletwe maji kidogo, kisha ninyi nyote mnawe miguu yenu na mpumzike chini ya mti huu. 5 Niruhusuni niwapatie chakula kidogo mle, ili mpate nguvu mwendelee na safari yenu, kwa kuwa mmekuja kwa mtumishi wenu.”

    Nao wakamjibu, “Vema sana, fanya kama unavyosema.”

    6 Hivyo Abrahamu akaharakisha akaingia hemani kwa Sara, akamwambia, “Chukua vipimo vitatu vya unga laini haraka, ukande na uoke mikate.”

    7 Kisha Abrahamu akakimbia kwenda kwenye kundi, akachagua ndama mzuri, laini na akampa mtumishi, ambaye aliharakisha kumtayarisha. 8 Kisha akaleta jibini, maziwa na nyama ya yule ndama iliyoandaliwa, akaviweka mbele ya wageni. Walipokuwa wakila, alisimama karibu nao chini ya mti.

  18. 8 Lakini chakula hakituleti karibu na Mungu, wala hatupotezi chochote tusipokula, wala hatuongezi chochote kama tukila.

    9 Lakini angalieni jinsi mnavyotumia uhuru wenu usije ukawa kikwazo kwao walio dhaifu.

  19. 1 Bwana akamwambia Mose, 2 “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Ikiwa mwanaume au mwanamke anataka kuweka nadhiri maalum, nadhiri ya kutengwa kwa ajili ya Bwana kama Mnadhiri, 3 ni lazima ajitenge na mvinyo na kinywaji kingine chochote chenye chachu, na kamwe asinywe siki itokanayo na mvinyo au itokanayo na kinywaji kingine chenye chachu. Kamwe asinywe maji ya zabibu wala kula zabibu mbichi au kavu. 4 Kwa muda wote atakaokuwa Mnadhiri, kamwe hatakula chochote kitokanacho na mzabibu, sio mbegu wala maganda.

  20. 22 Mahitaji ya Solomoni ya kila siku yalikuwa kori thelathini za unga laini, kori sitini za unga wa kawaida. 23 Ngʼombe kumi wa zizini, ngʼombe ishirini wa malisho, kondoo na mbuzi mia moja, pamoja na ayala, paa, kulungu na kuku wazuri sana.

  21. 24 Maneno ya kupendeza ni kama sega la asali,

    ni matamu kwa nafsi na uponyaji kwenye mifupa.

  22. 11 Basi baba yao Israeli akawaambia, “Kama ni lazima iwe hivyo, basi fanyeni hivi: Wekeni baadhi ya mazao bora ya nchi katika mifuko yenu na mpelekeeni yule mtu kama zawadi, zeri kidogo, asali kidogo, vikolezo, manemane, kungu na lozi.

  23. 11 Wakamkuta Mmisri katika shamba fulani, nao wakamleta kwa Daudi. Wakampa huyo Mmisri maji ya kunywa na chakula; 12 kipande cha andazi la tini na andazi la zabibu zilizokaushwa. Akala naye akapata nguvu, kwa kuwa hakuwa amekula chakula chochote wala kunywa maji kwa siku tatu usiku na mchana.

  24. 14 Huyafanya majani ya mifugo yaote,

    na mimea kwa watu kulima,

    wajipatie chakula kutoka ardhini:

    15 divai ya kuufurahisha moyo wa mwanadamu,

    mafuta kwa ajili ya kungʼarisha uso wake,

    na mkate wa kutia mwili nguvu.

  25. 1 Uketipo kula chakula na mtawala,

    angalia vyema kile kilicho mbele yako,

    2 na utie kisu kooni mwako

    kama ukiwa mlafi.

    3 Usitamani vyakula vyake vitamu

    kwa kuwa chakula hicho ni cha hila.

  26. 2 Kwa nini kutumia fedha kwa kitu ambacho si chakula,

    na kutaabikia kitu kisichoshibisha?

    Sikilizeni, nisikilizeni mimi na mle kilicho kizuri,

    nazo nafsi zenu zitafurahia utajiri wa unono.

  27. 31 Watu wa Israeli wakaita ile mikate mana Ilikuwa myeupe kama mbegu za mtama na ladha yake ilikuwa kama mkate mwembamba uliotengenezwa kwa asali.

  28. 18 Abigaili akafanya haraka, akachukua mikate mia mbili, viriba viwili vya divai, kondoo watano waliochinjwa vipimo vitano vya bisi, vishada mia moja vya zabibu kavu, mikate mia mbili ya tini, akavipakia juu ya punda.

  29. 10 Hivyo akaenda Sarepta. Alipofika kwenye lango la mji, mjane alikuwa huko akiokota kuni. Akamwita na kumwambia, “Naomba uniletee maji kidogo kwenye gudulia ili niweze kunywa.” 11 Alipokuwa anakwenda kumletea, akamwita akasema, “Tafadhali niletee pia kipande cha mkate.”

    12 Akamjibu, “Hakika kama Bwana Mungu wako aishivyo, sina mkate wowote, isipokuwa konzi ya unga kwenye gudulia na mafuta kidogo kwenye chupa. Ninakusanya kuni chache nipeleke nyumbani na nikapike chakula kwa ajili yangu na mwanangu, ili kwamba tule, kiishe, tukafe.”

    13 Eliya akamwambia, “Usiogope. Nenda nyumbani ukafanye kama ulivyosema. Lakini kwanza unitengenezee mimi mkate mdogo kutoka vile ulivyo navyo kisha uniletee na ndipo utayarishe chochote kwa ajili yako na mwanao. 14 Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Lile gudulia la unga halitakwisha wala ile chupa ya mafuta haitakauka hadi siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi.’ ”

    15 Akaondoka na kufanya kama Eliya alivyomwambia. Kwa hiyo kukawa na chakula kila siku kwa ajili ya Eliya, yule mwanamke na jamaa yake. 16 Kwa kuwa lile gudulia la unga halikwisha na ile chupa ya mafuta haikukauka, sawasawa na lile neno la Bwana alilosema Eliya.

  30. 14 Yesu alipofika kando ya bahari, aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia na akawaponya wagonjwa wao.

    15 Ilipofika jioni, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na muda sasa umekwisha. Waage makutano ili waende zao vijijini wakajinunulie chakula.”

    16 Yesu akawaambia, “Hakuna sababu ya wao kuondoka. Ninyi wapeni chakula.”

    17 Wakamjibu, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu.”

    18 Akawaambia, “Nileteeni hivyo vitu hapa.” 19 Yesu akaagiza makutano wakae chini kwenye nyasi. Akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi, nao wanafunzi wakawagawia makutano. 20 Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili. 21 Idadi ya watu waliokula walikuwa wanaume wapatao 5,000, bila kuhesabu wanawake na watoto.

  31. 10 Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walikuwa wakiandaa chakula, akalala usingizi mzito sana. 11 Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama nguo kubwa kikishushwa duniani kwa ncha zake nne. 12 Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao nchini, na ndege wa angani. 13 Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.”

    14 Petro akajibu, “La hasha Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu chochote kilicho najisi.”

    15 Ile sauti ikasema naye mara ya pili, “Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.”

  32. 10 Yeye ampaye mpanzi mbegu kwa ajili ya kupanda na mkate kuwa chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu.

  33. 16 Kwa hiyo mtu asiwahukumu ninyi kuhusu vyakula au vinywaji, au kuhusu kuadhimisha sikukuu za dini, au Sikukuu za Mwezi Mwandamo au siku ya Sabato. 17 Hizi zilikuwa kivuli cha mambo ambayo yangekuja, lakini ile iliyo halisi imo ndani ya Kristo.

  34. 17 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa. Nitampa pia jiwe jeupe ambalo juu yake limeandikwa jina jipya asilolijua mtu, isipokuwa yule anayelipokea.